Kitabu: Maisha ya Malcom X

Sura ya tano inaendelea.

Kufukuzwa kazi lilikuwa ni jambo ambalo halikwepeki. Kilichonimaliza ilikuwa ni barua ya hasira kutoka kwa mteja mmoja. Wasimamizi wa treni nao waliongezea kwa kusema jinsi walivyoletewa malalamiko mengi kunihusu, na maonyo niliyopata.

Lakini sikujali kitu, kwenye wakati ule wa vita, kazi nyingi nilitamani kufanya zilikuwa zinatafuta watu. Nlipolipwa stahiki zangu, nikaonelea ni vyema kwenda Lansing kuwasalimu ndugu zangu. Nilikuwa na ofa ya kusafiri bure kwa treni.

Hakuna hata mmoja kule Michigan aliyeamini kuwa ni mimi. Ni kaka yangu mkubwa tu, Wilfred ndiye hakuwepo. Alikuwa huko Chuo Kikuu cha Wilberforce, Ohio akijifunza ujuzi fulani. Philbert na Hilda walikuwa wakifanya kazi Lansing. Reginald, yule aliyekuwa akinitegemea, alikuwa mkubwa kiasi cha kuweza kudanganya umri, alikuwa amepanga kujiunga na meli za biashara karibuni. Yvonne, Wesley na Robert walikuwa shuleni.

Nywele zangu zilizotiwa dawa na mavazi yangu vilistaajabisha kiasi kwamba ningeweza chukuliwa kuwa ni mtu wa kutoka sayari nyingine. Hata nilisababisha ajali ndogo, dereva mmoja alisimama kunishangaa na wa nyuma yake akamgonga. Muonekano wangu uliwastaajabisha vijana wakubwa ambao hapo zamani niliwaonea wivu na kuwahususdu; wakati wa salamu nilitoa mkono na kusema “Skin me, Daddy-o!” Simulizi zangu juu ya New York, huku nikiwa bangi muda wote. “My man! . . . Gimme some skin!”

Kitu pekee kilichoninyenyekeza ni nilipotembelea Hospitali ya Kalamazoo. Mama yangu ni kama hakunitambua sawasawa.

Pia nilienda kumtembelea mama yake Shorty. Nilijua kuwa Shorty atathamini sana mimi kufanya hivyo. Alikuwa ni mwanamke mzee na alifurahi kusikia habari za Shorty. Nilimwambia kuwa Shorty anaendelea vizuri na siku moja atakuwa kiongozi mkubwa wa bendi yake. Aliniambia nimwambie Shorty amuandikie barua na kumtumia chochote kitu.

Nilipita pia Mason kumtembelea bibi Swerlin. Zoot yangu ya rangi ya papa, viatu vyangu virefu na vilivyotuna mbele na kofia yangu ya pama juu ya nywele zangu nyekundu zilizokolea dawa vilimuelemea vilimmaliza kabisa bibi Swerlin. Alijitahidi tu kuweza kunikaribisha. Namna nilivyoonekana na jinsi nilivyoongea vilimfanya awe na wasiwasi sana, kiukweli sote tulijihisi afadhali nilipoaga na kuondoka.

Usiku wa kuamkia kuondoka kulikuwa na dansi kwenye ukumbi wa shule ya sekondari ya Lincoln(Nilijifunza kuwa ukitaka kuwapata watu weusi kwenye mji wowote bila ya kuuliza, nenda kwenye kitabu cha orodha ya namba za simu na tafuta “Lincoln School” Mara zote ilikuwa kwenye maeneo ya watu weusi-hasa katika siku zile.)ningeondoka Lansing bila ya kuhudhuria dansi, lakini sasa nilikuwa ukumbini nikiwarusha wasichana wadogo kupita mabegani mwangu. Mara kadhaa bendi ilisimama na wachezaji wengine walikaa pembeni huku macho yamewatoka kama visosa. Usiku huo kuna watu hata waliniomba kusaini vitu vyao, “Harlem Red” Niliiacha Lansing ikiwa imepigwa na butwaa.

Niliporudi New York, nikiwa sina kitu wala kazi yoyote ya kunitegemeza, nikatambua kuwa kazi ya reli ndiyo ilikuwa kila kitu kwangu, basi nikaenda kwenye shirika la reli la Seaboard kuomba kazi. Mashirika ya reli yalikuwa na uhitaji mkubwa wa wafanyakazi kiasi kwamba nilichofanya ni kuwaambia tu kuwa nilifanya kazi kwenye shirika la New Haven na siku mbili mbele nilikuwa kwenye treni ya “Silver Meteor” iliyoelekea St. Petersburg na Miami. Nilikuwa nikikodisha mito na kusafisha mabehewa, na kuwafurahisha abiria wa kizungu. Nilitengeneza kiasi kama kile nilichotengeneza wakati wa kuuza sandwich

Haikuchukua muda nikawa nimegombana na mzungu mmoja kutoka Florida ambaye alikuwa ni msimamizi msaidizi. Niliporudi New York wakaniambia nitafute kazi nyingine. Lakini jioni hiyohiyo nilipoenda Small’s Paradise, mmoja wa wahudumu, kwa kufahamu jinsi nilivyoipenda New York, aliniita pembeni na kuniambia kuwa iwapo niko tayari kuacha kazi kwenye shirika la reli, nitaweza kumbadili mhudumu wa mchana ambaye alikuwa ameitwa kutumikia jeshini.

Mmiliki wa bar ile aliitwa Ed Small, yeye na kaka yake aliyeitwa Charlie waliivana sana, na nadhani Harlem hakukuwa na watu walioheshimika na maarufu kama hao. Walifahamu kuwa nilifanya kazi kwenye shirika la reli, jambo ambalo kwa mhudumu lilikuwa ni uzoefu muhimu sana. Niliongea na Charlie Small ofisini kwao. Nilikuwa na wasiwasi kuwa atawauliza baadhi ya rafiki zake wa siku nyingi waliofanya kazi kwenye shirika la reli wampe maoni yao kunihusu. Charlie asingekubali kufanya kazi na mtu yeyote mwenye sifa ya ujeuri. Lakini aliamua kutokana na maoni yake mwenyewe, baada ya kuwa ameniona kwenye baa yao mara nyingi, nikiwa mtulivu, nikiangalia tu pilikapilika zinavyoenda. Aliniuliza iwapo nimewahi ingia matatizoni na polisi nami nikajibu hapana, na mpaka wakati huo hilo lilikuwa ni kweli. Charlie akaniambia kuhusu sheria za wafanyakazi wa pale. Kuchelewa na uvivu ni marufuku. Wizi hautakiwi na hakuna kuwatoa pesa wateja kwa namna yoyote ile, hasa askari. Basi nikawa nimeajiriwa.

Hii ilikuwa ni mwaka 1942, ndiyo nilikuwa nimeingia umri wa miaka kumi na saba.

***

Kwa kuwa Small’s ilikuwa ndiyo kama katikati ya kila kitu, kuwa mhudumu pale ilikuwa mbingu ya saba mara saba. Charlie Small hakuwa na haja ya kunitahadharisha juu ya kuchelewa; nilikuwa na shauku kubwa ya kufika pale. Nilifika saa moja kabla ya zamu yangu kuanza. Mhudumu wa asubuhi alionelea kuwa zamu yangu mchana ilikuwa imelala sana, haina pilikapilika wala bakshishi. Mara kadhaa alibaki nami katika saa hilo na kunifundisha hiki na kile, maana hakutaka kuona nafukuzwa kazi.

Kwa msaada wake nilijifunza vitu vingi kwa haraka-vitu ambavyo vingemgombanisha mhudumu mpya na wapishi na mtu wa kaunta. Watu hawa wote-kulingana na jinsi walivyompenda mhudumu husika, waliweza kufanya maisha yake yawe machungu au matamu-nami niliazimia kupendwa. Ndani ya juma moja nikawa nimeelewana vyema na wote. Wateja ambao walikuwa wamezoea kuniona miongoni mwao ndani ya baa ile; na sasa wakiniona nimevaa sare ya wahudumu, walifurahia na kushangazwa; walinitendea kirafiki sana. Nami nilikuwa mkarimu mwenye kushawishi hasa”Kinywaji kingine? . . . Sasa hivi bwana . . . utapenda chakula? . . . kiko vizuri . . . unahitaji chakula gani bwana? . . . vipi kuhusu sandwich?

Si tu wahudumu wa kaunta na wapishi, watu ambao niliona kuwa wanajua kila kitu juu ya kila kitu; lakini na wateja pia walianza kunifundisha kupitia mazungumzo wakati ambao hakukuwa na pilika nyingi. Wakati mwingine mteja aliniongelesha alipokuwa anakula. Na wakati mwingine nilisikia mambo kwa kirefu kutoka kwa wakongwe ambao wameishi Harlem tokea mwanzo wa watu weusi kuhamia hapa.

Hilo jambo lilinishangaza sana; kwamba hapo mwanzo Harlem haikuwa sehemu ya watu weusi.

Nilijifunza kuwa mwanzo lilikuwa ni eneo la Wadachi. Kisha ukaanza uhamiaji wa watu masikini wenye njaa kutoka Ulaya, wakiwa wamebeba mali zote walizomiliki kwenye mifuko waliyobeba migongoni. Kwanza walianza kuja Wajerumani; Wadachi wakawakimbia na Harlem ikawa ya Wajerumani.

Kisha wakaja Wa-Irish, wakikimbia njaa ya viazi. Wajerumani wakakimbia, wakiwanyanyapaa Wa-Irish, hao wakaichukua Harlem. Kutoka hapa wakaja Waitaliano, kitu kilekile kikatokea, Wa-Irish wakawakimbia. Kisha wakaja Wayahudi na Waitaliano wakawakimbia.

Leo hii, wajukuu hawa wote wa wahamiaji wanakimbia kwa nguvu zao zote, kuwakimbia wajukuu wa watu weusi waliosaidia kupakua meli zilizobeba babu zao.

Nilishangaa mkongwe mmoja aliponiambia kuwa, wakati mchezo huu wa wahamiaji kupokezana ukiendelea, mtu mweusi amekuwepo kwenye jiji la New York tokea mwaka 1683, kabla ya yeyote kati ya wahamiaji hao hajaja, na aliwekwa kwenye maeneo ya maghetto sehemu mbalimbali za jiji. Mara ya kwanza walikuwa kwenye eneo la Wall Street; kisha wakahamishiwa Greenwich Village. Baada ya hapo wakapelekwa eneo la Stesheni ya Pennsylvania. Na kituo cha mwisho kabla ya kuja Harlem kilikuwa ni mtaa wa 52, na ndiyo sababu ya mtaa wa 52 kujulikana kama mtaa wa kujirusha, sifa ambayo imedumu muda mrefu hata baada ya watu weusi kuondoka.

Kisha mnamo mwaka 1910, mfanyabiashara mmoja wa majengo mweusi kwa namna fulani aliweza kuweka familia mbili au tatu za weusi kwenye jengo la wayahudi. Wayahudi walikimbia nyumba hiyo, kisha wakakimbia mtaa, na watu weusi wengi zaidi wakazidi kuhamia kwenye nyumba walizohama. Baadaye wayahudi wakahama kutoka mitaa kadhaa na watu weusi wengi zaidi wakazidi kuja, ndani ya muda mfupi Harlem ikawa kama ilivyo leo—eneo la watu weusi.

Kwenye mwanzoni mwa miaka ya 1920, kazi ya muziki ikaibuka huko Harlem, hasa ikichagizwa na wazungu ambao walifika kila usiku. Ilianza wakati ambao kijana mpiga tarumbeta kutoka New Orleans aliyeitwa Louis “Satchmo” Armstrong aliposhuka kwenye treni New York na kuanza kupiga muziki na Fletcher Hebderson. Small’s paradise ilifunguliwa mwaka 1925 ikiwa na wateja kutoka kotekote kwenye barabara ya saba. Mwaka 1926 ilifunguliwa Cotton Club, mahali ambapo bendi ya Duke Ellington ilipiga muziki kwa miaka mitano; pia mwaka huohuo wa 1926 ukumbi wa dansi wa Savoy ulifunguliwa, ukimbi mkubwa wenye na eneo la kuchezea la urefu wa futi mia mbili na majukwaa mawili.

Harlem ikawa maarufu na kuanza kujaa watu weupe kutoka kila kona ya dunia. Mabasi ya watalii yakaanza kwenda. Cotton Club ilihudumia watu weupe tu. Kulikuwa na mamia ya club zingine na baa za vichochoroni zilizohudumia wazungu. Baadhi ya zilizokuwa maarufu ni pamoja na Connie’s Inn, The Lenox Club, Barron’s, The Nest Club, Jimmy’s Chicken Shack na Minton’s. Kumbi za Savoy, The Golden Gate na The Renaissance ziligombania wacheza dansi—Savoy walianzisha vitu kama Alhamisi ya jikoni. Mashindano ya urembo na walitoa gari jipya kila usiku wa jumamosi. Walialika bendi kutoka kila kona ya nchi. Kulikuwa na viongozi wa bendi waliojipamba sana, kulikuwa na mtu kama Fess Williams ambaye alikuwa na suti na kofia zilizopambwa kwa almasi, Cab Collaway na zoot yake nyeupe iliyokuwa baba wa zoot zote , pamoja na kofia yake nyeupe, akiiwasha Harlem kwa vibao vyake kama “Tiger Rag” na “St James Infirmary” na “Minnie the Moocher.”

Basi mji wa watu weusi ulijaa wazungu, makuwadi, makahaba, wauza pombe, wachakarikaji wa kila namna, na polisi na maafisa waliokuwa wakikamata pombe za magendo. Watu weusi walicheza dansi kama vile hawajawahi kucheza maishani mwao. Nafikiri nimewahi kuwasikia wakongwe kama ishirini na tano hivi pale Small’s wakidai kuwa walikuwa ndiyo wa kwanza kucheza Lindy Hop ndani ya Savoy, mahali ambapo mtindo huo ulizaliwa mnamo mwaka 1927, ukiitwa jina la Lindbergh ambaye alikuwa ndiyo ametoka tu kurusha ndege kwa mara ya kwanza kutoka New York hadi Paris bila kutua.

Hata kumbi ndogo zilizokuwa na nafasi ya kutosha kinanda tu nazo zilikuwa na wapigaji mahiri kama James P. Johnson na Jell Roll Morton, na waimbaji kama Ethel Waters. Na ilipofika saa kumi za usiku, muda ambao club zote halali zilitakiwa kufungwa, wanamuziki weusi kwa weupe kutoka mjini kote walifika Harlem kwenye eneo walilopanga kukesha na kupiga nyimbo thelathini au arobaini hivi hadi asubuhi.

Hadi kufikia mdodoro wa uchumi wa mwaka 1929, na mambo yote kuisha- Harlem ilikuwa imeishajizolea sifa kama kama ngome ya Marekani, Small’s iliishi yote hayo. Basi niliwasikia wakongwe wakikumbuka nyakati hizo nzuri na kujawa na hisia.

Kila siku niliwasikiliza wateja waliotaka kuongea kwa umakini sana, na hilo liliongeza elimu yangu. Masikio yangu yalinyonya kama sifongo pale mmoja wao-labda kutokana na kunywa sana, aliponiambia siri ya kazi anazofanya kuendesha maisha. Basi nikawa nimepata elimu kubwa kutoka kwa manguli wa mambo kama kamari, ukuwadi, utapeli wa kila aina, kuuza madawa ya kulevya, wizi na unyang’anyi wa kutumia silaha.

Mwisho wa sura ya tano.​
 
SURA YA SITA

DETROIT RED

Kila siku nilichezea kamari bakshishi zangu zote—kama dola kumi na tano hadi ishirini.

Niliona watu wakitumia pesa kwa kutapanya mara baada ya kushinda bahati nasibu. Simaanishi wachakarikaji tu ambao karibu mara zote walikuwa na pesa za matumizi, namaanisha wafanyakazi wa kawaida. Watu ambao kwa kawaida huwa hawaji kwenye baa ya Small’s. Watu ambao baada ya kushinda donge nono waliacha kazi zao walizokuwa wanafanya kwa mzungu huko mjini-kati. Mara nyingi walinunua Cadillac, na mara nyingine-kwa siku tatu au nne walinunulia rafiki zao vinywaji na nyama choma. Nilikuwa nalazimika kuvuta meza mbili pamoja ili watoshe. Nao walikuwa wakinipa dola moja au mbili kila nilipowahudumia.

Mamia elfu ya watu weusi wa New York, kila siku isipokuwa jumapili—walicheza bahati nasibu kuanzia senti moja hadi mamia ya dola. Kushinda ilikuwa unahitajika kukisia namba tatu za mwisho za jumla ya mauzo ya hisa ya siku katika Marekani. Jumla hiyo ilichapishwa kila siku.

Kwa uwiano wa moja kwa mia sita, mtu aliyeweka senti moja angeshinda dola 6, dola moja kwa dola 600 na kuendelea. Kwa dola 15, mshindi alipata dola 9,000. Ushindi kama huo ilisababisha mshindi anunue hisa kwenye baa na migahawa ya Harlem au hata kuzinunua kabisa. Uwezekano wa kushinda ulikuwa ni moja kwa elfu moja. Wachezaji wengi walifanya kitu kinachoitwa”Kuunganisha” Kwa mfano akiwa na senti sita, ataweka senti moja kwenye mipangilio yote sita ya namba tatu. Kama amechagua namba 840, basi atacheza kila senti kwenye namba 840, 804, 048, 084, 408 na 480.

