SoC02 Tuimarishe mapambano dhidi ya ugonjwa wa akili nchini Tanzania

Stories of Change - 2022 Competition

Sagira

New Member
Jul 13, 2021
1
3

Unajiona sio mtu mwenye umuhimu tena kwenye haya maisha na hujui nini kimekukuta au wapi ulipokosea, unatamani kulia sana na upate mtu wa kumweleza unayoyapitia, umeamua kuwa mtu wa liwalo na liwe, sikia nafahamu maumivu uliyokuwa nayo unahisi watu hawajali kuhusu unayopitia siyo kweli fahamu kwamba wewe ni mtu muhimu sana.

Ugonjwa wa akili haupewi kipaumbele katika jamii yetu na umekuwepo kwa muda mrefu sana lakini haujapata msisitizo wa kutosha na wagonjwa wa akili mara nyingi hujiona wasiokuwa na shida na kuuficha ugonjwa mpaka pale wanapofanya matendo ya ajabu tusiyoyatarajia, tunaowazunguka wagonjwa wa akili tumekuwa tukiishi nao katika familia, kazini na mtaani bila kuwapa msaada wa kitabibu tukihusisha ugonjwa wa akili na imani za kishirikina wengine tukiwanyooshea vidole na kuwatenga.

Watu wengi tunajua ugonjwa wa akili ni ule wa kichaa tu, napenda kuwaongezea idadi ya magonjwa ya akili kama sonona( msongo wa mawazo), ugonjwa wa wasiwasi, ugonjwa wa kiwewe, mawazo ya kujiua, uraibu( madawa ya kulevya na pombe), ugonjwa wa tabia na sifa za mtu.

picha ya mtu mwenye ugonjwa wa akili


Kama tunavyopata magonjwa sehemu nyingine za mwili wetu kama tumbo, moyo na kifua ndivyo ilivyo hata kwa ubongo wa mwanadamu unaweza kushambuliwa na magonjwa, ni muhimu kufahamu dalili za magonjwa ya akili ili uweze kutafuta msaada wa kitabibu unapohisi afya yako ya akili imedhorota:-


  • Kuwa na wasiwasi au uwoga uliopita kiasi
  • Kujihisi kuwa na huzuni kupita kiasi
  • Kuwa na hali ya kuchanganyikiwa kufikiria na kuwa na tatizo katika kujifunza
  • Mihemko inayobadilika kupita kiasi na kushindwa kuimudu
  • Kuwa na hisia inayokereketa na kukupa hasira mara kwa mara
  • Kuepuka marafiki na kushindwa kuchangamana na watu kwenye shuhuli za kijamii
  • Kubadilika kwa tabia ya kula, kulala na kujihisi kuchoka kila wakati
  • Kushindwa kutambua ukweli ( kuona au kuongea na watu au vitu ambavyo havipo)
  • Matumizi kupita kiasi ya vitu kama vile pombe au dawa za kulevya
  • Kufikiria kuhusu kujiua
  • Hofu au wasiwasi wa muonekano wako
Kama unafikiri kuna mtu unamjua anapambana na ugonjwa wa akili kwa siri usiogope kuongea nae juu ya hisia zake.

Kwa kipindi kifupi kila kukicha nikiingia kwenye mitandao ya kijamii nimekuwa nikikutana na habari za kutisha kama zinazohusu vijana kujinyonga na mambo mengi yanayoleta giza kwenye jamii yetu, haya yote ni matokeo ya ugonjwa wa akili. Wapo wanaozaliwa na magonjwa ya akili kutokana kwa sababu za kibaiolojia na wengine hupata ugonjwa wa akili kutokana na sababu za kimazingira ambazo ndio zimeshamiri katika nchi yetu, zifuatazo ni sababu za magonjwa ya akili Tanzania.

maisha duni; umasikini ni janga linalochangia watu kushindwa kumudu uwezo wa kujipatia mahitaji muhimu na kuendesha familia zao, swala la ajira limekuwa fumbo kwa vijana wengi katika nchi yetu huku wengine wakikosa hata mtaji wa kujiajili, mbele tunaona giza nene uvumilivu unatushinda tunakosa tumaini la kesho tunabakiza wazo moja tu la kuondoa uhai wetu ili tuyakambie matatizo. Habari iliyowekwa kwenye ukurasa wa millardayo tarehe 20/01/2021 ilikuwa inaeleza mwanamke kutoka Dar es salaam anadaiwa kuwatupa watoto wake shimoni na kujinyonga baada ya kufiwa na mumewe na kuanza kulalamika maisha magumu huku watoto wakishindwa kwenda shule baada ya kukosa ada.

