Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,898
- 31,969
BURIANI BABA, RAFIKI NA MZUNGUMZAJI WANGU BALOZI ABBAS KLEIST SYKES
Mwezi October 1999 nilikuwa Dubai na nikikaa Carlton Hotel.
Siku moja jioni simu yangu ikalia.
Walikuwa BBC London Idhaa ya Kiswahili wanataka kunihoji kuhusu Mwalimu Julius Nyerere ambae wakati ule alikuwa amelazwa St. Thomas Hospital, London.
Ulikuwa mwaka wa pili toka kitabu changu, ‘’The Life and Times of Abdulwaid Sykes (1924- 1968) The Untold Story of the Muslim Struggle Aganst British Colonialism in Tanganyika,’’ kichapwe na kitabu hiki kikawa kimenifanya nifahamike na sababu kubwa ni kuwa kilikuja na historia mpya ya yeye Mwalimu Nyerere mwenyewe, historia ya TANU na historia nzima ya kudai uhuru wa Tanganyika.
Kitabu kilimweeleza Mwalimu Nyerere kwa namna ambayo hakuna mwandishi alipatapo kufanya hivyo.
Hii nadhani ndiyo ikawa sababu ya BBC kutaka kunisikia nikimzungumza Mwalimu Nyerere.
BBC wakawa wanataka tuzungumze kidogo kuhusu Mwalimu na jinsi Watanzania walivyoathirika na ile hali ya Mwalimu kuwa kwenye matibabu Uingereza.
Katika kipindi kile cha maradhi ya Mwalimu akiwa hospitali kila siku habari ya hali yake ilikuwa inatolewa na kwa kweli sote tukifuatilia kwa karibu sana hadi pale alipofariki tarehe 14 Oktoba 1999.
Kishindo chake kilikuwa kikubwa hakijapatapo kutokea na mazishi ya Mwalimu hayapata kutokea halikadhalika simanzi iliyoonyeshwa na Watanzania haijapatapo kutokea.
Umma mkubwa usio na kifani ulijitokeza kupokea jeneza lake Uwanja wa Ndege na maelfu ya watu walijipanga pembeni ya barabara kutoa heshima zao wakati jeneza lake lilipokuwa linapita kuelekea nyumbani kwake Msasani.
Mimi nilikuwa Tanga nikifuatilia kwenye TV na binafsi fikra nyingi zilipita katika kichwa changu.
Mimi sikupata kujuana na Mwalimu lakini katika utafiti wangu wa maisha ya Abdul Sykes na harakati za uhuru nimemjua kwa karibu Mwalimu Nyerere kushinda wale waliokuja kuwa karibu na yeye baada ya uhuru.
Katika utafiti nimekutana na Mwalimu Nyerere ndani ya Nyaraka za Sykes na ndani ya nyaraka hizi nimesoma barua zake akiwa Rais wa TAA na kisha TANU katika miaka ya mwanzoni ya 1950, nimezungumza na Ally Sykes na Dossa Aziz na Mama Daisy (mke wa Abdul Sykes) watu waliokuwanae toka siku ya kwanza wanaanza mapambano ya kudai uhuru.
Katika mikoa ya Tanzania nilikokwenda kwa utafiti nimekutana na kuzungumza na watu waliokuwanae bega kwa bega katika siku hizo za mwanzo wakati Mwalimu Nyerere ndiyo anaanza harakati za kudai uhuru wa Tanganyika akiwa kijana wa miaka 30.
Wakati naangalia TV usiku mmoja wakionyesha ndege ya Air Tanzania Corporation (ATC) iliyokwenda kuchukua mwili wa Mwalimu Nyerere London camera ikapita kwa Abbas Sykes kwa haraka lakini nilimtambua bila wasiwasi wowote kuwa ndiye yeye.
Wakati ule yeye alikuwa ndiye Mwenyekiti wa ATC nafasi aliyoteuliwa na Rais Benjamin Mkapa.
Nilikuwa na kawaida kila nikija Dar es Salaam kutoka Tanga lazima nipite ofisini kwa Bwana Ally Sykes kumjulia hali kisha niende nyumbani kwa Balozi Abbas Sykes.
