Nguvu ya Wosia kisheria: Jinsi ya Kupanga Mali Yako ukiwa hai na Kuepuka Migogoro ya Mirathi baada ya kifo.

Jan 28, 2024
82
110
Hii ni elimu kwa Umma, Karibu sana kujifunza
images (45).jpeg

Mara nyingi migogoro ya mirathi huanza pale mwenye mali anapofariki, na ni mara chache sana kuona viashiria ama hatari ya kuwapo kwa mgogoro wa mirathi ikiwa mwenye mali bado yupo hai. Hii inatuonyesha ni kwa jinsi gani kuna umuhimu mkubwa wa kujua na kuandaa namna nzuri ya kusimamiwa na kugaiwa kwa mali zetu baada ya vifo vyetu pindi tu hai. Hii itasaidia kuhakikisha kwamba mali zetu zitagawiwa kwa warithi wetu vile tulivyokuwa tunataka na kutamani zigaiwe baada ya vifo vyetu.

Kupitia uzii huu, nitakuongoza kwa ufasaha na kisheria kuhusu njia bora za kutayarisha mpango wa usimamizi na ugawaji wa mali zako baada ya kifo kwani ni ukweli usiopingika kwamba 'sisi ni udongo na mavumbini tutarudi Tu'
hivyo ni vyema kujiandaa mapema ili kuepusha migogoro kwa wale tutakao waacha.
ANGALIZO:
Makala hii imekusudiwa kutoa elimu kwa umma na kuongeza uelewa kuhusu masuala ya mirathi, pamoja na umuhimu wa wosia katika kupanga usimamizi na ugawaji wa mali baada ya kifo. Taarifa zilizomo zimeandaliwa kwa umakini na zinalenga kuelimisha wasomaji juu ya mada inayojadiliwa. Hata hivyo, ni muhimu kuelewa kwamba makala hii hayapaswi kuchukuliwa kama ushauri wa kisheria. Kwa masuala mahususi yanayohusiana na mirathi na wosia, ni vyema kushauriana na mtaalamu wa sheria ili kupata ushauri unaolingana na hali yako binafsi. Makala hii inapaswa kutumika kama chanzo cha taarifa za kielimu pekee na siyo kama mbadala wa ushauri wa kitaalamu.

NAMNA BORA YA KUEPUSHA MIGOGORO YA MIRATHI
Kisheria zipo njia mbalimbali za kuhakikisha mali zetu zinasimamiwa na kugaiwa kwa namna tutakavyo (as we wish) pindi mauti yatukutapo, lakini hapa nitazungumzia kwa undani sanaa juu ya njia moja tu ambayo ni 'Wosia'
Thread hii inakwenda kumsaidia msomaji kujifunza, kuelewa na kuyajua yafuatayo
  1. Umuhimu wa kupanga mirathi kabla ya kifo (Estate plan).​
  2. Wosia.​
    • Maana ya Wosia​
    • Sifa za wosia.​
    • Aina za wosia.​
    • Umuhimu wa wosia.​
    • Uandaaji wa Wosia​
    • uhalali wa wosia.​
UMUHIMU WA KUPANGA MIRATHI KABLA YA KIFO (Estate Planning)
Katika sheria ya mirathi nchini Tanzania, estate planning ni mchakato wa kupanga na kusimamia mali ya mtu kabla na baada ya kifo chake. Lengo la kufanya estate planning ni kuhakikisha kwamba mali za marehemu zinagawanywa kwa mujibu wa mapenzi yake na kwa njia inayozingatia maslahi ya warithi wake.

Umuhimu wa estate planning unajumuisha:
  • Kuhakikisha mali zinagawanywa kwa mujibu wa mapenzi ya mwenye mali: Hii inasaidia kuepuka migogoro kati ya warithi na kuhakikisha kwamba mali zinagawanywa kwa haki.
  • Kupunguza gharama na muda wa mchakato wa mirathi: Kwa kupanga mali mapema, inawezekana kupunguza gharama na muda unaotumika katika mchakato wa kisheria wa kugawa mali (mirathi) baada ya kifo.
  • Kulinda maslahi na haki za warithi wadogo na wale wasiojiweza: Estate planning inaweza kujumuisha uundaji wa amana (trusts) ambazo zinaweza kutoa ulinzi na usimamizi wa mali kwa niaba ya warithi ambao hawawezi kujisimamia wenyewe.
Tanzania tuna sheria mbalimbali kama Probate and Administration of Estates Act ambayo inatoa mwongozo wa jinsi mchakato wa mirathi unavyofanyika, ikiwa ni pamoja na jinsi ya kushughulikia mali za marehemu, kulipa madeni yoyote na kugawa mali zilizobaki kwa warithi halali. Ni muhimu kufanya estate planning kwa kuzingatia sheria hizi ili kuepuka matatizo yanayoweza kutokea wakati wa kugawa mali za marehemu.
MAANA YA WOSIA
images (52).jpeg
Naamini wengi tunalijua neno wosia, lakini nini maana yake? Wosia ni tamko au nyaraka ya kisheria ambayo mtu, anayeitwa mwosiaji, anaeleza matakwa yake kuhusu jinsi mali zake zitakavyogawanywa baada ya kifo chake, na kumteua mtu mmoja au zaidi, anayeitwa msimamizi wa mirathi, kusimamia mali hizo hadi zitakapogawanywa kwa warithi halali.

Kanuni ya 2 ya Amri ya Mila za Mahali (Declaration) inafafanua wosia kama uthibitisho uliotolewa kwa hiari na mtu katika uhai wake unaonyesha nia yake kuhusu jinsi angependa mali zake zigawanywe baada ya kifo chake. Amri hiyo unaweza kuipata kwa kubonyeza hapa.

