SoC03 Nani anatukwamisha Afrika?

Stories of Change - 2023 Competition

Davies Nicholaus

New Member
Jun 5, 2023
2
2
Zaidi ya Miongo mitano imepita baada ya mataifa mengi ya Kiafrika kupata uhuru wao kutoka Kwa wakoloni . Lakini Bado hali ya maendeleo katika sekta mbali mbali kama vile elimu, afya, miundombinu na sayansi na teknolojia hairidhishi Wala kuleta matumaini kwamba ipo siku itabadilika na kuwa nzuri. Lakini badala yake mkwamo umekuwa ukishuhudiwa kila Leo. Swali kubwa ni je nani anatukwamisha?. Je, ni muda mwingi ambao tumekuwa chini ya utawala wa kikoloni na kushindwa kujiendeleza wenyewe?, Ama nini zaidi kinaleta mkwamo?

Yapo mataifa ya Asia ambayo yalipata uhuru wao katika kipindi karibu sawa na mataifa ya Kiafrika lakini sasa yameendelea kuliko mataifa ya Kiafrika.

Maoni yangu kuhusu mkwamo huu ni kama ifuatavyo:
Mosi, Wanasiasa mbali mbali wa Afrika ambao hupata nafasi kuwa viongozi wa mataifa yao, wanapaswa kutambua changamoto mbali mbali zinazo yakabili mataifa yao kabla ya kupata nafasi ya kuingia katika madaraka kutafuta suluhu ya changamoto hizo wanapo kuwa madarakani na sio kutafuta kutimiza matakwa yao binafsi.

Pili, viongozi wa Kiafrika ni muhimu kuweka mbele uzalendo na utaifa kuliko kulinda maslahi ya vyama vyao vya siasa na maslahi yao binafsi. Aidha ni vizuri baada ya uchaguzi Wanasiasa wote ( walioshinda na walioshindwa) washirikiane kuhakikisha changamoto za kimaendeleo zinatatuliwa na sio kutumia muda mwingi kutupiana vijembe vya kisiasa na kupingana katika kila jambo.

Tatu, watumishi wa umma wanapaswa kuwatumikia Kwa uadilifu na Kwa nia ya kuwasaidia wananchi, na sio kuendekeza maslahi binafsi na kuomba rushwa Kwa wananchi. Wananchi hulipa Kodi ambazo serikali huzitumia kuwasomesha watumishi hao wa umma na wanapopata taaluma zao, serikali hutumia kodi hizo hizo kuwaajiri na kuwalipa mishahara, lakini watumishi hao wengi wao wamesahau fadhila hizo na wameishia kuwatesa wanao wapa huduma, mathalani muuguzi hospitalini anaweza kumtolea lugha chafu mgonjwa ambaye analipa kodi iliyo muwezesha yeye kuwa muuguzi na inayo wezesha ulipwaji wa mshahara wake.

Mambo hayo na mengine mengi yamekuwa chanzo Cha mkwamo wa kimaendeleo katika mataifa mengi ya bara la Aftika. Ni vema watumishi wa umma kuwajibika kikamilifu kuwapa huduma wananchi ili kuchochea shughuli za kimaendeleo.

Aidha ni muhimu kupunguza urasimu katika utoaji wa huduma za kijamii Kwa wananchi, ili kupunguza muda wa upatikanaji wa huduma na kuongeza wa kufanya shughuli za uzalishaji Mali.

Nne, ni muhimu pia Kwa wananchi kufahamu jukumu la kuleta maendeleo katika jamii na taifa Kwa ujumla, si kazi ya serekali pekee, ama viongozi wa kisiasa Bali ni jukumu la kila mmoja . Hivyo ni muhimu wananchi kuhakikisha wanawajibika kikamilifu katikati shughuli za uzalishaji mali Ili kukuza pato la taifa, pia wanalipa kodi kama inavyoelekezwa na sheria na kanuni mbali mbali za nchi. Aidha ni wajibu wa wananchi kujiepusha na vitendo vya rushwa ambavyo vinachangia Kwa kiasi kikubwa kurudisha nyuma maendeleo ya taifa . Pia ni wajibu wa kila mwananchi kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa amani kama maandamano yasiyofuata misingi ya kisheria vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa mfano wakulima na wafugaji. Kwani Kwa pamoja vitendo hivyo hurudisha nyuma maendeleo ya taifa.

Tano, ni vyema kila taifa barani Afrika likawa na dira ya maendeleo (mpango wa maendeleo wa taifa) inayo onyesha muda na hatua ya kimaendeleo inayotakiwa kufikiwa ndani ya huo muda (kwa mfano Tanzania mwaka 2025 upatikanaji wa maji na umeme 100%). Mipango ya dira ya maendeleo inapaswa kujulikana na kila mwananchi na iwe shauku ya kila raia kuona mipango hiyo inatekelezwa bila kujali itikadi za vyama, dini Wala kabila. Dira ya maendeleo haipaswi kuwa mpango wa chama kimoja Cha Siasa pekee bali uwe ni mpango wa taifa zima katika kujikwamua kutoka kwenye umaskini.

Ni vizuri dira hii ya maendeleo (mpango wa taifa wa maendeleo) ikatengenezwa na wataalamu mbali mbali waliopo katika taifa husika bila kujali itikadi zao za vyama, dini Wala kabila. Ikiwezekana Wanasiasa kutoka vyama vyote vya kisiasa washirikishwe. Pia liwepo azimio la kitaifa ya kwamba kiongozi yeyote au chama chochote Cha siasa kitakacho pata madaraka kinapaswa kusimamia utakelezwaji wa mpango huo (Dira ya maendeleo) na kuhakikisha mpango huo unakamilika Kwa wakati kama ilivyo ainishwa. Ni vema pia wakati wa chaguzi za kisiasa ilani za vyama vya siasa na sera za wagombea vikajikita katika kuelezea ni Kwa namna gani mpango wa maendeleo wa taifa utafikiwa kulingana na muda uliopangwa na wataalamu. Hii itawasaidia wananchi kufanya chaguo sahihi kirahisi wakati wa uchaguzi.

Mwisho, lakini siyo kwa umuhimu ni vyema Waafrika Kwa pamoja wakatambua kwamba wanalo jukumu la ziada la kubadilisha hali ya maisha waliyo kuwa nayo, na inawezekana kufanya hivyo. Ni muhimu wananchi kufanya kazi Kwa bidii na kulipa kodi, viongozi kujali maslahi mapana ya mataifa yao, na watumishi wa umma kupenda fani zao na kupenda kuwatumikia wananchi pia kuona mzigo wa kuwatumikia wananchi ni wao. Kwa pamoja wapinge rushwa Kwa vitendo.

Mkwamo wa kimaendeleo uliopo Afrika Kwa kiasi kikubwa sana umechangiw na Waafrika wenyewe, lakini pia upo uwezekano wa kupiga hatua za maendeleo Kwa haraka sana hasa Kwa kuzingatia zama hizi za maendeleo ya sayansi na teknolojia. Afrika haikuumbwa kuwa maskini tunaweza kutoka hapa tulipo uamuzi ni wetu soto

Na Davies Nicholaus
 
Elimu ya Africa bado haimkomboi,haimfundishi mwafrica kujitegemea,kujisimamia na kujiongoza hvy bado elimu inahitajika iboleshwe ili mwafrica ajitagemee
 
Back
Top Bottom