Safari hii nilikwenda kwa Balozi Sykes kwa nia khasa ya kutaka kujua safari yake ya London kwenda kuchukua mwili wa Mwalimu Nyerere.
Bwana Abbas tukiwa mimi nimekaa kwenye kiti changu ninachokipenda ndani ya ukumbi wake, kiti ambacho kinanipa mandhari ya mchanga mweupe wa bahari na bahari yenyewe na yeye kama kawaida amekaa kwenye kiti cha baba mwenye nyumba kwani huwa siku zote ndicho kiti chake nilianza mazungumzo kwa kumpa pole kwa msiba wa Mwalimu Nyerere.
Balozi Sykes akaitikia ile pole yangu kisha akasema, ‘’Unajua mimi kama Mwenyekiti wa ATC nilitiwa katika msafara wa kwenda kuuchukua mwili wa Nyerere.
Ingekuwa si hii nafasi yangu ya uenyekiti nisingepata fursa na heshima ile kwani hawa viongozi walioko madarakani hawajui kuwa Nyerere sisi ni ndugu yetu.’’
Nilijua bila ya kuuliza kuwa ile, ‘’sisi,’’ Balozi alikusudia wao Sykes Brothers.
Nilikuwa sijapatapo kumsikia Bwana Abbas akijinasibisha udugu na Nyerere.
Mara zote alipokuwa akieleza harakati za kudai uhuru alikuwa akimweleza Nyerere katika nafasi ya urafiki wake na kaka yake Abdul na kama kiongozi wa TANU, hili la udugu ndiyo siku ile nalisikia kwa mara ya kwanza.
‘’Mimi nimejaaliwa kumuona Nyerere siku ya kwanza kaja kwetu pale Mtaa wa Aggrey na Sikukuu kaja kumuona Bwana Abdul akiwa kaongozana na Joseph Kasella Bantu na kuanzia hapo tukawa kama ndugu mama yake Bi. Mugaya akafahamiana na mama yetu na akawa anamtembelea mama nyumbani kwake pamoja na Sophia dada yake Nyerere.
Nikajuana na Joseph mdogo wake na Mama Maria Nyerere ambae alikuja kuwa shoga mkubwa wa Mama Daisy.’’
Bwana Abbas alipomaliza utangulizi huu na hapa alinistua kwani ingawa vifo siku zote vinatokea lakini huwa hatupendi kusikia vile vitu vya karibu vinavyomgusa maiti kama jeneza sanda na kadhalika.
Bwana Abbas akanieleza hali ilivyokuwa ndani ya ndege, ‘’Mohamed Nyerere nimejuananae kuanzia mwaka wa 1952 mimi kijana wa miaka 23 mdogo sana hata Bwana Abdul alikuwa mdogo kwa Nyerere.
Ndani ya ndege tuliweka sanduku lililokuwa na mwili wake mbele kabisa tumelifunika na bendera ya Tanzania.
Ilikuwa tabu sana kwangu kukwepa kulitazama sanduku lile lenye mwili wa Nyerere.
Kila mara fikra zinakwenda mbele na kurudi nyuma zinakwenda mbele zinarudi nyuma namkumbuka Nyerere kijana na Bwana Abdul kijana wote vijana wako pale nyumbani kipindi kile ameacha kazi na siku za mwanzo za TANU.
Endapo mtu angelinambia kwa wakati ule kuwa Nyerere atakuja kuwa kiongozi mkubwa barani Afrika ingekuwa tabu kwangu kuamini kuwa mambo yale waliyokuwa wanayanzungumza wakipanga na kuoangua yatakuja kuwa makubwa kwa kiasi kile kilichofikia.
Nimekuwa na Nyerere kwingi Ulaya katika mikutano na nimeshuhudia kwa macho yangu viongozi wenzake na watu maarufu duniani wanavyokuwa wakiwa mbele yake.
Kwangu mimi ile ilikuwa historia inafunguka mbele ya macho yangu ya mtu niliyemuona akitembea kwa miguu mitaa ya Gerezani akiwa na mimi au na Bwana Abdul wakienda kumuona huyu au yule.
