SoC03 Njia za mawasiliano kwenye tovuti za taasisi za umma ziboreshwe

Stories of Change - 2023 Competition

EDOGUN

JF-Expert Member
Jul 9, 2023
256
299
Edogun Mzalendo ni kijana wa miaka ishirini na minne, muhitimu wa stashahada ya sayansi ya kompyuta na mmiliki wa steshenari ndogo inayopatikana mjini Kahama.

Ni miaka miwili tu imepita toka afungue steshenari yake hiyo lakini amejizolea umaarufu mkubwa sana kutokana na kipaji chake cha kucheza na kompyuta. Ni mara nyingi tu amekuwa akiletewa kazi nyingi za kompyuta tena wakati mwingine kutoka nje ya mji wa Kahama zisizohusiana kabisa na biashara yake mama ya steshenari.

Siku moja kijana Edogun wakati alipokuwa akimsaidia binti mmoja kutuma maombi ya ajira ya ualimu katika tovuti moja ya serikali inayojihusisha na upokeaji wa maombi ya ajira toka kwa wahitimu wa fani mbalimbali
aligundua kuwa tovuti hiyo ilikuwa na udhaifu fulani katika utendaji wake uliomuwezesha mtu yeyote kuweza kuingia kwenye akaunti ya mtumiaji mwingine bila idhini endapo tu angetumia nywira ya "$1234&"

Baada ya kuugundua udhaifu huo, kijana Edogun aliamua kuwasiliana na wasimamizi wa tovuti hiyo ili wafanye maboresho ya kuuondoa udhaifu huo kabla haujagunduliwa na wadukuzi.

Alizinakili namba za simu zilizoko kwenye ukurasa wa mbele wa tovuti hiyo na kuzipigia lakini simu haikupokelewa haraka kama alivyotegemea.Alisubiri kwa muda wa kama nusu saa kisha akarudia kupiga simu lakini hali ilikuwa kama mwanzo,simu yake haikupokelewa.

Kijana Edogun alifanya zoezi hilo la kuwapigia wasimamizi wa tovuti hiyo kwa siku zaidi ya kumi lakini hali ilikuwa ile ile;simu zake kutokupokelewa. Baada ya kuona simu zake hazipokelewi, kijana Edogun aliamua kutumia njia ya barua pepe ili kuwasiliana na wasimamizi wa tovuti hiyo,akaandika barua pepe yenye maelezo ya kutosha juu ya udhaifu aliokuwa ameugundua na kuituma.

Baada ya kutuma barua pepe hiyo yenye maelezo yote ya udhaifu aliokuwa ameugundua,Edogun aliamini kuwa tatizo hilo litarekebishwa ndani ya saa/siku chache tu lakini hali haikuwa hivyo.Kila alipoitembelea tovuti ile kwa muda wa zaidi ya siku ishirini aligundua kuwa udhaifu ule haukuwa umeondolewa.

Basi, kwa sababu Edogun hakuwa na njia nyingine ya mawasiliano zaidi ya namba za simu na anwani ya barua pepe zilizoko kwenye kurasa za tovuti hiyo,aliamua tu kuendelea na mambo yake mengine huku akiamini huenda labda wataalam watakuwa wametingwa na majukumu mazito ya kurekebisha udhaifu aliouibua kiasi cha kushindwa hata kupokea simu wala kuzijibu barua pepe zake.

Siku nyingine tena, kijana Edogun alipokuwa akimsaidia kijana mwingine kutuma maombi ya ajira ya Afya kwenye tovuti ile ile aligundua kuwa kurasa za tovuti hiyo zilichukua muda mrefu sana kufunguka na wakati mwingine hazikufunguka kabisa.

Kwa utaalam wake mdogo, Edogun aligundua kuwa hali hii ilisababishwa na mambo makuu mawili:-

Kwanza tovuti hiyo kuundwa kwa lugha ya kompyuta ya asp.net,

pili, taarifa za waombaji wa ajira kuhifadhiwa kwenye kanzidata ya mysql ambayo haiwezi kuhimili kuhudumia watumiaji wengi kwa wakati mmoja.

Ili kurekebisha tatizo hilo ilitakiwa taarifa za waombaji zihifadhiwe kwenye kanzidata kama vile mongoDb na pia node.js itumike badala ya asp.net kwani inaweza kuwahudumia watembeleaji wengi kwa wakati mmoja.

