JanguKamaJangu
JF-Expert Member
- Feb 7, 2022
- 2,323
- 5,493
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linafuatilia kwa karibu sana mchezo wa soka siku ya Jumamosi tarehe 20 Aprili 2024 saa 11:00 jioni kwenye uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es Salaam. Mchezo huo ni wa soka wa watani wa jadi kati ya klabu ya Yanga na Simba zote za Dar es salaam na utakaochezwa.
Kuelekea mchezo huo, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam limechukua tahadhari zote za kiusalama kabla, wakati na baada ya mchezo. Usalama siku ya mchezo utakuwa wa kiwango cha juu, maeneo yanayozunguka uwanja ndani, nje na barabara za kuingia na kutoka uwanjani. Ukaguzi utakuwa wa hali ya juu kabla ya kuingia uwanjani.
Hairuhisiwi mtu yeyote kwenda uwanjani na silaha ya aina yoyote, isipokuwa baadhi ya vyombo vya dola vyenye jukumu la usalama eneo hilo.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi Kanda Maalum limemkamata Abdulshahib Hegga @ GB 64 kwa tuhuma za kuhamasisha watu kufanya vurugu katika mchezo huo kupitia kipande cha video alichokisambaza kwenye mitandao ya kijamii. Mtuhumiwa huo anahojiwa kwa kina.
Jeshi la Polisi Kanda maalum ya Dar es salaam linatoa tahadhari kwa mashabiki wa soka watakaoanzisha vurugu zozote au kujihusisha na vitendo vya kihalifu ndani au nje ya uwanja watashughulikiwa haraka kwa mujibu wa sheria.
Imetolewa na ;
Muliro J. MULIRO - SACP
Kamanda wa Polisi
Kanda Maalum ya Dar es Salaam