Mtu yeyote angeangaia mikutano ile ya TANU mingine ikifanyika kwa Mzee Clement Mtamila aliyekuwa Mwenyekiti wa TANU pale Mtaa wa Kipata na Sikukuu wajumbe wakiwa akina Bi. Tatu bint Mzee na Bi. Titi Mohamed, Iddi Faizi Mafungo, Nyerere akiwepo na Dossa na Mzee Rupia haikuwa rahisi kuwaza kuwa Muingereza tutamtoa na Tanganyika itajitawala.
Nimekaa ndani ya ndege namwagalia Mama Maria.
Mama Maria amezeeka kawa mtu mzima sana kichwa chote cheupe.
Mama Maria alikuwa kazeeka hata kumpita Mama Daisy nikawa najisemea moyoni huenda labda kwa ajili ya kumuuguza mumewe.
Ilikuwa miaka mingi hatujaonana.
Namkumbuka Mama Maria siku zile msichana mwembamba mrefu, picha inanijia yuko na Mama Daisy wakati mwingine uani jikoni wanapika.
Nakumbuka Mama Daisy akimwambia Maria kuwa wakitoka nje kwenda mahali lazima wajitande kufunika vichwa vyao.
Wengi tuliokuwa pamoja miaka ile wametangulia mbele ya haki.
Nalitazama sanduku lililobeba mwili wa Nyerere namkumbuka Yusuf Bakis kijana wa Bantu Group aliingia hadi Halmashauri Kuu ya TANU lakini alikuwa matata Nyerere akamtoa.
Zuberi Mtemvu na yeye alikuwa katika Halmashauri Kuu na akawa anakwaruzana na Nyerere.
Nyerere akataka atolewe Halmashauri Kuu lakini Mzee Rupia akamtetea, siku zile Mzee Rupia Makamu wa Rais wa TANU.
Mzee Rupia tukimuheshimu sana na kama hataki jambo alikuwa hapingwi.
Kwetu sisi Mzee Rupia, Rajab Diwani walikuwa kama baba zetu kwa kuwa walikuwa wakifahamiana na baba yetu na akifika dukani kwake na kuhudhuria ile barza ya wazee maarufu kama Aziz Ali.
Uzee katika chama siku zile ulikuwa na nguvu sana achilia mbali mbali Baraza la Wazee wa TANU chini ya mwenyekiti wake Sheikh Suleiman Takadir.
African Association sisi ilikuwa kama chama chetu baba yetu alikuwa na ushawishi mkubwa katika chama kile na alipotoka katika uongozi chama kikawa chini ya uongozi wa Mwalimu Thomas Saudtz Plantan kama Rais na Clement Mtamila akiwa Katibu.
Bwana Abdul na Hamza Mwapachu walivyokuja kufanya mapinduzi na kumtoa madarakani Thomas Plantan ambae kwetu sisi alikuwa ni baba ikawa kama vile watoto wa Kleist wamewapindua ndugu zao watoto wa Plantan.
Kuwa sisi ni watoto wa Kleist hili lilitupa sisi nguvu kubwa sana katika TAA hadi kufikia TANU.
Hakuna ambacho sisi hakuwa tunakijua katika TAA.
Hawa akina Plantan na sisi ni ndugu kabisa babu zetu ndiyo walioingia Tanganyika kama askari mamluki chini ya Kamanda Mjerumani, Herman von Wissman kuja kuwasaidia Wajerumani kwenye vita yao na Bushiri na Mkwawa.
Baba zetu ni kizazi cha kwanza cha Wazulu waliozaliwa Tanganyika.
Baada ya vita hivi kumalizika na Wajerumani sasa wanatawala Tanganyika hili jeshi la Wazulu likawa kambini likijulikana kama Germany Constabulary na mkuu wa jeshi hili akiwa Affande Plantan baba yao Thomas Saudtz Plantan, Schneider Abdillah Plantan na Ramadhani Mashado Plantan.
Ukweli utabaki kuwa kama Nyerere asingepokelewa na sisi Dar es Salaam na sisi tukamkubali asingeweza kupata uongozi wa TAA wala TANU na historia ya Nyerere na Tanganyika kama nchi ingekuwa nyingine kabisa.
Nyerere aliitoa mbali sana TANU na kuipitisha kwingi na alikuwa na watu waliojitolea kwake na kwa Tanganyika kwa dhati ya nafsi zao – Mzee Rupia, Dossa, Bwana Abdul na Bwana Ally.
