Kitabu: Maisha ya Malcom X

Sura ya 17
MECCA
Hija ya Mecca ni takwa la kidini ambalo kila Muislamu, iwapo anaweza, anatakiwa alitimize walau mara moja katika maisha yake.
Quran Takatifu inasema kuwa “Hija ya Kaaba ni jukumu ambao binadamu anadaiwa na Mungu; wale wanaoweza wafanye safari.”
Allah anasema: “Natangaza hija kwa watu; watakuja kwako kwa miguu, juu ya ngamia, watakuja kutoka mabonde yote marefu.”
Kwenye vyuo kadhaa, ilitokea baada ya hotuba na tukiwa tumekusanyika kwa maongezi, nilifuatwa na watu kadhaa weupe weupe hivi. Walijitambulisha kuwa wao ni Waarabu na Waislamu kutoka Mashariki ya Kati au Afrika Kaskazini, na wapo Marekani kwa matembezi, kwa masomo au wanaishi hapa. Walisema kuwa, ukiachana na kauli zangu za kuwashutumu wazungu, walihisi kwamba nilikuwa muaminifu katika kujiita kwangu Muislamu, na walihisi kuwa iwapo nitaujua waliouita “Uislamu wa kweli.” “Nitauelewa na kuukubali.” Nikiwa kama mfuasi wa Elijah Muhammad, nilikasirika kila niliposikia hayo.

Lakini nilipokuwa nikitafakari nikiwa mwenyewe baada ya mambo yote yale kutokea, nilianza kujiuliza: kama mtu alikuwa ni mfuasi mzuri wa hiyo dini, kwa nini ajizuie kupata maarifa zaidi kuhusu dini hiyo?

Siku moja katika maongezi niligusia hili kwa Wallace Muhammad, mtoto wa Elijah Muhammad. Alisema ndiyo, hakuna shaka kuwa Muislamu anatakiwa kujifunza Uislamu kadri ya uwezo wake. Siku zote niliyaheshimu sana maoni ya Wallace Muhammad.

Wale Waislamu halisi niliokutana nao, kila mmoja wao alinihimiza kuonana na kuongea na Dr. Mahmoud Youssef Shawarbi. Niliambiwa kuwa ni msomi mkubwa wa dini ya Kiislamu. Mhitimu wa Chuo Kikuu cha Cairo, akipata shahada yake ya uzamivu kutoka Chuo Kikuu cha London., mhadhiri wa Kiislamu, mshauri wa Umoja wa Mataifa na muandishi wa vitabu vingi. Alikuwa ni profesa kamili katika Chuo kikuu cha Cairo, na atakuja likizo New York na kuwa kama mkurugenzi wa Shirikisho la Taasisi za Kiislamu katika Marekani na Kanada(F.I.A). mara kadhaa nilipokuwa nikiendesha maeneo ambayo kulikuwa na makao makuu ya F.I.A, nilizuia shauku ya kutaka kuingia kwenye jengo lao, lakini siku moja muuza magazeti Fulani alinitambulisha kwa Dr. Shawarbi.

Alikuwa mwenye urafiki sana. Alisema kuwa huwa ananifuatilia kwenye vyombo vya habari. Nilimjulisha kuwa niliambiwa kumhusu na watu mbalimbali. Basi tukazungumza kwa kama dakika kumi na tano hadi ishirini hivi. Sote tulikuwa na mihadi ya kwenda sehemu Fulani.
Kabla ya kuachana aliniambia jambo fulani ambalo halijawahi kunitoka kichwani. Alisema, “Hakuna mwenye imani kamili mpaka pale atakapotamani yampate ndugu yake yale anayotamani yampate yeye mwenyewe.”
Turudi kwa dada yangu Ella. Sikuweza kutoa akilini mwangu kile alichonifanyia. Nimekwisha sema alikuwa ni mwanamke mweusi shupavu kutoka Georgia. Msimamo wake na ukichwa ngumu wake vilisababisha atengwe kutoka Msikiti Namba Kumi na Moja wa Boston; walimrudisha lakini baadaye akaondoka mwenyewe. Akaanza kujifunza na Waislamu asilia, kisha akaanzisha shule ambayo ilifundisha na Kiarabu! Yeye mwenyewe hakuweza kukiongea, aliajiri waalimu wa kukifundisha. Huyo ndiye Ella! Alikuwa anafanya biashara ya majengo na alikuwa akitunza pesa kwa ajili ya hija. Karibu kila siku usiku tulikaa na kuzungumza; aliniambia kuwa suala hilo halina mjadala. Ni muhimu sana nikienda mimi hija. Wakati wote wa kurudi New York nilikuwa nikimfikiria Ella. Mwanamke shupavu sana. Amevunja ushupavu wa wanaume watatu, akiwa mshupavu kuliko wote watatu wakiwekwa pamoja. Alikuwa na nafasi muhimu sana maishani mwangu. Zaidi yake hakukuwa na mwanamke mwenye nguvu za kutosha kuniongoza; mimi ndiye niliongoza wanawake. Nilimvuta Ella kwenye Uislamu, na sasa alikuwa akigharamia safari yangu ya Mecca.

Sikuzote ukiwa pamoja na Allah, basi naye atakupa ishara kuwa yupo pamoja nawe.

Nilipoenda kuomba visa kwenye ubalozi wa Saudi Arabia, balozi wa Saudi Arabia aliniambia kuwa hakuna Muislamu aliyesilimu akiwa Marekani anayeweza kupata visa ya hija bila ya kupata saini ya kukubaliwa na Dr. Mahmoud Shawarbi. Huo ulikuwa ni mwanzo tu wa ishara kutoka kwa Allah. Nilipompigia simu Dr. Shawarbi, alishangaa sana. “Nilikuwa ndiyo najiandaa kukutafuta,” alisema, “Karibu uje.”

Nilipofika ofisini kwake, Dr. Shawarbi alinipatia barua iliyosainiwa ya kunikubalia kwenda hija, na kisha akanipatia nakala ya kitabu. Kilikuwa ni kitabu kilichoitwa The Eternal Message of Muhammad kilichoandikwa na Abd-Al-Rahman Azzam.

Dr. Shawarbi alisema kuwa mwandishi alikuwa ametuma nakala hiyo kwa ajili yangu. Aliendelea kunieleza kuwa mwandishi ni raia wa Saudi Arabia aliyezaliwa Misri, mwanadiplomasia mashuhuri na mmoja wa washauri wa karibu wa Mwanamfalme Faisal, mtawala wa Saudi Arabia. “Amekufuatilia sana kupitia vyombo vya habari.” Iliniwia vigumu sana kuamini.

Dr. Shawarbi alinipa namba ya mwanaye aliyeitwa Muhammad Shawarbi, alikuwa ni mwanafunzi huko Cairo, akanipatia na namba ya mwandishi wa kitabu kile, Omar Azzam ambaye aliishi huko Jedda, “Jitahidi uwapigie wote ukifika kituo cha mwisho kabla ya Mecca.”

Niliondoka New York kimyakimya(Sikujua kabisa kuwa kurudi kwangu kutakuwa kwa makelele sana). Ni watu wachache tu waliambiwa kuwa ninasafari. Sikutaka watu wa usalama au wengine wowote waniwekee vizuizi dakika za mwisho. Waliokuja kuniaga uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kennedy walikuwa ni mke wangu Betty, mabinti zangu watatu na watu wangu wa karibu wachache. Ndege ya shirika la Lufthansa ilipoacha ardhi, nilisalimiana na majirani niliokaa nao. Ishara nyingine! Wote walikuwa Waislamu. Mmoja alielekea Cairo kama mimi, na mwingine alielekea Jedda ambako ningefika baada ya siku chache. Tuliongea na majirani zangu wale kwa safari nzima hadi Frankfurt, Ujerumani. Tulipokuwa hatuzungumzi nilisoma kitabu nilichopewa. Tulipofika Frankfurt, ndugu aliyeelekea Jedda alituaga sisi tulioelekea Cairo. Tulikuwa na saa kadhaa kabla ya kuruka kuelekea Cairo hivyo nikaamua kutembeatembea kidogo kuiona Frankfurt.

Nilipokuwa maliwatoni pale uwanja wa ndege, nilikutana na Mmarekani wa kwanza aliyenitambua, alikuwa ni mwanafunzi wa kizungu kutoka Rhode Island. Aliniangalia kwa muda kisha akanifuata, “Wewe ni X?” Nilicheka na kumwambia ndiyo, sijawahi kusikia nikiitwa hivyo. “Haiwezekani!” alisema kwa mshangao. Hakuna mtu atakayeniamini nikimwambia hili!” Alisema kuwa alikuwa anasoma huko Ufaransa.

Mimi na yule ndugu yangu Muislamu tulishangazwa sana na urafiki wa watu wa Frankfurt. Tulitembelea maduka mengi, tuliingia kwenye duka na kupokelewa kwa bashasha sana. Ndani ya Marekani unaweza ingia dukani na kutumia dola mia moja na kuondoka na bado ukawa mpita njia tu.
Wote, wewe na muuzaji mnakuwa kama kila mmoja anamfanyia mwenzake hisani. Watu wa Ulaya wanaubinadamu zaidi. Ndugu yangu Muislamu ambaye aliweza kuzungumza Kijerumani kwa kiasi, aliwaeleza kuwa tulikuwa Waislamu, hapo niliona kitu kile kile pale watu waliponichukulia kama Muislamu na si mtu mweusi. Watu wakikuchukulia kama Muislamu wanakuchukulia kama binadamu, na wanakutendea kwa njia tofauti sana.

Tulirudi uwanja wa ndege na kuchukua ndege ya shirika la ndege la United Arab kuelekea Cairo. Watu wengi—bila shaka Waislamu waliokuwa wanaelekea hija, walikuwa wakikumbatiana na kusalimiana kwa bashasha. Walikuwa watu wa rangi na jamii mbalimbali, yalikuwa mazingira ya kirafiki sana. Niliingiwa na hisia kuwa hakukuwa na tatizo la rangi mahali hapa. Nilihisi kama vile mtu aliyetoka tu kutoka gerezani.

Nilimwambia ndugu yangu yule kuwa nilitaka kutalii jiji la Cairo kwa siku kadhaa kabla ya kuelekea Jedda. Alinipa namba yake na kuniambia nimpigie sababu alitaka kuniunganisha na rafiki zake ambao waliweza kuongea Kiingereza na walikuwa wakielekea hija, na kuwa watafurahi kuniongoza.

Basi nilitumia siku mbili za furaha kutalii jiji la Cairo. Nilipendezwa sana na shule za kisasa, nyumba za makazi za umma, barabara kubwa na maendeleo ya viwanda niliyoyaona. Nilikuwa nimesoma na kusikia kuwa Rais Nasser alikuwa amejenga moja ya nchi iliyoendelea zaidi kiviwanda katika Afrika. Jambo lililonishangaza zaidi nikuwa magari na mabasi yalikuwa yakitengenezwa pale pale Cairo.

Nilikuwa na wakati mzuri nilipokutana na mtoto wa Dr. Shawarbi, Muhammad Shawarbi, alikuwa ni kijana wa miaka kumi na tisa, alikuwa akisomea uchumi na sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Cairo. Aliniambia kuwa ndoto ya baba yake ni kujenga Chuo Kikuu cha Kiislamu ndani ya Marekani.

Watu wengi wenye urafiki niliokutana nao walishangaa sana kusikia kuwa nilikuwa Muislamu kutoka Marekani! Moja ya watu hao alikuwa mwanasayansi mmoja wa Misri pamoja na mkewe—nao wakiwa safarini kwenda hija Mecca. Bwana huyo alinisisitiza kwenda pamoja nao kwenye mgahawa uliokuwa eneo moja la Cairo lililoitwa Heliopolis. Walikuwa wenzi wenye akili na maarifa sana. Ukuaji wa kiviwanda wa Misri ilikuwa ndiyo moja ya sababu iliyofanya mataifa ya magharibi yaichukie sana. Mwanasayansi yule aliniambia kwa sababu ilikuwa ikizionyesha nchi zingine za kiafrika yale zinayozipasa kufanya. Mke wake aliniuliza, “Kwa nini watu duniani wanakabiliwa na njaa wakati Marekani inachakula kingi sana cha ziada? Wanakifanyia nini, wanakitupa baharini?” Nilimjibu “Ndiyo, lakini vingine wanaweka kwenye maghala na vyumba vya kutunza baridi na kuviacha huko, kukiwa na watu wa kuvitunza mpaka pale vitakapokuwa havifai tena kuliwa. Kisha watu wengine watakuja na kuvitoa ili kupata nafasi kwa ajili ya vipya.” Aliniangalia akiwa haamini kabisa. Pengine alihisi natania. Lakini walipa kodi wa Marekani wanafahamu kuwa ni kweli.

Lakini sikumwambia kuwa hata Marekani kwenyewe kuna watu wanateseka na njaa.

Nilimpigia simu yule rafiki yangu Muislamu kama alivyoniagiza, kisha nikaonana na rafiki zake waliokuwa wanakwenda hija. Jumla na mimi tulikuwa watu nane, kati yetu walikuwemo jaji na afisa kutoka wizara ya elimu. Waliongea Kiingereza kizuri na walinikubali kama ndugu yao. Niliichukulia hiyo kama ishara nyingine kutoka kwa Allah, kila nilikoenda kulikuwa na mtu aliye tayari kunisaidia na kuniongoza.

***

Maana halisi ya Hajj katika Kiarabu ni kuchukua hatua katika kufanya jambo fulani. Kwenye sheria za Kiislamu, inamaanisha kwenda Kaaba, Nyumba Takatifu, na kutimiza takwa la hija. Uwanja wa ndege wa Cairo ndipo palikuwa mahali ambapo vikundi kadhaa vya Mahujaji vinakuwa Muhrim yaani kuingia katika hali ya Ihram(Kunuia na kujiweka tayari kwa hija na kujitenga na mambo ya dunia). Baada ya kupokea ushauri, niliamua kuacha mizigo yangu yote pale Cairo, ikiwa pamoja na kamera zangu nne, moja ikiwa ya video. Pale Cairo nilinunua mkoba mdogo wa kutosha suti moja, shati, nguo za ndani na jozi za viatu. Kwenye safari ya kwenda airport nilikuwa na wasiwasi sana, nilifahamu kuwa kuanzia hapo itanipaswa kuwaangalia watu wanaofahamu wanachokifanya na kujaribu kuwaiga.

Katika kuingia hali ya Ihram, tulivua nguo zetu na kujifunga mataulo mawili meupe. Moja linaloitwa Izar, lilikuwa la kujifunga kiunoni. Jingine, Rida lilizungushwa shingoni na mabegani na kuacha bega na mkono wa kushoto wazi. Pia kulikuwa na’l , makubadhi ambayo yaliacha kifundo cha mguu wazi. Juu ya fundo la kiunoni la Izar kulikuwa na mkanda wenye mfuko wa pesa, na kwa ajili ya kubebea passport na nyaraka zingine muhimu, kama ile barua niliyopata kutoka kwa Dr. Shawarbi.

Kila mmoja kati ya maelfu ya watu waliokuwepo uwanjani pale wakijianda kwenda Jedda, alivalia namna hii. Unaweza kuwa mfalme au mkulima masikini na mtu yeyote asijue. Baadhi ya watu wakubwa ambao nilionyeshwa kwa siri walikuwa wamevalia kama mimi tu. Mara tu baada ya kuvalia hivi, wote tulianza kuita kwa kupokezana “Labbayka! Labbayka!” (Nakuja kwako Ee Mungu!) Uwanja wa ndege ulijaa sauti kubwa za Muhrim wakitaja nia yao ya kufanya Hija.

