NADHARIA Ulaji wa viazi vitamu huongeza nafasi ya kupata watoto Mapacha

Taarifa hii ni nadharia tu, tumeitolea ufafanuzi kwa kadiri ilivyowezekana
Ulaji wa viazi vitamu kwa kipindi kirefu unadaiwa kusaidia uzalishwaji wa mayai mengi kwa Mwanamke na hivyo kupelekea kupata watoto mapacha.

Jiji la Igbo-Ora lililopo nchini Nigeria ni jiji lenye mapacha wengi na Nigeria imepewa jina la mji mkuu wa Mapacha Duniani kwa kuwa na watoto mapacha wengi zaidi kuliko eneo lolote duniani huku viazi vitamu vikiliwa zaidi nchini humo.

figure-1.png

Ni kweli kuwa Viazi vitamu huongeza homoni aina ya ‘phytoestrogen’ ambayo huchangia kwenye kupevusha yai zaidi ya moja kwa wakati mmoja hivyo kusababisha kuzaliwa kwa watoto mapacha?
 
Tunachokijua
Mzunguko wa hedhi ya mwanamke hutawaliwa na vipindi vingi vinavyoongozwa na mabadiliko ya homoni za mwili ambazo kwa kiasi kikubwa ndio huratibu zoezi zima la mzunguko huo.

Miongoni mwa vipindi muhimu ni kile kinachohusisha utoaji wa mayai yaliyokomaa/pevuka ili ujauzito uweze kutungwa. Kipindi hiki kwa lugha ya mtaani iliyo maarufu sana hufahamika kama kipindi cha siku za hatari.

Ni wakati ambao mwanamke huwa kwenye uwezekano mkubwa zaidi wa kupata ujauzito ikiwa atashiriki tendo la ndoa na mwanamme ambaye atamwaga mbegu zake za kiume.

Aina za mapacha
Ikiwa mwanamke atatoa yai moja kisha likaungana na mbegu ya kiume, ambalo baadae likigawanyika kutengeneza watoto wawili, mapacha wa kufanana watazaliwa. Hata hivyo, mapacha wasiofanana hutokea pale ambao mwanamke hutoa mayai zaidi ya moja kisha yatarutubishwa na mbegu tofauti za kiume.

Uhusiano wa Jamii ya Igbo-Ora na uzao wa Mapacha
Igbo-Ora ni mji unaopatikana kusini magharibi mwa Nchi ya Nigeria kwenye jimbo la Oyo.

Aidha, mji huu hupatikana umbali wa kilomita 80 kaskazini mwa jiji la Lagos. Hufahamika zaidi kwa jina la utani la "Makao makuu ya mapacha Duniani".

Umaarufu wake ulianza kuibuka miaka ya 1972-1982 baada ya Daktari Bingwa wa Masuala ya wanawake kutoka Uingereza Patrick Nylander kugundua kuwa katika kila kundi la wanawake 1000 wanaojifugua kwenye mji huo, 45-50 kati yao walikuwa na watoto mapacha.

Takwimu hizi zilikuwa kubwa sana ikilinganishwa na Nchi za Ulaya zilizokuwa na wastani wa wananawake 16 katika kila kundi la wanawake 1000 wanaojifungua huku Marekani ikiwa ni wanawake 33 katika kundi la wanawake 1000 wanaojifungua.

Chanzo hasa ni nini?
Utafiti wa AA Omonkhua (2020) wenye kichwa cha habari "Community perceptions on causes of high dizygotic twinning rate in Igbo-Ora, South-west Nigeria: A qualitative study" ulibainisha mambo matatu yanayofafanuliwa na wananchi wa eneio hilo kuwa miongoni mwa vyanzo vya kutokea kwa idadi kubwa ya mapacha. Mambo hayo ni rehema za Mungu, Sababu za Urithi na Ulaji wa baadhi ya vyakula.

Mathalani, mwaka 2019, Kehinde Oyedepo (15) akihojiwa na kituo cha Reuters alisema "Kuna mapacha wengi sababu ya majani ya mmea wa bamia tunayokula". Oyenike Bamimore alinukuliwa pia akisemayeye binafsi alijifungua seti 8 za mapcha kutokana na ulaji wa majani ya Bamia.

Baadhi ya vyakula vingine vinavyohusishwa kuchochea suala hili ni Mihogo na Viazi vinavyopatikana maeneo hayo ambavyo hutumika kwa namna nyingi ikiwemo kama Amala, Garri, Fufu n.k

Vyakula hivi hutajwa kuwa na homoni nyingi za phytoestrogen zinazofanana na homoni za kike (estrogen) ambazo huwafanya wanawake watoe mayai zaidi ya moja kwenye mzunguko wa hedhi zao.

Vyakula hivi vinaweza kumfanya Mwanamke ajifungue watoto Mapacha?
Tafiti nyingi zimefanyika kuchunguza athari za homoni tajwa kwenye mwili wa binadamu. Mathalani, utafiti wa WN Jefferson et al (2012) wenye kichwa cha habari "Reproductive Consequences of Developmental Phytoestrogen Exposure" unabainisha kuwa homoni hizi zinaweza kuathiri afya ya uzazi kwa namna mbalimbali. Hata hivyo, athari hizi hutofautiana kulingana na muda wa matumizi,wingi wa dozi na umri wa mhusika.

Utafiti huu pamoja na tafiti nyingine hazijathibitisha moja kwa moja kuwa Phytoestrogen huchangia uzalishwaji wa mayi mengi kwenye mzunguko wa hedhi.

Aidha, hakuna pia uhusiano wa moja kwa moja wa Majani ya Bamia na kumfanya mwanamke atoe mayai mengi, hali inayoweza kuchangia kutokea kwa mapacha.

Katika kutafuta undani wa suala hii, JamiiForums imezungumza pia na wataalamu wa afya, ikiwemo Madaktari Bingwa wa masuala ya Wanawake waliothibitisha kuwa hadi sasa hakuna uhusiano wa viazi vitamu, mihogo au majani ya bamia katika kumfanya mwanamke apate ujauzito wa watoto mapacha.

Hivyo, kutokana na maelezo haya na uwepo wa takwimu halisi kutoka kwenye eneo la Igbo-Ora ambazo hazina mashaka, JamiiForums inachukulia jambo hili kama nadharia inayopaswa kufanyiwa uchunguzi zaidi wa kitafiti ili kubaini ukweli wake.

Similar Discussions

3 Reactions
Reply
Back
Top Bottom