MIMI NA MIMI

A Story by Elton Tonny

Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Tamaa, Hila, Usaliti, Siri, Mambo Yasiyotazamiwa

R-rated 18+

Enjoy!


β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…

SEHEMU YA KUMI NA NNE

β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…


Mama Chande akaendelea kusema, "Ile jana nilipata taarifa eti Joy alikuwa amevamiwa, akapigwa, lakini hakujua amepigwa na nani. Yaani wakaenda mpaka polisi... akawa amehojiwa. Aliulizwa kama alifahamu watakaokuwa wamefanya hayo kwa sababu mapolisi waliona hao watu walimlenga yeye kabisa, lakini akasema hajui. Leo ndo' tunapata hizi taarifa. Jamani!"

Nikamwangalia Ankia kwa ufupi, akiwa bado ameinamisha tu uso wake, nami nikauliza, "Ameuawa vipi?"

"Nasikia sijui amechomwa na visu, sijui amekatwa na mapanga... eh, yaani bado sijaelewa," mama Chande akasema.

Nikafumba macho kwa ufupi, kisha nikafumbua na kuuliza, "Wapi?"

"Nasikia alikuwa huko mitaa ya Buza. Jamani dada wa watu alikuwa mzuri! Alikuwa rafiki yetu sana, akija anatuchangamkia kweli, yaani ni kama tumetoka mbali kweli japo tumekutania huku tu. Sijui hao watu walikuwa wanamtaka nini! Na ni kweli kama mapolisi walivyosema, walikuwa wanamlenga yeye hata kwenye hiyo ya kupigwa. Nimeogopa sana jamani yaani... ah! Ankia... jikaze dada, ndo' maisha... yamempata mwenzetu, tuombe tu yasitufikie na sisi! Hei..." mama Chande akasema hayo kwa huzuni.

Safari ya kwenda bafuni kuoga ikawa imekatikia hapo hapo, nami nikakaa kwenye mkono wa sofa pembeni yake Ankia na kutulia hapo kwanza. Maswali kadhaa yalipita kichwani kwangu, na sikuweza kujizuia kuhisi vibaya sana moyoni kutokana na tukio hili kunihusu mimi pia kwa njia fulani.

Nikakumbuka namna ambavyo Joy alikuwa akiongea kwa huzuni sana jana aliponipigia na mimi nikampa bega la baridi kwa kudhani alikuwa ananifanyia tu kituko kingine. Nikawaza kuwa huenda kwa njia kubwa nilisababisha kilichompata kitokee, kwa sababu nilichukulia vitisho vya mke wa Gonga kuwa hewa tu japo alionekana kuwa serious. Na sasa akawa amethibitisha kwamba hakutania. Aisee!

Nilijua kabisa kwamba ingekuwa ni yeye ndiye aliyefanya hayo, na kama haikuwa yeye, basi ningehakikisha nafanya utafiti wa ndani zaidi kujua ni nani aliyemwondoa mwanamke yule duniani.

Sehemu hii sasa ikawa imejawa na simanzi kutokana na hii ishu, nami sikusema lolote lile na kuendeleza utulivu wangu tu. Mama Chande akasema kwamba amesikia mapolisi walikuwa wanafatilia sakata hilo la mauaji ya Joy ili wawapate waliohusika, nami nikawa nimeingiwa na wazo lililonitia wasiwasi kiasi.

Tesha alisema kitu kuhusu mke wa Chalii Gonga kuwa mtu mwenye hila sana, na kama ilikuwa yeye ndiye amemuua Joy, uwezekano wa kuligeuzia suala hilo kwangu ulikuwepo. Si alikuwa anataka kunikomesha? Huwezi jua, ningeshangaa tu mapopo hao wanafika mlangoni hapo na kusema niko chini ya ulinzi kwa sababu mimi ndiyo muuaji!

Huyo mwanamke angeweza kunikamatisha kinamna hiyo kabisa kwa kutumia hila zake, na hili lilikuwa ni wazo la kutochukulia kirahisi hata kama uhakika wa mambo kwenda namna hiyo haukuwa wa asilimia mia.

Nikiwa bado nawaza mengi, nikasikia sauti ya mlio wa simu yangu kutokea chumbani, nami nikanyanyuka kwenda kuona mpigaji ni nani. Nikakuta ni Tesha, na baada ya kupokea, rafiki yangu huyo naye akawa amenipa taarifa za kifo cha Joy. Ila yeye kama kawaida yake ndiyo alikuwa na habari kamili.

Akaniambia kwamba Joy aliuawa maeneo ya kule Buza baada ya kuwa ametoka kwenye ile hoteli yake Chalii Gonga kwenye mida ya jioni kabla giza kuingia, sehemu ya mauaji hayo ikiwa ni kwenye ghetto lake lililokuwa maeneo ya huko huko. Nikamuuliza ikiwa alisikia kuhusu kuvamiwa kwake pale Kongowe, na alipokubali, nikauliza Kongowe alivamiwa akiwa kwa nani. Akasema alivamiwa akiwa kwenye nyumba isiyo ya kwake, ila hakuwa na uhakika sana ni ya nani.

Akaeleza kwamba alikisia hayo yote yalihusiana na suala la mke wa Chalii Gonga kujua kuhusu Joy kutoka na mume wake, naye akaeleza kwamba alihuzunika sana. Alikuwa anatamani hata afanye jambo fulani ili kulipiza kisasi kwa ajili ya kifo cha mwanamke yule, kwa sababu aliuliwa vibaya sana kwa kuchomwa na visu mara nyingi mno mwilini. Roho iliniuma.

Tukaagana na Tesha baada ya yeye kuniambia yupo njiani kurudi kutokea Tandika, na hakuwa ameniambia alikwenda huko saa ngapi wala kufanya nini kwa hiyo nikachukulia alikuwa na mambo yake tu mengine. Mimi kiukweli nilivurugwa mno na msiba huo. Nikawa hadi nashindwa kuacha kumtafakari mwanamke yule japo nilijitahidi kiasi kuondoa fikira zangu zote kwake.

Mpaka mama Chande na mwanaye walipoondoka, nikakaa na Ankia kidogo na kumsikiliza alipotoa maneno yake yenye kuonyesha huzuni kuelekea kifo cha rafiki yake, nami nikajitahidi kumbembeleza kwa upole mwingi. Hapa kilichokuwepo kwa Ankia hiyo kesho ilikuwa kwenda msibani ili kuwaunga mkono ndugu na marafiki zake Joy, na mimi pia nikamwambia ningekwenda.

Nikiwa nimeshatafakari mambo mengi kuhusiana na hali hii, nikawa nimejiweka vizuri kiakili ili nifanye jambo fulani ambalo lingesaidia kurudisha haki ya kilichompata Joy. Siyo kwamba labda nilijiona kuwa na hatia sana ama kama mpelelezi mahiri mno, hapana, bali ikiwa kama ni kweli mke wake Chalii Gonga ndiye aliyekuwa amehusika na suala hilo, nisingemwacha salama. Ningehakikisha analipia.


β˜…β˜…β˜…


Asubuhi ikafika. Niliamshwa mapema kwa sababu ya simu yangu kuita mara kadhaa, na baada ya kuichukua nikaona mpigaji kuwa Tesha. Baada ya kupokea, jamaa akaniuliza ni muda upi tungeenda pamoja na Mariam kumwona daktari huko hospitali, akisema kuwa dada yake alimwambia kuhusu suala hilo, na wakati huu Miryam alikuwa anamwandaa Mariam kwa ajili ya kwenda huko. Nikamwambia ni muda siyo mrefu ningefika hapo kwao ili tushughulike na jambo hilo, naye akakubali.

Kwa hiyo nikaamka na kuanza kufanya maandalizi. Nikaoga, nikavaa vizuri, hii ikiwa ni saa tatu kasoro, na mwenye nyumba wangu alikuwa chumbani kwake tu mpaka wakati ambao nilikuwa nimemaliza kuuweka mwili wangu safi.

Nikaona niende huko chumbani kwake kumwona, nami nikamkuta amejilaza tu kitandani kwake huku akionekana kuchat kwenye simu ama kusoma; alijua yeye. Nilielewa kwamba tayari alijua nimeingia, lakini hakuniangalia hata mara moja, akionekana kuwa makini kweli, nami nikamsemesha.

"Ankia... umeamkaje?"

Akanitazama usoni, naye akasema, "Kawaida tu. Unataka kutoka?"

"Ndiyo."

"Sawa. Nisamehe sija... sijachemsha chai...."

"Usijali, we' pumzika mpaka utakapojisikia kunyanyuka," nikamwambia.

"Unaenda wapi?"

"Natoka na Tesha kumpeleka Mamu hospitali," nikamjulisha.

"Aaa... sawa."

"Na wewe? Umepanga kwenda msibani mida gani?"

"Baadaye. Si na wewe utakuja?"

"Ndiyo, nafikiri Tesha ata...."

Kabla sijamaliza kumjibu, simu yangu ikaanza kuita, nami nikaitoa na kuangalia mpigaji kukuta ni Chalii Gonga. Nikakaza macho kwa umakini.

"Vipi?" Ankia akauliza.

Nikamwangalia na kusema, "Ee... labda nitakuja na Tesha. Tukishatoka hospitali. Sipajui kwo' kuja naye lazima... ngoja nipokee simu," nikamwambia hivyo.

Akatikisa kichwa kukubali, nami nikatoka chumbani hapo na kusogea mpaka kufikia mlango wa kuingilia sebuleni. Mawazo yakiwa ni mengi kichwani kutokana na kujua mambo mazito yaliyokuwa nyuma ya mtu huyu aliyenipigia, nikapokea na kuiweka sikioni.

"Oya dogo langu..." sauti ya Chalii Gonga ikasikika.

"Naam kaka..." nikaitika.

"Mbona nakutafuta sana lakini unanikaushia?"

"Mambo mengi tu. Vipi kwani?"

"Umesikia kilichompata Joy jana?"

"Ndiyo nimesikia."

"Unaweza kuniambia nini kinaendelea?" akaniuliza hivyo.

Nikakunja uso kimaswali kiasi na kusema, "Kwa nini uniulize mimi hivyo?"

"Nimeuliza tu... labda ukawa unajua kitu fulani..."

"Ah... sijui. Hilo jibu linatosha au?"

"Mhm... usipandishe jazba mdogo wangu..."

"Sijapandisha jazba. Ongea point yako," nikamwambia hivyo kwa sauti makini.

"Nimeanza kusikia Joy kapigwa hiyo juzi. Sijui unanielewa? Na alipopigwa, mtu wa kwanza kupigiwa ilikuwa wewe. Nataka kujua alitaka nini kutoka kwako... ama labda na wewe pia ulihusika kwenye hiyo ishu," akaniambia hivyo.

"Ishu gani? Kumpiga? Kwa nini nimpige Joy?"

"Ndiyo uniambie..."

"Nisikilize Chalii. Wewe si una watu wako? Fanya utafiti mwenyewe uujue ukweli, sawa? Kama unafikiri mimi ndiyo nimemuua Joy, thibitisha, halafu uje kwangu umlipizie kisasi. Sawa?"

"Mbona unaenda mbali sana? Mimi nataka tu kujua ukweli..."

"Ndiyo maana nimekwambia fanya uchunguzi. Ukikuta nimehusika... nifanye chochote unachotaka. Si alikuwa mtu wako? Utaamua mwenyewe cha kufanya. Nimemaliza. Kuna kingine?" nikamwambia hivyo kwa ujasiri.

Akacheka tu na kusema, "Usijali. Uchunguzi nafanya. Sikutaka kuamini ni wewe ndiyo umemuua Joy, ila nikikuta ni wewe... utajuta mdogo wangu."

"Ah... utajua mwenyewe. Hivyo vitisho vyote ungevitunza kwa ajili ya wahusika halisi na si mimi Chalii. Hapa unapoteza tu muda wako... na naomba usinisumbue tena," nikamwambia hivyo kwa kukereka.

Kabla hajasema lolote tena, nikakata simu na kushusha pumzi kwa nguvu. Kuna mtu aliyekuwa anazungusha mchezo huu wa mauaji ya Joy kunielekea mimi, na tayari nilijua huyo kuwa mke wake Chalii.

Hako kajinga kalikuwa kanataka kuniharibia wakati wangu mzuri niliokuwa nimekuja kujijengea huku, na kitendo cha Chalii Gonga kunipigia wakati huu na kuanza kutema vitisho ndiyo kilichochea kuni za moto kwenye nia yangu ya kutaka kupambana nao na kuwaangusha. Wote kwa pamoja walikuwa wameshanigeuza mimi kuwa adui yao, na ningewaonyesha urafiki mzuri wa kuwa adui yangu.

Nikaweka suala hilo pembeni na kutafuta namba za daktari fulani pale Muhimbili, kisha nikampigia na yeye akapokea. Daktari huyu alibobea kwenye masuala ya maendeleo na ukuzi wa ubongo, hivyo alikuwa ni mtaalamu wa mambo mengi yaliyohusisha kichwa. Tulijuana sana na ni moja ya walimu niliowahi kuwa chini yao wakati ndiyo niko kwenye mbio za kuwa daktari rasmi hospitalini pale (tunaita internship).

Nikamwambia kuhusu ishu ya Mariam, nikimwomba nafasi ya kuonana naye kwa asubuhi hii ili anipatie ushauri mzuri kuhusu hali ya "mdogo wangu," naye akaridhia. Akaniambia niende tu na nikifika nimjulishe hasa kama nisingemkuta kwenye ofisi yake, nami nikamshukuru kwa hilo. Oh na ni mhindi, kwa hiyo maongezi yetu yalibeba kimombo sanasana!

Nikaweka simu mfukoni baada ya kumalizana naye, nami nikaelekea nyumbani kwao Tesha. Sikuwa hata nimempa Ankia kwa heri nyingine tena maana nilihisi kuvurugwa kiakili kiasi, na baada ya kufika getini pale, nikaligonga na kusubiri lifunguliwe.

Dakika moja nyingi nalo likawa limefunguliwa, na sikuwa nimetarajia mfunguaji awe bibie Miryam mwenyewe. Nikatoa tabasamu hafifu kama kumpa salamu, naye akawa ananiangalia kama vile anasubiria niseme kitu fulani. Nikampa hilo.

"Za asubuhi dada?" nikamsalimu.

"Nzuri. Karibu," akaniitikia na kuachia uwazi zaidi ili niingie.

Nikapita na kuingia sehemu hiyo ya ndani ila nje ya nyumba yao, na nilikuta mama mkubwa mweusi, Bi Jamila, akiwa ameshikilia mpira mrefu wa maji uliounganishwa kwenye bomba hapo nje, akimwangalia maua yaliyotunzwa kwenye vyombo kuzungukia nyumba yao.

Mwonekano wa Miryam uliniambia kwamba bado, ama labda hakuwa na mpango wa kwenda kazini kwa leo, kwa sababu alikuwa ndani ya T-shirt nyeusi yenye mikono mifupi pamoja na khanga kutokea kiunoni, na nywele zake hakuwa amezitengeneza vizuri kimtoko; zikiwa na mvurugo kiasi wa kazi za asubuhi nadhani.

Nikasimama usawa wa gari lake na kumwamkia Bi Jamila. "Mama shikamoo?"

Akaniangalia na kuitikia, "Marahaba baba. Hujambo?"

"Sijambo. Naona unawaogesha watoto," nikamjibu.

Akacheka na kusema, "Ee wanangu hawa wanapenda kweli maji, kila asubuhi na jioni lazima waoge."

"Ni vyema. Hapo lazima wanenepe mno," nikamwambia kiutani.

Alipotabasamu kidogo, nikamwangalia Miryam na kukuta ananitazama kwa yale macho yake yenye udadisi fulani hivi, nami nikashindwa kujizuia kutabasamu na kuangalia chini. Hata sikujua sababu ni nini!

"Nini?" akaniuliza hivyo.

Nikatikisa kichwa kuonyesha kwamba hamna kitu, nami nikamtazama machoni kwa mara nyingine.

"Ingia ndani. Mariam yuko tayari ila anapaswa anywe chai kwanza. Tesha ndiyo bado hata hajaoga," Miryam akasema hivyo.

"Dah! Halafu kameniwahisha kweli, kumbe bado hata hajaamka!" nikasema hivyo kiutani.

"Nini? Nani?" akaniuliza hivyo.

"Mdogo wako, tumeongea muda si mrefu, nikadhani na yeye alikuwa tayari tayari. Kwa hiyo nakaa kuwasubiri," nikasema hivyo.

"Yeah... au unapotezewa wakati?"

"Hapana. Nataka nitumie muda wangu wote nitakaokuwa hapa kumsaidia Mamu... kwa hiyo yeye ndiyo mmiliki wa wakati wangu," nikamwambia hivyo.

Itikio alilotoa baada ya mimi kusema hivyo lilikuwa kunishusha na kunipandisha mara moja kama vile anajaribu kunisoma, nami nikatabasamu kidogo.

"Mbona unaniangalia hivyo?" nikamuuliza.

Akaachia tabasamu hafifu la kuhukumu fulani hivi, naye akanipita na kuanza kuelekea ndani ya nyumba. Nikajizuia kutotabasamu zaidi kwa sababu ni wazi kwamba mwanamke huyu bado aliniona kuwa mtu asiyeeleweka, labda sijatulia kiakili, huenda akiniona kama Tesha vile, na mimi nikaridhia tu kuwa angalau mambo baina yetu yalikuwa sawa.

Nikaingia ndani kwao na kumkuta Mariam, akiwa amekaa upande wa dining, na akipata kiamsha kinywa pamoja na Bi Zawadi. Mwanamama huyo akanisalimu kwa uchangamfu wake na kunikaribisha ninywe chai, nami nikashukuru na kusema nilikuwa sawa kabisa, kisha nikakaa sofani kumsubiri binti.

Miryam alikuwa ameenda chumbani nadhani, na hakutoka tena tokea aliponikaribisha ndani hapo. Tesha akaja kutokea upande wa bafuni, akiwa amevaa pensi ya kijani pekee, huku mwili wake ukionekana kulowana. Bila shaka ndiyo alikuwa ametoka kuoga, nasi tukasalimiana vizuri na jamaa kwenda chumbani kwake kuvaa nguo ili tuondoke.

Nilikuwa nikipata mazungumzo mawili matatu pamoja na Bi Zawadi kuhusiana na masuala ya dawa za kienyeji na za hospitali, na mwanamke huyo alionekana kupenda sana matumizi ya dawa za kienyeji zaidi ya za hospitali kwa jinsi alivyozisifia.

Nilimtazama Mariam kwa usomi mwingi alipokuwa akila, nikiona jinsi alivyofurahia kupata chakula kwa njia kama ya mtoto mdogo. Akawa ameshiba, Bi Zawadi akamsaidia kunawa, kisha wakaja upande wa masofa hapo sebuleni na kukaa.

Binti alikuwa akionyeshwa mimi ili anisalimie, lakini akawa anaangalia chini tu kama hataki. Nilielewa kwamba bado hakuwa amejenga uzoefu kwangu, na njia ya kwanza ya kufanikisha kumsaidia vizuri ingenihitaji nijenge mazoea naye ili akishaweza kujiachia zaidi kwangu, ndiyo nianze kumwekea tiba akilini.

Wakati ambao Bi Jamila ndiyo alikuwa amerudi kutoka kumwagilia maua yake, Tesha naye akawa ametoka chumbani, akiwa amevaa vizuri sana, naye akamwita dada mkubwa ili apewe funguo za gari. Nikamwambia isingekuwa mbaya tukichukua usafiri tu maana bila shaka Miryam angehitaji gari kwenda kazini, lakini akasema ni yeye Miryam mwenyewe ndiye aliyetaka tuchukue pickup yake ili twende hospitali na Mariam akiwa ndani ya gari lisilo na purukushani nyingi. Upendo wa dada.

Kweli Miryam akawa ametoka na kumpa Tesha funguo, naye akamsihi mdogo wake awe makini sana na Mariam mpaka tutakaporudi. Nikamuuliza Miryam angekwendaje kazini, naye akasema angechukua usafiri. Basi kwa kuwa mambo yalionekana kunyooka kwa sehemu hiyo, tukatoka kwa pamoja, Mariam akaingia siti za nyuma ya gari, Miryam akafungua geti, nasi tukaingia mbele ya gari na Tesha kulitoa nje.

Niliona jinsi gani Mariam alimpenda sana dada yake, kwa kuwa aliweka uso wake kwenye kioo huku akimtazama sana huko nje kana kwamba ni mtoto asiyetaka kumwacha mama yake, nami nikaweka hilo akilini ili nije kulitumia katika msaada niliotaka kumpatia. Kila jambo lingekwenda taratibu tu mpaka ningehakikisha huyu binti amekaa sawa tena.

β˜…β˜…

Vuuu, mwendoni kuelekea hospitali. Gari hili lilikuwa modeli ya zamani ya manual kwa hiyo kulikuwa na gia ya kusukuma na kurudisha nyuma karibia kila dakika, na Tesha alitia mbwembwe kweli kwenye kuendesha ili kunionyesha kwamba alijua sana. Na alijua. Alikuwa dereva mzuri.

Nikamwangalia Mariam nyuma na kumwona akiwa ameshika simu ya Tesha akitazama katuni ambazo kaka yake alimwekea ili binti atulie, nami nikamtazama rafiki yangu.

"Oya unaona navyoweka vitu hapa?" akaniambia hivyo kwa kujisifu.

"Naona. Miryam ndiyo alikufundisha kuendesha?" nikamuuliza.

"Hamna, nimejifunzia Arusha. Miezi miwili tu Veta nikatoka nimeiva," akasema.

"Aaa sawa."

"Na wewe mtoto wa kishua? Unajua kuendesha?"

"Ahahah... ndiyo, najua."

"Ulijfunzia chuo gani?"

"Hamna, me sikujifunzia Veta wala popote. Nilichukua tu gari la mtu nikaanza kuendesha mwenyewe mpaka nikaweza..."

"Aa wewe... unazingua..."

"Kweli tena."

"Una leseni?"

"Ee."

"Uliitolea wapi sasa kama hukwenda chuo?"

"Ahahahah... shortcut tu. Yaani me nimeweza gari mdogo, nilipofika legal age nikamtafuta askari mmoja wa usalama barabarani... hadi nilishamsahau jina ila, yaani, yule ulikuwa unampa hela tu anaenda anakutengenezea leseni, fwii unaingia barabarani," nikamwambia.

"Kweli eh? Nishagasikia wanafanya hivyo ila siku hizi sidhani sana maana kuna kushikwa kwingi..."

"Ee, ndiyo hivyo. Me nilipita nayo namna hiyo."

"Ulikuwa unatoa shi'ngapi?"

"Kwa ajili ya leseni? Laki tatu tu."

"Laki tatu tu, au siyo? Kama buku tatu yaani..."

"Wee, nilihangaika kuipata! Hata kipindi hicho mambo hayakuwa easy sema ukishajuana tu na watu si unajua vichochoro vinajinyoosha..."

"Ahehehe... mwana me napenda sana hizi manual. Kucheza hapa mbele nakubali mno, yaani auto zinakera, unaweza hata ukanyoosha miguu hapa juu maana nyepesi mno," aksema hivyo.

"Na dada yako anapenda za hivi eh?"

"Da' Mimi? Sijui sana. Hii ni ya kuenzi tu unajua? Angeweza hata kuiuza na kuchukua nyingine ila anapenda mno kutunza kumbukumbu," akaniambia hivyo.

"Unamaanisha nini?" nikamuuliza.

"Hili lilikuwa gari la baba," akaniambia hivyo.

"Aaa..."

"Eee, walikuwa tight sana na da' Mimi."

"Sawa. Inaonekana ya zamani, lakini anajua kutunza."

"Ina muda. Sema mzee alipoenda, Miryam akaichukua. Sa' siunajua ye' mrembo kwa hiyo na gari lazima itarembwa tu hata kama ishazeeka," akasema hivyo.

Nikacheka na kumwambia, "Kweli. Hivi... yule jamaa, Joshua, umeshamwona tena?"

"Toka walipomwachia? Sijamwona. Wa kazi gani kwanza? Akae huko huko, next time akileta bangi zake nitamtoboa kabisa..."

Nilikuwa nimekumbuka namna ambavyo huyo Joshua alimtukana Miryam siku ile kuhusu mwanamke huyo kutumia gari hili aliloliona kuwa la kizee, na sasa baada ya mimi kuelewa kwa nini mwanamke huyo alilitumia, kweli kashfa za jamaa zilizidi kuonekana kuwa mbaya sana.

Lakini kitendo cha kumwona jana ofisini kwake Miryam akijionyesha kuwa mtakatifu na sasa Tesha kuonekana hajui kuhusiana na hilo, kilifanya nielewe kwamba kuna jambo lililokuwa likiendelea ambalo kijana huyu, labda na familia yao wote kwa ujumla, walifichwa kwanza, kwa hiyo nikaona nisimwambie kuhusiana nalo. Bila shaka dada yake alikuwa anapanga mambo fulani bila kuwaambia wengine, ama huyo Joshua alijipeleka huko kazini kwa Miryam yeye mwenyewe. Ningeona.

"Tuachane na habari za huyo mjinga. Oya, hivi... hii ishu ya Joy mwanangu unaionaje?" akaniuliza hivyo.

Nikawa makini zaidi na kusema, "Iko hivyo tu. Kauliwa... labda shauri ya yale mambo uliyoniambia."

"Yale yake na Chalii Gonga, au ile ishu nyingine?"

"Ishu gani?"

"Acha kujitoa akili JC. Mke wake Chalii si kakuita ile juzi kukutisha eti atafanya kitu kibaya, halafu kweli kimetokea. Hujahisi labda ni yeye?"

Nikamwangalia Tesha. Kijana alikuwa na akili nyepesi, lakini nikamwambia, "Huwezi kuwa na uhakika. Labda tu tuyaache jinsi yalivyo."

"Dah! Me naacha kwenda Masai kwa wiki kabisa. Nisije kujikuta naamkia motoni kesho tu. Sijasema mbinguni maana najua nishakataliwa huko," akasema hivyo

Nikacheka kidogo na kusema, "Kweli kaka, hilo ndiyo la muhimu kufanya. Jiweke kushoto kabisa."

"Fact," akasema hivyo.

Mawazo yake Tesha kuhusiana na jambo hilo yalifanana na ya kwangu, lakini sikutaka kuchangia sana upande wa mawazo yangu kwa sababu sikuhitaji kijana huyu avutwe kiundani zaidi kwa yale niliyofikiria kufanya. Ndiyo, bado nilikuwa na mpango wa kumtafutia haki Joy endapo kama kweli mke wake Chalii alihusika na kifo chake, lakini nilitaka Tesha akae pembeni kabisa na suala hili. Ingekuwa bora kwa ajili yake.

β˜…β˜…

Kwa hiyo mwendo wa kupita robo tatu ya saa kuelekea Muhimbili ukatufikisha hospitalini huko, nasi tukaelekea majengoni baada ya kuegesha gari. Sikudhani ningekuja kurudi hospitalini hapa mapema namna hiyo, yaani baada ya kuingia tu kwenye siku za likizo, lakini Mariam aliustahili umuhimu wa kilichofanya nirudi tena hapa.

Kwa kuwa tayari nilikuwa nimeshawasiliana na yule daktari, nikampigia simu tena kumjulisha kwamba tulikuwa tumefika, lakini hakupokea. Ah nikaona tu nitulie mpaka tukifika ofisini kwake, labda kwa sasa alikuwa bize kidogo. Lakini hazijapita sekunde nyingi akawa amenipigia na kusema kwamba niende tu moja kwa moja mpaka ofisini kwake, alikuwepo huko, maana hakusahau kuhusu ujio wangu. Hiyo ikawa imeenda!