Ndege zilizojaa mahujaji zilikuwa zikipaa kila dakika, lakini bado uwanja ukawa umejaa wengine wengi pamoja na ndugu na rafiki zao waliokuja kuwaaga. Wale ambao walikuwa hawaendi walikuwa wakiwaomba wengine wasali wa niaba yao huko Mecca. Tulikuwa tayari ndani ya ndege ndipo nilipotambua kwa mara ya kwanza kuwa hakukuwa na nafasi yangu lakini walikuwa wamefanya mipango na mtu fulani alishushwa sababu hawakutaka kumuangusha Muislamu kutoka Marekani. Nilipatwa na hisia mchanganyiko, dhamira ikinisuta kuwa nilisababisha mtu mwingine ashushwe kwa ajili yangu, na pia nilijihisi mnyenyekevu na mwenye shukrani sana kwamba niliheshimiwa kiasi kile.
Ndani ya ndege kulijaa watu weupe, wa kahawia, wekundu na wamanjano, wenye macho ya bluu, nywele za rangi ya dhahabu na mimi mwenye nywele nyekundu zilizojikunjakunja, wote kama ndugu! Wote tukimtukuza Mungu mmoja, Allah, wote tukiheshimiana.

Kutoka kwa mtu fulani wa kwenye kundi letu, habari zilianza kusambaa kiti hadi kiti kuwa nilikuwa Muislamu kutoka Marekani. Watu walinigeukia na kunisalimu kwa tabasamu. Chakula cha mchana kilipitishwa, tulipokuwa tunakula, habari zilifika chumba cha marubani kuwa ndani ya ndege kulikuwa na Muislamu kutoka Marekani.

Rubani wa ndege alikuja kunisalimu. Alikuwa ni Mmisri, alikuwa na weusi wa ngozi kuliko hata mimi; angeweza kutembea katika mitaa ya Harlem bila mtu hata mmoja kumshangaa. Alifurahi sana kukutana na Muislamu kutoka Marekani. Aliponialika kutembelea chumba cha rubani nilikubali mara moja.

Rubani msaidizi alikuwa ni mweusi kuliko hata yeye. Siwezi kukuelezea jinsi nilivyohisi. Sijawahi kuona mtu mweusi akirusha jeti. Ile paneli iliyojaa vitufe: hakuna mtu anayeweza kuelewa vilimaanisha nini. Marubani wote walijawa na tabasamu, wakinitendea kwa heshima kama nilivyotendewa tokea nitoke Marekani. Nilisimama ndani mle nikiangalia anga juu yetu. Katika Marekani nilipanda ndege mara nyingi pengine kuliko mtu mweusi mwingine yeyote
yule, lakini sijawahi karibishwa kwenye chumba cha marubani. Lakini tazama hapa nimekaa na Waislamu wenzangu wawili, mmoja kutoka Misri na mwingine kutoka Arabia, sote tukielekea Mecca, na mimi nikiwa kule kwenye chumba cha marubani. Ndugu! Nilijua kuwa Allah yuko pamoja nami.

Nilirudi kitini kwangu. Kwa safari nzima ya kama saa moja, mahujaji tulikuwa tukipiga kelele, “Labbayka! Labbayka!” Ndege ikatua uwanja wa ndege wa Jedda, ni mji wa bandari katika bahari ya Shamu. Ni sehemu ambayo mahujaji wote wanaoenda na kurudi kutoka Mecca hupita. Mji wa Mecca upo umbali wa maili arobaini mashariki ya Jedda.
Uwanja wa ndege wa Jedda ulionekana kujaa watu kuliko hata ule wa Cairo. Kikundi chetu kikawa moja tu ya vikundi vingi vya watu kutoka mataifa mbalimbali vilivyokuwa vikipishana pale uwanjani. Kila kikundi kilikuwa kinaelekea kupanga mstari mrefu kwenye ofisi za uhamiaji. Kabla ya kufika ofisi za uhamiaji, kila kikundi cha mahujaji kilipewa mtu aliyeitwa Mutawaf, huyu jukumu lake lilikuwa ni kusafirisha kikundi hicho kwenda Mecca. Baadhi ya mahujaji walikuwa wakipaza sauti wakisema “Labbayka!” wengine, baadhi yao wakiwa vikundi vikubwa, walikuwa wakisema sala kwa pamoja, nitaitafsiri sala hiyo, “Sijisalimishi kwa mwingine yoyote ila wewe. Ee Allah, sijisalimishi kwa mwingine ila wewe. Najisalimisha kwako kwa sababu huna mshirika. Sifa na Baraka zote zinatoka kwako. Nawe upo peke yako katika ufalme wako.” Dhumuni kubwa la sala hiyo ni kukiri Mungu mmoja.

Ni maafisa tu ndiyo hawakuvaa mavazi ya ki-Ihram au kofia nyeupe, kanzu nyeupe na makubadhi waliyovaa Mutawaf, yaani wale waliowaongoza mahujaji. Katika kiarabu neno Mutawaf linamaanisha “Yule anayeongoza” mahujaji kwenda “Tawaf” ambacho ni kitendo cha kuizunguka Kaaba.

Nikiwa katikati ya kikundi chetu, niilisonga kwenye mstari wa kusubiria passport zetu zikaguliwe, nilijawa na wasiwasi. Siamini kuwa nipo kwenye chimbuko la Uislamu, nawapatia passport ya Marekani ambayo inawakilisha kitu tofauti kabisa na kile ambacho Uislamu unakisimamia.

Jaji aliyekuwa kwenye kundi letu alihisi wasiwasi wangu, alinishika begani kunituliza. Upendo, unyenyekevu na undugu wa kweli ulionekana kila nilikogeuka. Mwishowe kundi letu likamfikia karani aliyechunguza passport na mikoba ya mahujaji kwa makini kabla ya kuwaruhusu kusonga mbele.
Nilikuwa na wasiwasi sana kiasi kwamba nilipofungua mkoba wangu kwa ufungua na ukagoma kufunguka, niliufungua kwa nguvu, nikiogopa kuwa wasije hisi kwenye mkoba wangu nina vitu nisivyotakiwa kuwa navyo. Karani akaona kuwa nina passport ya Marekani, aliishika huku akiniangalia, kisha akasema jambo fulani kwa kiarabu. Rafiki zangu niliokuwa nao wakaanza kuongea kwa ajili yangu haraka haraka kwa kiarabu. Jaji, kwa Kiingereza akaniuliza kuhusu barua kutoka kwa Dr. Shawarbi, aliichukua na

kuiweka mezani pa karani. Karani aliisoma na kuirudisha huku akisema kuwa nilitakiwa kusema mapema. Ubishi kunihusu ukaendelea, nilijihisi kama mpumbavu, sikuweza kusema chochote wala kuelewa kilichokuwa kikisemwa.Mwishowe, kwa unyonge, jaji alinigeukia na kusema kuwa nilitakiwa kupitia Mahgama Sharia. Ilikuwa ni mahakama kuu ya Kiislamu. Ilichunguza Waislamu wasio wa kweli waliojaribu kuingia Mecca. Ilikuwa wazi kuwa ni marufuku kabisa kwa asiye Muislamu kuingia Mecca.
Iliwabidi rafiki zangu wandelee kwenda Mecca bila ya mimi. Walionekana kujaa wasiwasi juu yangu. Nami nilijawa na wasiwasi lakini nilipata maneno ya kuwafariji, niliwaambia, “Nitakuwa sawa. Allah ananiongoza.” Walisema kuwa watasali kila saa kwa ajili yangu. Mutawaf woa aliwahimiza kuendelea mbele ili kuondoa msongamano pale uwanja wa ndege. Tulipungiana mkono, nikiwaangalia wakienda zao.
Wakati huo ilikuwa ni kama saa tatu asubuhi, siku ya Ijumaa. Sijawahi kuwa kwenye msongamano wa watu mkubwa kama ule, lakini sijawahi kujihisi mpweke na mnyonge tokea nilipokuwa mtoto. Mbaya zaidi ni kuwa, siku ya Ijumaa kwenye ulimwengu wa Kiislamu ni kama Jumapili kwenye ulimwengu wa Kikristo. Siku ya Ijumaa Waislamu wote hukusanyika kwa ajili ya kusali pamoja. Tukio hilo huitwa yawn al-Jumu’a “siku ya kukusanyika.” Ilimaanisha kuwa hakuna mahakama iliyofanya kazi siku ya Ijumaa. Itanibidi kusubiri hadi Jumamosi.

Afisa mmoja alimwita msaidizi wa Mutawaf. Kwa kiingereza kibovu afisa yule alinielekeza kuwa nitapelekwa eneo ambalo lilikuwepo palepale uwanja wa ndege. Passport yangu ilibaki ofisi za uhamiaji, nilitaka kupinga kwa sababu sheria ya kwanza ya msafiri ni kutoachana na passport yake, lakini sikufanya hivyo. Nikiwa kwenye mataulo na makubadhi, nilimfuata muongozaji yule aliyekuwa amevaa kofia nyeupe, kanzu nyeupe na makubadhi. Nafikiri ilivutia kututazama. Watu tuliopishana nao waliongea kila aina ya lugha. Sikuweza kuongea lugha yoyote nyingine. Nilikuwa kwenye hali mbaya sana.

Nje tu ya uwanja wa ndege kulikuwa na msikiti, na sehemu ya juu ya uwanja wa ndege kulikuwa na jengo kubwa lililokuwa kama bweni. Wakati huo ilikuwa karibu na mapambazuko, ndege zilikuwa bado zinaruka na kutua—taa zao za mkiani zikimulika-mulika anga. Mahujaji kutoka Ghana, Japan, Indonesia, Urusi na kwingineko, walikuwa wakiingia na kutoka kwenye jengo lile la bweni nilikokuwa napelekwa. Sidhani kama kuna kamera ya video imewahi chukua picha ya binadamu wenye pilika pilika kama niliyochukua kwa macho yangu. Tulifika kwenye jengo na kuanza kupanda hadi ghorofa ya nne, ghorofa ya juu kabisa. Njiani tulikutana na watu wa kila aina duniani. Wachina, Waindonesia, waafghanistani. Wengi wao wakiwa bado hawajavaa nguo za ki-Ihram, bado wamevalia mavazi ya kitamaduni ya nchi zao. Ilikuwa kama kuangalia kurasa za jarida la National Geographic.

Tulipofika ghorofa ya nne, muongozaji wangu alinielekeza kwenye chumba changu ambacho kilikuwa na watu wengine kama kumi na tano. Wengi wao wakiwa wamelala kwenye mazulia yao. Niliweza kuona kuwa wengine walikuwa ni wanawake, wakiwa wamejifunika kutoka usoni hadi miguuni. Kulikuwa na Muislamu mmoja mzee na mke wake ambao walikuwa macho. Walinishangaa kistaarabu. Waislamu wawili kutoka Misri na mwingine wa kutoka Iran waliamka wakati wakati muongozaji wangu aliponiingiza ndani. Kwa ishara, alisema kuwa atanionyesha njia sahihi ya kukaa wakati wa kusali. Fikiria kuwa Imam wa Kiislamu, kiongozi katika Taifa la Kiislamu la Elijah Muhammad lakini ukawa hujui taratibu za sala!

Nilijaribu kufanya alivyofanya, nilijua kuwa sikuwa nafanya sahihi. Niliweza kuona macho ya Waislamu wengine yakinitazama. Vifundo vya miguu vya mtu wa Magharibi haviwezi kufanya kile ambacho vifundo vya Muislamu vimekuwa vinafanya maisha yake yote. Watu wa Asia huchuchumaa wanapoketi, watu wa magharibi huketi wima vitini. Muongozaji wangu alipokuwa ameinama, nilijitahidi kila niwezavyo kufanya kama alivyofanya lakini sikuweza. Baada ya kama saa moja muongozaji wangu aliondoka na kuashiria kuwa atarudi baada ya saa moja.
Hata sikuweza kulala. Niliendelea kufanyia mazoezi mkao wa kusali. Nilijizuia kufikiria jinsi nilivyoonekana kituko mbele yao. Baada ya muda kidogo nikawa nimejifunza mbinu ya kuniwezesha kuinama hadi sakafuni, lakini baada ya siku mbili au tatu kifundo changu cha mguu kilikuja kuvimba.

Kulipokucha Waislamu waliamka na walitambua uwepo wangu mara moja, tuliendelea kushangaana huku wakiendelea na shughuli zao. Nilianza kuona jinsi ambavyo zulia ni muhimu sana katika maisha ya Waislamu. Kila mtu alikuwa na zulia dogo, na kila mtu na mkewe au na kundi kubwa, walikuwa na zulia kubwa. Waislamu hawa walisali kwenye mazulia yao mulemule chumbani. Baada ya hapo waliweka kitambaa cha mezani juu ya zulia na kuanza kula, hivyo zulia likawa chumba cha chakula. Baada ya kutoa vyombo na kitambaa cha mezani, waliketi zuliani, likawa sebule. Wanapolilalia linakuwa chumba cha kulala. Kabla ya kuondoka, ikanijia akilini na kuelewa kwa nini mtu yule aliyenunua vitu vya wizi nilipokuwa jambazi kule Boston alilipia pesa nyingi sana kwa ajili ya mazulia ya mashariki. Ni kwa sababu mazulia kutoka nchi ambazo mazulia ni muhimu sana yalishonwa kwa ustadi sana. Baadaye nilipokuwa Mecca, nilijionea umuhimu mwingine wa mazulia. Iwapo mzozo wowote ulitokea, mtu aliyeheshimiwa sana na ambaye hakuhusika na mzozo aliketi kwenye zulia huku wale wanaozozana wakimzunguka, na hilo lilifanya zulia kuwa mahakama. Nyakati nyingine lilikuwa darasa.

Mmoja wa Waislamu kutoka Misri alikuwa akiniangalia sana kwa jicho la wizi. Nilimuangalia na kutabasamu. Aliinuka na kunifuata. “Hel-lo-” alisema, alisikika kama wakati Lincoln anatoa hotuba kwenye makaburi ya Gettysburg. Nilimjibu, “Hello!” Nilimuuliza jina lake, lakini hakuelewa vizuri kiingereza. Nafikiri alikuwa na maneno ishirini tu ya kiingereza. Nilikuwa nasema chochote kilichonijia kichwani. Mwishowe nilisema, “Muhammad Ali Clay-”Waislamu wote waliokuwa wakisikiliza walinga’aa kwa shangwe kama mti wa Krismasi. “Ni wewe? Ni wewe?” alisema rafiki yangu akinionyeshea kidole. Nilitingisha kichwa na kusema, “Hapana, hapana, Muhammad Ali ni rafiki yangu!” Baadhi walielewa kiasi, wengine hawakuelewa kabisa na hivyo ndivyo ilivyoanza kusambaa kuwa nilikuwa Cassius Clay, bingwa wa ndondi wa uzito wa juu duniani. Baadaye nilikuja kufahamu kuwa karibu kila mwanaume, mwanamke na mtoto wa Kiislamu alikuwa amesikia jinsi ambavyo Sonny Liston(Mtu ambaye kwa Waislamu alikuwa kama zimwi mla watu) alipigwa na Cassius Clay kama vile Daudi alivyompiga Goliati, Cassius ambaye baadaye aliutangazia ulimwengu kuwa jina lake ni Muhammad Ali na dini yake ni Uislamu na Allah ndiye aliyempa ushindi.

Kuanza kuwasiliana kulisaidia sana. Kuwa kwangu Muislamu kutoka Marekani, kulibadili mtazamo wao, kutoka kuniangalia tu hadi kutaka kunisaidia. Sasa wengi wakaanza kutabasamu. Walikuja karibu na, walinitazama juu hadi chini-kistaarabu. Nilikuwa kama mtu kutoka sayari ya Mirihi.

Yule msaidizi wa Mutawaf alirudi na kuonyesha ishara kuwa nimfuate. Alionyeshea Msikiti ulikokuwa na nikafahamu kuwa alikuja kunichukua kwa ajili ya sala ya alfajiri, El Sobh iliyofanyika kabla ya jua kuchomoza.

Nilimfuata na njiani tulikutana na maelfu ya mahujaji, wakiongea lugha mbalimbali isipokuwa Kiingereza. Nilijichukia kwa kutojifunza taratibu halisi za sala kabla ya kuondoka Marekani. Kwenye Taifa la Kiislamu la Elijah Muhammad hatukuwahi kusali kwa Kiarabu. Miaka kadhaa nyuma, nilipokuwa gerezani, Muislamu mmoja asilia kutoka Boston aliyeitwa Abdul Hameed, alinitembelea na baadaye akanitumia sala zikiwa katika kiarabu. Wakati huo nilijifunza sala zile. Lakini sikuwahi kuzitumia tena.