Kwa namna nyingine, em fikiria una sanduku la mali ambalo lina vitu vyako vya thamani; inaweza kuwa pesa, thamani, nyaraka muhimu, au hata kumbukumbu za familia. Sasa, unataka kuhakikisha kwamba vitu hivi vinapata watu sahihi unapokuwa haupo tena. Hapa ndipo wosia unapoingia. Wosia ni kama barua unayoandika ukiwa hai, ukieleza ni nani apate nini kutoka kwenye sanduku lako la mali zako unapofariki. Kwa mfano, unaweza kuandika kwamba mkeo na wanao ndio watatakiwa kupata mirathi yako yote, ama vyovyote upendavyo.

Kwa kufanya hivi, unasaidia kuepusha migogoro kati ya ndugu na jamaa kuhusu nani apate nini. Pia, unaweza kuwa na uhakika kwamba matakwa yako yatafuatwa, na vitu vyako vya thamani vitatunzwa na kugaiwa kama ulivyotaka.
images (47).jpg

Changamoto kubwa nnchini kwetu wengi huona wosia ni kama kujichuria kifo lakini ukweli ni kwamba, wosia ni nyenzo muhimu ya kisheria inayohakikisha kwamba matakwa ya marehemu yanatekelezwa, haki za warithi zinalindwa, na mali za marehemu zinasimamiwa kwa njia iliyo sahihi na yenye haki. Ni muhimu kwa kila mtu kuwa na wosia, hasa kama ana mali ambazo angependa zisimamiwe kwa njia maalum baada ya kifo chake.

AINA ZA WOSIA
Kiujumla, wosia umegawanyika katika aina kuu mbili, amabazo ni wosia wa maandishi na wosia wa mdomo. Lakini aina mbili izi zipo katika makundi mbalimbali kama ifwatavyo;

A.
Wosia Maalumu (Privileged Wills)


Kama inavyoweza kueleweka kutokana na neno 'maalumu' wosia huu ni ule unaofanywa na askari yeyote, mwanajeshi wa anga, wanamaji, au mabaharia ambao wako katika hatari ya kupoteza maisha kutokana na shughuli ama kazi zao. Askari anajumuisha maafisa na maafisa wa vyeo vyote vya huduma lakini haimjumlishi mhandisi raia anayeajiriwa na jeshi, ambaye hana hadhi ya kijeshi.

Askari wakati wa kutengeneza Wosia lazima awe amefikia umri wa utu uzima (miaka 18) na ambapo wosia uliofanywa na askari ni wa mdomo; utakuwa halali kwa mwezi mmoja tu ingawa wosia ulioandikwa utaendelea kuwa halali. Wosia wenye maalum una sifa zifuatazo:
i. Wosia ulioandikwa na mwosiaji kwa mkono na kukamilika hauhitaji kusainiwa na/au kuthibitishwa.
ii. Ikiwa umeandikwa kwa mkono na mtu mwingine tofauti na mwosiaji lazima usainiwe na mwosiaji lakini hauhitaji kuthibitishwa.
iii. Ikiwa Wosia umeandikwa na mtu mwingine na haujasainiwa na mwosiaji, inapaswa kuthibitishwa kwamba Wosia uliandikwa kwa maelekezo ya mwosiaji au ulitambuliwa na yeye kama Wosia wake.
iv. Wosia usiokamilika (ulioandikwa nusu na mwosiaji kufariki kabla aujamaliza kuandikwa) huchukuliwa kuwa halali.
v. Ikiwa mwosiaji ametoa maelekezo ya kuandaa Wosia lakini amefariki kabla Wosia haujaweza kuandaliwa na kutekelezwa, basi maelekezo hayo yanapaswa kuchukuliwa kama Wosia wake, ingawa hayakuwekwa kwa maandishi mbele yake, wala kusomwa kwake.
vi. Ikiwa Wosia umetengenezwa na mwosiaji kwa mdomo mbele ya mashahidi wawili waliopo wakati huo huo, Wosia kama huo utakuwa batili na hauna nguvu baada ya mwezi mmoja kupita tangu kifo cha mwosiaji.


In short, wosia huu huwa maalumu kutokana na mazingira yake. Mfano: Katika kesi ya Gattward dhidi ya Knee, marehemu, askari wa jeshi, baada ya kupokea maelekezo ya kwenda vitani, aliandika barua isiyo na tarehe ilyokuwa na maneno kama: 'ikiwa utapata barua hii na ikitokea nimeuawa vitani, basi mali zangu zote zitakua zako'. Ilibainika kwamba barua hiyo ilikuwa nyaraka ya mwisho inayoweza kuchukua athari kama wosia wa askari huyo kulingana na maana ya Sheria ya Wosia. Barua hiyo ilikuwa wosia wenye haki maalum na kwa hivyo ilikubalika kutumika kama wosia.

B. Wo
sia Usio Maalum.


Wosia usio maalum ni ule unaotengenezwa na mwosiaji yeyote ambaye si askari, mwanajeshi wa anga, au mabaharia walioajiriwa. Wosia huu unaweza kufutwa na mwosiaji kwa kuandaa wosia mwingine au kwa maandishi fulani yanayotangaza nia ya kuufuta na kurekebisha (codicil) wosia huo. Kwamaana nyinginge huu tunaita ni Wosia wa maandishi kwa watu wakawaida wasio na kazi kazi maalumu.