Tulipita majengo ya chuo cha Muhimbili na aisee! Watoto! Kuna wanawake warembo ukanda huo wa wanavyuo mpaka Tesha alikuwa anashindwa kujizuia kuwaangalia. Hasa wale weupe wavaa shungi! Lakini hakuonekana kuwa na shobo za kishamba kama wanaume wengine wanavyokuwaga, na kwa hilo nilimkubali sana.

Ujio wangu kwa sehemu hiyo kama kawaida ulivuta macho ya baadhi ya watu walionifahamu na wasionifahamu, na wale walionijua wangenipa salamu kwa kupunga mikono na mimi pia kuwarudishia.

Mariam alikuwa amependezeshwa kiasi na dada yake isingekuwa rahisi kwa yeyote aliyemwona kwa mara ya kwanza kudhani ana tatizo kwenye akili yake. Alitembea kwa ukaribu sana na Tesha, akiung'ang'ania mkono wake ili asijikute anapotea kwenye mazingira hayo mapya kwake, na kwa kweli hiyo ilionyesha kwamba alijua dunia ni mbaya, na si kila mtu angepaswa kumwamini zaidi ya yule aliyejua angeweza kumwamini.

Kwa hiyo tukasonga mbele zaidi, tukipita majengo ya kantini, majengo ya vyumba vya madaktari, mpaka kufikia upande wa hospitali yenyewe. Kama kawaida watu walikuwa ni wengi, na kama isingekuwa ya mimi kuja na ndugu hawa basi wangekaa mno kusubiri, lakini nikawapeleka moja kwa moja mpaka kwenye ofisi ya yule daktari na kusimama nje ya mlango wa kuingilia ndani hapo.

Nikawaomba wanisubiri kwanza, kisha nikaingia na kumkuta daktari huyo akiwa na mgonjwa mwingine hapo. Alionekana kumjazia ripoti fulani, na baada ya kuniona, akatabasamu kiasi na kunisalimu. Nikamsalimu pia pamoja na huyo mgonjwa, kisha nikasimama pembeni kusubiri.

Daktari huyu aliitwa Roshan Sotto, naye alikuwa mtu mzima karibu kufikia kama miaka 60 hivi. Alipomaliza kuandika ripoti ya mgonjwa wake, akampa maelekezo fulani, kisha mgonjwa huyo akaipokea karatasi na kunyanyuka ili aondoke. Alipotoka ndiyo nikapata sasa nafasi ya kuongea na daktari mwenzangu, akiuliza naendelea vipi huko nilikokuwa nimeenda.

Mimi nikamwambia niliendelea vizuri tu, naye akasema kiukweli nilikuwa nimetia pengo fulani hapo hospitalini kwa kuondoka, akinitania ni namna gani muuguzi mmoja wa kike hapo hospitalini aliyeitwa Latifah alivyonitafuta sana. Si unajua sikuzote lazima uwe na yule mtu anayekupenda sana kazini mpaka unabambikiziwa ndoa ya kiutani pamoja naye? Ndiyo alikuwa huyo Latifah sasa.

Karibia kila mtu aliyenifahamu hapa hospitali aliniita mimi na Latifah mume na mke. Tulizoewa namna hiyo. Kwa hiyo daktari Roshan aliponikumbusha kumhusu, nikacheka sana na kumwambia kwamba nilijitahidi kuingia tena huku kisiri ili asinione maana kama angeniona ndiyo angening'ang'ania mpaka basi.

Baada ya kuweka utani pembeni, daktari mwenzangu akaniambia sasa nimlete mgonjwa wangu ili amcheki haraka, nami nikamfata Tesha na Mariam pale nje. Wakaingia na kukaa kwenye viti kutazamana na daktari Roshan, mimi nikiwa nimesimama, na baada ya utambulisho wa ndugu hawa wawili, Tesha akaombwa aelezee hali ya mdogo wake ilikuwa vipi. Akaeleza kila kitu kwa namna nilivyofahamu pia, naye daktari Roshan akajaribu kumsemesha Mariam.

Binti hakujibu hata mara moja, nami nikamwambia daktari kwamba kutokana na namna ya Mariam ya kuitikia kwa vitu fulani na dalili kadhaa alizozionyesha, nilifikiri alikuwa na tatizo lililofanana na ASD, na ndiyo nilikuwa nimekuja kupata uhakika kutoka kwake ili apendekeze tiba sahihi zaidi ya kumpa. Na nilikuwa natumia kiingereza.

Daktari Roshan akanyanyuka, akafata kifaa fulani cha kielektroni kwenye chumba cha pembeni ndani humo humo na kumfata Mariam, kisha akamvalisha kichwani na kuanza kusoma namba-namba na maherufi-herufi. Alikuwa akimpima, na baada ya kumaliza, akamtolea na kurudi kukaa kwenye kiti chake.

Akamuuliza Tesha, "Huyu mdogo wako, amekuwa hivyo kwa muda gani?"

Tesha akasema, "Ni... miaka kama mitatu na miezi kadhaa. Inaelekea miaka minne."

Daktari Roshan akasema, "Sawa. Sasa ni hivi... aam, utasamehe na Kiswahili changu, ila si kibaya sana..."

Nikatabasamu kidogo, naye Tesha akasema, "Haina shida doctor."

"Her brain isn't damaged... aah... ubongo wa Mariam uko sawa... kabisa, hakukuwa na kitu kama... uvimbe au shimo dogo kutokana na ugonjwa, ama accident... ajali, kwa hiyo bila shaka... alikuwa na tatizo kwenye... mishipa midogo iliyosawazisha taarifa kwenye ubongo wake..." daktari akaelezea.

Aliongea kwa kutumia kauli za wakati uliopita lakini sote tulielewa alimaanishia wakati huu aliotoka kumpima binti, na alielekeza maneno hayo kwangu. Nikatikisa kichwa kuonyesha uelewa.

Akaendelea. "Yaani... kwa wakati huu mishipa hiyo haikuweza kusawazisha... vizuri... taarifa mbalimbali ubongoni mwake, na... ni kweli... tatizo lililompata lilifanana na ASD."

"ASD ndiyo nini? Au... utanielezea baadaye JC?" Tesha akaniuliza.

"Yeah, nitakwambia. Ngoja nimuulize kuhusu tiba. Kwa hiyo doctor Rosh... what approach should be taken towards her treatment?" nikasema hivyo.

"It depends. Matibabu kwa ajili ya ugonjwa... wa ASD, yanalenga kupunguza... dalili zilizoingilia utaratibu mzuri wa kuishi au kutenda kwa njia kawaida... mtu aliyeathiriwa. ASD inawapata na... kuwaathiri watu... kwa njia tofauti, hiyo ilimaanisha kwamba waathiriwa hawawezi kuonyesha dalili zilezile... so... na njia za kuwatibu... haziwezi kufanana. Unaelewa... Tesha?" daktari Roshan akamuuliza hivyo.

"Ndiyo doctor," Tesha akajibu.

"Yes. Matibabu hayo ya ndani... tabia, maendeleo ya kiakili, kielimu, psychology, mazungumzo, na vitendo. Yanaweza kumix kwa... kwa pamoja... ama kukazia fikira kimoja tu kati ya hayo, ikitegemea na hali ya mwathiriwa. Kwa hiyo cha msingi kufanya kwa ajili ya binti huyo... ingekuwa kuangalia nini... kinavuta zaidi akili yake, kisha kutafuta njia za kumfanya akaze fikira... zake... kuzungukia kitu hicho... au vitu hivyo, ili ubongo wake... urudi kwenye ukuzi mzuri wa awali..."

Ah, blah blah blah kutoka kwa daktari mwenzangu zilikuwa nyingi sana, lakini nilielewa zaidi sasa kwamba Mariam angehitaji vitu viwili tu kwenye jambo moja; michezo ya kiakili, na mafundisho ndani ya hiyo hiyo michezo ya kiakili. Ningeweza kujua tayari alipenda mambo yapi yaliyoichezesha vyema akili yake, kwa hiyo ningeyatumia hayo hayo kwa njia ya kidaktari zaidi ili akili yake itiki.

Daktari Roshan alieleza kwamba kwa jinsi hali yake Mariam ilivyokuwa, angehitaji msaada wa kitaalamu kutoka kwa wataalamu ambao wangemwangalia kwa ukaribu. Hii ingemaanisha akae sehemu fulani hususa mbali na kwao, kama tu wodi za vichaa, lakini ya peke yake, na nilijua hiki ni kitu ambacho dada yake asingekubaliana nacho; achilia mbali tu na gharama ambazo zingehitajika kuwalipa wataalamu hao.

Kwa hiyo nikiwa na uhakika wa mambo ya kufanya sasa kutokea hapo, nikamshukuru tu daktari huyu na kumwambia tungeshughulika vyema kumpatia msaada binti huyo ili kusaidia hali yake irudi kuwa sawa tena, nasi tukamuaga upesi ili aweze kuangalia mahitaji ya wagonjwa wengine waliokuwa wakimsubiri.

Hivyo tukaondoka hatimaye sehemu hiyo ya hospitali, ikiwa ni mida ya saa sita kasoro sasa, nami nikawa natembea pamoja na ndugu hawa wawili kuelekea nje huku nikimwelezea Tesha vitu alivyotaka kujua.

Tesha kiukweli bado alikuwa haamini-amini ikiwa mimi nilikuwa daktari, maana aliniona kuwa wa aina ya kihuni zaidi, lakini nikamwambia hata madaktari huwa wana maisha mengine bwana. Na mimi nilikuwa nimeishi maisha mengi. Kwa hiyo baada ya kuwa ameelewa vizuri hali ya mdogo wake, akasema angesaidia pia katika chochote ambacho ningefanya kuipa akili ya Mariam "boost," yaani kuibustisha.

Nikawaongoza ndugu hawa wawili kuelekea kwenye jengo la maabara moja hospitalini hapo, nami nikamwomba Tesha anisubirie nje kwa ufupi tulipofikia mlango wa kuingilia ndani hapo. Nikaingia maabarani, kukiwa na vifaa vingi vya matumizi ya vipimo vya masuala ya kisayansi, nami nikamkuta mwangalizi wa sehemu hiyo ambaye ndiyo nilikuwa na lengo la kumwona.

Huyu hakuwa mwingine ila mwanadada Latifah, mke wangu wa hospitali. Yeye ndiyo alikuwa msimamizi kwa sehemu hii na kwa sababu nilikuwa na nia ya kupata vitu fulani kutoka kwenye maabara hii, kuonana naye ilikuwa lazima. Kama ingekuwa ni ndani ya uwezo wangu basi ningefanya kila kitu kumkwepa kabisa maana nilijua kama angeniona ndiyo angening'ang'ania mno, na sikuwa nimekosea.

Aliponiona tu ndani hapo, akaacha mambo aliyokuwa anafanya na kunifata kwa kasi huku akifurahi mno, naye akanikumbatia. Alikuwa mweusi wa maji ya kunde, mwembamba kiasi na mwenye miguu mirefu iliyoupa mwili wake umbo la umiss maridadi. Alikuwa na midomo minene na mizito kama vile iko tayari kudondosha udende muda wowote.

Ijapokuwa tulikuwa tumebambikiziwa ndoa ya kiutani hapa hospitalini, mimi na Latifah tulikuwa tumeshafanya michezo mingi sana kwa sababu alinielewa mno. Kwa wengine tulijionyesha kuwa wapenzi wa kikazi tu, lakini nilikuwa nimeshampigisha kazi nyingi sana huyu mwanamke kiasi kwamba alitamani hata nimuoe!

Kwa hiyo hata na hapa akaanza kudeka kwangu, akisema amenimiss, akiniambia mimi mbaya, nimeondoka bila kumuaga ili nimkimbie na niende kwa wanawake wengine. Nikamwambia hapana, ni mambo mengi tu yalikuwa yameingiliana na hata laini ya mtandao niliyokuwa natumia kuwasiliana naye awali ilikuwa imepotea kwa hiyo namba yake ilipotea pia nilipoingia likizo, lakini nilimmiss pia ndiyo maana nikaja wakati huu. Hizo zote zilikuwa fix tu.

Tukajuliana hali, kisha nikamweleza lengo langu la kuja hapo. Nilihitaji vifaa vichache vya maabara pamoja na kemikali kiasi za kugawanyisha virutubisho vya madawa, naye akaniuliza vya kazi gani. Nikamwambia kuna dawa nilikuwa nataka kutengeneza, na singechukua muda mrefu sana na vifaa hivyo ningevirudisha.

Akakubali ila akaniomba nimjali kidogo kwanza, unaelewa, lakini nikamwambia haingewezekana maana kuna Serikali ilikuwa inanisubiri hapo nje, lakini akasisitiza tu na kutaka kunibusu mdomoni. Nikamzuia, nikimkumbusha kwamba kuna CCTV camera humo, lakini akaendelea kufosi.

Alikuwa mkaidi kweli, lakini mara zote alipoona niko makini alitulia, na mimi nikamwonyesha kweli kwamba sikuwa na muda wa kufanya kile alichokuwa anakitaka. Nikamwambia kama hataki kunipa basi tu mimi niondoke, ndiyo akashusha makeke na kunituliza. Akanifatia vifaa hivyo, naye akaniwekea kwenye mfuko na kuniletea.

Latifah alikuwa mwanamke aliyezoea watu upesi sana na hapa hospitali alipendwa mno mpaka na wasimamizi wa majuu kutokana na utu wake wa kirafiki, kwa hiyo alijiachia sana kwa mambo mengi aliyofanya japo si kwamba alikuwa binti mapepe. Nasema hivyo kwa kuwa baada ya yeye kunipa vitu nilivyohitaji, akaanza kunipiga busu mdomoni bila kujali uwepo wa CCTV camera, nami nikamwambia awe makini asije kusababisha akajikuta anafutwa kazi kwa sababu ya kuchanganya kazi na starehe.

Akasema hiyo haiwezi tokea kamwe, naye akaniomba namba zangu za sasa ili tuanze kuwasiliana tena. Wala hata sikuwa nimepoteza laini na chochote bali nilikuwa nimempiga tu block ili wakati wa likizo uwe wa mambo mengine, lakini sasa nikawa sina jinsi. Nikampa namba ya laini nyingine, kisha ndiyo nikamuaga na kurudi kwa wenzangu.

Tesha na mdogo wake walikuwa wamesimama kwenye kingo ya pembeni karibu na ngome zilizoshika ukuta, nami nikamwambia nilikuwa nimepata nilivyovitaka kwa hiyo tuondoke hapo hatimaye. Hakuwa na habari yoyote kuhusu mimi kukutana na mke wangu wa kubambikiziwa, nasi tukaendelea tu kuongelea mambo mengine kadiri tulivyoelekea upande wa kutokea kwenye hospitali.

Tulipokuwa tumefika eneo lenye zile kantini, nikawaongoza ndugu hawa kwenye kantini moja ili tupate chakula chepesi. Nilihisi njaa kiasi na hata Tesha hakuwa amekunywa chai pia, kwa hiyo nikaagiza na kuwaagizia ndugu hawa msosi mtamu, nasi tukala kwa pamoja.

Kila mara ambayo Tesha angeona pisi kali zilizoelekeza umakini wao kwetu, angenibonyeza ili kunionyeshea bila yeye kufanya ionekane wazi kwamba ameukamata umakini wao, nasi tungeongea mengi kuhusiana na namna ambavyo wanawake wa chuo waliishi kihalisi tofauti na jinsi ilivyookekana waliishi. Wanaojua maisha yao wanaelewa, hata mimi niliyaona pia!

Mariam alipenda sana vyakula vitamu kama chips mayai na kuku, na alikula bila kujali nani anamwangalia. Midomo yake iling'aa mafuta kumfanya Tesha amfute kila dakika kwa tishu, na nilipenda sana kautoto alikokuwa nako huyo mwanadada. Ila ndiyo ningepaswa kumsaidia kukaondoa ili kasiteke maisha yake yote mpaka mwisho.

β˜…β˜…

Tulipomaliza kula na kujisafisha, tukaondoka hospitalini hapo hatimaye. Mwendo ungekuwa mmoja tu wa kuturudisha nyumbani ili Mariam akapumzike, na Tesha alikuwa analalama kuhusu kuondoka bila namba ya pisi yeyote wa hapo Muhimbili. Nikamwambia wa huko wangemsumbua tu kwa kumnyonya mno hela mpaka angekauka.

Lakini malalamiko yake ya kutaka pisi kali yakanifanya nikumbuke kitu fulani. Winny. Mmoja wa wale wadada niliokutana nao kwenye bajaji jana. Na nilikuwa nimemsahau kabisa maana mambo mengi yalikuwa yameingiliana. Nikamwambia Tesha kuhusu mwanamke huyo, nikisema ni mzuri na nilichukua namba yake.

Masikio yakamsimama jamaa akinitaka nimpatie, lakini nikamwambia atulie kwanza; mpaka nimtafute Winny mwenyewe, nimpange kuhusu rafiki yangu, halafu ikiwezekana niwakutanishe. Jamaa akakubali hilo huku akitaka nimhakikishie kwamba kweli huyo mwanamke alikuwa mzuri, nami nikamwambia nisingechukua namba yake endapo kama angekuwa wa ovyo.

Tukiwa tumekaribia kuifikia Mbagala, simu yangu ikaanza kuita. Mpigaji? Soraya. Tabasamu hafifu likaniponyoka, na sikuwa na mpango bado wa kumwambia Tesha lolote kuhusu mimi na yule mwanamke, lakini jicho la mwewe la jamaa likaona jina la huyo Mamacita hapo akinipigia, naye akaanza kunisema sasa.

Nikamwambia acha zako wewe, huyu anapiga kunisalimia tu, nami nikapokea na kumsikiliza mtoto mzuri. Alinijulia hali, akaniambia yuko kazini, na alitaka tuje tukutane tena. Yaani leo leo, maana kama tu msemo aliokuwa ametumia jana, ni kwamba bado "aliwashwa."

Sikujibu kauli zake za kimapenzi moja kwa moja, lakini kitendo cha mimi kusema kwa leo haitawezekana maana nilibanwa na mambo mengi, kikafanya Tesha ashtukie dili. Nikamwambia tu Soraya ningemtafuta baadaye maana hapa nilikuwa na mpango wa kuelekea kwenye msiba wa rafiki, naye akaridhia. Na alikuwa anataka kweli tuonane huyo mwanamke, lakini mie wala sikuwa na presha.

Baada ya mazungumzo pamoja na Soraya, Tesha akaanza kunichokoza sasa. Alitaka kujua. Ajue, ajue, ajue! Nikamwambia dogo tulia, Soraya anataka tu tuelekee kule kwenye mambo zetu lakini mimi nampiga chenga, ila Tesha hakutaka kukubali. Na akasema haina shida, mimi hata nikimficha, angejua tu. Alinifurahisha sana maana alikuwa na akili nyepesi na mwingi wa maneno, na mimi bado sikutaka tu kumwambia kuhusu jambo langu na Soraya ili asiwe na makeke mengi.

Kwa hiyo baada ya dakika kadhaa kupita kutokea hapo, tukawa tumefika Mzinga hatimaye na kuendelea kuelekea nyumbani, huku tukiwa tumeshaongelea suala la kwenda Buza kwenye msiba wake Joy. Kwa kuwa tulikuwa tumekula kule hospitali, hapo ilikuwa ni kumwacha tu Mariam nyumbani kisha sisi tugeuke tena; uzuri leo Miryam alikuwa amemwachia mdogo wake gari.

Lakini tulipofikia eneo la Masai, nikamwambia Tesha anishushie hapo kwanza. Akaniuliza nilitaka kwenda kunywa bia au, nami nikamwambia hapana, kuna deni nilikuwa naenda kulipa hapo, hivyo yeye ampeleke mtoto nyumbani kisha akigeuka atanikuta hapo ili tuondoke. Hakuwa na neno. Nikashuka, kisha nikaanza kwenda kule ndani kwenye bar.

Hii ikiwa ni saa saba mchana, bado Masai ilikuwa imetulia, kukiwa na watu watatu tu walioonekana kukaa na kunywa pombe, ikiwa wazi kwamba hata muda wa jirushe haukuwa umefika. Lengo langu kuja huku lilikuwa kumtafuta Bobo, nami nikawa nimemwona.

Mwanaume tolu, asiyeonekana kuwa na figisu za kijinga, Bobo alikuwa amesimama usawa wa kaunta akizungumza na wanawake wadogo wawili, bila shaka wahudumu wa hapo. Alikuwa akiwapa maelekezo sijui, na aliponiona, akanipa ile salamu yake ya uchangamfu ah nakuona mchina!

Nikatoa tabasamu hafifu na kuwasalimu wale wanawake, nao wakaitikia na kuendelea kunitazama. Bobo akaanza utani wake, akimsukumia mmoja kwangu na kusema kama nikitaka basi anilipie chumba hapo kwenye lodge ya Masai ili nikamtandike, lakini nikacheka tu na kumwambia ni yeye ndiye aliyefanya nikaja hapo. Nilitaka tuongee kibinafsi, na kwa hilo akasema hamna noma.

Tukasogea pembeni kabisa na kusimama kwa ukaribu.

"Oy, si unajua kilichomkumba Joy?" nikamuuliza.

"Ee, najua. Dah mwanangu! Wamemchana vibaya yaani! Wanaingiza vipisi kwenye jeneza. Inatisha kinyama," Bobo akasema.

"Dah! Kwa hiyo... utaenda msibani?"

"Nitaenda kuchungulia tena. Unajua... nilienda kuona tukio baada tu ya kusikia na... mambo kule hayaeleweki. Huo mwili wake wenyewe ungetakiwa kuachwa kwa mapolisi huko, lakini wameona waipe tu familia yake heshima ili uzikwe. Mwanangu, Joy hakuwa wa kufa kihivyo... tukiwapata waliomuua, hata mimi nitachangia kuwachinja..."

"Labda ni masuala ya makundi, si unajua? Ikiwa kuna kundi linalopingana na kundi la Chalii labda kumuua Joy ilikuwa kukomoana..."

"Ah mwana una akili! Umekuja juzi tu tayari umeshaotea hivyo..."

"Nimeshaona mengi."

"Ee, inawezekana masuala ya makundi. Sijui sana, ila... maneno ni mengi, si unajua? Maaskari wanaweza kuja hadi hapa kuipekenyua Masai wakijua Joy alipenda kutimkia na huku, kwo' tumejiweka sawa pote hapa ili hiyo ikitokea maelezo yanyooke. Sijaelewa undani wa kilichompata ila... Chalii na yeye anawatafuta hao mbwa wal'omuua. Si unajua alikuwa demu wake?"

"Najua."

"Ndo' hivyo. Amepanga fanya kitu mbaya akiwanasa. Me nasubiri mchezo tu," Bobo akasema.

Nikatulia kidogo kutafakari mambo. Aidha Bobo alijua ama hakujua kwamba Chalii Gonga alinishuku mimi pia mpaka kunipigia simu leo kunitisha, lakini hicho siyo kilichokuwa kimenileta hapa.

"Wewe unaenda huko?" akaniuliza.

"Ee, ndo' tunaenda sa'hivi na Tesha," nikamwambia hivyo.

"Aaa, isingekuwa ya biashara na mimi ningeunga. Ulikuwa umekuja kunipitia?"

"Hamna. Nilikuja kwa sababu... nataka tuwe washkaji Bobo. Tight yaani. Nimekuangalia... nimekusoma... wewe uko poa sana. Japo uko upande mbaya lakini naona unajua upande sahihi wa mambo ni upi," nikamwambia.

"Ehehe... sikuelewi mwanangu, sijui ndo' unaongea nini," akasema hivyo.

Nikacheka kidogo na kusema, "Nataka unisaidie kitu, lakini iwe baina yetu."

"Nambie kamanda... usikonde," akasema.

"Una namba za mke wa Chalii?"

"Mke... Bertha?"

"Yah."

"Aaaa... kumbe!" akasema hivyo.

Nikatabasamu kidogo.

"Ah! Mwanangu umezunguka kichizi. Si ungesema tu?"

"Ndiyo nimekwambia sasa."

"Ah, maji laini mbona? Unamkubali eh?"

"Sana. Sema shida... kama unavyojua..."

"Ah... wewe Chalii asikuumize kichwa. Sikiliza nikwambie. Huyo manzi huwa ni mtata, lakini we' kama mjanja pale unaingia vizuri mbona? Halafu tena wewe... yaani yule unakula mapema. Si ile juzi alikuita ye' mwenyewe hapa?" Bobo akasema.

"Mh! Habari zinasambaa haraka!" nikasema.

"Hahaha... watu tuna macho. Yaani wewe Chalii asikupe presha wala, usimwogope. Namba nakupa... ukitaka huyo mutoto unakula vizuri sana... ila uende na swaga zilizonyooka, maana..." akasema hivyo huku akitoa simu.

"Anaweza akazingua, namwelewa. Usihofu. Najua pa kumtekenyea. Sema tu Chalii asijue, au siyo?"

"Uhakika. Ila ukim(.....) chukua video uje unionyeshe. Nataka kuona kama ana mabaka au ngozi ya tembo!" Bobo akasema hivyo.

Nikacheka kidogo na kutoa simu yangu, nami nikaanza kuandika namba ya mwanamke yule na kisha kuitunza. Nikabadilishana namba na Bobo ili tuwe tunawasiliana pia, naye akanisevu kama alivyopenda kuniita, "Mchina."

Ilikuwa sawa kwangu kuigiza kwa Bobo kwamba nilimtaka kimapenzi huyo Bertha ili anipe namba yake, na nilipeleka maigizo haya mbali kwa kufanya ionekane kuwa nilimhofu sana Chalii, lakini nilikuwa na lengo lingine kabisa kwa kufanya haya yote. Baada ya kuwa nimeipata namba, sasa ingekuwa ni kula sahani moja na huyo Bertha.



β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…

ITAENDELEA

β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…

Full Story WhatsApp or inbox

Whatsapp +255 678 017 280
 
MIMI NA MIMI

A Story by Elton Tonny

Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Tamaa, Hila, Usaliti, Siri, Mambo Yasiyotazamiwa

R-rated 18+

Enjoy!


β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…

SEHEMU YA KUMI NA TANO

β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…


Nikatoa elfu kumi na kumpatia Bobo ili apige pombe mbili tatu, naye akaonyesha kukubali sana pigo zangu na kusisitiza nisije kusahau kuchukua mkanda wa video nikifanikisha kumvua nguo mke wake Chalii. Na mimi nikamwambia atunze jambo hilo kuwa siri yetu pekee, naye hakuwa na neno.

Hazijapita dakika nyingi sana Tesha akawa amefika hapo nje, naye akaegesha gari na kuja ndani ili asalimiane na Bobo pia. Wakazungumza kidogo kwa utani, kisha ndiyo tukamwacha Bobo hapo na kurudi garini ili kwenda msibani.

Kabla ya kuingia ndani ya gari, nikaenda kwenye duka moja lenye huduma ya kutoa pesa kwa wakala wa benki ya CRDB, nami nikatoa kiasi cha shilingi laki mbili kwenye akaunti yangu kupitia simu, na nikanunua bahasha ndogo hapo hapo, kisha nikaiweka pesa hiyo ndani.

Tesha alikuwa ananisubiria kwenye gari, nami nikaenda humo na kuingia pia. Akaniambia kwamba alimwacha mdogo wake kwao vizuri na kuwaeleza mama zake wakubwa kiufupi kuhusu yale ambayo daktari Roshan alituambia kumhusu Mariam; akisema wangemjulisha Miryam kuhusiana nayo maana yeye alikuwa ameenda kazini, na walinitumia shukrani kwa jitihada niliyoweka leo.

