NADHARIA Kenge akikupiga na mkia wake kuna athari anakuachia ya kufanana maisha yako na yake. Akiumwa, akikonda nawewe inakutokea

Taarifa hii ni nadharia tu, tumeitolea ufafanuzi kwa kadiri ilivyowezekana
Je, hili linalosemwa ni la kweli kwamba endapo kenge akikupiga na mkia wake kuna madhara unaweza kupata.

Kwa mfano akikonda na wewe unakonda akinenepa na wewe unanenepa akifa na wewe unakufa.

1920px-Nile_monitor_lizard_(Varanus_niloticus).jpg
 
Tunachokijua
Kenge au ni wanyama wafananao na mamba wadogo katika familia ya juu Varanoidea. Wana mwili mwembamba, miguu mirefu na mkia mrefu. Kenge ni mnyama ambaye watu wengi hushindwa kumtofautisha na mamba kwani wanafanana kwa mambo mbalimbali isipokuwa mamba ana umbo kubwa zaidi.

Kama alivyobainisha mleta mada hii, kumekuwapo na hoja za kijamii kwamba Kenge ni mnyama hatari
endapo ikitokea amekupiga na mkia wake kuna madhara unaweza kupata. Hoja hiyo inadai kuwa mtu aliyechapwa na mkia wa Kenge anapata athari za kufanana kimaisha na kenge huyo. Mathalani Kenge akikonda naye anakonda, Kenge akinenepa naye unanenepa na Kenge akifa naye anakufa.

Upi uhalisia wa hoja hii?
Katika kufuatilia uhalisia wa hoja hii JamiiCheck imefatilia vyanzo mbalimbali ikiwamo blogu za Wataalamu wa Wanyama inayoitwa A-Z Animals na AnimaliaBio ambazo zimefafanua kwa undani kuhusu Kenge na madhara yake:

A-Z Animals Waandishi wa masuala ya wanyama wameelezea hatari ya mnyama Kenge kwa kuweka andiko la mtindo wa swali na kisha wametoa majibu yake. Andiko hilo limebeba kichwa kinachouliza, 'Je, mnyama Kenge ni hatari?'. Majibu yao yanaonesha hatari inayoweza kumkumba mtu ambaye atachapwa na mkia au kuumwa na Kenge. Wakielezea kwa ufupi athari hizo:

Maranyingi, Kenge sio wakorofi, huweza kumshambulia binadamu iwapo tu watachokozwa. Ushambuliaji wao kwa binadamu hulenga zaidi kujilinda, au kujinasua katika hatari. Wana kucha ndefu, meno makali, na miili yenye nguvu, hii huwafanya kuwa hatari zaidi kuliko mijusi wengine. Lakini ni nadra sana kuwashambulia binadamu.
Inapotokea binadamu ameng'atwa au kushambuliwa na Kenge huweza kupata maumivu makali, kuvimba, kutokwa na damu, kuumwa na kichwa au kutoka jasho. Sumu ya Kenge haina nguvu ya kuweza kuua binadamu. Huweza kuua wanyama wadogo wadogo. Ikiwa mtu atapata dalili mbaya zaidi baada ya kung'atwa na Kenge wanapaswa kwenda hospitali kupata matibabu ya haraka. Kung'atwa na Kenge kunaweza pelekea kuambukizwa na bakteria. Kwa hivyo, ni muhimu kutibu jeraha lake kwa haraka.

Kwa upande wao, AnimaliaBio, wameka makala inayomchambua mnyama Kenge katika vipengele mbalimbali kama vile muonekano wake, mahali anapopatikana kwa Afrika, maisha na tabia zake. Katika kueleza tabia zake AnimaliaBio wanabainisha kwa ufupi mazingira ambayo Kenge anaweza kuwa hatari kwa binadamu. Wanasema:

Kenge Wakiona hatari yoyote, mara nyingi hukimbia au hata wanaweza kurukia ndani ya maji kutoka kwenye tawi la mti hasa wakiwa wadogo. Wanapokuwa wakubwa wakizidiwa huweza kutumia mkia wao au meno kushambulia kama mbinu ya kujilinda na hatari inayowakabili.

Kwa ujumla, maandiko hayo mawili hapo juu yanaonekana kukubaliana kuwa, Kenge hamshambulii binadamu bila kuchokozwa, Kushambilia kwake hulenga kujilinda zaidi. Binadamu anapong'atwa au kushambuliwa na Kenge huweza kupata maumivi na vidonda lakini sumu yake haina kuua mwanadamu.

Hata hivyo, pamoja na maandiko hayo kueleza athari za kushambuliwa na kenge lakini hakuna andiko lililoeleza ikiwa mnyama huyo akikushambulia atakuachia athari kuendana na hali maisha yake kama vile, kukonda, kunenepa, kufa nk.

Katika kutafuta ufafanuzi wa kitaalamu zaidi, JamiiCheck imawasiliana na Kamanda Mhifadhi wa Ikolojia kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Mhifadhi Lackson Mwamwezi ambaye anasimamia Mikoa ya Kilimanjaro na Tanga na kumpa hoja hii ambaye anafafanua:

Kenge ni Mnyama ambaye tunamhifadhi, kuhusu mkia wake kumchapa mtu kisha akawa ananenepa au kukonda hayo ni masuala ya imani kama ilivyo imani nyingine. Hatujawahi kukuta na changamoto ya aina hiyo na hata kitaalamu hatujakutana na suala hilo.
Unajua imani ukiiamini au kuipa kipaumbele inawezekana ikakutokea kweli lakini mimi kama Mhifadhi hilo ninajua ni suala la imani. Kwa kawaida Kenge akibananishwa ndio anautumia mkia kama kujilinda na sio mara zote anautumia kumshambulia mtu.
Hivyo, kutokana na ufafanuzi kutoka vyanzo hivyo JamiiCheck inaona kuwa hoja inadai kuwa binadamu kushambuliwa na kenge hupelekea maisha na afya yake ifanane na mnyama ni imani ya kijamii ambayo haina ushahidi wa kitaalamu.
2 Reactions
Reply
Back
Top Bottom