C. W
osia wa Mdomo
Wosia wa mdomo ni ule unaotolewa na kutengenezwa kwa mdomo. Wosia huu lazima ufanyike mbele ya mashahidi wenye uwezo (akili timamu na umri wa kwanzia miaka 18). Kulingana na kanuni ya 11 ya Amri ya Mila ya Mahali, Wosia wa mdomo lazima ushuhudiwe na si chini ya watu wanne. Kanuni inatoa kwamba mashahidi wawili lazima wawe kutoka ukoo wa mwosiaji na wawili wengine lazima watoke kwa watu wengine wasiohusiana.

Ikiwa mashahidi watafariki kabla ya mwosiaji, wosia uliotengenezwa chini ya ushuhuda wao hautakuwa na athari kisheria. Hivyo mtu aliyetengeneza wosia atachukuliwa kuwa amekufa bila wosia na sheria za urithi bila wosia zitatumika. Hata hivyo, ikiwa mashahidi waliosalia ni zaidi ya wawili, basi bado wosia huo utakua na athari na utatumika.

C.
Wosia wa Pamoja
Wosia utachukuliwa kuwa wa pamoja ikiwa wawosiaji wawili watapeana faida za pande zote, kila mmoja akimfanya mwingine kuwa mrithi wake. Ikiwa warithi ni tofauti na waosiaji, Wosia huo si wa pamoja. Kwa jina lingine huitwa, wosia wa mkataba.

Wosia wa Pamoja ni Wosia unaohusisha mkataba wa kutengeneza Wosia. Mkataba mara nyingi ni ule ambao mwosiaji atatengeneza na kudumisha Wosia kwa fomu maalum, kwa sharti la mwosiaji mwingine kutengeneza Wosia kwa fomu nyingine maalum.

Kimsingi wosia wa pamoja ni wosia ambao unajumuisha au unaambatana na mkataba wa kisheria kati ya pande zinazohusika (wahusiaji) ambao unatoa kwamba:
(i) Kila mmoja wao ataacha mali yake kwa warithi walioafikiwa kwa pamoja.
(ii) Hakuna upande utafuta au kufanya mabadiliko kwenye wosia wake bila idhini ya mwingine wakati wa maisha yao ya pamoja.
(iii) Baada ya kifo cha upande mmoja, aliyebaki hai hatafuta wosia wake au kubadilisha ili kubadilisha warithi walioafikiwa kwa pamoja. Ni muhimu kujua kwamba w
osia wa pamoja ni wosia tofauti wosia wa watu wawili.

Wosia wa pamoja ni nadra lakini uaweza kutumika kama njia ya Upangaji wa Mali ili kufikia matokeo maalum yanayohitajika na watengenezaji wa Wosia. Wosia wa pamoja hutumika hasa pale ambapo kuna haja ya kudhibiti biashara au mali kwa vizazi vijavyo kwa warithi maalum, au katika mazingira ya ndoa.

Faida kuu ya kuwa na Wosia wa pamoja ni kwamba wosiaji wana makubaliano ya pamoja yakimkataba. Hii inamaanisha kwamba Wosia wa mtu mwingine hauwezi kufutwa bila idhini ya wote. Hasara kuu ni kwamba ikiwa mwosiaji anataka kubadilisha Wosia wake, mwosiaji mwingine atahitaji kukubaliana, na kutia saini makubaliano yao kwa mabadiliko hayo. Ikiwa mwosiaji mwingine hakubaliani na mabadiliko hayo, Wosia hauwezi kubadilishwa.

D.
Wosia Jumuishi/ shirikishi.
Sasa huu ndio wosia wa watu wawili hutengenezwa pale ambapo kuna hati moja inayojumuisha Wosia wa watu wawili au zaidi, kila mmoja lazima uthibitishwe kwa utofauti. Kwamaana nyinginge, ni pale watu wawili au zaidi Wanapokubaliana kutengeneza Wosia wa pamoja. Wosia huu utakua na athari kisheria baada ya kila kifo cha mwosia yeyote aliyeandaa wosia huo.

Wosia uliotengenezwa na wosiaji wawili au zaidi kama hati moja iliyotekelezwa kwa usahihi na kila mwosiaji akigawa mali zake za pekee au mali zao za pamoja ni Wosia mmoja. Unafanya kazi kwa kifo cha kila mmoja, warithi watakuwa na haki ya mali za mwosiaji aliyekufa. Ni hati moja lakini kisheria, ni kama ina Wosia miwili. Ikiwa mmoja wao atakufa, inafanya kazi kama Wosia wa marehemu bila kusubiri kifo cha mtengenezaji mwingine wa wosia. Kwa hivyo, mirathi inaweza kugaiwa, baada ya kifo cha mtengenezaji yeyote wa Wosia kwa kutoa sehemu ya mali zake.

E.
Wosia wa Masharti.
Wosia ulioelezwa kuchukua athari ama kutumika katika kutokea au kutotokea kwa tukio fulani unaitwa Wosia wa Masharti. Wosia wa Masharti unategemea masharti fulani na ikiwa masharti haya yanakinzana na sheria, basi Wosia huo hauwezi kutekelezwa kisheria.

Wosia huu unaweza kutumika na kuwa na athari kisheria mara tu wakati masharti yaliyotolewa na mwosiaji yanatokea. Kwa mfano, wakati mtengenezaji wa Wosia anasema - "Ikiwa sitarudi" - basi Wosia kama huo ni 'Wosia wa Masharti' kwa sababu kuna masharti. Mtengenezaji wa Wosia anaweza kurudi au asirudi. Lakini pia ikiwa Mtengenezaji wa Wosia anasema - "ikiwa utamuoa binti yangu" basi Wosia kama huo ni 'Wosia wa Masharti' kwa sababu "ndoa" si lazima bali ni sharti la kutimizwa ili wosia huo uweze kutimia.

