SoC03 Watendaji wa serikali za mitaa na vijiji wajengewe uwezo wa kusimamia miradi

Stories of Change - 2023 Competition

Undava King

JF-Expert Member
Aug 11, 2017
3,224
5,384
Ninashauri serikali ije na mkakati mahususi kuwajengea uwezo watendaji wa serikali za mitaa,
Kupitia nguvu ya uhamasishi, ushauri na usimamizi wao wananchi unufaika na utekelezaji wa miradi kadhaa ya maendeleo katika maeneo yao kupitia dhana ya ushirikishwaji na wajibu.
Wakati mwingine watendaji ushindwa kujieleza kwa ufasaha katika vikao vyao na wananchi na kupelekea zoezi zima la utekelezaji wa miradi kukwama kwa dosari ndogo ndogo za kushindwa kuelewa saikolojia ya wananchi wao na kuijeuza saikolojia hiyo katika hali ya ujengefu na kudhibiti mihemko na kuamsha shauku ya wananchi wao katika kushiriki na kujihisi kuwa wao ni sehemu ya mradi husika.

Pendekezo langu kwa Serikali; iandae utaratibu wa mafunzo maalumu kazini na kabla ya kuanza majukumu rasmi ya kazi kwa watendaji wapya, mafunzo haya yajikite katika kozi ya saikolojia, uongozi na maadili.
Serikali isimamie gharama za mafunzo na lengo liwe nikuandaa viongozi watakao wajibika na kutenda kwa ufanisi ili serikali iweze kunufaika na ujuzi wao. Endapo zoezi litafanikiwa naamini serikali itaboresha zaidi mahusiano yake na wananchi, itadhibiti upotevu wa fedha na rasilimali, itarahisisha na kuongeza kasi na ufanisi katika utekelezaji wa miradi pia itawajengea watendaji uwezo wa kujiamini katika utendaji wao wa kazi.

Lakini pia serikali iwawezeshe watendaji kwa kuwapatia usafiri wa pikipiki ili waweze kufika na kutembelea miradi yote inayotekelezwa katika maeneo yao lakini pia kuweza kuwafikia wananchi kiurahisi katika kutekeleza majukumu yao bila kusahau kuwatengea bajeti ya mafuta, utaratibu wa matengenezo madogo madogo na bajeti ya mawasiliano (kila mwezi) Hivi sasa watendaji ulazimika kutumia sehemu ya ujira wao mdogo katika kulipia usafiri wa kuwafikisha katika sehemu mbalimbali za utawala, kulipia salio la muda wa maongezi kwa shughuli za kiofisi achilia mbali wengi ufanya kazi katika mazingira magumu na miundombinu isiyoridhisha ikiwemo uduni wa majengo ya ofisi za mitaa na vijiji.

Uanzishwe utaratibu rasmi wa kitabu cha stakabadhi ya michango ya maendeleo ya kijiji na mtaa (kitabu hiki kinaweza kuandaliwa na halmashauri husika) hili kila mwananchi anapochangishwa fedha yeyote ile kwa ajili ya kuchangia miradi katika eneo lake basi apewe stakabadhi ambayo ni kithibitisho kuwa katoa fedha, ikiwa na jina la mtoaji, kiasi, na sababu. Wananchi wamekuwa wakichangishwa fedha nyingi wakati mwingine na viongozi wasio waadilifu ila taarifa zao kwenye daftari la michango hazionekani na mtendaji anaweza kuamua tu kupotosha takwimu kwa kuhamua kuripoti kiasi anachoona yeye kinafaa mbele ya wananchi huku kiasi kingine kikifujwa pasipo walengwa kugundua.

Mtendaji atumie njia ya kunakili katika daftari majina ya watoaji wote pamoja na kutoa stakabadhi kwa kila mtoaji na wakati wa kuwasilisha taarifa ya mahesabu ya michango ya wananchi katika kikao ufanyike utaratibu wa kuteua idadi fulani ya mashuhuda miongoni mwa wananchi waliohudhuria katika kikao hicho ili kukagua na kujiridhisha kuwa mahesabu yaliyowasilishwa na kiongozi wao ni sahihi. Ikifanyika namna hii naamini itaondoa hali ya ubadhirifu, migogoro na kutoaminiana kati ya wananchi na viongozi wao kutokana na kuongezeka kwa uwazi na wajibu wananchi watahamasika kutoa michango yao kwa hiari kwa ajili ya kufanikisha shughuli za maendeleo.

Kudhibiti upotevu wa fedha za umma katika manunuzi na malipo ya miradi inayotekelezwa katika ngazi ya serikali ya kijiji au mtaa inayohusisha moja kwa moja watendaji, wadau na wasambazaji. Serikali ifanye utaratibu kama itawezekana basi kiundwe chombo maalumu ambacho ni rasmi na kitakuwa kinafanya kazi zake kwa siri, walengwa wasambazwe katika halmashauri zote nchini na kazi yao iwe ni moja tu; kufuatilia taarifa za bei za bidhaa mbalimbali katika eneo lao, malipo kwa ajili ya huduma mbalimbali, gharama za usafirishaji na watoe taarifa hizo kila mwezi kwa kusasisha katika kanzu data zao hili wawarahisishie idara ya ukaguzi na watoa maamuzi kuweza kupata taarifa sahihi za bei za bidhaa zilizopo sokoni kwa wakati huo, thamani halisi ya malipo yanayohitajika kutolewa kwa ajili ya huduma, yote hii ni katika kuongeza ufanisi na kudhibiti mianya ya rushwa na ufujaji wa pesa za umma.

Mwisho, tuwapatie watendaji wetu motisha kwa kuonesha kuguswa na kujituma kwao kazini, tunaweza anzisha ushindani miongoni mwao kila baada ya muda fulani wanaoibuka washindi wawe wanatunukiwa na wale wazembe wachukuliwe hatua, hili litaondoa tabia ya kufanya kazi kwa mazoea na kutanguliza maslahi mbele, mfano mdau wa maendeleo amefika ofisini kuomba apewe nafasi ya kuelimisha jamii na kuikomboa iondokane na umasikini badala mtendaji ndiye awe mstari wa mbele kuunga mkono suala hili, anakuwa ndiye kikwazo kwa kudai kulipwa hili haitishe mkutano na bado atahitaji posho na kama hasipolipwa basi tegemea suala hilo lazima liende kwa kusuasua, lakini endapo angekuwa anajua kuwa ikifika wakati fulani nitadaiwa matokeo na sina cha kuonesha nimefanya nini kwa ajili ya wananchi lazima angepambana kuhakikisha kila fursa inayomfikia katika eneo lake anahitumia vyema kunufaisha wananchi wake.
 
Back
Top Bottom