Pia, kijana Edogun aligundua kuwa tovuti hiyo inapokea taarifa nyingi zisizohitajika toka kwa watumiaji mfano jina la shule aliyosoma muombaji wakati taarifa hizo zingeweza kutolewa kwenye tovuti nyingine ya www.necta.go.tz kwa kutumia teknolojia ya API nk.

Siku nyingine tena kijana Edogun alipokuwa akimsaidia mzee mmoja kufanya usajili wa jina la biashara kwenye tovuti ya BRELA aligundua kuwa tovuti hiyo haiwezi kufunguka kwenye baadhi ya vivinjari na pia baadhi ya viunganishi/link vilivyoko kwenye tovuti hii vilikuwa havifunguki.

Edogun akaamua kuwasiliana na wasimamizi wa tovuti hiyo kwa kupiga namba za simu zilizoko kwenye kurasa za tovuti hiyo lakini kwa bahati mbaya mpokeaji wa simu hakuwa na uelewa wa kutosha kuhusiana na utendajikazi wa tovuti hivyo aliishia tu kuuliza maswali mwisho akakata simu kabisa.

Matatizo tajwa hapo juu yaliyogunduliwa na kijana Edogun Mzalendo hayakuwa hayo peke yake bali yalikuwa ni sehemu ndogo tu za changamoto chungu nzima wanazokutana nazo watembeleaji wa tovuti nyingi za taasisi za umma.

Baada ya kuutambua ukweli huo kuwa tovuti nyingi za taasisi za umma kutokuwa na njia za haraka,uhakika na rahisi za mawasiliano pindi mtumiaji akutanapo na changamoto katika utumiaji;Kijana Edogun aliamua kuandika barua pepe kwenda kwa katibu mkuu wa Wizara ya habari,mawasiliano na teknolojia ya habari akiwa ametoa ushauri na mapendekezo haya:-

-Uundwe mfumo maalum wa kidigitali utakaowawezesha watumiaji wa tovuti za taasisi za umma kuelezea kama wanaridhika na namna tovuti hizo zinavyoendeshwa au kutoa mapendekezo ya kipi kiboreshwe ili kuwa rafiki na salama kwa watumiaji wote.

- Kwenye kila tovuti ya taasisi za umma ziwepo njia tofauti tofauti za mawasiliano kama vile Ujumbe mfupi wa maneno(sms),ujumbe wa sauti(voicemail),whatsapp nk tofauti na sasa ambapo mara nyingi inakuwa ni njia ya simu ya mdomo au barua pepe.

– Kwenye kila tovuti ya umma ziwepo njia maalum za kutoa taarifa za haraka na dharura kama vile taarifa za udhaifu wa kiusalama nk ili ziweze kushughulikiwa kwa haraka kabla madhara hayajatokea.

- Ikiwezekana wawepo wakaguzi maalum watakaokuwa wakifanya kazi moja tu ya kuangalia kama utendaji kazi wa tovuti za taasisi za umma kama uko sawa na unaendana na mabadiliko ya teknolojia.

- Kwenye kila tovuti ya umma viwekwe vitengo tofauti tofauti vya mawasiliano kulingana na changamoto atakayokutana nayo mtumiaji kama vile usalama,malipo nk ili kufanya ushughulikiaji wa taarifa na malalamiko kuwa rahisi.

- Watoa huduma kwa wateja waongezwe kulingana na ukubwa wa tovuti husika.

- Ikiwezekana zitumike njia za kisasa za kiteknolojia kama vile Chatbot na Akili bandia(artificial intelligence) ili kuweza kutatua changamoto za watumiaji wa tovuti hizi kwa wakati

- Malalamiko yote yatakayowasilishwa na watembeleaji wa tovuti hizi yarekodiwe ili baadae yaweze kukaguliwa kama yalishughulikiwa kwa wakati.

Kijana Edogun ana matumaini makubwa kuwa mapendekezo yake yote aliyoyatoa yatashughulikiwa kwa wakati na anaamini kuwa yatazifanya tovuti zote za taasisi za umma kuwa salama na rafiki kwa watembeleaji wake kwani changamoto zote watakazokumbana nazo watumiaji wa tovuti hizo wataweza kuzitolea taarifa kwa urahisi na kwa wakati.​
 
Back
Top Bottom