SIFA ZA WOSIA
Wosia kama nyaraka ya maagizo ya mwisho haina athari yoyote ya kisheria hadi mwosiaji afariki. Athari zake ni za mfululizo. Sifa muhimu za wosia ni kama zifuatavyo:

1. Tamko la Kisheria.
Nyaraka inayodaiwa kuwa wosia au usia lazima iwe ya kisheria, yaani iendane na sheria na itekelezwe na mtu aliye na uwezo wa kisheria kufanya hivyo. Zaidi ya hayo, tamko la nia lazima lihusiane na mali ya mwosiaji. Wosia ni nyaraka ya kisheria, yenye nguvu ya kisheria juu ya mirathi ya mtengeneza wosia na warathi yake kiujumla.

2. Ugawaji wa Mali.
Katika wosia, mwosiaji anarithisha au kuacha mali yake kwa mtu au watu anaowachagua kuwalithisha mali zake.

3. Kueleza Nia.
Matakwa yaliyoonyeshwa katika wosia yanakusudiwa kutekelezwa tu baada ya kifo cha mtu aliyefanya wosia. Hivyo, nyaraka yoyote inayosemekana kuwa wosia wakati nia yake ni kutekelezwa kabla ya kifo cha mtengenezaji wa hati hiyo haina hadhi ya kuitwa wosia.

4. Unabadilika (Ambulatory)
Wosia hubadilika, yaani wosia hauanzi kufanya kazi hadi mtu afe. Kwa mfano, ikiwa mwosiaji anafanya wosia halali leo, wosia huo hauwezi kuwa na athari ya kisheria hadi mwosiaji afe. Kwa hivyo, mwosiaji yuko huru kubadilisha wosia wake mara nyingi kama anavyotaka hadi kifo chake. Kwa maneno mengine, warthi hawana haki ya kurithi chochote hadi mwosiaji afe na wosia ukubaliwe kwa ushahidi ili kuthibitisha yaliyomo kwenye wosia.

Kwa hivyo wosia hauhusishi uhamisho wowote, wala hauathiri uhamisho wowote wa kutoka kwa mtu mmoja aliye hai hadi mwingine, lakini ni hati ambayo mtu anabainisha mtu (msimamizi) pamoja na njia itakayotumika katika usimamizi na ugawaji wa mali yake baada ya kifo chake.

5. Uthibitisho wa Wosia.
Pia, wosia lazima ukubaliwe na mahakama kama ushahidi ili kuthibitisha yaliyomo kwenye wosia. Mahakama yenye mamlaka ya ushahidi ina jukumu la kutekeleza nia ya mwosiaji. Mahakama inafanya hivyo kwa kuhakikisha kwamba mahitaji yote rasmi yametimizwa, kusoma kile wosia unasema, na kisha kusikiliza ushahidi mwingine ikiwa ni lazima.

Ni lazima ieleweke kwamba mahakama kamwe haitaongeza maneno kwenye wosia, lakini inaweza kufuta sehemu za wosia (au wosia wote). Hata hivyo, kawaida maneno ya wosia yanatekelezwa, mradi tu maneno hayo siyo ya utata mwingi.

6. Nyaraka ya siri na umma.
Ndio, hujasoma vibaya. Wosia huwa ni siri ya mwandaa wosia, hata mashaidi wanapaswa kusaini tu bila kujua wosia umeandikwa nini, labda mwandaa wosia aamue kuwaonyesha. Lakini mwandaa wosia anapofariki wosia inakua nyaraka ya umma, which mean mtu yeyote anaweza kuupinga ikiwa anaweza kuthibitisha mapingamizi yake.

Hivyo, ni muhimu kutambua kwamba, wosia ni siri ikiwa mwosiaji bado yupo hai, ila anapofariki mtu yeyote anaruhusiwa kuuona na kuusoma na kuupinga pia.

7. Uwezekano wa Kufutwa
Kwa kuwa wosia unatekelezwa baada ya kifo cha mwosiaji na ni uonyeshaji wa nia ya mwosiaji, unaweza kufutwa wakati wowote wakati wa uhai wa mwosiaji. Inaweza kufutwa hata ikiwa wosia huo unasema kwamba hauwezi kufutwa.

UMUHIMU WA WOSIA
Katika kesi ya mgogoro wa mirathi ya Adv. Melchisedeck Sangalali Lutema, Jaji Mnyukwa wa mahakama kuu alianza kwa kueleza umuhimu wa wosia, nanukuu maneno yake kwa kiswahili 👇.
"Kifo ni msukosuko usiotarajiwa ambao hakuna mtu anayejua utatokea lini, hivyo, watu wanashauriwa kwamba, wakiwa bado na afya na hai waandike jinsi mali zao zitakavyosimamiwa baada ya kifo, ambacho kwa hakika kitapunguza migogoro mingi na mkanganyiko miongoni mwa warithi".
Screenshot_20240426-015905.jpg

Unaweza soma kesi hii yote hapa
Mtu anaweza kuhakikisha jinsi mali yake itakavyorithishwa na nani itarithishwa baada ya kifo chake kupitia Wosia. Ikiwa mtu atafariki bila kuacha Wosia, mali yake itarithishwa kwa njia ya sheria za urithi zisizo na wosia na si urithi wa wosia.
images (48).jpeg


I. Utekelezaji wa Nia ya Mwosiaji.
Ni bora mtu aandae Wosia ili kuhakikisha kwamba nia yake halisi inafuatwa na mali inarithishwa ipasavyo. Wosia ni chombo muhimu cha urithi ambacho mwosiaji anaweza kutoa mali yake kulingana na matakwa yake.

images (50).jpg


II. Ufichuzi wa Mali ya Marehemu.
Kutengeneza wosia kunamwezesha mwosiaji kufichua mali zote anazomiliki au alizokuwa nazo wakati wa kifo, ambazo hazijulikani kwa warithi na wenufaika na kuzigawa hata pale ambapo haiwezekani chini ya urithi usio na wosia kufichuliwa kwa urahisi.

