Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), kuzindua Maktaba Mtandao (TIE online library.) Jumamosi tarehe 30/03/2019 katika viwanja vya TET Mwenge Dar

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,925
12,208
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
TAASISI YA ELIMU TANZANIA KUZINDUA MAKTABA MTANDAO

Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) inatarajia kufanya uzinduzi wa Maktaba Mtandao (TIE online library.) Sherehe za uzinduzi zitafanyika siku ya Jumamosi tarehe 30/3/2019 kuanzia saa Tatu kamili asubuhi (3.00) katika viwanja vya TET vilivyopo eneo la Mwenge. Mgeni rasmi katika sherehe za uzinduzi huo atakuwa Mh. Prof. Joyce Ndalichako (Mb), Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia.
IMG_20190329_113907_8.jpg

Mkurugenzi mkuu Daktari Aneth A Komba akiongea na Waandishi wa habari, kulia kwake ni Mtafiti Kwangu M Zabrone ma kushoto kwake Peter Msangi

Malengo ya kuanzisha Maktaba mtandao ni kuwa na nyenzo mbadala na ya haraka ya usambazaji wa Machapisho ya TET katika Shule za Serikali na Binafsi za Jamhuri ya Mungano wa Tanzania pamoja na wadau wengine wa elimu. Maktaba hii itakuwa na faida mbalimbali ikiwemo:

1. Urahisi wa upatikanaji wa machapicho ya Kiada, Ziada, Mitaala,Mihtasari, Kiongozi cha Mwalimu, Miongozo mbalimbali, Moduli za kufundishia na kujifunzia kwa Wanafunzi, Walimu na watumiaji wengine;

2. utunzaji wa kudumu wa machapisho mbalimbali;

3. kupunguza gharama kwa shule katika kuendesha maktaba zao yaani badala ya kununua vitabu vingi na kujenga makabati mengi na kutumia nafasi kubwa ya kuhifadhi vitabu sasa shule itatumia nafasi ndogo kwa kuweka komputa na vifaa vingine vya electronic;

4. kurahisisha upatikanaji wa taarifa na mrejesho kutoka kwa watumiaji wa machapisho ya TET, hivyo kupanua wigo wa uboreshaji wa kazi na huduma za TET na hivyo kuiwezesha TET kuboresha huduma zake;

5. kuhamasisha matumizi ya TEHAMA kama nyenzo ya kujifunzia na kufundishia shuleni;

6. kukusanya takwimu sahii za watumiaji hasa Walimu na Wanafunzi ambazo zitasaidia TET kufanya bajeti na kutekeleza majukumu yake.

Matumizi ya maktaba
Shule za Serikali zitatumia maktaba hii bure ikiwa ni kuunga mkono juhudi za serikali ya Awamu ya Tano ambayo moja ya sera zake katika elimu ni Elimu Bure. Shule binafsi zitatozwa gharama kidogo kabisa kwa ajili ya kutumia Maktaba hii.Kwa mfano kwa shule za Msingi gharama haitazidi shilingi 400,000 kwa shule moja kupata machapisho 48 ya kiada pamoja na machapisho 2000 ya ziada.

Mmiliki wa shule wakati wa kufanya malipo atachagua kitabu au vitabu anavyotaka kisha ataenda kwenye kapu lake la manunuzi na kuchagua shule anayoinunulia. Baada ya hapo ataomba namba ya malipo kisha ataweza kulipia gharama kwa kutumia mitandao ya simu kama M-Pesa, Tigo Pesa, Airtel Money, Halo Pesa, Z- Pesa au Banki. Kwa mitandao ya simu mtumiaji atachagua kufanya malipo/lipia bili kisha atachagua namba 5 kufanya malipo ya serikali.

Maudhui ya Maktaba
Maktaba mtandao inayotarajiwa kuzinduliwa itajumuisha vitabu mbalimbali vya kiada kuanzia ngazi ya elimu ya awali, msingi na elimu ya Sekondari (Kidato cha 1-6) vinavyo chapishwa na TET na ambavyo ni lazima kutumika shuleni.
Vilevile kutakuwepo vitabu vya ziada kutoka nchini na nchi nyingine pamoja na machapisho mengine.

Watumiaji wataweza kutumia vitabu hivyo kupitia maktaba hiyo kwa mtindo wa kusoma na kuazima kupitia mtandao (on line).

Maktaba mtandao itapatikana katika simu za kiganjani baada ya kuipakua kupitia App ya Play store kwa Android.

Watumiaji watahitajika kufanyiwa usajili wa awali na Taasisi kisha wao watakamilisha usajili kwa kutoa taarifa sahihi kama majina yao, namba za simu, barua pepe na wanapoishi. Iwapo watumiaji watapata shida katika usajili au matumizi ya maktaba watawasiliana na kitengo cha huduma kwa wateja cha Taasisi ambao watapatikana kupitia mitandao ya kijamii kama facebook, twiter, instagram na whatsapp. Anwani za mitandao hii zinapatikana kwenye tovuti ya Taasisi ambayo ni tie.sc.tz.

Mpaka sasa katika kipindi cha majaribio kilichoanza mwezi wa kumi na mbili, 2018 mpaka Januari 2019 Taasisi imewafanyia usajili wa awali shule 6,639 za serikali za awali, msingi na sekondari katika mikoa tisa ya Tanzania Bara na Mmoja wa Zanzibar (Dar es salaam, Pwani, Simiyu, Dodoma, Kagera, Ruvuma, Rukwa, Lindi, Geita, Unguja Kusini).Kwa upande wa walimu Taasisi imesajili jumla ya walimu 88,596. Shule hizi na walimu hawa watatakiwa kukamilisha usajili ili kuweza kuitumia maktaba hii. Kwa upande wa shule binafsi Taasisi itashirikiana na TAMONGSCO yaani Umoja wa mameneja na wamiliki wa shule sisizo za Serikali kukamilisha usajili wa shule za Awali, Msingi na Sekondari Tanzania Bara na Visiwani ndani ya siku 15 kutoka sasa.
Maktaba hii imezingatia hatua mbalimbali za kiusalama wa kimtandao ikiwemo kumzuia mtumiaji kupakua vitabu pasipo idhini ya taasisi, kumzuia mtumiaji kufanya marekebisho katika machapisho, kuvamia akaunti ya mtu kwaajili ya kupata taarifa zake na kutumia machapisho pasipo kulipia.

Kwa kuandaa maktaba hii serikali ya Tanzania imekuwa nchi ya kwanza kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati kuandaa na kuratibu mfumo wa Kielectroni kwa usambazaji wa machapisho kwa shule za serikali, binafsi na watumiaji wengine. Utafiti unaonesha kuwa nchi nyingi duniani zinategemea kampuni binafsi katika kuratibu mifumo hii.

IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI NA MAWASILIANO.

29/3/2019
 
Back
Top Bottom