Matanga

JF-Expert Member
Nov 13, 2019
2,281
3,976
Luteni wa jeshi la Uganda (UPDF) alivyo ziingiza vitani Tanzania na Uganda.

#Sehemu #ya - 1

Kuanzia leo nitawaletea makala mfululizo zinazohusu Vita ya Kagera kati ya Tanzania na Uganda iliyodumu kwa miezi sita kati ya mwaka 1978 hadi 1979.

Vita hiyo ilianzia mkoa wa Kagera unaopatikana Kaskazini Magharibi mwa nchi ya Tanzania,kabla ya mapigano kuhamia Uganda ambako majeshi ya Tanzania kwa kushirikiana na majeshi ya waasi wa Uganda yalimuondoa kiongozi wa kijeshi wa wakati huo nchini Uganda,Field Marshal Idd Amin Dada.

Fuatilia kila siku safu hii upate na ufahamu kumbukumbu ya vita hiyo ya kihistoria kuwahi kutokea Tanzania.

Vita kati ya Tanzania na Uganda,au Vita ya Kagera ilidumu kwa miezi sita kuanzia Novemba 1978 hadi Aprili 1979.
Vita hiyo ndiyo iliyouangusha utawala wa Idi Amin Dada uliodumu kwa muda wa miaka minane madarakani.

Idd Amin aliingia madarakani Jumatatu ya Januari 25, 1971 alipoiangusha serikali ya Rais Dk. Milton Obote na aliondoka Jumatano ya Aprili 11, 1979 wakati majeshi ya Tanzania na yale ya waasi wa Uganda yaliposhirikiana kumuondoa.

Mgogoro wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Uganda ulianza Jumatatu ya Januari 25, 1971 baada ya Amin kuipindua Serikali ya Dk Obote.

Muda mfupi baada ya hapo,Rais wa Tanzania alimpa Dk. Obote hifadhi ya kisiasa.Akiwa Tanzania Dk Obote alianza mipango ya kurejea Uganda akitumia ardhi ya Tanzania.

Mambo mengi ambayo yangeweza kusababisha Vita ya Kagera yalikuwa yametendeka tangu Januari 1971 hadi Oktoba 1978, lakini kwa kipindi chote hicho hakuna vita iliyozuka.

Vita hiyo ilianza rasmi siku ileile ya maadhimisho ya Uhuru wa Uganda,yaani Jumatatu ya Oktoba 9, 1978 baada ya mwanajeshi mmoja wa Uganda kuvuka mpaka na kuingia Tanzania kupata kinywaji na kukutana na mpenzi wake ambaye alikuwa raia wa Tanzania.

Kwa mujibu wa gazeti la Daily Monitor la Uganda la Jumanne ya Oktoba 9, 2017, wakati mwanajeshi huyo akiwa mpakani upande wa Tanzania kwa starehe zake,alijikuta akipambana na wana usalama wa Tanzania.

Mwanajeshi huyo alikamatwa na kuwekwa rumande.Mapema asubuhi ya siku iliyofuata, aliachiwa aondoke. Kwa kudhani amedhalilishwa na wana usalama wa Tanzania, alikimbilia kambini kwake upande wa Uganda,akachukua bunduki na kurejea upande wa Tanzania ili kulipiza kisasi.

Alipofika umbali fulani kutoka kituo alichokuwa ameshikiliwa,alifyatua risasi kwa mbali. Askari wa zamu wa kituo hicho walilazimika kukimbia ila hakuna hata mmoja aliyejeruhiwa.

Alipojisikia vizuri kwa kitendo hicho,aliamua kurejea kambini kwake upande wa Uganda na kumdanganya kamanda wa kikosi chake aliyejulikana kwa jina la Luteni Byansi kwamba alitekwa na askari wa Tanzania, lakini akapambana nao.

Bila kutafakari sana,Luteni Byansi alimpigia simu Kamanda wa Kikosi cha Malire (MMRR) kilichoko Lubiri mjini Kampala, Kanali Juma Ali Oka (alikuwa maarufu kama Juma Butabika).