Nikamuuliza ikiwa aliangalia kama Ankia bado alikuwepo nyumbani, naye Tesha akasema kwamba bila shaka Ankia angekuwa ameshakwenda huko msibani tayari maana nyumbani hakuwepo, hivyo jamaa akawasha gari na mwendo ukaanza kuelekea Buza.

Tukiwa bado njiani ndiyo nikachukua nafasi hiyo kumtafuta yule Winny, nami nikaongea naye na kumpiga swaga laini mpaka akaeleweka. Alionekana kupenda ucheshi sana kwa hiyo niliweka utani mwingi, na ndiyo nikawa nimemwambia kwamba kuna ndugu yangu aliyekuwa akitamani sana kujuana naye ili waweze kuwa marafiki pia.

Niliingiza tu na uwongo kwamba huyo ndugu yangu alishawahi kumwona pia wakati fulani, na baada ya kuiona picha yake ya WhatsApp profile kwenye simu yangu akamtambua na kutaka nimpe namba. Alionekana kushangaa na kusema alijua hiyo ni michezo tu ya wanaume, ila nikamwambia hapana, na huyo ndugu yangu ni "gentleman" kama mimi tu.

Basi, akawa amekubali nimpe Tesha namba yake, lakini kabla ya hilo nimrushie picha zangu na za Tesha kwa WhatsApp. Sijui alikuwa anataka kutulinganisha? Kwa hiyo nikamwomba Tesha simu yake na kumwambia nilitaka kurusha picha zake chache kwangu ili Winny ajionee mwenyewe kwamba jamaa alikuwa wa ukweli, naye Tesha akasema sawa; ila na yeye huyo Winny atume za kwake nyingi tumwone. Mambo yetu vijana!

β˜…β˜…

Baada ya dakika kadhaa, tukawa tumeingia Buza, naye Tesha akapeleka gari hadi msiba wa Joy ulipofanyikia. Sikujua sana ikiwa ndiyo palikuwa kwao au kwa ndugu zake waliokuwa huku tu, lakini kwenye hiyo nyumba tulipofikia tulikuta watu wengi kiasi. Wanawake walikuwa upande wa ndani zaidi na wanaume walikaa kwenye viti sehemu ya nje zaidi, na ujio wetu hapo ulifanya fikira za wengi zielekezwe kwangu.

Hakukuwa na viti vya kutosha lakini hadi tukapishwa na wanaume watu wazima ili tukae, na kuna wanawake kadhaa waliokuja na kutupa salamu kwa mikono huku wakipiga na magoti kwa heshima kabisa. Sijui walidhani sisi ni akina nani? Labda shauri ya mionekano yetu na kuja na gari. Ah siyo mbaya kujivuna kidogo!

Kwa hiyo tukakaa tu kwa utulivu, na Tesha akawa amempigia simu Ankia ili kumwambia kwamba tulikuwa hapo nje. Kwa ufahamu wangu wa misiba, bila shaka leo ikiwa ni siku ya pili tokea kifo cha Joy basi hii ya kuja hapa ilikuwa kutoa tu pole na kuunga mkono wafiwa, na labda kesho ama kesho kutwa ndiyo wangezika.

Wanaume kadhaa waliokuwa nje hapo walizungumzia masuala ya mpira wa Uingereza kwa sauti ya juu sana, naye Tesha akasema yaani hao hata kama ungeamua kuwaletea pombe hapo wangekunywa na kucheza muziki kabisa. Misiba ya fashion kwao!

Muda si muda, Ankia akawa ametoka nje na kuja mpaka upande wetu. Alikuwa amevaa T-shirt ya mikono mirefu nyeusi na kitenge kwa chini, kilemba kichwani, na alishika khanga moja mkononi sijui kwa masilahi gani.

Watu walimwangalia mpaka alipokuja kufikia nilipokaa, halafu akachuchumaa kama vile amepiga magoti karibu kabisa na mimi, huku mikono yake akiiweka mapajani kwangu. Alijenga kataswira fulani hivi hapo kama vile kuonyesha ana ukaribu zaidi na mimi, nami kwenye kutazamwa kutokana hilo niliona wazi kwamba watu hawangeacha.

Akaanza kuongea na sisi, akisema yuko na wanawake wengine wakitengeneza chakula cha jioni kwa ajili ya wote walioko hapo, nami nikamuuliza ni ndugu gani wa karibu zaidi na Joy aliyekuwa hapo. Akasema ni mama yake mzazi pamoja na baba wa kufikia, na dada zake wawili wa damu pia.

Akatuonyesha huyo baba wa kufikia, mzee wa miaka iliyokimbilia 70 hivi ambaye aliketi mbele zaidi pamoja na wanaume wengine walioonekana kuwa marafiki zake. Hapo ndiyo palikuwa kwa wazazi wao, lakini mwili wa Joy ungesafirishwa kama siyo kesho, basi kesho kutwa kwenda Nachingwea; ndiyo iliposomeka kuwa kwao kihalisi na mwanamke huyo ili akazikwe huko.

Jeneza lake lingeletwa baadaye hapo nyumbani na lingelala mpaka kufikia wakati wa usafirishaji, naye Tesha akamwomba Ankia kuwa ingawa hakuwafahamu watu wa familia yake Joy, awaambie anatuma pole yake ya dhati kabisa kwao.

Mimi pia, ingawa najua nilikuwa nimepita kwenye mstari uliopinda sana pamoja na mwanamke yule niliyekutana naye na kumjua kwa kipindi kifupi, nilikuwa nimehuzunishwa sana na kifo chake. Achilia mbali tu kukisia ni nani aliyemsababishia kifo, ila ni ile hali ya "kujuana" zaidi kutokana na kushiriki mapenzi pamoja naye usiku ule iliyofanya nihisi ukaribu naye kiasi, na alikuwa mtamu kweli!

Nikatoa ile bahasha mfukoni na kumpatia Ankia, nami nikamwambia ampelekee mama yake Joy na kumpa; iwe kama rambirambi yetu sisi watatu kuielekea familia hiyo. Ankia akakubali na kusema angeenda kuwaambia kwamba mume wake ndiyo aliyeitoa hiyo rambirambi, eti mimi yaani, nami nikatabasamu tu kidogo na kusema sawa. Mwanamke huyo akaondoka zake kurudi sehemu ya ndani, nasi tukaendelea kusubiri tu hapo nje.

β˜…β˜…

Baada ya dakika kama kumi tu, Ankia akawa ametoka tena, zamu hii akiwa na mwanamke mwingine pamoja naye. Huyu alikuwa mrefu kiasi, mwenye mwili ulionawiri na ngozi rangi ya chocolate, akiwa amevaa nguo kama kijora ya kijani kibichi huku kiunoni akijifunga khanga, na alikuwa na rasta ndefu kweli mpaka kufikia kiunoni.

Sura yake ilikuwa na ufanano wa mbali kiasi na sura ya Joy, nami nikawa nimetambua huyo ni dada yake. Ankia akaja naye mpaka upande wetu lakini hakutufikia kabisa, kisha akaniita kwa ishara ya kiganja kuonyesha alitaka nimfate.

Nikanyanyuka, na sijui ni kwa nini lakini idadi ya wanawake waliokuwa wakija nje ilizidi kuongezeka tu, na walielekeza macho yao upande wetu. Nikawafata wanawake hao pembeni waliposimama, nami nikasimama karibu yake Ankia.

Kwa ukaribu huo, huyo dada yake Joy alionekana kuwa mrefu kiasi cha kunipita, lakini macho yetu yalilingana.

"JC... huyu ni Adelina. Ni dada yake Joy. Adela, huyu ndiyo JC," Ankia akatutambulisha.

"Ahaa... sawa. Habari yako kaka?" Adelina akanisalimu.

Alikuwa na sauti nzuri tu kutoka ndani ya midomo yake minene, nami nikajibu, "Salama dada. Poleni kwa msiba."

"Asante sana. Tunashukuru pia kwa rambirambi yako. Ni ukarimu mwingi sana ulionao kaka," Adelina akaniambia hivyo.

"Oh, haina shida... tuko pamoja. Mama anaendelea vipi?" nikamuuliza.

"Ah... amepigika yaani. Sisi wote. Unajua... kufa huwa ni... inatokea... lakini mtu akifariki kama mdogo wangu alivyofanywa... inaumiza kwa kweli," Adelina akasema hivyo, na machozi yakaonekana kumlenga.

Ankia akamshika begani kama kumpa faraja.

"Pole sana," nikamwambia hivyo Adelina.

"Asante. Ni mama ndiyo ameniambia nije nikupe shukrani kwa niaba yake... ameishiwa nguvu bado, yaani hata kutoka nje ameshindwa," Adelina akaniambia.

"Aaa sawa... haina shida. Utamwambia mimi ni rafiki yake Joy pia, kwa hiyo tuko pamoja," nikasema hivyo.

"Sawa," akaitikia.

"Naweza ku...kukuomba jambo fulani, dada?" nikamuuliza hivyo.

"Ndiyo, unaweza," akasema hivyo.

Nikamwangalia Ankia kiufupi, naye akajiongeza.

"Ngoja niende ndani, utanikuta," akamwambia hivyo Adelina.

Adelina akatikisa kichwa kukubali, naye Ankia akatembea.

Nikamwangalia mwanamke huyu na kusema, "Mmeshazungumza na mapolisi tena kuhusiana na yaliyotokea?"

"Hapana... bado wanafatilia. Sijui kama watawakamata waliomuua mdogo wangu ila... naombea kwa Mungu wawakamate," akaniambia hivyo.

"Yes, hata mimi pia. Kwa hiyo mlikuwa mmeachiana mawasiliano labda na maaskari au... yaani, askari aliyeshughulikia huo uchunguzi?"

"Ndiyo, tumepewa namba zake za mawasiliano."

"Ahaa... sawa. Naweza kuomba unipatie tafadhali?" nikamwambia hivyo.

Akanitazama usoni kiudadisi kiasi.

"Kama wewe ulivyoniambia dada, hata mimi nataka waliomfanyia Joy hayo wakamatwe. Ninataka kusaidia, na ndiyo maana nahitaji namba ya huyo askari ili niende sambamba na uchunguzi wao..."

"Kwa nini? Kuna kitu fulani unajua?" akaniuliza.

"Hapana, ila nataka kuhakikisha haki kwa ajili ya mdogo wako inapatikana. Kama unavyojua... hawa maaskari wanaweza wakasinzia, na mimi nina uwezo wa kuharakisha huo uchunguzi tukawagundua wauaji... kwa hiyo... nikipata chochote kile, inakuwa vizuri kama nina namba zao ili niwapasie tu taarifa. Si unaelewa?" nikamwambia hayo.

Akatikisa kichwa kukubali, naye akasema, "Sawa. Ngoja nikafate simu ndani nije nikupe."

"Sawa, nashukuru. Nakusubiri hapa," nikasema hivyo.

Mwanamke huyo akaelekea kule ndani tena, nami nikabaki kusubiri hapo hapo nilipokuwa nimesimama.

Tesha alikuwa akinitumia ishara za mikono kuuliza 'vipi,' nami nikamwambia kwa ishara atulie tu ningemwelezea. Kusimama hapo kulinifanya nione namna ambavyo baba wa kufikia wa kina Joy alivyoniangalia sana, na najua angedhani labda nafahamiana sana na Adelina baada ya kuniona napata maongezi pamoja naye.

Dakika mbili hivi naye dada mkubwa wa Joy akarejea tena, zamu hii akiwa na simu mkononi, naye akaja kwangu tena ili anipe namba. Nikafungua simu yangu pia, nami nikamsikiliza aliponitajia namba za huyo askari/mpelelezi, kisha nikazitunza kwenye simu.

"Asante dada," nikamshukuru.

"Usijali. Hivi... unaitwa nani kweli?" akaniuliza.

"JC."

"J..C. Sawa. Nataka nikuombe kitu, samahani lakini..."

"Usiwaze. Niambie," nikamkatisha.

"Naomba na mimi unipatie namba yako kama hutojali... ikitokea umepata lolote basi na mie unaweza kuniambia, si ndiyo?"

"Okay, haina shida. Nitajie zako nikubipu."

Akafanya hivyo, nami nikazitunza zake na kumpigia, kisha akatunza zangu pia.

"We' haukai huku?" nikamuuliza.

"Ee, me nakaa Mbezi. Wewe je? Mnaishi wapi na mke wako?"

"Mke? Aa huyu Ankia? Tupo Mbagala huku..."

"Aaa ndiyo mmejuana na Joy huko eh?"

"Ndiyo."

Akatikisa kichwa kidogo kuonyesha uelewa na kusema, "Sawa. Haya, baadaye. Tuta...wasiliana."

"Haya."

Akaondoka baada ya hapo, nami nikawa nimeridhika baada ya kuzipata namba za huyo askari. Taratibu tu, na mpango niliokuwa nao ungezaa matunda yake.

Nikarudi pale kwenye kiti changu na kukaa, naye Tesha akanisogelea karibu zaidi.

"Vipi? Nani huyo?" akaniuliza.

"Dada yake Joy," nikamjibu.

"Ahaa... lizuri kweli. Mlikuwa mnapeana hadi manamba kila mtu kakuona bonge la fisadi..."

"Kwenye kipi labda? Je kama tunajuana?"

"We' usikimbie maana, watu washasoma mambo kivingine. Ndiyo maana nampendaga Dulla Makabila, kashaimba hivi vitu hadi msibani vinatokea. Utasababisha Joy aghairi kufa!" akasema hivyo.

Nikabana cheko yangu na kumwambia, "Acha ujinga, tuko msibani. Na nilikuwa naongea naye mambo ya maana siyo upuuzi."

"Hahah... haya bana. Kwa hiyo hapa tunasubiri maiti iletwe halafu ndiyo tunaosha, au siyo?"

"Ee lakini... si tunaondoka na Ankia?"

"Akijichelewesha je?"

"Tutaongea naye," nikamwambia hivyo kwa utulivu.

Baada ya dakika chache kupita, nikatoka hapo na kwenda pembeni kidogo, kisha nikatoa simu na kupiga kwa namba za mke wake Chalii Gonga. Nilikuwa nataka nianze kukichokonoa kichuguu alichokuwa amejifichia huko aliko, ama labda kama ni kasri la kifalme, basi niyavunje malango yake.

Piga ya kwanza, hakupokea. Ya pili, ya tatu, kimya. Nikaona nimweke pembeni kwanza ili baadaye nije kuendelea kumchokoza, labda kwa sasa alikuwa bize kutafuta watu wengine wa kuua, nikiomba Mungu nisiwemo kwenye hiyo orodha!

β˜…β˜…

Basi, kutokea hapo tukaendelea kusubiri tu mpaka ilipofika mida ya saa kumi jioni. Mida hiyo ndiyo mwili wa Joy, au niseme "vipande" vya Joy ndiyo vikawa vimeletwa. Ulikuwa ndani ya jeneza jeupe lenye msalaba kwa juu, likiwa limebebwa kwenye pickup nyeupe ya Toyota Hilux iliyoonekana kuwa ya gharama.

Wanaume wakaanza kuchangamka kuliondoa hapo ili liingizwe ndani ya nyumba, vilio kutoka kwa wanawake vikisikika kutokea huko ndani jeneza lilipokuwa linapelekwa, na kama ni kwenda kushoto zaidi na matarajio yangu ambayo sikuwa nayo kabisa mpaka kufikia sasa, basi ilikuwa ni kumtambua dereva aliyeendesha gari hilo. Aliposhuka, mimi na Tesha tukatazamana kimshangao kiasi, kwa sababu ilikuwa ni Chalii Gonga.

Oh, hii ndiyo ilikuwa mara yangu ya pili kumwona kutokea mara ya kwanza kule kwenye bar yake, maana hata aliponipa elfu kumi kama nauli ya kuja kwenda kukutana naye, nilimpiga chini, na baada ya yeye kuniona, akanipungia kiganja chake hewani huku akiniangalia kwa umakini, nami nikamtikisia kichwa mara moja tu kurudisha salamu yake.

Sikufikiri ningemwona hapo leo, lakini jinsi ambayo alijichanganya na watu wa familia yake Joy hapo ilinifanya nitambue kwamba alikuwa akifahamiana nao. Na si ajabu aligharamia mambo mengi yaliyoendeshwa kwenye huu msiba.

Baada ya kuona ameongea machache pamoja na baba wa kufikia wa akina Joy, yeye pamoja na aliokuja nao wakarudi kwenye gari, kisha wakaondoka hapo. Bize kama kawaida yake. Alitendewa kama taita hapo, na sidhani ikiwa kuna yeyote kati ya watu wa familia hiyo waliofikiri mke wa Chalii alichangia kwa kiasi fulani katika mauaji ya Joy, ijapokuwa hata na jamaa hakuonekana kujua, na mimi bado sikuwa na uhakika. Yote kwa yote, ingefahamika tu.

Baada ya Chalii kuondoka, wanawake wakaanza kufanya matayarisho kwa ajili ya chakula. Walianza kusambaza sahani zenye wali na maharage kwa wazee-wazee, kisha watu wazima vijana, nami nikamwambia Tesha kwamba kiukweli sikujihisi vizuri sana kula msibani. Akauliza kwa nini, nami nikamwambia iko hivyo tu.

Akasema nisiwe hivyo, nikipokee tu chakula kikiletwa na nile mpaka kiishe, la sivyo ningemkasirisha Joy huko mbinguni kwa kuacha kula kwenye msiba wake. Akanifanya nitabasamu kwa hisia, kwa sababu alinifanya nitilie maanani ukweli kwamba ingawa Joy aliuwawa vibaya, angalau alikuwa amepumzika. Kwa amani. Labda.

Anyway, chakula kilikuwa kinasambazwa kwa wengine na sisi tukawa tunapitwa tu, kana kwamba hatungepewa. Sikuelewa sababu, lakini Tesha akatania kwa kusema sisi tulikuwa kama wageni rasmi hapo, kwa hiyo msosi ungeletwa kimtindo. Na alikuwa sahihi!

Msosi ambao uliletwa kwangu, ulibebwa na Adelina mwenyewe, naye Tesha akapewa na Ankia. Cha kushangaza kwa upande wangu ni kwamba, Adelina alifikiri Ankia ni mke wangu, si ndiyo? Lakini yeye ndiyo akanipa chakula. Na pamoja na kwamba alikuwa mkubwa zaidi yangu, nilipokipokea akashuka mpaka chini kwa kupiga goti moja ili kunionyesha heshima. Dah!

Nikabaki nikimwangalia mwanamke huyo kwa umakini, sura yake bado ikionekana kuwa na simanzi lakini akijitahidi mno kuwa imara, nami nikamshukuru na kumwacha aende. Tesha sasa! Akaanza mambo yake. Nikamwambia komea hapo hapo!

Tukala, tukamaliza, tukaweka sahani pembeni. Saa kumi na mbili haikukawia kufika, na baadhi ya watu walikuwa wameshaondoka baada tu ya kula. Ngoja nisafishe koo kwanza! Imeeleweka hiyo.

Ikiwa inakimbilia kuingia saa moja usiku, Ankia akaja, naye akatuambia kwamba kama ni kuondoka hapo basi mimi na Tesha tutangulie na yeye angekuja baadaye. Kuna vitu bado alikuwa anataka kusaidia kufanya hapo nyumbani kwao Joy, kwa hiyo akanipa funguo za nyumba yake na kutuaga. Kukawa hamna noma kwa hilo, nasi tukaingia kwenye gari ili kurudi Mzinga.

β˜…β˜…

Saa mbili usiku tu ndiyo inaingia nasi tukawa tumefika pande za maskani yetu. Nilikuwa nimeshamuungishia Tesha namba ya Winny ili waanze kuwasiliana pia, na kwa kuwa mwanamke huyo alikuwa ametuma picha zake maridadi sana, Tesha akasema ndiyo keki ambayo angeanza nayo kuila kabla ya zingine.

Nikamwambia awe makini ili Winny asimpeleke sana, maana mwanamke huyo alionekana kupenda gharama mno. Akanitolea hofu kwa kusema nimwachie ulingo tu. Kwa kuwa nilihitaji kumwona Mariam kwanza, nikaamua kwenda naye pale kwao ili nimjulie hali binti huyo pamoja na mama zake wakubwa. Bado mfuko wa vifaa nilivyochukua hospitali leo uliokuwa ndani ya gari hilo, nami nikauacha tu humo mpaka kufikia wakati wa kuondoka ndiyo ningeuchukua.

Nikafikiria kwamba huenda Miryam bado angekuwa kazini, lakini tulipofika ndani, tukawakuta wanawake wote wa hapo wakiwa sebuleni, kutia ndani Shadya. Bibie Miryam alikuwepo sebuleni pia wakati tunaingia, kisha akaelekea upande wa jikoni; ikionekana alikuwa anapika.

Wanaume tukapokewa kwa salamu nzuri sana, nasi tukakaa kwenye sofa moja huku Tesha akianza kuelezea namna ambavyo mambo yalikuwa huko msibani; kuanzia wakati tulipofika mpaka tulipoondoka. Wakawa wanachangia mada kuhusiana na janga lililomkumba Joy, huku Shadya akisema kwa njia yake ya umbeya kwamba umalaya ndiyo uliomponza Joy mpaka kukutwa na masaibu hayo, lakini hakuona kuwa haki kwa mwanamke yule kufa kikatili namna hiyo.

Kuanzia hapo sasa ndiyo Tesha akaanza kupewa somo la kujitahidi kuachana na masuala ya kukesha Masai, kwa sababu mama zake wakubwa hawakutaka aje kujikuta kwenye hali kama ya Joy, na kwa wakati huu Tesha alikuwa msikivu kweli, akiunga mkono pointi zao kwa kusema angekuwa mwangalifu sana.

Kwa upande wangu mimi nilikuwa kimya tu, nikimtazama binti Mariam sanasana. Alikuwa amekaa chini karibu na miguu ya Bi Zawadi, akiwa anatazama katuni kwenye TV huku amekilaza kichwa chake kwenye paja la mwanamke huyo, na Bi Zawadi alikuwa akizilaza-laza nywele laini za binti taratibu kama kumbembeleza.

"Kwa hiyo kesho ndo' watafanya na ibada eh?" akauliza hivyo Shadya.

"Eee kesho. Halafu hazikiwi hapo Buza. Ankia amesema mwili wa Joy utapelekwa huko Nachingwea... ndiyo kwao kabisa," Tesha akamwambia.

"Aaa kumbe?" Shadya akauliza.

"Eeeh," Tesha akasema.

"Ankia je? Mmerudi naye?" Bi Jamila akaniuliza hivyo.

"Ye' amebaki huko. Kuna mambo anamalizia kufanya, atakuja baadaye," nikamjulisha hilo.

"Si mngemsubiria? Masuala ya usiku siyo mazuri kwa wanawake mnajua," Shadya akasema.

"Ye' mwenyewe ndo' katuambia tutangulie. Sidhani kama atachukua muda mrefu sana..." Tesha akasema.

Ni wakati huu ndiyo bibie Miryam akawa amerudi tena sehemu hii ya sebule, naye akakaa kwenye mkono wa sofa walilokaa mama wakubwa na Mariam kwa chini. Wakati huu ndiyo nikaweza kumchora vyema zaidi.

Alikuwa amevaa nguo kama Punjabi yenye rangi ya zambarau, pamoja na kilemba kilichofunika nywele zake. Ingawa suruali ya nguo hiyo ilikuwa pana, umbo lake lilichoreka vizuri hasa alipokaa namna hiyo kwa kunyanyua mguu mmoja juu kiasi, nasi tukaangaliana kwa njia ya kawaida tu machoni na kisha kuwatazama wengine.

"Mariam anapenda katuni eh? Naona ametulia kweli," nikasema hivyo.

Binti akanitazama usoni, nafikiri kwa sababu alisikia nimetaja jina lake.

"Ahahah... sana. Muziki, katuni, anapenda sana. Si unakumbuka ulivyomkuta anacheza "Kwikwi"?" Bi Zawadi akasema hivyo huku akiigiza vipapatio kwa mikono yake.

Nikatabasamu kidogo na kusema, "Ndiyo nakumbuka. Na alikuwa anapatia."

Bi Zawadi akacheka kidogo, nami nikamwona Miryam akitabasamu kwa hisia.

"Hapo ukimtolea anaanza kulia," Shadya akasema hivyo.

Wote tukacheka kidogo pia, nami nikiwa nasugua-sugua magoti yangu kwa viganja, nikasema, "Sawa. Basi, ngoja me niwaache jamani."

"Ih? Wapi tena?" Tesha akaniuliza.

"Naenda ndani tu," nikasema hivyo.

"Kwani hapa nje?" Shadya akauliza.

Nikacheka kidogo kwa pumzi.

"Tulia bwana, sister anataka kuturekebishia matumbo," Tesha akasema.

"Ndiyo baba, kaa tu. Kwanza... Ankia bado si hajarudi? Utaenda kukaa mwenyewe?" Bi Zawadi akaniuliza.

Nikatabasamu tu.

"Au umechoka sana?" akauliza Bi Jamila.

"Hapana, sijachoka wala," nikajibu.

"Eeeh... kaa tu baba'angu. Mimi anaandaa mirosti huko. Si unakumbuka nilivyosema kuhusu mapishi yake?" Bi Jamila akaniambia hivyo huku akimzomea Bi Zawadi kiutani.

Shadya na mimi tukacheka kidogo, nami nikamwona Miryam anamtazama mama mkubwa wake kimaswali kiasi; bila shaka akijiuliza kauli yake ilimaanisha nini, naye Bi Zawadi akamwangalia mwenzake kwa njia ya kununa.

"Ee mwanangu, kaa uonje mapishi ya sister. Anajua huyu!" Tesha akamsifia dada yake.

"Eti Mimi, wananisema me sijui kupika. Eti unanizidi," Bi Zawadi akamwambia Miryam hivyo kama anadeka eti.

"Aa wapi! Akuzidi nani? Wewe ndiyo unajua bwana. Waambie wakuache," Miryam akambembeleza eti.

"Anakupa kichwa tu. Ngoja JC ale chake leo uone kama atagusa chako tena," Bi Jamila akamwambia mwenzake hivyo kwa utani.

Eh! Kauli hiyo ya Bi Jamila ilikuwa inalenga suala la chakula, lakini ilikuja kwa njia ambayo iliingiza jambo lingine akilini, na nafikiri Miryam pia alielewa kwa njia hiyo hiyo kwa sababu nilimwona akishtuka machoni kiasi na kumtazama Bi Jamila kimaswali, kisha akanitazama kwa njia ya kuhukumu.

Nikaangalia pembeni na kujikaza nisicheke, kwa kuwa najua hata Miryam alidhani kilichoongelewa kuliwa kilikuwa chake kingine! Aisee! Hii familia ilinipa raha sana. Wengine hawakuelewa mambo kwa njia hiyo, lakini kwa namna tu ambayo Miryam aliniangalia ilionyesha alielewa vitu vingi kwa mapana mno, na alikuwa na akili iliyonolewa vizuri sana.

Tesha akaniangalia kwa umakini, kisha akauliza, "Vipi kaka? Umefurahi sana eh?"

Nikaibana cheko yangu zaidi na kumwambia, "Ee... ndiyo... ahah... sawa. Nita... nitakaa kukionja."

Niliposema hivyo, nikamwangalia Miryam usoni, naye akatazama pembeni akiwa kama ameudhika vile, nami nikaelewa kwamba alikuwa ameshasoma kile ambacho kilipita akilini mwangu pia, nami nikainamisha uso na kuweka kiganja changu kwenye paji ili nijisitiri zaidi kutocheka. Dah! Haya bwana.