Niliamua akilini kuwa nitamuacha muongozaji wangu afanye kila kitu kwanza nami nitamuangalia. Haikuwa kazi ngumu kumfanya aanze kufanya kwanza, alikuwa na shauku ya kunionyesha. Nje ya msikiti kulikuwa na mabomba yamejipanga. Udhu ulifanyika kabla ya sala. Hilo nililifahamu. Lakini hata baada ya kumuangalia sikuweza kufanya kwa usahihi. Kulikuwa na njia sahihi ya kujiosha, na kufanya kwa njia sahihi ilikuwa muhimu sana.

Nilimfuata kuelekea msikitini, nyuma yake nikimuangalia kwa makini. Aliinama, kichwa chake kikagusa chini. Nami nikafanya hivyo. “Bi-smi-llahi-r-Rahmain-r-Rahim-” (“Kwa jina la Allah, mwenye kuruzuku na mwenye rehema”) sala zote za Waislamu huanza hivyo. Baada ya hapo nadhani nilikuwa nasema vitu visivyo sahihi, lakini niliendelea kusema.

Si nia yangu jambo hili lionekane kama mzaha. Kwangu haukuwa mzaha hata kidogo. Hakuna ambaye alikuwa karibu ambaye angeweza kusema kuwa nilikuwa sisemi yale waliyokuwa wanasema wengine.

***

Baada ya sala hiyo, muongozaji wangu alinipeleka hadi kwenye makazi yangu. Kwa ishara, aliniambia kuwa atarudi baada ya saa tatu, kisha akaondoka.

Sehemu tuliyokuwa ilituwezesha kuona eneo la uwanja wa ndege vizuri sana. Nilisimama kwenye kibaraza nikiangalia. Ndege zilikuwa zinaruka na kutua bila kupumzika. Maelfu elfu ya watu kutoka kote duniani walipita huku na kule. Niliona vikundi vilivyokuwa vinaelekea Mecca kwa mabasi na magari madogo. Niliona wengine walioamua kutembea maili zile arobaini. Nilitamani name ningeanza kutembea. Walau hilo nilijua jinsi ya kulifanya.

Nilikuwa naogopa hata kufikiri yatakayotokea. Je nitakataliwa kuingia Mecca kuhiji? Niliwaza maswali ya kunipima yatakuwaje na muda gani nitafika mbele ya Mahakama Kuu ya Kiislamu.

Yule Muislamu kutoka Iran alinifuata. Alinisalimu kwa kusita kidogo, “Mmare . . . Mmarekani?” alionyesha ishara kuwa anataka niende kujumuika naye na mkewe kwenye kupata kifungua kinywa, kwenye zulia lao. Nilifahamu kuwa ni ukarimu mkubwa sana alikuwa akinifanyia. Haunywi chai na Muislamu pamoja na mkewe kirahisirahisi. Sidhani kama Muiran yule alinielewa nilipotingisha kichwa na kutabasamu, nikimaanisha “Hapana, ahsante.” Hata hivyo aliniletea chai na biskuti. Mpaka wakati ule nilikuwa sina kabisa wazo la kula.

Wengine walifika na kunisalimu kwa ishara ya kichwa huku wakitabasamu. Rafiki yangu wa kwanza, yule aliyeongea kiingereza kidogo alikuwa amekwishaondoka. Nilikuwa sifahamu kinachoendelea, lakini alikuwa amesambaza taarifa kuwa kwenye ghorofa ya nne kulikuwa na Muislamu kutoka Marekani. Msongamano wa watu ukaanza kupita kuelekea kwenye makazi yetu. Waislamu wakiwa wamevalia mavazi ya ki-Ihram, na wengine wakiwa bado wamevaa mavazi yao ya kitamaduni, walinipita polepole huku wakitabasamu. Jambo hilo liliendelea kwa muda mrefu niliokuwepo eneo lile. Lakini sikufahamu kuwa mimi ndiye nilikuwa kivutio.

Siku zote nimekuwa mtu asiye na utulivu na mwenye wasiwasi. Maidizi wa Mutawaf hakurudi baada ya saa tatu kama alivyokuwa amesema na hilo lilinifanya niingiwe na wasiwasi. Niliogopa kuwa atakuwa ameamua kuachana na mimi kwa kuona kuwa siwezi kusaidika. Na wakati huo njaa nayo ilianza kunibana. Waislamu wote katika chumba chetu walikuwa wamenikaribisha chakula nami nilikataa. Naomba nikiri kuwa tatizo ni sikudhani kama nitaendana na namna yao ya ulaji. Kila kitu kiliwekwa kwenye poti moja juu ya zulia lililokuwa chumba cha chakula, na niliona wote wakila humo kwa kutumia mikono yao.

Niliendelea kusimama kibarazani pale nikiangalia uwanja wa ndege kule chini, mwishowe nikaamua nitembee-tembee kidogo. Nilishuka chini mpaka kwenye ua, nilionelea kuwa nisiende mbali, mtu anaweza kuja kunitafuta. Basi nikarudi chumbani kwetu. Baada ya kama dakika arobaini na tano nikashuka tena chini, safari hii nilienda, mbali kidogo. Niliona mgahawa mdogo uliokuwa karibu na ua. Niliingia ndani moja kwa moja. Ulikuwa umejaa huku lugha mbalimbali zikisikika. Kwa kutumia ishara, nilinunua kuku mzima wa kukaanga na chips nene za viazi. Nilirudi uani na kumchanchana kuku yule, nikitumia mikono yangu. Waislamu wote walionizunguka walikuwa wanafanya hivyo hivyo. Niliona wanaume wa walau miaka sabini wakikaa kwa kukunja miguu mpaka wakawa wanaonekana kama wamejifunga hivi. Wakila kwa furaha na kuridhika kama vile wapo ndani ya mgahawa mzuri, wakiwa wamezungukwa na wahudumu. Wote walikula pamoja na kulala pamoja. Kila kitu kuhusu mazingira ya hija, kilionyesha umoja wa binadamu chini ya Mungu mmoja.

Siku ile nilifanya safari kadhaa kati ya chumbani kwetu na kwenye ua wa jengo, kila wakati nikienda kutembea mbali kidogo. Nilikutana na wanaume wawili weusi na nikawasalimia kwa kichwa. Ilikuwa karibu nipige kelele kwa shangwe baada ya mmoja wao kunisalimu kwa Kiingereza chenye lafudhi ya Uingereza. Hatimaye nilikutana na Waislamu wawili waliozungumza kiingereza, bahati mbaya ndiyo walikuwa wanaondoka. Kabla ya kikundi chao kuondoka kuelekea Mecca, tulizungumza kidogo. Nikajitambulisha kuwa ni Mmarekani na wao wakaniambia ni Waethiopia. Waethiopia wale walikuwa wamepata elimu yao katika jiji la Cairo na sasa walikuwa wakiishi na kufanya kazi katika jiji la Riyadh, mji mkuu wa Saudi Arabia. Baadaye nilishangaa sana baada ya kufahamu kuwa kati ya raia milioni kumi na nane wa Ethiopia, milioni kumi walikuwa ni Waislamu. Watu wengi hudhani kuwa Ethiopia ina Wakristo wengi. Lakini ni serikali yake tu ndiyo ina Wakristo wengi. Siku zote nchi za magharibi zimeisaidia serikali ya Kikristo kubaki madarakani.

Nilikuwa nimeishasali sala yangu ya jioni, El Maghrib; nikawa nimelala kitandani kwangu kwenye chumba chetu. Nikijihisi mpweke na mnyonge ndipo ghafla ukaja mwanga!

Lilikuwa ni wazo la ghafla. Katika safari zangu za kwenda kwenye ua wa jengo lile, mahali palipokuwa pamejaa watu, nilikuwa nimewaona maafisa wanne waliokuwa wamekaa karibu na simu. Nikakumbuka namba alizonipatia Dr. Shawarbi kule New York, namba ya mtoto wa mwandishi wa kile kitabu alichonipatia, ambacho tayari nilikuwa nimekimaliza kukisoma. “Baba yangu atafurahi sana kuonana nawe,” alisema Dr. Azzam.

Nilimuuliza maswali kuhusu baba yake. Abd-Al-Rahman Azzam alijulikana zaidi kama Azzam Pasha, au Bwana Azzam mpaka wakati wa mapinduzi ya Misri pale Rais Nasser alipofuta vyeo vyote vya “kibwana.” “Nadhani atakuwepo nyumbani kwangu tukifika huko,” alisema Dr. Azzam. “Anatumia muda mwingi New York kwenye kazi yake ya Umoja wa Mataifa, amekufuatilia kwa ukaribu sana.”
Nilibaki mdomo wazi.

Ilikuwa ni alfajiri tulipofika kwenye nyumba ya Dr. Azzam. Baba yake alikuwepo pale. Pia walikuwepo kaka wa baba yake, ambaye alikuwa ni mkemia na rafiki yao mwingine, wote wakiwa macho mapema ile wakitusubiri. Kila mmoja alinikaribisha kwa bashasha kama vile nilikuwa mwana wao niliyepotea kwa muda mrefu. Sikuwahi kuwaona watu hao maishani lakini walinitendea kwa ukarimu sana! Nikuambie tu kuwa sijawahi heshimishwa namna ile maishani mwangu wala kuona ukarimu wa kweli kiasi kile.

Mhudumu alituletea chai na kahawa, kisha akaondoka. Niliambiwa nijisikie nipo nyumbani. Hakuna mwanamke aliyeonekana. Ukiwa Arabia unaweza dhani nchi haina wanawake.

Dr. Abd-Al-Rahman azzam ndiye aliyeongoza mazungumzo. Kwa nini sikupiga simu mapema? Hawakuelewa kwa nini sikufanya hivyo. Walionekana kufedheheka kuwa nilikaa uwanja wa ndege; na kwamba nilicheleweshwa kuingia Mecca. Nilijitahidi kuwaaminisha kuwa nilikuwa sawa na hakuna shida yoyote hawakukubali. “Unatakiwa kupumzika,” alisema Dr. Azzam, kisha akaenda kupiga simu.

Sikujua mtu huyu muungwana alikuwa anafanya nini. Nilipoambiwa nitarudishwa baadaye kwa ajili ya chakula cha jioni, na kuwa wakati huo nirudi garini, sikujua kabisa kuwa nilikuwa naenda kupokea ukarimu mkubwa kabisa wa Kiislamu.

Abd-Al-Rahman Azzam anapokuwa nyumbani Saudi Arabia huwa anaishi kwenye hoteli ya Jedda Palace. Kwa sababu niliwatembelea nikiwa na barua kutoka kwa rafiki yao, yeye aliamua kuishi nyumbani kwa mwanawe na kuniacha mimi nitumie makazi yake ya hotelini mpaka nitakapokwenda Mecca.

Nilipokuja kufahamu jambo hilo nilikuwa nimeishachelewa na sikuweza tena kupinga; tayari nilikuwa ndani ya makazi yale na Dr Azzam mdogo akawa ameishaondoka. Hakukuwa na wakumbishia. Makazi yake ya hotelini yalikuwa na vyumba vitatu vikubwa vya kulala. Kulikuwa na bafu kubwa kama mara mbili ya yale ya hoteli ya Hilton ya New York. Yalikuwa makazi namba 214. Na hata kulikuwa na kibaraza nje yake na hivyo kukuwezesha kuona vizuri mji ule wa pwani ya bahari ya Shamu.

Hapo kabla hisia zangu hazijawahi guswa kusali kama siku ile-na nikafanya hivyo. Nikasali kwenye zulia lililokuwako sebuleni.

Katika maisha yangu ya aina mbili niliyoishi kama mtu mweusi wa Marekani, hakuna hata moja iliyonipa mtazamo wa kiitikadi. Siku zote akili yangu ilichunguza sababu la lengo la mtu yeyote liyenitendea jambo ambalo sikustahili. Na siku zote, kama mtu huyo ni mzungu niliweza kuona lengo lake la kibinafsi.

Lakini siku ile hotelini pale ilikuwa ni moja ya mara chache sana ambazo nilipigwa na butwaa kiasi cha kushindwa kupinga. Mzungu yule—walau kwa Marekani angechukuliwa kuwa ni mzungu, alikuwa na undugu na mtawala wa Saudi Arabia ambaye alikuwa ni mshauri wake, mtu mkubwa kimataifa ambaye hana lolote la kupata kwa kunikarimu aliniachia makazi yake ya hotelini! Hakuwa na uhitaji wowote na mimi. Alikuwa na kila kitu. Ukweli ni kuwa alikuwa na vingi vya kupoteza kuliko kupata. Alikuwa amenifuatilia kwenye vyombo vya habari vya Marekani. Na kama alifanya hivyo, alifahamu vyema kuwa sikuwa na chochote zaidi ya kupewa sifa mbaya na kunyanyapaliwa. Nilikuwa dubwana lenye mapembe. Nilikuwa “mbaguzi wa rangi.” Nilikuwa “Mchukia wazungu” na yeye kwa muonekano alikuwa mzungu. Nilitwa mhalifu; na si hilo tu, bali kila mtu alikuwa akinishutumu kutumia dini yake ya Uislamu kama kichaka cha falsafa zangu na matendo yangu ya kihalifu. Na hata kama alikuwa na lengo la kunitumia, alifahamu vyema kuwa nilitengana na Elijah Muhammad na Taifa la Kiislamu, “nguzo zilizonipa nguvu,” kama vilivyodai vyombo vya habari vya Marekani. Taasisi pekee niliyokuwa nayo ilikuwa na majuma machache tu tokea ianzishwe. Sikuwa na kazi. Sikuwa na pesa. Na hata kufika pale nilikuwa nimekopa pesa kutoka kwa dada yangu.

Asubuhi ile ndipo nilipoanza kumtafakari “mzungu” tena. Ndipo nilipoanza kuchukulia kuwa neno “mzungu”, kama ambavyo limezoeleka kutumika, halimaanishi kutokana na rangi yake hasa, bali hasa linamaanisha tabia na matendo yake. Ndani ya marekani “mzungu” linamaanisha tabia na matendo fulani kuelekea mtu mweusi na watu wengine wote wasio weupe. Lakini kwenye ulimwengu wa Kiislamu, niliona watu wenye rangi nyeupe wakiwa na upendo wa kweli kuliko niliowahi kuuona kutoka kwa yeyote yule.

Asubuhi ile ndipo ndipo mtazamo wangu mzima juu ya “mzungu” ulipobadilika.

Ngoja ninukuu kutoka kwenye kijitabu changu. Niliandika haya mchana ule nilipokuwepo hotelini: “Siwezi kuelezea shangwe niliyonayo nikiwa nimekaa hapa nikisubiri kwenda mbele ya Kamati ya Hajj. Dirisha langu linaangalia upande wa Magharibi, iliko bahari. Mitaa imejaa mahujaji kutoka kote duniani. Sala zinatolewa kwa Allah na aya za Quran zipo kwenye midomo ya kila mmoja. Sijawahi ona jambo zuri kama hili, wala kushuhudia, wala kulihisi.

Ninajihisi salama, maelfu ya maili kutoka kwenye maisha tofauti kabisa niliyoishi. Piga picha kuwa saa ishirini na nne zilizopita nilikuwa kwenye chumba kilichokuwa katika ghorofa ya nne pale uwanja wa ndege, nikiwa nimezungukwa na watu ambao siwezi kuwasiliana nao, nikiwa sijui kabisa mustakabali wangu utakuwaje na kujihisi mpweke sana, lakini simu moja tu kama Dr. Shawarbi alivyonielekeza, imefanya nikutane na mmoja ya watu wenye nguvu sana katika Ulimwengu wa Kiislamu. Muda si mrefu nitalala kitandani pake ndani ya hoteli ya Jedda Palace. Natambua vyema kuwa nimezungukwa na rafiki ambao hawana unafiki na ni watu ninaoweza kuhisi nguvu ya imani yao. Inanipasa kusali tena kumshukuru Allah kwa Baraka hii, inanipasa kusali kwa ajili ya mke wangu na watoto wangu waliopo Marekani ili nao wapokee Baraka siku zote kutokana na kujitoa kwao.”