Bila kuwajulisha maofisa wa ngazi za juu wa Jeshi la Uganda (UPDF),Kanali Butabika aliviamuru vikosi vya jeshi vilivyokuwa Ziwa Victoria kwenda kuongeza nguvu kwenye kikosi cha Luteni Byansi kuishambulia Tanzania.

“Nilikuwa kamanda wa kwanza wa vifaru kuingia Tanzania,tuliamriwa kushambulia,tulikaa Tanzania kwa wiki mbili kabla ya kuamriwa kuondoka na kurejea Uganda,” Luteni Muzamir Amule wa UPDF alimwambia mwandishi Faustine Mugabe wa Daily Monitor katika mahojiano aliyofanyiwa mwaka 2015 nchini Uganda.

Kwa maoni yake, Kanali Butabika aliingiza Uganda vita isiyo na ulazima wowote. “Unawapelekaje vitani wanajeshi kutoka Malire (Kampala) hadi Mutukula (Tanzania) bila kumtaarifu Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama au hata kamanda yeyote wa juu wa jeshi?” anahoji Luteni Amule katika habari hiyo.

Ijumaa ya Oktoba 27, 1978, mara baada ya uamuzi wa Kanali Juma Butabika, zilitumwa ndege tatu za kivita aina ya ‘MiG-21’ (Mikoyan-Gurevich) za Kirusi.

Marubani bora zaidi wa ndege hizo nchini Uganda, Luteni David Omita, Luteni Atiku na Luteni Abusala walichaguliwa kwa kazi hiyo maalumu.

Kumbukumbu nyingine zinaonyesha kulikuwa na rubani mwingine aliyeitwa Walugembe.Mwaka mmoja kabla, marubani hao watatu—Luteni Omita, Luteni Atiku na Luteni Abusala—walikuwa wamerejea kutoka mafunzoni nchini Urusi.

Uganda ilinunua ndege 20 za aina hiyo mwaka 1977 kuziba pengo la zile aina ya MiG-15 zilizoharibiwa Jumapili ya Julai 4, 1976, wakati makomandoo wa jeshi la Israel walipoivamia Uganda katika shambulio linalojulikana kama Operation Entebbe.

Ndege hizo zilipaa kutoka Entebbe kwenda kuishambulia Tanzania.Ndani ya muda mfupi zikawa zimeshambulia na kurejea Uganda.
Zilipogeuka,ndege ya Luteni Omita ilipigwa kombora na wanajeshi wa Tanzania.

Kombora hilo liliharibu bawa lake la kushoto na ikashika moto.Lakini kati ya sekundi chache kabla ya kushika moto,Luteni Omita alifanikiwa kuruka kwa parachuti.

Hadi wanajeshi wa Tanzania wanafika yalipokuwa mabaki ya ndege hiyo, rubani huyo alikuwa ameshatoweka.

Nchini Uganda, wanajeshi wenzake wakiamini kuwa Luteni Omita ameuawa na majeshi ya Tanzania, walimwona akirejea kambini kwa mguu. Baadaye alipelekwa Entebbe kukutana na Idi Amin ambaye alimpongeza kwa ujasiri wake.

Jumapili ya Oktoba 29, 1978, kwa mujibu wa matangazo ya kituo cha redio cha "Voice of Uganda" ya Oktoba 30, 1978, Idi Amin aliwapandisha vyeo Omita, Atiku, Abusala na Walugembe kuwa makanali na kuwafanyia tafrija.

Tafrija ya kuwapandisha vyeo ilifanyika mjini Entebbe kwenye Uwanja wa Ndege wa Jeshi. Wakati Idi Amin akiwa katika sherehe hiyo, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lilifanya shambulio lake la kwanza kabisa eneo la Kikagati ndani ya Uganda na kuingia kilometa kadhaa bila ya upinzani wowote.



 
Lisu alikuwa anapewa na nani taarifa za kwamba Magufuli anaumwa na hatapona?

Bila shaka laptop za mbowe zilizokamatwa zimesema mengi kuhusu kundi la kigaidi.
Wee acha ujinga wee wee, dunia ya leo mikakati yoote ya 'harakati' hai hifadhiwi kwenye laptop.
 
#HISTORIA #YA #VITA #YA #KAGERA:

Wanajeshi wa jeshi la Uganda wavamia Kagera wateka,wapora,wabaka raia wa Tanzania.