Bi Jamila alikuwa amenifurahisha mno bila yeye mwenyewe kutambua umbali wa furaha hiyo, na maongezi zaidi yalipokuwa yakiendelea, simu yangu ikaita. Nikatoa ili nione mpigaji kukuta ni "Beth." Yeah. Mke wake Chalii Gonga. Hivyo ndivyo nilivyomtunza kwenye simu yangu.

Muda mwafaka wa kunitafuta ukawa sasa hivi, labda alikuwa na mambo mengi leo, na mimi nilikuwa nimemtunza akiba tu, hivyo nikaomba wenyeji wangu samahani ya kuwapisha ili niende nje kuzungumza na simu, nami nikatoka hapo ndani upesi.

Nikiwa kibarazani nikapokea. "Hallo?"

"We' nani?" sauti ya mke wake Chalii ikasikika ikisema hivyo.

"Huwezi kukisia? Hata sauti tu hujaitambua?"

"Bwana, sema we' ni nani. Nimekuta umenipigia. Sema we' ni nani, una shida gani..."

"Me JC," nikamwambia.

"Nani?"

"JC."

"Wa wapi?"

Nikabaki kimya tu baada ya yeye kuuliza hivyo.

"Aaa... lover boy wa Joy?" akasema hivyo.

"Mmm... ndiyo mimi."

"Ehe... kulikoni?"

"Naomba kukutana na wewe tafadhali," nikamwambia kwa sauti ya upole.

"Unataka nini?"

"Nataka tu tongee."

"Kuhusu?"

"Mambo mengi. Sikia... juzi ile tulivyoongea... nilikuja juu sana. Najutia kuongea kwa hasira mbele yako, eh? Nataka mambo yanyooke kati yetu..."

"Ahhahaaa... Naona umepunguza kibesi leo. Yamekukuta yapi huko HB wa Masai?"

Nikakunja ngumi yangu na kumwambia kwa sauti tulivu, "Sina haja ya kuzunguka popote. Nilitafakari tu uliyoniambia... na nimeona uko sahihi. Mimi sikuwezi, na sitaki uje uniumize wala nini maana... me bado mdogo, sitaki kutengeneza maadui. Ni bora zaidi nikijiweka upande wako badala ya kuwa dhidi yako... na naweza kuwa rafiki mzuri kwako kwa saabu' naweza kukupa vitu vyenye faida."

"Mhm... ahahah... a-ah. We' unaweza kunipa nini mimi? Unafikiri nahangaishwa na kasura kako? Mimi ni malikia. Nimeshaona wengi zaidi yako, em' niambie una nini cha kunioffer mimi..."

"Wala sijafikiria masuala kama hayo. Naongelea vitu vitamu hata zaidi ya heroo dada'angu," nikamwambia hivyo.

"Unamaanisha nini?"

"Nipange. Tukutane hata kesho sehemu yoyote unayotaka wewe. Nitakuonyesha," nikamwambia.

"Kwa hiyo we' kijana unataka kunifanyia mimi mchezo wa kipuu...."

"Hapana, Bertha. Niko serious. Ndiyo maana nimekwambia wewe mwenyewe unipange tukutane unapotaka. Nataka niwe upande wako, sawa? Na lazima nikupe kitu kizuri kama zawadi ya urafiki... au hata kama siyo urafiki basi tu iwe njia ya kuomba msamaha. Nimekuelewa sana... na... ukikuta nazingua, una ruksa ya kunifanya chochote unachotaka," nikamwambia hivyo kwa uhakika.

Nilikuwa makini sana kuhakikisha maneno hayo hayasikiki kule ndani kwa kuongea kwa sauti ya chini, naye akauliza, "We' ni mjanja eh?"

Nikajibu, "Ndiyo. Me ni mjanja."

Akatulia kidogo, kisha akasema, "Haya. Tutaona. Nitakutafuta. Usinitafute mpaka nikutafute. Sijui umenielewa?"

Nikatabasamu kidogo kwa kiburi, kwa sababu tu ya kuhisi jinsi ambavyo mwanamke huyo alijipa wadhifa fulani kana kwamba alikuwa mtu mwenye kutiiisha mno, nami nikamwambia, "Poa. Nitasubiri. Nishtue tu muda wowote unipange."

Akakata simu.

Raa! Hapo nikawa nimechukua, nikaweka, halafu sasa ikawa imebaki tu kufanya Waah! Angalau nilikuwa nimeweza kuipika vizuri akili ya mwanamke huyo ili aone kwamba nina kitu kizuri cha kumfaidisha nacho katika mambo aliyopenda zaidi; madawa. Ah mi' si daktari bwana?

Ningehakikisha namchanganya mwanamke huyo mpaka ingeeleweka kwake kwamba si yeye tu ndiye aliyetakiwa kujiona wa kuogopwa, bali kuna watu ambao hawakutaka kuogopwa, lakini walistahili kuogopwa. Achana na mimi kabisa nikiwa nimekaza nia kwenye jambo fulani, na huyo Bertha angelipia kwa kucheza na mimi. Kila kitu kingekwenda taratibu tu, lakini angejikuta anaanguka chini kwa kasi sana!



β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…

ITAENDELEA

β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…

Full Story WhatsApp or inbox

Whatsapp +255 678 017 280
 
MIMI NA MIMI

A Story by Elton Tonny

Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Tamaa, Hila, Usaliti, Siri, Mambo Yasiyotazamiwa

R-rated 18+

Enjoy!


β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…

SEHEMU YA KUMI NA SITA

β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…


Nikatoka hapo kibarazani na kurudi tena ndani, nami nikamkuta Miryam akiwa sebuleni tena, akiwa amekaa kwenye mkono wa sofa alilokalia Bi Zawadi na Bi Jamila, wakati huu wote wakipata mazungumzo. Harufu nzuri sana ya chakula alichokuwa anaandaa mwanamke huyo ilipenya vizuri zaidi puani mwangu, nayo ikaongeza hamu yangu ya kutaka kuonja mahanjumati yake.

Mazungumzo yao yalikuwa kama mabishano mepesi baina ya Shadya na bibie Miryam mwenyewe, nami nikawa nimekaa sofani karibu na Tesha kwa mara nyingine.

"Hapana, unakosea. Ni nje, siyo ndani. Hivi unafikiri ukimwambia nani hivyo atakubali?" Shadya akamwambia hivyo Miryam.

Miryam akatabasamu kiasi na kutikisa kichwa kidogo.

"Ametoka ndani ya... ametoka nje ya... eh! Pana ugumu hapo..." Tesha akasema hivyo kwa utafakari.

"Me naona kama vile Mimi yuko sahihi," Bi Jamila akasema.

"Mm-mm, haiwezekani. Basi tumuulize msomi... daktari, JC," Shadya akasema hivyo.

Mimi nikawa bado sijaelewa na kuendelea kuwaangalia tu kwa utulivu.

"Kwani nani hapa hajasoma? Au Mimi siyo msomi?" Bi Zawadi akamuuliza hivyo Shadya.

"A-aah, ye' anao wa kivyake. JC yeye anao kama wa kwangu... na mimi ningekuwaga daktari," Shadya akasema hivyo.

"Daktari wa porojo," Tesha akasema hivyo.

Mama zake wakubwa wakacheka.

Nikiwa bado sijaelewa, nikauliza, "Ni kuhusu nini?"

Shadya akasema, "Kuna mama mmoja pale juu ile juzi amefumaniwa na mume wake akiwa na hawala. Ametoka nje ya ndoa, si ndiyo?"

Nikatikisa kichwa kukubali.

"Sasa je!" Shadya akamwambia hivyo Miryam.

Miryam akatabasamu kiasi na kusema, "Hujaelezea vizuri kwa nini tunapingana."

Nikamwangalia Tesha, naye akasema, "Yaani eti... sawa si kama hivyo huyo mwanamke kafumaniwa? Sasa, huwa kuna hiki kitu kwamba mtu kama huyo tunasema ametoka nje ya ndoa. Da' Mimi anasema kwamba kwa Kiswahili fasaha inatakiwa kuwa ametoka ndani ya ndoa, Shadya hataki. Hapo inakaaje?"

Nikamwangalia Miryam usoni, naye alikuwa ananiangalia kwa macho yenye subira.

"Eti JC, si ni kutoka nje ya ndoa? Utatokaje ndani ya ndoa... hai-make sense," Shadya akaniambia hivyo.

Nikamwangalia na kusema, "Hapana Shadya. Miryam yuko sahihi."

"Si nimekwambia!" Bi Jamila akamwambia hivyo Shadya.

"Eeh, hata me naona kama dada yuko sahihi. Ni kutoka ndani ya ndoa, si ndiyo?" Tesha akaniuliza.

Nikatikisa kichwa kukubali.

"Mmm... JC na wewe!" Shadya akasema hivyo.

"Ahahah... Kiswahili tunakikuza na kukiharibu sisi wenyewe maana maneno mengi tunayaongea kimazoea. Ukiangalia hata kwa mfano... tuseme labda mtu akaja hapa na kupiga hodi, ikiwa utasema "toka nje," ataelewaje?" nikamuuliza hivyo Shadya.

"Atajua unamfukuza," akajibu hivyo.

"Eee... ndiyo ilivyozoeleka. Lakini kwa ufasaha zaidi, unamaanisha kwamba atoke nje, aingie wapi...?"

"Ndani," Tesha akamalizia maelezo yangu.

"Umeona?" nikamuuliza hivyo Shadya.

Bi Zawadi na Bi Jamila wakacheka kidogo, naye Shadya akacheka kwa mguno.

"Miryam ndiyo ana maana hiyo. Mtu akifanya usaliti kwenye ndoa, ameenda nje ya ndoa yake, kwa hiyo anakuwa ametoka ndani ya ndoa. Umeelewa?" nikamwambia Shadya.

"Mhm... haya bwana, nyie mpeane pambe tu," Shadya akasema hivyo.

Sote tukacheka kidogo, naye Tesha akasema, "Ni kweli bwana. Kwa hiyo... kama da' Mimi anavyosema, inapaswa kuwa "amekwenda nje ya ndoa," siyo "ametoka nje ya ndoa." Dah, kweli maana, huwezi kutoka nje kama tayari uko nje, au siyo? Ni lazima uwe ndani ili uende nje. Yeah, hiyo ndiyo imepafektika! Nimeipenda hii sana, ngoja niweke na status WhatsApp."

Wengine wakacheka kidogo, nami nikamtazama Miryam machoni na kukuta anatabasamu. Shadya akaanza kuridhia ukweli wa mambo, na nilipenda sana namna ambavyo hali ya kirafiki baina yangu na familia hii ilivyozidi kuongezeka hatua kwa hatua. Miryam aliponitazama na kukuta namwangalia, tabasamu lake likafifia kiasi, naye akanyanyuka na kuelekea jikoni.

Nikajikuta natabasamu tu, kwa sababu ingawa sikuwa nimejenga ukaribu naye wa kirafiki zaidi, kuna haka kahali kapya ka mazoea ya mbali kalikokuwa kameanza kujijenga kati yetu, na ilinifanya nitake kukakuza zaidi ili ikiwezekana nije kuwa hata na urafiki pamoja naye. Ila huko bado palikuwa mbali sana kufika. Huyo mwanamke alikuwa wa kivyake mno, kwa hiyo alikuwa ni wa kumwacha tu. Hivyo hivyo.

Basi, muda si muda nikaanza kumwona bibie Miryam akiwa anaandaa meza upande wa dining kwa ajili ya vyakula, akiweka vyombo kwa ajili yetu sote pamoja na vyakula alivyotengeneza. Akatukaribisha, nasi tukaenda na kukaa vitini ili tuyape matumbo yetu upendo.

Nikapakua kwa upande wangu na kuanza kula, na aisee! Huyu dada kweli alijua kupika. Yaani vyakula vilivyokuwepo havikuwa tofauti na vyovyote ambavyo nimewahi kula lakini upishi wake ndiyo uliokuwa mpya kwenye ladha niliyopata ulimini.

Wali wa nazi, maharage sijui aliyachanganyia maziwa na vitu gani, pamoja na nyama laini iliyoungwa kwa kiungo fulani kilichofanya ionekane kuwa na rangi ya kahawia iliyokoza na tamu vibaya mno. Nikamaliza zamu ya kwanza na kuongeza bila kusukumwa, na Bi Jamila alipouliza nimeonaje, nikamwambia kwa kweli nimeona.

Sikumsemesha Miryam moja kwa moja lakini nikasifia upishi wake, nikisema anajua sana na wala hata haringi. Nikamwona tu akitabasamu kiasi huku akiendelea kula taratibu na kumlisha binti Mariam, akimtendea vizuri sana kwa njia fulani utadhani alikuwa kama mama yake.

Baada ya kushiba, nikatoa shukrani na kurudi tena kukaa sofani. Tesha akajiunga nami pia, kisha wakubwa wakafata, nami nikamwona Miryam akimnawisha mdogo wake kabla ya kumleta upande wetu tena na yeye kurudi mezani kupasafisha.

Sisi wengine tulikuwa tunaendelea na maongezi yenye kufurahisha, lakini sijui kwa nini tu jicho langu la pembeni lilikazia fikira zaidi upande aliokuwepo Miryam. Nadhani sababu ilikuwa kwamba, nilipendezwa tu na ile kuanza kumjua vizuri mwanamke huyo. Alikuwa mnyenyekevu sana.

Ni yeye ndiye aliyehangaika kuiandalia familia hiyo mahitaji yao na hata kuwabebea mizigo mingi mizito, lakini bado hata kwa mambo madogo tu alijishusha na kuwafanyia pia. Katika kila sense, alikuwa dada na mwanamke bora, na utu wa namna hiyo ulimfanya apendeze sana.

Hii ikiwa ni saa nne usiku sasa, Mariam alionekana kuwa na usingizi baada ya kuwa ameshiba, hivyo Bi Jamila akaongozana naye kuelekea chumbani ili wakapumzike pamoja. Shadya alikuwa amesema kwamba kwa sababu mume wake alikuwa safari na hangerudi mpaka wiki ijayo, angetumia muda huo kuwa huku zaidi, kwa hiyo hata na leo angelala hapa.

Miryam akawa amemaliza usafi wa vyombo na kuja tena sebuleni, naye akakaa sofa moja na Bi Zawadi na kuchukua laptop yake iliyokuwa chini ya meza ndogo hapo sebuleni, naye akaanza kupitia mambo yake humo; bila shaka ya kikazi labda.

Sikumaliza dakika kumi na tano baada ya hapo nami nikawa nimetoa heri ya kuaga kwa mara nyingine tena, naye Bi Zawadi na Shadya wakaipokea vizuri na kunitakia usiku mwema pia. Niliona kwamba, nilipoaga tu, Miryam aliondoa umakini wake kwenye laptop na kunitazama, kisha akaiweka mezani kabisa.

Niliposimama pamoja na Tesha ili kwenda nje, mwanamke huyo akasimama pia, ikionyesha alitaka kutoka nje pamoja nasi pia ili labda aongee nami, hivyo nikatangulia kutoka mpaka kufikia kibarazani na kusimama. Tesha akatoka, kisha dada yake akafata nyuma yake.

"Oy, wingu limetanda... sijui itashuka?" Tesha akaniambia hivyo.

Nikaangalia juu na kusema, "Yeah, inaweza ikanyesha. Angalau ianze kutuondolea vumbi."

"Na joto ndiyo liongezeke kubabake..."

Tesha aliposema hivyo, akajishtukia na kumwangalia Miryam usoni. Nafikiri alihisi hiyo "kubabake" haingesomeka vizuri kwa dada yake, na kweli Miryam akawa anamwangalia kwa njia ya kuonyesha amekerwa.

Tesha akatoa simu yake na kuvaa ndala, kisha akaiweka sikioni na kuigiza amepokea huku akisema, "Eeh oya nakusikia... ngoja niongee na huyu jamaa hapa."

Akasogea mpaka kufikia kwenye gari, nami nikatabasamu na kumwangalia Miryam usoni, ambaye alikuwa na tabasamu hafifu huku akitikisa kichwa taratibu.

"Utaenda msibani kwa Joy?" nikamuuliza hivyo.

Hilo swali lilikuja ghafla tu yaani hata sijui kwa nini niliuliza hivyo.

"Bee?" akaitika.

"Msibani... kwa Joy?" nikauliza tena.

"Aaa... mimi kwenda? Sidhani. Kwanza hata nilikuwa simfahamu, na... nina mambo mengi," akaniambia.

Nikabana midomo yangu ili tabasamu langu lisionekane wazi, kwa kuwa nilichokuwa nataka tu ilikuwa ni kusikia kasauti kake kazuri, nami nikatikisa kichwa kuonyesha uelewa.

"Nilikuwa nataka nikuulize..." akaniambia.

"Ndiyo, niulize chochote," nikamwambia hivyo kwa umakini.

"Hayo mazoezi utakayokuwa unafanya na Mamu... ni vitu practical sana, au? Maana... mdogo wangu hayuko vizuri sana na interaction pamoja na watu asiowafahamu, so... nataka tu kujua ni approach zipi unazotaka kutumia pamoja naye, zaidi tu ya kusema kwamba mtafanya michezo..." akaongea hayo.

Nilikuwa nimebaki kumtazama usoni tu, na kwa kiasi fulani nikawa nimezubaa. Sababu? Sauti yake.

Nafikiri akawa ameona hilo, naye akauliza, "Umenielewa?"

Nikatazama pembeni kiufupi nikiwa najaribu kuisawazisha vyema taarifa ya maneno aliyotoka kusema, nami nikamwambia, "Ndiyo, nimeelewa. Yaani... nakuelewa. Najua unahangaikia hali njema ya mdogo wako, na nakuhakikishia mambo nayotaka kufanya pamoja naye... hayatapita mipaka... hayatakuwa ya gusa-nikuguse, no. Kuwa na amani kabisa."

Akaangalia chini kiasi na kusema, "Sawa. Usichukulie vibaya lakini... labda hata ukafikiri nakuona kama muhuni sana."

"Ahahah... usijali, ninaelewa. Kila kitu tutakifanyia hapa hapa kwako hasa kwa sababu ni sehemu aliyoizoea, kwa hiyo atakuwa kwenye mazingira salama. Nitaanza na vitu vyepesi tu ili anizoee haraka, kisha tutaendelea na mengi zaidi. Itakuwa vizuri kama siku moja ukija kutuona pia," nikamwambia hivyo.

"Sister anatupenda mno JC, yaani hataki hata tujikwae," Tesha akadakia.

"Yeah, ni jambo zuri sana," nikamwambia hivyo.

"Mpaka kero," Tesha akatania.

Nikamwangalia Miryam usoni na kuona anatabasamu, naye akasema, "Sawa, basi... ndiyo hivyo. Nashukuru pia kwa jitihada zako japo... sikulipi."

"Ahah... ondoa shaka," nikamwambia.

Kuna kitu kilichokuwa kikinisukuma nitake kumuuliza kuhusu suala la Joshua kwenda kazini kwake ile jana, ikiwa imeingia tu akilini wakati huu ambao angalau tulikuwa tumepata mazungumzo mafupi, lakini nikaona niache tu hasa kwa sababu sidhani ingekuwa busara kumuuliza kitu kama hicho na Tesha akiwa hapo; na labda hata Miryam angeniona kuwa mfukunyuku.

Sauti ya bajaji ikasikika ikifika nje ya geti na kuendelea kuungurumia hapo hapo.

"Atakuwa Ankia huyo," Tesha akasema hivyo.

"Ndiyo, halafu funguo ninazo... ngoja nimwahi," nikasema hivyo.

Nikavaa vya miguuni na kumwomba Tesha anitolee ule mfuko wa vifaa nilivyochukua hospitali leo, uliokuwa ndani ya gari la Miryam bado, naye akaufungua na kunitolea. Nikamwona Ankia kupitia matundu ya ukuta akiwa upande wa geti la nyumba yake, nami nikamwambia nipo huku.

Kwa kuwa Ankia alimwona Miryam, akaamua kuja upande wetu ili aweze kumsalimia. Tesha akamfungulia mlango mdogo wa geti, naye Ankia akaenda kupena salamu fupi za kirafiki pamoja na Miryam, kisha ndiyo tukaondoka kwa pamoja kuelekea "kwetu."

Ilionekana kuwa siku ndefu kweli leo ingawa muda haukuwa umeenda sana, na Ankia alionekana kuchoka sana. Hakuwa na mpango wa kupika maana alikuwa ameshakula, nami nikamwambia kweli apumzike tu maana hata mie nilikuwa nimeshakula. Akaona uhitaji wa kwenda kujimwagia maji kisha ndiyo arudi kupumzika, nami nikamwacha aanze ili mimi nipange vitu fulani kwanza ndiyo nikajimwagie pia.

Nikaingia chumbani kwangu. Kitu cha kwanza kabisa kufanya ikawa ni kupiga simu kwa namba ya yule askari mpelelezi ambayo dada yake Joy alinipatia huko msibani. Ikapokelewa, nami nikaanza kuzungumza na mtu huyo kwa kujitambulisha na kusema dhumuni la kumpigia.

Aliitwa Ramadhan Hamisi huyo jamaa, akiwa ni mwenye sauti yenye amri kwelikweli, na alipouliza nimepata wapi namba yake, nikamweleza kuhusu Adelina kunipatia, nikionyesha kwamba nina ukaribu na familia ya mwanamke huyo.

Kwa sababu alitaka tuongee vizuri zaidi ana kwa ana, akaniuliza niko maeneo gani, nami nikamwambia Mbagala. Akasema sawa, naye akaniambia kwamba kesho niende kwenye kituo cha polisi kilichopo Mbagala Maturubai sijui, nikaonane naye hapo, kwenye mida ya saa tisa alasiri.

Alikuwa amesema kabisa kwamba angepita huko ili ndiyo tuonane, kumaanisha labda yeye hakufanyia kazi kwenye kituo hicho, nami nikakubali tu kisha kumuaga. La kwanza hilo nikalimaliza, na la muhimu ingekuwa kutafuta eneo la kituo hicho baadaye.

La pili, ilikuwa ni kutoa vifaa nilivyochukua hospitali pamoja na dawa, kisha nikaingia mtandaoni ili kutafuta ujuzi hususa wa kutengeneza madawa fulani. Nilikuwa najua kwa kiasi chake lakini nilitaka kujipa uhakika zaidi.

Baada ya kujua mambo niliyohitaji kufanya ili zoezi nililotaka kufanikisha likamilike, nikatunza kumbukumbu fupi kwenye simu, kisha nikaweka vifaa hivyo pembeni ili kesho niamkie kwenye matengenezo hayo ya kisayansi. Hii yote ilikuwa kwa ajili ya nia fulani niliyokuwa nimeijenga upesi sana, na mambo yangekwenda taratibu tu mpaka nifanikishe mipango yangu. Kama stelingi wa kihindi kweli!

Ankia akawa amerejea kutoka bafuni na kunishtua ili nikajimwagie pia, hivyo nikaenda kufanya hivyo na upesi kurudi ndani. Nilikuwa na mpango wa kuiwahi asubuhi ya mapema kwa kesho, kwa hiyo nilipoingia tu ndani nikafunga milango na kumtakia Ankia usingizi mnono, kisha nami nikaenda kulala.


β˜…β˜…β˜…


Asubuhi ikafika kama kawaida yake. Kweli nikawa nimeiwahi mapema kama nilivyodhamiria, nami bila kutoka nje hata mara moja nikaanza kushughulika na experiment yangu ya kisayansi kwanza kabla ya mengine kufuata.

Nikachukua ma-conical flask na kemikali, nikaichanganya na dawa zilizokuwepo na kutengeneza dawa ya mwanzo kwa ajili ya mchanganyiko niliotaka kuupata, kisha nikaiweka pembeni. Sitasema nilichokuwa nakifanya kwa undani ili wahuni wasiige, lakini kwa wajanja itakuwa wazi zaidi nilitaka kutengeneza nini nikisema kwamba ili mchanganyiko huu ukamilike, nilipaswa kuongezea na soda ya Coca cola! Hapo ishaeleweka.

Kidogo tu baada ya kumaliza mchakato huo wa mwanzo, nikamsikia Ankia akiwa ameanza kufanya usafi wa ndani, nami nikatulia tu na simu yangu nikisubiri amalize ndiyo nitoke. Nikakuta nimetafutwa na yule Winny niliyemuunganisha kwa Tesha, Soraya, Latifah, pamoja na ndugu na marafiki zangu wengine. Ilinibidi nimpigie mmoja wao ili tuzungumze kabisa, na nadhani Ankia akawa amenisikia na kutambua kwamba nilikuwa macho tayari.

Akawa amekuja chumbani baada ya muda mfupi na kunisalimia, akisema kuwa anataka kwenda kuemea vile ambavyo tungetumia kwa ajili ya kunywea chai na mboga kwa ajili ya usiku. Alitaka tu kutosumbuka kuja kufata vya usiku baadaye tena kwa kuwa alikuwa na mpango wa kwenda msibani akishamaliza kupata kiamsha kinywa, na kwa sababu sasa ilikuwa ni saa tatu hilo lilionekana kuwa wazo zuri. Kwa hiyo akaniaga na kuondoka.

Nilikuwa na mipango kadhaa ya kushughulika nayo kwa leo, binti Mariam akiwa ndiyo mpango wa kwanza. Latifah pamoja na Soraya ningewapanga baadaye, ila huyo Winny, inaonekana alikuwa amenielewa mimi zaidi hata ya Tesha kwa namna tu ambavyo alionyesha kutuma umakini wake kwangu zaidi.

Labda ni kwa kuwa tayari aliniona mubashara, kwa hiyo ingebidi kweli nimshauri Tesha akakutane naye ili aache kunisumbua. Nikawa nimechat naye kwa ufupi na kutoa kisingizio cha kwenda kazini wakati huu ili niikatishe mazungumzo naye, naye akasisitiza nimtafute baadaye.

Nikaamua kutoka hatimaye, cha kwanza ikiwa ni kwenda kujisafisha, nami nikabeba mswaki, taulo, na sabuni. Nikaenda kusafisha kinywa na mwili kwa kuoga kabisa, kisha nikarejea ndani na kuvaa nguo nyepesi. Nikatengeneza nywele zangu kichwani na kuchukua hela, moja kwa moja mpaka dukani pale nje ili ninunue soda niliyohitaji.

Wakati huu nilipofika hapo, yule mwanamke muuzaji alinisalimia kwa uchangamfu na hata kunisemesha kiasi, akiniuliza kwa nini nilipenda kukaa ndani tu badala ya kutoka hata hapo nje kuongea na wenyeji. Nikamwambia hapana, kutoka nilitoka, ila sikuwa na mazoea ya namna hiyo kwa sababu nilipotoka ilikuwa kwa ajili ya jambo fulani hususa nililokusudia kufanya; kama hivyo kuja kuchukua soda.

Akacheka kidogo na kunipa soda yangu, naye akasema kwamba toka nimefika hapo na kumwokoa Mariam siku ile, nilikuwa nimewaogopesha waume za watu eti kwa kuwa wengi wa wanawake mtaani hapo walinizungumzia sana, wakitaka mazoea, lakini kwa sababu nilionekana mkali basi hawakuweza kusogea.

Nikatabasamu kidogo tu baada ya kuelewa kwamba hata mwanamke huyu alitaka kunizoea, lakini nikamwambia ndiyo, nina ukali kwa sababu sipendi mazoea yasiyo na faida yoyote pamoja na kila mtu, kwa hiyo hata hao wanawake wakae mbali kabisa. Akacheka sana, nami nikamwacha tu japo alionekana kutaka kuendeleza mazungumzo, na alionekana kuwa mbeya kweli!

