Kumekuwepo na madai yanayosambaa mtandaoni kuwa makasha ya dawa za meno huwa na rangi (code) za aina mbalimbali zinazofafanua aina ya kemikali zilizotumika kutengenezea dawa hiyo.
Aidha, madai hayo yanafafanua zaidi kuwa kemikali husika ni hatari kwa afya na husababisha saratani, na kwamba makampuni yanayozalisha dawa hizi hayawezi kukupa siri hii.
Ukweli wake upoje?
- Tunachokijua
- Dawa ya meno ni bidhaa ya kisayansi inayotumiwa pamoja na mswaki kusafisha na kudumisha uzuri na afya ya kinywa na meno.
Pamoja na uwepo wa kampuni tofauti zinazotengeneza dawa ya meno, muundo wa kikemikali unaotumika kwenye utengenezwaji wake hufanana kwa kiasi kikubwa.
Kwa ujumla wake, pamoja na uwepo wa viambato vingine, dawa za meno hutengenezwa kwa kutumia maji, kemikali mbalimbali, sabuni, madini ya fluoride na rangi.
Madai ya uwepo wa kemikali sumu zinazosababisha saratani
Kwa muda mrefu sasa yamekuwepo madai yanayotoa taarifa kwamba miraba midogo unayoona chini (Sehemu ya mwisho) ya kasha la dawa ya meno ni aina fulani ya msimbo (Code) wa rangi ya dawa ya meno, inayoonesha asili ya kemikali zilizopo ndani ya dawa hizo.
Chapisho hilo linadai kuwa alama ya kijani inamaanisha kuwa dawa ya meno yote ni ya asili, alama ya bluu inamaanisha kuwa ina mchanganyiko wa viambato asilia na dawa, alama nyekundu inamaanisha ina viambato asilia na viambato vya kemikali, na alama nyeusi ina viambato vyote vya kemikali.
Chapisho hilo linaonya watu dhidi ya kutumia dawa za meno zenye alama nyeusi au nyekundu na kuwahimiza watu kuchagua dawa za meno zenye kijani kibichi au bluu.
Mojawapo ya picha ya madai hayo
Ukweli wa madai haya upoje?
JamiiCheck imefuatilia suala hili na kubaini kuwa halina ukweli.
Watoa madai haya wameshindwa kutofautisha kati ya viambato vya asili na kemikali. Kitaalamu, sio kila kemikali ni mbaya. Hata hivyo, biadhaa za asili pamoja na viambato vyake navyo pia kimsingi huwa ni kemikali.
Pia, madai haya yamebeba maelezo ya jumla pasipo kuweka wazi aina ya kemikali zinazohusishwa na kusababisha saratani.
Makampuni hayaweki alama kwenye sehemu ya mwisho ya kasha la dawa ya meno kwa miraba yenye rangi kama sehemu ya kuhada watumiaji.
Alama zenye rangi hizo huwekwa ili kurahisisha zoezi la utengenzaji wa dawa husika kiwandani. Alama hizo husaidia vitambuzi vya mwanga kutambua mwisho wa makasha hayo, ili mashine zinazotumiwa kutayarisha makasha zijue mahali pa kukata na kufunga dawa hiyo.
Kwa lugha za viwandani zinazotumika kwenye uzalishaji wa bidhaa mbalimbali, alama hizi hufahamika kama Eye Marks au Colour Marks, sehemu zinazotoa utambuzi kwa mashine ili bidhaa husika iweze kukatwa na kufungwa inapokuwa inatembea kwenye mashine. Alama hizi huhusisha bidhaa zilizoungana, ambazo huhitaji kukatwa ili kuzitenganisha.
Madai haya yaliwahi pia kukanushwa na Snopes, taasisi inayojihusisha na uhakiki wa taarifa pamoja na kampuni ya Colgate inayozalisha mojawapo ya bidhaa hizo.
Ufafanuzi mwingine wa madai haya uliwahi pia kutolewa kwenye mtandao wa Facebook, Julai 19, 2019 na Dr. Sohail Khan na Februari 17, 2020 kwenye Mtandao wa Linkedin.
Unawezaje kufahamu viambato vya dawa ya meno?
Kama ilivyo kwa vyakula na dawa, maelezo ya viambato vya biadhaa hizi hupatikana kwenye sehemu ya maelezo ya "Ingredients", ambapo kampuni na wazalishaji huwajibika kisheria kuwajulisha watumiaji viambato vilivyotumika katika kutengeneza bidhaa husika.
Mfano wa Maelezo ya Viambato (Ingredients) vya dawa ya meno ya Colgate.Pamoja na uwepo wa viambato vingi vinavyotumika kwenye utengenezwaji wa dawa ya meno, wataalamu wa afya hushauri matumizi ya dawa za meno zenye kiambato cha Fluoride ili kuongeza uimara wa meno.