#SEHEMU #YA - 2

Jana tuliona jinsi Luteni wa Jeshi la Uganda alivyosababisha Uganda ivamie na kuanza kuishambulia Tanzania,baada ya kuingia katika mzozo na wana usalama wa Tanzania wakati alipovuka mpaka kuja nchini kunywa pombe na kukutana na mpenzi wake.

Askari huyo alikamatwa na baadaye kuachiwa,lakini cha kustaajabisha baada ya kuachiwa huru na wana usalama wa Tanzania, alidanganya kuwa alitekwa na akapambana nao.

Sasa endelea............

Mbali na mipaka yetu na nchi jirani kama Malawi, Kenya, Zaire (Congo DRC) na Msumbiji,eneo moja lililokuwa katika hatari kubwa ya kushambuliwa na maadui wa nje ni mpaka wetu na Uganda,lakini haukulindwa vya kutosha.

Chokochoko kati ya Tanzania na Uganda zilianza mwaka 1971.Mwaka uliofuata kukawa na makubaliano yaliyojulikana kama mazungumzo ya Mogadishu,yaliyofanyika nchini Somalia Alhamisi ya Oktoba 5, 1972.

Mazungumzo hayo yalikuwa ni usuruhishi wa mgogoro kati ya Tanzania na Uganda.Kwa maana hiyo,Somalia iliepusha vita kati ya Tanzania na Uganda kwa miaka sita tangu 1972 hadi hali ilipovurugika mwaka 1978.

Walioshiriki katika mazungumzo hayo ni mawaziri wa mambo ya nje, ambao ni John Samuel Malecela (Tanzania), Joshua Wanume Kibedi (Uganda) na Umar Arteh Ghalib au Omer Carte Qalib (Somalia). Mwingine ni katibu mkuu wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) wakati huo, Nzo Ekangaki.

Mazungumzo ya Mogadishu yalifikia makubaliano kwamba majeshi ya Tanzania yakae kilomita 16 kutoka mpaka wa Uganda au hata nje kabisa ya umbali huo,vile vile majeshi ya Uganda yaliamuriwa kukaa umbali huo huo sawa na majeshi ya Tanzania ingawa Tanzania haikufikiria kuwa Idi Amin angeishambulia.

Kikosi kilichokuwa na jukumu la kuulinda mpaka wa Uganda na Tanzania ni Brigedi ya 202 ya jeshi la wananchi Tabora,chini ya Brigedia Kamanda Yusuf Himid,ambaye alikuwa akisimamia Kanda ya Magharibi.

Mpakani palikuwa na Bataliani ya tatu,yaani kikosi cha askari ambacho kina Kombania kadhaa na ambacho ni sehemu ya brigedi au rejimenti,kwa wale ambao mlipitia mafunzo ya kijeshi kama Mgambo au JKT,mtakuwa mnafahamu mgawanyo wa vikosi ndani ya jeshi la Tanzania,kuanzia mfumo wa Brigedia,Bataliani,Kombania,Kikosi,Coy,platoon hadi section.

Hiki kilikuwa chini ya Luteni Kanali Morris Singano, ambaye miezi miwili kabla alihamishwa kutoka Mbeya kwenda Kanda ya Ziwa.

Mara baada ya zile ndege tatu za kivita za Uganda zilizoishambulia Tanzania zikiendeshwa na maluteni David Omita, Atiku na Abusala, Singano alituma taarifa hizo Brigedi ya Tabora, lakini Brigedi ilifikiria anachofanya Idi Amin ni kilekile alichokuwa akikifanya kwa zaidi ya miaka sita, kumbe hali ilikuwa tofauti.

Alhamisi ya Oktoba 20, 1978, baada ya mji wa Bukoba kushambuliwa,Mkuu wa Mkoa wa Kagera wakati huo ukiitwa Ziwa Magharibi,Mohamed Nassoro Kissoky,aliitisha mkutano wa viongozi wa CCM na Serikali na kuwaambia kwamba kinachoendelea mpakani ni hali ya kutoelewana tu na kwa sababu hiyo hakuna haja ya kuwa na hofu,kitu ambacho hakikuwa kweli na uhalisia,ukilinganisha na hali tete iliyokuwa ikiendelea baina ya mpaka wa Tanzania na Uganda.