Nilisali sala mbili zaidi kama nilivyoandika kwenye kijitabu changu. Baada ya hapo nikalala kwa saa nne mpaka pale simu ilipoita. Alikuw ani Dr. Azzam mdogo. Alisema kuwa baada ya saa moja atakuja kunichukua kwa ajili ya kwenda kupata chakula cha jioni. Nilijiumauma wakati wa kujaribu kutafuta maneno ya shukrani. Alinikatisha kwa kusema, “Ma sha’a-llah” neno linalomaanisha, “Mungu ndiye aliyepanga.”

Wakati wa kumsubiri Dr. Azzam, nilikimbia mara moja kwenda ukumbi wa mapokezi ya hoteli. Nilipokuwa natoka nilionana koridoni na mtu mmoja aliyevalia kiramsi huku akiwa amezungukwa na wahudumu. Ilionekana wazi kuwa anaishi pale. Naye alikuwa anashuka chini. Nilifuatana nao walipokuwa wanashuka hadi kupita ukumbi wa mapokezi. Nje kulikuwa na msafara mdogo wa magari ukiwasubiri. Jirani yangu yule alipotokea mlango wa mbele wa hoteli, watu walimkimbilia na kumbusu mkono. Nilikuja kutambua kuwa alikuwa ni Mufti Mkuu wa Jerusalem. Baadaye hotelini pale nilipata wasaa wa kuongea naye kwa kama nusu saa. Alikuwa mtu mwenye urafiki na mwenye kujiendesha kwa heshima sana. Alifahamu vyema mambo ya dunia, na hata matukio yaliyokuwa yanaendelea Marekani.

Sitakuja kusahau ule mlo wa jioni nyumbani kwa Azzam. Nitanukuu daftari langu tena: ‘Akilini mwangu sikuweza kujiambia kuwa watu hawa ni ‘wazungu.’ Kwa nini, kwa sababu walinitendea kama vile ni ndugu yao, Dr. Azzam mkubwa kama baba yangu. Maneno yake ya kibaba na kiuanazuoni yalinifanya nimhisi kama baba yangu. Haikuwa kazi ngumu kugundua kuwa alikuwa mwanadiplomasia mbobezi, mtu mwenye maarifa mengi. Alifahamu mambo yanayoendelea duniani kama mtu anavyofahamu yanayoendelea sebuleni kwake.

‘Kadri tulivyozungumza, ndivyo maarifa yake juu ya mambo mbalimbali yalivyoonekana hayana kikomo. Aliongelea jamii ya vizazi vya Mtume Muhammad, na alionyesha jinsi ambavyo walikuwepo weupe na weusi. Alionyesha pia jinsi ambavyo tatizo la ubaguzi wa rangi kwenye ulimwengu wa Kiislamu lipo kwenye maeneo yale tu yaliyoathiriwa na nchi za magharibi. Alisema kuwa kiasi cha ubaguzi wa rangi anachokutana nacho mtu sehemu fulani kinaashiria kiasi cha ushawishi wa magharibi katika eneo hilo.’

Wakati wa chakula nilifahamishwa kuwa nilipokuwa hotelini, Kamati ya Hajj ilijulishwa kuhusu suala langu, na kwamba asubuhi natakiwa kufika huko. Nilifanya hivyo.

Jaji alikuwa ni Sheikh Muhammad Harkon. Mahakamani hakukuwa na watu isipokuwa mimi na dada mmoja kutoka India ambaye zamani alikuwa ni mprotestanti na sasa amesilimu, na kama mimi tu, naye alikuwa anajaribu kufanya hija. Alikuwa na rangi ya kahawia na sura ndogo ambayo ilikuwa imezibwa kwa sehemu kubwa. Jaji Harkon alikuwa mtu mpole na thabiti, tuliongea na aliniuliza maswali kadhaa, akijaribu kuona kama nimeamini kweli. Nilimjibu kwa ukweli wangu wote. Si tu kuwa alinitambua kama Muislamu wa kweli, bali pia alinipatia vitabu viwili. Kimoja kimeandikwa kwa Kiingereza na kingine kwa Kiarabu. Aliandika jina langu kwenye orodha takatifu ya Waislamu wa kweli na tukawa tumemaliza. Aliniambia, “Natumaini utakuwa mhubiri mkubwa wa Uislamu katika Marekani.” Nilimwambia kuwa nami nina matumaini hayo na nitajaribu kuyatimiza.

Familia ya Azzam ilifurahi sana kusikia kuwa nimekubaliwa kwenda Mecca. Nilipata chakula cha mchana kwenye hoteli ya Jedda Palace kisha nikalala tena kwa saa saba, simu ndiyo iliyoniamsha.

Alikuwa ni Muhammad Abdul Azziz Maged, makamu mkuu wa protokali wa Mwanamfalme Faisal. “Gari maalumu itakusubiri kwenda Mecca mara tu baada ya chakula cha jioni,” aliniambia. Aliniambia nile vya kutosha sababu taratibu za Hajj zinahitaji nguvu nyingi. Mpaka wakati huo sikuwa nashangaa tena.

Waarabu wawili vijana waliambatana nami kwenda Mecca. Barabara kubwa ya kulipia iliyokuwa na mwanga wa kutosha ilifanya safari iwe rahisi sana. Walinzi wa njiani walitizama ndani ya gari mara moja na dereva aliwaonyeshea ishara na tukaruhusiwa kupita, bila hata ya kupunguza mwendo. Kwa wakati huohuo mmoja, nilikuwa mtu niliye muhimu na mnyenyekevu na mwenye shukrani.

Mji wa Mecca ulionekana kama mji wa kale sana. Gari letu lilipita kwenye barabara za mitaa zilizojipindapinda, zikiwa
zimejaa maduka pembeni yake. Mabasi, magari na makumi elfu ya mahujaji kutoka duniani kote walifurika mitaani.
Gari ilisimama mahali ambapo Mutawaf alikuwa akinisubiria. Alivalia kofia nyeupe na kanzu nyeupe, kama wale wa uwanja wa ndege. Alikuwa mwarabu mmoja mfupi na mweusimweusi hivi, jina lake aliitwa Muhammad. Hakuongea kiingereza hata kidogo.

Tulipaki karibu na Msikiti Mkuu wa Mecca. Tulifanya udhu na kuingia. Ndani kulijaa mahujaji waliosongamana. Wengine wakiwa wamelala, wengine wamekaa, wanaotembea na wengine wakisali.

Sina maneno ya kuuelezea msikiti mpya uliokuwa unajengwa kuzunguka Kaaba. Nilifurahi kufahamu kuwa ulikuwa ni moja ya miradi mikubwa ya ujenzi kati ya ile iliyosimamiwa na Dr. Azzam mdogo, mtu aliyekuwa mwenyeji wangu. Msikiti Mkuu wa Mecca utakapokamilika, utalipita jengo la Taj Mahal la India kwa uzuri.

Nilimfuata Mutawaf nikiwa nimebeba makubadhi yangu. Kisha nikaiona Kaaba. Jengo kubwa katikati ya Msikiti Mkuu. Lilikuwa linazungukwa na maelfu-elfu ya mahujaji wanaosali, watu wa jinsia zote, rangi, maumbo na kila aina kutoka pande zote duniani. Niliifahamu sala iliyopaswa kutolewa mara tu mahujaji anapoiona Kaaba. Tafsiri yake inasema, “Ee Mungu, wewe ni amani na amani inatoka kwako. Tunaomba Ee Mungu utukaribishe kwa amani.” Baada ya kuingia ndani ya Msikiti Mkuu, mahujaji anatakiwa kuibusu Kaaba iwapo anaweza, lakini kama umati unamzuia kuifikia, anapaswa kuishika. Na kama umati unamzuia kufanya hivyo, anatakiwa kuinua mkono juu na kupaza sauti, “Takbir!” (“Mungu ni Mkubwa”). Sikuweza kufika karibu. “Takbir!”

Hisia zangu mahali pale katika Nyumba ya Mungu zilikuwa kama nimepigwa ganzi. Mutawaf wangu aliniongoza hadi kwenye umati wa mahujaji waliokuwa wakitoa sala huku wakiizunguka Kaaba mara saba. Wengine walikuwa wamepinda na ngozi zao kujikunja sababu ya uzee; ilikuwa taswira ambayo si rahisi kukutoka kichwani. Niliona mahujaji walemavu wakiwa wamebebwa. Sura zao ziking’aa kwa furaha. Kwenye mzunguko wa saba, nilisali Rak’a mbili, nikiinama hadi kichwa kugusa chini. Nilianza kwa kusali aya ya Quran “Sema yeye ni Mungu, Mungu pekee”, sala ya pili: “Sema ee nyinyi msioamini, siabudu kile mnachoabudu ”

Nilipokuwa nikisali, Mutawaf wangu aliwazuia mahujaji wengine wasije kunikanyaga-kanyaga.

Kisha mimi na Mutawaf wangu tukanywa maji kutoka kisima cha Zamzam. Baada ya hapo tukakimbia kati ya vilima viwili, Safa na Marwa, mahali ambapo Hagari alitangatanga akitafuta maji kwa ajili ya mwanawe Ishmaeli.

Baada ya hayo, nilitembelea Msikiti Mkuu mara tatu na kuizunguka Kaaba. Asubuhi iliyofuata tulienda kwenye mlima Arafat, tulikuwa maelfu ya watu, tukipaza sauti kwa pamoja, “Labbayka! Labbayka!” na “Allah Akbar!” Mecca imezungukwa na milima ya kutisha ambayo sijawahi kuona mahali pengine; ni kama vile ilitengenezwa kwa uji wa chuma kutoka kwenye tanuri. Hakuna kitu chochote kilichoota juu yake. Tulipofika ilikuwa tayari mchana, tulisali mpaka jua lilipozama, tulifanya huko sala maalumu za mchana na jioni.

Mwishowe tuliinua mikono yetu na kutoa sala na shukrani, tukirudia maneno ya Allah: “Hakuna Mungu isipokuwa Allah. Hana mshiriki. Yeye ni mwenye mamlaka na sifa. Mema yanatoka kwake naye ni mwenye nguvu juu ya vitu vyote.”

Kusimama juu ya mlima Arafat ndiyo jambo la mwisho kwa mahujaji wa Mecca kutimiza. Hakuna mtu anayeweza kujiita mahujaji iwapo hajatimiza hilo.

Ihram ikawa imeisha. Tulimtupia shetani mawe saba. Wengine walikata nywele na ndevu zao. Niliamua kuwa nitaziacha ndevu zangu. Nilijiuliza mke wangu Betty na binti zangu wadogo watasema nini baada ya kuniona na ndevu nitakaporudi New York. New York ilionekana kama ipo umbali wa maili milioni moja. Sikuona gazeti lolote ninaloweza kusoma toka nitoke New York. Sikujua chochote juu ya yanayoendelea huko. Chama cha watu weusi waliomiliki bunduki ambacho kilikuwepo Harlem kwa miaka mingi kilikuwa “Kimegunduliwa” na polisi; ilikuwa inatangazwa kuwa nilikuwa nyuma ya suala hilo. Taifa la Kiislamu la Elijah Muhammad lilikuwa limenifungulia kesi, wakitaka kunitoa mimi na familia yangu kwenye nyumba tuliyoishi huko Long Island.

Magazeti makubwa, vituo vya redio na televisheni vya marekani vilikuwa na wawakilishi jijini Cairo waliokuwa wakijaribu kuniwinda kila sehemu, kujua niko wapi ili wanihoji juu ya mambo yanayoendelea huko New York, mambo niliyoshutumiwa kusababisha wakati sikujua chochote kuyahusu.

Kitu pekee nilichofahamu ni yale niliyoyaacha nilipoondoka Marekani, mambo ambayo ni kinyume kabisa na niliyoyakuta kwenye ulimwengu wa Kiislamu. Waislamu kama ishirini hivi tuliokuwa tumemaliza Hajj tulikuwa tumekaa kwenye hema kubwa lililokuwepo kwenye mlima Arafat. Nikiwa kama Muislamu kutoka Marekani, macho mengi yalinielekea. Waliniuliza ni kitu gani katika Hajj kilichonipendeza sana. Mmoja ya walioweza kuzungumza Kiingereza aliuliza na kisha kuwatafsiria wengine majibu yangu. Jibu langu kwa swali hilo halikuwa lile walilotegemea, lakini walielewa vyema nilichomaanisha.

Nilisema “Undugu! Kitendo cha watu wa kila aina na rangi, kutoka kote duniani kuja pamoja kama kitu kimoja! Kimenithibitishia nguvu za Mungu Mmoja.”

Pengine hapakuwa mahala pake, lakini hilo lilinipa nafasi ya kuwahubiria kidogo kuhusu ubaguzi wa rangi uliopo Marekani na madhira yake.

Niliweza kuona jinsi hilo lilivyowagusa. Walikuwa wanafahamu madhira waliyokutana nayo watu weusi wa Marekani, lakini hawakujua kama walitendewa kama wanyama, kwamba kilichofanyika kilikuwa sawa na kuhasiwa kisaikolojia. Watu hawa kutoka maeneo mbalimbali ya dunia walishangazwa sana. Wakiwa kama Waislamu, walikuwa na mioyo ya huruma sana kwa wale waliokuwa wanapitia taabu, na watu waliguswa sana haki na kweli. Walielewa vyema mtazamo wangu wa mambo—kwamba kwangu mimi uovu mkubwa sana duniani ni ubaguzi wa rangi, na viumbe wa Mungu kushindwa kuishi kama kitu kimoja katika ulimwengu wa Magharibi.

***
 
Sura ya 17 inaendelea.​

Niliketi na kuandika barua iliyofunua mambo yaliyokuwa yanapita akilini mwangu.

Upofu wa kutoona rangi uliopo katika jamii ya kidini ya Waislamu. Na upofu wa rangi uliopo kati ya jamii ya binadamu wa Kiislamu.
Barua ya kwanza ilikuwa ni kwenda kwa mke wangu Betty. Sikuwa na shaka kuwa baada ya kushangazwa mwanzoni, ataungana na namna yangu ya kufikiri. Nilikuwa na uhakika mara elfu kuwa imani ya Betty juu yangu ilikuwa ni kamili
kabisa.Nilifahamukuwa ataona
nilichoona—kwamba​
kwenyenchi yaMuhammad na
Abraham, nilikuwa​
nimebarikiwa na Allah kwa kupewa mtazamo mpya juu ya dini ya kweli ya Kiislamu, na uelewa mzuri juu ya tatizo la rangi la Marekani.

Baada ya kuandika barua kwa mke wangu, niliandika nyingine ya namna ile ile kwa dada yangu Ella. Nilijua Ella amesimama upande gani. Yeye mwenyewe alikuwa akitunza pesa kwa ajili ya kwenda hija Mecca.

Nilimuandikia Dr. Shawarbi ambaye imani yake juu yangu ilifanya niweze kupata passport ya Mecca.

Usiku mzima nilikuwa ninanakili barua ile kwenda kwa watu wangu wa karibu. Mmoja wao alikuwa ni kijana wa Elijah Muhammad, Wallace Muhammad ambaye alikuwa amekiri kwangu kuwa njia pekee kwa Taifa la Kiislamu kusonga mbele ni kuukubali na kuutenda Uislamu wa asili.

Pia niliwaandikia wasaidizi wangu waaminifu kwenye taasisi yetu mpya ya Muslim Mosque, Inc huko Harlem. Niliambatanisha na ujumbe kuwa barua yangu itolewe nakala na zisambazwe kwenye vyombo vya habari.
Nilifahamu kuwa mara tu barua yangu itakapochapwa magazetini, wengi watashangazwa sana-wapendwa wangu, rafiki na adui pia. Na mamilioni wengine ambao sikuwafahamu wangeshangazwa pia-watu ambao kwa miaka kumi na mbili niliyokuwa na Elijah Muhammad walikuwa wanataswira ya “chuki” juu ya Malcom X.

Hata mimi mwenyewe nilishangazwa. Lakini barua hii haikuwa bahati mbaya. Maisha yangu yote yamekuwa ya kubadilikabadilika.

