Shirika la Bima la China (SINOSURE) kuisaidia Tanzania kutafuta Fedha za ujenzi wa SGR Lot 5

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,488
8,353

Shirika la Bima la China - SINOSURE linaendelea na taratibu za upatikanaji fedha za kugharamia ujenzi wa Kipande cha Tano cha Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Isaka hadi Mwanza chenye urefu wa Kilomita 341 na kuonesha nia ya kusaidia upatikanaji fedha za ujenzi wa kipande cha sita cha ujenzi wa Reli hiyo kutoka Tabora hadi Kigoma chenye urefu wa zaidi ya Kilomita 411.

Hayo yameelezwa jijini Dodoma na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. @mwigulunchemba (Mb) alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe kutoka Shirika la Bima la China (SINOSURE), ukiongozwa na Meneja Msaidizi wa Shirika hilo, Bi. Bi Xiaonan.

Dkt. Nchemba amelishukuru Shirika la SINOSURE kwa kuendelea na taratibu za upatikanaji fedha za ukamilishaji wa mradi huo kwa kuwa vipande hivyo ni muhimu katika ukamilishaji wa mradi huo.

“Tumekuwa na kikao kizuri katika kujadiliana ushirikiano wa kimaendeleo kati ya Tanzania na China hususan kwenye eneo la ugharamiaji wa miradi ya kimkakati ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Reli ya Kisasa Kipande cha Tano kutoka Isaka hadi Mwanza ambapo SINOSURE ilikubali kushiriki katika upatikanaji wa fedha wa kukamilisha ujenzi huo na kipande cha Tabora hadi Kigoma”, alisema Dkt. Nchemba.

Alisema Wizara ya Fedha kwa niaba ya Serikali inawahakikishia SINOSURE na Serikali ya China kwamba itaendeleza ushirikiano na kuimarisha Maendeleo ya Uchumi kwa manufaa ya wananchi wa pande hizo mbili.

Dkt. Nchemba alisema kuwa Timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Fedha itaendelea kushirikiana na Timu kutoka Shirika hilo ili kuhakikisha vipande hivyo muhimu vinakamilika.

Alisema kuwa Reli ni moja ya miradi ambayo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeuweka kwenye miradi ya kielelezo na kipaumbele.

Aidha, ameshukuru ujio wa Meneja huyo Msaidizi wa SINOSURE pamoja na utayari wa Shirika hilo kushirikiana na Serikali katika ugharamiaji wa miradi ya maendeleo nchini.

Kwa upande wake Meneja Msaidizi wa Shirika la Bima la China (SINOSURE), Bi. Bi Xiaonan, amesema Shirika lake lipo tayari kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha miradi ya kimkakati inatekelezwa kwa ufanisi.
 
Back
Top Bottom