Kissoky aliwasihi viongozi hao wawaambie wananchi kuwa, “sisi ni marafiki wa Uganda na Idi Amin alikuwa mpakani akishikana mikono na watu wetu”.

Lakini wananchi wengi hawakuridhishwa na maneno ya Kissoky kwa sababu ndege za Amin zilikuwa zikionekana mara kwa mara na bado kulikuwa na wasiwasi wa mashambulizi mengine.

Kwa muda wote huu,ukiacha kauli ya Kissoky, hakuna ofisa mwingine yeyote wa CCM wala Serikali ambaye alikuwa ametoa kauli yoyote hadharani kuhusu kinacho endelea kati ya Tanzania na Uganda.

Jumapili ya Oktoba 22,1978 kundi la wanajeshi wa Uganda lilivuka mpaka kuingia Tanzania kunywa pombe.Waliendelea kunywa hadi askari wa Tanzania walipoingia eneo hilo.
Huku wakiwa wameanza kulewa,walianza kufyatua risasi ovyo.Askari wa Tanzania nao wakajibu mapigo.Katika mapambano hayo mwanajeshi mmoja wa Uganda aliuawa.

Siku tatu baadaye, asubuhi ya Jumatano ya Oktoba 25, ikaripotiwa kuwa Mutukula ilikuwa ikishambuliwa vikali.

Kikosi cha wanajeshi wa Tanzania kilichokuwa mpakani kikiongozwa na Kamanda Kanali Singano kilikuwa na wanajeshi wachache na kilielekea kuzidiwa,japo alifanikiwa kunasa mawimbi ya redio iliyokuwa ikitumiwa na Jeshi la Uganda kutokea Kampala.

Kwa mujibu wa kitabu "War in Uganda: The Legacy of Idi Amin, mawasiliano ya redio yalifanywa na Luteni Kanali Marajani,lakini Uganda hawakuweza kuyanasa.

Asubuhi ya Ijumaa ya Oktoba 27, ndipo ndege tatu za kivita za Uganda aina ya MiG-21 ziliposhambulia mji wa Bukoba. Kombora moja kutoka katika ndege hizo lilianguka mita chache kutoka ilipo Hospitali ya Bukoba. Mojawapo ya ndege hizo ilitunguliwa.

Kwa wakati wote huu, vyombo vya habari vya Tanzania havikutangaza chochote kuhusu matukio hayo.Habari za matukio hayo zilisambazwa na wale waliokuwa wakikimbia vita.

Ingawa madhara hayakuwa makubwa, shambulio la Bukoba lilifanya raia kutaharuki na wengi kuukimbia mji.Hadi jioni ya siku hiyo, barabara zote za kutoka Bukoba zikawa zimefurika watu.

Jumatatu,asubuhi ya Oktoba 30 maelfu ya wanajeshi wa Uganda waliingia tena Tanzania kupitia maeneo manne ya mpaka wa Kukunga, Masanya,Mutukula na Minziro.Raia wa Tanzania waliojaribu kupambana na majeshi hayo waliuawa.

Mamia ya wananchi wa Tanzania, hususan wanawake,walichukuliwa mateka na kupelekwa Uganda kwenye kambi ya Kalisizo.Kwa mujibu wa kitabu "Great Britain’s Policy on the Uganda-Tanzania War (1978-9)" cha Elisabeth Stennes Skaar, baada ya kuteka eneo lenye ukubwa wa kilomita 1,800 za mraba, wanajeshi wa Uganda walianza kupora,kubaka na kuua raia wa Tanzania.

Kwa mujibu wa kijitabu cha Daniel Acheson-Brown cha "The Tanzanian Invasion of Uganda: A Just War? kwa siku hiyo moja tu zaidi ya Watanzania 1,500 waliuawa.Wanajeshi wa Uganda walipora kila walichoweza kupora, yakiwamo magari.
Na magari ambayo yalikuwa mabovu, yaling’olewa vipuri.Uporaji huo ulihusisha hata masufuria na vijiko jikoni.