Karibu kila mtu kwenye maeneo yaliyojaa umasikini ya Harlem alicheza namba. Kila siku kulikuwa na uwezekano wa mtu unayemfahamu kushinda na hiyo ilikuwa habari ya mtaa mzima. Kawaida watu walishinda pesa ndogo tu, senti tano, kumi au senti ishirini na tano. Watu wengi walikuwa wakijitahidi walau kucheza dola moja kwa siku, lakini hiyo dola waliigawanya kwa kuweka kwenye namba mbalimbali.

Kamari ya Harlem ilichanganya kuanzia asubuhi hadi mida ya mchana. Wachezesha kamari wakikimbia huku na huko kuandikisha namba za za bahati kwenye kwenye karatasi, walienda kwenye majumba, baa, saluni, madukani na hata njiani.

Polisi waliangalia tu; hakuna muandikisha wacheza bahati nasibu ambaye alidumu kwenye kazi yake kama hakumnyamazisha kwa chochote polisi aliyeshika doria kwenye eneo lake, na ilijulikana wazi kuwa wakubwa wa kuchezesha namba walitoa rushwa kwa uongozi wa juu wa idara ya polisi.

Waliokuwa wakiandikisha wacheza bahati nasibu walijipatia asilimia kumi ya kiasi walichoandikisha. Kilichobaki alimpelekea msimamizi pamoja na risiti za aliowaandikisha (Na ikitokea ukashinda, ulimpatia muandikishaji wako asilimia kumi kama bakshishi). Msimamizi mmoja aliweza kuwa na waandikishaji hata hamsini. Msimamizi alipata asilimia tano ya kiasi alichowakusanyia wakuu wa kamari. Wakuu hao walilipa washindi, walilipa polisi na kujitajirisha kwa kilichobaki. Watu wengine walicheza namba moja mwaka mzima. Wengine walikuwa na orodha ya namba zilizoshinda kila siku ambazo walikuwa wameziandika kwa miaka mingi, na kuangalia iliyojirudia mara nyingi. Wengine walicheza kulingana na machale yalivyowatuma: wakitumia namba za anuani zao, namba za magari yanayopita, namba zozote kwenye barua, telegram na risiti-kifupi namba za kutoka kokote kule.

Vitabu vya ubashiri vilivyogharimu dola moja, viliweza kukwambia ndoto ipi inawakilisha namba ipi. Wahubiri ambao jumapili walihubiri kuhusu Yesu na miujiza, waliweza kukuchezea namba ya bahati kwa ada fulani.

Hivi karibuni namba tatu za mwisho kwenye namba ya utambulisho wa posta ya Harlem ilishinda, karibu bosi mmoja wa kamari afirisike maana watu wengi hucheza namba kama hizo. Kitabu hiki kikisambaa kwa watu weusi wanaoishi maeneo ya maghetto, nakuhakikishia kuwa mamilioni ya dola yatachezwa kamari na kaka na dada zangu weusi walio masikini na wajinga kwa kutumia namba za kurasa za kitabu hiki, jumla ya kurasa kwenye kitabu hiki au namba zozote zilizomo kitabuni humu.

Kila siku yangu kwenye baa ya Small’s Paradise ilikuwa ni ya kufurahisha. Na kwa eneo la Harlem, hakukuwa na sehemu nzuri zaidi ya mimi kuelimika kuliko pale. Baadhi ya watoto wa mjini, manguli wa jiji la New York walianza kupendezwa nami. Na kwa vile kwa mtazamo wao bado nilikuwa mshamba, mara moja wakaanza mpango wa “Kuniweka sawa.”

Mbinu yao haikuwa ya moja kwa moja. Mtu mmoja mweusi sana na mkubwa aliyekuwa na asili ya visiwa vya Karibeani alikaa kwenye meza yangu mara nyingi. Siku moja nilipomletea bia alisema, “Red hebu simama tuli,” alitoa tepu ya kupimia, zile za njano. Alinipima na kuandika kwenye kijidaftari. Nilipofika kazini siku iliyofuata, mhudumu mmoja akanipatia kifurushi. Ndani yake kulikuwa na suti ghali ya rangi ya bluu iliyokolea. Ilikuwa ya kawaida bila manjonjo yoyote. Zawadi ilikuwa ni nzuri sana na ujumbe iliyouleta ulifahamika vyema.

Wahudumu walinifahamisha kuwa mteja yule alikuwa ni mmoja wa viongozi wakubwa wa genge la kihalifu la Forty Thieves, hilo lilikuwa ni kundi la watu ambao waliweza kukupatia ndani ya siku moja nguo za aina yoyote uliyohitaji. Na bei yake ilikuwa theluthi ya bei ya dukani.

Nilisikia jinsi wanavyofanya kazi yao. Mwanakikundi aliyevalia nadhifu, mtu ambaye hatahisiwa vibaya, alienda kwenye duka lililochaguliwa wakati wa kufunga, alijificha humo ndani na kufungiwa wakati wa duka kufungwa. Hapo tayari wanakuwa wanajua doria ya polisi itapita muda gani. Baada ya giza kukolea alijaza suti kwenye mabegi na kuzima king’ora cha kuashiria wezi. Baada ya hapo alipiga simu kwenye gari kulikokuwa wenzake wanaomsubiri. Gari ilifika, ilipakia na kuondoka ndani ya dakika chache tu. Baadaye nilikuja kuwafahamu washiriki kadhaa wa genge la Forty Thieves.

Pia haikuchukua muda nikawa nimejulishwa juu ya wapelelezi waliokuwa wanavaa kiraia, nilijulishwa kwa kukonyezwa au kutingishiwa kichwa. Kuwajua askari wa eneo lile lilikuwa ni jambo muhimu sana kwa wachakarikaji, na kama wao, baada ya muda nami nikawa nimejifunza kutambua uwepo wa wapelelezi wa aina yoyote ile. Mwishoni mwa mwaka wa 1942, kila kitengo cha jeshi kilikuwa na wapelelezi wake waliovaa kiraia, wakichunguza yote yanayoendelea, mfano kazi ambazo watu walitumia ili kukimbia kujiunga na jeshi, nani ambaye hajajiandikisha au utapeli uliokuwa wakifanyiwa wanajeshi.

Makuli wa bandarini au mawakala wao walifika kwenye baa wakiuza bunduki, manukato, kamera, saa na vitu kama hivyo—vitu walivyoiba bandarini. Wezi hawa weusi walikuwa wanapata vitu ambavyo makuli wa kizungu walikuwa wameviacha. Mara nyingi mabaharia wa meli za kibiashara walikuja na bidhaa nzuri za kigeni kwa bei rahisi sana. Mfano Sigara-bangi bora kabisa zilikuwa ni zile zilizotengenezwa kwa Gunja na Kisca. Hizo mabaharia waliziingiza kimagendo kutoka Africa na Uajemi.

Wazungu waliofika mchana walihudumiwa kwa tahadhari sana, lakini wazungu waliofika usiku walikaribishwa vizuri sana. Club za usiku walizozitembelea zilifanya kila ziwezavyo kuhudumia vizuri wazungu ili kupata pesa zao. Na kutokana na uwepo mkubwa wa wapelelezi waliokuwa wakilinda “maadili” ya wanajeshi, kila aliyefika alihudumiwa vyema na kuongeleshwa pale tu alipoanza yeye kuongea, isipokuwa mtu awe anawafahamu kuwa ni wenyeji wa Harlem.

Nilichokuwa najifunza ilikuwa ni sheria namba moja ya wachakarikaji. Kwamba hutakiwi kumuamini yeyote nje ya wasiri wako wa wa karibu, na hao-kabla ya kushirikiana nao unatakiwa kuwachagua polepole na kwa uangalifu.

Wahudumu wa kaunta waliniambia ni yupi kati ya wateja wa mara kwa mara ni kibaraka tu na yupi ni hasa ni bosi, nani hasa walikuwa kwenye ulimwengu wa uhaifu, nani wanajuana na polisi na wanasiasa; yupi alikuwa na pesa na yupi alikuwa anabangaiza. Nani walikuwa wacheza kamari hasa na nani walikuwa wamebahatisha mara moja tu; na yupi hutakiwi kugombana naye hata kidogo.

Hao wa mwisho walijulikana vema katika Harlem, waliogopwa na kuheshimiwa hasa. Ilijulikana wazi kuwa iwapo umewakasirisha, waliweza kukupasua kichwa na wala wasijali. Hawa walikuwa ni wakongwe, achana na vijana waliokuwa wakijitia vichaa, wakijaribu kujenga heshima kwa kutishia visu na bastola. Wakongwe ninaowazungumzia ni kama “Black Sammy,” “Bub” Hewlett, “King” Padmore na “West Indian Archie.” Wengi wa wababe hawa walifanya kazi kama mabaunsa wa Dutch Schultz, zamani hizo alipokuwa anataka kuingia kwenye biashara ya kamari ya Harlem baada ya wahalifu wa kizungu kuzinduka na kugundua kuwa wanaweza kutengeneza pesa nyingi kwa kitu walichofikiri ni biashara ya senti chache inayowafaa manigger.

Wakongwe hao waliwika kabla ya upelelezi mkubwa wa Seabury uliofanyika mwaka 1934, uchunguzi ulioanza kummaliza Dutch Shultz hadi alipoishia kuuwawa mnamo mwaka 1935. Nilisikia simulizi za jinsi walivyokuwa “Wakishawishi” watu kwa kutumia mabomba, marungu ya kuchezea baseball, ngumi, mateke na fimbo.

Karibu kila mmoja wao alikuwa amewahi kufungwa na kutoka. Na toka watoke gerezani wamekuwa wakifanya kazi ya uandikishaji wacheza kamari kwa mabosi wakubwa wa kamari ambao walikuwa na wateja waliocheza pesa nyingi.

Kulikuwa kama na maelewano ya kutoingiliana kati ya wakongwe hawa na polisi weusi; nadhani wote walifahamu kuwa hilo likitokea kuna mtu atakufa. Harlem pia kulikuwa na polisi weusi wabaya. Askari mweusi aliyekuwa mbaya kuliko wote huko Harlem alikuwa ni mwenye asili ya visiwa vya Karibeani aliyeitwa Brisbane. Alipokuwa akifanya doria kwenye eneo lake lililokuwa kwenye mtaa 125 na barabara ya saba, watu walivuka barabara kumkwepa. Nilipokuwa gerezani mtu mmoja alinipa habari kuwa Brisbane aliuawa kwa risasi na kijana mmoja mdogo, kijana huyo alikuwa ametokea majimbo ya kusini karibuni na hakujua Brisbane ni mkubwa kiasi gani.
 
Sura ya sita inaendelea
Kuwadi wa kustaajabisha kabisa alikuwa ni “Cadillac” Drake, alikuwa na kichwa kama yai kilichokuwa na upara unaong’aa. Alikuwa anaikiita kitambi chake “uwanja kuchezea makahaba.” Alikuwa na makahaba wa kizungu na weusi watata sana, waliokondeana kuliko wote katika Harlem.

Nyakati za mchana kwenye baa pale, wakongwe ambao walimfahamu Cadillac vyema, walikuwa wakimtania. Walimwambia inawezekanaje, makahaba wake kwa jinsi walivyo-kutengeneza pesa za kuwatosha wao, achilia mbali yeye. Alikuwa akilipuka kwa kicheko; hata sana naweza kumsikia akisema, “Wanawake wenye muonekano mbaya hufanya kazi kwa bidii zaidi.”

Kulikuwa na kuwadi mwingine ambaye alikuwa tofauti kabisa na Cadillac, kijana mjanja aliyeitwa “Sammy The Pimp(Kuwadi Sammy).” Kama nilivyoeleza, Sammy aliweza kumtambua iwapo mwanamke ni kahaba kwa kumuangalia sura yake wakati wa kucheza dansi. Mimi na Sammy tulikuja kuwa marafiki wa karibu sana. Sammy ambaye alikuwa ni mzaliwa wa Kentucky, alikuwa ni mtu aliyeijua kazi yake vyema, na kazi yake ilikuwa wanawake. Kama Cadillac, naye pia alikuwa na makahaba weusi na wakizungu wakimtengenezea pesa. Lakini wanawake wa Sammy, ambao wakati mwingine walikuja kwenye baa kumletea pesa au kumfuata awanunulie vinywaji walikuwa wazuri kama tu makahaba wa maeneo mengine.

Mmoja wa wanawake wake wa kizungu aliyekuwa na nywele za dhahabu aliitwa “Alabama Peach.” Lafudhi yake ya kusini ilikuwa nzito sana. Alipendwa na watu, hata wanawake weusi waliosimamia kamari ya namba maeneo ya Small’s walimpenda. Kilichowachekesha sana watu weusi pale baa ilikuwa ni jinsi alivyo tamka neno “Nigger,” yeye alitamka “Ah jes’ luuv ni-uh guhs-“ Mpe kinywaji naye ndani ya dakika moja ataanza kukusimulia historia yote ya maisha yake. Atakusimulia jinsi ambavyo kwenye mji mdogo wa Alabama alikotoka; kitu cha kwanza kujifunza mara tu alipojitambua kilikuwa ni kuchukia watu weusi. Kisha baadaye akiwa shuleni akaanza kusikia kutoka kwa wasichana wakubwa kuwa wanaume weusi wana nguvu na wanajua mapenzi, na kisha kwa siri akaanza kutamani kumjaribu mmoja. Mwishowe, ndani ya nyumba yao wakati wazazi wake hawapo, alimtishia mtu mmoja mweusi aliyekuwa mfanyakazi wao kuwa akikataa kufanya naye ngono atamshtaki kuwa alitaka kumbaka. Mfanyakzi yule hakuwa na namna japo baadaye aliacha kazi. Na kuanzia hapo hadi alipomaliza sekondari alitembea na watu weusi kadhaa—na alipofika New York alielekea Harlem moja kwa moja. Baadaye Sammy alikuja kunisimulia jinsi alivyomvumbua kwenye ukumbi wa Savoy. Na wala alikuwa hachezi na mtu, alikuwa amesimama tu pembeni lakini aliweza kumtambua. Na kwa vile alikuwa akipendelea watu weusi hiyo ikawa nzuri zaidi kwa Sammy. Nimekuwa nikijiuliza nini kilikuja kumpata.

Pia kulikuwa na kuwadi mmoja mkubwa na mnene sana. tulikuwa tukimuita “Dollarbill.” Alikuwa akipendelea kukunja pesa na kutengeneza duara kama bomba, mtindo ulioitwa “Kansas City Roll.” Burungutu lake hilo lilikuwa na noti za dola mojamoja hamsini sehemu ya katikati. Kwa ndani aliweka noti ya dola ishirini, na kwa nje noti ya dola mia moja. Siku zote tulikuwa tunajiuliza dollarbill atafanya nini iwapo mtu akimuibia ile dola mia moja ya nje.

Mtu ambaye ingekuwa enzi zake angeweza kumuibia Dollarbill burungutu lake huku amefungwa macho alikuwa ni mzee “Fewclothes” Fewclothes alikuwa ni mmoja wa wezi wa mifukoni bora kabisa katika Harlem, zamani hizo miaka ya 1920 wakati wazungu walipokuwa wakija Harlem nyakati z usiku. Lakini kipindi cha mdororo mkubwa wa uchumi alipata ugonjwa mbaya wa baridi yabisi kwenye vidole vyake. Vifundo vya vidole vyake vilivimba na kuharibika kiasi kwamba viliwatisha watu walipoviangalia. Kila siku mchana wa kama saa sita hivi Fewclothes alifika Small’s, kuwe na mvua au theluji. Alipenda kusimulia visa vya zamani. Ilikuwa ni kawaida ya kila siku kwa mmoja wa wateja aliyezoeleka kumwambia mtu wa kaunta ampatie kinywaji na mimi nimpe chakula.

Tulikuwa na bahati sana sisi ambao nyakati zile tulikaa kwenye baa ya Small’s na kusikiliza simulizi za Fewclothes. Natamani ungemuona, akiwa amechangamka kwa kinywaji, aliketi kwenye kiti kwa heshima, hakuwa akiomba wala hakutegemea msaada wa mtu yeyote. Alisoma orodha ya vyakula vilivyopo niliyompa na kuagiza. Niliwaambia wapishi kuwa kilikuwa chakula cha Fewclothes nao walimpatia chakula bora kabisa kilichokuwepo. Nilirudi na chakula kumhudumia kama vile namhudumia milionea.

Mara nyingi nimefikiria kuhusu maana hasa ya jambo lile. Kwa namna moja tulikuwa tumejikusanya pale pamoja, tukitafuta joto na usalama na kufarijiana, na wala hatukujua hilo. Sote ambao pengine tungekuwa wanaanga au madaktari wa saratani au wenye viwanda, na badala yake tulikuwa wahanga wa mfumo wa jamii wa Marekani uliowekwa na mzungu. Kwa maneno mengine, masahibu ya nguli wa wizi wa mifukoni yaliwakumbusha wale wapambanaji wakongwe kuwa wanaishi kwa rehema za Mungu tu. Kwa mbwa mwitu ambao bado waliweza kukamata sungura, ilimaanisha kuwa mbwa mwitu mzee ambaye amepoteza meno yake bado alikuwa na uhakika wa kula.

Kisha kulikuwa na mwizi wa majumbani aliyeitwa “Jumpysteady”. Kule kwenye maghetto ambayo mzungu alitujengea, alikuwa ametulazimisha kutokuwa na matarajio makubwa bali kutafuta tu mkate wa kila siku—na kwenye aina hiyo ya jamii, kupata mkate wa kila siku ndiko kunakoheshimika. Kwenye baa ya kawaida katika maeneo ya wazungu, usingeweza kukuta mwizi anayejulikana akijitaja waziwazi mara kwa mara na kutokea kuwa mmoja ya watu maarufu kwenye baa hiyo. Lakini iwapo Jumpsteady alikaa siku chache bila ya kufika baa pale Small’s watu tulianza kumuulizia.

