Nilitengenezewa zengwe na mzazi wa mwanafunzi mpaka nikafukuzwa kazi

Makox

Senior Member
Jan 19, 2014
108
130
Ninawasalimu kwa heshima za hadhi zote ndugu zangu wa JF.
Kwa heshima kubwa ninawashukuru sana kwa mawazo yenu yote juu ya maada niliyoileta kwenu iliyosema "NILITENGENEZEWA ZENGWE NA MZAZI WA MWANAFUNZI MPAKA NIKAFUKUZWA KAZI".

Nimeona nisikae tu kimya bila kuwafahamisha kinachoendelea kama maendeleo ya ushughulikiwaji wa tatizo langu kubwa.

Niliupokea kila ushauri niliopewa na ndugu zangu wote wa Jamii forum. Aidha yapo mambo mengi mno niliyojifunza kipindi hiki cha changamoto yangu. Machache ya mambo hayo ni pamoja na kuendelea kuipambania haki yangu kwa moyo wa ujasiri, Kuamini kuwa zipo fursa nyingine zinazoweza kunifanya niendelee na maisha kama wengine wanavyoishi, Umuhimu mkubwa wa kuomba ushauri mapema, Utofauti wa mitizamo ya watu [Hatupendani], Kuwa makini wakati wa kuwasaidia watu hasa wanawake, Umuhimu wa kutenda wema [Tenda wema nenda zako, Kupuuzia baadhi ya mambo n.k.
Zipo hatua nilitakiwa nizichukua baada ya kupewa ushauri na nyie jamaa zangu, lakini napata ugumu kwa kuwa tayari nilikwisha kukata rufaa TSC Makao makuu na haijafanyia maamuzi inasubiri uteuzi wa wajumbe ambao walimaliza muda wao. Nahisi nikiendelea kufuatilia kwa njia nyingine kama kwenda kwa RASI mamlaka ya TSC itaniona nimeidharau. Hivyo nafikiri ni vema nisubiri maamuzi yao, tatizo hapa sijui kama TSC makao makuu wakitoa maamuzi je protocal itakuwa inaruhusu kuleta tatizo langu tena kwa RAS wakati nitakuwa ninatakiwa kukata Rufaa kwa Raisi?
Kuhusu kuendelea na fursa nyingine; ndugu zangu wana Jamii Forum; Mapema sana baada ya kupewa barua ya maamuzi nilipambana sana kutuliza akili ili niweze kushughulikia tatizo langu huku nikiendelea na majukumu mengine. Ninamshukuru Mungu niliweza kufanikiwa kukata rufaa ndani ya muda pamoja na changamoto nilizokutana nazo. Kwa upande wa kujikita katika shughuli zangu ndugu zangu hapa ilinilazimu nianze kubadirisha ile miradi yote niliyokuwa nikiifanya katika mazingira ya kazini iwe miradi ya mazingira mengine.
Ndugu zangu, Nilifanikiwa kwa kiasi kidogo sana kwani nilipata changamoto kubwa ya kimazingira. Niliamua niende kwenye fursa za kilimo, Nilifanikiwa kupata mashamba nikayasafisha na kuanza shughuli za kilimo kwa kuwa nina uzoefu na shughuli hizo kutokana na jamii niliyolelewa. Hapa nilipata changamoto ya migogoro ya wakulima na wafugaji, na ukosefu wa nguvu kazi. Hivyo ufanisi ulikuwa mdogo katika kilimo naamini kwa kuwa ilikuwa mara yangu ya kwanza kufanya hili.
Niwe muwazi kidogo nilichokipata kimenisaidia kuendesha familia na kufanya maandalizi muhimu ya wato wanaoendelea na masomo. (Kuna mtoto alikuwa anajiunga na masomo ya sekondari, mmoja elimu ya msingi, na nipo na mdogo wangu (Mtoto wa baba yangu mdogo) pia ninayemsaidia kutokana na changamoto za kifamilia za wazazi wake.