III. Maelekezo ya Ugawaji wa Mali.
Kwa kuwa na Wosia mwosiaji anaweza kuacha maelekezo ya ugawaji wa mali yake na mwosiaji anaweza kumteua mtu kama msimamizi wa Wosia wake ili kutekeleza maelekezo haya kwa niaba yake.
images (49).jpeg


IV. Maelekezo ya Utunzaji wa Mwili wa Marehemu.
Pia, Wosia ni nyaraka inayobeba maelekezo na matakwa ya mwosiaji jinsi angependa mwili wake ushughulikiwe au kuzikwa baada ya kifo. Wosia unamwezesha mwosiaji kuelekeza njia sahihi za mazishi yake au utoaji wa mwili wake kwa utafiti wa matibabu au kisayansi.

images (53).jpeg


V. Kueleza Matakwa ya Mwisho.
Wosia unamruhusu mwosiaji kueleza matakwa yake ya mwisho na kuwaarifu wapendwa wake kwamba alitenga muda kufikiria na kuwapangia urithi wao baada ya yeye kuondoka.

images (53).jpg


VI. Uhifadhi wa Mali Baada ya Kifo.
Katika maisha yetu mwosiaji anazingatia jinsi ya kukusanya na kusimamia mali yake ili awe na utajiri wa kutosha wakati wa uhai wake. Hata hivyo, mwosiaji pia anahitaji kuzingatia kuhifadhi mali hizo baada ya kifo na kuhakikisha kwamba utajiri unahamishiwa kizazi kijacho. Wosia uliopangwa vizuri ni sehemu muhimu na ya msingi ya mpango wa mali ya mwosiaji. Pia, Wosia unamruhusu mwosiaji kuamua wapi au kwa nani mali zake zitagawanywa baada ya kifo chake, na kwa kufanya hivyo, huhifadhi na kulinda mali ambazo mwosiaji ametumia maisha yake yote kuzikusanya.

VII. Kuepuka Migogoro Juu ya Mali.
Mgawanyo wa mali baada ya kifo huja na hisia nyingi. Tofauti ndogo zinaweza kusababisha majonzi na lawama. Kadri mirathi inavyozidi kuwa migumu ndivyo familia zinavyozidi kuwa na migogoro ya ugawaji wa mali unavyozidi kuwa mgumu zaidi.

Wosia unaoeleza wazi matakwa ya mwosiaji unaweza kupunguza migogoro na uvumi kuhusu mwosiaji.
Kwa mfano, ikiwa mwosiaji yuko katika ndoa ya pili na ana watoto kutoka ndoa yake ya kwanza anaweza kutaka kutumia wosia kugawa mali yake kwa wazi kati ya mke wake wa pili na watoto.
images (51).jpeg


VIII. Kuepuka Sheria za Urithi Bila Wosia.
Nadhani tunatambuwa kuwa sheria za urithi zinatofautiana kulingana na either dini ama kabila. Hivyo basi bila wosia mirathi itagawanywa kulingana na sheria za mirathi (kidini au kikabila) ambayo inaweza kutoa matokeo yasiyoridhisha.

Kuwa na wosia kunaweza kumpa mwosiaji amani ya akili na kuzuia familia yake kupigania mali. Mtu anapofariki bila wosia au mpango mwingine wa mali, sheria za serikali zinazojulikana kama 'sheria za urithi bila wosia' zinaamua ni wanafamilia gani watarithi mali ya mwosiaji na kwa uwiano gani.

IX. Uteuzi wa Wasimamizi.
Wosia pia unamruhusu mwosiaji kuepuka kuwa na msimamizi aliyeteuliwa na mahakama na gharama zinazohusiana. Kuwa na wosia kunahakikisha kwamba sheria za serikali hazitaamua ugawaji wa mali za mwosiaji, ulezi wa watoto wa mwosiaji, au utunzaji wa wale walio chini ya jukumu lake wenye mahitaji maalum.

X. Uteuzi wa Walezi.
Kuandika Wosia ni muhimu hasa ikiwa kuna watoto kwani inampa mwosiaji fursa ya kuteua walezi. Matukio kadhaa yanaweza kuathiri nani anaweza kudai dhidi ya mali. Wosia pia unaweza kutoa maelekezo kuhusu ulezi wa kisheria wa watoto wa mwosiaji na mali zao.

UTENGENEZAJI WA WOSIA
Kutengeneza Wosia kunasaidia kupanga kinachotakiwa kutokea baada ya kifo, lakini hakuna kinachoweza kutuandaa vya kutosha kwa msiba wa kupoteza mpendwa. Shughuli nyingi za kila siku zinahitaji umakini na maamuzi muhimu yanaweza kuhitajika kufanywa kuhusu mali na vitu binafsi vya marehemu kwa mfano, iwapo nyumba inapaswa kuuzwa.