Jumpsteady aliitwa hivyo kwa sababu ilisemwa kuwa anapokuwa anafanya kazi yake kwenye makazi ya wazungu huko mjini, aliruka toka paa moja hadi jingine kwa ufanisi mkubwa sana, na alikuwa mtaalamu kiasi kwamba aliweza kutambaa kwenye madirisha, akiwa amejishililia kwa vidole vya miguu. Alipita maeneo ambayo kama angeanguka basi angekufa. Aliingia kwenye majumba kupitia madirishani. Ilisemwa kuwa alifanya kazi yake kimya kimya kiasi aliweza kuiba huku kwenye chumba kinachofuata kuna watu. Baadaye nilikuja kufahamu kuwa alikuwa akitumia kwanza dawa za kulevya kabla ya kuanza kazi. Alinifundisha vitu kadhaa ambavyo nilikuja kuvitumia hapo baadaye baada ya hali ngumu kunilazimisha kuwa na genge langu la wezi.

Nisisitize kuwa Small’s hakikuwa kijiwe cha wahalifu kabisa. Nimewazungumzia sana wachakarikaji sababu ndiyo walionivutia sana. Ukweli ni kuwa kwa burudani za usiku, Small’s palikuwa ni moja kati ya sehemu mbili au tatu za kistaarabu sana katika Harlem. Na hata polisi wa mji wa New York waliwashauri wazungu walioulizia sehemu salama ya kwenda katika Harlem watembelee Small’s.

Chumba cha kwanza kupata baada ya kuachana na kazi ya reli kilikuwa kwenye jengo nambari 800 katika barabara ya St Nicholas. Kwenye jengo hili uliweza kwenda kwenye chumba chochote na kujipatia makoti ya manyoya, kamera nzuri, manukato mazuri, bunduki, yaani kila kitu-kuanzia wanawake wazuri hadi magari ya wizi. Nilikuwa mmoja ya wanaume wachache sana walioishi kwenye jengo hili.

Hiki kilikuwa ni kipindi cha vita ambacho haikuwezekana uwashe redio bila kusikia habari za Guadalcanal au Afrika ya Kaskazini. Kwenye vyumba kadhaa walikaa wanawake wanaojiuza. Wachache waliobakia walikuwa wanafanya shughuli zingine kama kuandikisha wacheza kamari, kuuza dawa za kulevya nk. Nadhani kila aliyeishi kwenye jengo lile alitumia aina fulani ya dawa za kulevya. Hili lisijenge picha mbaya kuhusu jengo lile maana karibu kila mkazi wa Harlem alifanya uhalifu fulani ili kuishi.

Ni katika jengo hili ndimo nilijifunza kuhusu wanawake kuliko mahali popote pale. Ni makahaba hawa ndiyo walinifundisha vitu ambavyo kila mke na mume wanapaswa kuvifahamu. Baadaye, ilikuwa hasa ni wanawake ambao hawakuwa makahaba ndiyo walionifunza kutoamini kabisa wanawake. Ilionekana kuna ustaarabu na kujaliana kwa hali ya juu kati ya makahaba hawa kuliko ilivyo kwa wanawake waendao kanisa, wanawake ambao wana wanaume wengi kwa ajili ya starehe kuliko walionao makahaba wanaojiuza. Na hapa naongelea wanawake wote, weusi na wazungu. Wanawake wengi weusi wa wakati huo wa vita, walikuwa kama tu wale wa kizungu—wakilala na wanaume wengine huku waume zao wakiwa vitani, na hata wakiwahonga wanaume hao pesa za waume zao. Na wanawake wengi walijifanya ni mama na wake wema huku wakifanya mambo ya kikahaba-watoto na waume zao wakiwa hapo hapo New York.

Nilipata somo langu la kwanza juu maadili “maji taka” ya wanaume wa kizungu kutoka kwenye chanzo cha kuaminika kabisa, kutoka kwa wanawake wao wenyewe. Na kadri nilivyozidi kuzama kwenye maisha yangu ya upotofu, ndipo nilipojionea mwenyewe kwa macho yangu maadili ya wanaume wa kizungu. Na hata niliendesha maisha yangu kwa kuwapeleka kwenye mambo mapotofu waliyotaka.

Nilikuwa kijana mdogo aliyefanya kazi kwenye baa hivyo sikujishughulisha na wanawake hawa. Pengine walinichukulia kama mdogo wao wa kiume. Wengine walifika chumbani kwangu wakati ambao hawana shughuli na tukavuta bangi na kuongea. Mara nyingi ilikuwa ni baada ya pilika zao za asubuhi, acha nikueleze kuhusu pilika hizo za asubuhi.

Kuona kuna shughuli nyingi kwenye ngazi nyakati za usiku-wanaume wakizungu na weusi wakija na kwenda hakikuwa kitu cha kushangaza kwa mtu aliyeishi kwenye jengo ambalo makahaba walifanyia kazi zao. Lakini kilichonishangaza ni umati mkubwa ulioingia kati ya saa kumi na mbili na saa moja asubuhi, kisha ukatokomea kufikia saa tatu asubuhi. Kutoka hapo nilibaki mwanaume pekee mjengoni.

Walikuwa ni waume za watu ambao wametoka nyumbani kisha wakapitia kwenye jengo hili kabla ya kwenda kazini. Ni kweli kuwa hawakuwa watu wale wale kila siku, lakini siku zote walikuwa wa kutosha kusababisha kutokea kwa pilikapilika nyingi. Katika watu hao walikuwepo wanaume wa kizungu waliokuja kwa taxi kutoka mbali kabisa, huko katikati ya mji.

Wake wasumbufu na wenye malalamishi mengi, ambao “waliwahasi” wanaume zao kwa tabia zao hizo, walikuwa ndiyo chanzo cha msongamano huu wa asubuhi. Wanawake hawa walikuwa wanakera sana na kuwasababishia waume zao mkazo kiasi kwamba hawakujiona kama ni wanaume kamili tena. Kuepuka mkazo huo na gubu la wake zao, wanaume hawa waliwahi mapema kuja kwa makahaba hawa.

Iliwalazimu makahaba kujifunza hasa kuhusu wanaume. Walisema kuwa baada ya wanaume wengi kupita nguvu zao za kwenye miaka ya ishirini, walilala na wanawake ili tu kulinda heshima zao. Na kwa sababu wanawake wengi hawaelewi hili, huishia kuwaharibia wanaume heshima hiyo. Haijalishi mwanaume amebakiwa na nguvu kiasi gani, makahaba humfanya ajione ni mwanaume bora kabisa duniani. Wake wengi wasingepoteza waume zao iwapo wangefahamu kuwa takwa lako kubwa kabisa ni kujihisi vidume.

Wanawake wale walinisimulia kila kitu. Visa vya kuchekesha kuhusu tofauti ya wanaume weusi na wazungu kitandani. Mambo ya ajabu watu wayapendayo! Nilidhani nimesikia habari zote juu ya watu wapendayo wakati wa ngono hadi pale nilipokuja kuwa kuwadi wa kuwapeleka wanaume wa kizungu kwenye mambo wayatakayo. Kila mtu mjengoni pale alikuwa akimcheka mwanaume mmoja wa kiitaliano mwenye umbo dogo. Walimwita, “Dola kumi kwa dakika.” Alikuwa akija kila siku mchana bila kukosa, alikuwa akimiliki mgahawa karibu na viwanja vya polo; walimtania kuwa hajawahi enda zaidi ya dakika mbili lakini mara zote aliacha dola ishirini.

Makahaba walikuwa wanaona kuwa wanaume wengi walikuwa ni wapole sana. Kila siku makahaba hawa walisikia malalamiko ya wateja wao kwamba wanawake wao wanaowapa kila kitu na kuwajali hawana shukrani. Makahaba wale walisema kuwa wanaume wote wanatakiwa kuwa na maarifa kama ya makuwadi. Mwanamke anatakiwa kubembelezwa hapa na pale ili kuonyesha kuwa mume wake anampenda, lakini zaidi anatakiwa kutendewa kwa uthabiti na msimamo. Wanawake hawa manguli walisema kuwa hilo lilifanya kazi kwao wenyewe. Kwa asili wanawake wote ni dhaifu: wanavutiwa na wanaume ambao wanaona kuwa wana nguvu.
***​
 
Baada ya muda fulani Sophia akaanza kuja kunitembelea kutoka Boston. Muonekano wake ulinipa heshima hata kwa watu weusi wa Harlem. Walikuwa tu kama watu weusi wa sehemu zingine. Na hiyo ndiyo sababu makahaba wa kizungu walitengeneza pesa nyingi sana. Haijalishi ulikuwa Lansing, Boston au New York—kitu ambacho mzungu mbaguzi alisema, na anachoendelea kusema, alikuwa sahihi kabisa katika siku hizo! Ulichotakiwa kufanya ni kumuweka tu msichana wa kizungu karibu na mwanaume mweusi naye ataitikia. Wanawake weusi pia waliwafanya wanaume wa kizungu macho yawatoke lakini walikuwa wajanja na kuficha wasionekane.

Sophia alikuwa anakuja kwa treni ya adhuhuri. Alikuwa akifika Small’s nami nilimtambulisha kwa watu pale, tulikaa naye mpaka wakati wangu wa kutoka. Alikuwa na wasiwasi kwa mimi kuishi na makahaba hadi pale nilipomtambulisha kwa baadhi yao, na baada ya kuongea nao akasema kuwa walikuwa watu wazuri sana. Walimwambia kuwa watanitunza kwa ajili yake. Usiku tulikuwa tukienda kwenye baa ya kwenye hoteli ya Braddock, huko tulikutana na wanamuziki ambao walikuwa wakinisalimia kama rafiki yao wa siku nyingi, “Hey Red, tutambulishane.” Walikuwa wakimshobokea sana Sophia kiasi kwamba sikuweza hata kununua kinywaji. Hakuna watu weusi duniani waliokuwa wanazuzuka na wanawake wa kizungu kama wengi wa wanamuziki wa kipindi kile. Wasanii huwa hawajali sana miiko ya kijamii.

Wabaguzi wa kizungu hawawezi kukuambia kuwa hata wanaume wa kizungu wko hivyo kwa wanawake weusi. Ilipofika usiku mwingi, nilienda na Sophia kwenye maeneo yaliyokuwa yakikesha na baa za vichochoroni. Baada ya club za mjini kufungwa, maeneo haya yalijaa wazungu. Wazungu hawa walikuwa tu na shauku ya kuona mambo ya watu weusi. Hasa kwenye maeneo ambayo ungeweza kuita yalikuwa na roho ya watu weusi. Wakati mwingine ungeweza kusikia watu weusi wakizungumza jinsi ambavyo wazungu wengi wanapenda kuwa karibu nasi na kati yetu muda wote. Ilionekana wazungu wote, wake kwa waume walistaajabishwa sana na watu weusi. Nakukumbuka kisa cha msichana mmoja wa kizungu ambaye alikuwa hakosi kwenye dansi katika ukumbi wa Savoy. Alikuwa amemvutia rafiki yangu Sammy. Alikuwa amemchunguza kwa mara kadhaa. Siku zote alicheza na watu weusi na alionekana kama akili zinampotea anapokuwa akicheza. Iwapo mwanaume mzungu akimuomba kucheza naye alikuwa akikataa. Kisha asubuhi wakati wa kufunga dansi, alisindikizwa na mwanaume mweusi hadi kwenye kituo cha treni. Basi ndiyo iliyokuwa kawaida yake, hakuwahi kumwambia yeyote jina lake, achilia mbali kusema alikoishi.

Sasa nikusimulie kisa kingine ambacho kilikuwa na mwisho tofauti, kisa kilichonifundisha kitu ambacho baadaye nimekuja kujifunza kwa njia nyingine zaidi ya elfu. Kisa hiki ndicho kilikuwa somo langu bora la kwanza juu ya jinsi ambavyo mioyo ya wanaume wakizungu inavyoweza kubadilika kabisa. Vyovyote vile watakavyotaka kukuaminisha-wewe elewa kuwa kila wanapoona ukaribu wa mwanaume mweusi na mwanamke wa kizungu, matumbo huwacheza na roho zao hulipuka.

Kulikuwa na wanaume wachache wakizungu walioshi Harlem, vijana ambao tulikuwa tukiwaita “Hippies,” hawa walikuwa wakiigiza maisha ya watu weusi kuliko watu weusi wenyewe. Mmoja wao alikuwa akiongea kama mtu mweusi kuliko sisi wenyewe. Alikuwa akigombana na kila mtu aliyefikiri kuwa kuna tofauti kati ya watu wa rangi mbalimbali. Haikuwa rahisi kwa wanamuziki wa Braddock kujisogeza bila ya kugongana naye. Kila nilipokutana naye ilikuwa ni maneno ya kisela. Alimker sana Sammy; alikufuata popote ulipokwenda. Na hata alivaa suti kituko ya zoot na alipaka mafuta mengi kwenye nywele zake ili zionekane kama za mtu mweusi zilizotiwa dawa. Pia alivaa viatu vilivyotuna mbele na bila kusahau mnyororo kwenye suruali, yaani kila kitu. Na hata wanawake wake wote walikuwa ni weusi, aliishi na wawili kwenye makazi yake madogo madogo. Sikujua waliwezaje kufanya vile.

Siku moja kama saa tisa au kumi hivi ya usiku tulikutana na kijana huyu kwenye bay a kichochoroni ya Creole Bill. Alikuwa yuko bangi tupu kichwani. Nilimtambulisha kwa Sophia kisha nikawaacha wakiongea nami nikaenda kumsalimia mtu mwingine; niliporudi nilimkuta Sophia kabadilika lakini hakuniambia kinachomsumbua hadi tulipoondoka. Yule kijana alikuwa amemuuliza, “Kwa nini msichana wa kizungu kama wewe unaharibu maisha yako kwa mtu mweusi huyu?”

Creole Bill kutoka New Orleans alikuwa rafiki yangu wa karibu. Baada ya Small’s kufungwa niliwapeleka wazungu waliokuwa bado wanataka kutumia kwenye baa ya kichochoroni ya Creole Bill. Baa ya Bill ilikuwa nyumbani kwake. Nafikiri alikuwa amevunja ukuta ili kuongeza ukubwa wa sebule. Mazingira yake na chakula kilichopikwa pale vilifanya mahali pale pawe moja ya vijiwe safi kabisa katika Harlem. Kulikuwa na kila aina ya vinywaji. Pia Bill aliuza vyakula vyake vitamu vya kicreole, vyakula kama Gumbo na Jambalaya. Mpenzi wa Bill, msichana mmoja mweusi na mzuri ndiye alikuwa anahudumia wateja. Bill alimwita “Brown Sugar,” na baadaye kila mtu alimwita hivyo. Iwapo kulikuwa na wateja wengi wa kuhudumia, basi Bill alileta mapoti na Brown Sugar alileta sahani, Bill alimpakulia kila mtu chakula cha kutosha, kisha naye alijijazia sahani na kula pamoja nasi. Ilifurahisha sana kumuona akila; alipenda mno chakula chake, na kwa kweli kilikuwa kitamu hasa. Bill aliweza kupika wali kama Mchina—namaanisha wali uliochambuka kila punje peke yake, lakini sijawahi kuona Mchina akipika maharage na vyakula vya baharini kama alivyopika Bill.

Bili alitengeneza pesa za kutosha kwenye ile baa yake ya kichochoroni hadi kuweza kufungua mgahawa maarufu sana wa kicreole katika Harlem. Alikuwa ni mpenzi mkubwa wa mchezo wa baseball. Kote ukutani mwake kulikuwa na picha za wachezaji wakubwa, tena zenye saini zao. Pia kulikuwa na picha za wasanii maarufu na wanasiasa ambao waliwahi fika pale kupata chakula-wakileta na rafiki zao. Sijui ni nini kilichokuja kumpata Creole Bill. Eneo lake limeuzwa, na wala sijasikia chochote kumhusu. Nitajaribu kuwauliza wakongwe wa barabara ya saba, watakuwa wanajua.

Siku moja nilimpigia simu Sophia naye akaniambia kuwa hataweza kuja mpaka mwisho wa juma lililofuata. Alikuwa tu ametoka kuolewa na mzungu mmoja mwenye fedha wa Boston. Alikuwa ni mwanajeshi. Alikuwa amekuja nyumbani likizo na sasa alikuwa amerudi kazini. Sophia alisema hilo halitabadilisha chochote kati yetu. Nami nilimwambia haitaathiri chochote. Siku nyingi nilikuwa nimemtambulisha Sophia kwa rafiki yangu Sammy, na hata mara kadhaa tulitoka pamoja usiku. Nilijadiliana na Sammy juu ya saikolojia ya mwanamume mweusi na mwanamke wa kizungu. Sammy ndiye alinisaidia kujiandaa na suala la Sophia kuolewa.

Sammy aliniambia kuwa wanawake wa kizungu hawana mchezo; amewasikia wengi wao wakijieleza jinsi wanavyohisi. Walifahamu kuwa mwanaume mweusi alikuwa na hali mbaya kwenye kila nyanja, kwamba mwanaume wa kizungu anamkandamiza mwanaume mweusi, akimuweka chini ya viatu vyake, akimfanya ashindwe kwenda popote pa maana. Lakini pia mwanamke wa kizungu alihitaji maisha mazuri, alihitaji kutazamwa vyema na watu wake, lakini pia alihitaji kutimiza starehe zake. Kwa hiyo, baadhi yao huolewa na wanaume wa kizungu kwa ajili tu ya maisha mazuri na usalama huku wakiendelea kutoka na mtu mweusi. Na si kwamba lazima walikuwa wanawapenda wanaume hao weusi, bali hasa ni sababu ya tamaa ya ngono tu, hasa ngono ambazo ni mwiko.

