JamiiTalks
JF Advocacy Team
- Aug 7, 2018
- 631
- 960
JamiiForums imepata wasaa wa kuongea na Dr. Chris Mauki, Mtaalamu wa Saikolojia, Ndoa na Mahusiano, Malezi na Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam juu ya suala hili la Kataa Ndoa, mjadala ambao umekuwa mkali sana hasa kwa vijana wa zama hizi, twende kazi....
SWALI: Ndoa ni nini? Je, ni suala la Kisaikolojia?
JIBU: Ndoa ni muunganiko wa mwanume na mwanamke, ampao muunganiko huu unaweza ukawa umeunganishwa kiimani, kijamii, kimilia, kiserikali, lakini pia wote tunajua kwamba ipo sheria kwamba unapokaa na mtu wa jinsia ya tofauti kwenye nyumba yako zaidi ya siku 90 mkiwa na mahusiano ya kindoa basi inakuwa mmeona.
Pamoja na kuwa ndoa ni suala la kibaiolojia, kwasababu inahusisha vitu vya kibaiolojia ikijumuisha suala la ngono, pamoja na kwamba ndoa inahusisha pia suala la kisaikolojia ya kwamba ndani kuna mambo ya hisia, kuchukuliana kihisia, hisia za kuumia, hisia za furaha, na vitu kama hivyo, lakini pia ndoa ni jambo la kiimani. Wale wanaoamini kwenye Imani wanazungumza kwamba ndoa iliasisiwa na Mungu mwenyewe, alivyosema sio vyema mtu awe peke yake na hata ukiangalia Imani nyingi kabisa zinaonesha watu hao wa Imani zile kwamba Mungu alikuwa chanzo cha ndoa.
Sasa muundo wa ndoa unakuja kutofautiana na mwandamu anavyoendelea kijamii, nk.
Sio lazima, kwasababu kuna baadhi ya imani ambazo watu wa Imani hizo viongozi wao hawaoi, ingawa inaanza kwenda kwenye mjadala sasa kwamba labda waruhusiwe kuoa kwasababu tunaona kwamba kuna vitendo vinavyohusika wao kufanya ambavyo kama vinalazimisha kutaka kuwa na mahusiano lakini hawana mahusiano hayo kirasmi.
Inawezekana siyo lazima lakini ni muhimu, hoja iko wapi ya kwamba ni muhimu kuwa na ndoa. Hoja ni kwamba alivyoumbwa mwanaume ndani yake amewekewa uhitaji wa kihisia na uhitaji wa kibaiolojia ambaye hakuna wa kutumiza au wa kumtosheleza isipokuwa mwanamke, na ndani ya mwanamke alivyoumbwa kwa asili yake amewekewa mahitaji ya kihisia na mahitaji ya kibinadamu, yaani ya kibailojia ambayo hakuna wa kuyatosheleza isipokuwa mwanaume.
Baada ya hayo mahitaji ya kibaiolojia yakaja mahitaji mengine – Mahitaji ya Kijinsia, ambayo haya yanatokana na tamaduni na maisha ya watu tofauti tofauti ambayo wameyafanya, yakafanya sasa mwanaume amuhitaji mwanamke, na mwanamke amuhitahi mwanaume. Kuna jamii ambazo mwanaume hawezi kuishi peke yake mpaka apate mtu wa kumpikia, maana yake ni kwamba inabidi aoe, kuna jamii ambazo manamke hawezi kuishi peke yake mpaka apate mtu wa kumhudumia mahitaji yake maana yake itabidi apate mwanaume.
Kwahiyo ukifikiria utakuja kugundua kwamba hata kama siyo lazima, kwasababu kuna watu ambao hawajaoa na hawaolewa na hawafi lakini ni muhimu sana kuwa na mwenza. Sasa kwenye kutosheleza haya mahitaji ya kihisia na kibaiolojia mtu anaweza kuwa na mwanamke tu bila ndoa au anaweza kuwa na ndoa. Unapokuwa na mwanamke bila ndoa mahitaji hayo utayatimiza kabisa lakini kijamii bado watu wataona siyo halali wewe kuwa na huyo mtu, ni mpaka uwe na ndoa. Sasa ndoa ni chombo cha kuhalalisha yale mahusiano ya mwanamke na mwanaume ili jamii pamoja na Imani ifahamu kabisa kwamba unaishi na yule mtu.
Swali: Je, malezi (Trauma kwenye Makuzi na Malezi) yanaweza kuchagia mtu Kuchukia/Kupenda wazo la kuoa?
Jibu: Ni kweli kwamba maumivu yoyote ya kihisia au nafsi katika makuzi yam toto wakike au wakiume (kitaalamu Trauma) inaweza ikachangia kuharibu mtazamo wa mtu kwenye kuingia katika mahusiano pamoja na ndoa?
Wako watu leo wameshindwa kuingia kwenye mahusiano na ndoa na hata walipojaribu meshindwa na kutoka. Wale walioingia nao kwenye ndoa hawakuwahi kujua ni nini lakini wanaona kabisa hakuwa sawa na alikuwa hapendeki na wengine jinsi unavyojaribu kumpenda sana na unashindwa kwasababu hapendeki ndio maana watu wana matatizo ya kisaikolojia yanayoitwa “Dismissive attachment Disorder”, yaani jinsi unavyompenda ndio jinsi anavyokuumiza kwasababu ndani yake aliumizwa akiwa mdogo. Picha yake ya mahusiano na ndoa ilikuwa mbovu katika hali ambayo imeharibu mtazamo wake wa mahusiano. Kwahiyo ni ngumu yeye kukubali mahusiano au kuingia kwenye mahusiano pampja na ndoa, n ahata katika nyakati atakazojikuta kaingia basi mafanikio yake au kukaa kwenye hayo mahusiano yake kutakuwa kudogo.
