Watoto wa Kazi Kazini: Ona Stories na Historia ya Bibi Titi

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
21,948
32,056
VIJANA WA KAZI KAZINI: ONA STORIES NA HISTORIA YA BIBI TITI MOHAMED

Nimealikwa kwenye studio nyingi ndani na nje ya Tanzania kuzungumza na wakati mwingine kwa mahijiano maalum.

Kwa kiasi changu naweze kusema nazijua studio na watu wake.
Lakini na narudia lakini, studio hii niliyotia mguu leo ni ya kipekee sana,

Studio nzima ni ''vitoto.''
Nikawaambia waliponikaribisha ndani, ''Nyie vitoto ndiyo mnaniita mimi hapa mnihoji?''

Kisha nikaongeza, ''Wanangu nakutanieni kukuiteni ''vitoto'' lakini leo mimi nikikuangalieni mnanikumbusha ujana wangu.''

Hakika studio nzima ni vijana wadogo.
Hili liligusa sana nafsi yangu.

Studio nzuri inapendeza mandhari yake.

Wakaniambia wao wamepata kunisikia nikimzungumza historia ya Bibi Titi Mohamed na imewagusa wameona na wao wafanye kipindi kuhusu mama huyu mzalendo mpigania uhuru wa Tanganyika.

Ikawa sasa sote mimi na Bibi Titi Mohamed tumeingia kwenye utafiti wa hawa vijana.
Mwindaji anawindwa.

Matokeo yake ndiyo leo nimekaribishwa kwenye Studio za Ona Stories, Kijitonyama.

Vijana wamenionyesha kazi zao.
Miujiza.

Kwanza ni jinsi wanavyoweza kuchukua somo ambalo kwa akili ya kawaida haikupitikii kama ni kitu kinachohitaji jamii isomeshwe historia yake.

Mathalan.
Kaunda Suti.

Daladala.
Kiswahili.

Nani anahitaji kufunzwa vitu hivi?

Nimetazama video fupi vinazoeleza historia ya vitu hivi hakika ikawa kama naingizwa katika dunia sikujua ipo.

Naomba niishie hapo utaendelea mwenyewe kutafuta kazi za hivi ''vitoto'' mtandaoni.

Wamenitoa kwenye hii studio niliyokuwa nimejisahau nikiiangalia historia za Daladala na kazi zake na vipi zinavyounganisha watu na kuyafanya maisha yawe mepesi na fedha zitembee barabarani zikijenga hali za watu na kuondoa kila aina ya shida unazoweza kufikiri.

Kiingereza katika video hizi kimenyooka unapenda kusikiliza.

Kwa akili zetu za kawaida tunaona Daladala ni gari tu limepakia abiria linatoka Kariakoo linakwenda Buguruni.

Kwisha.
Hapana.

Vijana wamenisomesha.
Kila anaedhani yeye anajua ni bingwa basi afahamu kuwa yuko anaejua kumshinda.

Wamenitoa kwenye hii dunia ngeni kabisa kwangu sasa naingia studio kukutana na vijana kwa mahojiano ya maisha ya Bibi Titi Mohamed.

Vijana wanataka kuisikia historia ya maisha ya Bibi Titi Mohamed.
Nawatazama hawa watoto.

Nawauliza kama walipata kumuona au kumsikia Bibi Titi Mohamed akizungumza.
Hawajapata kumfahamu hata kidogo ila wanasema wao wanaujua ule mtaa wake maarufu Dar es Salaam.

Bibi Titi Mohamed alipata kusema watakuja watu wataandika historia yangu.
Nawaangalia hawa vijana.

Nachukua kitambaa changu najifuta uso wangu kwani nahisi machozi yangu ya uzee hayako mbali.
Hawa ni wajukuu wa Bibi Titi Mohamed wameniita kunidai historia ya bibi yao.

Nina deni hapa lazima nililipe.
Naiuliza nafsi yangu.

''Hivi vitoto vidogo mbele yangu ndiyo wale Bibi Titi aliwatabiri katika uhai wake kuwa watakuja kuandika historia yake?''

Camera zina roll.
Studio iko kimya.

Vijana wananisikiliza.
Sauti niisikiayo ni yangu mwenyewe.

Maswali ni machache hapa na pale lakini maswali mazito.
Tumezungumza kwa saa mbili kasoro dakika 15.

Si kila siku nakutana na watu kama hawa.

1740674942317.png

1740675011596.jpeg
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom