Songwe: Polisi yawakamata wanaotoa Mikopo ya Kausha Damu

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,879
12,133
Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe kwa kipindi cha mwezi Aprili, 2024 linawashikilia watuhumiwa 424 kwa tuhuma ya kujihusisha na matukio ya Ukatili wa kijinsia, Uvunjaji, Wizi, mauaji, utapeli kwa njia ya mtandao, Kujifanya mtumishi wa serikali, Kughushi nyaraka, dawa za kulevya, ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani na kusababisha ajali za vifo.

kufuatia malalamiko ya wananchi kuhusu huduma za mikopo midogo maarufu kama kausha damu tumeendelea na operesheni kali ya kukusanya ushahidi na kuwakamata wamiliki wa makampuni na watu binafsi wanaotoa huduma ndogo za kifedha bila kuwa na leseni.

Katika operesheni hiyo inayoendelea kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania tumefanikiwa kuwakamata Watuhumiwa sita (06) ambao wanafanya biashara ya huduma ya mikopo pasipo kuwa na leseni toka Benki Kuu ya Tanzania Kwa mujibu wa Sheria ya Mikopo Midogo, Sheria Namba 10 ya Mwaka 2018 ya Tanzania, Kifungu cha 16 ambacho kinapiga marufuku biashara ya mikopo midogo pasipokuwa na leseni ya Benki kuu.

Aidha, watoa huduma wa mikopo midogo midogo waliosajiliwa wanapaswa kufuata taratibu za usajili na miongozo iliyowekwa na Benki Kuu ya Tanzania.

Watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo kwa Mujibu wa Sheria ya Huduma ndogo za Fedha ya Mwaka 2018 na Kanuni zake za Mwaka 2019 na adhabu kwa mtu atakayepatikana na hatia ni faini isiyopungua Shilingi Milioni Ishirini lakini isiyozidi Milioni Mia Moja au Kifungo kwa kipindi kisichopungua Miaka Miwili lakini kisichozidi Miaka Mitano Jela au vyote kwa pamoja.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe linawashikilia wanaume sita (06) waliokamatwa kwa tuhuma za Kughushi nyaraka mbalimbali ambazo ni barua ya kusitishwa mikataba ya kazi katika maeneo yao ya kazi, mihuri ya taasisi binafsi na za serikali ikiwa ni pamoja na fomu za kuchukulia mafao katika taasisi ya NSSF ili waweze kujipatia pesa kwa njia ya udanganyifu. Watuhumiwa hao walikamatwa kwa nyakati tofauti tofauti katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania kuanzia tarehe 22 hadi 29, Februari 2024 baada ya kutenda makossa hayo Mkoani Songwe. Upelelezi wa mashauri haya bado unaendelea na pindi utakapokamilika watafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi.

Vilevile Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limemkamata mwanaume mmoja mwenye umri wa miaka 41, mwandishi wa habari, mkazi Magomeni Dar es salaam Aprili 13, 2024 huko mtaa wa Majengo mapya Wilayani Momba kwa kujitambulisha kuwa yeye ni afisa usalama wa taifa kutoka Ikulu ndogo Dar es salaam kwa lengo la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kwa kupita Mikoa mbalimbali na kukutana na watu wanaotarajia kugombea nafasi mbalimbali kuelekea kipindi cha uchaguzi 2024-2025. Upelelezi wa shauri hili umekamilika na mtuhumiwa alifikishwa mahakamani April 19, 2024 kwa hatua zaidi.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe katika kipindi cha mwezi Aprili, 2024 limeendelea kupata mafanikio mahakamani kwa watuhumiwa wa makosa mbalimbali ambapo jumla ya watuhumiwa 18 wamepatikana na hatia na kufungwa gerezani kama ifuatavyo:

Mtuhumiwa Osea Mbalwa Sungura, miaka 35 na Shomari Amiri Hamis, miaka 32 walifikishwa mahakamani kwa kosa la kubaka kesi namba 83/2023 na 9231/2024 na kuhukumiwa miaka 30 jela katika mahakama ya Wilaya ya Songwe na Mbozi kila mmoja.

Mtuhumiwa Kelvin Disco Msukuma, miaka 30 na wenzake 08 walifikishwa mahakamani kwa kosa la kujaribu kufanya unyan’ganyi wa kutumia silaha kwa kesi namba 31/2023 na kuhukumiwa miaka 15 jela katika mahakama ya Wilaya ya Songwe kila mmoja.

