KERO Halmashauri ya Mji Kibaha amkeni, tatueni kero za barabara mbovu

Hii ni kero ambayo mwananchi ameiwasilisha JF akitaka wahusika kuchukua hatua

proisra

JF-Expert Member
Jun 14, 2012
214
158
Kama kuna aibu inayoinyemelea Halmashauri ya Mji Kibaha ni ubovu wa miundombinu ya barabara zake, na hasa zilizopo katikati ya Mji (Kata ya Maili Moja). Hii ni kero ya muda mrefu sana, kwa Halmashauri ya Mji Kibaha kushindwa kuweka vipaumbele vya ujenzi wa barabara za pembezoni na hasa katika Kata ya Maili Moja iliyopo katikati ya Mji ili kufanya mazingira ya Mji wa Kibaha kuvutia.

Mfano mmojawapo wa Barabara Korofi ni hii ya kutokea “SHELI - MAILI MOJA SHULENI HADI MPIJI NA MUHEZA”, ambako idadi ya Wananchi ni wengi na inazidi kuongezeka siku hadi siku bila uwepo wa huduma za msingi. Maeneo ya Hifadhi ya Barabara yamevamiwa kwa kujengwa maduka na vibanda vya biashara na kufanya magari kupishana kwa taabu au kwa kusubiriana. Wananchi wa kawaida, Bodaboda, Wanafunzi na Wafanyabiashara wa “Soko la Kwa Mchicha” tunapata taabu za kutembea katika Tope la Uji-Uji misimu ya Mvua kama sasa.

Imefikia hatua hata waendesha Bajaji wamegoma kabisa kutoa huduma kwa barabaa hii wakihofia vyombo vyao kuharibika. Nyakati za kiangazi hali ni hiyohiyo, Mashimo na Makorongo huongezeka na hivyo kufanya wagonjwa na Mama wajawazito kuathirika wakipelekwa kupata huduma za afya Hospitali ya Rufaa Tumbi na nyinginezo.

Sisi Wananchi tunayo Maswali tunayojiuliza ingawa hatupatiwi majibu:-

  1. Yuko wapi Mbunge wetu SYLVESTA KOKA, mbona hazungumzi chochote pale Bungeni au kufuatilia Maendeleo ya barabara za Kata ya Maili Moja angalau zitengenezwe kwa kiwango cha Lami?
  2. Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha uko wapi?! Hivi hujui kero hii ilihali barabara hii inatizamana na Makao Makuu ya Halmashauri?! Ni lini utasikia kilio cha Wananchi Wapiga Kura na kutupa majibu?!
  3. TARURA mpo na Ofisi Kibaha Mji au mpo tu Dar es Salaam?! Ziko wapi alama za hifadhi za barabara?! Mbona mmeachia Wananchi kujenga Vibanda vya Biashara kiholela maeneo yanayopaswa kuwa ya hifadhi za barabara na kuhatarisha Usalama wa magari, bodaboda na wapita kwa miguu?!
  4. Mkuu wa Wilaya ya Kibaha unafahamu kero za sisi wapiga kura?! Au Viongozi wote ninyi mnasubiri Wananchi tuandamane na “Mabango yenye Picha za Kero” hadi Ikulu ya Magogoni ndiyo muamke?!
  5. Mwenyekiti na Katibu wa Chama Tawala (CCM) Wilaya ya Kibaha mko wapi?! Hebu tokeni Ofisini sasa mtutembelee kuona hali halisi ya kero hii. Mbona Wananchi tunateseka na hatuoni juhudi zozote za kutembelea Kata yetu na kutatua kero zetu, au mnasubiri muda wa Uchaguzi ufike?!
Tafadhalini, Amkeni, Tatueni Kero Hizi za Wananchi –

Wapiga Kura wa Kibaha Mji.
 
Back
Top Bottom