Nikarudi mpaka chumbani kwangu na kurudia zoezi langu la kisayansi. Zamu hii nikawa natenganisha virutubisho fulani ndani ya soda hiyo ili nipate nilichohitaji kwa ajili ya experiment yangu. Kwa maneno mengine, nilikuwa naiondoa 'cola' kwenye soda, ili ibaki 'coca.' Kisha baada ya kufanikiwa, nikaichanganya na ile kemikali-dawa niliyoitengeneza mara ya kwanza, na mchanganyiko wangu ukawa umemalizika.

Siyo jambo la ajabu wala, ila kama ni kuwa makini na yale niliyofundishwa, kiukweli darasani nilikuwaga vizuri. Na ni kitu ambacho kilinisaidia kwa mengi hasa nilipokuwa na nia kuu za kufanya mambo mengi muhimu. Na hii ilikuwa muhimu sana wakati huu.

Sasa kilichokuwa kimebaki ilikuwa kuikausha dawa hii, aidha kwa kuichoma na moto au ipigwe na jua, nami nikaona uchaguzi wa pili ndiyo uliofaa. Nikiwa nimeiweka ndani ya chombo chake, nikapeleka nje na kuiweka juu ya dari kabisa ili itandikwe jua kali mpaka ikauke. Nilipoangalia upande wa pili kwa jirani yetu, sikuliona gari la Miryam, hivyo nikaelewa lazima bibie angekuwa ameshakwenda kazini.

Baada ya hapo nikarudi ndani na kuingia chumbani tena kuichukua simu yangu, nami nikakuta missed call moja kutoka kwa mama yangu. Nikatabasamu kiasi na kurudi tena sebuleni, nami nikakaa sofani na kumpigia.

Alipopokea, nikasema, "Damastee..."

Sauti yake ikasikika akicheka kidogo, naye akaniambia, "Ni NamastΓ© mwehu wewe!"

"Ahahahah... mama na wahindi bwana! Ilikuwaje ukazaliwa Tanzania na siyo Mumbai?"

"Ilikuwa kwa bahati mbaya tu..." akasema hivyo.

Nikacheka kiasi.

"Ndiyo umenigaya hivyo?" akaniambia.

"Aa wee... nikugaye wewe tena? Haiwezi tokea."

"Mm... hata kunijulia hali tu mimi mama yako jamani..."

"Sorry... mambo yamekuwa mengi kidogo."

"Mambo gani? Wakati umeenda huko kupumzika?"

Ni wakati huu ndiyo Ankia akawa amerejea hatimaye, naye akiwa ameshika mfuko mkononi, akanipita na kuelekea jikoni baada ya kuona nilikuwa nazungumza kwenye simu.

"Kuna maisha huku mama, siyo kwamba nimekaa tu muda wote. Ila pole mpenzi, nimekuweka pembeni sana. Za huko?" nikaendeleza mazungumzo na mama.

"Nzuri tu. Wewe?" akauliza.

"Fresh. Kuna vitu nafanya kidogo huku angalau na mimi najiona shujaa wa kihindi kama wa tamthilia upendazo," nikamwambia.

Akacheka kidogo na kusema, "Wewe ndiyo Amitabachani kutokea zamani sana. Najua hiyo inamaanisha unatoa msaada kwa mtu. Endelea tu hivyo hivyo kusaidia watu, Mungu anapenda sana, na atakuzidishia."

"Amen," nikamwambia.

"Umeshamwona Jasmine?" akaniuliza.

"Ee ndiyo, nimemwona juzi hapa aliweka picha zake status. Aisee amekuwa bonge!"

"Ahahaha... ni kweli. Shauri ya ujauzito, na ninamwombea sana Mungu amfanyie wepesi aje kujifungua salama."

"Ishaenda hiyo mama. Jasmine atajifungua salama kabisa, afya yake iko poa," nikamwambia hivyo.

"Sawa kabisa. Halafu... kuna kitu nilikuwa nataka nikwambie," akasema hivyo.

Ankia akawa amerejea hapo pamoja na sahani iliyowekewa chapati, na vikombe pamoja na chupa ya chai. Akaviweka mezani na kisha kuelekea jikoni tena.

"Mh? Kizuri au kibaya... maana hiyo gia uliyoiingiza naielewa hahah," nikamwambia hivyo mama kwenye simu.

"Siyo kibaya... ila sijui we' ndiyo utachukuliaje," akasema.

Ankia akawa amerejea hapo tena na kopo la kutunzia sukari na kijiko, naye akaanza kumimina chai kwenye vikombe.

"Hauhitaji kuomba ruhusa mama, we' niambie tu. Kuna nini?" nikamwambia hivyo.

"Stella alikuja hapa," mama akaniambia hivyo.

Kauli hiyo ikanifanya niondoe sura nyepesi usoni na kuwa makini zaidi.

"Alikuja hiyo juzi tu hapa nyumbani. Halafu alikuja na..."

"Mama ishia hapo hapo," nikamkatisha kwa sauti makini.

Ankia akanitazama usoni.

"J..." mama akaniita kwa sauti ya kubembeleza.

"Hapana mama... tuta... tutaongea baadaye. Ndiyo nataka kunywa chai... kuna na chapati, karibu," nikasema hivyo.

Nikamwona Ankia akitabasamu na kuendelea kukoroga sukari kwenye chai.

Niliweza kuhisi mama akishusha pumzi upande wa pili wa simu, kisha akasema, "Sawa. Ukipata nafasi utanijulisha ili tuongee. Mapumziko mema."

"Haya," nikajibu hivyo, nayo simu ikakatwa.

Ankia akasogeza meza yenye chakula karibu zaidi na nilipokaa, naye akakaa sofa moja nami na kuuliza, "Mama JC huyo?"

Nikamwangalia na kutabasamu kiasi, nami nikatikisa kichwa kukubali.

"Kwa jinsi ulivyo mzuri hivi, mama yako si ndiyo mwisho?" akasema hivyo.

"Ahahah... acha mambo yako bana. Hizi ungezileta na supu, au ulikosa?" nikabadili mada.

"Hamna, sema... hela haikutosha..."

"Aaa, unazingua. Si ungeniambia? Unajua navyopenda kula chapati na supu..."

"Basi nisamehe mume wangu... sitarudia," akaongea kwa sauti ya deko eti.

"Ahahah... yaani wewe..."

Makamuzi yakaanza baada ya hapo, nami nikajitahidi kumpigisha story mwanamke huyu mbali na suala la mama yangu mzazi.

Ankia alikuwa na udadisi lakini sikutaka kupita huko kwa wakati huu, kwa sababu kuna maisha niliyokuwa nimeyaacha kwa kitambo kifupi huko nyuma na ndiyo kuja Mbagala ilikuwa kwa lengo la kuishi mengine. Sababu nilizijua mimi mwenyewe na sikutaka kuzipitia tena kwa muda huu niliokuwa likizoni, na ingetakiwa kubaki kuwa namna hiyo hiyo. Labda.

β˜…β˜…

Kwa hiyo tulipomaliza chai, Ankia akaondoa vyombo nikiwa nimemtekenya-tekenya kiasi pia, nami nikaenda chumbani kuvaa suruali na T-shirt nadhifu ili nielekee kwa mgonjwa wangu hatimaye. Nikainywa soda ya Coca cola iliyokuwa imebaki kwenye chupa na kwenda sebuleni tena.

Ankia alikuwa na mpango wa kwenda tena kule msibani hasa kutokana na kufahamiana vyema na ndugu za marehemu, na kweli ilionekana walikuwa na ukaribu maana hata Joy aliwahi kuniambia kwamba alipaona hapa kwa Ankia kuwa kama nyumbani. Kwa hiyo nilipofika sebuleni, nikamkuta hapo, naye akawa amenipatia funguo za nyumba yake za ziada.

Akasema alikuwa tu amesahau kunipa mapema lakini hii ilikuwa muhimu sana kwa nyakati ambazo tungekuwa sehemu tofauti kimaeneo, na hivyo kila mmoja wetu kuwa na funguo ingeepusha usumbufu wa kuhitaji kusubiriana. Na ilionyesha kwamba aliniamini sana.

Basi, tukaagana, akisema leo hangekawia kurudi, nami nikatoka nje na kuiangalia ile dawa niliyoweka juu ya bati. Bado ilikuwa kwenye hatua za mwanzo za kukauka, nami nikaombea wingu lisitande kama lilivyotishia kuishusha mvua usiku uliotangulia. Nikatoka hapo mpaka kufika nje kwenye geti la jirani yetu, nami nikagonga na kusubiri.

Kidogo tu na mlango wa geti ukafunguka, ikiwa ni Tesha ndiye aliyefungua, akiwa ndani ya jezi yake ya Simba na pensi ya kijani.

"Oy, oy," akaniambia hivyo kwa shauku.

"Nakuona mkali," nikamwambia.

"Karibu bro," akanikaribisha.

Nikapita na kuingia ndani hapo, nami nikaona rundo kubwa kiasi la nguo pale kibarazani, pamoja ndoo na mabeseni yaliyowekewa nguo na maji yenye sabuni. Bila shaka ni Tesha ndiye aliyekuwa akifua maana mikono yake ilionekana kulowana kiasi, na kamba za kuanikia nguo tayari zilikuwa na nguo chache zilizoanikwa.

Nikamgeukia, naye akanisogelea na kusema, "Oy furushi hilo... nina miezi sijafua."

"Ahahah... ndiyo inabidi ukomae," nikamwambia.

"Ah... kufua naonaga kero kinyama. Eh, oya... yule mtoto kichaa..."

"Nani? Winny?"

"Ee. Mwana, demu anatoa zile vibe za wale wanawake wanaofanyaga kuuzia telegram sijui?"

"Ahahahah... kweli?

"Ah, siyo poa. Jana nilikuwa namchatisha, nikawa nampanga, unajua alichosema? Eti nikitaka anipee, matunzo kwanza ni lazima, ndiyo maua atachanua!"

"Ahahah... Mbagala, tumefika Mbagala," nikamwambia hivyo kiutani.

"Ahahaaa... anaonekana anapenda sana bata, sasa me nataka nije nimmwagie laana mpaka akome!"

"Umemwelewa, eh?"

"Ah, yuko vizuri. Sema nikitaka kupanda pale ndo' kujipanga kwanza..."

"Ndo' ujipange sasa."

"Nishaanza mbona... si unaona nafua?"

"Hahah... haya bwana."

"Ngoja niumalizie huu mkasa wa nguo tuje tuongee. Mamu ameshaamka, si ndiyo unataka kwenda kuanza kumsaidia?" akaniuliza.

"Ndiyo. Mama wakubwa?" nikauliza pia.

"Wako ndani hapo. Ingia tu, nitafata," akasema hivyo.

Nikamwacha kweli akiendelea kupalangana na furushi hilo hapo nje, nami nikafungua mlango wa kuingilia ndani hapo huku nikisema, "Hodi, hodii..."

Nikawakuta mama wakubwa wakiwa wamekaa kwenye sofa walilopendelea kuketi, nao wakanikaribisha vizuri kabisa. Nikaenda kukaa sofani pia, nami nikawaamkia na wao kuniitikia vizuri tu.

"Za hapo kwenu?" Bi Jamila akaniuliza.

"Nzuri tu mama, sijui hapa?" nikamjibu hivyo.

"Kwema. Umekuja muanze mazoezi na Mamu eh?" Bi Jamila akaniuliza tena.

"Ndiyo," nikajibu.

"Yuko chumbani. Mamu... njoo..." Bi Zawadi akamwita.

"Nina hamu kubwa kuona namna utakavyomsaidia JC," Bi Jamila akaniambia hivyo.

Nikatabasamu kidogo na kusema, "Ndiyo. Mdogo mdogo tu mpaka kieleweke."

"Ahahah... umemwona mwenzio anafua hapo?" Bi Zawadi akaniuliza.

"Eeh... dah! Me kufua zote kama hivyo siwezagi yaani. Anajitahidi," nikawaambia.

"Hamna, yaani Tesha mvivu sana kufua. Anarundika nguo, matokeo ndiyo hayo, anakuja kufua zikiwa nyingi," Bi Zawadi akasema.

"Ni kitu ambacho wanaume tunacho, yaani sijui kufua tunaonaje tu!" nikasema.

"Ih, kumbe hata na wewe?" Bi Zawadi akaniuliza.

"Yeah, naonaga kero kufua. Kwa hiyo huwa situnzi nguo chafu kabisa maana kwanza sipendi uchafu ukomaze nguo. Nafua kila wiki yaani zikiwa chache," nikawaambia.

"Ee hiyo ndiyo busara. Tesha angekuwa anafanya hivyo asingekuwa anahangaika na minguo ujazo," Bi Zawadi akasema.

"Kulikuwaga na kadada alikuwa anatoka nako ndiyo kalikuwa kanakuja kumfulia. Wakawa wameachana sijui, ndiyo maana sa'hivi anasota," Bi Jamila akaniambia hivyo kwa sauti yake ya kistaarabu.

Nikacheka kidogo.

"Halafu hako kadada nilikuwa sikapendi!" Bi Jamila akaniambia.

"Ih, kweli? Kwa nini sasa?" nikamuuliza hivyo kwa njia ya kuomba nipewe ubuyu zaidi.

"Kalikuwa na nyodo kupita nyodo! Yaani kuna kipindi walikafukuzaga huko kwao sijui kwa kutoelewana, ndiyo Tesha akakaleta hapa mpaka hali itulie. Sasa kalipokaa-kaa hapa, kakawa hakasikii, hata ukikaambia kafanye hivi hakataki... kanajiona kamefika sasa, yaani hakaambiliki... mpaka Tesha mwenyewe akaja kukatimua," Bi Zawadi akaniambia.

"Aisee!" nikasema hivyo.

"Kuna wakati waliwahi hadi kusemana hapa na huyu, kisa kalimtania kwamba eti amezeeka mno kwa hiyo hafai kujitengeneza kama mwanamke kijana," Bi Jamila akaniambia hivyo.

"Aaa... jamani!" nikaonyesha mshangao wa kumpamba Bi Zawadi.

Akaweka sura yake ya deko, naye akasema, "Tena siyo kwamba alikuwa anatania. Alinisema kabisa kwamba eti mimi mzee sana, kwa hiyo hata kupaka vipodozi na lipstick hainifai. Eti mimi hapa hata namzidi mama dangote umri? Mbona ye' anajipambaga? Au kwa sababu ya kuonekana mzee basi...."

"Aliyekwambia we' mzee nani?" nikamkatisha kwa hiyo kauli.

Wote wakaniangalia kwa pamoja.

"Hivi haujui ukitembea tu hata hapo barabarani unaweza ukasababisha watu wajikwae wakikuona?" nikamwambia hivyo Bi Zawadi.

Mwanamke huyo akaachia tabasamu hafifu huku akiniangalia kwa macho yaliyoonyesha furaha, na Bi Jamila akamwangalia.

"Huyo alikuwa anakuonea gere tu. Yaani wewe kama ungekuwa na ngozi nyeusi bado ungeweza kufanya hadi magaidi wasahau bunduki kwa kukutazama, sasa ndiyo umebarikiwa kuwa mweupe yaani ndiyo kabisaa! Ungewafanya hadi wasahau na vita," nikampamba namna hiyo.

Akaweka kale kasura kake ka maringo, naye akasema, "Weewe! Unasema kweli?"

Bi Jamila akacheka kidogo kwa pumzi na kuangalia pembeni.

Nikamwambia Bi Zawadi, "Siyo kwamba kwa sababu mimi ndiyo nimesema, ila ni kwamba mpaka ukweli wenyewe unajua ni kweli. We' ni Zawadi cheupe, mrembo."

"Kumbe ni kweli, alikuwa ananionea gere," Bi Zawadi akasema hivyo kwa nyodo kabisa.

"Haya JC, ndo' umeshampa na kichwa huyu. Utakuja kumkuta amevaa suruali za Mimi," Bi Jamila akaniambia hivyo.

Sote tukacheka pamoja.

"Na sisi tulio weusi, tunakaa kundi gani?" Bi Jamila akauliza.

"Wewe ni mrembo black beauty. Hata bila makeup unang'ara sana," nikamsifia namna hiyo.

Bi Jamila akacheka kidogo na kusema, "Haya bwana, ya leo kali."

Nikacheka kidogo kwa kufurahia maongezi yetu haya yaliyokuwa yanaongeza zaidi mazoea. Bi Zawadi alipenda sana hali ya urembo kama mwanamke kijana, na inaonekana alipenda kusifiwa kwa kuwa alikuwa na mwonekano mzuri japo alikuwa na umri mkubwa.

Bi Zawadi akawa amemwita Mariam kwa mara nyingine tena, naye binti akaja sebuleni hapo baada ya sekunde chache. Alikuwa amevaa dera lile nililomkuta nalo siku ile nimefika hapa kwa mara ya kwanza, nywele zake ndefu zikiwa zimesukwa kwa mtindo wa Yebo rasta fupi, na mkononi alishikilia mdoli wenye kufanana na paka.

Mama zake wakubwa wakamwelekeza aje kukaa kwenye sofa nililokalia, naye akaonyesha kukubali japo kwa njia ya kujihami na kuja kukaa pamoja nami. Nikaanza kumsemesha vitu ambavyo nilijua asingejibu, nikimwambia mambo mengi kwa njia ya kirafiki na kwa uchangamfu ili mazoea yaanze kweli kujengeka.

Nikaanza kufanya michezo rahisi ya watoto pamoja naye, nikijaribu kumfundisha na kumkaririsha kwa kuirudia-rudia, na mama zake wakubwa walikuwa wananiunga mkono sana kwa kujumuika pamoja nasi.

Mariam akaanza kujiachia zaidi kwangu. Alipenda michezo ya 'shuadina' na 'mapera' zaidi kwa kuwa ilichezwa kwa kuimba, na tabia yake ya kupiga-piga makofi kila mara alipocheka ilionyesha furaha ya kina ndani yake. Hakuwa na maneno hususa ya kuzungumza kila mara nilipomjaribu kwa kuuliza jambo lolote upesi ili nilazimishe furaha yake imsukume aongee.

Lakini najua uwezo wa kuongea vizuri ulikuwepo, sema kwa wakati huu ulikuwa umefungwa, hata mara ya kwanza mimi kuja hapa niliita jina lake bila kukusudia na yeye akaitika kabisa, na shikamoo aliweza kuisema vizuri kabisa, kwa hiyo ndiyo ningetakiwa kuwa na subira ili mazoezi haya yaje kutia tiki mbele zaidi ya hii safari.

Tukaendelea kucheza ndani hapo, huku Tesha akija ndani mara kwa mara pia na kurudi tena kufua, na Bi Zawadi akaanza kutengeneza chakula cha mchana ilipoingia mida ya saa sita.

Wakati huu, nikawa pamoja na Mariam upande wa dining, akiwa ameleta makopo yake na vijiti ili anifundishe kupika wali. Alikuwa amechukua na mchele kabisa, akiniongoza mwenyewe ili nisije kuunguza na mboga ya majani kwenye kopo lingine, naye Bi Jamila akawa anatutazama tu huku akicheka.

Mariam alianza kunizoea upesi sana kiasi kwamba akafata mtandio chumbani na kuja kunifunika nao kichwani; sababu ikiwa kwamba na mimi ni mwanamama mpishi kwa hiyo lazima nionekane kuwa kama maman'tilie kabisa! Nami kweli nikauvaa na kuendelea kuigiza pamoja naye. Vitu nilivyokuwa nafanya hapo ndani viliwafurahisha sana mama zake wakubwa, na Mariam mwenyewe alikuwa makini kweli kwenye kuhakikisha mapishi yake "yanaiva."

Tukiwa tunaendelea na mambo yetu pamoja na binti, Tesha akawa ameingia ndani tena, lakini wakati huu pamoja na bibie Miryam. Sikuwa nimetegemea kabisa kumwona hapo muda huo, naye akamwamkia Bi Jamila na mwanamama huyu akaitikia huku akisimama kutoka sofani.

Miryam hakuwa ameniona kutokea sehemu aliyokuwa amesimama, nami katika kubaki nimemtazama, nikajisahau kwa kuwa niliondoa umakini wangu kwa binti Mariam kwa makusudi. Alikuwa akiniita kwa ishara za mikono ambazo niliziona, lakini sikuzipa umakini kwa muda huo mfupi, ndipo akanipiga begani kwa nguvu kiasi.

Nikamwangalia kwa kushangaa kidogo, nikalishika bega kuonyesha nimeumia, naye akawa ameweka sura ya kununa. Nikaweka uso wa kununa pia na kutazama pembeni, kwa njia ya utoto ili iendane na tabia yake pia.

Bi Zawadi akawa ametoka sehemu ya jikoni baada ya kusikia Miryam akiongea hapo, naye akafikia sebuleni na kumuuliza, "Mimi, vipi? Mbona umewahi, unaumwa au?"

"Hapana, nilikuwa nimeenda hapo Kongowe mara moja, ndiyo nikaona nipite. Shikamoo?" Miryam akaongea hivyo.

"Marahaba mama," Bi Zawadi akamwitikia.

"Za hapa?" Miryam akasema hivyo.

Wakati akiwa anajibiwa, Mariam alikuwa akinivuta mkono ili niendelee kupika pamoja naye, lakini nikamwonyesha kwamba nimenuna bado. Akaniacha na kwenda upande wa dada yake.

"Na Mamu amekula?" Miryam akauliza.

"Eee, chai kanywa. Huyu hapa, yuko na...."

Kabla Bi Jamila hajamaliza kuongea, Mariam akawa amemfikia dada yake na kuanza kuivuta nguo yake kwa chini huku akimwangalia kwa njia ya kukwazika. Nikaelewa tu kwamba hapo binti alikuwa anataka kunisemea, nami nikabana tabasamu langu na kuendelea kujifanya nimenuna.

"Nini Mamu? Umekuwaje?" Miryam akamuuliza kwa kujali.

Nikamwona Mariam akinyoosha kidole chake kuelekea upande wangu, nao wote wakaniangalia. Ilimbidi Miryam achungulie kiasi ili aweze kuniona, naye akaniona nilivyokuwa nimejifunika kichwa kwa mtandio huku nikionyesha madoido ya kununa.

Wengine wakaanza kutabasamu, naye Miryam akakunja uso wake kimaswali na kuniuliza, "Wewe... ndiyo unafanya nini sasa?"

Nikiwa naendelea kuigiza kimaringo, nikamwambia, "Usinisemeshe... nimenuna."

Bi Zawadi, Bi Jamila, pamoja na Tesha wakacheka kidogo na kumwangalia Miryam, naye bibie akaonekana kutonielewa vizuri na kuwatazama kimaswali.

"Wameanza kucheza na Mamu," Tesha akamwambia hivyo.

Miryam akamtazama Mariam, naye akasema, "Mamu... usiwe hivyo... kwani mmefanyaje? Mbona amekasirika?"

Nikamwangalia Mariam na kuona kweli alionyesha hisia za kuumia, nami nikatabasamu tu kidogo. Hilo kwangu lilikuwa goli la kwanza kuelekea kwenye ushindi. Binti akachukua mdoli wake na kuelekea chumbani, akionekana kukasirika kweli.

Miryam alionekana kuchanganywa sana na jambo hilo, naye akanitazama usoni tena kwa umakini. Nikatoka hapo nilipokuwa nimekaa na kuutoa mtandio kichwani, nami nikaenda waliposimama wenzangu.

"Za saa hizi dada?" nikamsalimu Miryam.

"Unafanya nini we' kijana? Umesema unataka kumsaidia mdogo wangu lakini nakuja kukuta unataka kumliza?" Miryam akaongea kwa hisia kali kiasi.

Tesha na mama wakubwa wakawa makini zaidi, nami nikasema, "Hapana Miryam... siyo unavyodhani."

"Ila nini? Me sitaki mdogo wangu ajazwe presha ya aina yoyote, nilikwambia ni ngumu kwake kwa watu ambao hajawazoea. Hii michezo haimpi faida yoyote, sioni ikimsaidia, kwa hiyo kama ni sawa kwako... nakuomba uache," akaniambia hivyo.

Wengine wakabaki kututazama kwa utulivu baada ya Miryam kuniambia hivyo. Sijui kama alikuwa ametibuliwa huko Kongowe alipotoka ama labda tu alikuwa na hasira kunielekea isiyoeleweka sababu yake, lakini njia aliyotumia kunisemesha ilionyesha kwamba alimjali sana Mariam; yaani kupita kiasi, kiasi kwamba angekuwa tayari kuondoa jambo lolote lile ambalo lilisababisha mdogo wake huyo aumie bila kujali nani wala nini.

Lakini bado hakuwa ameelewa vizuri nilichokuwa nakifanya, kwa hiyo nikaweka uso makini pia na kumwambia, "Hapana. Siyo sawa kwangu... kwa hiyo siwezi kuacha."

Kauli hiyo ikafanya wote waniangalie, kwa sababu ilianza kuonekana kuwa mabishano baina yangu na dada mtu. Hali ikageuka kuwa nzito baina yangu na mwanamke huyu, naye akanikazia macho kana kwamba alikuwa na bifu na mimi.



β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…

ITAENDELEA

β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…

Full Story WhatsApp or inbox

Whatsapp +255 678 017 280
 
MIMI NA MIMI

A Story by Elton Tonny

Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Tamaa, Hila, Usaliti, Siri, Mambo Yasiyotazamiwa

R-rated 18+

Enjoy!


β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…

SEHEMU YA KUMI NA SABA

β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…


Tesha akaona aingilie kati. "Mimi... hakuna presha wala, ndiyo wameanza tu, kwa hiyo...."

Miryam akanyanyua kiganja chake kumkatisha. "Unataka kusema nini?" akaniuliza hivyo.

"Mtoto hawezi kuanza kutembea kabla hajasimama Miryam. Na akianza kusimama, kudondoka mara kwa mara ni lazima. Lakini atatembea tu. Huoni kwamba Mariam ameonyesha kudondoka sasa hivi nilipokuwa namfundisha kutembea tena?" nikamwambia hivyo.

Miryam akabaki kunitazama tu usoni.

"Una maana gani baba?" Bi Jamila akaniuliza.

Nikamwangalia na kusema, "Tulikuwa tunacheza... nikaigiza kununa. Ameonyesha anayajua maumivu ya kihisia kwa sababu ya mimi kumnunia kwa hiyo akamfata dada yake kunisema. Japo hajaongea, lakini amenisonta kabisa, si ndiyo?"

"Eeh... ni kweli!" Tesha akasema.

"Alishawahi kufanya kitu kama hicho... toka ameanza kuumwa?" nikawauliza.

"Ha..pana... sijawahi kuona. Eti?" Bi Zawadi akasema hivyo.

"Hata mimi sijawahi kumwona hivyo. Anacheza kama mtoto lakini... anune? Amfate Miryam kusema? Ahah... eh Mungu... hiyo inamaanisha nini JC?" Bi Jamila akaongea kwa matumaini.

"Inaonyesha amenizoea haraka... na akili yake ya kuelewa hisia inavizia," nikamwambia hivyo na kumtazama Miryam.

Tesha akamsogelea dada yake na kumshika mabegani huku akisema, "Sasa je! Si unaona Mimi? JC ni hatari! Mamu ashaanza kutoa cheche, fire linakuja. Oya... nakubali sana."

Miryam akawa ananiangalia kama vile bado hajaniamini.

"Wala hata usifikiri kila siku nitakuwa nakuja kumkwaza tu... ila sasa na wewe nisaidie kwenda na muziki," nikamwambia hivyo Miryam

"Kwendaje na muziki?" Miryam akaniuliza hivyo.