Hiki ndicho nilichoandika . . .kutoka moyoni kabisa: ‘Kamwe sijawahi kushuhudia ukarimu wa kweli na undugu wa kweli kati ya watu wa kila rangi kama nilioshuhudia hapa kwenye nchi takatifu, nyumbani kwa Abraham, Muhammad na manabii wengine watakatifu walioandikwa katika Maandiko Matakatifu. Katika juma lililopiata, nimepigwa na butwaa na kushindwa kuongea kutokana na ukarimu nilioonyeshwa na watu walionizunguka, watu wa kila rangi.

‘Nimebarikiwa kuweza kutembelea Mji Mtakatifu wa Mecca. Nimeizunguka Kaaba mara saba, nikiongozwa na Mutawaf kijana aitwaye Muhammad. Nimekunywa maji kutoka kisima cha Zamzam. Nimekimbia mara saba kati ya vilima vya Al-Safa na Al-Marwah. Nimesali kwenye mji wa kale wa Mina, na nimesali kwenye mlima Arafat.

‘Kulikuwa na makumi elfu ya mahujaji kutoka duniani kote. Watu wa kila rangi, kutoka wenye macho ya bluu na nywele za rangi ya dhahabu hadi waafrika wenye ngozi nyeusi. Wote tulifuata taratibu zilezile, tukionyesha roho ya umoja na undugu, vitu ambavyo kuishi kwangu Marekani kuliniaminisha kuwa haviwezekani kutokea kati ya mzungu na mtu asiye mzungu.

‘Marekani inatakiwa kuuelewa Uislamu kwa sababu hii ndiyo dini pekee inayofuta tatizo la ubaguzi wa rangi kwenye jamii. Katika kutembea kwangu kote kwenye ulimwengu wa Kiislamu, nimekutana, nimeongea na hata kula na watu ambao Marekani wangechukuliwa kuwa ni ‘wazungu’ lakini dini ya Kiislamu imeondoa mtazamo wao wa ‘kizungu’ katika akili zao. Kamwe sijawahi ona undugu wa kweli ukifanywa na watu wa kila rangi, bila kujali rangi zao.

‘Unaweza kushangazwa kusikia maneno hayo yakitoka kwangu. Lakini katika hija hii, yale niliyojionea na kuyaishi, yamesababisha kubadili sehemu kubwa ya mtazamo wangu niliokuwa nao hapo kabla, na kuachana na baadhi ya mambo niliyoamini hapo kabla. Hili halikuwa jambo gumu kwangu. Pamoja ya kuwa mimi ni mtu thabiti katika misimamo, lakini siku zote nimekuwa mtu ninayejitahidi kukubaliana na ukweli na hali halisi ya maisha kadri mambo na maarifa mapya yanavyojifunua. Siku zote nimekuwa na akili huru, kitu ambacho ni muhimu ili kuendana na mabadiliko yanayoambatana na kutafuta ukweli.

‘Katika siku kumi na moja zilizopita nilizoishi hapa katika ulimwengu wa Kiislamu, nimekula kutoka kwenye sahani moja, na kunywa kutoka kwenye glasi ileile, na kulala katika kitanda kimoja(Au kwenye zulia moja)-nikisali kwa Mungu yuleyule na Waislamu wenzangu, watu ambao macho yao yalikuwa ya bluu hasa, na nywele zao za dhahabu hasa, na ngozi zao nyeupe hasa. Niliona maneno na matendo yasiyo na unafiki kutoka kwa Waislamu weupe kama tu niliyoona kutoka kwa Waislamu weusi wa Afrika kutoka Nigeria, Sudan na Ghana.

‘Sote tulikuwa sawa(Ndugu)-sababu imani yao katika Mungu mmoja iliondoa ‘weupe’ katika akili zao, ‘weupe’ kutoka katika tabia zao, na ‘weupe’ kutoka kwenye mitazamo yao.

‘Katika hilo niliona kuwa, pengine wazungu wa Marekani wakikubali Mungu mmoja, pengine pia nao watakubali ukweli kuwa binadamu wote ni wamoja-na kuacha kuwapima, kuwadhuru na kuwakwamisha wengine kutokana na rangi ya ngozi zao.

‘Ugonjwa wa ubaguzi wa rangi ukiwa umeiandama Marekani kama kansa. Mioyo ya wakristo wa Marekani inatakiwa kukubaliana na suluhisho lililothibitika kutibu ugonjwa huo mbaya. Pengine haitakuwa kuchelewa kuiokoa Marekani kutoka kwenye janga linaloikabili-janga la maangamizi kama lile lililoikuta Ujerumani sababu ya ubaguzi, janga ambalo mwishowe liliwaangamiza Wajerumani wenyewe.

‘Kila saa inayopita katika hii Nchii Takatifu, inanifanya nielewe vyema kiroho hali ya mambo yanayoendelea Marekani kati ya wazungu na watu weusi. Kamwe mtu mweusi wa Marekani hawezi kulaumiwa kuwa ni mbaguzi wa rangi-anachofanya ni matokeo ya ubaguzi wa rangi aliokabili waziwazi kwa miaka mia nne.

‘Lakini kadri ambavyo ubaguzi wa rangi unaipeleka Marekani kwenye kujiangamiza, nina imani kuwa kizazi cha vijana wa Marekani, kutokana na uzoefu niliopata kwa kukaa nao-vijana walioko vyuoni wataona maandishi ukutani na wengi wao watageukia njia ya kweli ya kiroho-njia pekee kwa Marekani kuepuka janga ambalo litaletwa na ubaguzi wa rangi.

‘Kamwe sijawahi heshimiwa namna hii. Wala sijawahi nyenyekezwa na kufanywa nihisi sistahili. Nani ataamini Baraka zilizojazwa kwa mtu mweusi wa Marekani? Siku chache zilizopita, mtu ambaye Marekani angeitwa ‘mzungu’,mwanadiplomasia wa Umoja wa Mataifa, balozi, mwambata wa Wafalme-alinipatia makazi yake ya hotelini, kitanda chake. Kupitia mtu huyu, Mtukufu Mwanamfalme Faisal, mtawala na nchi hii Takatifu, alijulishwa uwepo wangu katika mji wa Jedda. Asubuhi iliyofuata, mwana wa Mwanamfalme Faisal mwenyewe, alinijulisha kuwa kwa mapenzi ya baba yake, nitakuwa mgeni wa kitaifa.

‘Makamu mkuu wa protokali, alinichukua yeye mwenyewe kwenda mahakama ya Hajj. Mtukufu Sheikh Muhammad Harkon mwenyewe ndiye aliyeniruhusu kwenda Mecca na kunipatia vitabu viwili vya Kiislamu, vikiwa na muhuri wake binafsi na sahihi yake, na kuniambia kuwa anasali ili niwe mhubiri wa Uislamu mwenye mafanikio katika Marekani. Nimepewa gari, dereva na muongozaji na hivyo kuniwezesha kusafiri katika nchi hii Takatifu nipendavyo. Serikali imenipatia makazi yeye kiyoyozi na wahudumu katika kila mji niliotembelea. Kamwe sijawahi ota kuwa nitakuja pokea heshima kubwa namna hii-heshima ambayo Marekani hutolewa kwa Wafalme, si kwa mtu mweusi.

‘Sifa zote zimuendee Allah, Bwana wa Ulimwengu wote. “Wako Muaminifu,” El-Hajj Malik El-Shabazz “(Malcom

X)”

Mwisho wa sura ya 17​
 
Sura ya 18
El-HAJJ MALIK EL-SHABAZZ
Mwanamfalme Faisal, mtawala wa Arabia alinifanya kuwa mgeni wa kitaifa. Hadhi hii iliambatana na huduma nyingi, moja ambayo niliifurahia na kuitumia bila kujivunga ilikuwa ni usafiri wa gari, gari ilinitembeza maeneo mbalimbali ya mji wa Mecca huku muongozaji akinionyesha maeneo mbalimbali ya muhimu. Baadhi ya maeneo ya Mji Mtakatifu yalionekana kuwa ni ya kale sana na mengine yalikuwa ya kisasa kama vile upo vitongoji vya Miami. Siwezi kuelezea hisia nilizopata pale nilipoweka mkono wangu kwenye ardhi ambayo manabii wakubwa waliikanyaga miaka elfu nne iliyopita.

Jina “Muislamu kutoka Marekani” lilizua udadisi wa watu kote nilikoenda. Mara kadhaa nilidhaniwa kuwa ni Cassius Clay. Gazeti moja lilichapisha picha yangu na Cassius Clay tukiwa Umoja wa Mataifa. Kupitia kwa dereva-muongozaji na mtafsiri wangu, niliulizwa maswali mengi kuhusu Cassius. Kwenye ulimwengu wa Kiislamu hata watoto walimfahamu na kumpenda. Cinema kotekote Afrika na Asia zilikuwa zimeonyesha pambano lake. Katika siku hizo za mwanzo za kazi yake, Cassius alikuwa ameteka nyoyo za dunia yote ya watu wasio weupe.

Gari ilinichukua kwenda kushiriki maombi maalumu kwenye mlima Arafat na Mina. Barabarani kulikuwa na vurugu ambazo sijawahi ona, msongamano wa kutisha, breki na matairi yakipiga kelele na honi zikilia (Naamini uendeshaji magari wote katika Mji Mtakatifu unafanyika kwa jina la Allah.) Nilikuwa nimeishaanza kujifunza sala kwa kiarabu, lakini jambo lililokuwa gumu kwangu ni mikao ya sala. Mikao ile ambayo sikuizoea ilisababisha kidole gumba changu cha mguu kivimbe na kuuma.

Lakini mila za ulimwengu wa Kiislamu nilikuwa nimeishazizoea. Mkono wangu ulikuwa upo tayari kuchota chakula kutoka kwenye chombo ambacho tulishirikiana na ndugu wengine wa Kiislamu; nilikunywa kutoka kwenye kikombe tulichoshirikiana na wengine bila kusita; nilinawa kutoka kwenye jagi moja; na kulala zuliani kwenye sehemu ya wazi na watu wengine nane hadi kumi. Nakumbuka usiku mmoja huko Muzdalifa, nilijilaza nikitazama anga katikati ya ndugu wa Kiislamu waliokuwa wamelala usingizi, nilitambua kuwa mahujaji wa rangi, vyeo, hadhi na kazi tofauti wote walikoroma kwa lugha moja.

Ninadhani kuwa kwenye baadhi maeneo ya Nchi Takatifu niliyotembelea, mamilioni ya chupa za vinywaji yalinywewa- na sigara milioni kumi zitakuwa zilivutwa. Waislamu, hasa Waarabu, walivuta sigara karibu muda wote, hata wanapokuwa kwenye hija ya Hajj. Jambo ovu la uvutaji wa sigara halikuwepo enzi za Mtume Muhammad-kama lingekuwepo ninaamini kuwa angelipiga marufuku.

Baadaye nilikuja kuambiwa kuwa Hajj ya mwaka ule ilikuwa ndiyo kubwa kuliko zote katika historia. Kasem Gulek kutoka bunge la Uturuki, kwa majivuno, aliniambia kuwa Uturuki peke yake kulitoka mabasi zaidi ya mia sita na zaidi ya mahujaji elfu hamsini walifanya hija. Nilimwambia kuwa ninaota siku ambayo meli na ndege zilizojaa Waislamu wa Marekani zikija Mecca kwa ajili ya Hajj.
Kulikuwa na watu wa kila rangi kwenye umati. Mara tu nilipoliona hilo, nilianza kulichunguza kwa umakini zaidi. Kuwa kwangu Mmarekani kulifanya niwe mtu wa kutilia maanani sana rangi za watu. Niliona kuwa watu waliofanana walitembea pamoja. Hili lilifanyika kwa hiari yao wenyewe; hakukuwa na sababu nyingine nyuma yake. Waafrika walikuwa na Waafrika wenzao, Wapakistani na wapakistani wenzao nk. Niliweka akilini kuwa nitakaporudi nyumbani, nitawaambia Wamarekani juu ya jambo hili; kuwa mahali ambapo kuna undugu wa kweli kati ya watu wa rangi zote, ambapo hakuna anayehisi kubaguliwa, mahali ambapo hakuna anayejiona bora wala anayejiona duni-hapo ndipo watu wanaofanana huja pamoja kwa hiari yao wenyewe, huvutwa na kule kufanana kwao.
Nia yangu ni kuwa kwenye hija inayofuata niwe tayari nafahamu lugha ya Kiarabu kwa kiasi. Katika ujinga wangu wote nilikuwa na bahati ya kupata marafiki wavumilivu walioniruhusu niongee kupitia mtafsiri. Kamwe maishani mwangu sijawahi kujihisi kiziwi na mjinga kama wakati ambao hakukuwa na mtafsiri wa kuniambia kinachoongelewa na Waislamu wengine kabla hawajafahamu kuwa “Muislamu kutoka Marekani” anafahamu sala chache tu kwa Kiarabu, zaidi ya hapo alitikisa kichwa na kutabasamu tu.

Lakini nyuma ya tabasamu langu na kutikisa kichwa nilikuwa natafakari. Niliona kuwa usilimuji wa watu unaweza kuongezeka mara mbili hadi mara tatu iwapo undugu unaokuwepo wakati wa hija ungetangazwa na kujulishwa kwa watu wa nje. Niliona kuwa Waarabu si wazuri katika kutambua saikolojia ya watu wasio Waarabu, na umuhimu wa mahusiano na umma. Waarabu walisema “insha Allah”(“Mungu akipenda”) na kisha wakaaa kusubiria watu wasilimu. Lakini hata kwa njia hii bado Uislamu ulikuwa unakua kwa kasi, lakini nilifahamu kuwa kwa kuboresha mahusiano ya umma, watu wapya wanaosilimu wangeweza kufikia mamilioni.

Kila nilikokwenda, muda wote nilikuwa nikiulizwa maswali juu ya ubaguzi wa rangi unaoendelea Marekani. Pamoja na historia ya maisha yangu, lakini nilishangazwa sana kuwa sifa kuu ya Marekani ilikuwa ni ubaguzi wa rangi.
Kwenye mamia ya mazungumzo niliyofanya na Waislamu kwenye nchi Takatifu, wenye vyeo na wadogo, na kutoka kote duniani-na baadaye nilivyokwenda nchi za Waafrika weusi, sikujivunga hata mara moja au kuacha nafasi ipite hata mara moja bila ya kueleza ukweli kuhusu uhalifu, uovu na udhalilishaji unaowakumba watu weusi wa Marekani. Kupitia mtafsiri wangu-sikupoteza hata nafasi moja madhira halisi yanayowakabili watu weusi wa Marekani. Nilihubiri hilo kwenye mlima Arafat, nililihubiri kwenye ukumbi wa mapokezi wa hoteli ya Jedda Palace. Niliwanyooshea vidole mmoja baada ya mwingine ili wanielewe vizuri; “Wewe . . . wewe . . . sababu ya rangi yako yenye weusi, ungekuwa Marekani nawe pia ungeitwa ‘Negro.’ Ungeweza pigwa mabomu, pigwa risasi, au kupigwa na maji yenye presha na kupigwa ngumi na mateke sababu tu ya rangi yako.”

Kama ambavyo mahujaji masikini walivyonisikia, ndivyo mahujaji ambao ni watu wakubwa walivyonisikia. Niliongea kwa kirefu na Hussein Amini, Mufti Mkuu wa Jerusalem-mtu mwenye macho ya bluu na nywele za rangi ya dhahabu. Tulitambulishwa na mbunge kutoka uturuki, Kasem Gulick, tulipokuwa kwenye mlima Arafat. Wote walikuwa ni watu wenye elimu; wote walisoma vizuri mambo yahusuyo Marekani. Kasem Gulick aliniuliza kwa nini nimetengana na Elijah Muhammad. Nilimwambia kuwa nilipendelea kutoelezea tofauti zetu ili kuendelea kulinda umoja wa watu weusi wa Marekani. Wote walielewa na kukubaliana na hilo.

Nilizungumza na Meya wa Mecca, Sheikh Abdullah Eraif, mtu ambaye wakati alipokuwa muandishi wa habari alikuwa ameshutumu uendeshwaji wa Manispaa ya Mecca. Mwanamfalme Faisal alimfanya kuwa Meya ili kuona kama anaweza kufanya vizuri zaidi. Watu wengi walikubali kuwa Sheikh Eraif alikuwa akifanya kazi nzuri. Kipindi cha televisheni kilichoitwa “Muislamu kutoka Marekani” kilitengenezwa na Ahmed Horyallah na mwenzake Essid Muhammad wa kutoka kituo cha televisheni cha Tunis.

Wakati fulani huko Chicago, Ahmed Horyallah alimfanyia Elijah Muhammad mahojiano.
Ukumbi wa mapokezi wa hoteli ya Jedda Palace iliniwezesha kuongea na watu wengi mashuhuri kutoka nchi mbalimbali waliokuwa na hamu ya kumsikia “Muislamu wa Marekani.” Nilikutana na Waafrika wengi ambao wamewahi kuishi Marekani au kusikia ushuhuda kutoka kwa Waafrika wenzao juu ya jinsi ambavyo Marekani ilikuwa ikiwatendea watu weusi. Nakumbuka wakati fulani waziri mmoja kutoka nchi za Waafrika weusi(alifahamu mambo yanayoendelea duniani kuliko mtu mwingine yeyote niliyewahi kukutana naye) alinisimulia juu ya safari zake za mara kwa mara za kwenda Marekani, kote, Marekani kusini na kaskazini, na kwa makusudi kabisa akiacha kuvaa mavazi ya kitamaduni ya nchini kwake. Kukumbuka tu udhalilishaji aliokutana nao kama mtu mweusi kulionekana kuamsha hisia kali kwa afisa huyu mkubwa. Macho yake yalikuwa mekundu kwa hasira, mkono wake ukipiga hewani. “Kwa nini mtu mweusi wa Marekani anaridhika na kukandamizwa? Kwa nini mtu mweusi wa Marekani hapiganii haki yake ya kuwa binadamu?”

Afisa mmoja wa ngazi za juu kutoka Sudan alinikumbatia na kusema, “Wewe ni shujaa wa watu weusi!” afisa mmoja kutoka India alilia kwa uchungu akisema, “Kwa ajili ya ndugu zangu katika nchi yenu.” Mara nyingi sana nimetafakari jinsi ambavyo mtu mweusi wa Marekani alivyochotwa akili kabisa ili asione wala kujifikiria mwenyewe kwa namna inayotakiwa, yaani kama mmoja wa watu wa duniani wasio wazungu. Mtu mweusi wa Marekani hafahamu juu ya mamia ya mamilioni ya watu wengine wasio wazungu wanavyomjali: hafahamu juu ya hisia zao za kindugu walizonazo juu yake.

Ilikuwa ni kule kwenye Nchi Takatifu na baadaye katika Afrika ndiko nilikofikia hitimisho ambalo naliamini hadi leo- kwamba takwa la kwanza kwa kiongozi yeyote wa watu weusi ndani ya Marekani linatakiwa kuwa kusafiri vya kutosha kwenda kwenye nchi za wasio wazungu, na safari hizo zinatakiwa kuhusisha vikao vingi na watu wakubwa wa nchi hizo. Nina hakika kuwa kiongozi yeyote wa kweli wa watu weusi na aliye tayari kujifunza atarudi nyumbani akiwa na fikra bora zaidi juu ya njia za kutatua tatizo linalomkabili mtu mweusi wa Marekani. Na zaidi ya yote, viongozi hao watagundua kuwa viongozi wengi wakubwa wa huko, hasa wa kutoka Afrika watawaambia-kwa faragha kuwa watapenda kutoa msaada wao kusaidia harakati za mtu mweusi huko Umoja wa Mataifa na kwa njia nyingine pia. Lakini viongozi hawa wanafahamu vyema kuwa mtu mweusi wa Marekani hajielewi na amegawanyika kiasi kwamba yeye mwenyewe hafahamu harakati zake zinahusu nini. Ni Waafrika ndiyo walioniambia kuwa hakuna anayetaka kuabika kwa kumsaidia ndugu ambaye haonyeshi kama anataka msaada huo-na ambaye anaonekana kukataa kutoa ushirikiano kwa jambo lenye maslahi kwake mwenyewe.
Tatizo kubwa la “viongozi” wa watu weusi wa Marekani ni kukosa maono! Namna yake ya kufikiri na mbinu zake(kama anazo) zimeishia pale aliposhauriwa au aliporuhusiwa na mzungu. Na kitu cha kwanza ambacho utawala wa Marekani hautaki ni kwa mtu mweusi kuanza kufikiri kimataifa.

Nafikiri kosa baya kabisa lililofanywa na taasisi za watu weusi wa Marekani na viongozi wao ni kushindwa kujenga mahusiano ya kindugu kati ya watu weusi wa Marekani na nchi huru za Afrika. Inatakiwa kila siku viongozi wa mataifa ya weusi ya Afrika wawe wanapokea taarifa ya yale yanayoendelea kwenye harakati za mtu mweusi wa Marekani-badala yake, Idara ya Taifa ya Marekani ndiyo inawapatia Waafrika taarifa, taarifa ambazo zinaonyesha kuwa matatizo yanayowakumba watu weusi wa Marekani yameshapatiwa ufumbuzi.

Waandishi wawili wa kimarekani ambao vitabu vyao vimeuza sana katika Nchi Takatifu wamesaidia sana kujulisha watu juu ya hali ya mtu mweusi wa Marekani. Kitabu cha James Baldwin kilichotafsiriwa kimekuwa na matokeo makubwa sana, kama tu kiitabu Black Like Me chake John Grin. Kama hukifahamu kitabu hicho-kinaelezea kisa cha Grin, mzungu, alivyojidai mtu mweusi na kusafiri sehemu mbalimbali za Marekani kama mtu mweusi kwa muda wa miezi miwili; baada ya safari hizo akaandika kuhusu mambo yaliyompata. “Mambo ya kuogofya kabisa!” nilisikia mara nyingi watu waliosoma kitabu hicho maarufu wakisema kule kwenye Nchi Takatifu. Lakini kila niliposikia hilo, nilijaribu kufunua fikra zao zaidi, “Kama yalikuwa mambo ya kuogofya kwake aliyejidai mtu mweusi kwa muda wa siku sitini tu, hebu fikiria waliyopitia watu weusi halisi wa Marekani kwa muda wa miaka mia nne.”
Jambo moja la heshima ambalo nilikuwa nimesali linikute lilikuwa ni kualikwa kuonana ana kwa ana na Mtukufu Mwanamfalme Faisal.

Sitasahau fikra nilizokuwa nazo wakati nilipokuwa ninaingia ofisini kwake, kwamba mbele yangu alikuwepo mmoja wa watu muhimu zaidi duniani, lakini pamoja na heshima yote aliyokuwa nayo, mtu aliweza kuona unyenyekevu wake wa kweli. Nilipoingia, Mwanamfalme Faisal, mrefu na nadhifu, aliinuka kunikaribisha. Alinielekeza kuketi kwenye kiti kilichoangaliana na chake. Mtafsiri wetu alikuwa ni makamu mkuu wa protokali, Muhammad Abdul Azziz Maged, Mwarabu mzaliwa wa Misri ambaye kwa muonekano alikuwa kama mnegro wa Harlem.

Mwanamfalme Faisal alinikatisha mara moja pale nilipoanza kujiumauma nikijaribu kutoa shukrani zangu kwa kunifanya kuwa mgeni wa kitaifa. Alisema kuwa ulikuwa ni ukarimu tu ambao Muislamu mmoja alimfanyie mwingine, na kuwa mimi kuwa Muislamu kutoka Marekani halikuwa jambo la kawaida. Aliniomba nielewe kuwa yote aliyofanya ni kwa sababu alipenda kufanya, hakukuwa na lengo lingine.

Mwanamfalme Faisal alipokuwa anaongea, mhudumu alituandalia aina mbili ya chai maalumu. Mwana wake, Muhammad Faisal alikuwa ameniona kwenye vituo vya televisheni vya Marekani alipokuwa akisoma chuo kikuu cha Northern California. Mwanamfalme Faisal alikuwa amesoma magazeti ya Misri kuhusu “Waislamu wa Marekani.” Kama wanachosema waandishi hao ni kweli, basi Waislamu weusi wa Marekani wana Uislamu usio sahihi,” alisema. Nilieleza nafasi yangu katika kuratibu na kujenga Taifa la Kiislamu kwa miaka kumi na mbili iliyopita. Nilisema kuwa lengo langu la kufanya Hija lilikuwa ni kuuelewa Uislamu wa kweli.

“Hilo ni jambo zuri,” alisema Mwanamfalme Faisal na kueleza kuwa kulikuwa kuna machapisho mengi yanayoelezea Uislamu katika lugha ya Kiingereza-hivyo hakukuwa na sababu ya msingi ya kutoufahamu, na hakuna sababu kwa watu wanaotaka wanaotaka kujua kweli kupotoshwa.

***

Mwezi wa nne mwaka jana, 1964, nilisafiri kwenda Beirut, mji mkuu wenye bandari wa Lebanon. Kuna sehemu yangu nilikuwa nimeiacha kwenye Mji Mtakatifu wa Mecca, na kwa kufanya hivyo nikawa nimeondoka na sehemu fulani ya Mecca.
Nilikuwa safarini kwenda Ghana na Nigeria. Lakini rafiki fulani niliokutana nao kwenye Nchi Takatifu walikuwa wamenisisitiza nipite sehemu kadhaa nami nikakubali. Kwa mfano, ilipangwa kuwa kituo cha kwanza nipitie na kuhutubia wahadhiri na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Beirut. Kwenye hoteli ya Beirut Palm Beach nililala mustarehe kwa mara ya kwanza toka nitoke Marekani. Kisha nikatoka kwenda matembezini. Nikiwa tu nimetoka Nchi Takatifu- mara moja tabia na mavazi ya wanawake wa Lebanon​

yalishtua akili yangu. Kwenye Nchi Takatifu kulikuwa na wanawake wa kiarabu waliovalia kwa staha sana-lakini hapa ghafla kuna wanawake; nusu Wafaransa na nusu Waarabu wa Lebanon ambao kwa mavazi yao walionyesha mtazamo wao wa kuwa huru na kujiamini zaidi katika kujiamulia mambo. Niliona wazi athari za Ulaya kwenye utamaduni wa Lebanon. Ilinionyesha jinsi ambavyo maadili ya nchi yanaweza kupimwa kwa haraka kwa kuangalia tabia na mavazi ya wanawake wao wanapokuwa nje, hasa wanawake vijana. Sehemu yoyote ambayo thamani ya mambo ya kiroho imeshushwa kama siyo kutoweka kwa kupenda mambo ya kimwili, mara zote hilo hujionyesha kwa wanawake. Angalia wanawake wa Marekani-wakubwa kwa wadogo-mahali ambapo hakuna maadili yoyote yaliyobakia. Inaonekana nchi zingine nazo ziko zimeegemeo upande mmoja au mwingine. Ukweli ni kuwa tunaweza kuwa na paradiso iwapo mambo ya kimwili nay a kiroho yatafanywa kwa uwiano mzuri.

Niliongea kwenye Chuo Kikuu cha Beirut kuhusu hali halisi ya mtu mweusi wa Marekani. Huko nyuma nilisema kuwa mzungumzaji mwenye uzoefu anaweza kuhisi muitikio wa wasikilizaji wake. Nilipokuwa ninaongea, niliweza kuhisi kujitetea kutoka kwa wanafunzi wazungu wa Kimarekani waliohudhuria-lakini upinzani wao ulipungua polepole kadri nilivyoendelea kumwaga ukweli ulio wazi. Siwezi kuelezea wala kusahau jinsi wanafunzi kutoka Afrika walivyoonyesha hisia zao.

Baadaye, kwa mshangao nilisikia kuwa magazeti ya Marekani yalikuwa yameandika kuwa hotuba yangu ya Beirut ilikuwa imesababisha “vurugu.” Vurugu gani? Sifahamu ni jinsi gani mwandishi wa habari mwenye dhamira njema anaweza kutuma taarifa kama hiyo. Gazeti la Beirut, Daily Star liliandika kuhusu hotuba yangu kwenye kurasa ya mbele, lakini halikuandika habari yoyote kuhusu vurugu-sababu hazikutokea. Nilipomaliza hotuba yangu, wanafunzi karibu wote kutoka Afrika walinizingira wakitaka saini yangu; kuna baadhi walinikumbatia. Hata wasikilizaji weusi wa Marekani hawajawahi kunikubali kama Waafrika wale wanyenyekevu na wenye kuonyesha hisia zao waziwazi.
Kutoka Beirut nilipanda ndege hadi Cairo, huko nilipanda treni hadi Alexandria. Nilipiga picha kwa kamera yangu kila kituo. Nilipofika nikachukua ndege kwenda Nigeria.

Kwenye safari hiyo ya saa sita, nilipokuwa sizungumzi na rubani(ambaye alikuwa muogeleaji kwenye mashindano ya olimpiki ya mwaka 1960), niliketi na mwanasiasa mmoja wa Afrika. Alikuwa karibu kupiga kelele kwa hamasa “watu wanapokuwa katika hali ya mkwamo na wanatolewa wanatolewa, kunakuwa hakuna muda wa kupiga kura.” Wazo lake ni kuwa hakuna nchi mpya ya Kiafrika inayotaka kuondoa athari za ukoloni kisha ikaweka mfumo wa kisiasa unaoruhusu migawanyiko na mabishano. “Watu hawajui kura zinamaanisha nini! Ni jukumu la viongozi walioelimika kuwatoa watu wao kutoka kwenye ujinga.”

Nilipofika Lagos, nilipokelewa na Profesa Essien-Udom kutoka Chuo Kikuu cha Ibadan. Sote tulifurahi sana kuonana. Tulikuwa tumekutana kwa mara ya kwanza nchini Marekani alipokuwa akifanya utafiti wa kitabu chake, Black Nationalism. Jioni hiyo mlo wa jioni uliandaliwa kwa heshima yangu, ulihudhuriwa na maprofesa na wataalamu wengine. Tulipokuwa tunakula, daktari mmoja kijana aliniuliza iwapo ninafahamu kuwa magazeti ya New York yalichukizwa sana kwa mauji ya mwanamke wa kizungu yaliyotokea huko Harlem hivi karibuni, na kulingana na magazeti hayo, watu wengi walikuwa wananilaumu mimi kwa namna fulani. Wanandoa fulani wazee wa kizungu walikuwa wameshambuliwa na vijana kadhaa weusi, na mwanamke alikuwa amechomwa visu hadi kufa. Baadhi ya vijana hao walikamatwa na polisi, na katika kuhojiwa walisema kuwa wao ni washiriki wa taasisi iitwayo “Blood Brothers.”(Ndugu wa damu) Vijana hao walisema, au waligusia kuwa wanauhusiano na “Waislamu Weusi” ambao walijitenga na Taifa la Kiislamu na kuungana nami.

Nilimwambia wageni kuwa ndiyo mara ya kwanza kusikia kisa hicho, lakini kuwa sikushangazwa kwa kwa matendo ya ukatili kutokea kwenye eneo lolote la maghetto ndani ya Marekani, mahali ambako watu weusi waliishi kama wanyama au watu wenye ukoma. Nilisema kuwa shutuma dhidi yangu ni mbinu ya kawaida ya mzungu kutafuta mbuzi wa kafara-kwamba kila mara kwenye maeneo ya watu weusi kinapotokea kitu ambacho wazungu hawakipendi, basi macho ya wazungu hayakuelekezwa kwenye kiini cha tatizo bali kwa mbuzi wa kafara.
Na kuhusu “Ndugu wa damu,” nilisema kuwa niliwachukulia watu weusi wote kuwa ndugu zangu wa damu. Nilisema kuwa jitihada za mzungu kuchafua jina langu zimefanikiwa kwa kufanya mamilioni ya watu weusi kunichukulia kama Joe Louis.