Kiwanda cha Sukari cha Kagera kiliathirika zaidi na uporaji huo pamoja na ranchi ya Misenyi.Mifugo iliyoporwa Kagera ikapelekwa Mbarara Uganda ambako iligawiwa kwa askari na ndugu na marafiki wao.

Baadaye siku hiyo, Redio Uganda ikatangaza kulikomboa eneo la Kagera na kusema sasa mpaka halali wa Tanzania na Uganda ni Mto Kagera.

Idi Amin mwenyewe alizuru eneo hilo na kupiga picha na silaha zilizoachwa na wanajeshi wa Tanzania waliokimbia.

Habari za kutekwa kwa sehemu ya ardhi ya Tanzania huko mkoani Kagera,zikamfikia Rais wa Tanzania Mwalimu Julius Nyerere,jumatatu ya Oktoba 30, 1978.

Mwalimu Nyerere aliwaita makamanda wa JWTZ nyumbani kwake,miongoni mwao alikuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama wakati huo,Luteni Jenerali Abdallah Twalipo.

Mkutano huo kati ya Mwalimu Nyerere na makamanda wa jeshi la wananchi ulimalizika saa nne asubuhi na Mwalimu aliamuru kazi ianze mara moja.

Siku iliyofuata,Jumanne ya Oktoba 31,katika taarifa ya habari ya saa 1:00 asubuhi, Redio Tanzania Dar es Salaam ilitangaza kwa mara ya kwanza matukio ya kivita katika mpaka wa Tanzania na Uganda.

Je unataka kujua nini kilifuatia baada ya Ameir Jeshi mkuu wa majeshi yote ya ulinzi na usalama ya Tanzania wakati huo Mwalimu Julius Kambarage Nyerere baada ya kukutana na mkuu wa Majeshi ya Tanzania,Luteni Jenerali Abdallah Twalipo na makamanda wengine wa vikosi vya ulinzi na usalama!?

Fuatilia makala hizi motomoto ya vita hii ya Kagera,kuanzia mida ya saa 2 kamili usiku kila siku kupitia ukurasa na "page" yangu kila siku.

Itaendelea .......
 
Aisee mleta mada na wewe ulishiriki hivi vita?

Let me follow this story?

Ni kweli iddi Amin alikuwa anakulaga nyama za watu au uzushi?
 
#HISTORIA #YA #VITA #YA #KAGERA:*

Mwalimu Nyerere atangaza rasmi vita dhidi ya Majeshi ya uvamizi ya Nduli Idd Amin Dada wa Uganda.

#Sehemu #ya - 3.

Katika toleo lililopita tulisimulia namna majeshi ya Nduli Idi Amin Dada yalivyoivamia Tanzania Jumatatu ya Oktoba 30, 1978 kupitia mpaka wa Kukunga,Masanya,Mutukula na Minziro na kuua raia na hatimaye kuteka eneo la kilomita za mraba 1,800,na kutangaza kuwa mpaka halali wa Tanzania na Uganda kuwa ni Mto Kagera,na kwamba eneo hilo lililotekwa nalo litatawaliwa kijeshi kama maeneo mengine ya nchi ya Uganda.

Habari za kutekwa kwa Kagera zilimfikia Rais wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere ambaye siku hiyo hiyo aliwaita makamanda wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) nyumbani kwake na kukubaliana kuwa kazi ya kumng’oa Idi Amin ianze mara moja.

Siku mbili baada ya kukutana na makamanda wa Jeshi la Wananchi Novemba mosi, 1978, Mwalimu Nyerere alilitangazia Taifa na Dunia kuhusu uvamizi wa Idi Amin na uamuzi wa Tanzania wa kumpiga.

Akizungumza na viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kwenye ukumbi wa mikutano wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam, Mwalimu Nyerere alieleza uvamizi huo na jinsi Tanzania ilivyoamua kupambana na majeshi ya Idd Amin.

Nimewaombeni mkusanyike tena hapa niwaelezeni jambo ambalo kwa sasa wote mnalijua.Lakini naona si vibaya nikieleza na kulitolea ufafanuzi zaidi.

