- Source #1
- View Source #1
- Source #2
- View Source #2
Katika mitandao ya kijamii nimeona video inayohusishwa na Rais Mpya wa Senegal, Bassirou Diomaye Faye, akikemea Ufaransa kuwa ni wakati wa kuondoka bara la Afrika.
Video hiyo inamuonesha Rais Faye akiimbia Ufaransa kuwa "Inakuwa wakati wa Ufaransa kuinua magoti yake kutoka shingoni mwetu na kumaliza ukandamizaji huu usio wa haki. Karne nyingi za mateso, biashara ya binadamu, ukoloni, na ukoloni mamboleo vimesababisha mateso yasiyohesabika. Ni wakati wa kumaliza mzunguko huu wa ukandamizaji,"
Wachangiaji wengi kwenye video hizo zinazozunguka mitandaoni walionesha furaha kwamba Rais Faye ameonesha msimamo imara dhidi ya Ufaransa kulikandamiza bara la Afrika.
Video hiyo inanipa mashaka.
- Tunachokijua
- Video imeibuka kwenye mitandao ya kijamii ikimhusu mwanasiasa mmoja nchini Senegal akiiomba Ufaransa kutoingilia masuala ya ndani ya Senegal. Kwa mujibu wa maelezo yaliyoambatanishwa kwenye video hii, Mwanasiasa anayezungumziwa hapa ni Bassirou Diomaye Faye, Rais wa sasa wa Taifa hilo.
Katika video hiyo, Mtu anayedaiwa kuwa Rais mteule wa Senegal anaonekana akizungumza Kiingereza, ingawa midomo yake na sauti ya video hiyo haviendani.
"Ni wakati mwafaka kwa Ufaransa kuachana na suala hili na kukomesha uonevu huu usio wa haki. Karne nyingi za taabu, biashara haramu ya binadamu, ukoloni na ukoloni mamboleo zimesababisha mateso yasiyopimika. Ni wakati wa kukomesha mzunguko huu wa uonevu.”
Aliongeza kuwa Ufaransa inapaswa kuacha mara moja kuingilia masuala ya Senegal.
Anayeonekana ni Bassirou Diomaye Faye?
Ufuatiliaji wa JamiiCheck umebaini anayeonekana si Rais wa Senegal, Bassirou Diomaye Faye bali ni Ousmane Sonko, kiongozi wa upinzani wa Senegal wa chama cha PASTEF ambaye kwa sasa ni Waziri Mkuu wa nchi hiyo..
Kupitia utafutaji wa Kimtandao kwa kutumia nyezo ya Google Image Search, JamiiCheck imebaini kuwa video hii siyo ya sasa, ilichapishwa kwa mara ya kwanza mtandaoni Julai 2, 2017 na Ukurasa wa Mtandao wa YouTube wa Senegal7.
Wakati wa mkutano huo, Sonko alizungumza kwa lugha ya Wolof na Kifaransa na si Kiingereza kama inavyodaiwa. Hata hivyo, kauli alizotoa zinafanana na kile ambacho video hii isiyo halisi inavyobainisha.
Katika kutafuta asili ya video hii, JamiiCheck ilikutana pia na ukurasa wa Mtandao wa TikTok unaoitwa The New African News ambapo ilichapishwa Novemba 12, 2023.
Teknolojia ya Akili Mnemba imetumika kufanya ulinganisho wa Midomo ya Sonko na tafsiri ya Maneno ya kiingereza yanayotamkwa.