"Unamfata, unamdekeza kidogo, halafu akija kuniona tena tunaendelea na michezo yetu. Taratibu tu Miryam... wala usiogope dada. Taratibu," nikamwambia hivyo kwa njia ya kirafiki.

Lakini kiukweli, alikuwa amefanya mapigo yangu ya moyo yakimbie kwa kasi sana, nisielewe sababu kuwa aidha kumhofia yeye ama tu kuhofia kumwacha Mariam bila msaada. Hii kitu ikawa mpya sana kwangu maana kuogopa halikuwa jambo lililo ndani ya mfumo wangu kabisaaa.

Mwanamke huyo akashusha pumzi ya utulivu, na ndiyo hapa nikawa nimepata nafasi ya kumwangalia vizuri zaidi. Alikuwa amevaa shati la kike la satini, lenye rangi nyekundu mchanganyiko na nyeupe kwa mtindo kama wa kumwagiwa rangi bila mpangilio, na kwa chini alivaa sketi ya blue-bahari iliyoishia magotini na kuiacha wazi miguu yake myeupee. Kichwani alikuwa amezilaza nywele zake ndefu kuelekea nyuma, huku mbele akiacha chache pembeni ya paji la uso wake. Na nakazia hili. Alikuwa mrembo sana!

Akaniangalia na kusema, "Sawa. Samahani nime..."

"Wala hata usiseme samahani. Kwani kuna mtu alijua ungekuja muda ambao nilitaka kumnunisha Mamu kwa makusudi?" nikaongea kiutani.

Mama wakubwa wakacheka kidogo, na ni hapa ndiyo simu yangu ikaanza kuita kutokea mfukoni mwa suruali yangu.

Tesha akasema, "Umeona? Si unakumbuka nilivyosema jana? Sister anatupenda mno, mpaka..."

"Kero," nikamalizia maneno yake.

Sote tukacheka kidogo, naye Miryam akatabasamu kiasi.

Nikaitoa simu yangu na kukuta mpigaji ni mke wake Chalii Gonga. Nikaitolea sauti na kuirudisha mfukoni upesi.

"Yaani ungekuwepo Mimi! Ungependa sana. JC ana vituko," Bi Zawadi akamwambia.

"Noma sana. Oy, si bado mnaendelea au Mamu kazira kimoja?" Tesha akaniuliza.

"Nitaishia hapa kwa leo. Angalau nimetikisa nyuzi ndogo," nikamwambia.

"Natamani hata mwendelee," Bi Zawadi akasema hivyo.

"Mimi... kaa basi, nanii... Zawadi anakaribia kuivisha," Bi Jamila akamwambia Miryam.

"Hapana mama... nahitaji kwenda dukani. Sijaingia huko tokea asubuhi," Miryam akamwambia.

"Ulienda Kongowe kufanya nini?" Tesha akamuuliza.

Miryam akatulia kidogo, kisha akasema, "Ni... kwa rafiki. Na... masuala ya kazi pia."

Nikamwangalia kwa uangalifu na kutambua kwamba alikuwa anadanganya ama kuna kitu tu alikuwa anaficha, na hakuwa mwongo mzuri sana huyu mwanamke japo kwa sababu watu wake wa familia walimwamini basi hilo halikuonekana wazi.

"Ngoja nikamwone huyu halafu ndiyo niende huko," Miryam akasema hivyo, akimaanisha kwenda kumwona Mariam.

Mama wakubwa wakakubali, naye Miryam akaniangalia machoni kwa njia ya kawaida. Nikampa tabasamu dogo la utakatifu, naye akanipita na kuelekea chumbani.

"Nimemaliza kufua. Nataka nikaoge, kaa sasa hapa kaka tu..."

Tesha akiwa ameanza kusema hivyo, nikamkatisha kwa kumwambia, "Hapana, ninaondoka sasa hivi. Kuna sehemu nilikuwa nimepanga kwenda."

"Ah... wapi nawe JC? Acha kuzingua..." Tesha akaniambia hivyo.

"JC, mbona ghafla? Na ndiyo namalizia kupika jamani..." Bi Zawadi akasema hivyo kwa kubembeleza.

"Usijali mrembo wangu, msosi nitakuja tu kuula. Sema... nilikuwa nimepanga kwenda sehemu hii saa saba, na ni suala la kikazi," nikamwambia hivyo Bi Zawadi.

"Eh! Bro? Ma' mkubwa kageuka mrembo wako lini tena? Tesha akaniuliza hivyo.

Sote tukacheka kidogo, naye Bi Zawadi akamwambia, "Usingekuwa unatunza minguo mingi sana ya kufua, ungejua."

"Poa basi. Kwa hiyo... vipi baadaye?" Tesha akaniuliza.

"Tutaongea. Ngoja niwahi, maana muda ushaanza kwenda. Asanteni warembo wangu, tutaonana baadaye..." nikaaga na kuelekea mlangoni.

Mama wakubwa wakaniaga pia kwa shauku yao ya kiutu uzima, naye Tesha akasema, "Oya, bado hiyo warembo inanisumbua. Kuwa makini na mimi hapa!"

Nikacheka kidogo, naye Bi Zawadi akasema, "Kwenda huko! Sisi ni warembo kweli, kusifiwa lazima."

"Mwambieni huyo!" nikasema hivyo na kisha kutoka, nikiwasikia vyema wote walipodheka kwa pamoja.

Hali ya furaha niliyokuwa nayo baada ya kutoka hapo ingepeswa kuendelea, lakini mimi mwenyewe nikaikatisha upesi kwa kuwa wakati huu nilihitaji kuwa makini. Nikaitoa simu yangu mfukoni na kumpigia mke wa Chalii haraka, nami nikatoka getini kwao Tesha na kuelekea upande wa nyumba ya Ankia.

Nikakuta geti likiwa limefungwa kabisa, hivyo nikatoa funguo na kuanza kulifungua, na simu ikiwa sikioni kusubiri huyo mwanamke apokee. Ikiwa wazi kwamba Ankia alikuwa ameshaondoka, nikaelekea tu mpaka ndani bila ya jaribu langu la kwanza kumpigia huyo mwanamke kufanikiwa, nami nikarudia kwa mara nyingine tena.

Hakupokea kabisa, kwa hiyo nikaamua kwenda nje tena kuichukua ile dawa niliyoweka darini na kurudi nayo ndani. Kichupa hicho kilikuwa cha moto mno kutokana na kuunguzwa haswa na jua, na dawa ile ikawa imekauka.

Haikuwa na utofauti sana kama tu kuanika viazi mpaka vinapogeuka kuwa mapalage. Kama hujui muulize msukuma ndiyo utajua! Isipokuwa tu haya yalikuwa ni madawa, na kukauka huku kukayafanya yawe na ule ukavu uliokithiri kiasi kwamba kama ungeyashika na kupekecha vidole, yangepukutika kabisa na kuwa kama unga. Ndiyo. Unga!

Nikayatoa kwenye hicho kifaa na kuyaweka kwenye kingine ili yapoe, kisha nikaanza kuyapukutisha kwa makusudi ili kweli yawe unga. Wakati nikiwa nafanya hivi, simu ikaanza kuita, na kwa uhakika ilikuwa ni mtarajiwa wangu; mke wa Gonga.

Nikaweka simu sikioni baada ya kupokea, na kabla sijasema lolote, sauti ya mwanamke huyo ikasikika ikisema, "Njoo Royal Village Hotel. Ndani ya saa moja uwe umeshafika."

Ka!

Nikamuuliza, "Royal Village ya wapi... Makumbusho? Sinza?"

"Acha maswali. We' si mjanja? Njoo," akasema hivyo.

"Okay sawa, haina shida. Lakini... huo muda dear. Niko Mbagala, unajua ni mbali na usafiri sometime unaweza ukazingua, bora kama ungekuwa umeniambia mapema," nikamwambia hivyo.

"Wewe njoo Royal Village. Ukifika niambie," akasema hivyo.

"Yes madam," nikamjibu hivyo kizembe.

Akakata simu.

Nikacheka kidogo kwa mguno, kwa sababu nilijua vizuri kile ambacho nilikuwa nimekusudia kufanya, na angalau mambo yalikuwa yakienda kwa jinsi nilivyotaka yaende kwa mwanzo huu. Kama kunitafuta alikuwa ameshanitafuta, ila sasa akawa amenipata, na sikuwa na mpango wa kujiondoa kwake mpaka kile nilichotaka kieleweke, kieleweke.

Nikaingia chumbani na kujitengeneza vyema zaidi, uzuri nilikuwa nimeshaoga, kwa hiyo nikavaa jeans yangu nyeusi pamoja na lile T-shirt jipya kabisa nililonunua majuzi nimeenda Kariakoo, nami nikavaa na viatu vyangu vyeupe. Nikatia kacha aliyoninunulia Tesha pamoja na saa yangu kali mkononi pia. Hapo nikawa poa. Nikaiweka dawa ile kwenye kifuko kidogo na kukikunja vizuri kabisa, ndwii mfukoni.

β˜…β˜…

Safari ya kwenda kuitafuta hiyo Royal Village ikaanza baada ya kuondoka hapo. Watu kunikazia macho lilikuwa jambo la kawaida, kwa hiyo mpaka kupanda daladala za kwenda Rangi Tatu na kupanda za kwenda Makumbusho hadi kufika huko yaani ni kama nilikuwa nimeshibishwa kwa kutazamwa.

Ah hapa jijini Dar hakuna kigeni bwana, lakini mimi sijui nilionwa tu kama nini. Usafiri haukuwa wa tabu mno kwa muda huo na kwa hilo nikashukuru Mungu tu, sikuwa nimechelewa sana; saa tisa tu na nusu nilikuwa Makumbusho tayari.

Hapo Makumbusho sasa! Kuanzia eneo hilo mpaka Sinza ndiyo moja kati ya sehemu zenye wanawake wakali vibaya mno! Siyo ule ukali wa ukali, uzuri yaani, tena ule uzuri wa nje ila tabia sasa! Ukimsemesha tu "mambo?" anakuuliza "una shi'ngapi?" Ila siyo wote, japo wa hivyo kila sehemu wapo.

Kwa hiyo kama ilivyo ada, hapo kilichokuwepo ilikuwa kuita Uber ili nipaishwe fasta mpaka kwenye hoteli aliyonitaka nifike mrembo wa Chalii Gonga, na hilo sikulikawiza. Nikabofya kwa simu yangu kutafuta Uber driver, na mmoja akawa amefika sehemu niliyokuwa nikimsubiri nje kidogo ya stendi ya Makumbusho.

Nikapanda, ikiwa ni IST ya silver, na mwendo ukaanza. Hoteli ya Royal Village ikaonekana kuwa karibu kutokana na mwendo wa haraka wa usafiri huu, nami nikafikishwa kwenye malango ya jengo hilo refu lenye maghorofa mengi na kushuka baada ya kulipa.

Nikaelekea ndani huko, kukiwa na eneo pana la kuegeshea magari kwa nje, miti-maua mengi yaliyopamba ardhi, sehemu za kupumzika kwa kukaa kwenye viti au kujilaza kwa wateja na kantini ndogo ya nje. Watu walioonekana walijiwekea mionekano yenye hadhi ya juu, magari yalikuwa mengi na ya kifahari, nami nikaishia kwenye mti mmoja ufananao na mnazi na kutoa simu yangu.

Nikampigia mke wake Chalii Gonga mara mbili bila ya yeye kupokea, nami nikaona nitulie kwanza. Kwa ufahari wa hoteli hii kwa kiasi chake, inaonekana huyu mwanamke alikuwa anataka tu kunionyesha kwamba yeye ni wa gharama sana, ama kuna jambo lingine lililokuwa likiendelea hapo lililofanya ndiyo iwe sehemu ya kuniitia. Kwa vyovyote vile, ningepaswa kuwa makini kwa kile nilichotaka kufanya, kwa sababu nilikuwa nimekuja hapa kama mtu mwingine kabisa tofauti na nilivyokuwa kihalisi.

Ujumbe ukaingia kwenye simu, nami nikatabasamu kiasi baada ya kuona ni Soraya. Alikuwa akitaka kujua ikiwa leo tungeweza kuonana, lakini sikumjibu. Hata Latifah alikuwa ameshanitafuta sana toka nimeondoka Mzinga lakini hawa viumbe niliona niwaweke pembeni kwanza; mapenzi baadaye.

Nikatoka sehemu hiyo niliyosimama na kwenda upande wa ndani wa jengo hilo, na kama ilivyo kawaida ya hoteli kubwa, hapa pia palikuwa na mwonekano maridadi sana. Watu wengi walikuwa sehemu kwa sehemu wakifanya mambo yao, nami nikatumia muda mfupi kutalii huku na kule.

Bado tu mke wa Chalii hakuwa amenipigia, hivyo nikajaribu tena kumtafuta bila ya kupata fanikio. Nikiwa nimeamua kutafuta sehemu ya kukaa kwa muda mfupi ili kusubiri, mwanamke huyo akanipigia. Nikapokea.

"Umefika?" akasikika.

"Ee, uko wapi?" nikamuuliza.

"Njoo ghorofa ya saba. Ingia room namba 101," akasema hivyo.

"Ndiyo nitakukuta humo?" nikamuuliza hivyo.

Simu ikakatwa. Khh!

Hakutaka mazungumzo marefu, au siyo? Na hiyo kitu ya kwenda ghorofa ya saba kwenye vyumba vya gharama zaidi ilikuwa inanithibitishia zaidi kwamba alikuwa anaonyesha thamani yake.

Hoteli hii ni kubwa na pana sana, yenye maghorofa mengi yenye vyumba vya maana, na kuanzia ghorofa la tano mpaka mwisho ndiyo kuna vyumba, kumbi, na huduma za gharama zaidi. Lakini haikuwa kitu ya kunitetemesha kwa lolote hata kama mwanamke huyo alikuwa anaoshea ushua wake kwangu, nami nikaelekea kwenye milango ya lifti kuchukua lifti.

Nikaingia na kukutana na mwanadada mweusi aliyevaa hijab, akionekana kuwa mfanyakazi hotelini hapo maana alivalia suti nyeusi ya kike pamoja na kitambulisho alichovaa shingoni mpaka kufikia kifuani.

Nikamwambia, "Habari yako?"

Akajibu, "Salama tu."

Alionekana makini sana, nami nikabonyeza kitufe cha namba ili lifti iendelee kupanda mpaka kufikia ghorofa ya saba. Milango ikafunga, nami nikauhisi vyema ule mvuto wa lifti inapotembea kama kawaida yake. Sikumsemesha tena mwanamke huyo na wala hatukuangaliana, lakini ghafla tu akanyoosha mkono wake kwa chini kunielekea.

Nikauangalia na kukuta umeshikilia kadi kwenye vidole viwili, yenye rangi ya shaba iliyo na ufanano na kadi za benki, nami nikamtazama usoni. Hakuniangalia hata mara moja, akiwa na uso makini kweli, nami kwa haraka nikawa nimetambua kwamba huyu alikuwa ametumwa.

"Nini?" nikamuuliza hivyo.

"Shika. Utafungulia mlango," akanijibu hivyo bila kuniangalia.

Nikatulia kidogo nikitazama kadi hiyo, kisha nikaippkea. Sikuweza kujizuia kutabasamu kiasi kwa sababu ya maigizo haya yote yaliyokuwa yanafanywa ili ionekane kama niko ndani ya himaya ya mtu fulani hatari, kama kwenye filamu vile, nami nikamtazama huyo kijakazi wa bosi aliyekuwa makini kweli utadhani Black Widow!

Lifti ilipofika ghorofa ya tano, milango ikafunguka, na mwanamke huyo akatoka. Wakaingia watu wengine pia waliotaka kuelekea juu zaidi, nami nikabaki nikimuwaza huyo mtu aliyetumwa anipe hii kadi/funguo. Sijui hata alijuaje kwamba ningeingia kwenye lifti hiyo!

Kwa vyovyote vile, haya maigizo ningesonga nayo hivyo hivyo mpaka nifike kule nilikotaka kufikia, nami kweli nikawa nimefika ghorofa la saba. Mandhari ya ndani safi kabisa na mpangilio mzuri ulipendezesha mno sehemu hiyo, nami nikaendelea kutembea mpaka kufikia bhumba namba 101.

Nilikuwa napishana na watu walioonekana kuwa na maisha haswa, lakini akili yangu ilikuwa ikikazia fikira zaidi kile ambacho kingetokea ndani ya chumba hicho ambacho nilipaswa kuingia. Nikiwa natembea, nikatoa simu yangu na kuiweka katika mfumo fulani maalumu, kisha nikailaza na kuiweka mfukoni tena. Nikawa nimefika chumba namba 101.

Hapa hapakuhitaji hodi maana funguo nilikuwa nimekabidhiwa. Ilikuwa kama kuingia chooni tu. Nikapitisha kadi ile pale ilipotakiwa kupitishwa, na mlango ukatoa sauti ya kufungua lock. Nikausukuma na kuingia ndani humo nikiwa makini sana, nami nikakuta mazingira yenye kutegemeka lakini kwa asilimia kadhaa tu.

Chumba hicho kilikuwa na mwonekano mzuri kutokana na vifaa vingi vya gharama na mpangilio wake safi, na ndani hapo nikakutana na sura mbili. Moja niliifahamu, nyingine ilikuwa ngeni. Niliyoifahamu ilimilikiwa na mke wake Chalii mwenyewe, Bertha yaani, ambaye alikuwa ameketi kwenye sofa ndani hapo kwa kukunja nne kama malikia vile.

Alikuwa amevaa nguo kama gauni lenye rangi ya kijivu lililoishia mapajani, lililoubana mwili wake kama linautesa, likiacha miguu yake myeupe wazi mpaka kufikia chini alikovaa viatu vya kuchuchumia vyenye rangi nyekundu. Wakati huu alikuwa amesuka nywele za rasta nene ambazo aliziachia zimwagikie mgongoni, na lipstick yake nyekundu ilipendezesha sana mdomo kwenye huo uso wake. Na alimfanana kweli Rose Ndauka.

Pembeni yake alisimama mtu mwingine, sura nisiyoifahamu, mwanaume mwenye mwili mkubwa na mpana sana wa mazoezi. Alikuwa mweusi, mwenye ndevu nyingi kutokea kwenye timba mpaka kidevuni. Alikuwa amevaa nguo kama mwanajeshi fulani hivi, nami nikapata picha kwamba jamaa alikuwa ndiyo bodyguard wa bibie kama siyo fuckboi!

Kiukweli haya maigizo yalikuwa ya kipuuzi sana. Watu walikuwepo ndani, lakini eti wakajifungia ili tu nifungue mlango na kuwakuta wameweka pozi. Basi tu. Nikaingia tu kitakatifu na kuanza kuwafata, lakini baunsa akanionyesha ishara ya kiganja kwamba nisimame. Nikatii.

Mwanaume huyo akanifuata na kunifikia karibu zaidi, naye akaanza kunipekua mwilini kwa kupapasa, naye akatoa simu yangu mfukoni pamoja na kile kimfuko nilichokuwa nimewekea ile dawa. Akavitazama kwa umakini na kuniangalia.

"Hayo ni madini kaka. Ikiwa unaelewa. Kila mtu ana yake, au siyo?" nikamwambia hivyo kwa ujasiri.

Akawa ananitazama kwa umakini sana, kisha akarudisha vitu vyangu mfukoni na kumgeukia malikia.

"Yuko safi," jamaa akamwambia hivyo kwa sauti ya besi nzito.

Bertha akasimama taratibu, na ni hapa ndiyo nikawa nimetilia maanani uwazi wa duara katikati ya kifua chake uliofanya matiti yake yaonekane kwa juu, na jinsi nguo hiyo ilivyoyaficha kwa chini ilikuwa kama vile imeyabeba nusu kidogo tu kuyaangusha kama uwazi huo ungeachia kidogo.

Akatembea kwa mbwembwe kiasi kunielekea, akiwa ameunganisha vidole vyake kwa mbele usawa wa tumbo, vyenye makucha marefu yaliyopakwa rangi ya blue-bahari, naye baunsa wake akasogea pembeni mwanamke huyo aliponikaribia.

"HB wa Masai huyo! Inaonekana unapenda kujiweka vizuri sana," Bertha akaniambia hivyo.

"Asante, ila siyo zaidi yako. Unajua sana kupendeza," nikamwambia.

"Mwingi sana wa maneno we' mtoto. Haya... sema haraka ulichomaanisha kwenye simu jana. Nina mambo mengi ya kufanya," akasema hivyo.

"Sawa. Kwanza... nataka kuomba radhi kwa...."

"Kwa kuniita mjinga?" akanikatisha.

"Aa.."

"Tena hicho ni kidogo, hadi ukathubutu kunitukana kwa kusema nitakalia chupa ya moto. Unakumbuka?" akaniuliza hivyo kwa sauti tulivu.

"Bertha... naomba tu..."

"Usilitaje tena jina langu, mbuzi wewe!" akaniambia hivyo kiukali.

"Samahani. Naomba unisamehe," nikaweka upole.

"Unajua kwamba ninaweza kukufanya jambo baya sana na hakuna mtu atakayekusaidia?"

"Ndiyo. Naelewa," nikamwambia.

"Hapana. Hauelewi. Haujui umegusa wapi we' mtoto. Nipe sababu nzuri... moja tu... yaani moja tu ya ni kwa nini nisiukate ulimi wako hapa sasa hivi kwa kunitukana namna ile," akaongea kwa hisia kali.

"Ndiyo maana niko hapa Be... aa... boss. Ndiyo maana niko hapa. Sitaki kugusa upande wako mbaya maana nimeelewa sasa kwamba una nguvu sana boss... sina... sitaki yaani unifanye niwe adui kwako... boss," nikajing'atang'ata kwa makusudi.

Akacheka kidogo na kumwangalia baunsa wake, ambaye naye alikuwa anatabasamu kibabe, kisha akanitazama na kusema, "Eti boss. Nani boss wako hapa? Unanifanyia kazi gani mimi we' mtoto wa mwanamke malaya?"

Nikainamisha uso, nikiwa nazuia hisia zangu za hasira kutokana na maneno yake, na ikiwa angethubutu tu tena kunirushia kashfa ya namna hiyo, ningebadilika hapo hapo haijalishi matokeo.

"Si ulikuwa unajiona mjanja? Mbona umekuja kunipigia magoti sasa?" akaniuliza hivyo.

"Kama nilivyosema... sitaki niwe adui yako. Nimejifunza. Na... najua unamkubali sana Gonga... kwa sababu zako wewe mwenyewe, maana mnajua mlikotoka na vitu mlivyoshare... ila me naweza kukupa vitu vizuri zaidi ya vile anavyoweza kukupa. Na siongelei pesa," nikamwambia.

Akatulia kidogo, kisha akauliza, "Ila?"

Nikamsogelea karibu zaidi na kusema, "Vibe."

Akacheka kwa mguno, kisha akauliza, "Sasa wewe utanipa nini mimi ambacho sijawahi kupata, ama kufanyiwa labda? Unafikiri hako kasura kako kananihangaisha mimi?"

"Usinichukulie poa kwa sababu ya sura yangu. Nikikwambia naweza kukupeleka high kuliko hata kwa msisimko unaopata kwa heroin je?"

Sura yake ikageuka kuwa makini kiasi, naye akauliza, "Una maana gani?"

"Niruhusu nikuonyeshe."

"Nionyeshe, kwani we' unaogopa nini? Nionyeshe kama we' mwanaume kweli," akaniambia hivyo kwa mkazo.

Nikatabasamu kidogo, kwa kuwa niliona wazi kwamba tayari hamu yake ya kutaka kwenda 'high' kuliko alivyozoea ilikuwa imepanda. Nafikiri kwa sababu ya mimi kutabasamu akadhani nilikuwa namfanyia masihara, kwa hiyo akaudhika na kuikaba shingo yangu kwa kiganja chake chenye vidole vyenye kucha ndefu.

"Unataka kucheza na mimi, si ndiyo?" akaniongelesha kiukali.

"Tulia. Usiwe na papara. Si unataka nikupe?"

"Ni nini hicho... nionyeshe..."

"Mazingira ya hapa hayaruhusu sana..."

"Mazingira gani unayotaka? Chooni au? Acha ujinga, nitakufanyia kitu mbaya, hivi hauni...."

Nilikuwa namwangalia tu kwa macho makini, nikiona namna ambavyo suala la madawa lilimfanya awe dhaifu sana na kutaka kuonjeshwa hata kidogo tu aliposikia nimemwambia kumpeleka juu zaidi ya 'heroin,' nami nikaona niache kumtesa.

Kutoka kwenye mfuko wa suruali yangu nikakichomoa kile kimfuko nilichokuwa nimeweka ile dawa, nami nikakiinua mbele ya uso wake, na macho yake yakakitazama kwa mkazo.

"Nini hiki?" akaniuliza.

"Niachie sasa kwanza nikwambie..." nikasema hivyo.

"Ongea kwanza! Nini umeniletea hiyo? Unafikiri me mlevi wa ugoro, au?" akaniuliza kiukali.

"Hii ni coke," nikamwambia hivyo.

Akanitazama usoni kwa umakini na kuniachia shingo. "Coke? Cocaine?" akauliza kwa sauti ya chini.

"Ndiyo. Na una makucha marefu boss! Shingo imekwanguka hapa," nikamwambia hivyo kwa kujiamini.

"Wewe... umetoa wapi hii?" akaniuliza.

"Nimeitengeneza," nikamwambia.

Akionekana kutoniamini, akauliza, "Umeitengenezaje?"

"Kama nilivyokwambia... me ni mjanja," nikasema hivyo.

Akakishika kimfuko hicho na kukiangalia kwa umakini, kisha akasema, "Hii siyo coke wewe. Na kama ni coke basi kuna sehemu unatoa. Niambie ni wapi, usijichetue eti umetengeneza. Umeinunua kwa wakala gani?"

"Najua bado huamini ila hii ndiyo point ya mimi kuja hapa."

"Kwamba utakuwa unaniuzia coke?"

"Hapana. Kwamba nitakuwa nakutengenezea coke nzuri sana bila gharama yoyote. Ndiyo faida niliyokwambia ningekupa ukiniweka upande wako," nikamwambia hivyo.

"Ahah... nani anakupa mawazo kwamba nina upande wowote ambao naweza nikakuweka wewe? Na ni nani aliyekupa wazo ufikiri kwamba nafagilia hivi vitu?"

Nikaweka uso makini, nami nikamwambia, "Nina akili pia Bertha. Nimeshakuelewa. Najua una mambo kubwa, na mimi hapa... bado niko chini chini, ndiyo maana kuwa na watu wakubwa kama wewe najua itanipa faida kama ambazo na we' nataka upate. Nina mwonekano mzuri, eh? Nina mvuto yaani halafu najua sasa kutengeneza vibe la ukweli kama hili. Nipe tu nafasi, nitakufanyia manuva, huwezi amini."

Akabaki kuniangalia kwa mkazo kiasi, kisha akasema, "Kilichokubadilisha ghafla ni nini?"

"Sihitaji mpaka kusomewa manual kuelewa maana ya kilichompata Joy. Unajua jinsi ya kutia tiki maneno yako aisee, na umetisha sana... salute. Sitaki tu na mie yanikute kama hayo ndo' maana nimejileta mapema kutoa dhabihu," nikamwambia hivyo.

Akatabasamu kwa njia ya kuhukumu, kisha akapiga hatua chache kukielekea kitanda huku akiyatazama hayo madawa kama vile amepata madini.

"Unaogopa sana kufa eh?" akauliza hivyo yule baunsa.

"Ah kufa najua nitakufa, ila sitaki kufa kama mlivyom...."

"Ishia hapo hapo," Bertha akanikatisha.

