Sera mpya ya elimu na ukombozi wa fikra kwa mtanzania

Muttaline

Member
Apr 21, 2012
80
10
Katika moja ya matamko yaliyotelewa na Serikali kupitia Sera Mpya ya Elimu ni kuifanya lugha ya Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia katika ngazi zote za elimu nchini.

TAMKO:

3.2.19. Lugha ya Taifa ya Kiswahili itatumika kufundishia na

kujifunzia katika ngazi zote za elimu na mafunzo na
Serikali itaweka utaratibu wa kuwezesha matumizi
ya lugha hii kuwa endelevu na yenye ufanisi katika
kuwapatia walengwa elimu na mafunzo yenye tija
kitaifa na kimataifa.

Kwa imani yangu nia hii njema itamfanya mwanafunzi na mtanzania kujikomboka kifikra. Pamoja na kwamba hili jambo limeonekana kuchelewa lakini naamini hatujachelewa sana. Mbio za kuelekea kujitegemea na kisha kupata maendeleo endelevu.

Aliwahi kusema mtaalamu wa lugha Robinson (1996) kuwa; namnukuu.. “The use of African languages in complementary and equitable fashion, alongside other languages, will be part
of the full development of Africa's own genius and of the continent's search for its own path of development.” Ni ukweli uliowazi kwamba baada ya ukoloni wa muda mrefu sasa Afrika pia itafute namna ya kujinasua kwenye makucha ya wakoloni.

Lugha ni nyenzo muhimu sana katika mchakazo mzima wa kujifunza. Tafiti mbalimbali zinaonesha kwamba mwanafunzi hujifuza na kuelewa kwa kupitia lugha mama. Kiswahili Tanzania sio tu lugha yenye kutuunganisha bali pia ni lugha ambayo inazungumzwa na kueleweka na kila mtanzania. Hivyo elimu kupitia lugha mama ni sababu ya mafanikio ya mwanafunzi kielimu kuwa mazuri sana, hasa pale lugha hii inapokuwa inafahamika vizuri kwa mfundishaji na mfundishwaji.

Kwa namna hali ilivyo sasa (ambapo lugha ya kufundishia katika shule za msingi ni Kiswahili; na Kiingereza katika shule za sekondari) mhitimu anakuwa katika hali ya kutozifahamu vizuri lugha zote mbili yaani Kiswahili na Kiingereza. Ni aibu iliyoje mhitimu wa Chuo Kikuu kushindwa kujieleza kwa Kiswahili(hapa wengi huwa wanachanganya lugha) pia hata kwa Kiingereza(hapa utakutana na makosa mengi sana ya sarufi)

Lugha za kigeni, Kiingereza miongozi mwazo zina umuhimu mkubwa katika dunia tuliyonayo nyakati hizi na hata nyakati zijazo. Miongozi mwa umuhimu wa lugha ya kiingereza ni kwamba ni lugha inayotumika sehemu nyingi duniani katika biashara, diplomasia, misada ya masomo(scholarships) n.k. Pia ujuzi wa lugha ya Kiingereza imekuwa kama alama ya utambulisho wa usomi na nguvu fulani katika jamii.

Ukweli kwamba lugha hii ni ya kigeni hauwezi kupingwa. Waswahili husema nguo ya kuazima haistili makalio. Ndio maana kwa kiasi kikubwa lugha hii haifundishiki (katika maana ya umilisi) kwa waalimu. Mwalimu asiye mzawa wa lugha hii ni ngumu kuimudu hasa katika matamshi na weledi wa msamiati. Hapa nchini wale waliopitia katika mifumo ya kuwawezesha kuielewa vizuri lugha hii ni wachache sana. Kitu ambacho hupelekea waonekane kama tabaka jingine ndani ya jamii moja. Pia sote hapa ni shahidi kwamba pamoja na kuwa idadi kubwa ya wanachama humu ndani ni wahitimu walau wa shahada za kwanza lakini wengi wetu hatuwezi kujenga hoja na kuiendeleza kwa lugha ya Kiingereza. Ni wazi pia kuwa ndio maana hata mada yinazotetwa humu ndani kwa lugha ya Kiingereza kuwa hazipati wachangiaji wengi kupitia lugha hiyo hiyo.