Hivyo, katika mhadhara huu, tunatakiwa kuwa na maarifa na ujuzi kuhusu jinsi Wosia unavyotengenezwa na nini kinachoamua uhalali wake. Tutaelewa mahitaji ya kisheria kwa utengenezaji wa Wosia na taratibu za utengenezaji wa Wosia. Mwishowe tutakuwa na ufahamu wa uamuzi wa uhalali wa wosia.

Kutengeneza Wosia ni mchakato unaohusisha hatua kadhaa za kisheria na taratibu ambazo zinapaswa kufuatwa ili kuhakikisha kwamba Wosia ni halali na unaweza kutekelezwa kama ilivyokusudiwa na mwosiaji. Hii inajumuisha kuhakikisha kwamba Wosia umeandikwa kwa njia inayokubalika kisheria, umesainiwa na mashahidi, na unawakilisha nia ya kweli ya mwosiaji.

Uhalali wa Wosia unaweza kuathiriwa na mambo kama vile uwezo wa kiakili wa mwosiaji wakati wa kutengeneza Wosia, ushawishi wa nje, na uwepo wa masharti yasiyokubalika kisheria. Ni muhimu kwa mtu yeyote anayetengeneza Wosia kushauriana na mtaalamu wa sheria ili kuhakikisha kwamba taratibu zote zinafuatwa ipasavyo. Katika kuandaa wosia kuna mambo mawili muhimu yakuzingatia, ambayo ni
uwezo wa kuandaa wosia na taratibu za kisheria.

i) Uwezo wa Kuandaa Wosia (Testamentary capacity).
Uwezo wa kuandaa wosia hutumika kuelezea uwezo wa kisheria na kiakili wa mtu kufanya au kubadilisha wosia halali. Dhana hii pia imeitwa akili timamu na kumbukumbu au akili ya kufanya maamuzi na kumbukumbu. Hivyo kisheria, si kila mtu anaweza kuandaa wosia.

images (54).jpeg

Je, ni nani anayeweza kuandaa wosia? Sheria inamruhusu mtu yeyote mwenye uwezo wa kuandaa waosia, kuandaa wosia (japo inashauriwa kutafuta mwanasheria ili kuandaa wosia genuine). Mtu atachukuliwa kuwa ana uwezo wa kuandaa wosia ikiwa:
i. Anaelewa asili ya wosia na matokeo yake.
ii. Anaelewa ukubwa, wingi na aina ya mali anayogawa.
iii. kwamba hakuna na ugonjwa wa akili utakaoharibu uwezo wake, kupotosha hisia zake za haki, au kuzuia utekelezaji wa uwezo wake wa asili. Mfano; ikiwa mwosiaji ni maututi.
v. kwamba hakuna upotoshaji wa akili utakaomshawishi katika ugawaji wa mali ya mwosiaji na kuleta ugawaji ambao, ikiwa akili ingekuwa timamu, usingefanyika.

Msingi katika sheria ya kawaida ni kwamba wosia ni batili isipokuwa ikiwa umetengenezwa na mtu ambaye wakati huo alikuwa na uwezo wa kufanya hivyo. Ni kanuni ya jumla kwamba watoto wadogo na watu wenye akili punguani hawana uwezo wa kuandika wosia halali. Hata hivyo, wosia uliofanywa wakati wa utoto wa mtu unaweza kuthibitishwa kwa kutekelezwa tena au kwa marekebisho, wakati mwosiaji anapofikia umri wa utu uzima. Kuwa kiziwi, bubu au kipofu hakumfanyi mtu asiweze kutengeneza wosia ikiwa yuko katika hali timamu ya akili na anaelewa vitendo vyake. Mtu ambaye kawaida ni mwendawazimu pia anaweza kutengeneza wosia wakati wa vipindi ambavyo yuko katika hali timamu ya akili.

Pia imethibitishwa vizuri kwamba wosia uliofanywa na mtu ambaye amelewa au kutokana na kuwa chini ya ushawishi wa pombe amepoteza uwezo wake wa kiakili na uelewa hivyo ni batili na hauna athari yoyote kisheria.
Also, wosia au sehemu yoyote ya wosia ambao utengenezaji wake umesababishwa na udanganyifu au nguvu au kwa ushawishi kama huo unaondoa hiari ya mwosiaji au umesababishwa na kosa ni batili.

b) Taratibu za Kisheria za Wosia.
Wosia umeelezwa kama tamko la kisheria la nia ya mwosiaji kwa ajili ya ugawaji wa mali yake baada ya kifo chake, hivyo ni muhimu kutambua kwamba nyaraka zinazodaiwa kuwa wosia lazima ziwe za kisheria; matumizi ya neno wosia kwenye nyaraka pekee hayatoshi kuhalalisha wosia. Hivyo, ni muhimu kuzingatia taratibu zifuatazo ili kuweza kutengeneza wosia halali kisheria.

1. Uandishi.
Wosia unaweza kuandikwa katika fomu yoyote maalum ya wosia iliyoandikwa inadhaniwa kwamba wosia unaweza kuwa wa mkono, typed, printed au katika fomu ya lithographed. Uandishi unaweza kuwa wa mwosiaji au wa mtu mwingine yeyote. Unaweza kuwa katika lugha yoyote. Kesi za sheria zinaonyesha kwamba inaweza hata kwa code ilimradi code hiyo inaweza kufumbuliwa. Ipo kesi mashughuli kati ya
Hodson na Barnes ambapo wosia ulioandikwa kwenye ganda la yai na ulikubaliwa kwawua ulifata matakwa ya kisheria. Unaweza soma kisi hiyo hapa

2. Saini.
Kwa ujumla mahakama zimetafsiri saini ni kuweka alama yoyote ya mwosiaji ambayo inakusudiwa kama saini kwa mfano alama ya kidole gumba, herufi za kwanza, alama kwa muhuri wa mwosiaji na vyote vimehesabiwa kama saini halali. Hata hivyo, haina haja hata ya kuwa na jina. Katika kesi ya
Re Cook’s Estate (1960) maneno "your loving mother (mama yako kipenzi)" yaliyowekwa mwishoni mwa wosia na yalihesabiwa kuwa saini halali.