Nikatulia.

"Sitaki tena kukusikia unaongelea suala la huyo mwanamke, unanielewa?"

"Ndiyo, nimeelewa," nikamjibu.

"Wewe... ahah... una bahati sana. Yaani kwa jinsi ulivyonisemesha sjku ile nilikuwa nimepanga nikufanyie kitu kibaya zaidi ya nilichokifanya kwa huyo mwanamke. Ila naona akili imekusogea ingawa moto sikuwa nimekuwashia bado," akaniambia hivyo.

"Na ni kweli, akili imenisogea. Sitarudia. Nisamehe tena," nikamwambia.

Akanitazama usoni kwa umakini, kisha akasema, "Njoo hapa."

Nikamfata mpaka kufikia aliposimama, huku baunsa wake akiwa ametulia tu pembeni akituangalia.

"Nipe uhakika kwamba hii kitu ni OG," akaniambia hivyo huku akinionyeshea hayo madawa.

"Hauwezi kujua kwa kuambiwa. Ni tamu balaa, lakini ndo' mpaka uonje. Nilichofanya kuitengeneza ni project moja kali sana, na nimeiongezea madini kuifanya iwe nzuri kuliko kawaida. We' mwenyewe utaona," nikamwambia hivyo.

Akawa ananitazama kwa yale macho makini, na yule baunsa wake akasogea karibu nasi na kuniuliza, "Umeiwekea madini gani labda? Sumu?"

Nikatabasamu kidogo na kufungua kiganja changu kumwelekea Bertha, nikiwa namwomba anipe dawa hiyo, naye akanipatia. Nikaifungua kwa uangalifu na kisha kulamba kidole changu kimoja kidogo, halafu nikachovya kwenye hiyo dawa na kisha kuiweka ulimini mwangu.

Nilikuwa nafanya hivi huku nikitazamana sawia na mwanamke huyo aliyekuwa makini kweli, nami nikamumunya dawa hiyo na kisha kuonyesha msisimko kwa kutetemesha uso huku nimefumba macho.

Oh siyo jambo la kushangaa wala kwamba JC pia aliwahi kutumia kitu kama hiki, ingawa ulikuwa umepita muda mrefu tokea mara ya mwisho nimetia madawa ndani ya mfumo wangu, na kwa wakati huu hali ilinilazimu nifanye hivi ijapokuwa nafsi haikutaka.

Nikiwa nahisi mwili unapandisha kasi ya nguvu sana kiuchangamfu, nikamwambia Bertha, "Hakuna sumu humo. Vibe tu."

Baunsa wake akafanya kama mimi nilivyofanya pia, naye akatikisa kichwa kwa msisimko kuonyesha vibe kweli imemwingia.

"Mh! Shemeji... ni hatari," baunsa akasema hivyo.

Inaonekana walikuwa na ukaribu zaidi mpaka jamaa kumwita Bertha shemeji, na mwanamke huyo akanitazama usoni kwa umakini.

"Umeitengenezaje hivi? Yaani nimeilamba tu ikanigonga..." jamaa akaniuliza.

"Me mtu wa manuva kaka, mkemia mkemia. Hii weka kwenye ulimi, ama fizi, ama puani, hata kunani, yaani utajiona kilele cha mlima Kilimanjaro," nikasema hivyo.

Jamaa akacheka kidogo, naye akamwambia Bertha, "Kitu safi sana. Huyu white yupo vizuri kama anavyojitangaza."

"Ah, uhakika kamanda," nikamwambia hivyo.

Nilikuwa nimeanza kuhisi nguvu zikiikimbia miguu maana ni kweli kwamba niliifanya dawa hiyo iwe kali, lakini nikatulia tu ili nione itikio la mke wake Chalii.

Bertha akasema, "Tuliza makeke dogo. Unaongea sana, na mimi sipendi mtu anayeongeea mno."

"Sawa. Niko kimya. Nakusikiliza," nikamwambia.

"Kwa hiyo unaweza kutengeneza coke wewe mwenyewe, si ndiyo?" akaniuliza.

Nikatikisa kichwa kukubali.

"Sawa. Nataka nipime vitu fulani. Nitakufatilia. Kuna business naendesha kwa hiyo... kama uko vizuri namna hii... nitakuweka sehemu. Umeelewa?" akaniambia hivyo.

Kauli aliyoitoa ikanifanya nibaki kumtazama kwa umakini. Ni ile hisia unayopata unapojua kwamba unaelekea kushinda jambo fulani, lakini bado unakuwa hujui ni mambo gani yanahusika zaidi katika kuutwaa huo ushindi.

Alipoona nimekaa kimya tu, akauliza tena, "Umenielewa HB wa Masai?"

Nikatabasamu kidogo na kusema, "Nimeelewa."

"Utakuwa unanipa nachotaka kwa muda wowote napokitaka, na si umesema hauhitaji malipo?" akaniuliza.

"Ndiyo. Yote itakuwa kwa ajili yako boss," nikamwambia.

"Usiniite hivyo. Niite madam," akaniambia hivyo kibabe.

"Madam," nikasema hivyo kiutiifu.

Akanisogelea karibu zaidi na kusema, "Kuwa makini sana na unayotaka kufanya ukiwa upande wangu kijana. Nikinusa mchezo wowote wa kipuuzi..."

"Haiwezi tokea. Niamini,* nikamwambia.

"Hapana... bado sijakuamini," akaniambia hivyo.

Nikainamisha uso tu na kutulia. Alikuwa sahihi kutoniamnini bado maana nilikuwa na lengo la kumpindua vibaya mno, na pamoja na ushenzi wake wote lakini alikuwa makini, na mimi ningehitaji kuwa mwerevu kweli nikiwa nimeshajiingiza kwenye himaya yake.

Akawa ananitazama kwa njia ya kibabe kama kawaida yake, naye akasema, "Ila tutaona. Nenda. Nikikuhitaji nitakupa maagizo."

Nikatikisa kichwa kuonyesha uelewa, na yule baunsa akanitikisia kichwa kwa njia ya kuaga.

Nikageuka na kuuelekea mlango, nami nikatoka ndani ya chumba hiki kimya kimya bila kuwaangalia watu hao tena. Nikaanza kujiona kama vile nimeingia ndani ya kisa chenye uzito zaidi ya nilivyotarajia, lakini ndiyo nilikuwa na hamu kubwa ya kutaka kufika hatua za mbele zaidi ili malengo yangu yatimie.

Likizo yangu fupi ingejaa uhondo mkubwa sana ambao sikuwa nimeutarajia, na hilo lilinisisimua. Bertha angelipia kwa kifo cha Joy tu, lakini pamoja na hilo, nilikuwa nataka kuhakikisha na mambo yake mengi haramu yanaanguka pamoja naye. Na ingekuwa kwa mwendo wangu kama kawaida; taratibu.

Nikatoka kwenye jengo la hoteli hiyo na kuamua kwenda Makumbusho upesi. Safari ilikuwa moja tu ya kurudi tena Mbagala, ingawa kuwa huku kulinifanya nivutwe na wazo la kwenda kumwona mama yangu.

Sikuwa nimesahau mazungumzo yetu mapema ya leo, ambayo yalikaribia kuelekea kwenye pande ambazo sikutaka yaende kwa wakati huu, hivyo kama ningesema nipite kumsalimu mzazi wangu huenda masuala hayo yangezushwa tena na kunivuruga tu. Ndiyo. Yalikuwa ni mambo yenye kuvuruga akili ambayo nilijua ipo siku tu ningetakiwa kuja kuyapa za uso, lakini kwa sasa nilitaka akili yangu ikazie fikira zaidi yale ya kule Mbagala.

Hisia za hatia kutokana na kifo cha Joy ndiyo zilikuwa zimenisukuma kufika huku na mke wake Chalii Gonga, lakini sasa kukawa na mengine zaidi yaliyojiongeza. Mwanamke huyo pamoja na mume wake walionekana kufanya mambo mengi haramu, na mimi wala hata nisingejishughulisha nao endapo kama baadhi ya hayo mambo yasingeniathiri.

Gonga alifikiri nahusika na kifo cha Joy, na mhusika halisi alikuwa mke wake ambaye alijionyesha wazi kwangu kwamba ni yeye ndiye aliyekuwa amemuua. Sijui kwa nini tu Chalii Gonga hakuona kwamba mke wake ndiye aliyekuwa msababishi, ama labda alijua lakini na yeye alikuwa anamhofia mke wake. Sijui ni yale mambo ya kufichiana siri nyingi labda? Ama tu ni kutafuta watu wa kurushia lawama hata kama ukijua fulani ndiyo mbaya maana unakuwa huwezi kumgusa kwa sababu moja au nyingine.

Kwa vyovyote vile, wawili hao walikuwa wameuvuta umakini wangu kwao, na walikuwa wameupata kweli kweli. Lilikuwa ni suala la kuwakamata tu katika udhaifu wao na kuugeuza uwe nguvu yangu ili niitumie kuwamaliza; Chalii Gonga wanawake, na madam Bertha madawa. Kwisha kazi.

β˜…β˜…

Nikawa nimechukua usafiri wa daladala kuelekea Mbagala, na nikiwa njiani, simu yangu ikaita. Nilikuwa nimetunza jina la mpigaji kwa maandishi ya kichina, lakini nilielewa huyo kuwa askari mpelelezi Ramadhan Hamisi. Nikapokea.

Akawa ameniuliza ikiwa ningeenda kituoni muda huo kama nilivyokuwa nimemwambia, nami nikamjulisha kwamba bado nilikuwa njiani kutokea Sinza hivyo kama ingemfaa basi ningefika hapo baadaye. Akasema hakuna shida, lakini tubadili sehemu ya kukutana maana muda huu alikuwa anatoka kituoni na kwenda Temeke mara moja, kwa hiyo ikiwa ningeweza kwenda huko tungekutana na kuongea.

Nikamwambia haina shida na kumwomba anipangie sehemu hususa na kunielekeza namna ya kufika. Akaniambia atanitumia ujumbe, kisha simu ikakatwa. Wito mwingine huo niliopaswa kuitikia upesi. Uzuri ni kwamba nilikuwa na jambo fulani la kumpatia askari huyo ili aweze kuona uzito wa yale niliyotaka kufanikisha katika suala la kutafuta haki ya kifo cha Joy, na nilitaka aniunge mkono kwa hatua nilizotaka kuchukua; na hiyo ni kama tu angekuwa mwelewa maana hawa watu huwa wana mambo ya kikuda sana.

Nilikuwa nimesimama kutokana na abiria kuwa wengi ndani ya gari, mpaka tumefika maeneo ya Uhasibu ndiyo nikapata nafasi ya kukaa. Nikatoa simu yangu tena na kukuta ujumbe kutoka kwa mpelelezi Ramadhan, naye akawa amesema kwamba nichukue usafiri wa kuelekea Tandika, kisha usafiri mwingine kuelekea Kijitonyama na nishukie kituo cha Ali Maua halafu nimjulishe. Dah!

Bado nilikuwa naona kama ni ngumu kuelewa somo maana kuna kauchovu nilikohisi mwilini kalikonitaka nirudi tu Mzinga na kupumzika, lakini hiki hakikuwa kitu cha kuepuka tena. Askari mwenyewe hata nilikuwa simwelewi, mara aseme anaenda Temeke halafu ananiambia tukutane tena Ali Maua. Ila nikamjibu kifupi tu kwamba nimeelewa.

β˜…β˜…

Vuuu hazikupita dakika nyingi sana nami nikawa nimeshuka. Niliamua kushukia Sabasaba na kuvuka barabara ili nikapande daladala za Temeke. Sikuwa mkongwe bado wa haya maeneo lakini angalau nilionekana kama mwenyeji kwa kwenda moja kwa moja kwenye kile nilichohitaji.

Nikawa nimesimama ndani ya usafiri kwa mara nyingine tena, na macho yangu yalinionyesha wazi ni jinsi gani watu ndani humo walinitazama sana. Sasa unakuta kuna ile naamua kumwangalia mtu fulani moja kwa moja usoni, halafu anaangalia pembeni kidogo kama vile hana habari na mimi, kisha tena anaendelea kuniangalia akiona nimegeukia kwingine! Nakuwa nashindwa kuizuia ile hisi ya kupenda sana jambo hilo japo nimeshazoea na kuliona kuwa la kawaida.

Nikiwa naelekea Tandika, Tesha, Ankia, pamoja na Bi Zawadi wakawa wamenipigia na kunisalimu. Bi Zawadi alikuwa ananiambia ni kama vile Mariam alijihisi upweke sana pale nyumbani baada ya mie kuondoka, maana alitoka nje ubarazani kwao na kuchungulia upande wa nyumba ya Ankia ili aangalie kama nipo. Nikafurahi sana na kumwambia asiwaze kwa sababu nisingekawia sana kurudi jioni, nami ningeendelea kucheza na binti huyo.

Basi, nikawa nimefika Tandika, nikaulizia daladala ambazo zingenipeleka Kijitonyama na kuelekezwa zilipokuwa, nami nikafanikiwa kuzipata na mwendo ukaanza kuelekea huko. Nilikuwa nimeshaongea na konda, nikimwomba anishushie kituo dha Ali Maua, na mwendo wa dakika kadhaa ukanifikisha huko hatimaye.

Nikatoka kwenye gari na kusimama pembezoni mwa barabara ya lami, kisha nikampigia mpelelezi. Akapokea, nami nikamjulisha kwamba nimefika. Akaniambia nisimame hapo hapo nilipokuwa naye angenifikia. Haya. Nikatulia.

Upande wa pili wa barabara kulikuwa na uwazi zaidi uliotoshea kusimamisha biashara ndogo ndogo pamoja na pikipiki za mabodaboda. Walikuwepo boda wanne pamoja na wanawake watatu waliouza vitafunwa kama mihogo ya kukaanga, sambusa, na viazi vya kukaangwa; ingawa wenyewe walikaa pembeni zaidi.

Nikavuka barabara na kwenda upande huo, magari yakiwa yanapita huku na huko, na mabodaboda wale wakiwa wameshaanza kuwasha pikipiki kabisa, lakini nikawatuliza kwa kusema kuna mtu namngoja. Nikasimama pembeni yao, nami nikaanza kupiga nao story.

Niliongea nao kwa uchangamfu wa kadiri, nao wakaonyesha utashi wao wa kuongea pia. Nilikuwa naua muda tu, nikiwafanya wanione kuwa bonge moja la mtoto wa mjini kwa ujuzi wa mambo mengi niliyozungumzia, na ndipo gari jeupe aina ya Toyota Land Cruiser, kama tu yale ambayo watanzania tumeyazoea kuwa ndiyo ambulance, likawa limefika upande ule nilioshukia na kusimama.

Nikiwa nakisia kuwa bila shaka gari hilo lilimhusu mhusika niliyemsubiria, nikaamua kuwaacha mabodaboda wale na kuvuka barabara tena ili nilifate. Kabla sijalifikia, simu yangu ikaanza kuita, nami nikaona mpigaji kuwa huyo huyo afande. Nikapokea.

"Hello..." nikasema hivyo.

"Uko wapi?" Ramadhan akauliza.

"Ni mimi nakuja nyuma ya gari," nikamwambia.

Inaonekana alinitazama kupitia kioo cha pembeni mlangoni mwa gari, naye akakata simu.

Nikawa nimefikia mlango wa mbele upande wa dereva, nami nikamkuta mwanaume mtu mzima wa miaka ya thelathini na kitu akiwa ananiangalia kwa njia ya kawaida. Alikuwa mweupe wa kadiri, mwenye mwili mkubwa na nadhani alikuwa mrefu kunifikia. Alikuwa na kipara lakini kutokea kwenye timba aliacha ndevu hafifu kiasi mpaka kidevuni, na mavazi yake yalikuwa ya kiraia; si kiaskari.

"Habari za kazi bwana Ramadhan?" nikamsalimu.

Akiwa ananiangalia machoni sawia, akasema, "Ni nzuri. Ndiyo wewe eh?"

Nikatikisa kichwa kukubali.

"Ingia kwenye gari tuongee," akasema hivyo.

Nikazungukia upande wa pili wa gari na kuingia kukaa siti ya pembeni na askari huyu. Kiukweli nilikuwa nina msisimko kutokana na yale niliyokuwa nimepanga kufanya, na mpaka kufika hapo tayari nilikuwa nimejipanga vya kutosha kiakili ili na huyu mtu anielewe.

"Kwanza pole na kazi mkuu. Najua una mambo mengi," nikamwambia hivyo.

"Ndiyo mambo ni mengi. Kutenga muda kwa ajili ya kila kitu sometime ni ngumu, hapa pia ninahitajika kufika mahala. Kwa hiyo kama vipi hii kitu tuipe spidi," akaniambia hivyo.

"Sawa, sitakula muda wako."

"Uliniambia huyo Joy alikuwa rafiki yako?"

"Ndiyo, na... tumefahamiana kwa muda mfupi tu lakini mazoea yalikuja kiuwepesi. Najua kuingiliana kwa vitu vingi kikazi kunaweza kufanya iwe ngumu kufanikisha uchunguzi wa mauaji ya huyu mwanamke, na ndiyo maana nataka kusaidia ili kuhakikisha haki inatendeka kwake na... kwa watu wa familia yake."

"Unamjua aliyemuua?" akaniuliza hivyo.

Nikatikisa kichwa kukubali, nami nikasema, "Lakini bado sijawa na ushahidi wa kutosha. Nataka tusaidiane... mimi na wewe... mpaka aje kukamatwa na...."

"Subiri. Kama unamjua aliyemuua, niambie ni nani, sisi tutafatilia ili..."

"Hapana kaka, nisikilize tafadhali. Najua mna hizo taratibu lakini kwa hili suala mambo ni tofauti. Ona... mazingira yote yanayozungukia kifo cha Joy ni mapana sana. Yanahusisha mambo mengi ambayo ndiyo yamenifanya nikutafute namna hii. Watu waliosababisha hilo ni wakubwa, yaani wana njia nyingi haramu za kubadili hata hali mbaya kwa upande wao ziwe nzuri."

"Hakuna mtu mkubwa zaidi ya sheria. Hata awe nani lazima apewe adhabu kwa kosa la kuua. Au unataka kumaanisha tuwaogope sasa?"

"Hapana, sina maana hiyo..."

"Sasa unataka tufanye nini? Si ni bora uniambie hao ni akina nani ili wafatiliwe mpaka wabainishwe na kuchukuliwa hatua? Najua ndiyo, mazingira ya kifo cha huyo mwanamke ni tata ndiyo maana mpaka sasa hivi hata upande wetu haujapata kitu... mpaka inaweza kusahaulika. Kama unawajua na hauna ushahidi wa kutosha, nipointie wako wapi, uchunguzi ufanywe, basi."

"Lengo langu siyo kuwakamata tu kwa kifo cha Joy. Hawa watu wanajua kuficha mambo vizuri, wanaendesha mambo illegal na hakuna mtu ambaye amewagusa mpaka leo... na ninamaanisha hata maaskari pia. Wana mambo zao haramu, sehemu zao haramu, lakini sijazijua bado, kwa hiyo muda pia unahitajika siyo kuingia tu kichwa kichwa. Bwana Ramadhan... kuwakamata mtawakamata tu. Lakini mimi nataka wakomeshwe kabisa kwa maovu yote wanayofanya... waporomoke, siyo waingizwe ndani siku mbili wametoka... maana wana huo uwezo kwa sababu wako makini. Ninataka kufanya hivi... kwa njia fulani ambayo italeta matokeo mazuri baadaye, lakini ni kama tu utani-support na kuiacha iwe kama... upelelezi wetu sisi wawili," nikaongea kwa kusihi.

Alikuwa ananiangalia kwa macho yenye umakini, naye akaniuliza, "Sisi wawili? Ni njia gani unaongelea?"

Nikashusha pumzi kiutulivu, nami nikatoa simu yangu na kuanza kubofya. Nikamwekea rekodi moja ya sauti ambayo nilichukua muda ule niko kule hotelini kuonana na mke wake Chalii Gonga. Ndiyo. Muda ule niliiweka simu katika mfumo maalumu wa kurekodi sauti kabla sijaingia ndani ya kile chumba mpaka wakati nilipotoka, na ilikuwa imekula nafasi kubwa ya memory kwenye simu.

Kwa hiyo nikaanza kumsikilizisha askari huyu, huku nikielezea jinsi mambo yalivyokuwa, na nani alikuwa nani, na mimi nilijiingiza katika sakata hilo kwa sababu gani. Kuna nyakati fupi ambazo mpelelezi huyu alikuwa akitabasamu na kutikisa kichwa kuonyesha namna alivyoona jambo hili lote kuwa kama mchezo wa kitoto, lakini nikamsihi kwa bidii mpaka nikaona ameanza kunielewa. Mwishowe uamuzi wa hatamu ungekuwa wake, nami nikamuuliza kwa mara nyingine tena anaonaje kuhusu wazo hili nililokuwa nimemfikishia.

Akaniangalia tu kwa utulivu, naye akasema, "Yaani ili kuwakamata wanaharamu inabidi tuungane mkono kufanya mambo haramu pia, eh? Huoni kwamba unaweza ukajiweka hatarini?"

"Najua. Hatari ipo, lakini siyo kwangu tu, bali kuzungukia wengine naowafahamu pia. Ndiyo maana nakuomba tusaidiane ili tulimalize hili jambo kiaina bila mtu mwingine yeyote kuumia. Si unajua wakati mwingine ni vyema kutuma mwizi ili mwizi akamatwe? Ndiyo tutakachofanya mkuu," nikamwambia hivyo.

Akacheka kidogo na kutikisa kichwa, kisha akasema, "Unajiamini sana. Sawa. Nimekubali. Itabidi tuje tukutane tena ili tupange hii ishu vyema zaidi, umeelewa?"

"Kabisa. Nashukuru kwa kukubali kaka," nikamwambia hivyo.

"Mhm... sawa, lakini uwe makini. Uko vizuri pia, ungefaa hata kuwa askari."

Nikatabasamu na kusema, "Asante. Siyo mbali sana kufika huko maana hata sa'hivi niko kama askari wa mchongo."

"Eeh, naona. Ila nisije tu kukukuta siku moja unawatengenezea watu wengine madawa. Hatutaelewana," akaniambia hivyo.

Nikatabasamu kidogo na kusema, "Hamna, siwezi. Hii ni kwa ajili ya mission tu."

Akatabasamu kidogo, kisha akawasha gari lake na kusema anaelekea pande zingine kikazi kwa hiyo angeniacha eneo la Mawasiliano. Nikamkubalia, naye akatuondoa hapo.

Tukiwa mwemdoni ndiyo akapata nafasi fupi ya kuuliza majina yangu kamili na nilikotokea, nami nikawa nimemweleza yale aliyotaka kujua. Nilifarijika rohoni kwamba zoezi la kumshawishi askari huyu lilikuwa limefanikiwa, na sasa ambacho kingefuata ilikuwa ni moto tu!

Niseme nilikuwa tu na nyota nzuri, hasa kwa siku ya leo. Vita yangu dhidi ya wauaji wa Joy ingepata ushindi kwa msaada wa mtu mwenye nguvu kisheria kama askari Ramadhan, na matendo ya watu kama Bertha yangekomeshwa kimtindo kabisa. Lingekuwa ni suala la muda tu, tena mfupi sana.



β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…

ITAENDELEA

β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…

Full Story WhatsApp or inbox

Whatsapp +255 678 017 280
 
Nikweli kabisa, ukimwambia jamaa hataki kuelewa, maelezo ni mengi sanaaaaa
Unataka niandikeje rafiki yangu? "JC alikuwa sebuleni, kanyanyuka kafika mbinguni, kapigwa risasi kaamka kanunua bastola kalipiza kisasi, apalakachapalakacha, everybody goes home happy, hadithi ikaisha." Ndiyo unavyotaka?

Ni muhimu kukuambia msomaji alichofanya mhusika kabla ya tukio unalotazamia au kungojea kutokea, kwamba alikuwa sebuleni, kafikaje mbinguni? That's my flow. Respect it, or kindly lay off
 
Unataka niandikeje rafiki yangu? "JC alikuwa sebuleni, kanyanyuka kafika mbinguni, kapigwa risasi kaamka kanunua bastola kalipiza kisasi, apalakachapalakacha, everybody goes home happy, hadithi ikaisha." Ndiyo unavyotaka?

Ni muhimu kukuambia msomaji alichofanya mhusika kabla ya tukio unalotazamia au kungojea kutokea, kwamba alikuwa sebuleni, kafikaje mbinguni? That's my flow. Respect it, or kindly lay off
Mwanzoni nilikua sikuelewi ila ni homge la story lenye ihalisia,Kila tukio mbele lina maana yake.Mfano pale uliposema umetoa simu kisha ukaconect na recording.

Wengine hawawezi elewa mzee waonee tu huruma
 
Unataka niandikeje rafiki yangu? "JC alikuwa sebuleni, kanyanyuka kafika mbinguni, kapigwa risasi kaamka kanunua bastola kalipiza kisasi, apalakachapalakacha, everybody goes home happy, hadithi ikaisha." Ndiyo unavyotaka?

Ni muhimu kukuambia msomaji alichofanya mhusika kabla ya tukio unalotazamia au kungojea kutokea, kwamba alikuwa sebuleni, kafikaje mbinguni? That's my flow. Respect it, or kindly lay off
Usimuliaji wako ni mzuri sana yaani kuna namna unamfanya msomaji awe part ya hicho kisa.usisumbuke na wasio kuelewa sisi wengine tunaelewa sana flow zako sana
 
Mwanzoni nilikua sikuelewi ila ni homge la story lenye ihalisia,Kila tukio mbele lina maana yake.Mfano pale uliposema umetoa simu kisha ukaconect na recording.

Wengine hawawezi elewa mzee waonee tu huruma
Asante sana bro
 
MIMI NA MIMI

A Story by Elton Tonny

Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Tamaa, Hila, Usaliti, Siri, Mambo Yasiyotazamiwa

R-rated 18+

Enjoy!

β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…

SEHEMU YA KUMI NA NANE

β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…


Wiki moja ikawa imepita baada ya mambo hayo yote. Oh tena ni siku nane kabisa zilikuwa zimepita sasa toka nilipoanza kumsaidia Mariam na kuanza kushughulika na mke wake Chalii Gonga, yaani madam Bertha. Mambo bado yalikuwa yanakwenda taratibu, lakini nilijua tu matokeo yangekuja kwa kasi sana.

Suala la mke wa Chalii kuhusika na mauaji ya Joy niliendelea kulifungia kapuni na kufanya ionekane kwamba msiba huo ulikuwa umeshapita kwangu pia kama ilivyokuwa kwa watu wengine, na toka ile siku nimeenda kwenye ile hoteli kuonana na mwanamke huyo, hakuwa amenitafuta tena.

Najua alikuwa na mambo yake mengi labda pamoja na mume wake ambaye naye pia alikuwa amenikaushia tu toka mara ya mwisho tumeonana msibani kwa Joy, lakini nilijua angenitafuta tu. Nilielewa kwamba muda si mrefu angehitaji tu dawa kama niliyokuwa nimemtolea mfano, kwa hiyo angenitafuta tu. Na siyo kwamba nililala juu ya hilo.

Ndani ya hizo siku chache ambazo hakunitafuta, nilikuwa nimefanya experiment za ziada kutokeza madawa ya cocaine kwa kiasi kingi, ili ikitokea ameniita, niwe na jambo alilohitaji la kumpa. Lengo langu lilikuwa wazi si kwangu tu, bali na kwa askari Ramadhan. Tulikuwa tumekutana tena katikati ya wiki hiyo na kuzungumza kwa mapana zaidi.

