SoC02 Dhana ya adhabu kwenye mfumo wetu wa elimu

Stories of Change - 2022 Competition

mesahani6129

New Member
Jan 11, 2020
1
2
Ndugu wasomaji, salaamu.

Elimu ni zana muhimu sana katika kupigana na adui ujinga. Elimu inatupatia maarifa ambayo hasa ndicho kila mtu hukitafuta.

Elimu inapatikana katika mifumo rasmi na ile isiyo rasmi. Mifumo rasmi ni kwa maana ya shule ambako kunakuwa na mihutasari na miongozo mbalimbali katika utoaji wa elimu hiyo. Na mifumo mingine isiyo rasmi hasa kwenye jamii (ndugu, jamaa na marafiki wanaotuzunguka).

Katika andiko hili, ninajikita zaidi katika mifumo yetu rasmi ya elimu kuanzia ngazi ya awali hadi elimu ya juu. Nitaangazia baadhi ya kasoro ambazo hakika zinakuwa na tafsiri tofauti na uhalisia au maisha halisi tunayoishi.

Lengo kubwa linalotufanya tuende shule ni kutafuta elimu ili ndani yake tupate maarifa. Maarifa haya yatusaidie kurahisha kazi na kutatua changamoto mbalimbali. Wakati mwingine tunashindwa kuona madhara ya moja kwa moja ya elimu wanayopata wanajamii wetu kwa sababu mbalimbali kama vile;

(i) kuiga mifumo ya elimu ya kizungu isiyoaksi uhalisia wa maisha yetu.
(ii) tafsiri hasi ya neno adhabu katika utoaji wa elimu.

Nitaelezea masuala haya kwa upana kidogo.

Kuiga mifumo ya elimu ya kizungu isiyoaksi uhalisia wa maisha yetu.
Tumekuwa tukitumia mifumo ya elimu ya mkoloni tangu hapo awali. Hata mabadiliko kadhaa ya mitaala yanayofanywa bado hayaendi mbali na mifumo hiyo na haigusi maisha na uhalisia wa jamii husika. Mitaala mingi inamwandaa mtoto aweze kuajiriwa. Ndiyo!

Ni elimu inayomweka mbali zaidi na jamii yake kuliko hapo awali. Nirejee mifano hii:
Tumezaliwa na wazazi wetu ambao wengi ni wakulima, wafugaji, wafanyabiashara, madaktari nk. Katika makuzi yetu ya awali, wazazi wetu walilenga kutufundisha namna ya kutengeneza/kuandaa chakula cha kuku au mifugo mingine.

Tungelitakiwa kwenda shule kujifunza njia bora zaidi za kufuga, kulima, kuvua, tiba na mambo mengine ili tunaporudi tufanye kwa ubora zaidi ya vile walivyofanya/wanavyofanya waliotutangulia. Lakini leo hii tunapeleka watoto shule wakasomee kilimo ili waje kuagiza vyakula vya mifugo kutoka nchi za nje.

Tunapeleka watoto shule wanarudi hawawezi hata kulisha mifugo wakati ni kazi iliyowapa kipato wazazi wao na wakaweza kuwasomesha kupitia kazi hiyo.

Tunazalisha vijana ambao leo hii ukiwaambia hakuna ajira wanawaza kukupiga mawe kwa sababu wanakuona kama mchawi usiyependa maendeleo yao. Kwa sababu ni moja ya maneno yaliyowahamasisha kusoma kwa bidii. "Ukisoma kwa bidii, utafaulu vizuri na utakuwa na kazi nzuri." Ni baadhi ya kauli za kutia moyo na ushawishi kutoka kwa walimu na wazazi wetu. Waliamini matunda ya elimu ni ajira tu, hakuna kingine.

Hivyo, vijana hawana njia mbadala zaidi ya ajira. Ni vijana ambao kufanya kazi za kilimo kwao ni ADHABU na siyo hadhi yao kabisa.

Tafsiri hasi ya neno adhabu katika utoaji wa elimu.
Katika makuzi yetu tumekuwa tukipewa adhabu pale tunapokosea. Adhabu inaweza kuwa kazi anayopewa mtoto kama onyo pale anapofanya kinyume na maelekezo ya jambo fulani. Tulipokuwa shuleni tulipewa adhabu au kushuhudia wanafunzi wenzetu wakitekeleza adhabu mbalimbali kama vile;

  • Kufyatua tofali,
  • Kulisha mifugo,
  • Kusafisha mabanda ya mifugo,
  • Kufyeka viwanja na maeneo ya shule,
  • Kuchimba mashimo ya taka, choo nk,
  • Kung'oa visiki,
  • Kujenga mabanda ya mifugo, vichanja, vizimba nk.