Mwanaume wa kizungu aliyetengeneza dola elfu kumi, ishirini, thelathini au hamsini kwa mwaka alionekana wa kawaida tu. Lakini mwanaume mweusi aliyetengeneza dola elfu tano kwa mwaka katika ulimwengu wa kizungu alionekana siyo wa kawaida. Mwanamke wa kizungu aliweza kuwa na mwanaume mweusi kwa sababu moja kati ya hizi: labda mapenzi yamemkolea sana au ili kutimiza tama zake za ngono.

Nilipoishi Harlem kwa muda mrefu hadi kuwa kama mwenyeji, nikawa nimepata jina, jina lililonitofautisha na “Red” wengine wawili maarufu, ambao nao walitia nywele dawa. Nilifahamiana nao wote, na hata baadaye nilikuja kufanya nao kazi. Mmoja aliyeitwa “St. Louis Red,” alikuwa ni mnyang’anyi wa kutumia silaha. Nilipoenda gerezani nilimkuta akitumikia kwa kujaribu kumpora msimamizi wa mgahawa wa kwenye treni iliyofanya safari kati ya New York na Philadelphia. Baadaye aliachiwa huru. Nasikia sasa anatumikia kifungo kwa kupora duka la vito jijini New York.

Mwingine alikuwa ni “Chicago Red,” Tulikuja kuwa marafiki wa karibu kwenye baa moja ya kichochoroni ambayo baadaye nilikuja kufanya kazi; Chicago Red alikuwa muosha vyombo mcheshi kuliko wote duniani. Sasa anaendesha maisha yake kwa kuchekesha kwenye majukwaa na vilabu vya usiku, amekuwa mchekeshaji maarufu nchini. Sioni sababu kwa nini Chicago Red achukizwe kwa mimi kutaja jina lake!-ni Redd Foxx.

Basi haikuchukua muda nikawa nimepata jina. Sijui ni lini, lakini watu kwa kujua kuwa natokea Michigan walikuwa wakiniuliza jiji ninalotokea. Sababu watu wa New York wengi hawajawahi usikia mji wa Lansing, niliwaambia natoka Detroit. Polepole nikaanza kuitwa “Detroit Red” na jina likaniganda.

***​
 
Sura ya sita inaendelea

Siku moja mchana, mwanzoni mwa mwaka 1943, kabla tu ya umati wa saa sita mchana haujajaa, nilimkuta mwanajeshi mmoja mweusi amekaa moja ya meza ninazohudumia akinywa. Atakuwa alikuwa amekaa pale kwa kama saa moja hivi. Alionekana kama mzembe na aliyetia huruma, ni kama alitoka huko kusini vijijini. Baada ya kumhudumia kinywaji cha nne au cha tano, niliinama nilipokuwa nafuta meza na kumnong’oneza iwapo anahitaji mwanamke.

Nilifahamu vyema sheria za pale. Na haikuwa tu sheria ya Small’s, ilikuwa ni sheria ya kila baa iliyotaka kuendelea na biashara kutojihusisha na jambo lolote linaloweza kutafsiriwa kama “kuharibu”maadili ya askari, au kufanya nao biashara ya aina yoyote ile. Mambo haya yalikuwa yamezisababishia matatizo baa kadhaa: zingine jeshi liliwazuia askari wake kwenda, na zingine zilipoteza leseni zao.

Nilijiingiza mzimamzima kwenye mikono ya mpelelezi wa jeshi. Aliigiza kutaka mwanamke na alishukuru sana. Na hata aliongea kwa lafudhi nzito ya watu wa kusini ili kuzidi kuniaminisha ushamba wake. Alipokubali, nilimpatia namba ya mmoja wa rafiki zangu wa karibu kwenye nyumba ya makahaba niliyoishi.

Lakini nilihisi kuna kitu hakiko sawa. Nilijua ndani ya nusu saa mwanajeshi yule atakuwa ameishafika hivyo nilipiga simu kwa yule rafiki yangu kahaba. Nilijibiwa nilichotarajia—hakuna mwanajeshi aliyekuwa amefika kule.

Hata sikujihangaisha kurudi ndani ya baa. Nilienda moja kwa moja kwenye ofisi ya Charlie Small.

“Charlie, kuna kitu nimefanya,” nilisema. “Sijui ni nini kimenipitia,” kisha nikamwambia kilichotokea. “Natamani usingefanya hivyo Red.” Sote tulifahamu alichomaanisha.

Joe Baker, mpelelezi aliyevalia kiraia alipofika nilikuwa namsubiri, sikumuuliza swali lolote. Tulipofika kituo cha polisi kilichokuwa mtaa wa 135, tulikuta kimejaa polisi na wanajeshi. Nilifahamiana na baadhi ya wapelelezi kama ambavyo nilifahamiana na Baker, walikuwa wakifika mara kwa mara pale Small’s.

Vitu viwili vilinisaidia. Kwanza sijawahi kukorofishana na polisi kwa namna yoyote ile. Pili nilikataa bakshishi aliyotaka kunipa yule mwanajeshi mpelelezi, nilimwambia nilikuwa tu namsaidia. Watakuwa walikubaliana kuwa Joe Baker anipe tu onyo.

Nilikuwa sielewi mambo vizuri kiasi kwamba sikujua kuwa sikuandikishwa. Joe baker alinichukua mpaka kwenye chumba kidogo kilichokuwa ndani ya kituo kile. Kwenye chumba kinachofuata tulisikia mtu akichapwa. Whop! Whop! Alisikika akilia, “Tafadhali usinipige usoni, ndiyo nautumia kujipatia riziki!” kusikia hivyo nilijua anayelia atakuwa ni kuwadi. Whop! Whop! “Tafadhali! Tafadhali!”

“Si muda mrefu kutoka siku hiyo nikasikia kuwa Joe Baker alinaswa huko New Jersey akijaribu kuchukua rushwa kutoka kwa kuwadi mweusi na kahaba wake wa kizungu. Alifukuzwa kutoka jeshi la polisi la New York, jimbo la New Jersey lilimshtaki na alifungwa kwa muda fulani)

Kilichoniumiza zaidi kuliko kufukuzwa kazi ni kupigwa marufuku kufika baa ya Small’s. Lakini nilielewa. Japokuwa sikuwa mtu unayeweza kusema “mhalifu,” lakini sasa ningekuwa chini ya upelelezi na wamiliki wa Small’s walihitajika kulinda biashara yao dhidi ya mambo kama hayo.

Sammy alithibitika kuwa rafiki yangu wa kweli. Alinipigia simu niende kwake. Nilikuwa hata sijawahi kufika nyumbani kwake. Kwangu makazi yake yalionekana kama ikulu ndogo; hakika wanawake wake walimtunza. Tulipokuwa tunaongea ni shughuli gani nitafanya, Sammy alinipatia bangi bora kabisa niliyowahi kutumia.

Baadhi ya wasimamizi wa waandikisha wacheza kamari, wale waliozoea kufika Small’s , waliniambia wana kazi iwapo ninataka. Lakini hilo lilimaanisha kuwa nitakuwa napata pesa kidogo sana mpaka hapo nitakapopata wateja wa kutosha. Haikuwezekana kuwa kuwadi kama Sammy. Nilijiona kuwa sina uwezo wa kufanya kazi hiyo, na kuwa nitakufa njaa wakati nikijaribu kutafuta makahaba wa kufanya nao kazi.

Baadaye tukakubaliana na Sammy kuwa kuuza bangi ndiyo kazi itakayo nifaa zaidi. Ilikuwa ni kazi ambayo mtu angeweza kufanya peke yake, na ingeniwezesha kuanza kuingiza pesa haraka. Pia ni kazi ambayo haikuitaji uzoefu wala akili kubwa, hasa ikiwa mtu anaweza kuongea vizuri na watu.

Sote mimi na Sammy tuliwafahamu mabaharia na watu wanaoweza kutujumlishia bangi, na wanamuziki—ambao wengi nilifahamiana nao, walikuwa ni wavutaji wakubwa wa bangi. Na pia walitumia sana dawa za kulevya iwapo hapo baadaye ningetaka kuyauza. Kuuza dawa za kulevya kulikuwa hatari zaidi lakini pia kuliingiza pesa nyingi zaidi. Kuuza heroin na cocaine kuliweza kuingiza dola mia moja kwa siku. Lakini kulihitaji mtu kuwa na uzoefu wa kushughulika na kikosi cha kuzuia dawa za kulevya ili kudumu kwenye biashara hiyo na kutengeneza pesa ya maana.

Nilikuwa nimekuwa mwenyeji wa kutosha kuweza kuwatambua polisi na wapelelezi mara moja, lakini watu wa dawa za kulevya nilikuwa bado sijawajua. Pia nilikuwa na ukaribu na baadhi ya wakongwe wa uchakarikaji waliohudhuria mara kwa mara baa ya Small’s. Hili lilikuwa ni muhimu sana, kama ambavyo Sammy aliweza kunisaidia kupata bangi ya kuuza, moja ya nguzo kuu ya mafanikio ya mchakarikaji ni kujua wapi pa kupata msaada akipatwa na tatizo. Msaada ungeweza husisha polisi, wapelelezi au wakuu wao. Lakini nilikuwa bado sijafikia hatua hiyo. Sammy aliniazima mtaji, nafikiri ilikuwa dola ishirini.

Baadaye usiku wa siku ileile nilimrudishia pesa yake na kumuuliza kama alitaka kukopa. Nilipotoka kwa Sammy nilikwenda moja kwa moja kwa muuzaji wa jumla aliyenielekeza. Nilijumua kiasi kidogo tu cha bangi na kiasi kidogo cha karatasi za kusokotea. Kwa sababu misokoto ilikuwa ukubwa wa njiti ya kiberiti, niliweza kutengeneza ya kutosha, baada ya kuuza kwa wanamuziki niliowafahamu kule hoteli ya Braddock, niliweza kumlipa Sammy na kubakiwa na faida ya kutosha kuweza kuendelea na biashara. Wanamuziki wale walipoona rafiki na shabiki wao anafanya biashara walisema: “My man!” “Crazy Red!”

Karibu nusu ya wanamuziki wa kila bendi walivuta bangi. Sitataja majina yao, lakini walikuwemo wanamuziki wakubwa sana, na wengine wakubwa hata sasa. Kuna bendi ambayo ni maarufu hadi leo ambayo kila mwanamuziki wake alivuta bangi. Mwanamuziki yeyote anaweza kukuambia ninamaanisha nini ninaposema mmoja ya wanamuziki maarufu zaidi alikuwa akivuta bangi yake kupitia mfupa wa paja la kuku. Alikuwa kavuta sana kwa kutumia mfupa huo kiasi kwamba aliweza tu kuwasha tu njiti ya kiberiti mbele ya mfupa huo, kisha akavuta na kupata “stimu.”

Niliendelea kuingiza faida na kuongeza mzigo, niliuza bangi kama mwendawazimu. Nililala muda mchache sana. Nilienda popote walipokusanyika wanamuziki. Mfukoni nilikuwa nakuwa na burungutu la pesa. Kila siku niliingiza dola hamsini hadi sitini. Kwa wakati huo(Na hata sasa) zilikuwa ni pesa nyingi sana kwa kijana mweusi wa miaka kumi na saba. Kwa mara ya kwanza maishani nilipata zile hisia nzuri za kuwa huru. Ghafla nikawa mmoja wa wale wachakarikaji vijana niliokuwa nawahusudu sana.

Ni wakati huu ndipo nilianza kuwa mpenzi wa filamu. Nyakati nyingine niliangalia hata tano kwa siku. Nilikuwa nikiangalizia Harlem au mjini-kati. Nilipenda filamu za wababe, mapigano, Humphrey Bogart kwenye “Casablanca”, pia nilipenda uchezaji dansi wa kwenye filamu kama “Stormy Weather” na “Cabin in the Sky.” Baada ya kutoka kwenye filamu nilikwenda kwa wajumlishaji wangu kujumua na kunyonga misokoto. Giza lilipoingia nilianza mizunguko. Nilikuwa nikitoa msokoto wa ziada iwapo mtu alinunua misokoto kumi, na bei ya msokoto mmoja ilikuwa ni senti hamsini, sikuwa nikiuza tu na kuondoka. Wateja wangu wengi walikuwa ni rafiki zangu, mara nyingi nilivuta pamoja nao. Hakuna aliyekuwa “Yuko bangi” kuliko mimi.

Kwa kuwa sasa nilikuwa huru kufanya nitakavyo, niliweza kwenda Boston wakati wowote niliopenda. Nilikuwa nikifika kwa Ella na kumpatia pesa kidogo, nilimwambia kama shukrani kwa kunisaidia nilipotoka Lansing. Hakuwa Ella yule niliyomzoea—alikuwa bado hajanisamehe kuhusiana na Laura lakini hatukuwahi kuongea kuhusu hilo. Hata hivyo Ella alikuwa ananichukulia vizuri kuliko pale nilipoondoka kwenda New York. Wilfred alifanya vizuri sana kwenye mafunzo yake huko Wilberforce kiasi kwamba aliombwa abaki kama mkufunzi. Na pia Ella alikuwa amepata kadi kutoka kwa Regnald ikimjulisha kuwa alikuwa amefanikiwa kuwa baharia.

Nilimpigia simu Sophia kutoka nyumbani kwa Shorty. Alifika wakati ambao Shorty ndiyo alikuwa akienda kazini. Nilitamani tutoke kwenda kwenye club za Roxbury lakini Shorty aliniambia kuwa kama ilivyokuwa kwa New York, polisi wa Boston nao walikuwa wakitumia kisingizio cha vita kusumbua wapenzi wa rangi tofauti, wakiwasimamisha na kumsumbua mwanaume mweusi juu ya habari za kujiunga na jeshi. Na pia kwa sababu sasa Sophia alikuwa ameolewa, tulikuwa makini zaidi.

Sophia alipochukua taxi kurudi nyumbani, nilitoka kwenda kuona bendi ya Shorty. Sasa alikuwa na bendi yake! Alikuwa amefanikiwa kupata daraja la 4-F na nilifurahia sana mafanikio yake na kwenda kumsikiliza. Bendi yake ilipiga mziki mzuri kiasi chake. Shorty alitengeneza pesa nzuri kwa kupiga muziki kwenye club ndogondogo. Tuliporudi nyumbani tulizungumza hadi asubuhi. “Mwanakwetu mambo yamekunyokea!” Alisema Shorty mara kwa mara. Nilimsimulia juu ya mambo ya ajabu niliyofanya kule Harlem na marafiki niliokuwa nao. Nilimsimulia pia hadithi ya Kuwadi Sammy.

Sammy alikuwa amempa mimba msichana mmoja huko kwao Paducah, Kentucky. Wazazi wa msichana huyo walikasirika sana hadi ikambidi Sammy kukimbilia Harlem, alipofika alipata kazi kama mhudumu mgahawani. Alikuwa akiangalia mwanamke aliyekuja kula akiwa peke yake, baada ya kugundua kuwa hajaolewa wala haishi na mtu, alifanya mbinu kumzoea. Haikuwa vigumu kwa mtu mjanja kama Sammy kukaribishwa nyumbani kwa mwanamke. Alipofika aliomba kwenda nje mara moja kununua chakula. Alipotoka alienda haraka kuchongesha funguo ya pili. Siku alipofahamu kuwa mwanamke yule amesafiri, alienda na kukomba vitu vyake vya thamani vyote. Kisha baada ya hayo alijitolea kumsaidia mwanamke huyo pesa kidogo za kuanzia upya. Huo ulikuwa mwanzo wa utegemezi wa kifedha na kihisia ambao Sammy alijua kuuendeleza hadi mwanamke yule alipokuwa kama mtumwa wake.
 
Sura ya sita inaendelea

Haikuchukua muda kwa wapelelezi wa kikosi cha kuzuia madawa ya kulevya cha Harlem kugundua kwamba nilikuwa nikiuza bangi, hapa na pale mmoja wao alikuwa akinifuatilia. Wauzaji wengi walikuwa jela kwa sababu walikutwa na ushahidi; nilibuni mbinu ya kuepuka hilo. Sheria ilisema kama kitu hakijakutwa mwilini mwako hauwezi kukamatwa. Kuweka mali kwenye soli za viatu zilizotobolewa na pindo za kofia yalikuwa ni mambo ya kale kwa wapelelezi.

Nilikuwa nikibeba kama misokoto hamsini kwenye kikasha kidogo ndani ya koti, chini ya kwapa. Nilitembea nikiwa nimebana mkono kwapani. Kama kuna mtu nilimtilia mashaka, nilivuka barabara haraka, au kuingia sehemu, au kukatisha kona kisha nikachia mkono na kudondosha kile kikasha. Wakati wa usiku, muda ambao nilifanya biashara haikuwa rahisi kwa mtu kugundua hilo. Kama nikiona kuwa ilikuwa ni wasiwasi wangu tu, nilirudi na kuchukua mzigo wangu.

Nilipoteza misokoto mingi sana kwa njia hii. Niliwahangaisha sana wapelelezi na kuepuka kushtakiwa.

Siku moja asubuhi niliingia chumbani kwangu na kugundua kuwa kilikuwa kimepekuliwa. Nilifahamu kuwa watakuwa ni wa wapelelezi tu. Nilisikia jinsi ambavyo huwawekea watu vitu baada ya kushindwa kuwakamata kwa muda mrefu. Usipokikuta na kukitoa, watakuja na kukikuta. Sikufikiri mara mbili juu ya ninachopaswa kufanya. Nilichukua vitu vyangu vichache na sikurudi tena. Nilihamia chumba kingine.