Mtuhumiwa Emmanuel Nikutusya Kibona, miaka 24, alifikishwa mahakamani kwa kosa la wizi kesi namba 11022/2024 na Frank William Mwasambile alifikishwa mahakamani kwa kosa la uvunjaji kesi namba 11035/2024 na wote kwa pamoja wamehukumiwa miaka 08 jela katika mahakama ya Wilaya ya Ileje na Songwe kila mmoja.

Mtuhumiwa Sufuph Ausi Mzee, miaka 30, alifikishwa mahakamani kwa kosa la wizi kesi namba 9694/2024 na kuhukumiwa miaka 07 jela katika mahakama ya Wilaya ya Mbozi.

Mtuhumiwa Yusuph Laiton Simbeye, miaka 28 na mwenzake Given Shilonde Mkisi, miaka 32 walifikishwa mahakamani kwa kosa la kuvunja nyumba usiku na kuiba kwa kesi namba 98/2023 na wamehukumiwa miaka 05 jela katika mahakama ya Wilaya ya Momba kila mmoja.

Mtuhumiwa Emmanuel Steward Kahinga, miaka 35 na mwenzake Neto Alinani Buya miaka 29 walifikishwa mahakamani kwa kosa la kuvunja nyumba usiku na kuiba kwa kesi namba 80/2023 na wamehukumiwa miaka 04 jela katika mahakama ya Wilaya ya Momba kila mmoja.

Katika muendelezo wa misako dhidi ya dawa za kulevya jumla ya watuhumiwa 25 walikamatwa na dawa za kulevya aina ya bhangi kilo 45 na gramu 905 na bidhaa za magendo zenye thamani ya zaidi ya Tshs.2,700,000/= ikiwemo mifuko ya plastiki na sukari aina ya whitespoon za Zambia.

Wakati huo huo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe linawashikilia watuhumiwa 11 kwa makosa ya wizi wa pikipiki 4 ambazo ni pikipiki aina ya Huasha rangi nyekundu yenye chasis no LFFCKO107AZD10966 ikiwa haina namba za usajili, pikipiki aina ya Kinglion nyekundu yenye usajili namba MC.683 DCP, pikipiki aina ya Fekon yenye namba za usajili MC 305 AWR rangi nyekundu, pikipiki moja aina Kingboss nyekundu yenye namba za usajili MC 981 DWQ.

Vilevile kulikuwa na makosa 07 ya Uvunjaji ambapo walikamatwa watuhumiwa 14 na vielelezo ambavyo ni magunia 151 pamoja na pikipiki mbili zenye namba za usajili MC.192 DYD aina ya Kinglion rangi nyeusi na MC. 695 CMS aina ya Boxer rangi nyeusi ambazo zilitumika kubebea magunia hayo kutoka kiwandani MCCCO, tv aina G-STAR nchi 22 pamoja na sabufa aina ya MR-UK, tv aina AILYOINS nch 32 yenye rangi nyeusi pamoja na sabufa nyeusi Sea Piano, TV inch 19 aina ya zone, Sabufa 01 aina ya Zoom na Spika 02 ndogo, Chaja ya Laptop aina ya Dell 01, Pikipiki yenye namba za MC 513 BDC aina ya T- BETTER ikiwa haina blue card pamoja na tv mbili flat screen aina ya zone, pikipiki yenye namba za usajili MC 366 DTB aina ya Honda, Pasi moja ya umeme, Stata ya Gari 01. Upelelezi wa baadhi ya kesi hizi umekamilika na watuhumiwa wamefikishwa mahakamani.

Sambamba na hayo kwa kipindi cha Aprili, 2024 jumla ya makosa mbalimbali ya usalama barabarani 4,465 yalikamatwa na watuhumiwa baadhi walifikishwa mahakamani na wengine kulipa faini.

Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Songwe kuwa zoezi la operesheni ya kuwabaini na kuwakamata wafanyabiashara wote wanaojihusisha na kutoa huduma ya mikopo pasipo kuwa na leseni toka benki kuu ya Tanzania na wale wanaochukua kadi za benki kama sehemu ya dhamana jambo ambalo ni kinyume na sheria ni endelevu lakini pia linatoa onyo kwa watu wote wanaojihusisha na biashara hiyo kuacha mara moja kwani Jeshi la Polisi litachukua hatua za kisheria dhidi yao ikiwemo kuwafikisha mahakamani.

Pia Jeshi la Polisi linatoa rai kwa wananchi wa Mkoa wa Songwe ambao wanajihusisha na uhalifu na kughushi nyaraka za kiserikali na sizizo za kiserikali kuacha mara moja kwani hawatoweza kukwepa mkono wa sheria.
 
Back
Top Bottom