SoC03 Kuelekea mapinduzi ya kilimo na maendeleo ya mkulima

Stories of Change - 2023 Competition

Igokoi Dawili

New Member
Jun 12, 2023
1
1
Kwa miongo mingi sasa kilimo kimekuwa uti wa mgongo wa Taifa letu, si ndani tu bali tumeweza kuwa na akiba ya mazao na kuuza pia kwa nchi jirani, haya yamekuwa yakitangazwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari nchini.

Kwa sehemu kubwa mapinduzi ya kilimo nchini yamechelewa au yapo katika hatua ambayo yanaenda kwa mwendo wa kobe, hii ni kutokana na zana duni zinazotumika katika uzalishaji. Hili limechangia kwa kiasi kikubwa kuwa na uzalishaji mdogo na kwa sehemu mabadiliko ya tabia ya nchi ambayo tumeyashuhudia kwa kasi sana nchini na duniani kwa ujumla yamesababisha kiwango cha uzalishaji kuzidi kuwa chini.

Japokuwa mkulima ni kama uti wa mgongo wa uchumi wa Taifa, mchango wake umeonekana kuwa hafifu sana ukilinganisha na sekta nyingine ambazo zinachangia pato la uchumi kwa Taifa. Naweza kusema ndiyo maana kilimo kimeonekana kuwa ni kitu duni na watu wengi haswa vijana kuwa na upofu wa kuona fursa zilizopo kwenye sekta ya kilimo.

Kilimo kina changamoto nyingi kama zilivyo sekta zingine na wakulima wanajitahidi sana kukabiliana nazo. Kwa kipindi kirefu sasa kilimo kimekuwa hakina tija kwa mkulima kutokana na changamoto mbalimbali. Wakati wa masika ni kipindi ambacho mkulima huwa na ari mpya ya kuuendea msimu wa kilimo na hutumia nguvu nyingi sana kufanya uzalishaji iwe ni kimwili, kiroho na kiakili pia. Mavuno yanapofika mkulima hujawa na uso wa matumaini kwa kile kidogo alichozalisha anaweza kupata fidia ya muda, nguvu na sehemu ya uhai wake aliotumia wakati wa msimu wa kulima. Kitu cha kustaajabisha ni pale anapokutana na watu wanaojidhania kuwa ni werevu kuliko yeye, wenye ujanja mwingi kama sungura kuliko yeye, watu wasiojali utu na thamani ya muda, nguvu na sehemu ya maisha ya mkulima. Kwa jina linalotambulika na wengi watu hawa ni walanguzi, wanaokwenda mashambani na kuwanyonya wakulima nguvu kazi zo walizozitoa kwa jasho.

Kuna umuhimu wa kuwa na taasisi au bodi ya wakulima ambayo itaratibu na kusimamia upangaji wa bei kwa mazao husika na itaratibu namna ya uuzaji mazao hayo kuanzia hatua ya kwanza kabisa yakiwa shambani. Hii itamsaidia mkulima kujua gharama alizotumia kwenye uzalishaji na kipato anachokipata kupitia mazao aliyolima. Mathalani kinachotokea kwa mkulima mazao yake yakiwa shambani ni kulazimishwa kuuza mazao yake kwa bei ya chini sana na wapangaji wa bei hizo wakiwa hawajulikani. Mkulima kwa sababu anataka kupata pesa ya kuikimu familia yake na mazao yake yasiharibike shambani akapoteza utu wake, nguvu zake na thamani yake, mwisho wa siku anaamua kufanya maamuzi magumu na ya kuumiza moyo ya kuuza mazao yake kwa bei yeyote inayokuja mbele yake. Hatimaye mkulima huyu kwa sababu kipato chake hakikidhi mahitaji anabaki kuwa kama mtu aliyevuliwa nguo mbele za watu na kukosa nguvu za kuchutama. Mkulima hubaki na aibu hiyo maana baada ya muda kidogo ataanza kuhamaki kutafuta chakula kwa ajili yake na familia yake. Na mzunguko hurejea tena na tena kila mwaka na hayo ndiyo maisha ya mkulima Mtanzania masikini.

Napongeza jitihada nyingi zinazofanywa na Serikali yetu tukufu haswa Wizara inayosimamia sekta ya kilimo. Serikali kuzuia uuzaji wa mazao nje ya nchi ni hatua nzuri sana lakini haimsaidii mkulima kwa sababu sio yeye anayeuza mazao nje ya nchi. Nafikiri namna sahihi ya kumsaidia mkulima ni kwenda kwenye mzizi wa tatizo ambalo linaanza kwenye bei ya mazao yakiwa shambani, kwa maana mkulima hulanguliwa mazao yake kwa bei ya chini sana isiyo na thamani wala yenye kuleta tija.

