Wazo zuri sana kama litakubaliaka.Wanabodi,
Loe nchi yetu tumeadhimisha miaka 60 ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar, na kuwa nchi moja ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Muungano wetu ni muungano adimu na muungano adhimu, kwasababu hapa duniani hakuna muungano mwingine wowote kama huu muungano wetu. Ni muungano wa nchi mbili kuungana na kuunda nchi moja ya JMT, yenye nchi mbili ndani yake, Tanzania na Zanzibar, wenye marais wawili, rais wa JMT na Rais wa Zanzibar, wenye Katiba mbili, katiba ya JMT na Katiba ya Zanzibar, wenye mabunge mawili, Bunge la JMT na Baraza la Wawakilishi, lenye mahakama mbili, mahakama kuu ya Tanzania na Mahakama kuu ya Zanzibar. Kwa maoni yangu, muungano wa aina hii kudumu kwa miaka 60, itoshe, sasa twende kwenye muungano kamili wa nchi moja, serikali moja na rais mmoja!.
Kuungana kwa TANU na ASP
Vyama vya TANU na ASP vilipoungana ile 1977, sii wengi humu walikuwa wamezaliwa!, wengi humu wamezaliwa, wameikuta CCM, hawakuikuta TANU na ASP, hivyo hawajui kwanini TANU na ASP viliungana, na viliungana ili iweje?.
Mimi ni mtu wa 60s, hivyo ile 1977, TANU na ASP zilipoungana nilikuwa darasa la tatu, kijijini Itonjanda, nikikaa kwa bibi mzaa Baba, Bibi Wakawombwe, (RIP) baada ya Baba Mzee Mayalla(RIP) kuhusika na yale mambo fulani ya Mwanza ya 1976!.
Sababu ya TANU na ASP kuungana, ni kuelekea kwenye serikali moja!. Baba wa taifa, Mwalimu Nyerere alisema huu muungano wa vyama vya TANU na ASP na kuzaliwa chama kipya, Chama cha Mapinduzi, CCM, ni mwanzo wa safari ya kuondoka kwenye serikali mbili, kuelekea kwenye serikali moja!. Jee ndoto hii ya Mwalimu Nyerere, kwa Tanzania kuwa nchi moja ya JMT yenye serikali moja na rais mmoja, itakuja kutimia?.
Watanzania wanahitaji sana kuelimishwa kuhusu huu muungano wetu adimu na adhimu, tena ni Rais Samia, ndie kiongozi wa kwanza wa juu aliyetoa ruhusa watu waachwe huru kujadili muungano. Baada ya muungano, nchi zote mbili zilitoweka, hakuna nchi ya Tanganyika wala hakuna nchi ya Zanzibar, bali nchi ya Tanzania ni nchi moja ya JMT yenye sehemu mbili, Tanzania Bara iliyokuwa Tanganyika na Tanzania Visiwani au Tanzania Zanzibar iliyokuwa Zanzibar.
Elimu ya Uraia Kuhusu Muungano wetu adimu na adhimu!.
Duniani kuna miungano ya aina mbili Kuu,
1. Miungano ya union, nchi mbili au zaidi zinaungana kuunda nchi moja. Zile nchi zote zinakufa na inazaliwa nchi moja mpya.
2. Miungano ya federation, ni nchi mbili au zaidi zinaungana na kuunda nchi moja, ila zile nchi zote zinakuwa na serikali ya muungano, Federal Government na State Government, kila nchi ina utawala wake wa ndani.
Muungano wetu ni very unique, ndio maana unaitwa muungano adimu na adhimu, kwasababu ni muungano pekee duniani ambao upande mmoja ni muungano wa union kwa nchi mbili kuungana kuunda nchi moja ya JMT, na upande wa pili ni muungano wa federation wenye serikali mbili, marais wawili, mabunge mawili na mahakama mbili.
Muungano wetu kimataifa ni muungano wa union, Tanzania kimataifa ni nchi moja ya JMT, yenye serikali moja ya JMT, chini ya rais mmoja wa JMT, ambaye ni mkuu wan chi, mkuu wa serikali na amiri jeshi mkuu.
Lakini Kitaifa, nchi ya Tanzania ni nchi moja ya JMT yenye sehemu mbili, Tanzania Bara na Tanzania Visiwani au Tanzania Zanzibar, yenye katiba mbili, katiba ya JMT, na katiba ya Zanzibar, yenye serikali mbili, serikali ya JMT na serikali ya Zanzibar, SMZ, yenye marais wawili, rais wa JMT na rais wa Zanzibar
Mkanganyiko wa Katiba.
Kama nilivyosema kimataifa Tanzania ni nchi moja ya JMT, hakuna mkanganyiko wowote wa kimataifa kuhusu Tanzania.
Lakini Kitaifa kuna mkanganyiko wa katiba kati ya katiba ya JMT na katiba ya Zanzibar.
Kwa mujibu wa katiba ya JMT, ya mwaka 1977, Tanzania ni nchi moja ya JMT yenye sehemu mbili, Tanzania Bara na Tanzania Visiwani au Tanzania Zanzibar. Zanzibar sio nchi bali ni sehemu ya JMT yenye utawala wake wa ndani.
Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, inaiita Zanzibar ni nchi, ni moja ya nchi mbili zinazounda JMT!. Kitendo cha katiba ya Zanzibar kuuita Zanzibar ni nchi, kinawakanganya Watanzania kudhani kuwa nchi ya Tanganyika ndio pekee iliyokufa ila nchi ya Zanzibar ipo haikufa.
Naomba niwahakikishie Tanzania ni nchi moja ya JMT, ile nchi inayotajwa na katiba ya Zanzibar kuwa ni nchi ya Zanzibar, sii kweli kuwa Zanzibar ni nchi, bali ni jina tuu, hayo mabadiliko ya katiba ya Zanzibar kujiita nchi, kimuungano ni mabadiko batili, ila, kwa vile mabadiliko hayo ni kwaajili ya Zanzibar tuu, na hayatambuliwi na katiba ya JMT, serikali ya JMT, imeamua kuyapuuza!, lakini kufuatia hizi kelele, tutapuuza mpaka lini?. Si ni bora twende kwenye serikali moja, haya yote yaishe?.
Hitimisho
Kwa vile Rais Samia, anakwenda kutupatia katiba mpya, nashauri hili la mkanganyika wa katiba kati ya katiba ya JMT na Katiba ya Zanzibar, pia litarekebishwa, na kwa maoni yangu, dawa pekee ya uhakika na ya kudumu ambayo ni mwarobaini wa kuzimaliza kero zote za muungano, ni kwenda kwenye serikali moja. Nimalizie na hili swali, je, Tanzania sasa tumefika wakati wa kutimiza ndoto ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, ya uzalendo wa kweli wa JMT, wa kwenda kwenye nchi moja, yenye serikali moja na rais mmoja?
Hongera kwa miaka 60 ya Muungano wetu adimu na adhimu,
Sasa twende kwenye nchi moja, serikali moja na rais mmoja!.
Mungu Ibariki Tanzania.
Paskali