Nitajaribu kueleza kwa ufupi.
“Wakati nilipokuwa ziarani Songea kuanzia juma la pili la mwezi uliopita (Oktoba), zilitangazwa habari kutoka Uganda kwamba jeshi la Tanzania limeingia Uganda na limechukua sehemu kubwa na kuua watu hovyo.

“Siku zilipotangazwa habari hizo nilikuwa nimekaribishwa chakula cha jioni na vijana wetu wa jeshi pale Songea,na mimi nikakanusha.
Na kwa kweli nikachukua nafasi hiyo kuvishutumu vyombo vya habari vya nje ambavyo vinapenda kutangaza tangaza uongo wa Amin,” alisema Nyerere.

“Kila anapotangaza uongo, wao huurukia na kutangaza kama kwamba ni kweli. Huo ndio uliokuwa uongo wake wa kwanza, na aliendelea kupotosha Dunia".

“Baadaye akabadili sura, akaongeza uongo wa pili katika shabaha hiyohiyo kuwa Watanzania wanaua watu ovyo na kwamba wanasaidiwa na majeshi kutoka Cuba na uongo huo nao tukaukanusha.

“Kwa hivyo, alivyozidi kusema habari hizo za uongo tuliendelea kuzikanusha na kuzipuuza.
Lakini Alhamisi akatuma ndege za kivita Bukoba. Vijana wetu walizitupia risasi zikakimbia.Siku hiyohiyo ikarudi tena moja, ikaangushwa.

“Ijumaa zikaja ndege eneo la Kyaka zikatupa mabomu. Vijana wetu walizitupia risasi, na mbili zikaangushwa.”

Nyerere pia alizungumzia ndege za Tanzania zilizopotea uwanjani wakati zikitoka Dar es Salaam kwenda Mwanza ambazo kutokana na kasi yake zilihisiwa kuwa ni za adui na kutunguliwa na vikosi vya jeshi la anga la Tanzania kwa bahati mbaya.

Nyerere alisema Tanzania imechoshwa na uongo huo wa Idi Amin na hivyo wameamua zikionekana ndege za kivita, zitunguliwe.

“Kwa hiyo vijana wetu wamekwisha ambiwa kuwa ndege za kivita zikionekana, zipigwe.Kama vile zile za Bukoba na Kyaka zilipigwa, basi na hizi zikapigwa kwa bahati mbaya zilipofika Musoma walidhani ni za adui.

Tukapoteza ndege tatu,” alisema Nyerere.

“Lakini katika mambo ya vita ajali hutokea na vijana hawa walisha ambiwa ndege zikionekana zipigwe,wangeziacha? Wanajuaje ni za adui? Kwa hiyo ikatokea bahati hiyo mbaya.

“Matukio haya hatukuyatangaza hata kule kupigwa kwa ndege za Amin hatukutangaza. Hatukutangaza kwa sababu hatukutaka jambo lenyewe kulipa uzito mno.Tulisema akiendelea endelea kuleta ndege zake,tutaendelea kuziangusha kila zinapokuja.

“Uwezo wa kuziangusha upo,na mwenyewe alijua uwezo upo.Ni vizuri akijua yeye. Tulikuwa tunaepuka kulipa uzito jambo lenyewe ambalo mwanzo wake ni uongo kabisa wa kuzusha.”

Nyerere alisema jinsi Idd Amin alivyoendelea kuidanganya dunia na jinsi Tanzania ilivyomjibu hadi alipoamua kuvamia.
“Sasa Jumatatu ndiyo akaivamia nchi yetu. Akaingiza majeshi yake kwa nguvu, nguvu kubwa.

Yakachukua sehemu kubwa yakaingia ndani mpaka Kyaka,hii tukatangaza kwa sababu lilikuwa ni jambo la kweli na yeye kama kawaida yake akakana akasema haikutokea hivyo,” alisema Nyerere.

“Akaendelea kusema kwamba Watanzania ndio wako Uganda, ndio wamechukua sehemu ya Uganda. Akakana ukweli huo. Lakini tukawaeleza jamaa na mabalozi walioko Dar es Salaam kuwa huo ndio ukweli.