Nilimwelewesha namna ambavyo nilitaka kujishikiza upande wa mke wake Chalii ili aniamini vya kutosha kuniweka ndani ya mambo yake haramu aliyoendesha, kisha nikishaelewa namna ambavyo mtandao wake unafanya kazi, nitumie kila njia kwa fursa ambazo ningepata ili kusomba ushahidi dhidi ya mwanamke huyo na mume wake, halafu nimkabidhi Ramadhan na maaskari wenzake ili waweze kuwaharibu wawili hao.

Na uzuri ni kwamba askari huyu alikuwa mwelewa sana, akisikiliza mawazo yangu na kuniongoza vizuri pia kwa mbinu za hivi ama vile, na jambo hilo lilibaki kuwa baina yetu sisi wawili tu; hata hakuwa amewaambia maaskari wenzake ili kweli njia hii ije kumletea faida kubwa yeye kama mpelelezi wa mauaji ya Joy.

Tukiweka hayo pembeni, upande wa pili wa vita yangu dhidi ya ugonjwa uliomsumbua binti Mariam ulianza kuonyesha kuzaa matunda mazuri. Hakukuwa na mabadiliko makubwa sana, lakini yalikuwepo baadhi ambayo yaliendelea kunipa matumaini kwamba njia niliyotumia kumsaidia binti huyu ingeleta manufaa.

Niliendelea kufanya michezo rahisi pamoja naye, na yeye alikuwa ameshanizoea mno kufikia sasa. Nilikuwa nimeanza na kumfundisha vitu rahisi kushika kama kugonga tano, kupangilia vifaa vyake vya kuchezea kwa utaratibu mzuri alipomaliza kuvitumia, nami nikawa nimeona badiliko dogo lakini lenye maana kubwa kiasi katika utendaji wake.

Kufikia sasa, Mariam akawa ameacha kutafuna-tafuna kucha zake na kutetemeka kwa kichwa kulikokuwa ni jambo la muda wote, kwa sababu akili yake ilikuwa imeanza kutafuta utulivu zaidi kupitia mazoezi tuliyofanya na hivyo nikaona hata mwili wake unaanza kutulia.

Kilichokuwepo hapa ilikuwa ni kuhakikisha naendelea kucheza naye kwa kubadilika, yaani kubadili michezo, ili mdogo mdogo tu nimsaidie mpaka apate utulivu mzuri zaidi wa kumwezesha kuongea vizuri tena na kufungua ufahamu wake wa kiakili.

Na familia yake iliniunga mkono sana, yaani hawakuwa na mbambamba. Waliamini kabisa kwamba mtoto huyu angepona tu, na hilo liliniongezea nguvu ya kuendelea kujitahidi kumpambania Mariam.


β˜…β˜…β˜…


Sasa ikawa ni siku ya Jumamosi iliyokuwa na mambo mengi yenye kuburudisha kwa sehemu hii niliyokuwa. Nilitumia muda mwingi pamoja na familia yake Mariam, nikiendelea kucheza pamoja naye na kupatana zaidi na mama wakubwa.

Ni leo ndiyo siku ambayo hatimaye Tesha alikuwa ameweza kwenda kukutana na yule Winny, na alikuwa ameshajipanga vyema sana ili aende kujilia vyake kwa mwanamke huyo. Mie nilikuwa nawasiliana na Winny bado, na kama ni kitu ambacho sikuwa nimemweka Tesha wazi ni kwamba mwanamke huyo alinitaka.

Lakini nilikuwa nikimkwepa na kuendelea kumuunga mkono Tesha ili afanikiwe kumgalagaza kisha ndiyo mengine yafuate. Ilikuwa ni heshima ya kishkaji tu kumwachia mwenzangu meza kuu aliyotaka kulia chakula, na ndiyo leo ningeona matokeo ya kumwaga jasho lake kwa huyo manze. Angenisimulia tu!

Mimi kwa upande wangu sikuwa nimejihusisha na makutano ya kimwili pamoja na mwanamke yeyote yule kwa hizo siku. Ankia alikuwa ameingia kipindi cha hedhi, kwa hiyo sikutaka kumgusa. Basi tu, ndiyo niko hivyo. Ni Latifah na Soraya ndiyo ambao niliendelea kuwapiga kalenda tu.

Latifah alikuwa analazimisha tuonane tena, Soraya yeye alikuwa anaomba tukutane tena. Wote niliwakubali lakini kwa hizi siku nilikuwa tu nimewekeza akili yangu kwenye masuala mengine muhimu zaidi, kwa hiyo tamaa za mwili nilikuwa nimeamua kuziweka benchi kwanza.

β˜…β˜…

Basi, kwa hiyo nikawa hapo na akina Bi Zawadi mpaka jioni, nasi tukiwa sebuleni pamoja na Bi Jamila, Mariam, na mwanamama mwingine ambaye alikuwa ni rafiki kwa mama wakubwa, Tesha akawa amenipigia. Ilikuwa imeshaingia saa moja kabisa na bibie Miryam hakuwa amerejea nyumbani bado; sijui alikuwa kazini ama kwenye harakati zake nyingine, alijua mwenyewe. Na kiukweli alikuwa na mambo mengi ya kivyake mno mpaka alitisha.

Namaanisha hata pale kazini kwake, Soraya aliondoka mida ya saa kumi na moja kiukawaida, kumaanisha walifunga mapema tu, lakini yeye Miryam angerudi usiku kabisa mara kwa mara. Huenda alikuwa na mikutano na watu wake wengine, nani angejua? Na mimi sikuwa mtu wa kuanza kufatilia maisha yake japo nilijihusisha na mengi yaliyohusu familia yake kwa wakati huu.

Kwa hiyo nikapokea simu ya rafiki yangu na kumsikiliza. Alikuwa ananiambia kwamba mambo yalimwendea vyema sana kwenye date yake na Winny, naye angekuja kunisimulia kila kitu kilichotokea. Ndiyo mida hii alikuwa njiani kurejea huku nyumbani, naye akasema kwamba anampitia Shadya pale kazini kwake na kuja pamoja naye.

Baada ya Tesha kuniambia hivyo, akawa amenifanya nifikirie jambo fulani. Ikanibidi nitoke nje ili nimpange kuhusiana na jambo hilo, lililokuwa linamhusu Mariam pia, naye akacheka kidogo na kusema ananiunga mkono kwa hilo. Nikamaliza kuongea naye, nami nikarudi ndani tena.

Nikawa nimewaambia mama wakubwa kuhusu ujio wa Tesha na Shadya, nami nikawahusisha pia katika jambo hilo nililotaka kufanya kwa ajili ya Mariam. Walicheka, lakini Bi Jamila akawa hana uhakika sana ikiwa ni wazo zuri. Ilikuwa ni mchezo mdogo tu niliotaka kufanya pamoja na binti Mariam mwenyewe, nami nikamhakikishia Bi Jamila kwamba mambo yangekwenda vizuri tu.

Baada ya kuwa tumekubaliana, kilichobaki ikawa ni kumpanga Mariam mwenyewe, kisha kuwasubiri wakina Tesha wafike.

β˜…β˜…

Hazikupita dakika 40 naye Tesha akawa amenipigia kuniambia ndiyo wameshukia hapo Mzinga pamoja na Shadya, na mwendo wa mguu kuelekea huku nyumbani ndiyo ulikuwa umeanza. Nikamwambia poa, kisha nikasema ajitahidi kumtembeza Shadya taratibu na wakifika tu eneo la bar ya Masai anitumie ujumbe mfupi ili nijue wamekaribia, halafu ndiyo nifanye harakati niliyokuwa nimeipanga.

Alipokata simu, nikawaambia mama wakubwa kwamba mpango wangu ungetakiwa kuanza kazi sasa hivi kwa kuwa walengwa walikaribia kufika, nao wakanipa ruhusa ya kuanza kazi. Nikamchukua binti Mariam na kwenda naye pale kwa Ankia.

Binti alikuwa anatabasamu tu kwa sababu ya kujihisi uhuru mzuri wa kuambatana nami bila ya kuelewa kikamili tulichokuwa tunaenda kufanya ndani ya muda mfupi, nami nikamfikisha sebuleni na kumkuta Ankia akiwa pamoja na mama Chande.

Rafiki yake huyo ndiye aliyekuwa mwenye kufika hapo mara nyingi zaidi ya watu wengine waliofahamiana na Ankia, na japo tulikuwa tukiongea kawaida tu, sikujenga mazoea naye kabisa. Hata kuna siku Ankia alikuwa ameniambia kwamba kuna watu waliniogopa kutokana na kuhisi sifikiki kirahisi sana, ukiondolea mbali watu wa familia yake Miryam na Ankia mwenyewe, na mimi nilielewa mmoja wa hao watu kuwa ni mama Chande pia.

Kwa hiyo hata tulipoingia hapo ndani na binti Mariam, ni salamu tu ndiyo tuliyopeana na mwanamke huyo, nami nikamwambia Ankia anifuate chumbani mara moja ili nimpange juu ya ishu fulani. Nikaendelea kumvuta mkono Mariam kuelekea chumbani kwangu huku Ankia akitufata, nasi tukakaa kitandani baada ya kuingia na Ankia akawa amesimama karibu yetu akitutazama.

"Vipi JC? Mbona umekuja na Mamu?" Ankia akaniuliza.

"Kuna mchezo nataka tufanye. Nataka kuona kama Shadya anajua kukimbia," nikamwambia hivyo huku nikitabasamu.

"Mchezo gani?" akaniuliza tena.

"Una nguo ama labda... kanzu nyeupe? Yaani nguo ndefu nyeupe?" nikamuuliza.

Akatikisa kichwa kidogo kukanusha, lakini akasema, "Labda mashuka ndiyo ninayo meupe, ila..."

"Sa' na yenyewe si ni nguo Ankia!"

"Unataka ya nini kwani?"

"Chukua ile sabuni pale, huwa ina povu jeupe linalobaki ukilishindilia kwenye ngozi. Kampake Mamu upesi halafu mvalishe shuka jeupe mwilini... mzungushie yaani... ahahah... harakisha..." nikamwambia hivyo kwa furaha.

"Nimpake wapi? Sielewi JC, mnataka kucheza mchezo gani?" Ankia akawa hanielewi.

"We' kafanye tu hivyo Ankia, utaona. Harakisha sasa!" nikamwahisha.

Ingawa hakuelewa, akatii tu na kuifata sabuni yangu chini ya meza, kisha akamshika Mariam mkono na kuongozana naye chumbani kwake. Nikawa nimetoka kwenye cha kwangu na kufika sebuleni, nami nikasimama usawa wa sofa nikiwa makini na simu yangu.

Mama Chande alikuwa akitazama tu TV, na baada ya dakika chache Ankia akawa amemtoa Mariam chumbani. Nikatabasamu baada ya kumwona binti akiwa amefunikwa kwa shuka kuanzia shingoni mpaka kufikia miguuni, likiwa limekazwa kwa kuuzunguka mwili wa binti, lakini lilimruhusu atembee vizuri tu.

Ankia alikuwa ananiangalia huku akitabasamu, naye mama Chande akamwangalia binti kimaswali. "Kulikoni tena? Anaenda wapi huyo?" akauliza hivyo.

"Mi' mwenyewe sielewi," Ankia akasema na kunitazama.

"Mamu, njoo," nikamwita binti.

Akanisogelea huku akiniangalia usoni.

"Ankia, wahi... pakaa sabuni mikononi uje umpake huyu usoni," nikamwambia hivyo.

"Usoni tena?" mama Chande akauliza.

"Ahahah... ila JC! Nimeshaona unachotaka kufanya," Ankia akaniambia hivyo.

"Harakisha sasa, ndege wako njiani, nataka tuwakamate," nikamwambia hivyo.

Akacheka kwa mguno, naye akaelekea upande wa jikoni ili kuilowanisha sabuni.

Mama Chande akaomba kujua ni nini ambacho tulitaka kufanya, nami nikamwelezea kwamba tulitaka kumfanyia Shadya kamshtukizo kadogo kwa kumtengeneza Mariam aonekane kama mzimu. Akacheka na kuanza kusimulia visa kama vya namna hiyo ambavyo alifahamu, naye Ankia akarudi akiwa amejaza mikono yake povu jeupe.

Nikamwelekeza Mariam afumbe macho yake, na baada ya binti kutii, Ankia akaanza kumpakaa usoni. Lilikuwa povu zito ambalo liliacha weupe wake usoni hata baada ya kukauka, nalo likaupendezesha kweli uso wa Mariam kwa njia ya uzimu! Yaani mzimu beautiful!

Wanawake wakawa wanacheka baada ya Mariam kufumbua macho, na ndipo Tesha akawa amenitumia ujumbe kwenye simu akisema kwamba walikuwa wamefika Masai. Ikabidi nianze kuwaharakisha wanawake hawa, nikimwelekeza Ankia sehemu niliyotaka asimame pale nje pamoja na simu yangu ili arekodi video ya kile ambacho kingetokea.

Tukatoka ndani na kwenda nje, Ankia akiwa amewapigia simu mama wakubwa pale kwao ili waje nje pia kushuhudia, lakini kwa sehemu ambayo waja wasingewaona mpaka tukio likamilike. Mama Chande akatumia akili ya kwenda pale dukani kumwomba yule mwanamke muuzaji, ambaye sasa nilikuwa nimefahamu anaitwa Fatuma, azime taa ya nje kwa kitambo kifupi kwa sababu kuna ishu tulikuwa tunataka kuifanya.

Nilikuwa nimepata support kubwa kweli ijapokuwa jambo hili lilionekana kuwa la kitoto sana, lakini nilielewa kwamba watu hawa walitaka kuona tu itikio la Shadya lingekuwaje kwenye mchezo huu tuliopanga. Bi Zawadi na Bi Jamila walitoka ndani kwao na kusimama kwenye ukuta wa uzio lao, ambapo matobo yake yaliwawezesha kuona mpaka upande wa nje wa nyumba ya Ankia kwa kiasi fulani.

Ankia akawa ametoka kabisa na kwenda kujibanza nyuma ya kibanda kidogo upande wa pili wa barabara, palipokuwa na giza kiasi, nami nikawa nimesimama pamoja na Mariam na mama Chande mwanzoni mwa geti la nyumba yake Ankia kwa kificho. Kungekuwa na wapita njia kadha wa kadha na watu mmoja mmoja waliokuja dukani kwa Fatuma, nami nikaanza kuwaona Tesha na Shadya wakikaribia eneo hili la duka. Nikamwonyesha Ankia ishara ya dole gumba kuwa aanze kurekodi.

Nikamshika Mariam mabegani na kumwambia, "Shangazi kafika Mamu. Sasa... nikikwambia nenda, anza kwenda ukiwafata, sawa Maimuna?"

Mariam mwenye kufanana na mzimu akawa ananiangalia tu usoni, na mama Chande akacheka kidogo.

Nikaona Tesha na Shadya wamekaribia zaidi, nami nikamwambia Mariam, "Haya nenda," huku nikimgeuza na kumsukuma kiasi.

Mariam akatii bwana.

Najua Tesha alikuwa ameshajiweka tayari kwa kile ambacho kingetokea, kwa hiyo alikuwa anakuja na Shadya huku wakiongea ya kwao na yeye akijifanya kama vile haelewi somo. Mariam akatoka hapo nje na kusimama usawa wa duka la Fatuma, akiwaangalia wawili hao, nasi tukiwa tunachungulia tukamwona Shadya anamsimamisha Tesha kwa kumshika mkono huku akimwangalia Mariam kwa kukodoa.

Nikamwona Tesha akimtazama Mariam huku akijifanya kushangaa, nami nikamsikia anasema, "Toba!"

Kuna wapita njia wengine waliokuwa wanatokea upande walikotokea akina Tesha, nao pia wakasimama. Sasa sijui Mariam alipata wapi hii akili. Ghafla tu binti akachomoka na kuanza kukimbia kuwaelekea! Wee! Shadya akamsukuma Tesha na kuanza kukimbia kurudi Masai!

Tesha akabaki kusimama hapo hapo huku akicheka sana, nasi tukawa tunachteka pia kwa kushindwa kujizuia. Bi Zawadi alicheka mpaka machozi kumtoka, kwa kuwa Shadya alikimbia mpaka kufikia bar ya Masai!

Mariam alikuwa ameacha kuwakimbiza baada ya mwendo mfupi, naye akaanza kurudi mpaka alipomfikia kaka yake. Sisi wengine tukatoka na kwenda nje kabisa, baadhi ya watu wakiwa wamekuja ili kujua nini kilikuwa kinaendelea maana waliona Mariam alionekana kutaka kutafuna nyama ya mtu!

Tukawaelewesha kilichotokea hapo kihalisi, na wengi wao wakacheka pamoja nasi. Ilipendeza sana kumwona Mariam akifurahia mno kioja alichokuwa amefanya, kwa sababu yeye pia alicheka kwa furaha iliyotoka moyoni. Ikambidi Tesha amkimbilie Shadya ili amrudishe huku kwa sababu alikuwa amegoma kurudi, naye akatuacha tukiwa tumesogea dukani kwa Fatuma kuiangalia video aliyorekodi Ankia.

Hakuna kitu kilichokuwa kinawaua mbavu hawa watu zaidi ya kuona jinsi Shadya alivyomsukuma Tesha na kuanza kukimbia! Bi Zawadi, Fatuma, na Ankia walicheka mno. Tena Tesha alipofanikiwa kumfikisha Shadya hapo ndiyo kicheko kikalipuka kwa nguvu zaidi. Wanawake hawa waliongea sana, Tesha akakaa chini kabisa baada ya kuiangalia video hiyo, na Mariam akawa anamwangalia Shadya na sura yake iliyotisha huku akicheka.

Shadya alikuwa anasema ameishiwa nguvu miguuni, nami nikaelewa kwamba adrenaline kwenye mwili wake ilikuwa imepanda sana muda ule amekimbia na sasa ndiyo akawa anahisi nguvu kumtoka. Dah! Nilipenda sana. Akawa ananiambia nimemfanyia kitu mbaya sana na asingenisemesha daima, nami nikamwambia ningempa pole yake kwa kufanya atimue mbio namna ile, kisha nikawaomba wote kwa pamoja tuelekee ndani ili kutuliza hali.

Tukaelekea ndani kwao wakina Tesha, Shadya akionekana kuchoka vibaya mno, naye akafikia kukaa kwenye sofa kama vile ametoka kutua mzigo mzito. Muda ule tuko nje kabisa, ni Bi Zawadi pekee ndiye aliyekuwa ametoka kwa upande huu, yaani alimwacha Bi Jamila arudi kwa yule mwanamama mgeni aliyekuwa hapo mpaka wakati huu.

Mariam akawa ameondoa lile shuka jeupe mwilini mwake lakini ile sabuni usoni pake iliendelea kuwepo. Ankia akamfatia Shadya maji ya kunywa na kumletea, naye akaanza kunywa huku mama wakubwa, Tesha, Mariam, pamoja na huyo mwanamke mgeni wakiwa wanacheka kwa kuitazama ile video.

"Ahahaha... Mamu umeua! Ona Shadya anavyokimbia kama Chaplin!" Tesha akasema hivyo, na wengine wakacheka.

Nilikuwa nimekaa tu kwenye sofa pembeni nikitabasamu.

"Wee! Kwenye hali kama hiyo unadhani hata wewe ungebaki? We' si ulikuwa unajua ndiyo maana... kwani hujaona wale watu wengine wamekimbia?" Shadya akamwambia hivyo.

"Tena siyo kukimbia tu... Shadya umenisukuma! Yaani ilikuwa ni ile 'kufa mwenyewe huko!' Ahahahah aisee!" Tesha akasema hivyo.

"Shadya, mbona hukutuambia kama uliwahi kushiriki mashindano ya marathon jamani?" yule mmama mgeni akamuuliza.

Wengine wakacheka, naye Bi Zawadi akasema, "Mwenzangu! Ona hiyo miguu ilivyopauka, yaani katimua vumbi mpaka Masai huko! Hehehee nitalala nacheka leo."

Nikatabasamu na kumwangalia Mariam usoni. Nikaanza kuona kitu fulani kwenye uso wa binti huyo. Ni kama alikuwa anajaribu kuonyesha furaha yake kwa kuongea, lakini kwa sababu ya wengine kuendelea kuzungumza akawa anasita.

Hii ikanifanya nitamani kuwaambia wengine watulie ili Mariam aseme kitu fulani, lakini hiyo ingekuwa ngumu maana najua angebaki tu kimya kama ningefanya hivyo. Ingetakiwa kitokee kitu fulani cha kumsukuma yeye mwenyewe azungumze, na nilikuwa na hamu sana ya kuona hilo linafanikiwa.

"Mwanangu, nataka ni-edit kipande kidogo hii video nirushe tiktok. Itasumbua sana," Tesha akaniambia.

"Wee! Thubutu! Tena naomba muifute," Shadya akasema.

"Hakuna kuifuta. Leo Mamu kakuweza," Tesha akasema.

"Ifute! Ankia ifute," Shadya akaongea kwa mkazo.

"Subiri kwanza... nataka Miryam aje kuiona," Ankia akamwambia hivyo.

"Ahahaha... kweli Mimi inabidi aje acheke," Bi Jamila akasema.

"Sitaki, nimesema ifute. Ifute, ifute," Shadya akasisitiza.

"Mmm... we' naye! Kwani kuna ubovu gani Mimi akija kuiona?" Bi Zawadi akamwambia.

"Eti? Kwanza si na JC amekwambia atakupa pole?" Ankia akamwambia hivyo.

"JC ni mkuda tu na ye' naye. Kama vipi unipe tu pole yangu sasa hivi, ndiyo mtakuja kumwonyesha Mimi," Shadya akaniambia.

"Sasa pole gani unataka? Hela au?" Tesha akamuuliza.

Nikatabasamu kidogo na kutoa shilingi elfu kumi, na Shadya akaonekana kufurahi kwa jinsi alivyoniangalia.

"Hee! Baba, unataka kumpa yote hiyo kisa katimua mbio?" Bi Jamila akaniuliza.

"Eti mwanangu? Hapa anayepaswa kulipwa ni Mamu, hajatumia hata stunt double na akafanya improvisation. Usimpe huyo," Tesha akasema.

Kauli yake ikanifanya nicheke kidogo.

Shadya akamwambia, "We! Mimi hapa ndiyo wa kupewa pole, ningepata presha nikaanguka je? Si mngetoa zaidi ya hii pole anayonipa? Em' leta hapa."

Akaikwapua kutoka mkononi mwangu, huku wanawake wengine wakiguna kwa njia ya michambo. Shadya akaiingiza noti hiyo ndani ya nguo sehemu ya kifua chake, huku akiwa amekunja midomo yake kwa nyodo.

Nikamwambia Tesha, "Siyo mbaya akipoza koo kidogo maana najua ni lazima liwe kavu... kakisanua ile mbaya."

Wengine wakacheka kidogo, naye Shadya akasema, "Ila wewe Mamu wewe! Kwanza si mmnawishe huo uso mwishowe tuote vinyemela usiku."

"Eeh kweli, Tesha kamnawishe mtoto basi, yasije yakamwasha machoni hayo masabuni," Bi Jamila akamwambia.

Ni hapa ndiyo tukasikia honi ya gari nje ya geti, nasi kwa pamoja tukaelewa kwamba ilikuwa ni Miryam.

"Hah! Ngoja nikamfungulie Mimi aje kucheka hapa," Tesha akasema hivyo na kuelekea nje upesi.

Hii ilikuwa ni mida ya saa tatu kasoro sasa, na Ankia akamwambia Mariam, "Twende ukanawe uso my. Miryam asikukute hivi."

Lakini Mariam akatoka upande aliokuwa amekaa karibu na Ankia na kuja kwangu, naye akakaa karibu nami huku akiniangalia kwa shauku na kunishika mkononi kwa nguvu. Nikawa nimemwelewa.

"Ih, vipi tena Mamu?" Ankia akauliza.

"Anataka dada yake amwone akiwa hivi, ndiyo atanawa baadaye," nikamwambia.

"Aaa... ili Mimi acheke vizuri? Hahahah Mariam leo umetukosha sana jamani," akasema hivyo yule mwanamke mgeni.

Tulikuwa tunasikia jinsi geti lilivyofunguliwa, gari kuingia, na kisha likafungwa tena. Baada ya sekunde chache, Tesha akawa ameingia ndani tena akiwa amebeba mifuko miwili mikubwa yenye vyakula inaonekana, na dada yake ndiyo akafuata. Wote walikuwa wanatabasamu baada ya Miryam kuingia, nami nikamtazama kwa upendezi.

Wakati huu alikuwa amesuka nywele zake ndefu kwa mtindo wa rasta zilizokwenda pande tofauti, lakini mwanzoni tu mwa kichwa chake kufikia utosini, halafu kutokea hapo ziliachwa zile laini ambazo zilimwagikia nyuma mpaka kufikia mgongoni. Alizipamba kwa kuziwekea urembo wa vidude vidogo-vidogo vyeupe kwenye kila pande ya kichwa, na mtindo huo ulimpendezesha sana kuunganisha na sura yake hapo kati ambayo ilikuwa ni nzuri vibaya mno.

Leo alikuwa amevaa blauzi laini yenye mikono mirefu iliyofanana na ngozi ya twiga, pamoja na suruali nyeusi pana ya kitambaa laini ambayo pamoja na upana wake bado umbile hilo lilichoreka vizuri. Akiwa tu ndiyo ameingia kabla hata ya kutoa salamu, akawa amemwona Mariam pembeni yangu, naye akabaki akimtazama kimaswali. Wengine wakaanza kutabasamu na kucheka, ndipo Mariam akaniachia na kumfata dada yake upesi.

Tesha ndiyo akawa amerejea hapo baada ya kutoka kuipeleka mifuko ile jikoni, naye akaanza kusema, "Yaani Mimi hauwezi...."

Nikasimama na kunyanyua kidole changu kimoja kumwelekea, kwa njia ya kumzuia asiendelee kuongea, naye akatulia. Wengine wakaona hilo, nami nikarudisha umakini wangu kwa Mariam, hivyo wote wakamwangalia.

Mariam alikuwa amemshika Miryam mikononi huku akitabasamu na kupumua haraka-haraka, naye Miryam akamuuliza, "Mamu? Mbona... umepaka nini usoni?"

Mariam akanyanyua kidole juu, akipindisha shingo yake kiasi na kuonekana akitaka kuongea, nasi wote tukawa tumebaki kumtazama kwa matarajio mengi.

"Dada... hhh... dada... nihhh... nimemkimbiza... sshangazi!"

Nilipandwa na msisimko fulani mzuri sana baada ya kumsikia binti huyo akizungumza namna hiyo. Nikamtazama Tesha na kukuta ameachama kwa kushangaa, Bi Zawadi akiwa amefunika mdomo wake kwa kiganja, Ankia akiwa ndiyo anasimama kutoka sofani kwa njia ya mshangao, na hata Shadya akasimama pamoja na Bi Jamila.

Nikamwangalia Miryam na kuona akimtazama mdogo wake aliyekuwa anacheka kwa furaha, naye akasema kwa sauti ya chini, "Umefanyaje?"

"Nimemkimbiza... ssh.. Shadya!" Mariam akajibu.

Miryam alikuwa ameshika mkoba mkononi, lakini ukamdondoka kwa kile kilichoonekana kuwa mshangao. Sote hapo tulijawa na furaha sana yaani, sikujua kiwango cha furaha hiyo kwa wengine lakini mimi hapa, nilikuwa narukaruka sana ndani ya moyo wangu.



β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…

ITAENDELEA

β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…β˜…

Full Story WhatsApp or inbox

Whatsapp +255 678 017 280
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom