Arusha: Prof. Kitila na Angela Kairuki kuongoza Kongamano la Uwekezaji katika Sekta ya Utalii na Ukarimu

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,884
12,133
Kitila.jpeg
Kufuatia agizo la Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alilolitoa Aprili 4, 2024 akiwaapisha viongozi mbalimbali alitoa maelekezo mahususi kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, kuhusu kuhamasisha uwekezaji katika sekta ya utalii kwa kushughulikia changamoto ya upatikanaji wa vyumba vya kulala kwa wageni wanaotembelea Mkoa wa Arusha na Tanzania.

Waziri wa nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo (Mb.), kesho April 30, 2024, kwa kushirikiana na Angela Kairuki (Mb.), Waziri wa Maliasili na Utalii na Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Arusha ataongoza Kongamano la Uwekezaji katika sekta ya Utalii na Ukarimu katika Ukumbi wa Gran Melia mkoani Arusha.

Kongamano hilo, litajumuisha Viongozi wa Serikali na Wadau katika Sekta ya Utalii kwa lengo la kuona namna ya kukuza uwekezaji katika sekta hiyo hususani kuongeza ujazo wa vitanda (Bed Capacity) ili kuwakarimu watalii na wageni jijini Arusha na Tanzania kwa ujumla.

Itakumbukwa kuwa, tangu kuzinduliwa kwa “Program ya Tanzania the Royal Tour” Aprili 2022, kumekuwepo na ongezeko kubwa la watalii wa ndani na nje ya nchi mathalani, Mwaka 2022 Watalii wa nje walikuwa 1,550,333, lakini mwaka 2023 wakaongezeka kufikia 1,881,823 huku idadi ya Watalii wa ndani ikiongezeka kufikia zaidi ya milioni 1.9 mwaka 2023. Hata hivyo, pamoja na ongezeko hilo, hotel zilizopo nchini zina uwezo wa vitanda 132,676.

Vile vile, tangu programu ya Tanzania the Royal Tour kuzinduliwa, sekta ya utalii imechangia ongezeko la fedha za kigeni kiasi cha zaidi ya dola za Marekani bilioni 3.4 kwa mwaka 2023, ukilinganisha na dola bilioni 2.5 kwa mwaka 2022, kiasi hicho kimeongezeka kutoka dola za Marekani bilioni 1.3 mwaka 2021. Kongamano hilo, linatarajia kutatoa suluhu ya namna ya kuongeza vitanda (Bed capacity) ili kukabiliana na changamoto za huduma za malazi.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji.
 
Back
Top Bottom