Ni wakati huo ndipo nilianza kutembea na bastola ndogo. Niliipata kutoka kwa teja mmoja kwa malipo ya bangi. Nilifahamu kuwa kaiiba sehemu. Niliichomeka, nyuma, katikati ya mkanda. Kuna mtu alikuwa ameniambia kuwa polisi huwa hawakagui sehemu hiyo wakiwa wanafanya ukaguzi. Na nilikuwa sijichanganyi kwenye mikusanyiko ya watu hadi niwe nawafahamu watu nilionao. Watu wa kikosi cha kuzuia madawa ya kulevya walijulikana kwa kuvamia mikusanyiko na kupandikizia watu vitu wakati wa kuwakagua. Niliona kuwa kadri ambavyo sitatulia sehemu moja na kuwa maeneo ya wazi, nitakuwa salama. Lakini sikumbuki nilikuwa nawaza nini kutembea na bastola. Nafikiri nilikuwa nimepanga kujitetea iwapo mtu akitaka kunibambika kesi.

Mauzo yangu yalianza kupungua sababu kuchukua tahadhari kulichukua muda mwingi wa kazi. Kila mara machale yaliponicheza nilihama chumba. Sikumwambia mtu yeyote nilipolala isipokuwa Sammy tu.

Mwishowe nikapata taarifa kuwa kikosi cha kuzuia dawa za kulevya cha Harlem kilikuwa kimeniweka kwenye orodha maalumu.

Kuanzia wakati huo, walinisearch mtaani kila baada ya siku moja au mbili hivi. Lakini niliwaambia mara moja kuwa sina kitu, na kuwa sitaki wanipandikizie chochote-kwa sauti kubwa ili kila mtu asikie. Hapo walinywea maana watu wa Harlem hawakuogopa dola hivyo walipaswa kuwa makini kuepuka baadhi ya watu weusi kuingilia na kuzua vurugu. Watu weusi wa Harlem walianza walianza kuwa watata sana. Mtu aliweza kunusa na kuona kuwa machafuko hayako mbali-na kweli hayakuwa mbali.

Lakini nyakati hizo maisha yangu yalikuwa magumu sana. Ilinibidi kuficha misokoto yangu maeneo mbalimbali ya karibu na nilipouza. Niliweza kuweka misokoto mitano ndani ya boxi tupu la sigara na kulidondosha chini ya nguzo au nyuma ya pipa la taka. Kwanza niliwaambia wateja wanilipe kisha niliwaelekeza kwa kupata mzigo.

Lakini wateja wangu wa siku zote hawakuweza hilo. Huwezi tarajia mwanamuziki maarufu kwenda kuchukua kitu nyuma ya pipa la taka. Nikawa nabadili mbinu hii na ile, hilo lilisaidia kiasi.

Lakini watu wa kikosi cha dawa za kulevya cha Harlem ya kati kilikuwa na njia nyingi za kunihangaisha hadi nikalazimika kubadili eneo langu la biashara. Nilihamia Harlem ya chini, maeneo ya mtaa wa 110. Huko kulikuwa na wavuta bangi wengi zaidi lakini hawakuwa na pesa, haya yalikuwa ni maeneo duni ya maghettoni, maeneo ya watu masikini ambao hukaa ndani wakijidunga madawa ya kulevya ili kuepuka uhalisia wa maisha yao. Huko nako sikudumu sana. nilipoteza bidhaa nyingi sana. Baada ya kuwauzia wavutaji kadhaa, wavutaji waliokuwa wananusa kama wanyama wakaanza kunifuatilia na kujua mbinu zangu, walitokea ghafla mlangoni. Nilipodondosha bidhaa zangu walizishambulia kama kuku anavyoshambulia muhindi. Unapokuwa mnyama wa maghettoni kama nilivyokuwa, unakuwa umeingia dunia ya wanyama. Hakika ilikuwa ni mwenye nguvu ndiye anayeishi.

Haikuchukua muda nikajikuta nikikopa pesa ndogondogo kutoka kwa Sammy na kutoka kwa baadhi ya wanamuziki. Pesa za kutosha kununua mahitaji, mimi mwenyewe kuweza kuvuta na wakati mwingine pesa ya kula.

Baadaye Sammy akanipa wazo. “Red si bado una kitambulisho chako kama mfanyakazi wa shirika la reli?” Bado nilikuwa nacho, walikuwa hawajaninyang’anya. “Kwa nini usikitumie kusafiri na kufanya biashara kwa muda mpaka upepo utakapopoa?” Alikuwa sahihi kabisa.

Niligundua kuwa ukienda kituo cha treni na kuonyesha kitambulisho cha mfanyakazi, basi msimamizi-na hata yule mzungu kauzu sana atakuruhusu kuingia. Unatakiwa tu kujiamini. Na wakati wa kukagua tiketi atakukatia.

Nikapata wazo la kusafiri maeneo yote ya Pwani ya Mashariki, nikiwauzia bangi rafiki zangu waliokuwa wakisafiri pamoja na bendi zao.

Nilikuwa na kitambulisho cha treni za New Haven. Nilifanya kazi kwa wiki kadhaa kwenye mashirika mengine na kupata vitambulisho vyao pia. Hapo nikawa kamili.

Nilisokota misokoto mingi na kuiweka ndani ya chupa. Vitambulisho vile vilifanya kazi vizuri sana. Ukiweza kumshawishi msimamizi kuwa ni mfanyakazi mwenzake na unaenda nyumbani kwa mambo ya kifamilia hivyo unahitaji msaada wake, alikusaidia mara moja. Wazungu wengi wanadhani kuwa watu weusi hawana akili au ujasiri wa kuweza kuwalaghai.

Nilifika kwenye mji ambao rafiki zangu walipiga mziki. “Red!” waliniita kwa furaha, nilikuwa mtu wao wa nyumbani. Na kwenye upande wa bangi, nilikuwa na bangi za New York. Hakuna mtu aliyewahi kusikia muuza bangi anayesafiri.

Sikuwa na bendi moja ya kuifuatilia. Kila bendi ilifahamu ratibu ya zingine, hivyo hazikugongana. Nilipoishiwa mzigo nilirudi New York na kujumua mwingine na kuondoka. Kwenye kumbi za muziki, nilijitambulisha mlangoni kama kaka wa mmoja wa wanabendi, lakini mara nyingi walidhani ni mmoja wa wanamuziki. Wakati wote wa dansi nilikuwa nikiwaonyesha watu wa vijijini mitindo mbalimbali ya kucheza Lindy Hop. Wakati mwingine nililala kwenye mji huo na wakati mwingine nilisafiri na basi la bendi kwenda mji mwingine, au nilirudi New York na kupumzika kwa muda kidogo. Mambo yalikuwa yameanza kupoa. Taarifa zilienea kuwa nimehama mji, na hilo lilitosha kuwaridhisha watu wa kikosi cha kuzuia dawa za kulevya. Kwenye baadhi ya miji midogo watu walidhani nami ni mwanamuziki hivyo walinizonga nisaini vitu vyao. Wakati fulani huko Buffalo walikuwa karibu wanichanie suti yangu.

Siku moja niliporudi New York nilimkuta mdogo wangu Reginald akinisubiria. Meli yao ilikuwa imetia nanga kwenye bandari ya New Jersey siku moja iliyopita. Alikwenda moja kwa moja Small’s akidhani bado nafanya kazi pale. Mhudumu wa kaunta alimuelekeza kwa Sammy ambaye alimpokea vizuri.

Nilijisikia furaha kumuona ndugu yangu. Haikuwa rahisi kuamini kwamba juzi tu alikuwa ni mtoto anayenifuata. Sasa alikuwa na urefu wa karibu futi sita, nilimzidi urefu kidogo tu. Alikuwa ni mweusi kuliko mimi lakini macho yake yalikuwa na ukijani hivi.

Nilimtembeza Reginald kotekote na kumtambulisha. Baada ya kumsoma vizuri tabia nilipendezwa naye sana. Alikuwa anajitambua sana kuliko mimi nilivyokuwa nilipokuwa na umri wa miaka kumi na sita.

Wakati huo sikuwa na chumba, lakini nilikuwa na pesa na Riginald naye alikuwa nazo. Basi tulikodi chumba kwenye hoteli ya St. Nicholas iliyokuwa eneo la Sugar Hill. Hoteli hiyo ilikuja kubomolewa.

Tuliongea na Reginald usiku mzima kuhusu miaka yetu ya zamani kule Lansing na kuhusu familia yetu. Nilimsimulia mambo ambayo hakukumbuka kuhusu baba na mama yetu. Reginald alinisimulia habari za ndugu zetu wengine. Wilfred alikuwa bado mkufunzi huko chuo kikuu cha Wilberforce. Hilda alikuwa anajiandaa kuolewa huko Lansing, Philbert naye alikuwa akijiandaa kuoa. Mimi na Reginald ndiyo tulikuwa tunafuata. Yvonne, Wesley na Robert walikuwa bado wapo shule huko Lansing.

Tulicheka kuhusu Philbert ambaye mara ya mwisho kuonana naye alikuwa amekuwa mtu wa dini sana; alikuwa akivaa zile kofia za mviringo zilizotengenezwa kwa nyasi.

Meli ya Reginald ilikuwa na ratiba ya kukaa pale kwa muda wa juma moja. Ilikuwa inafanyiwa marekebisho kwenye injini. Nilifarijika kuona Reginald anaheshimu mtindo wa maisha yangu, japo hakusema hilo kwa sauti. Niliona kama Reginald alivalia nguo “zilizopiga sana kelele.” Nilimtafuta mteja wangu mmoja wa bangi na kumwambia amtafutie suti ya kawaida. Nilimwambia Reginald kuwa kama unataka kupata kitu fulani, basi unatakiwa kuonekana kama vile tayari umeishakipata.

Kabla hajaondoka nilimshawishi aachane na kazi ya ubaharia nami nitamsaidia kuanza maisha pale Harlem. Nafikiri nilidhani kuwa karibu na mdogo wangu litakuwa ni jambo zuri. Hapo nitakuwa na watu wawili wa kuwaamini, yeye na Sammy.

Reginald alikuwa mtaratibu sana. Ningekuwa ni mimi, ningekuwa tayari kukimbia kwa miguu nikifuatilia treni nyuma hadi kufika New York kisha Harlem. Lakini yeye wakati wa kuondoka alinijibu, “Nitafikiria kuhusu hilo.”

Muda mfupi baada ya Reginald kuondoka nilinunua zoot moja matata sana ya. Hii ilikuwa ni mwaka 1943. Bodi ya kuandikisha watu jeshini huko Boston ilikuwa imeniandikia barua iliyomfikia Ella. Walipokosa majibu kule, waliiarifu bodi ya New York, nilipata barua hiyo nikiwa kwa Sammy.

Wakati huo ni vitu vitatu tu duniani ndivyo viliniogopesha: Jela, kazi na jeshi. Nilipewa siku kumi niwe nimeripoti. Mara moja nikaanza kupambana kujinasua. Harlem kulikuwa na wanajeshi wapelelezi weusi waliovalia mavazi ya kiraia. Masikio yao yalikuwa wazi muda wote kwa ajili ya mzungu aliyekaa mjini-kati. Mara moja nilifahamu kwa kupeleka maneno. Nilianza kupayuka kwa watu kuwa nina hamu ya kujiunga na jeshi la Wajapan.

Nilipohisi kuwa wapelelezi wananisikia, nilijidai mwehu na nimelewa madawa. Wachakarikaji wengi wa Harlem walikuwa hivyo kiukweli—kama ambavyo nami nilikuja kuwa. Hali hiyo ilikuwa haikwepeki kwa mtu ambaye ametumia madawa makali ya kulevya kwa muda mrefu, tena chini ya maisha magumu. Nilitoa barua yangu na kuisoma kwa sauti kuhakikisha wananijua vyema hivyo wakaniripoti mjini-kati(Pengine huu ndiyo wakati pekee jina langu halisi lilisikika maeneo ya Harlem)

Siku niliyoenda kuripoti nilivalia kama muigizaji. Nilivaa zoot yangu kituko na kiatu cha njano ambacho kilituna kwa mbele. Nilizitibua nywele zangu, zikawa kama kichaka chekundu.

Nilienda kwa mwendo wa kudunda na kutupia barua yangu kwenye meza ya mwanajeshi mzungu wa mapokezi-“Crazy-o, Dady-o, get me moving. I can’t wait to get in that brown,”-kuna uwezekano mkubwa mwanajeshi yule bado hajapona hali niliyomsababishia.

Hakukuwa na shaka kuwa walikuwa wamepata taarifa zangu kutoka Harlem. Lakini bado walinisaili. Chumbani mle tulikuwa watu kama thelathini au arobaini hivi. Chumba kilikuwa kimya kabisa, ni mimi tu niliyekuwa nikipiga domo kama cherehani, Niliongea lugha ya kijiweni tu. Nilidhamiria kupambana kwa kila njia. Ingenibidi kuwa jenerali ili kuacha kuongea vile. Wengi wa watu mle ndani walikuwa ni wazungu, wale walionekana wapole walikuwa karibu kunikimbia. Wengine waliniangalia vile wazungu ambavyo wazungu huwaangalia “watu weusi wa hovyo kabisa.” Wachache walikuwa wanafurahia, wakiniona kama tu msela mweusi kutoka Harlem.

Waliofurahi wengine walikuwa ni watu weusi kama kumi au kumi na mbili hivi. Lakini wengine waliokuwa na sura za kikauzu walionekana wako tayari kujiandikisha kwenda kuua watu—na wangependa kuanza na mimi.
 
Sura ya sita inaendelea
Foleni ilitembea na zamu yangu ilipofika nikavuliwa nguo na kubaki na bukta tu. Wakati wa vipimo vya afya niliendelea kuongea kuhusu hamu yangu ya kujiunga. Wote sura zao zilionyesha kuwa waliniona sifai kujiunga na jeshi. Baada ya muda kidogo mtu aliyevalia koti jeupe alikuja kunichukua. Nilifahamu kuwa nilikuwa napelekwa kwa mwanasaikolojia wa jeshi.

Mtu wa mapokezi pale alikuwa ni muuguzi mweusi. Nakumbuka alikuwa kama wa miaka ya ishirini na kidogo. Alikuwa mzuri kumtazama. Alikuwa ni mmoja wa wale watu weusi waliotangulizwa mbele.

Watu weusi wanajua ninachoongelea. Wakati wa vita mzungu alihitaji sana watu kiasi kwamba alianza kuwaruhusu watu weusi kutumia kalamu na kukaa kwenye meza na kutupa chini madekio, ndoo na vitambaa vya usafi.

Kuna mtu alikuwa ofisini kwa mwanasaikolojia. Sikuhitaji kuigiza chochote mbele ya msichana huyu. Alikereka nami mara moja.

Mara kengele ya mezani pake ikalia, hakuniruhusu niingie moja kwa moja, aliingia yeye kwanza. Nilifahamu alichokuwa akifanya, alikuwa anaenda kutoa taarifa mapema ya jinsi nilivyo. Hili bado ni tatizo kubwa linalomkabili mwanaume mweusi hata leo. Wengi wa wanaojiita watu weusi wa “Daraja la juu” wanahangaika sanakujaribu kumuaminisha mzungu kwamba wako “Tofauti na wale wengine” hawawezi kuona kuwa hilo linamfanya mzungu adharau watu weusi wote.

Basi alipokwisha jisafisha huko ndani, alirudi na kuniruhusu niingie.

Niseme hivi kuhusu yule mwanasaikolojia. Alijaribu kuwa muelewa na kufanya kazi yake kwa weledi. Alinisikiliza kwa kama dakika tatu au nne hivi kabla hajauliza swali.

Alianza kwa kuniuliza maswali yaliyotaka kufahamu kwa nini nilikuwa na wasiwasi. Sikumjibu moja kwa moja. Nilijizungusha, nikimuangalia kwa makini na kumuacha aone kuwa anapata anachokitaka. Niliendelea kuongea mambo mengi kama vile kuna mtu mwingine anasikiliza. Nilijua kuwa kutoka pale atakwenda vitabuni kupekua ili kufahamu nilikuwa nasumbuliwa na tatizo gani.

Ghafla niliinuka na kuchungulia chini ya milango—mlango nilioingilia na mwingine ambao nadhani ulikuwa ni kabati. Kutoka hapo niliinama na kumnong’oneza sikioni, “Daddy—oo, mimi nawe sote tunatokea kaskazini, basi usimwambie mtu kuwa ninataka kutumwa huko kusini. Nikawakusanye wanajeshi kadhaa weusi, si unajua? Tuibe bunduki na kuua wazungu!”

Kalamu ilimdondoka mwanasaikolojia yule. Utulivu wake kama mtaalamu ulimtoka. Aliniangalia kama vile nilikuwa yai la nyoka linaloanguliwa. Nilijua kuwa nimempata. Nilikuwa nampita yule bibie wa mapokezi nilipomsikia akisema, “basi wanatosha.”

Nilipata barua ya 4-F(kuonyesha sifai kutumikia jeshini) na sikusikia tena kutoka jeshini, na wala sikujihangaisha kujua kwa nini nilikataliwa.

Mwisho wa sura ya sita​
 
SURA YA SABA

MCHAKARIKAJI

Sikumbuki kazi zote nilizofanya kwenye miaka miwili iliyofuata pale Harlem, baada ya kuacha kusafiri kwa treni ili kuuza bangi kwa wanamuziki wa bendi zilizosafiri.

Wafanyakazi weusi wa shirika la reli walikuwa wakisubiria treni zao kwenye chumba kikubwa kilichokuwa ghorofa ya chini ya kituo cha Grand Central. Kamari ilichezwa muda wote chumbani mle. Wakati mwingine hadi kiasi cha dola mia tano kilikuwa mezani. Siku moja wakati wa kucheza kamari ya karata, mzee mmoja mpishi aliyekuwa akichanga karata akataka kujidai mjanja hivyo nikamtolea bastola.

Safari zilizofuata za kwenye kamari hizo, machale yaliniambia kuweka bastola, ndani mkanda mgongoni. Mtu mmoja akawa amenichongea. Polisi wawili wakubwa wa ki-Irish waliingia. Walinikagua lakini hawakuipata bastola mahali walikotegemea. Waliniambia kuwa sitakiwi kabisa kuonekana kituo cha Grand Central isipokuwa niwe na safari. Na nilifahamishwa kuwa kuanzia siku inayofuata ofisi zote za wafanyakazi wa reli zimenipiga marufuku, kuanzia hapo sikujaribu tena kupata kazi kwenye shirika la reli.

Basi nikarudi mitaa ya Harlem kujumuika na watafutaji wengine. Sikuweza tena kuuza bangi; watu wa kikosi cha kuzuia dawa za kulevya walinifahamu vyema. Nilikuwa mchakarikaji halisi—sina elimu, wala sina ujuzi wa kazi yoyote ya heshima lakini nilijiona mjanja na akili kuweza kuishi kwa ujanja-ujanja, kumnyonya mnyonge yeyote aliyekatiza mbele yangu.

Siku hizi kwenye maeneo ya maghetto ya miji mikubwa kuna makumi elfu ya watu walioacha shule wanaopambana kuendesha maisha kwa kutumia njia nilizotumia. Nao hawawezi kuepuka kuzama zaidi na zaidi kwenye uhalifu na ukosefu wa maadili mbaya hata zaidi na zaidi. Wachakarikaji wa muda wote hawastarehi na kujipongeza juu ya wanachofanya na. Kama ilivyo ndani ya msitu wowote, kila saa ambayo mtafutaji yuko macho anakuwa anaelewa vyema kuwa iwapo akistarehe, kama akizubaa mbwa mwitu na wanyama wengine wenye njaa waliomzunguka hawataacha kumtafuna.

Ndani ya miezi sita au nane iliyofuata nilianza kufanya ujambazi. Ulikuwa ni ujambazi mdogomdogo tu. Mara zote ilikuwa ni kwenye miji ya karibu. Nilifanikiwa kutokamatwa. Kama wakongwe walivyofanya, nami nilijiandaa kufanya kazi hizi kwa kutumia madawa ya kulevya vya kutosha. Nilianza kama alivyonishauri Sammy—kunusa cocaine.

Wakati huo mara nyingi nilitembea na bastola yenye risasi za .25. Lakini kwa kazi nilibeba yenye risasi za .32 , .38 au .45. niliona jinsi ambavyo watu waliokuwa wakiangalia mdomo wa bastola nyuso zikiwashuka na midomo ikiwalegea. na nilipoongea, walionekana kusikiliza japo akili zao ni kama zilikuwa mbali-walifanya kila nilichowaamuru.

Dawa za kulevya zilinituliza na kuniondolea wasiwasi baada ya kazi. Lakini bado, ili kuwa salama nililazimika kuhama vyumba mara kwa mara, mara zote nikiwa meneo yangu pendwa ya mtaa wa 147 hadi wa 150, pembezoni mwa Sugar Hill.

Siku moja tukiwa kazini na Sammy tuliponea chupu chupu kukamatwa. Kutakuwa na mtu alituona. Tulikuwa tunakimbia tukiondoka na ghafla tukasikia ving’ora vya polisi vikilia, hapo hapo tukaanza kutembea kawaida. Gari ya polisi ilipokuwa ikija kasi, tulijitokeza barabarani na kuipungia mkono tukijidai kuulizia uelekeo. Lakini wao nadhani walifikiri kuwa kuna taarifa tunataka kuwapa. Walitutukana na kuondoka kwa kasi. Kwa mara nyingine haikuingia akilini mwa mzungu kuwa mtu mweusi anaweza kumfanyia ujanja kama ule.

Nilikuwa navaa suti bora kabisa, zilikuwa ni za wizi na nilinunua kwa dola thelathini na tano hadi hamsini na tano. Nilifanya kuwa kanuni yangu kutoiba zaidi ya ninachohitaji ili kuishi. Mchakarikaji yeyote mwenye uzoefu atakwambia kuwa tama ndiyo njia ya haraka ya zaidi ya kukuingiza gerezani. Nilifanya kazi pale tu nilipoanza kuishiwa.

Nilicheza sana kamari, majuma mengine nilipinga kiasi sana. Nilikuwa bado namtumia muandikisha wacheza kamari yuleyule niliyekuwa namtumia tokea nipo Small’s Paradise. Siku zingine nilicheza hadi dola arobaini, nikiigawanya kwenye namba mbili. Nilikaa nikitegemea kushinda mara mia sita ya nilichoweka. Lakini kamwe sikuwahi kushinda pesa kubwa. Sijui ningefanya nini iwapo ningeshinda dola 10,000 au 12,000 mara moja. Mara moja moja nilishinda pesa ndogo ndogo. Wakati mwingine ghafla tu nilijikuta nikimpigia simu Sophia aje New York kwa siku kadhaa.

Nikaanza tena kwenda kuangalia filamu mara kwa mara. Pia nilikuwa sikosi kwenda kuwaangalia rafiki zangu wanamuziki kokote walikopiga, iwe ni Harlem, kwenye kumbi kubwa za mjini-kati au mtaa wa 52.

Ukaribu wangu na Reginald uliongezeka sana meli yao ilipokuja New York kwa mara nyingine. Tulizungumza kuhusu familia, na kusikitika kuwa kaka yetu mpenda vitabu—Wilfred alishindwa kujiunga na moja ya vile vyuo vikuu vikubwa, jambo ambalo lingemfanya afike mbali. Pia tulibadilishana mawazo ambayo hatukuwahi kuongea na mwingine yeyote yule.

Japo Reginald alikuwa ni mpole, lakini alikuwa ni shabiki mkubwa wa muziki na wanamuziki. Siku moja meli yake ilipong’oa nanga na kumuacha, ilikuwa ni sababu nilikuwa nimemtambulisha kwenye ulimwengu wa muziki. Tulikuwa na shangwe sana pamoja na wanamuziki nyuma ya jukwaa. Baada ya kuwauzia bangi wanamuziki walipokuwa wakisafiri, ikatokea karibu wanamuziki wote weusi waliokuwa maarufu jijini New York kwenye mwaka 1944-1945 walinifahamu.

Nilienda na Reginald ukumbi wa Apollo, Baa ya hoteli ya Braddock, club za usiku na baa za vichochoroni, kote ambako wasanii weusi walipiga muziki. Nilimtambulisha kwa wasanii kadhaa, hata Billie Holiday “Lady Day” alimkumbatia na kumwita kaka mdogo. Reginald alihisi kama ambavyo maelfu ya watu weusi wengine walivyohisi, kwamba bendi bora kuliko zote ilikuwa ni ile ya Lionel Hampton. Nilikuwa na ukaribu na wanamuziki wengi wa bendi ya Hampton; nilimtambulisha Reginald kwao na hata kwa Hamp mwenyewe na mkewe, Gladys Hampton ambaye alikuwa pia ni meneja wa bendi. Hampton ni moja ya watu wakarimu zaidi duniani. Kila anayemfahamu atakwambia kuwa mara nyingi aliwafanyia ukarimu watu asiowajua kabisa. Lakini pamoja na pesa zote ambazo Hamptona alitengeneza, na anazendelea kutengeneza-leo hii angekuwa amefirisika iwapo Gladys hangekuwa msimamizi wa biashara yao. Gladys ni moja kati ya wanawake wenye akili sana niliowahi kukutana nao. Frank Schiffman, mmiliki wa ukumbi wa Apollo anaweza kukuthibitishia hilo. Mara nyingi alikubaliana na bendi kupiga hapo kwa malipo fulani ya kila juma, lakini nafahamu kuwa Gladys alifanya mipango ili bendi ya Hampton ipate mgao kutokana na mapato ya mlangoni. Kisha, kama nakumbuka vizuri akaongeza idadi ya shows mara mbili. Gladys Hampton alikuwa akiongea nami mara nyingi, akijaribu kunipa ushauri, “Kuwa mtulivu Red.” Gladys aliona jinsi nilivyokuwa siambiliki. Aliniona nikielekea mwisho mbaya.
 
Sura ya saba inaendelea

Kitu nilichompendea Reginald ni kuwa nilipomuacha na kwenda “Kazini” hakuniuliza maswali. Alipohamia Harlem, nilianza kwenda kazini mara nyingi kuliko kawaida. Nafikiri hilo pia ndilo lililonisukuma kutafuta nyumba ya kuishi, sikutaka Reginald kurandaranda mitaa ya Harlem bila ya sehemu anayoweza iita nyumbani. Nyumba yangu ya kwanza ilikuwa na vyumba vitatu, nafikiri kodi ilikuwa dola mia moja kwa mwezi, ilikuwa ni makazi ya chini kwenye nyumba iliyokuwa mtaa wa 147, kati ya barabara ya St. Nicholas na Convent. Kwenye makazi ya chini ya nyuma yetu aliishi mmoja wa wauza madawa ya kulevya aliyekuwa maarufu sana kwenye vitongoji vya Harlem.

Polepole nilianza kumtambulisha Reginald kwa Creole Bill na maeneo mengine ya Harlem yaliyokesha. Kama saa nane usiku hivi kila siku, wakati ambao club nyingi za kizungu huko mjini-kati zilipokuwa zinafunga, nilikuwa nikisimama na Reginald mbele ya eneo fulani lililokesha na kumfundisha jinsi mambo yanavyoenda.

Baada ya ya club za mjini kufungwa, taxi na limousines ziliongozana kuja Harlem zikiwaleta wazungu ambao shangwe la watu weusi halikuwakinai. Maeneo ambayo wazungu hawa walipenda kutembelea yalianzia maeneo maarufu kama Jimmy’s Chicken Shack na Dickie Wells, hadi club ndogo ambazo unakuta leo ipo na kesho imepotea-club za wanachama tu-ziliitwa hivyo kwa sababu zilitoza dola moja kama ada ya “Uanachama.”

Kwenye kila moja ya maeneo haya yaliyokesha kulikuwa na moshi wa kuweza kukuumiza macho. Kwa kila mweusi mmoja kulikuwa na wazungu wanne, wakinywa wiski kwa kutumia vikombe vya kahawa na kula kuku wa wakukaanga. Wanawake kwa wanaume wa kizungu walikuwa wakipongezana huku wakipiga kelele na wakifurahia muziki. Wazungu wengi waliolewa walikuwa wakiwafuata watu weusi-wahudumu, wamiliki au walioketi mezani, huku wakipepesuka, wameweka mikono tayari kuwakumbati, “Wewe hauna tofauti yoyote na mimi, nataka ufahamu hilo!”

Kwenye maeneo maarufu zaidi walijaa watu maarufu, weupe kwa weusi. Walichangamana na kufurahi pamoja. Umati wa watu saa kumi na nusu alfajiri huko Jimmy’s Chicken Shack au Dickie Wells’ waliweza kufurahia muziki muda huo kutoka wakali kama Hazel Scott akimpigia piano Billie Holiday aliyeimba blues. Baadaye nilikuja kufanya kazi kwa muda mfupi kama mhudumu wa Jimmy’s Chicken Shack. Hapo ndipo Redd Foxx alifanya kazi kama muosha vyombo huku akiwavunja mbavu wafanyakazi wenzake.

Baada ya muda kidogo ilibidi Reginald naye apate shughuli ya kufanya. Nilifikiri sana juu ya kazi itakayomfaa—kazi nzuri na salama. Aanze na hiyo kwanza, baada ya kujua mji vizuri, utakuwa ni uamuzi wake kufanya za hatari zaidi-kama angetaka kutengeneza pesa ya haraka.

Kazi niliyomtafutia ilikuwa rahisi sana. Nilitumia saikolojia ya kighetto. Alienda mjini-kati na kulipa kama dola mbili kwa ajili ya leseni ya umachinga. Kisha nikampeleka kwenye duka la jumla na tukanunua mashati, nguo za ndani, pete, saaa na vitu vingine vilivyotoka haraka. Vitu hivyo vilikuwa ni vya kiwango cha chini na bei yake ilikuwa chini.

Baada ya kuniona ninavyouza vitu hivyo, mara moja Reginald alifahamu jinsi ya kuingia kwenye saluni na baa, akijidai ana wasiwasi sana pale wateja walipokuwa wanakagua mzigo wake wa “Wizi.” Sababu ya wezi wengi waliokuwepo, wakitaka kuuza vitu vyao walivyoiba kwa haraka—vitu bora kwa bei rahisi. Kutokana na hili watu wengi walikubali kulipa bei nzuri kwa vitu halali japo vilikuwa na vya kiwango cha chini, wao wakiamini ni vya wizi na ni vya kiwango cha juu. Haikuchukua muda kumaliza mzigo na kupata walau mara mbili ya bei ya kujumulia. Na iwapo polisi walimsimamisha, walimkuta Reginald ana leseni ya umachinga na risiti kutoka kwa muuzaji wa jumla. Reginald alitakiwa tu kuhakikisha kuwa hakuna mteja wake aliyefahamu kuwa anauza mali halali.

Nilidhani kuwa Reginald atatataka kuwa na mwanamke wa kizungu kama walivyokuwa wanaume weusi wengine. Nilimuelekeza kwa wanawake wa kizungu waliopenda wanaume weusi na kumueleza kuwa, mwanaume mweusi yeyote mwenye kujielewa anaweza kuwadhibiti wanawake hao. Lakini niseme hili kuhusu Reginald: hakupenda wanawake wa kizungu. Nakumbuka mara ya kwanza alipokutana na Sophia hakushoboka kabisa, na jambo hilo lilimtatiza Sophia kwa kiasi fulani.

Reginald alijipatia mwanamke mweusi, alikuwa ni mwanamke mkubwa anayekaribia miaka thelathini. Tulizoea kuwaita wanawake hao wakoloni. Alikuwa ni mhudumu kwenye mgahawa mmoja wa hali ya juu huko mjini-kati. Alimpenda na kumhudumia Reginald kwa uwezo wake wote. Alikuwa na furaha sana kwa kupata mwanaume kijana. Alimnunulia nguo, alimpikia na kumfulia nguo. Alimfanyia kila kitu. Kama vile alikuwa ni mtoto.

Jambo hilo lilikuwa ni moja ya sababu iliyofanya heshima yangu kwa mdogo wangu kuongezeka. Reginald alionyesha kuwa anaakili kuliko wachakarikaji wengi waliokuwa na umri mara mbili yake. Wakati huo Reginald alikuwa na miaka kumi na sita tu, lakini akiwa na urefu wa futi sita. Kwa muonekano na tabia alikuwa kama mtu wa miaka mingi zaidi.

***

Wakati wote wa vita hali ya Harlem ilikuwa tete sana. Wakongwe walikuwa wakiniambia kuwa Harlem haijawahi kutengamaa tangia zitokee vurugu za mwaka 1935, vurugu zilizosababisha maelfu ya watu weusi kuharibu mali zenye thamani ya mamilioni ya dola. Chanzo ilikuwa ni kuchukizwa na kitendo cha wafanyabiashara wa kizungu wa Harlem kukataa kuajiri watu weusi kwenye maduka yao, japo watu weusi ndiyo walikuwa wateja wao wakuu.

Wakati wa vita ya pili ya dunia, Meya wa New York, La Guardia, aliufunga rasmi ukumbi wa Savoy. Watu wa Harlem walisema sababu hasa ilikuwa ni kuzuia wanaume weusi wasicheze na wanawake wa kizungu. Adam Clayton Powell alipambana vikali na kampuni za Consolidated Edison na kampuni ya simu ya jiji la New York hadi zikakubali kuanza kuwaajiri watu weusi. Kisha akasaidia kupambana na jeshi la majini na la nchi kavu la Marekani juu ya suala lao la kubagua wanajeshi weusi na wazungu. Lakini Powell hakuweza kushinda hii vita ya Savoy. Jiji liliufunga ukumbi wa Savoy kwa muda mrefu sana. lilikuwa ni moja ya matendo ya “waliberali wa kaskazini” ambayo hayakusaidia kwenye suala la watu weusi kuwapenda wazungu

Mwishowe, kukasambaa tetesi kuwa polisi wa kizungu alikuwa amempiga risasi mwanajeshi mweusi ndani ya hoteli ya Braddock. Nilikuwa natembea kwenye barabara ya St. Nicholas; ghafla nikaona watu weusi wengi wakipiga kelele na kukimbia wakitoka mtaa wa 125. Baadhi yao wakiwa wamebeba bidhaa za kila aina. Nakumbuka ni “Shorty” Henderson, mpwa wa kiongozi mmoja wa bendi aliyeitwa Fletcher Handerson ndiye aliyenijulisha kinachoendelea. Watu weusi walikuwa wakivunja madirisha ya maduka na kubeba kila kitu walichoweza kubeba. Walibeba samani, chakula, urembo, wiski, nguo nk. Ndani ya saa moja ikiwa kama kila polisi wa jiji la New York alikuwa yupo Harlem. Meya La Guardia na katibu mkuu wa NACCP(National Association for Advancement of Colored People(Chama cha Kitaifa cha Kuendeleza watu wenye Rangi )) wa wakati huo, Walter White walikuwa kwenye gari jekundu la kikosi cha zimamoto, wakiongea kupitia kipaza sauti-wakiomba watu weusi wenye hasira warudi majumbani mwao na kukaa ndani.

