Kitaalam imekaa vipi?
- Tunachokijua
- IQ ni ufupisho wa maneno Intelligent Quotient, kwa tafsiri isiyo sahihi sana kwa Kiswahili tunaweza kuita kipimo cha akili ambacho hupatikana baada ya kufanyika kwa majaribio maalum.
Majaribio haya hulenga kupima mambo mbalimbali ikiwemo lugha, uwezo wa kufikiri, utunzaji wa kumbukumbu, kufanya hesabu pamoja na uwezo wa kutatua changamoto mbalimbali za Maisha ya kila siku.
Baadhi ya watu waliowahi kuthibitishwa kuwa na IQ kubwa
Mtaalam wa hisabati, Terence Tao anatajwa kuwa na IQ inayokadiriwa kufikia 220-230. Alianza Shule ya Msingi miaka ya 1980 akiwa na umri wa miaka 7, alipata shahada ya kwanza akiwa na umri wa miaka 16 na na Shahada ya uzamivu akiwa na umri wa miaka 21.
Mwaka 2017, Jarida la Indian Times lilichapisha makala inayomtaja binti wa miaka 11 anayeishi Uingereza kuwa na IQ ya 162. Pia, chapisho hilo lilibainisha kuwa Wanasayansi Albert Einstein na Steven Hawking wanadhaniwa kuwa na IQ inayofikia 160.
Vitu vinavyochangia uwezo wa IQ
Kiasi cha IQ ya binadamu huathiriwa na mambo mbalimbali ikiwemo;
- Lishe
- Hali ya afya ya Mhusika
- Mfumo wa Elimu
- Utamaduni na mazingira
Kwa mujibu wa utafiti uliofanyika kwa miaka 40 unabainisha kuwa mabadiliko mbalimbali yanayotokea duniani yamefanya takwimu za IQ zinazohusianishwa na umri wa mama zibadilike pia. Mathalani, kati ya mwaka 1958-1970, watoto waliozaliwa na wanawake wenye umri wa kati ya miaka 25-29 walikuwa na IQ kubwa zaidi kuliko watoto waliozaliwa na wanawake wenye umri wa miaka 35-39.
Takwimu za utafiti huu zinaonesha kuwa, kuanzia mwaka 2001, watoto waliozaliwa na wanawake wenye umri wa miaka 35-39 au hata zaidi ya hapo walionekana kuwa na IQ kubwa kuliko wale waliozaliwa na wanawake wenye umri wa miaka 25-29.
JamiiForums imefanya marejeo ya tafiti mbalimbali, taarifa za kisayansi na maelezo ya wataalam wa afya na kubaini kuwa;
- IQ ya mtu huchangiwa na mambo mengi, hasa yale yanayoathiri makuzi ya mtoto kama vile mazingira, tamaduni, elimu anayopatiwa pamoja na mfumo mzima wa maisha ya kila siku.
- Kwa uchache wake, tafiti za sasa zinadai kuwa wanawake wenye umri mkubwa, walau kuanzia miaka 35-40 huwa na uwezekano mkubwa zaidi wa kupata mtoto mwenye IQ kubwa kuliko wale wenye umri chini ya hapo.
- Watu wenye IQ kubwa huwa pia na uwezo mkubwa wa kufikiri na kutatua kwa haraka changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Hivyo, Kutokana na uwepo wa taarifa kinzani zinazohusianisha umri wa mama na ukubwa wa IQ ya mtoto, JamiiForums inachukulia hoja hii kama nadharia inayopaswa kufanyiwa uchunguzi zaidi ili kubaini ukweli wake.