Ndugu wana JF, Kwa sasa nipo katika kipindi cha mpito ambacho ninaendelea kufuatilia na kusubiri majibu ya rufaa yangu. Hata hivyo nipo tayari kuendelea na majukumu hata nje ya mfumo wa Serikali, Ninao uwezo wa kufanya kazi yoyote kutokana na elimu yangu ya kazi niliyoisomea ya Ualimu. Ndugu zangu mimi ni mwalimu wa elimu ya Shahada ya kwanza, masomo yangu ya kufundishia ni Kiingereza kwa msingi na sekondari na Kiingereza, Saikolojia na Filosofia kwa vyuo vya kati. Kwa miaka yangu kumi nimekuwa nikifundisha Somo la kiingereza elimu ya sekondari kwa vidato vya 1 - 6. na matunda yangu yalikuwa ni bora sana kutokana na matokeo ya wanafunzi wengi niliowahi kuwafundisha. Pamoja na kufundisha nimeshiriki kazi mbalimbali maalumu za kitaaluma kama vile kutunga na kusahihisha mitihani mbalimbali hivyo ninazijua changamoto na njia nyingi za kutatua matatizo ya wanafunzi.
Mbali na kazi yangu zipo kazi nilizowahi kuzifanya kabla ya kuajiriwa, Kazi hizo ni kama vile Kazi za ujenzi (Kama fundi ujenzi na fundi chuma) niliifanya kazi hii kama kazi niliyoipenda nikiwa katika elimu ya sekondari baada ya kupata mafunzo kwa mafundi wa mitaani. Nimewahi kufanya kazi hii chini ya mafundi binafsi na Kampuni pia katika ujenzi wa nyumba, mifereji ya maji ya umwagiliaji, Ujenzi wa Water Intake, na Madaraja.
Nimewahi kufanya pia kazi ya Kiwandani kama mzalishaji na mwendeshaji wa mitambo katika kiwanda fulani nchini. Ufanisi wangu wa kazi ulikuwa mzuri pia.
Nikiwa kazini nje ya kazi yangu muda usio wa kazi niliwahi kujishughulisha na shughuli za biashara ya Mafuta, ufugaji, Saluni, Mazao, Kibanda cha Chipsi na mradi wa duka dogo.
Ndugu wana Jamii Forum; Ninatambua kuwa mpo ambao mnajishughulisha na shughuli mbalimbali; nimeona niyaandike haya katika ukurasa huu ili kwa yeyote atakayeweza kuguswa nami aweze kunitumia katika kuendesha shughuli zake ama hata za jamaa yake kwani nipo tu sina kazi yoyote wala tatizo la afya nikiwa na uwezo mzuri kabisa wa kufanya kazi mbalimbali kwa ufanisi mzuri.
Biashara ya pikipiki, Ndugu wana JF ili mambo yaweze kwenda ninahitaji kuwa na pesa (Mtaji) ninayoikosa kwa sasa, hivyo kuna mambo hayaendi. Nimeamua kuunza pikipiki yangu aina ya Boxer BM 150 Mali yangu, ili niweze kuendesha mambo yangu muhimu. Kwa aya hii ninawakaribisha kwenye biashara hii, kwa yeyote atakayeguswa na tatizo langu basi naomba msaada japo wa kubadirishana Chombo na fedha kwa njia yoyote ile halali. Karibu pm kwa yeyote mwenye Uhitaji.
Wakubwa wangu wa Familia hii; katika fursa ya kilimo yapo mashamba mazuri yenye ardhi nzuri na maji yakutosha, yanayofaa kulimwa kipindi cha kiangazi mazao mbalimbali natamani sana kuifanyia kazi changamoto ni mtaji. Kwa yeyote mwenye mtaji na wazo la kilimo namualika pia anaweza kunitumia kama mwendeshaji na msimamizi wa mradi huu, namhakikishia kutokujutia mradi huu kwa kuwa maeneo ni mazuri sana kwa mazao mbalimbali.
OMBI: Kwa mikono miwili, napiga magoti mbele yenu wanafamilia hii nikiwaomba Nafasi ya kazi yoyote ile iliyo halali kwa kuzingatia maelezo yangu ya hapo juu. Ninawahakikishia kuwa nipo tayari kufanya kazi yoyote ile iliyokuwa halali kwa jitihada na umakini mkubwa kwa kuzingatia mahitaji ya mwenye kazi (Bosi) nikiiheshimu kama kazi yangu mwenyewe.​
Ninatanguliza Shukrani zangu za dhati.
MUNGU AWABARIKI SANA.
 
Back
Top Bottom