Hivi karibuni nilikutana na Shorty Handerson kwenye barabara ya saba. Tulikumbushana na kucheka kuhusu mtu mmoja ambaye baada ya vurugu alipachikwa jina “Miguu ya Kushoto.” Wakati wa kung’ang’aniana bidhaa kwenye duka la viatu vya kike alifanikiwa kubeba viatu vitano, lakini vyote vilikuwa vya miguu ya kushoto! Pia tulicheka juu ya Mchina mmoja aliyejawa na uoga lakini mgahawa wake haukuguswa hata kidogo. Waandamanaji walishia kucheka tu baada ya kuona bango ambalo alikuwa ameliweka harakaharaka, lilisomeka: “Na mimi ni mtu mwenye rangi(Mimi siyo mzungu).”

Baada ya machafuko yale hali ilikuwa ngumu sana pale Harlem. Watu waliotegemea biashara za usiku na wachakarikaji waliotegemea wateja wa kizungu walikuwa na hali mbaya zaidi. Machafuko ya mwaka 1935 yalikuwa yamebakiza pesa kidogo sana kati ya pesa nyingi zilizomiminika Harlem kwenye miaka ya 1920. Machafuko haya yakawa yamemaliza hata hicho kiasi kidogo.

Leo hii wazungu wanaotembelea Harlem, na wengi wao mwishoni mwa juma huwa hawazidi kumi kadhaa, wanakuja kucheza twist, frug, watusi na mitindo mingine ya dansi inayobamba kwenye baa ya Small’s Paradise. Baa hiyo sasa inamilikiwa na mcheza kikapu maarufu, “Wilt the stilt” Chamberlain. Huyo anavutia watu wengi kutokana na umaarufu wake. Wazungu wengi leo wanaogopa kufika Harlem—na wana sababu za msingi. Hata kwa watu weusi, biashara za usiku za Harlem zilikuwa zimefika mwisho. Watu weusi wengi wenye pesa za kutumia wanatumia huko mjini-kati, kwenye maeneo yaliyo ruhusu uchangamano wa kinafiki-maeneo ambayo hapo zamani polisi waliitwa kuwatoa watu weusi waliokuwa wabishi na kujaribu kuingia. Tajiri wa kizungu hawezi kumalizia hoteli yake kabla ya hawa watu weusi, ambao wao hata hawamiliki banda la kutunzia zana-hawajaanza kulipia hoteli hiyo mpya kwa ajili ya dansi na makongamano. Wazungu wale waliokuja Harlem kutapanya pesa walikuwa na pesa za kutosha. Lakini watu weusi si matajiri wa kupeleka pesa mjini-kati kwa mzungu.

***
 
Sura ya saba inaendelea.

Tulipokuwa kwenye kazi yetu ya ujambazi na Sammy tulikutana na hatari moja mbaya sana.

Mambo yalikuwa yamekuwa magumu sana pale Harlem hadi baadhi ya wachakarikaji wakaingia kutafuta kazi. Hata baadhi ya makahaba wakawa wametafuta kazi kama wahudumu wa majumbani na wafanya usafi maofisini nyakati za usiku. Kazi ya ukuwadi ilikuwa imedorora sana hivyo Sammy akajiunga rasmi kwenye ujambazi. Tulikuwa tumechagua moja ya zile kazi ambazo huonekana kuwa haziwezekani. Watu wakiwa na fikra hizo, walinzi huanza kuzembea polepole, mpaka inafikia wakati zinakuwa ni moja ya kazi rahisi zaidi. Lakini katikati ya kazi bahati mbaya ikatukuta. Risasi ilimchubua Sammy na tukaokoka kwa bahati tu. Bahati nzuri hakuumia. Tuliachana na kila mtu kwenda njia yake, na mara zote ilikuwa ni busara kufanya hivyo.

Kabla hakujakucha nilienda nyumbani kwa Sammy. Mwanamke wake mpya, mmoja wa wale wanawake weusi wa kihispania-wazuri lakini vichaa—alikuwa akilia na kufanya matata. Alinifuata na kuanza kunipigia kelele; alifahamu kuwa nilikuwa na Sammy kwenye sekeseke la jana. Sikujua kwa nini Sammy hakumnyamazisha—nikamnyamazisha . . . kwa jicho la pembeni nikamuona Sammy akiiendea bastola yake.

Pamoja na ukaribu wangu na Sammy lakini nilikuwa bado kugundua udhaifu wake. Kitendo chake baada ya kuwa nimempiga mwanamke wake kilinifanya nigundue udhaifu wake. Mwanamke wake alipiga kelele na kumuangukia kumzuia. Kama mimi, mwanamke wake naye alifahamu kuwa rafiki yako wa karibu anapokutolea bastola anakuwa ameshindwa kabisa kudhibiti hasira zake, na amedhamiria kukupiga risasi. Alimzubaisha Sammy kiasi cha kunipa nafasi ya kukimbia. Sammy alinikimbiza umbali wa karibu mtaa mzima.

Baadaye tulikuja kuyaweka sawa—lakini kamwe mambo hayawezi tena kuwa sawa na mtu uliyeona akijaribu kukuua.

Machale yalituambia kuwa ni vyema tukatulia kwa muda fulani. Kitu kibaya zaidi ni kuwa tulikuwa tumeonekana. Polisi wa ule mji wa jirani walikuwa wamesambaza taarifa ya jinsi tulivyo.

Sikuweza kusahau kirahisi tukio lile juu ya mwanamke wa Sammy. Kutoka hapo nikaanza kumtegemea zaidi ndugu yangu Reginald kama mtu pekee ninayeweza kumuamini kabisa.

Nilikuja kugundua kuwa Reginald ni mvivu. Aliacha kazi yake. Lakini sikujali sana, mtu anaweza kuwa mvivu atakavyo iwapo anaweza kutumia kichwa chake kuendesha maisha yake, kama alivyokuwa akifanya Reginald. Wakati huo alikuwa amehama kwangu na kwenda kuishi na mwanamke wake. Nilikuwa nimemfundisha Reginald jinsi anavyoweza kufanya kazi kwa muda kwenye shirika la reli na kisha kutumia kitambulisho chake kusafiri bure. Reginald alipenda sana kusafiri. Kwa mara kadhaa alikuwa ameenda kusalimia ndugu zetu ambao kufikia sasa walikuwa wametawanyika kwenye miji mbalimbali. Huko Boston, Reginald alikuwa karibu zaidi na Mary kuliko Ella, tofauti na mimi. Wote Reginald na Mary walikuwa ni wakimya, lakini mimi na Ella tulikuwa watu wachangamfu sana. Shorty alikuwa amempokea mdogo wangu vizuri sana.

Kutokana na sifa zangu, ilikuwa rahisi kwangu kuingia kwenye mchezo wa kamari. Pengine ile ndiyo ilikuwa biashara pekee ya Harlem ambayo ilikuwa haijadorora. Kwa kuwafanyia hisani fulani wakubwa wa magenge ya kizungu, bosi wangu mpya alikuwa amepewa ruhusa ya kuendesha biashara ya kamari kwa miezi sita kwenye eneo la reli la Bronx lililoitwa Motthaven Yards. Wahalifu wa kizungu walikuwa wamegawanya maeneo ya kamari kwenye maeneo mbalimbali. Mtu alipewa eneo fulani kufanya kazi kwa muda fulani. Mke wa bosi wangu aliwahi kuwa katibu wa Dutch Schultz kwenye miaka ya 1930-, wakati ambao Shultz aliingia kibabe kwenye biashara ya kamari ya Harlem.

Kazi yangu ikawa ni kusafiri kwa basi kuvuka daraja la George Washington na kumkabidhi mtu fulani begi lenye risiti za kamari. Hatukuwahi kuongea, nilivuka tu barabara kisha nikapanda basi na kurudi. Sikuwahi kujua aliyekuwa akienda kuchukua pesa za zile risiti. Hutakiwi kuuliza maswali kwenye biashara kama zile.

Mke wa bosi wangu na Gladys Hampton walikuwa ndiyo wanawake pekee niliokutana nao Harlem ambao niliheshimu uwezo wao wa kibiashara. Mke wa bosi wangu alipokuwa na muda wa kuzungumza alinisimulia mambo mengi ya kushangaza, alinisimulia mambo ya wakati wa Dutch Shultz—juu ya biashara haramu alizozifahamu. Juu ya hongo walizopewa polisi, wanasheria na hadi uongozi wa juu kabisa wa polisi na wanasiasa. Kwa uzoefu wake, alijua ni kiasi gani cha uhalifu vyombo vya dola huweza kuvumilia na kutoa ushirikiano. Alinionyesha jinsi ambavyo nchini kote huwezi kuwatenganisha, wahalifu, dola na wanasiasa.

Ni wakati huo ndipo nilipobadili muandikisha wacheza kamari wangu, yule niliyefanya naye kazi tokea nipo Small’s Paradise. Aliumia kupoteza mcheza kamari mkubwa kama mimi, lakini alielewa kwa nini sasa nilitaka kutumia watu wa kwenye genge langu. Hapo ndipo nilipoanza kumtumia West Indian Archie. Nimeisha mtaja kama mmoja wa watu weusi katili kabisa katika Harlem; mmoja wa wale waliokuwa mabaunsa wa Dutch Shultz alipoingia Harlem.

West Indian Archie alikuwa ametoka gereza la Sing Sing muda mfupi tu kabla ya mimi kufika Harlem. Mke wa bosi wangu hakumuajiri Archie kwa sababu anamjua, ni kwa sababu Archie alikuwa na kichwa kizuri cha kumbukumbu. Jambo hilo lililomfanya afae sana kwenye kazi ya kamari. Archie kamwe alikuwa haandiki namba yako, hata kama ulicheza zaidi ya namba moja. Alikuwa anaweza kutunza namba zote kichwani. Aliziandika pale tu alipompelekea muhasibu pesa. Hili lilimfanya awe muandikishaji anayefaa sana maana polisi wasingeweza kumkamata akiwa na risiti za kamari.

Mara zote nimetafakari juu ya wakongwe wa kamari kama Archie. Iwapo wangekuwa kwenye jamii ya aina tofauti, uwezo wao mkubwa wa hesabu ungeweza kutumika kwa manufaa zaidi. Lakini tatizo lao walikuwa watu weusi.

Ilikuwa ni sifa kujulikana kuwa ni mteja wa West Indian Archie maana alishughulika na wateja wenye pesa. Pia alihitaji wateja wake wawe waaminifu na wenye kulipa madeni: haikuwa lazima kuwa na pesa ili ucheze; ungeweza kumlipa Archie kwa juma. Mara zote alitembea na dola elfu kadhaa, pesa zake mwenyewe. Iwapo mteja wake amemfuata na kumwambia kuwa kashinda kiasi fulani cha kati, labda baada ya kucheza senti hamsini au dola moja, Archie alitoa dola mia tatu au mia sita kwenye pesa zake mwenyewe na kumlipa, baadaye alienda kuchukua pesa zake kwa bosi mkubwa.

Kila mwisho wa juma nililipa deni langu kwa Archie, kati ya dola hamsini na hata wakati mwingine dola mia moja iwapo nilicheza sana. Niliposhinda-kama mara moja au mara mbili hivi, Archie alinilipa kwa pesa zake mwenyewe.

Hatimaye miezi sita ya bosi wangu na mke wake kufanya kazi eneo lile ilitimia. Walikuwa wametengeneza pesa za kutosha. Waandikishaji wao walipata ahsante nzuri na mara moja wakawa wamechukuliwa na mabosi wengine. Niliendelea kufanya kazi kwao kwenye sehemu ya kuchezesha kamari waliyoifungua.

***

Madam(Mwanamke mwendesha danguro) mmoja ambaye nilimfahamu baada ya kumfanyia hisani rafiki yake, alinitambulisha kwenye ulimwengu wa usiku wa pekee sana pale Harlem. Ulimwengu ambao machafuko hayakuuathiri zaidi ya kuusimamisha kwa muda tu. Ulikuwa ni ulimwengu ambao kwenye nyumba za siri watu weusi walikuwa wakiwatimizia wazungu tamaa za ajabu-ajabu za ngono.

Wazungu niliowafahamu walikuwa ni wale waliopendelea kuchanganyikana na watu wa Harlem. Lakini wazungu hawa hawakutaka hata kidogo ifahamike kuwa wamefika Harlem. Machafuko yalikuwa yamewafanya wateja hawa wa pekee kuwa na wasiwasi sana. Kuja na kuondoka kwao Harlem kulikuwa hakuonekani kirahisi wakati wazungu wengi walipokuwa wanafurika Harlem. Lakini sasa ilikuwa ni rahisi kuonekana, na pia waliogopa hasira iliyowapanda watu weusi wa Harlem hivi karibuni. Basi madam yule alikuwa alilinda biashara yake kwa kunipa kazi ya kupokea na kuongoza wateja wake.

Ilikuwa ni vigumu sana kupata simu wakati ule wa vita. Siku moja madam yule aliniambia nisitoke nyumbani asubuhi inayofuata. Alizungumza na mtu fulani, sikujua ni nani, lakini kabla ya mchana wa siku iliyofuata nilimpigia simu madam yule kutokea nyumbani kwangu-haikuwa simu iliyosajiliwa.

Madam huyu aliijua vyema kazi yake. Iwapo wasichana wake walishindwa au walikataa kumridhisha mteja, alinituma sehemu nyingine, mara nyingi kwenye nyumba fulani pale Harlem-mahali ambapo huduma iliyohitajika ilitolewa.

Eneo langu la kupokelea wateja lilikuwa nje ya hoteli ya Astor. Eneo moja lenye pilika nyingi sana kwenye makutano ya mtaa wa 45 na Broadway. Nilitumwa na madam kuwa eneo hilo muda fulani. Muda wa miadi ulizingatiwa sana. Niliweza kutambua magari ya wateja mara moja kabla hata hayajapunguza mwendo—ndani yalikuwa na wazungu wenye wasiwasi, wakichungulia nje kumtafuta mtu mrefu, mwenye rangi nyeupe hivi, ambaye amevalia suti nyeusi au koti la mvua, huku akiwa kaweka ua jeupe kwenye kola.

Kama walikuwa kwenye gari binafsi, nilikuwa nashika usukani na kuwaendesha hadi tuendako. Lakini kama walikuwa kwenye taxi, nilimwambia dereva atupeleke ukumbi wa Apollo maana taxi kadhaa za New York zilikuwa zikiendeshwa na polisi. Tukifika ukumbi wa Apollo tulichukua taxi nyingine iliyoendeshwa na mtu mweusi, huyo ndiye alitupeleka tuendako.

Mara tu nilipokamilisha zoezi hilo nilimpigia simu madam. Mara nyingi aliniambia nichukue taxi na kuwahi kwenye makutano ya mtaa wa 45 na Broadway kumpokea mteja mwingine muda fulani. Wateja walijali sana muda. Ni mara chache sana nilisubiria mteja kwa zaidi ya dakika tano. Nilipokuwa pale nilijizungusha zungusha ili polisi wasinitilie shaka.

Bakshishi ilikuwa nzuri sana. Wakati mwingine nilipata hadi zaidi ya dola mia moja kwa usiku mmoja baada ya kuelekeza wateja kama kumi kwenda kuona kila kitu, kufanya na kufanyiwa chochote walichotaka. Sikuwa nawafahamu wateja wangu wengi, niliwatambua wachache tu baada ya kusikia majina yao. Leo hii jambo lile linanikumbusha kesi ya John Profumo. Waingereza hawatofautiani sana na Wamarekani linapokuja suala la tama za ngono za ajabu-ajabu.

Wateja walikuwa ni matajiri, watu wa umri wa kati na kuendelea; watu waliopita ujana tayari; hawakuwa wanafunzi wa vyuo—walikuwa ni baba zao, na pengine babu zao. Watu wanaoheshimika kwenye jamii, wanasiasa wakubwa. Matajiri wakubwa. Marafiki wa wakubwa kutoka nje ya mji. Viongozi wakubwa wa jiji. Wataalamu wa kila aina. Wasanii maarufu. Waigizaji wakubwa kutoka Hollywood na bila kusahau mabosi wa makundi ya kihalifu.

Harlem ndiyo ilikuwa pango lao la kufanyia dhambi. Walijiachia katikati ya watu weusi. Walivua vinyago walivyovaa wanapokuwa kwenye jamii ya wazungu. Hawa walikuwa ni watu waliomudu kutumia pesa nyingi kwa ajili ya masaa matatu au manne ya kutimiziwa tamaa zao za ajabu.

Kwenye ulimwengu huu mchanganyiko hakuna aliyemhukumu mteja. Chochote walichosema wanataka na chochote walichowaza, walifanya na kufanyiwa, ilimradi tu walilipa.

Kwenye kesi ya Profumo huko Uingereza, rafiki wa Christina Keeler alidai kuwa baadhi ya wateja wake walikuwa wanaomba kuchapwa mijeledi. Sehemu ambayo niliwapeleka wateja wengi kutoka kwa madam kwenda kwenye nyumba ambazo zilitoa kila huduma, ilikuwa ni kwenye nyumba moja ya msichana mmoja mkubwa na mweusi ti, alikuwa na nguvu kama ng’ombe dume, misuli kama kuli wa bandarini. Kitu cha kushangaza ni kuwa wengi wa wanaume hawa wa kizungu walikuwa kwenye miaka ya sitini na wengine labda sabini. Wakiwa wamepiga magoti, wakilia na kubembeleza-wasiendelee kupigwa mijeledi na mwanamke yule mkubwa. Wengine walinilipa pesa zaidi ili niwatazame wanapokuwa wanatandikwa. Binti yule alikuwa anapaka mwili wake wote mafuta kiasi kwamba uling’aa na kuonekana mweusi zaidi. Alikuwa akitumia mijeledi midogo iliyokuwa na vinundu, hadi aliwatoa damu. Alikuwa anatengeneza pesa za kutosha kutoka kwa wazee wale wa kizungu.