Kwenye hotuba yangu ndani ya ukumbi wa Trenchard, katika Chuo Kikuu cha Ibadan, nilisema kuwa nchi huru za Afrika zinatakiwa kuona umuhimu wa kusaidia kupeleka suala la watu weusi wa Marekani mbele ya Umoja wa Mataifa. Nilisema kama tu ambavyo Wayahudi wa Marekani wanavyoshirikiana kisiasa, kiuchumi na kitamaduni na Wayahudi wengine duniani, ninaamini sasa ni wakati wa watu weusi wa Marekani kuungana na umoja wa watu wenye asili ya Afrika duniani. Nilisema kuwa kimwili, Wamarekani weusi tutabaki Marekani tukipigania haki zetu za kikatiba, lakini kifalsafa na kitamaduni, Wamarekani weusi tunahitaji sana “kurudi” Afrika, na kuunda kitu kimoja juu ya nguzo ya umoja wa watu wenye asili ya Afrika.

Vijana wa Kiafrika waliniuliza maswali ya kisiasa yenye akili kuliko mtu anayoweza kuyasikia kutoka kwa watu wazima wa Marekani. Kisha likatokea jambo la kushangaza baada ya mzee mmoja mwenye asili ya visiwa vya Karibeani kusimama na kuanza kunishutumu kuwa nilikuwa nikiishambulia Marekani. “Kaa kimya! Kaa Kimya!” wanafunzi walipiga kulele huku wakizomea. Mtu yule alijaribu kubishana nao, lakini ghafla kundi la wanafunzi lilimrukia na kuanza kumkimbiza. Aliponea chupuchupu. Sijawahi ona kitu kama kile. Walimpigia kelele na kumtoa nje ya eneo la chuo. (Baadaye nilikuja kufahamu kuwa mtu yule alikuwa ameoa mwanamke wa kizungu, na alikuwa akijaribu kupata kazi kutoka shirika fulani la wazungu na ndilo lililompa kazi ya kunipinga. Hapo nikawa nimeelewa tatizo lake.)
Hii haikuwa mara yangu ya mwisho kushuhudia Waafrika wakionyesha unazi wa kisiasa.

Baadaye kwenye mkutano na umoja wa wanafunzi, niliulizwa maswali mengi na kufanywa kuwa mwanachama wa heshima wa chama cha Wanafunzi wa Kiislamu wa Nigeria. Ninayo kadi ya uwanachama hapa kwenye pochi yangu: “Alhadji Malcom X. Namba ya usajili M-138.” Baada ya kuwa mwanachama nilipewa na jina jipya: “Omowale.” Kwa lugha ya Kiyoruba linamaanisha, “Mwana aliyerejea nyumbani.” Sikudanganya nilipowaambiwa kuwa sijawahi pokea heshima yeye thamani kama ile.

Nigeria kulikuwa na washiriki wa Peace Corps mia sita, nilikuja kufahamu kuwa baadhi ya wana-peace corps wazungu nilioongea nao walijisikia aibu kwa yale yanayofanywa na wazungu wenzao ndani ya Marekani. Kati ya wana-peace corps ishirini weusi nilioongea nao, aliyenivutia zaidi alikuwa ni Larry Jackson, mhitimu wa chuo cha Morgan. Alikuwa mwenyeji wa Fort Lauderdale, Florida. Alijiunga na Peace Corps mwaka 1962.

Nilitembelea vituo vya radio na televisheni vya Nigeria. Ninapokumbuka kuona watu weusi wakiendesha vyombo vyao vya habari wao wenyewe najawa na hisia kali. Mmoja ya waandishi wa habari walionihoji alikuwa ni Mmarekani mmoja mweusi kutoka jarida la Newsweek-jina lake lilikuwa William. Alikuwa anasafiri sehemu mbalimbali za Afrika, hivi karibuni alikuwa amemhoji Waziri mkuu wa Ghana, Kwameh Nkrumah.

Tulipokuwa faragha, kikundi fulani cha maafisa wa Nigeria kiliniambia jinsi ambavyo idara ya habari ya Marekani ilikuwa ikijitahidi kuwasambazia Waafrika habari kuwa watu weusi wa Marekani walikuwa wanapiga hatua vizuri sana, na kuwa tatizo la ubaguzi wa rangi litatatuliwa hivi karibuni. Afisa mmoja mkubwa aliniambia, “Viongozi wetu na watu wengine wengi wanaelewa kuwa mambo ni kinyume chake.” Aliongeza kuwa wanadiplomasia wa Afrika katika Umoja wa Mataifa walielewa kuwa mzungu alikuwa amepanga hila za kuwatenganisha watu wenye asili ya Afrika.

“Nchini kwako ni watu wangapi wanafahamu kuwa Amerika ya Kaskazini, Kati na Kusini ina watu milioni themanini wenye asili ya Afrika?” aliniuliza.
“Hakuna shaka kuwa dunia itabadilika siku ambayo watu wenye asili ya Afrika watakuja pamoja kama ndugu!”
Sikuwahi kusikia mtazamo huo wa kumfikiria mtu mweusi kidunia kutoka kwa Mmarekani mweusi yeyote.
Kutoka Lagos, Nigeria, nilipanda ndege hadi Accra, Ghana.

Nadhani katika bara la Afrika hakuna nchi tajiri na yenye watu wenye uzuri wa asili kama Ghana, nchi ambayo inajivuna kuwa kisima cha Umoja wa Waafrika.

Nilishuka kwenye ndege na kupokelewa na mshtuko. Kuna mzungu wa Marekani alikuwa amenitambua; alikuwa na ujasiri wa kunifuata na kuniambia kuwa alitokea Alabama, na kunialika nyumbani kwake kwa chakula cha jioni!
Kwenye chumba cha chakula cha hoteli niliyofikia kulijaa wazungu waliokuwa wakiongelea utajiri wa Afrika ambao haujatumiwa bado, kama vile wale wahudumu Wakiafrika walikuwa hawana masikio. Hilo karibu liniharibie mlo wangu-kufikiri jinsi ambavyo katika Marekani waliwafungulia mbwa wa polisi wawashambulie watu weusi, na kurusha mabomu kwenye makanisa ya watu weusi huku wakifunga milango ya makanisa yao ili watu weusi wasiingie- na sasa kwa mara nyingine mzungu huyohuyo yupo nchi ambayo babu zake waliwaiba watu weusi na kuwafanya watumwa.

Palepale kwenye kifungua kinywa niliazimia kichwani mwangu kuwa, katika siku nitakazokuwepo Afrika, nitahakikisha nafanya maisha ya mzungu yule anayekenua na kutaka kuinyonya Afrika kwa mara nyingine kuwa magumu sana-mara ya kwanza alinyonya utajiri wake wa watu, sasa anataka utajiri wake wa madini.

Nilifahamu vyema kuwa mtazamo wangu haukupingana na ule wa kindugu nilioupata kwenye Nchi Takatifu. Waislamu wenye muonekano wa “kizungu” ambao walibadili mtazamo wangu walikuwa ni watu walionionyesha kuwa walikuwa na undugu wa kweli. Na nilifahamu vyema kuwa ni vigumu sana kumpata mzungu wa Marekani mwenye undugu wa kweli na watu weusi, haijalishi anakenua namna gani.

Muandishi Julian Mayfield alionekana kuwa ndiye kiongozi wa kikundi kidogo cha Wamarekani weusi walioishi Ghana. Nilimpigia simu Mayfield, kufumba na kufumbua nikawa nimekaa nyumbani kwake nikiwa nimezungukwa na Wamarekani weusi kama arobaini hivi; walikuwa wakisubiri ujio wangu. Kulikuwa na wafanyabiashara na watu wenye taaluma mbalimbali, kama wanandoa na wanaharakati kutoka Brookyln, Dr Roberts E. Lee na mkewe, wote wakiwa ni madaktari wa meno ambao wamekana uraia wao wa Marekani. Wengine walikuwa Alice Windom, Maya Angelou Make, Victoria Garvin na Leslie Lacy-walikuwa wameunda “Kamati ya Malcom X” ambayo kazi yake ilikuwa kuniongoza kwenye ratiba waliyonipangia.

Hapa kwenye mkoba wangu kuna baadhi ya habari zilizoandikwa kwenye magazeti ya Afrika baada ya kufahamu kuwa nilikuwa natembelea nchi za Afrika.

“Jina la Malcom X ni maarufu kwa watu wa Ghana kama ilivyo kwa mbwa, maji yenye presha, fimbo na sura zenye chuki za wazungu wa kusini ya Marekani. . . .” “Uamuzi wa Malcom X kuingia kwenye harakati za watu wote unatoa ishara mpya ya matumaini kwenye mapambano ya amani ambayo ni ya kinyonge na yanayosuasua ”

“Jambo la muhimu kabisa ni kuwa Malcom X ni kiongozi wa kwanza wa Wamarekani weusi anayejulikana kitaifa kufanya ziara ya Afrika tokea Dr. Du Bois alipokuja Ghana. Pengine huu ni mwanzo mpya wa harakati zetu. Acha tusidharau jambo hili kama ambavyo serikali inafanya.”

Na jambo jingine: “Malcom X ni mmoja ya viongozi wetu muhimu sana ambao tuko nao katika mapambano. Jitihada zitafanyika ili kumchafua na kufanya aonekane hana maana. . . .”

Sikuamini hata kidogo aina hii ya mapokezi niliyopata maili elfu tano kutoka Marekani! Maafisa kutoka vyombo vya habari walifanya mipango ya kulipia gharama zangu za hoteli, na hawakutaka kusikia hata kidogo nikipinga hilo. Maafisa hao walitia ndani T. D. Baffoe, mhariri mkuu wa gazeti la Ghananian Times; G. T. Anim, mkurugenzi mkuu wa Idara ya habari ya Ghana; Kofi Batsa, mhariri wa Spark na katibu mkuu wa chama cha waandishi wa habari wa Kiafrika; bwana Cameron Duodu; na wengineo. Sikuwa na kingine zaidi ya kuwashukuru. Wakati wa mlo mzuri ulioandaliwa na Ana Livia, mke mrembo mwenye asili ya Puerto Rica wa bwana Julian Mayfield(Ana Livia alikuwa ndiye msimamizi wa mpango wa afya wa wilaya ya Accra)-niliulizwa maswali mengi na watu weusi wale wenye shauku, watu waliotoka Marekani na kurudi kwenye bara lao la asili.

Natamani kila Mmarekani angeshiriki kuona, kusikia na kuhisi pamoja nami yale yaliyonitokea kule Ghana. Na lengo la kusema hivyo si kuzungumzia mapokezi niliyopokea nikiwa kama mtu ambaye tayari walikuwa wameisha msikia, bali mapokezi niliyopata nikiwa kama alama ya wanaharakati weusi wa Marekani.

Kwenye mkutano uliojaa niliofanya na klabu ya waandishi wa habari, nakumbuka swali la kwanza kuulizwa lilikuwa ni kwa nini nilitengana na Elijah Muhammad na Taifa la Kiislamu. Waafrika walikuwa wamesikia tetesi kuwa Elijah Muhammad alikuwa amejijengea jumba la anasa huko Arizona. Nilirekebisha uzushi huo na kuepuka kutoa shutuma zozote. Nilisema kuwa kutokubaliana kwetu kulikuwa juu ya muelekeo wetu wa kisiasa na ushiriki wetu kwenye harakati za kupigania haki za binadamu nje ya dini. Nilisema kuwa nililiheshimu Taifa la Kiislamu likiwa kama chanzo cha mabadiliko ya kisaikolojia, kimaadili na kijamii, na kuwa ushawishi wa Elijah Muhammad kwa mtu mweusi wa Marekani ulikuwa ni wenye manufaa.

Nilivisisitiza vyombo vya habari juu ya umuhimu wa uwepo wa mawasiliano na kusaidiana kati ya Waafrika na Wamarekani wenye asili ya Afrika, watu ambao mapambano yao yanafanana. Nakumbuka kuwa kwenye mkutano huo nilitumia neno “Negro,” na nikasahihishwa mara moja. “Hilo neno halikubaliki hapa bwana Malcom X. Jina Wamarekani wenye asili ya Afrika ni la heshima na lenye maana zaidi.” Niliomba radhi mara moja. Sidhani kama nilitamka neno “Negro” tena kwa muda wote niliokuwepo Afrika. Nilisema kuwa Wamarekani wenye asili ya Afrika milioni ishirini na mbili wanaweza kuwa na mchango mkubwa kwa Afrika-wakati huo huo mataifa ya Kiafrika yanaweza na yanatakiwa kutoa mchango wao katika kupambana na ubaguzi wa rangi unaoendelea Marekani. Nilisema kuwa ‘Afrika yote imeungana kupinga ubaguzi wa rangi unaofanyika huko Afrika Kusini na kwenye makoloni ya Ureno. Lakini mnapoteza muda wenu kama hamtatambua kuwa Verwoerd, Salazar, Uingereza na Ufaransa hawawezi kudumu hata siku moja bila ya msaada wa Marekani. Kwa hiyo basi, mpaka pale mtakapomuumbua mtu wa Washington, D.C., hamtakuwa mmefanya chochote kile.’

Nilifahamu kuwa G. Mennen Williams, kutoka Idara ya Taifa alikuwa anatembelea Afrika wakati huo kwa ziara rasmi. Nilisema, “Aminini maneno yangu, kuweni makini na hawa maafisa wa Marekani wanaokuja Afrika wakiwakenulia wakati kule nyumbani hawatukenulii.” Niliwaambia kuwa baba yangu mzazi aliuawa na wazungu kwenye jimbo la Michigan, jimbo ambalo wakati fulani G. Mennen Williams amewahi kuwa Gavana wake.

Kwenye klabu ya waandishi wa habari niliheshimishwa zaidi na wawakilishi mbalimbali wa vyombo vya habari. Nilikuwa mgeni nyumbani kwa binti wa Richard Wright, mwandishi Mmarekani mwenye asili ya Afrika ambaye sasa ni marehemu. Binti huyo aliitwa Julia na mumewe wa Kifaransa alikuwa akichapisha gazeti moja pale Ghana. Siku za baadaye nilipokuwa Paris, nilipata nafasi ya kuonana na Hellen, mjane wa Wright, na Rachel, binti yao mdogo.

Nilienda kwenye balozi mbalimbali na kuzungumza na mabalozi. Balozi wa Algeria alinivutia sana kwa sababu alikuwa amejitoa kabisa kwenye mapambano ya kijeshi na mapinduzi duniani, kama njia ya watu wanaokandamizwa duniani kujikomboa. Maono yake hayakuishi tu kwa Waalgeria, bali yalihusisha watu weusi wa Marekani na wengine wote-popote walipokandamizwa. Balozi wa China, Bwana Huang Ha, mtu mwenye maono sana na mwanaharakati hasa, alikazia juu ya jitihada za nchi za magharibi kuwatenganisha Waafrika na watu wenye asili ya Afrika duniani kote. Balozi wa Nigeria aliguswa sana na madhira yanayowapata watu weusi wa Marekani. Alijua vema matatizo yao kwa sababu aliwahi kusoma na kuishi jijini Washington, D.C. Mtu mwingine aliyeguswa namna hiyo alikuwa balozi wa Mali, aliwahifika New York kwenye Umoja wa Mataifa. Nilipata kifungua kinywa na Dr. Makonnen wa British Guiana. Tulizungumza juu ya umuhimu wa kuwa na umoja wa Waafrika ambao utahusisha Wamarekani wenye asili ya Afrika. Pia nilizungumza kwa kirefu na waziri wa utamaduni wa Ghana, Nana Nketsia, juu ya matatizo ya wamarekani wenye asili ya afrika.

Niliporudi hotelini nilikutana na simu kutoka New York ikinisubiria, ilikuwa inatoka kwa Mai Goode, wa shirika la utangazaji la Marekani. Mai Goode aliniuliza maswali nami niliyajibu naye aliyarekodi. Aliniuliza kuhusu “Ndugu wa damu” wa Harlem. Chama cha wamiliki wa bunduki weusi na mambo mengine niliyohusishwa nayo na vyombo vya habari vya Marekani.

Kwenye ukumbi mkubwa wa Chuo Kikuu cha Ghana nilihutubia umati mkubwa kuliko yote niliyohutubia katika Afrika. Wengi wao walikuwa ni Waafrika na baadhi wazungu. Mbele ya umati huu nilijitahidi kila niwezavyo kuondoa uzushi juu ya mahusiano ya watu wa rangi mbalimbali huko Marekani, uzushi niliofahamu kuwa ulikuwa ukienezwa na idara ya habari ya Marekani. Nilijaribu kuwajengea picha halisi ya madhira wanayokutana nao watu weusi wa Marekani katika mikono ya wazungu. Niliwapa ukweli wao wazungu wale waliokuwa kwenye hadhara.