Trauma hizi zinaweza kusababishwa na vitu kama kubakwa katika umri mdogo tunasema kisaikolojia kwenye umri wa miaka 2 mpaka 12, kuishi katika familia (ndoa) ambayo ilikuwa katika magomvi sana kati ya baba na mama, kukosa mahusiano mazuri ya baba kwa hasa kwa mabinti (father-daughter relationship) kumsaidia kwenye kujiamini nk, lakini pia kuona ndoa au kukaa na ndoa iliyovunjika (wazazi waliotengana) katika umri mdogo pamoja na malezi ya mzazi mmoja (single parenting) yenye changamoto, sababu kuna malezi ya mzazi mmoja yanaweza yasiwe na changamoto lakini kwa kiasi kikubwa malezi ya mzazi mmoja yanaweza kuwa na changamoto yakamfanya mtoto wa kike au wa kiume akaumia hisia zake, akabalisha mtazamo wake kuhusu mahusiano na ndoa kwahiyo kesho na keshokutwa akawa na mtazamo hasi sana kuhusu ndoa na mwisho ikaathiri uwezo wako wa kuingiz, kukaa, kufanikiwa na kufurahia ndoa
Swali: Je, utandawazi unachangia vipi kwenye suala hili la vijana kukataa/kukubali ndoa?
Jibu: Kubadilika kwa maendeleo ya kijamii na maendeleo ya kiteknolojia (sayansi ya teknolojia) kunachangia kwa kiasi kikubwa sana. Utandawazi umechangia kwa kiasi kikubwa, utandawazi umewafungua na kuwaweka watoto wengi na vijana wengi kwenye urahisi wa kufikia na kupata hamu au haja ya tendo landoa au kufikia mshindo kwa mambo mengi. Teknolojia imeleta midoli, mashine, uwezekanao au urahisi wa kumpata mwanamke wa kulala naye kwa siku moja au kwa dakika chache kutoka kwa wanaoitwa Malaya (sex workers) wanaofanya kazi za kujiuza, ambapo kuna watu wa miaka 45, 50, nk hajaoa lakini ana uwezo wa kufanya ngono kila anapotaka kwasababu anawanunua kwa bei rahisi tu .
Kwahiyo maendeleo ya kijamii na maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia hasa katika utandawazi kuna baadhi ya vitu vimekuja vimethiri kwa kiasi kikubwa mitazamo ya watu au watu kuona ndoa ni muhimu, lakini kingine kibaya zaidi ni kwamba utandawazi umerahisisha na kuweka bayana taarifa nyingi za watu wanaolaumu, kuua, na kukejeli, kuonesha waliyoumizwa kwenye ndoa. Kwahiyo jamii kubwa inaanza kupata picha kwamba ndoa siyo kitu tena cha furaha, bali ndoa ni kitu cha maumivu n ani kitu cha kukwepa na baadhi ya mitazamo hii hasi ndio zimehusika kuchangia sana kuku ana kuongezekakwa spidi kwa jamii la LGBTQAI+
SWALI: Peer pressure/Mtandaoni/Jamii inaweza kuwa sababu ya kufanya vijana Kuchukia/Kupenda ndoa?
JIBU: Swali la msukumo wa makundi (peer pressure) linajibuwa na swali nililojibu hapo juu, kwamba watu wengi ambo ni wa rika la kufanana unapoona kwamba wengi wanatoka kwenye ndoa, unapoona kwamba wengi wanalaumu mambo ya ndoa au mahusiano, unapoona kwamba wengi wanakuonesha kwamba kuwa na mwanaume mmoja sio dili tafuta hela, au unapokuwa na mwanamke mmoja hufurahii (huinjoy) na wewe inakushawishi vilevile kutokana na nadharia mbalimbali kama za Albert Bandura - social learning theory zinaonesha kwamba watu wengi wanajifunza kwa kuiga, kwa kuona (modeling imitation) wanaona na kujifunza mwishowe wanakuwa hivyo hivyo.
Lakini pia unaonawaona watu wa rika lako kwa jinsi ambavyo alikuwa kwenye ndoa na kutoka, au alikuwa kwenye mahisano nab ado yupo lakini akaamua kubadilisha jinsia yake, kitendo hiki cha kuona watu wengi unaofanana nao, au wa umri wako au watu unaowajua wameenda kwenye mtazamo fulani kunashawishi kwa kiasi kikubwa na wewe kuchagua mtazamo ule au maisha yale kwasababu unaona kwamba hayo ndio maisha ya kuishi. Kwahiyo ni kweli kabisa kwamba awatu wa rika moja kwa namna ambayo wana mtazamo hasi katika ndoa inachangia sana watu wengi kuona ndoasiyo kitu cha kufurahisa tena kama ilivyokuwa zamani ambapo watu wengi walikuwa wanajivunia sanakuishi na kusubiri ndoa zao.
Je, nini maoni yako kwa haya machache aliyotueleza Dr. Mauki?
Itaendelea.....
Pia soma:
- Mjadala kwa wanaokataa Kuoa (Ndoa)
- Mjadala kwa wanaokubali kuoa (Ndoa)
======
Kwa muendelezo wa mahojiano haya soma: Dr. Chris Mauki vs Kataa Ndoa 2: Feminists wanachangia kwa kiasi kikubwa watu kukataa ndoa. Kwa bahati mbaya sana asili haitakaa ibadilike!