Mambo yote haya ni mafunzo ambayo ndani yake kuna elimu kubwa vijana walikuwa wanapatiwa. Lakini kwa kuwa ni elimu iliyofunikwa na mwamvuli wa neno adhabu, hawakupata fursa ya kujifunza zaidi ya kutekeleza.

Lakini huwezi kulima bila kufyeka shamba, huwezi kuwa mfugaji wakati hujui kuandaa chakula cha mifugo.

Wapo watu wanayaishi mambo waliyoyafanya kama adhabu kwenye maisha yao ya leo.

Mifano halisi:
Rafiki yangu Medo anaishi maisha mazuri kupitia kazi ya kufyatua tofali. Baada ya kuhitimu masomo, maisha ya kitaa yalimpokea tofauti na alivyoahidiwa shuleni. Ajira zilikuwa ngumu na ushindani ulikuwa mkubwa.

Akaamua kuanzisha mradi wa tofali. Anasema alikumbuka shuleni aliwahi kupewa adhabu ya kufyatua tofali 1,000 za tope baada ya kufanya kosa. Uongozi wa shule ulimwambia achague kufayatua au kufukuzwa. Alichagua kufaytua tofali.

Alianza kwa ugumu na baada ya miaka miwili akawa na mtaji akajiimarisha zaidi. Mpaka sasa ana miaka zaidi ya kumi na anamiliki mashine kadhaa za kufyatua tofali, magari ya kusomba mchanga na maisha yanaenda vizuri.

"Niliwahi kumchukia mwalimu aliyenipa adhabu kipindi kile mpaka nikamwombea kwa Mungu afe nipumzike. Mungu alinisamehe, kwa sasa namwona kama mwalimu aliyenionyesha njia. Nilimpelekea zawadi ya tofali 1,000 za block siku alipositafu, kisha nikamkumbusha adhabu aliyonipatia na jinsi ilivyonisaidia. Alifurahi sana", anaeleza Medo.

Rafiki yangu Kusaka ni mjasiliamali anayefuga kuku pale Dumila, Morogoro. Nilipomtembelea miaka kadhaa baada ya kuhitimu masomo yetu nilishangaa kukuta banda kubwa la kuku zaidi ya elfu tano anaomiliki. Nilipatafursa ya kuongea nae kwa kina.

"Baada ya kuhitimu elimu ya juu bwana Mesahani, nilitafuta kazi kila ofisi sipati.", anaendelea kusimulia.

"Nilichoka na kukata tamaa. Niliishiwa hata nauli ya kuzunguka kwenye usahili ambao niliamini ungeweza kunipa ajira. Nilikuwa na kishikwambi changu nilichonunua chuo kwa pesa ya mkopo niliamua kukiuza na kurudi kijijini".

Anaendelea kusimulia, "kijijini hali ilikuwa mbaya zaidi maana kila niliyekutana nae alijua nimefeli. Nilijaribu kuwaelezea lakini haikusaidia. Nilipojaribu kuomba vibarua pia walininyima. Waliniambia siwezi kazi maana mimi ni msomi. Ndugu zangu walikata tamaa. Wazazi wangu walidhihakiwa kwa sababu yangu kwa kuwa wazazi walinisomesha kwa kuuza mashamba".

"Baba yangu aliniambia nijaribu kufuga kuku maana ni shughuli aliyoifanya kwa muda mrefu. Alinipatia jogoo moja na majike kumi nikaanza. Nilikuwa naingia pia mtandaoni (google) kujifunza zaidi. Leo hii ninauzoefu mkubwa sana kwenye ufugaji wa kuku.

Huwezi kunidanganya kitu maana hata wasomi wengi wanakuja kujifunza hapa kwa vitendo. Nimetengeneza ajira nyingi kwa jamii yangu mpaka sasa. Nimejenga, nina familia, ninalima pia kupitia mradi huu..."

Ni ushuhuda kutoka kwa bwana Kusaka.
 
Back
Top Bottom