“Huyu mtu ameivamia nchi yetu,sasa jana ametangaza mwenyewe kwamba ni kweli majeshi yake yameivamia nchi yetu na yamechukua sehemu hiyo ya Tanzania iliyoko kaskazini mwa Mto Kagera na kwamba tangu sasa, eti sehemu hiyo ni ya Uganda na itatawaliwa kijeshi kama Uganda inavyotawaliwa.”

Alisema kauli hiyo ya Idi Amin iliisaidia Tanzania kutangaza kutokea kwa uvamizi huo.
“Sasa hiyo ndiyo hali.

Tufanye nini!?

"Tunayo kazi moja tu,Watanzania sasa tunayo kazi moja tu—ni kumpiga,”

Alisema Mwalimu Nyerere.

“ #Uwezo wa kumpiga #tunao. #Sababu ya kumpiga #tunayo, #na nia ya kumpiga #tunayo".

"Tunataka dunia ituelewe hivyo kwamba hatuna kazi nyingine"
“Na tunaomba marafiki zetu wanaotuomba maneno ya suluhu,waache maneno hayo"

"Kuchukua ardhi ya nchi ya watu wengine siyo kwamba majeshi yamekosea njia na kusema kuwa sasa sehemu hiyo umeichukua na kutangaza vita kwa nchi ile nyingine"

"Si sisi tuliofanya hivyo. Amefanya hivyo mwendawazimu"

“Na amefanya hivyo kwa jambo ambalo aliwahi kutangaza zamani.Aliwahi kusema zamani kidogo kuwa mpaka wa haki wa Uganda na Tanzania ni Mto Kagera,na kuwa siku moja atachukua sehemu hiyo.

"Ametimiza hivyo.”
Nyerere aliwaomba marafiki wa Tanzania kuielewa hali hiyo na kuisaidia katika kuyaondoa majeshi ya Uganda na kwamba wale waliokuwa wakitaka suluhu haitawezekana.

“Hatukupenda kufanya hivyo.Maadui zetu ni mabeberu,na kwa hivi sasa wako Kusini.

Serikali ya Afrika,hata kama hatupendi matendo ya viongozi wao, hatuwahesabu kama adui wetu,” alisema Nyerere.

“Na kama Amin angekuwa amesema tu kwamba Tanzania ni adui wetu,sisi tungeendelea kumpuuza kama ni maneno hayo. Lakini kafanya kitendo cha uadui,hatuwezi.

“Ameingia Tanzania mwenyewe na mtu huyu ni mshenzi.Ameua watu wengi sana.Kwa hiyo nasema tuna kazi moja tu,Tutampiga.

Vijana wetu wako mpakani sasa hivi. Wako kule. Wako kule na mapambano yanaendelea.

“Sasa hayo si mapambano ya TPDF peke yake, ni yetu wote.Kwa hiyo ninachowaombeni wananchi,hiyo kazi iliyoko mbele yetu muielewe.

“Pili, tuwasaidie vijana wetu,kila mtu kwa mahali alipo.Tutaendelea na kila mapambano yanavyoendelea kueleza nini la kufanya na nani afanye nini.

“Tutaelezana wakati wote huo mpaka tumemuondoa huyu nyoka katika nyumba yetu.Na tunawaomba mtulie.Katika mambo haya ya vita,na hasa kama watu mlikuwa mmezoea amani mnaweza kubabaika sana.

“Msibabaike, tulieni. Fanyeni kazi kama kawaida. Lakini mjue vitendo hivyo kazi yake ni hiyo moja; kumpiga mshenzi huyu aliyekuja katika nchi yetu.”

Alimalizia hivyo Nyerere baada ya kuzungumza na Watanzania kupitia vyombo vya habari.

Je,unataka kufahamu nini kilifuatia baada ya baba taifa kulitangazia taifa na Dunia,kuhusu vita rasmi baina ya Tanzania na majeshi ya uvamizi ya Nduli Iddi Amin Dada!?

Fuatilia ukurasa wangu huu sehemu ya 4 hapo kesho majira kama haya ili uendelee kujuzwa vita hii iliyopiganwa na majirani hawa wawili wa Jumuia ya Afrika Mashariki.

Itaendelea...
 
Back
Top Bottom