Dhana ya “uwepo” ina vipimo vya kimwili na kiakili. Kwa kuwa saini inapaswa kutiwa chini ya maelekezo ya mwosiaji, hali ya kimwili na kiakili ya mwosiaji inapaswa kuwa kiasi kwamba anaweza kupinga au kukubali saini iliyotiwa kwa niaba yake. Wosia kawaida utatiwa saini kwa niaba ya mwosiaji katika mazingira ambapo yeye ni dhaifu mno kupitia ugonjwa ama sababu nyingine inayosababisha ashindwekutia saini yeye mwenyewe.

Mtu anayetia saini kwa niaba ya mwosiaji anaweza kutia saini yake mwenyewe au kwa jina la mwosiaji na mtu huyo anaweza kuwa mmoja wa mashahidi wa wosia. Hata hivyo, itakuwa busara zaidi kwa mtu anayetia saini kwa niaba ya mwosiaji kutia saini yake mwenyewe na kueleza kwamba anatia saini kwa niaba ya mwosiaji, mbele ya mwosiaji na chini ya maelekezo yake. Hii ingeondoa utata wowote kama mtu huyo anatia saini kama mwosiaji au kama shahidi anayethibitisha.

3. Mashahidi.
Sheria inahitaji kuwepo kwa idadi ya mashahidi wakati wosia unapotengenezwa. Ingawa hakuna sifa rasmi za kuwa shahidi, ni muhimu kwamba shahidi asiwe na maslahi katika wosia. Ikiwa shahidi ana maslahi, ushahidi wake kuhusu mazingira utakuwa wa shaka kwa sababu atafaidika kutokana na kukubaliwa kwake kwa ushahidi. Wosia unatakiwa kusainiwa na mashahidi kwanzia wawili ambao hawana haja ya kuwepo wakati huo huo, yani kila mtu anaweza kusign kwa muda wake. However, ikiwa shahidi atasign lakini hajui kama anasaini wosia, saini yake itakuwa batili.

Wosia uliosainiwa na shahidi mmoja, kama ilivyokuwa katika Kesi ya ya mirathi ya Mali za Susan Kanini Kilonzo (marehemu) Nairobi HCSC Na. 2669 ya 2002), utakuwa batili na hauna athari. Kuwepo wakati wa kusaini kunamaanisha mashahidi lazima waweze kumuona mwosiaji akisaini. Kushuhudia kunamaanisha saini yaani ukweli wa kusaini. Mashahidi hawana haja ya kuangalia saini au hata kujua kwamba nyaraka ni wosia.

5. Dhana ya Utekelezaji Sahihi.

Wosia unatakiwa uwe na uwezo wa kutekelezeka kisheri. Mfano, hauwezi kuandika wosia eti "nikifa mke wangu asiolewe" wosia unatakiwa uwe na uwezo wa kutekelezeka kwa usahihi.
UHALALI WA WOSIA
Uhalali wa wosia unaweza kuamuliwa na mahitaji mbalimbali ya kiutaratibu na kisheria kama tulivyokwishi yaona katika kipengele cha utengenezaji wa wosia hapk juu. Ukosefu wa mahitaji na taratibu yoyote ya kunafanya wosia uliotengenezwa kuwa batili machoni mwa sheria. Hivyo, mwosiaji aliyetengeneza wosia uliotangazwa kuwa batili anachukuliwa kuwa amekufa bila wosia.

Animus Testandi “nia ya kutengeneza wosia”

Ili wosia uwe halali machoni mwa sheria, lazima uwe umetengenezwa kulingana na nia ya mwosiaji. Mwosiaji lazima awe na nia ya hiari ya kutengeneza wosia kama huo. Hivyo, kikwazo chochote kwa animus testandi ya mwosiaji kinaharibu uhalali wa wosia kwa sababu mwosiaji hakukusudia kwa hiari yake mwenyewe. Ikiwa mtu ataandika wosia akiwa amelewa, wosia huo utakua batili.

Uwezo wa Kutengeneza Wosia
Pia, sheria ya urithi inahitaji wosia uwe umetengenezwa na mtu mwenye uwezo ili kufanya uhamisho wa mali yake kwa mtu mwingine baada ya kifo chake. Uwezo wa kutengeneza wosia unapimwa kupitia umri wa utu uzima, akili timamu, kumbukumbu timamu na uelewa timamu. Hivyo, bila ya kuwa na uwezo wa kutengeneza wosia, wosia uliotengenezwa ni batili hivyo hauwezi kugawa mali ya mwosiaji baada ya kifo chake.

Uhalisi wa Wosia.
Wosia lazima uwe halisi ili kutosheleza ugawaji wa mirathi ya kwenye wosia kwa haki. Wosia unapochafuliwa na udanganyifu, ughushi na mambo mengine yanayoathiri uhalisi wake, wosia huo unakuwa batili hivyo hauwezi kutekeleza ugawaji wa wosia.