1661440036940.png


Unyanyasaji katika mahusiano; wanadamu tumeumbwa na hisia ya kupendana lakini mapenzi yamegeuka silaha inayotuangamiza wenyewe, unaishi kwenye mahusiano unayokosa furaha kila siku licha ya kuwa mvumilivu mpaka unakumbwa na msongo wa mawazo utakaoleta jeraha kwenye akili yako, mahusiano yaliyojaa sumu yamekuwa kinara kuchangia ongezeko la magonjwa ya akili, husababisha hisia za kutokujithamini, wasiwasi, mafadhaiko, kutojiamini na hata ugomvi na wivu uliopita kiasi, haya ni hatari kwa afya yako ya akili. Habari iliyowekwa na millardayo tarehe 11/09/2021 ilikuwa inaeleza namna kijana kutoka mkoa wa Pwani aliyetengeneza juisi yenye sumu na kumpatia mpenzi wake kisha na yeye kuinywa na wote walifariki sababu ikiwa ni wivu wa mapenzi.


picha ya malumbano katika mahusiano


Kupata au kushuhudia matukio ya kuogofya; wapo wanaokutana na matukio yanayotisha na kuumiza kama vile ukatili wa kijinsia, ukatili wa kimwili, kushuhudia vita na ajali za kutisha barabarani hasa katika rika ya watoto na watu wazima, watu hawa wapo kwenye hatari ya kupata magonjwa ya akili. Hii ni moja katika ya sababu ya magonjwa ya akili kwa askari wetu kutokana na kushuhudia matukio ya kutisha katika mazingira ya vitani na mafunzoni. Habari iliyowekwa katika ukurasa wa Jamii Forums tarehe 16/02/2018 ilikuwa inaelezea hukumu ya kijana kutoka Iringa mwenye umri wa miaka 24 baada ya kumbaka mtoto wa kike mwenye miaka 3, tukio hili la kubakwa kwa mtoto huyu linaweza kudumu kwa miaka, ikiwa na vichochezi vinavyoweza kurudisha kumbukumbu za kiwewe zikiambatana na miitiko mikali ya kihisia na ya kimwili.

picha ya muhanga wa tukio la ubakaji

Nimegundua nina dalili za magonjwa ya afya ya akili nifanye nini?

Tembelea kituo cha afya ya akili kwa tiba na ushauri
; kwenye hospitali nyingi kama Muhimbili na Bugando kuna kitengo cha afya ya akili kinachosimamiwa na madaktari bingwa waeleze hisia uliyonayo na matatizo yanayokusibu, tuache uoga wakutafuta tiba kwenye vituo vya afya tukiogopa jamii inayotuzunguka watakuwa na mtazamo gani juu yetu.

Epuka kujitenga na marafiki na familia; jenga mtandao na marafiki na ndugu watakaoweza kukusikiliza na kukupa ushauri mzuri, shiriki shughuli mbalimbali za kijamii kama sherehe itasaidia kupunguza msongo wa mawazo.

1661439089858.png


Jifunze kukabiliana na uhalisia wa maisha; ugumu wa maisha ni changamoto ya wengi hatuhitaji kukimbia tatizo bali kulitatua tafakari njia sahihi za kujikwamua kimaisha omba ushauri kwa watu unaowaamini, kesho yetu ni fumbo lakini tunaweza kuijenga kwa juhudi zetu, pia tusilazimishe kuwa kwenye mahusiano yasiyo na tija ongea na mwenzako mwambie ukweli juu ya mtazamo wako, furahia mafanikio yako hata kama ni madogo.

Ukweli ni kwamba unaweza ukawa na wasiwasi lakini bado ukajiamini, unaweza ukawa na sonona lakini ukaishi kwa furaha hata watu wenye nguvu wanavunjika moyo, ni wakati wa kuielimisha jamii juu ya ufahamu wa magonjwa ya akili, hali ya afya ya akili siyo ishara ya udhaifu na watu wenye ugonjwa wa akili hawapaswi kutengwa ama kunyanyapaliwa na jamii. Ni muhimu walezi kutenga muda wa watoto wadogo hasa waliopo mashuleni kufahamu yanayowasibu kwenye akili zao, Ni muda wa kutumia teknolojia ya vifaa kama michezo ya ukweli halisia hii itasaidia akili kupata burudani na kujenga afya ya akili.

picha ya mtoto akicheza mchezo wa ukweli halisia

Mwandishi: Sagira Wanna
sagirawanna@gmail.com
 
Back
Top Bottom