Lengo langu sio kupinga matumizi ya lugha ya Kiingereza nchini mwetu lahasha. Lugha ya Kiingereza ifundishe kama yanavyofundishwa masomo ya Uchumi, Historia, Fizikia n.k. Tena ufundishwaji wake uboreshwe ili tuweze kupata wasomi wenye uwezo wa kuwasiliana na wenye ujuzi wa kuitumia lugha hii kuliko hali ilivyo sasa ambapo wengi hujikuta wanaisoma lugha hii kwa kukariri tu na mwisho hujikuta wanakosa ujuzi wa kuwasiliana kwa kutumia lugha hii.
Kwa nini ni muhimu kutumia Kiswahili badala ya Kiingereza kama lugha ya kufundishia? Kiswahili kitamuwezesha mwanafunzi kuwa na fikra huru, Kitamuwezesha kuelewa vizuri somo na taaluma, kitamzidishia umakinifu (critical thinking), Kiswahili kitapanuka sana kimatumizi kama kikitumika katika elimu ya juu, na matumizi ya lugha isiyoyako katika kujifunza hukunyima fursa ya kufikiri sawasawa kwa kuwa huwezi kufikiri dhana/wazo katika lugha ambayo huilewi vizuri.

Kuna baadhi ya wasomi hutoa hoja mbalimbali za kupinga matumizi ya Kiswahili kama lugha ya kufundishia katika mfumo wetu wa elimu wakidai kwamba Kiswahili hakina misamiati ya kutosha katika taaluma hasa za sayansi, hivyo tuendelee kutumia Kiingereza chenye misamiati hiyo. Hoja hii si ya kweli. Kiswahili kama lugha nyingine chaweza kukopa (Kiswahilify) misamiati ya sayansi kutoka lugha mbalimbali ikiwa kuna haja ya kufanya hivyo. Neno kama computer linaweza kuwa kompyuta n.k. Hii ni tabia ya lugha, lugha hukopa. Msamiati mkubwa wa teknolojia katika lugha ya Kiingereza umetoka katika lugha ya Kilatini.Nchi kama Urusi, Ujerumani, Uswizi, Japani, Norway n.k hufundisha sayansi kwa kutumia lugha zao na wanatengeneza na kuzalisha wanasayansi wazuri sana kuliko hata Tanzania ambayo inatumia lugha ya Kiingereza. Pia kuna hoja ya kuwa ni vigumu kwa nchi inayoendelea kuwa na fedha za kufasili vitabu ambavyo vimeandikwa kwa lugha ya Kiingereza labda kutokana na ukweli kwamba taaluma nyingi zimeingizwa kutokea huko. Hoja hii haina ukweli wowote pakiwa na utashi wa kisiasa kazi ya tafrisi itafanyika, na kwa taarifa tu kazi hiyo ilishaanza kufanyika chini ya ufadhili wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) na kazi mbalimbali kama vile za Kemia na Fizikia zilifasiliwa. Mwenye kuhitaji kuiona miswada ya kazi hizo anaweza kwenda BAKITA ataoneshwa.
Kuna uwezekano wa msomaji kuifasili kazi yoyote kutegemeana na mahitaji yake hasa pale lugha ya Kiingereza itakapokuwa imefundishwa vizuri na kueleweka vizuri. Huko mashuleni masomo mengi yanayofundishwa kwa Kiingereza walimu huyafasili kwa kiswahili ili yaeleweke kwa wanafunzi wao. Hivyo kazi ya tafsiri inawezekana.

Nihitimishe kuwaomba watanzania kufikiri sana juu ya tulikotoka tulipo na tuendako na kisha tufanye maamuzi yenye busara. Nafahamu kwamba sio rahisi maamuzi ya namna hii kukubalika mapema kwa sababu kuna mifano; huko Uingereza haikuwa rahisi kukubali Kiingereza kitumike kama lugha ya kufundishia enzi za Chaucer. Waingereza waliona Kiingereza hakikuwa na msamiati wa kutosha kutumika katika taaluma kama ilivyokuwa Kilatini. Hapa kwetu pia haikuwa rahisi kukubali Kiswahili itumike kama lugha ya kufundishia katika shule za msingi kwa kisingizio cha kukosa msamiati. Wataalamu wakafanyia kazi msamiati na mwisho hakuna mtu anayehoji juu ya msamiati katika ngazi ya shule za msingi.

Mwisho niseme kuwa watanzania tujenge utamaduni wa kukuza na kuthamini amali zetu. Aliwahi kusema; (Robert Armstrong 1963) 'If we are ashamed of our own language, then we must certainly lack that minimum of self−respect which is necessary to the healthy functioning of society'. Akaongezea.. “if the young people come to despise their father's language, the chances are that at the same
time they will reject their father's wisdom”.

Na, Muttaline 2015
 
Back
Top Bottom