Sitasema mambo yote niliyoona. Baadaye nilipokuwa gerezani nilikuwa natafakari jinsi ambavyo wanasaikolojia watayaona mambo yale. Wengi wa wanaume hawa walikuwa wameshika nafasi nyeti katika jamii; walikuwa ni watu wenye mamlaka na viongozi wa watu. Pia niliona jambo jingine. Kama tu ambavyo wazungu wale walivyoonyesha kupenda wanawake weusi ti, madam naye, kwa kulijua hilo—nyumbani kwake aliweka wanawake weusi hasa.

Katika maisha yangu yote ya Harlem sikuwahi kuona mzungu akichukua kahaba wa kizungu. Kulikuwa na wanawake wa kizungu kwenye madanguro haya maalumu. Lakini mara nyingi walifanya kazi pale mteja alipotaka kuona mwanaume mweusi akifanya ngono na mwanamke wa kizungu. Jambo hili lilipendwa sana. Najiuliza iwapo hii ilikuwa ni kwa sababu wanaume wa kizungu walitaka kushuhudia suala la ngono waliloliogopa sana? Mara chache nilihudhuria ngono za namna hii ambapo kulikuwa na wanawake wa kizungu walioletwa na wanaume wao kushuhudia. Sikuwahi kupokea wanawake wa kizungu zaidi ya nyakati kama hizi au pale walipounganishwa kwangu na madam fulani wa kizungu ambaye alikuwa ni msagaji. Huyu naye alitoa huduma zake maalumu.

Msagaji huyu alikuwa ni mwanamke mzuri wa kizungu. Maneno yake yote yalikuwa ni matusi. Alikuwa akiwakuwadia wanaume weusi kwa wanawake matajiri wa kizungu.

Mara nyingi nilimuona msagaji huyu akiwa na mpenzi wake, mwanamke wa kizungu mwenye nywele za rangi ya dhahabu. Wakinywa na kuzungumza kwenye baa, mara zote wakiwa pamoja na vijana weusi. Hakuna ambaye angeweza kuhisi kuwa msagaji huyu alikuwa mawindoni. Siku moja niliwapati bangi yeye na msichana wake, walisema kuwa hwajawahi vuta bangi bora kama ile. Walikuwa wakiishi hotelini huko mjini-kati. Mara kwa mara walikuwa wakinipigia nami niliwapelekea bangi na tukawa tunazungumza.

Alinisimulia jinsi alivyoingia kwenye kazi yake bila kutarajia. Akiwa kama mwenyeji wa Harlem, alikuwa anafahamiana na wanaume weusi wa Harlem waliotaka wanawake wa kizungu. Kazi yake ikabadilika baada ya kusikia mara kwa mara wanawake matajiri wa kizungu wakizungumza ndani ya saluni aliyokuwa akifanya kazi huko East Side. Baada ya kuwasikia wakilalamika kutoridhishwa na wenzi wao, aliwaambia kuhusu aliyosikia juu ya wanaume weusi. Baada ya kuona shauku ya baadhi ya wanawake, aliwafanyia mipango wakutane na wanaume weusi wa Harlem alioishi nao kwenye jengo moja.

Baadaye alikodi nyumba tatu huko Harlem ya kati. Huko wateja wake walikutana na wanaume weusi kwa miadi. Wateja wake nao waliwaeleza rafiki zao kuhusu huduma yake. Mwishowe aliachana na kazi ya saluni na kuanzisha ofisi ya kupeleka mizigo majumbani na maofisini kama geresha. Biashara zake zote alifanya kwa njia ya simu.

Pia alikuwa amesoma rangi ambayo wateja wake wanapenda. Siku moja aliniambia kwa utani, aliniambia kuwa hata ikitokea dharura hawezi kunichukua kama mbadala kwa sababu nilikuwa mweupe sana. Aliniambia kuwa karibu kila mteja wake alipendelea mwanaume mweusi. Wakati mwingine walisema kuwa wanataka mweusi wa kweli, yaani si wa kahawia wala mwekundu.

Dada yule alifikiria kuanzisha biashara ya kupeleka mizigo kama geresha kwa sababu baadhi ya wateja wake walihitaji wanaume wawafuate majumbani mwao. Wanawake hawa waliishi kwenye maeneo ya kitajiri, kwenye yale majengo ambayo walinzi wa mlangoni walivaa kama majemedari wa jeshi. Wazungu hawakuwazia kabisa kumtilia mashaka messenger mweusi. Mlinzi alipiga simu na kuambiwa amruhusu messenger mweusi aingie kupeleka “mzig,” kwa wanawake wale matajiri. Cha kushangaza ni kuwa wanawake wale wa kizungu waliwaheshimu wanaume wale weusi kuliko jinsi ambavyo wanaume wa kizungu waliheshimu wanawake weusi, wanawake waliowatumia tokea enzi za utumwa. Mwishowe watu weusi hawakuwaheshimu kabisa wazungu waliolala nao. nafahamu hilo vyema kutokana na jinsi nilivyohisi juu ya Sophia ambaye bado aliendelea kuja New York kila nilipomhitaji.

Christina Keeler wa kashfa ya Profumo alikuwa na mpenzi mwenye asili ya visiwa vya Karibeani aliyeitwa Lucky Gordon. Pengine Lucky Gordon alihisi namna hiyo pia. Baada ya viongozi wa Uingereza kuwatumia mabinti wale wa kizungu—mabinti wale ili kuridhika, walienda kwa wanaume weusi. Huko walivuta bangi na kuwadhihaki watu wazito wa Uingereza kama wapumbavu. Sina shaka kuwa Lucky Gordon aliwafahamu baadhi yao. Iwapo Gordon angesema yote aliyoambiwa na wasichana wale, angezua kashfa nyingine ndani ya Uingereza.

Kitu hichohicho kinatokea ndani ya Marekani kwa baadhi ya wazungu wa daraja la juu. Miaka ishirini iliyopita niliwaona kila usiku kwa macho yangu mwenyewe, niliwasikia kwa masikio yangu mwenyewe.

Mzungu mnafiki anaongea kuhusu maadili mapotovu ya watu weusi, lakini ni nani hasa ana maadili mabovu zaidi duniani kama si mzungu? Na kwa kuongezea, ni mzungu wa “daraja la juu.” Hivi karibuni taarifa ya kina imechapishwa ikihusu kundi la wake na mama wa kizungu kutoka maeneo ya watu wa daraja la kati waliofanya kazi kama makahaba. Na kwenye visa fulani wanawake hawa walifanya ukahaba huo kwa ruhusa au ushirikiano wa waume wao, hata baadhi ya wanaume hao walibaki nyumbani kuhudumia watoto. Na kulingana na gazeti moja maarufu la jijini New York: “Kuna vitabu vyenye majina 200 ya wanaume waliokuwa wateja wao, wengi wao wakiwa wafanyabiashara na wanasiasa wakubwa. Vitabu hivyo vilikamatwa kwenye msako uliofanyika usiku wa Ijumaa iliyopita.”

Na pia hivi karibuni nimesoma habari kuhusu….waume zao waliweka funguo za nyumba zao ndani ya kofia, kisha wanaume hao mmoja mmoja, akiwa amefumbwa macho; alichagua funguo ndani ya kofia hiyo. Usiku huo alienda kulala kwa mwanamke ambaye alipata funguo ya nyumba yake. Sijawahi kusikia jambo kama hilo likifanywa na watu weusi, hata watu weusi wanaoishi kwenye maeneo ya hovyo kabisa.

Alfajiri moja huko Harlem, mwanaume mmoja wa kinegro, mrefu, mweupe, akiwa amevalia kofia na na kitambaa cha kujificha uso, aliwashikia silaha na kuwapora pesa mhudumu wa kaunta na meneja wake walipokuwa wakihesabu mauzo ya usiku. Kama zilivyokuwa baa nyingi za Harlem, mtu mweusi ndiye alikuwa msimamizi lakini hasa zilimilikiwa na Myahudi. Ili kupata leseni ya vileo ilitakiwa kufahamiana na mtu fulani kwenye mamlaka ya vileo ya jimbo, na Wayahudi walionekana wana watu kwenye mamlaka hiyo. Meneja yule aliajiri wahuni weusi kwenda kumuwinda jambazi yule. Maelezo ya jinsi jambazi yule alivyo yalifanya wanihusishe na mimi kati ya watu waliohisiwa. Kulipopambazuka siku hiyo wakafika nyumbani kwangu na kufungua mlango kwa teke.

Niliwaambia kuwa sijui chochote kuhusu tukio hilo na wala sihusiki kwa vyovyote. Niliwaambia nilikuwa kwenye kazi yangu ya kupokea na kuelekeza wateja hadi karibu na saa kumi za alfajiri, na hapo nikaja moja kwa moja nyumbani kulala.

Mabaunsa wale walikuwa wananipiga tu mkwara. Walikuwa wanajaribu kumtoa mtu aliyehusika mafichoni. Bado kulikuwa na watu wengine waliowashuku—hicho ndicho kilichoniokoa.

Nilivaa nguo harakaharaka, nilichukua taxi na kuwaamsha watu wengine wawili-Madam na Sammy. Nilikuwa na pesa kiasi lakini Madam aliniongezea, nilimwambia Sammy kuwa nilikuwa naenda kumtembelea ndugu yangu Philbert huko Michigan. Nilimpatia Sammy anuani ili aweze kunijulisha mambo yatakapotulia. Huu ndiyo wakati wa baridi kule Michigan ambao nilipaka nywele zangu dawa na kuja kugundua kuwa maji yameganda ndani ya bomba na hayatoki, ili kuepuka kichwa change kuungua ilinibidi kutumbukiza kichwa chooni na kuflashi mara kadhaa ili kusuuza dawa.

Niliishi kwenye baraidi kali la Michigan kwa kama juma moja kabla ujumbe wa Sammy haujaja. Kuna mtu alikuwa amekiri kufanya uhalifu ule hivyo ningeweza kurejea Harlem.

Lakini niliporudi sikuendelea kazi yangu ya kuongoza wateja. Sijui sababu ilikuwa nini hasa. Nahisi nilionelea nikae mbali na uchakarikaji kwa muda, na kwenda club usiku na kulewa madawa na rafiki zangu. Sikurudia tena kazi ya kwa madam.

Nakumbuka ni wakati huu pia ndipo nilipoanza kuwa mgonjwamgonjwa. Nilisumbuliwa na mafua kila mara. Muda wote nikivuta pua, usiku na mchana. Nilikuwa nimelewa muda wote kiasi kwamba ni kama niliishi dunia ya ndotoni. Wakati mwingine nilikuwa nikivuta kasumba(Opium) na marafiki na rafiki zangu wa kizungu kutoka mjini-kati, wengi wao wakiwa waigizaji. Kipindi hicho nilivuta bangi kwa wingi kuliko wakati wakati mwingine wowote. Sikuvuta misokoto ya kawaida yenye ukubwa wa njiti, sasa nilivuta misokoto mikubwa.

***
 
Sura ya saba inaendelea
Baada ya muda nikapata kazi kwa Myahudi mmoja aliyekuwa akiitwa Hymie huko mjini-kati. Alinipenda kwa sababu kuna kitu nilikuwa nimemfanyia. Alikuwa akinunua migahawa na baa zilizochoka na kuzikarabati, kisha alifanya uzinduzi mkubwa kwa mataa na mabango. Sehemu hiyo iliyojaa huku nje ikiwa na bango lililosomeka “Chini ya uongozi mpya” ilivutia watu wengi, hasa Wayahudi wenzake waliokuwa wanatafuta sehemu ya kuwekeza pesa zao. Baada ya hapo Hymie aliiuza sehemu hiyo kwa faida, wakati mwingine ndani ya juma moja tu toka aifungue.

Hymie alinipenda nami pia nilimpenda. Alipenda kuongea. Nilipenda kusikiliza. Nusu ya maongezi yake yalikuwa juu ya Wayahudi na watu Weusi. Hymie aliwachukia sana Wayahudi waliochukua majina ya kizungu, huku akitaja majina ya watu kadhaa aliowashutumu kufanya hivyo. Baadhi yao walikuwa ni watu maarufu ambao watu wengi hawakuwahi kudhani kuwa ni Wayahudi. “Red mimi ni Myahudi nawe ni Mweusi. Wazungu wanatuchukia sote. Kama Myahudi asingekuwa na akili kumshinda mzungu, angetendewa vibaya kuliko hata watu wako.”

Hymie alinilipa pesa nzuri kipindi chote nilichomfanyia kazi, nyakati nyingine dola mia mbili hadi mia tatu kwa juma. Nilikuwa tayari kumfanyia Hymie jambo lolote. Na nilimfanyia mambo mengi, lakini kazi yangu kubwa ilikuwa ni kusafirisha pombe za magendo alizouza, mara nyingi kwenda kwenye zile baa alizowauzia watu.

Nikiwa na mtu mwingine, tulienda kwa gari hadi Long Island ambako kulikuwa na kiwanda kikubwa cha wiski za magendo. Tulienda na maboksi kadhaa ya chupa tupu za wiski. Tulinunua madumu ya kama lita ishirini ya wiski na kuijaza kwenye zile chupa, kisha tukazisambaza kulingana na maelezo ya Hymie.

Watu wengi wanaojidai kuwa wanakunywa pombe ya aina fulani tu, hawawezi kugundua tofauti ya pombe hiyo na wiski iliyoivishwa kwa juma moja kwenye kiwanda haramu huko Long Island. Wanywa wiski wengi wa kawaida hawawezi kugundua brand zao. Pia, kwa ruhusa ya Hymie nilikuwa nachukua wiski kidogo na kuzisambazia baa kubwa kadhaa za Harlem na baa chache za uchochoroni ambazo zilibaki.

Lakini siku moja huko Long Island lilitokea jambo lililohusisha watu wa mamlaka ya vileo. Moja ya kashfa kubwa iliyokuwa inavuma wakati huo ilikuwa ni juu ya rushwa ndani ya mamlaka ya vileo. Kukawa na tetesi juu ya kuwepo kwa shushushu ndani ya genge la Hymie. Siku moja Hymie hakutokea mahali aliponiambia tutakutana. Tokea hapo sijawahi kumsikia tena . . . nilikuja kusikia kuwa alipelekwa baharini na nilifahamu vema kuwa hajui kuogelea.

Siku moja huko Bronx, mnegro mmoja aliwavamia waitaliano waliokuwa wakicheza kamari. Nilipata habari kuwa, mtu aliyefanya hivyo-mbali ya kuwa mpumbavu—alikuwa ni mrefu, mweupe, na usoni alijiziba kwa kitambaa. Mara zote nilikuwa najiuliza iwapo uporaji uliotokea kwenye baa ile ulishughulikiwa kweli. Iwapo labda mtu asiyehusika alikiri tu kosa baada ya kipigo. Basi kushukiwa kwangu wakati ule kulifanya nishukiwe tena.

Nilikuwa tu ndiyo nimeingia kwenye kibanda cha simu huko kwenye baa ya Fat Man’s, maeneo ya karibu na viwanja vya polo. Kila mtu kwenye baa ile na Harlem nzima alikuwa akinywa kufurahia habari njema za mmiliki wa timu ya Brookyln Dodgers, Branch Rickey, kumsaini Jackie Robinson kucheza ligi kuu ya baseball.

Mchana ule nilikuwa nimechukua ushindi wangu kwa West Indian Archie baada ya kucheza senti hamsini; alikuwa amenilipa dola mia tatu kutoka mfukoni mwake. Nilikuwa nampigia simu Jean Parks. Jean Parks alikuwa mmoja wa wanawake warembo sana kuwahi kuishi Harlem. Kuna wakati amewahi kuimba na Sarah Vaughan. Kwa muda mrefu tulikuwa tumeahidiana na Jean kuwa tutatoka na kusherekea pamoja iwapo mmoja wetu atashinda kwenye kamari. Tokea mara ya mwisho niliposhinda, Jean alikuwa ameshinda na kunitoa mara mbili. Tulicheka na kusema walau sasa na mimi nitapata nafasi ya kumtoa. Tulipanga kwenda kwenye club ya usiku iliyokuwa mtaa wa 52 kumsikiliza Billie Holiday akitumbuiza.

Nilipokuwa nakata simu niliwaona waitaliano wawili waliojazia wakiniangalia. Sikuhitaji kufikiria mara mbili. Sikuwa na bunduki. Boksi la sigara ndiyo kitu pekee kilichokuwamo mfukoni mwangu. Nilijifanya naingiza mkono mfukoni ili kuwatisha lakini mmoja wao alifungua mlango kwa nguvu.

“Njoo nje tuzungumze,” alisema mmoja wao.

Hapo hapo polisi alitoka nje ya baa na wahuni wale wakatokomea. Maishani mwangu sijawahi furahia kumuona polisi kama siku ile. Nilikuwa natetemeka hata nilipofika nyumbani kwa Sammy, Sammy aliniambia kuwa muda si mrefu West Indian Archie alifika kuniulizia.

Wakati mwingine nikikumbuka yote haya huwa sielewi imekuwajekuwaje nipo hai leo kuweza kuyasimulia. Wanasema kuwa Mungu huwalinda watoto na wapumbavu. Mara nyingi nimefikiria kuwa Allah alikuwa akinilinda. Kwenye kipindi chote hicho cha maisha yangu nilikuwa nimekufa kabisa kiakili. Ni kuwa tu sikujua kuwa nimekufa.

Ili kupoteza muda, tulivuta cocaine na Sammy mpaka wakati wa kwenda kumchukua Jean Parks ulipofika na kwenda kumsikiliza Lady Day huko mjini-kati. Wakati huo sikuelewa kwa nini West Indian Archie alikuwa akinitafuta.

Mwisho wa sura ya saba
 
Back
Top Bottom