Ni vizuri Serikali ikaunda mfumo ulio rasmi wa kuweka bei elekezi tangu mazao yakiwa shambani. Bei hizo zipangwe kwa kuwashirikisha wakulima kupitia taasisi au bodi za wakulima ambao watakuwa ni sehemu ya wakulima wavuja jasho, watakaojadili na kuja na mapendekezo ya bei ambayo inaendana na thamani ya kilimo wanachofanya. Baada ya hayo yote kufanyika ndipo wanunuzi wafanya biashara ya mazao wanaweza kwenda shambani wakiwa tayari wanafahamu bei ya kununulia mazao hayo. Hii ni sawa tu na mtu anayeenda kituo cha mafuta kwa ajili ya kununua mafuta ya gari lake akiwa anafahamu anapesa kiasi gani na mafuta kiasi gani anayokwenda kununua.

Aghalabu tumeona Serikali ikikaa kitako na sekta nyingine muhimu kwa uchumi wa nchi na kujadili namna sahihi ya upangaji wa bei ya bidhaa husika, lengo likiwa ili mwananchi wa kawaida asiumie na mtoa bidhaa asipate hasara. Hili pia linaweza kufanyika kwenye sekta ya kilimo ili kuweza kuongeza pato la Taifa kupitia kilimo, kuboresha maslahi ya mkulima na kutanua fursa zaidi na uwekezaji katika sekta hii.

Si hivyo tu lakini pia sheria inaweza kuundwa inayolinda na kuratibu masuala ya kilimo, ambapo kwa upande wetu tumekuwa tukiongozwa na Sera ya Kilimo. Sheria tulizonazo za masuala ya ardhi zimeongelea ardhi kwa ujumla, masuala ya umiliki na umilikishwaji, urasimishaji, uhifadhi na utunzaji wa mazingira. Sheria kama (The Village Land Act, Land Act CAP 113&114, Land Registration Act, Environmentak management Act 2004). Hatuna sheria rasmi inayoratibu masuala ya kilimo yenye lengo la kukuza kilimo, kuinua wakulima kwa kanuni na taratibu zitakazokuwepo kwenye sheria hiyo. Uuundaji wa sheria hii itafanya sekta ya kilimo kuwa rasmi haswa sio tu kwa manufaa ya Taifa lakini pia kwa mkulima mmoja mmoja. Ikizingatiwa kwamba eneo kubwa la nchi yetu imezungukwa na ardhi yenye rutuba ambayo inahitaji mambo yawekwe sawa ili kutumika kikamilifu.

Kwa mantiki hii, kwa kufanya hivyo Serikali itakuwa imechukulia jambo hili la sekta ya kilimo kwa uzito ili pale kunapotokea maendeleo ya kilimo yaweze kwenda sambamba na maendeleo binafsi ya mkulima. Hii itamfanya mkulima kuongeza juhudi na ubunifu kufanya kilimo chenye tija. Kilimo kinakuwa ni uti wa mgongo ambao utawavutia wengi kufanya uwekezaji na kuongeza uzalishaji wa mazao, kwa ajili ya maslahi ya Taifa na wakulima kwa ujumla.
 
Umesema vizuri, tena vizuri sana. Lakini wazia pia hii ambayo huenda ndio ajenda unayopenda iwekwe sawa.
Mkulima wa mpunga ambaye ananufaika na soko la nje kwa kuwepo kwa ushindani mkubwa wa bei, jambo linalopelekea kupanda kwa mchele katika soko la ndani, serkali kupitia malalamiko ya wafanyakazi ambao wanategemea mchele wa mkulima wanaishikiza serkali kuzuia soko la nje ili kusiwe na kupanda kwa bei, na serkali kwa kuwasikiliza inazuia,bei inaporomoka maradufu.

Mara nyingi soko la bidhaa huongozwa pia na soko la dunia au uhitaji wa bidhaa yenyewe( demand). Kama serkali inazuia kuuza nje basi soko la ndani liendane na soko la nje, au inapotangaza kununua mahindi serkali isinunue bei ambayo iko chini ya soko la nje.

Nakubaliana na walanguzi kununua mashambani ,lkn naamini katika ushindani kama mlanguzi akienda na bei ndogo wakulima hawawezi kumuuzia maana wanajua kuwa watauza kwa mlanguzi mwingine.

Kama ulivyosema sekta ya kilimo ni uti wa mgongo lkn hakuna mtu anatamani aifanye kwasababu haina faida, maana mkulima anapotoka shambani mazao yake yanaanza kuwekewa bei na mtu mwingine apendavyo. Leo bei ya kilo ya mahindi mtaani kwetu Kijichi ni sh 1,500 hiyo ni sawa na sh 150,000 kwa gunia la kilo mia . Huenda mkulima ameuza gunia hilo kwa sh 100,000, hivyo mlanguzi pamoja na ushuru atauza bei hiyo, lkn kama Kenya na nchi jirani wakija kununua mahindi hayo mkulima atauza 150,000.

Kuhusu bodi ni sahihi lkn wasomi watatumia nafasi ya kuwapiga wakulima . Hili nisiseme maana imetokea taasisi moja imejadili bei ya zao la mkulima na kuamru walipwe pasipo wao kujua wala kuwepo uhuru wa kujadili bei mbele yao
 
Back
Top Bottom