Safari ya kurudi Dar es Salaam kutoka London tukiwa na mwili wa Nyerere ilikuwa ndefu sana kwangu.
Nikisinzia na kuamka na nikiamka kumbukumbu nyingi zikinija za furaha na za masikitiko.
Inanijia picha ya Bi. Titi Mohamed kafungwa maisha kisha namuona Bi. Titi Mohamed tuko Mnazi Mmoja miaka ya mwanzo ya TANU.
Uwanja umefurika na wananchi wanamsubiri Nyerere apande jukwaani ahutubie.
Tuko chini ya jukwaa Nyerere anatuambia kuwa leo hana la kusema.
Anamwangalia Bi. Titi kisha anasema, ‘’Titi hebu panda wewe uzungumze leo sijisikii vizuri.’’
Bi. Titi anapanda kwenye jukwa, msichana mdogo wa kipwani siku zile za mwanzo akivaa baibui jukwaani.
Bi. Titi alikuwa mzungumzaji anashindana na Nyerere kwa kusema.
Uwanja unawaka moto kwa vimondo anavyorusha Bi. Titi.
Waingereza wanasimangwa kuwa hawana kwao wanang’ang’nia nchi za wenzao.
Nyerere kwa hotuba ya Bi. Titi anachukua ‘’cue’’ kutoka kwake anapanda jukwaani na anapita mle mle alimopita Bi. Titi lakini kwa staili yake.
Mimi nilikuwa kijana mdogo sana mwaka wa 1952 nilipomjua Nyerere ni bwana mdogo wa kutumwa na kaka zangu pamoja na Nyerere kuwafanyie mengi, ‘’Abbas lete kile nenda kwa fulani,’’ nk.
Kiasi kuwa Nyerere alipoacha kazi na kuja kukaa kwetu mimi ndiye niliyehamishwa kwenye chumba changu kumpisha nami nikenda kwenye nyumba yetu nyingine.
Pale jirani tulikuwa na nyumba mbile nyingine Kirk Street na New Street pale lilipo Jumba la Ushirika.
Hii nyumba ya Bwana Abdul kwa viwango vya nyakati zile ilikuwa nyumba ya kusifika.
Ilikuwa na mlango mkubwa ukiangalia Mtaa wa Aggrey ambao ndiyo wa kuingilia nyumba kubwa kisha kulikuwa na mlango mwingine ukiangalia Sikukuu Street, huu ulikuwa ndiyo mlango wa kuingia kwangu kwenye nyumba ndogo yenye chumba na varanda yake.
Hapa ndipo alipokaa Nyerere mwaka wa 1955 hadi alipotafutiwa nyumba Magomeni Majumba Sita.
Nyumba hii imeacha historia kubwa sana kwani hakuna mtu mashuhuri wa nyakati zile ambae alikuwa hajakaribishwa katika nyumba ile hadi Wazungu maofisa wa kikoloni.
Bahati mbaya sana historia hii le haitakiwi.
Hamza Mwapachu kafariki mapema sana mwaka mmoja baada ya uhuru mwaka wa 1962 na halikadhalika Bwana Abdul akafariki mwaka wa 1968.
Hawa ndiyo wangeliweza kuieleza historia ya TANU kwa uhakika wake.
Bahati mbaya sana inaelekea kama vile Nyerere hakuipenda sana historia hii.
Ni katika maajabu mengi na qudra ya Allah kuwa katika ndege nzima ile na naamimi Tanzania nzima ni mimi peke yangu niliyekuwa hai ambae nilimuona Nyerere toka siku ya kwanza anakuja kwetu kuonana na Bwana Abdul nikawa na yeye kwa takriban kwa miaka 40 hadi siku ile nakwenda London kuchukua maiti yake kurudi nayo Dar es Salaam kwa mazishi.
Kuwa leo nakuhadithia historia hii yote haya ni mipango ya Allah.’’
Miaka inakimbia ishafika miaka 20 toka Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere afariki dunia na sasa ninavyoandika mazungumzo yangu na Balozi Abbas Sykes yeye ameshatimiza miaka 90.