Taratibu za Kisheria za Wosia.
Pia, sheria inahitaji baadhi ya mahitaji muhimu ya kisheria yanayohitajika wakati wa kutengeneza na kutekeleza wosia. Kushindwa kufanya hivyo, kunaweza kufanya wosia kuwa batili. Taratibu hizo ni kama: kurithi warithi halali (legal heir) ikiwa wosia hatomrithisha mrithi halali, ni lazima atoe sababu pamoja na kufata misingi ya sheria ya urithi (law of inheritance/ succession).

Hapa itakumbukwa kesi mashughuli ya mirathi ya Mengi baada ya Mengi kutowarithisha watoto wake wakubwa chochote na kusema yeyote akayepinga mirathi yake alipwe buku. Ambapo Jaji Mlyambina aliamua kwamba, iwapo mwosiaji hatorithisha mrithi halali, sharti atoe sababu za kufanya hivyo. Unweza soma kesi hii hapa.


Natumai elimu hii itakua imemuwezesha msomaji kujua mambo mengi kuhusu wosia na umuhimu, hata hivyo bado nimeacha mambo mengi, hivyo nitashare baadhi ya vitabu vilivyoandikwa kwa kiswahili na uraisi juu ya maswala ya mirathi as PDF pamoja na mfano wa Wosia as Word (ili iwe rahisi ku edit kwa atakayetaka kutumia) hapa chini 👇. #JielimisheKisheria
 

Attachments

  • images (51).jpeg
    images (51).jpeg
    56.2 KB · Views: 3
  • images (54).jpeg
    images (54).jpeg
    71.5 KB · Views: 3
  • images (50).jpg
    images (50).jpg
    43.7 KB · Views: 3
  • images (54).jpeg
    images (54).jpeg
    71.5 KB · Views: 2
  • images (54).jpeg
    images (54).jpeg
    71.5 KB · Views: 2
  • Mirathi wosia na taratibu zake.pdf
    2.8 MB · Views: 3
  • WOSIA.pdf
    2.2 MB · Views: 3
  • Wosia - Mfano na 1.docx
    31.1 KB · Views: 2
Mada yenye faida sana kwangu. Je, ni lazima uzingatie mgao wa kisheria katika wosia? Mfano mke anatakiwa kupewa nusu kwenye mirathi, je ni kazima wosia uzingatie hilo au naweza hata nikampa tofauti?
 
Mada yenye faida sana kwangu. Je, ni lazima uzingatie mgao wa kisheria katika wosia? Mfano mke anatakiwa kupewa nusu kwenye mirathi, je ni kazima wosia uzingatie hilo au naweza hata nikampa tofauti?
Kuandika wosia inategemeana na sheria ya urithi inayotumika either ya kidini ama kimila (kitamaduni). Sheria hizi Tanzania zimegawanyika kama ifuatavyo:
  • Za Kiislamu (Quran). Ikiwa utafata sheria hizi kuandika wosia basi utatakiwa kuandika vile surat An-Nisa aya ya 11 inavyoelekeza.​
  • Za kikristo (Indian Succession Act). hapa utaandika vyovyote utakavyo kwakua sheria hizi zina total testamentary capacity(uwezo kamili wa kuandika wosoi vile utakavyo), isipokua tu pale utakapo muondoa / kumnyima mirathi mrithi halali (legal heir) katika wosia wako ni lazima utoe sababu ya kufanya hivyo.​
  • Za kitamaduni (hizi utofautiana kulingana na kabila na tamaduni za watu wa jamii husika)​
Nadhani nimejaribu kujibu swali lako, japo swala hili la sheria za urithi (Law of succession or inheritance) nimeshawahi kulielezea kidogo, unaweza kulisoma hapa. Hata hivyo, bado ni muhimu kushauriana na mtaalamu wa sheria kabla ya kuandika wosi.
 
Kuandika wosia inategemeana na sheria ya urithi inayotumika either ya kidini ama kimila (kitamaduni). Sheria hizi Tanzania zimegawanyika kama ifuatavyo:
  • Za Kiislamu (Quran). Ikiwa utafata sheria hizi kuandika wosia basi utatakiwa kuandika vile surat An-Nisa aya ya 11 inavyoelekeza.​
  • Za kikristo (Indian Succession Act). hapa utaandika vyovyote utakavyo kwakua sheria hizi zina total testamentary capacity(uwezo kamili wa kuandika wosoi vile utakavyo), isipokua tu pale utakapo muondoa / kumnyima mirathi mrithi halali (legal heir) katika wosia wako ni lazima utoe sababu ya kufanya hivyo.​
  • Za kitamaduni (hizi utofautiana kulingana na kabila na tamaduni za watu wa jamii husika)​
Nadhani nimejaribu kujibu swali lako, japo swala hili la sheria za urithi (Law of succession or inheritance) nimeshawahi kulielezea kidogo, unaweza kulisoma hapa. Hata hivyo, bado ni muhimu kushauriana na mtaalamu wa sheria kabla ya kuandika wosi.
Asante mkuu swali langu umelijibu. Swali la nyongeza. Mirathi bila wosia, mke ana haki ya kurithi mali alizozikuta?
 
Asante mkuu swali langu umelijibu. Swali la nyongeza. Mirathi bila wosia, mke ana haki ya kurithi mali alizozikuta?
Ndio, anayo haki kwani yeye pia ni moja ya ma legal heir, legal heirs inajumuisha; mwenza (mke au mume) na watoto. Na kama ni mke, lazima awe ni mke halali wa ndoa katika uso wa sheria.
 
Back
Top Bottom