- Source #1
- View Source #1
- Source #2
- View Source #2
Nimeona taarifa mtandaoni ikisema watumishi wa Umma na Binafsi ambao wamechangia kwa zaidi ya miezi 108 yaani miaka 9 katika NSSF au PSSSF sasa rukhsa kutumia michango yao kama dhamana ya kuchukulia mkopo wa kujenga, kuboresha au kununua nyumba nchini Tanzania.
Kanuni namba 141 za Mwaka 2024 zimeanza kazi tangu Machi 8, 2024.
JamiiCheck tusaidieni kujua ukweli wake.
- Tunachokijua
- Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeanzishwa chini ya Sheria ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii Sura ya 50 marejeo ya mwaka 2018 kwa lengo la kutoa huduma ya Hifadhi ya Jamii kwa wafanyakazi walio katika sekta binafsi na sekta isiyo rasmi.
Mfuko huu huwa na Majukumu ya Kuandikisha wanachama kutoka sekta binafsi na isiyo rasmi, Kukusanya michango, Kuwekeza na Kulipa mafao.
Aidha, Serikali kupitia Sheria namba 2 ya Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma mwaka 2018, ilifuta Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya LAPF, PSPF, GEPF, PPF na kuanzisha Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF).
Hivyo kuanzia Agosti 1, 2018 waliokuwa wanachama wa Mifuko iliyounganishwa yaani LAPF, PSPF, GEPF na PPF walihamishiwa katika Mfuko wa PSSSF na wataendelea kuwa wanachama na kuchangia katika Mfuko (isipokuwa wanachama wote waliokuwa watumishi wa sekta binafsi kutoka Mifuko iliyounganishwa walihamishiwa NSSF, na watumishi wa Umma waliokuwa NSSF walihamishiwa PSSSF kuanzia Februari, 2019).
Kuibuka kwa Madai tajwa
Machi 14, 2024 kupitia Mtandao wa X, Taarifa za Watumishi wa Umma/binafsi ambao wamechangia Kwa zaidi ya miezi 108 yaani miaka 9 NSSF/PSSSF kuruhusiwa kutumia michango yao kama dhamana ya kuchukulia mkopo wa kujenga, kuboresha au kununua nyumba nchini Tanzania zilianza kusambaa.
Madai haya yalichapishwa tena kwenye Mtandao huo huo Machi 15, 2024. Tazama hapa.
Ufuatiliaji wa JamiiCheck
Ufuatiliaji wa JamiiCheck umebaini mambo kadhaa kuhusu taarifa hii.
Mosi, ni taarifa ya kweli, ilitangazwa kupitia tangazo la Serikali Namba 141 toleo la Machi 8, 2024 ikiwa na Jina la 'Social Security (Use of Members Benefit Entitlements as Collateral for Home Mortgage) Regulations, 2024.'
Picha ya kipengele kinachoonesha jinsi Mafao yanavyoweza kutumika kama DhamanaPili, tofauti na inavyodaiwa kuwa mtu anayepaswa kuomba ni yule aliyechangia kwa miezi 108 (Miaka 9), JamiiCheck imebaini ni Miaka 15 (Miezi 180). Mtanzania aliyetimiza kigezo hiki anaweza kuchukua mkopo kwa kutumia dhamana ya mafao yake ili ajenge nyumba, kununua nyumba au kufanya ukarabati wa nyumba.
Aidha, Mwanachama hatopaswa kuomba mkopo unaozidi 50% ya Mafao yake wakati wa kuomba mkopo na marejesho ya mkopo huo hayatakwenda zaidi ya muda wa kawaida wa kustaafu kazi kwa lazima.
Kwa mujibu wa kifungu cha 3(2) cha kanuni hizo, mifuko haitatoa dhamana zaidi ya moja kwa wakati mmoja na kifungu cha 3(3) kinasema dhamana hiyo itatolewa baada ya mwanachama mwenyewe kuomba kwenye mfuko.
Kifungu cha 4(1) (b) kimeweka sharti kuwa bei ya kununulia nyumba haitapaswa kuzidi thamani ya soko la nyumba inayohusika kwa wakati husika.
Aidha, kifungu cha 7 (1) kinataka taasisi ya fedha inayotaka kutoa mkopo hiyo, iwasilishe ombi hilo kwa maandishi na ndani ya siku 30, mfuko utatoa idhinisho la maandishi na endapo utakataa utatoa sababu kwa maandishi.
Hivyo, JamiiCheck imejiridisha kuwa taarifa hii kama ilivyochapishwa na Sildenafil Citrate ni ya kweli, isipokuwa muda wa uchangiaji wa Mwanachama aliyekidhi vigezo vya kuomba dhamana ya mkopo huo ni Miaka 15 (miezi 180) na siyo miezi 108 (Miaka 9) kama alivyobainisha.