“Sijawahi kuona wazungu wengi wakiwa wema kwa watu weusi kama nilivyoona hapa Afrika. Huko Marekani watu wenye asili ya Afrika wanapambania uchangamano. Wanatakiwa kuja hapa Afrika na kuona jinsi mnavyowakenulia Waafrika. Hakika hapa kuna uchangamano. Lakini mnaweza kuwaambia Waafrika kuwa huko Marekani mnawakenulia watu weusi? Hapana hamuwezi! Na kusema ukweli si kwamba mnawapenda Waafrika hawa zaidi, bali mnachopenda ni madini ambayo yamo ndani ya ardhi ya Afrika . . .”

Wazungu wale walibadilika rangi na kuwa wekundu. Walifahamu kuwa nilikuwa ninaongea ukweli. “Siichukii Marekani na sijaja hapa kuishutumu Marekani-nataka kuweka hilo wazi!” Niliwaambia. “Nimekuja hapa kuongea ukweli, na kama ukweli unaishutumu Marekani basi inastahili kushutumiwa!”

Jioni moja nilikutana na maafisa wengi wa Ghana-wengi wao tayari tulikuwa tumeishazungumza hapo kabla, na tuliongea zaidi katika tafrija niliyoandaliwa na mheshimiwa Kofi Baako, waziri wa ulinzi wa Ghana na kiongozi wa bunge. Niliambiwa kuwa hiyo ni mara ya kwanza kwa mgeni kuheshimishwa namna hiyo tokea Dr. W. E. B. Du Bois alipofika Ghana. Kulikuwa na muziki, dansi na vyakula vitamu vya kighana. Watu kadhaa kwenye tafrija ile walikuwa wakicheka, wakisema kuwa kwenye tafrija ya mapema siku ile, balozi wa Marekani, bwana Mahomey, alionekana kituko wakati akijaribu kuwa mkarimu na mcheshi kupita kiasi. Wengine walisema kuwa alikuwa anafanya jitihada kupinga ukweli kuhusu Marekani, ukweli niliokuwa nauweka wazi kila nipatapo nafasi.

Kisha nikapata mualiko ambao sijawahi hata kuota. Sikuwahi wazia kabisa kuwa nitakuja kupata nafasi ya kuhutubia wabunge wa Ghana!

Nilitoa hotuba yangu kwa ufupi lakini nilihakikisha ni yenye nguvu: “Mnawezaje kuilaani Ureno na Afrika Kusini wakati watu weusi wa Marekani wanaumwa na mbwa na kupigwa kwa marungu?” nilisema kuwa nilihisi sababu pekee kwa ndugu zetu wa Afrika kukaa kimya juu ya yale yanayoendelea Marekani ni kwa sababu wamelishwa uongo na propaganda na serikali ya Marekani.

Mwisho wa hotuba yangu nilisikia, “Ndiyo! Tunawaunga mkono Wamarekani wenye asili ya Afrika . . .kimaadili, kimwili, na hata kwa mali ikibidi!”

Huko Ghana au niseme katika Afrika nzima, heshima kubwa niliyopewa ilikua ni kukutana na Osagyefo(mwokozi)Dr. Kwame Nkrumah.

Kabla ya kukutana naye nilipekuliwa vya kutosha. Naheshimu ulinzi ambao waghana wanampa kiongozi wao. Ilinifanya niwaheshimu zaidi watu weusi walio huru. Nilipoingia ofisi ya Dr. Nkrumah, aliinuka kutoka kitini. Dr. Nkrumah huvalia mavazi ya kawaida tu, alinyoosha mkono kunisalimia huku akitabasamu. Tulikaa kwenye kochi na kuzungumza. Nilifahamu kuwa alikuwa na taarifa za kutosha juu ya madhira ya Wamarekani wenye asili ya Afrika maana ameishi na kusoma Marekani kwa miaka mingi. Tulizungumza juu ya umoja wa Waafrika na watu wenye asili ya Afrika. Tulikubaliana kuwa umoja ndiyo msingi kutatua tatizo la watu wenye asili ya Afrika. Niliweza kuona ucheshi na unyenyekevu wa Dr. Nkrumah. Nilihisi kama muda wangu pamoja naye uliisha haraka sana. Niliahidi kuwa nitakaporudi Marekani, nitawapelekea Wamarekani wenye asili ya Afrika salamu zake.

Mchana wa siku ile, maili thelathini na tisa huko Winneba, nilihutubia kwenye taasisi ya itikadi ya Dr. Kwame Nkrumah- mahali ambapo wanafunzi mia mbili walikuwa wanafundishwa ili kuendeleza mapinduzi ya kifikra ya Ghana, hapa pia nilishuhudia unazi wa kisiasa wa vijana wa Kiafrika.

Wakati wa kipindi cha maswali na majibu baada ya kuhutubia, kijana wa kimarekani mwenye asili ya Afrika alisimama, “Mimi ni Mmarekani mweusi,” alijitambulisha. Kwa namna fulani akaanza kumtetea mzungu wa Marekani. Wanafunzi wakiafrika walianza kumzomea na kumzonga. Mara tu baada ya mkutano kuisha, walimbana na kuanza kumshambulia kwa maneno, “Wewe ni wakala wa wakina-Rockfeller?” . . . “Acha kupotosha watoto wetu!” (Ilikuja kufahamika kuwa kijana yule ni mwalimu wa shule ya sekondari ya karibu, akiwekwa kwenye kazi hiyo na Wamarekani) . . . “C. I. A” . . . “Shushushu wa Marekani!”

Balozi wa China, bwana Huang Ha na mkewe waliandaa mlo wa kitaifa kwa ajili yangu. Kati ya wageni walikuwepo mabalozi wa Cuba na Algeria, pia ni kwenye karamu hii ndipo nilikutana na bibi W. E. B. Du Bois. Baada ya mlo mzuri, filamu tatu zilionyeshwa, filamu moja ya rangi ilihusu sherehe ya maadhimisho ya miaka kumi na nne ya kuanzishwa kwa Jamuhuri ya watu wa China. Mtu ambaye alijitokeza mara kwa mara kwenye filamu hii alikuwa ni mwanaharakati aliyeitwa Robert Williams, alikuwa ni Mmarekani mweusi kutoka Carolina ya Kaskazini, alikuwa amekimbilia Cuba baada ya kusema kuwa watu weusi wa Marekani wanatakiwa kubeba silaha ili kujilinda. Filamu ya pili ilikazia jinsi watu wa China wanavyounga mkono harakati za watu weusi wa Marekani. Mwenyekiti Mao Tse-tung alionyeshwa akitoa tamko juu ya uungwaji mkono huo. Ndani ya filamu kulikuwa na vipande vya kutisha vikionyesha ukatili mbaya wa polisi na raia wa kizungu dhidi ya Wamarekani wenye asili ya Afrika waliokuwa wakiandamana kwenye majiji mbalimbali ya Marekani, wakidai haki za kiraia. Filamu ya mwisho ilihusu mapinduzi ya Algeria.

“Kamati ya Malcom X” ilinikimbiza haraka kutoka kwenye tafrija ya Ubalozi wa China hadi mahali ambapo klabu ya waandishi wa habari ilikuwa imeandaa tafrija kwa ajili yangu, tafrija yenyewe tayari ilikuwa imeishaanza. Ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kuona Waghana wakicheza dansi. Kila mtu alikuwa na wakati mzuri sana. Nilisisitizwa kutoa hotuba fupi. Kwa mara nyingine nilisisitiza umuhimu wa umoja kati ya Waafrika na Wamarekani wenye asili ya Afrika. Nilisema kutoka moyoni, ‘Kwa sasa cheza dansi na imba! Lakini unapofanya hivyo mkumbuke Mandela, mkumbuke Sobokwe! Mkumbuke Lumumba akiwa ndani ya kaburi lake! Wakumbuke Waafrika Kusini walio gerezani!’
Nilisema, ‘Mnajiuliza kwa nini sichezi dansi? Kwa sababu nataka muwakumbuke Wamarekani weusi milioni ishirini na mbili waliopo Marekani!”

Lakini ukweli nilitamani sana kucheza dansi. Waghana wanacheza dansi kama vile wameshikwa na pepo. Binti mmoja mrembo Wakiafrika aliimba “Blue Moon” kama Sarah Vaughan. Wakati mwingine bendi ilipiga kama Milt Jackson, na wakati mwingine kama Charlie Parker.

Asubuhi iliyofuata, Jumamosi, nikapata habari kuwa Cassius Clay na watu wake waliwasili. Kulikuwa na mapokezi makubwa uwanja wa ndege. Niliwaza kuwa iwapo mimi na Cassius tutaonana, litakuwa jambo la kufedhehesha sana kwake, maana alikuwa amechagua kubaki na Uislamu wa Elijah Muhammad. Binafsi nisingefedheheka lakini nilifahamu kuwa Cassius alipigwa marufuku kujihusisha nami. Nilifahamu vyema kuwa Cassius alijua nilikuwa pamoja naye, kwa ajili yake na nilikuwa na imani naye wakati ambao wale ambao baadaye walikuwa karibu naye walipomuona kuwa hawezi kufika popote. Niliamua kumuepuka Cassius ili nisimuweke katika nafasi mbaya.
Mlo wa mchana wa siku ile niliandaliwa na balozi wa Nigeria, mheshimiwa Alhadji Isa Wali, mtu mmoja mfupi, aliyevaa miwani, mcheshi na mwenye urafiki sana. Aliwahi kuishi Washington D.C. kwa miaka miwili. Baada ya mlo, alizungumza na wageni wake jinsi alivyokutana na ubaguzi alipokuwa Marekani, na urafiki aliofanya na Wamarekani wenye asili ya Afrika na kukazia undugu uliopo kati ya Waafrika na Wamarekani wenye asili ya Afrika.

Kabla ya mlo, mheshimiwa alikuwa amewapatia wageni jarida la Kimarekani liitwalo horizon. Lilikuwa limefunguliwa sehemu ambayo kuliandikwa makala kuhusu Taifa la Kiislamu iliyoandikwa na Dr. Morroe Berger kutoka Chuo Kikuu cha Princeton. Kurasa moja nzima ilikuwa na picha yangu; kurasa nzima upande wa pili kulikuwa na mchoro wa Muislamu mweusi aliyeishi Nigeria, miaka mia moja iliyopita. “Nilipoangalia picha hizi, nilijua watu hawa ni wamoja,” alisema mheshimiwa. ‘Tofauti pekee ni kwenye nguo walizovaa-na mmoja alizaliwa Marekani na mwingine Afrika.​

“Kwa hiyo basi, ili kumfanya kila mtu aamini kwamba sisi ni ndugu, nitampatia Alhadji Malcom X vazi kama lile lililovaliwa na mnaigeria wa kwenye picha.”

Niliachwa mdomo wazi kwa uzuri wa vazi lile la bluu na kitambaa cha rangi ya machungwa ambacho mheshimiwa yule alinipatia. Alikuwa ni mfupi, hivyo niliinama ili aweze kunivisha kilemba. Kisha mheshimiwa Alhadji Isa Wali alinipatia matoleo mawili ya tafsiri ya Quran Takatifu. Baada ya mlo huu wa mchana usiosahaulika, bibi Shirley Graham Du Bois aliniendesha mpaka nyumbani kwake ili kwenda kuona na kupiga picha nyumba ambayo mume wake na mtu mashuhuri, Dr. W. E. B. Du Bois aliishi katika siku za mwisho za maisha yake. Bi Du Bois alikuwa ni mwandishi na mkurungenzi wa kituo cha televisheni cha Ghana, kituo ambacho lengo lake kuu lilikuwa kutoa elimu. Aliniambia kuwa Dr. Du Bois alipofika Ghana, Dr. Nkrumah alimpokea mwanaharakati na mwanazuoni yule mzee kutoka Marekani kama mfalme, akimpatia Du Bois kila kitu alichohitaji. Bi Du Bois aliniambia kuwa afya ya Dr. Dubois ilipoanza kukungoroka kwa kasi, Dr. Nkrumah alimtembelea na wawili hao waliongea maneno ya kwaheri, wote wakifahamu kuwa kifo cha mmoja wao kilikaribia-na kuwa Dr. Nkrumah aliondoka huku machozi yakimtoka.
Tukio langu la mwisho la kijamii pale Ghana ilikuwa ni kwenye tafrija iliyoandaliwa kwa heshima yangu na mheshimiwa Armando Entralgo Gonzalez, balozi wa Cuba nchini Ghana. Siku iliyofuata ilikuwa ni Jumapili-“Kamati ya Malcom X” ilikuwa inanisubiri nje ya hoteli kunisindikiza uwanja wa ndege. Tulipokuwa tunaondoka hotelini, tulikutana na Cassius Clay na baadhi ya watu wake wakitoka matembezi ya asubuhi. Kwa sekunde kadhaa Cassius alikuwa kama ameshikwa na kigugumizi, kisha akaongea kitu, nadhani alisema “Habari yako?” taswira ya jinsi tulivyokuwa karibu kabla ya pambano lililobadili maisha yake ilinijia kichwani. Nilimjibu kuwa nzuri au kitu kama hicho, na kuwa ni matumaini yangu kuwa naye ni mzima pia-na hilo lilitoka moyoni. Baadaye nilimtumia Cassius ujumbe nikimwambia kuwa natumaini anatambua jinsi anavyopendwa na Waislamu kokote waliko; na kwamba hataruhusu mtu yeyote amtumie na kumpotosha kusema mambo ambayo yatachafua taswira yake.

Tulikuwa uwanja wa ndege nikiagana na “Kamati ya Malcom X” na ghafla msafara mdogo wa mabalozi matano ulifika kuniaga. Mpaka hapo nilikuwa nimeishiwa maneno ya kusema.

Nikiwa kwenye ndege kuelekea Monrovia, Liberia ambako ningetumia siku moja, niliwaza kuwa baada ya mambo yaliyonipata kwenye Nchi Takatifu, jambo jingine nitakaloenda nalo Marekani ni jinsi ambavyo Waafrika wanavyojitambua, utajiri wake na nguvu zake na nafasi yake katika dunia.
Kutoka Monrovia, nilipanda ndege mpaka Dakar, Senegali. Wasenegali waliokuwepo uwanja wa ndege baada ya kusikia kuhusu Muilsmu kutoka Marekani, walisimama kwa mstari ili kunisalimu kwa mkono, na niliandika saini nyingi. “Watu wetu hawazungumzi Kiarabu, lakini Uislamu upo mioyoni mwetu,” alisema Msenegali mmoja. Nikasema kuwa iko hivyo pia kwa Waislamu wenzao Wamarekani wenye asili ya Afrika.

Kutoka Dakar nilipanda ndege hadi Morocco ambako nilitumia siku moja kutembea hapa na pale. Nilitembelea Casbah, eneo la maghetto ambalo lilitokea baada ya wakoloni wa Kifaransa kuwakataza wazawa wasio wazungu kuishi maeneo fulani ya Casablanca. Maelfu kwa maelfu ya wazawa waliokandamizwa waliishi kwa kusongamana kwenye maghetto, kama tu ambavyo Harlem, New York ilivyokuja kuwa Casbah ya Marekani.

Nilipowasili Algiers ilikuwa ni Jumanne, tarehe 19 ya mwezi wa tano, mwaka 1964, siku yangu ya kuzaliwa. Mambo mengi yamepita tokea ziku zile. Kwa namna fulani nilikuwa na uzoefu kuliko dazani ya watu. Dereva wa taxi aliyenichukua kwenda hoteli ya Aletti, alinielezea ukatili uliofanywa na Wafaransa na hatua alizochukua yeye binafsi ili kulipa kisasi. Nilitembea katika jiji la Algiers nikisikia maneno ya chuki dhidi ya Marekani kwa kitendo chake cha kuunga mkono ukandamizaji wa Waalgeria. Walikuwa ni wanamapinduzi hasa, hawakuogopa kifo. Kwa muda mrefu sana wamekabiliana na kifo.

***​
 
Back
Top Bottom