SI KWELI Unaweza kupunguza Makali ya UKIMWI kwa kubadilisha damu

Baada ya kuitathmini taarifa hii, tumebaini kuwa si ya kweli.
Wakuu mko vyede?

Kuna kipindi fulani hili suala lilizuka sana kuwa wanaoishi na HIV hasa matajiri walikuwa wanaenda South Afrika kubadilisha damu ili kupunguza makali ya ugonjwa huo.

HIV-Lifecycle.jpg

Hii ilikuwa kweli? Maana mpaka leo naamini walikuwa wanafanya hivyo, ila swali likaja wanabadilishaje? Wanamtoa damu nusu halafu wanamuongezea nyingine ambayo haina virusi ama?

Msaada wenu kung'amua hili wajuvi.
 
Tunachokijua
HIV (human immunodeficiency virus) ni kirusi kinachoshambulia mfumo wa kinga mwili, na kumfanya mhusika awe na kinga dhaifu zinazomfanya awe kwenye hatari kubwa ya kuugua na kuambukizwa magonjwa mengine.

Virusi hivi visipodhibitiwa mapema husababisha Upungufu wa Kinga Mwilini (UKIMWI). Ni muhimu kufahamu kuwa sio kila mwenye virusi (HIV) huugua UKIMWI, bali hali hii hutokea kwenye hatua ya mwisho ya maambukizi, kipindi ambacho kinga ya mwili huwa dhaifu.

ili mtu mwenye VVU aweze kutambulika kama amefikia hatua ya kuwa na UKIMWI, mambo mawili ya msingi huzingatiwa;
  1. Idadi ya nakala za seli za CD4 ziwe chini ya 200 kwa kila mililita ya damu (200 cells/mm3).
  2. Aanze kupata maambukizi ya magonjwa nyemelezi yanayokwenda sambamba na VVU.
Takwimu za Maambukizi
Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2022, inakadiriwa kuwa zaidi ya watu milioni 39 duniani walikuwa wanaishi na VVU, 630,000 walipoteza maisha kwa ugonjwa huu na watu milioni 1.7 walipata maambukizi mapya.

Aidha, tangu kugunduliwa kwake, zaidi ya watu milioni 40.4 wamepoteza maisha kutokana na janga hili.

Njia za Maambukizi
Maambukizi ya VVU humpata mtu baada ya kukutana na mazingira yanayoruhusu ubadilishanaji wa virusi husika. Mtu anaweza kuambukizwa virusi hawa kutoka kwa mwathirika kwa;
  • Kushiriki tendo la ndoa
  • Kushirikiana vitu vyenye ncha kali
  • Kubadilishana damu
  • Mama kwenda kwa mtoto wakati wa kujifungua na kunyonyesha
Tiba za ugonjwa huu
Matibabu ya VVU/UKIMWI huhusisha matumizi ya dawa za kufubaza virusi ambazo kitaalam huitwa Antiretroviral Therapy (ART).

Ikitumiwa kama ilivyoagizwa, ART hupunguza kiwango cha VVU kwenye damu hadi kiwango cha chini sana, ambacho huweka mfumo wa kinga kufanya kazi na kuzuia magonjwa.

Hii inaitwa ukandamizaji wa virusi au udhibiti mkubwa wa virusi, unaofafanuliwa kuwa na chini ya nakala 200 za VVU kwa mililita ya damu.

Watu wenye VVU ambao wanajua hali zao, wanaotumia dawa kama walivyoagizwa pamoja na kufuata masharti sahihi ya kuishi wanaweza kuishi maisha marefu na yenye afya.

Aidha, hadi sasa, kuna watu watano pekee waliowahi kuthibitika kupona ugonjwa huu kupitia matibabu ya upandikizaji wa uboho kutoka kwa kundi dogo la watu wasio na sifa ya kuambukizwa VVU.

Kubadili damu kunaweza kupunguza makali ya VVU?
Nadharia ya kubadilisha damu ili kupunguza makali ya VVU/UKIMWI imekuwepo wa muda mrefu hasa miaka mwanzoni mwa miaka ya 2000, kipindi ambacho matibabu ya kutumia dawa za kufubaza virusi hayakuwa maarufu sana.

Hii inathibitishwa pia na Mdau wa JamiiForums ambaye Februari 19, 2008 aliweka chapisho linalohoji uwepo wa aina hii ya matibabu. Mdau huyu alihoji;

"Swali lenyewe ni hivi ni kweli kwa baadhi ya ndugu zetu ambao ni waathirika wenye uwezo kifedha, eti wanaweza kwenda nje na kubadilisha damu nzima ya mwili wao na kuwekewa damu mpya kabisa thats why wanaweza kuishi kwa muda mrefu wakiwa na afya njema na its very impossible kugundulika kuwa ni waathirika..."

Madai haya hayatofautiani sana na hoja ya Precious Diamond aliyoianzisha tena Agosti 10, 2023 kwenye jukwaa hili akitaka ufafanuzi wa suala hili kama linawezekana, na jinsi lilivyofanywa.

Kwa mujibu wake, Wagonjwa wengi wenye uwezo mkubwa wa kifedha walikuwa wanaenda Afrika Kusini kubadili damu kama sehemu ya kupunguza makali ya ugonjwa huu.

JamiiForums imefuatilia suala hili na kubaini kuwa Kitaalam haliwezekani. Huu ni uvumi usio na uhalisia kisayansi.

Kama ilivyobainishwa awali, njia pekee iliyopo hadi sasa inayoweza kutumiwa na waathirika wa VVU/UKIMWI ni kutumia dawa za kufubaza virusi.

Ubadilishaji wa damu (kuongezewa damu) hufanyika kwa watu walio na uhitaji wa damu kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ajali, upasuaji, maambukizi makubwa ya magonjwa, upungufu wa damu (anemia) na magonjwa mengine ya kijenetiki kama hemophilia.

Ufafanuzi huu hautofautiani na jibu la mdau wa JamiiForums, Kizimkazimkuu alilotoa Machi 17, 2008 wakati akichangia jukwaani mjadala wa Februari 19, 2023. Alisema;

"Mtaalam, kubadilisha damu kitaalamu huitwa exchange blood transfusion. Hii, mara nyingi hufanywa kwa watu wenye matatizo yatokanayo na kasoro za cells mabalimbali katika damu.

Hata hivyo, sijapata kusoma literature yeyote inayotaja kuwa exchange blood transfusion ni njia mojawapo ya kutibu UKIMWI.

Unapaswa kuelewa yafuatayo kuhusu UKIMWI:
1. Virusi vya UKIMWI huishi katika chembechemebe za damu ziitwazo Lymphocytes zenye CD4 receptors.
2. Pia huishi katika lymphoid tissues ambapo huko virusi huwa dormant na pia dawa (ARV) haziwezi kuwafikia.(Ndio maana ARV hunywewa kwa maisha yote ili kuzuia virusi walio dormant kujitokeza na kuzailiana mara mtu aachapo dawa). Hivyo, kubadili damu hakutaweza kuondoa virusi kutoka katika lymphoid tissues na sehemu zingine kitaalamu huita sanctuary sites.

Fahamu kuwa kuna dawa nyingi (ARV) zenye ubora mkubwa, matokeo mazuri na side effets chache katika nchi zilizoendelea kuliko hizi tunazotumia nchini. Pengine hao unaowasema wanatumia hizi.

Hivyo, kumalizia, kwangu mimi hili la kubadili damu naliona kama uzushi tu."


Majadiliano ya aina hii yaliwahi pia kuibuka Februari 3, 2011 kwenye chapisho ndani ya JamiiForums.com lenye kichwa cha habari "Sababu ya kifo cha Steven Kibona na Gilman Rutihinda" ambapo baadhi ya wachangiaji walidokeza uwepo wa aina hii ya tiba kwa waathirika wa VVU/UKIMWI ambapo Ozzie alitoa ufafanuzi mzuri unaopinga madai haya.

"Mkuu na watu wengine, katika matibabu ya HIV hakuna suala la kubadirisha damu. Nenda uendano hilo suala halipo kisayansi.

Tena kwa dawa za HIV zilizopo sasa, ikiwa mwathirika wa VVU anatumia vizuri dawa, unaweza usimpate kabisa mdudu wa HIV ndani ya damu isipokuwa katika baadhi ya cells zenye CD4+ maeneo yaliyofichika katika mwili.

Naamini kama kweli ulipewa taarifa kama hiyo, huyo mtu aliyekupa taarifa hiyo si daktari; na kama ni daktari basi ni daktari kihiyo maana taarifa alizokupa si sahihi."


Kwa kurejea tafiti mbalimbali, michango ya watumiaji wa JamiiForums.com na maelezo ya wataalamu wa afya ambayo JamiiForums imeyapata, ni dhahiri kuwa aina hii ya matibabu haipo na haiwezi kupunguza makali ya VVU.
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom