Mtutura: Mbolea ya Ruzuku haiwafikii wananchi, fedha zinazotengwa zinakwenda wapi?

ACT Wazalendo

JF-Expert Member
May 5, 2014
617
1,541
Waziri Kivuli wa Kilimo, Umwagiliaji na Maendeleo ya Ushirika, Ndugu Mtutura Abdallah Mtutura, ameitaka Serikali ieleze fedha za ruzuku zimepelekwa wapi ikiwa wakulima milioni 2.55 sawa na asilimia 75 ya wakulima waliosajiliwa katika mpango wa ruzuku hawakupata wala kutumia mbolea hiyo licha ya kuwa na sifa
Aidha ndugu Mtutura amesema Halmashauri 41 kati ya Halamashauri 181 kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali hazikupata kabisa mbolea hiyo ya ruzuku na kuitaka Serikali kuingilia kati mfumo wa uagizaji na usambaziji kwa kuiwezesha kibajeti kampuni ya taifa ya mbolea (TFC) kuagiza nje na kusambaza mbolea nchini, kwa ajili ya kuongeza uwezo wa usambazaji wa mbolea unaotokana na kulegalega kwa waagizaji na wasambazaji binafsi.

Waziri Kivuli Mturura ametoa kauli hiyo leo Ijumaa tarehe Mei 03, 2024 wakati akizungumza na waandishi wa Habari jijini Dar Es Salaam juu ya uchambuzi wa bajeti ya Kilimo iliyofanywa na Chama cha ACT Wazalendo, kufuatia Waziri wa Kilimo kuwasilisha bajeti yake jana Bungeni jijini Dodoma

Pia ameitaka Serikali illipe kwa wakati madai ya wasambazaji wa mbolea na kuchukua hatua ya kudumu, kuondoa utegemezi wa mbolea kutoka nje, kwa kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji ili watu waweze kujenga viwanda vya kuzalisha bidhaa hiyo nchini na kuimarisha uzalishaji kwa viwanda vilivyopo.

Akizungumzia kushuka kwa bei za mazao ya wakulima nchini, ndugu Mtutura ameitaka Serikali ipunguze utitiri wa kodi, ushuru na tozo kwenye mazao ili kuwanusuru wakulima. Vilevile, ametaka wakulima washirikishwe kikamilifu kwenye mfumo wa upangaji wa bei kwa kufanyia maboresho vyama vya ushirika ili viwe na uhuru na uwezo wa kuamua juu ya mustakabali wao.

Amesema ACT Wazalendo inaendelea kutoa wito wake kwa Serikali itunge mfumo wa kodi unaoeleweka na usiotetereka (stable fiscal regime) katika sekta ya kilimo ili kuhakikisha mkulima anabakia na sehemu kubwa ya mapato yake.

Juu ya kushuka kwa uzalishaji na kasi ndogo ya ukuaji wa Sekta ya Kilimo Ndugu Mtutura amesema ACT Wazalendo inaiweka kilimo katikati ya vita ya kupambana na umaskini na inaamini Tanzania haiwezi kuondoa umaskini kwa kauli mbiu peke yake bali kwa kuwa na mwono wa wazi katika mipango ya kilimo jambo aliloeleza Waziri Bashe hajaainisha katika hotuba yake ya bajeti

Amesema Waziri Bashe na Serikali ya CCM wanapaswa kulieleza Taifa tunafikiaje kasi ya ukuaji wa sekta ya Kilimo kuanzia Mwaka huu na kuendelea kwa kuwa takwimu zinaonyesha Mwaka jana pekee uzalishaji wa mazao umeshuka kwa asilimia 15 hali inayotia shaka kama sekta ya Kilimo itawezaje kuwa injini ya kuondoa umaskini.

Katika hatua nyengine Ndg. Mtutura ameonesha hofu juu ya msada wa Mchele uliongezwa virutubisho kutoka Marekani katika mradi wa “PAMOJA TUWALISHE” unaotekelezwa katika shule mbalimbali nchini Ameitaka Serikali kutoa kauli ya kusisitiza msimamo wake wa kupinga matumizi ya GMO nchini.

Pia ndugu Mtutura amezungumzia Uporaji wa ardhi ya wakulima na migogoro ya wakulima na watumiaji wengine na kusema inazidi kushika kasi nchini na kuwa tishio kwa wakulima na wazalishaji wa vyakula, hali inayohatarisha usalama wa nchi
Amesema ni lazima Serikali iharakishe na kukamilisha zoezi la kupima, kurasimisha na kumilikisha ardhi kwa wananchi ili kuepusha migongano na mivutano. Vilevile, Mamlaka za Halmashauri zijengewe uwezo stahiki na kuwezeshwa ipasavyo ili ziweze kushugulikia migogoro ya ardhi upesi na kwa ufanisi pamoja na kuhakikisha ardhi imepimwa na kurasimishwa kwa wananchi pamoja na kusitisha tabia ya kupanuwa maeneo ya hifadhi kwa kuwanyang’anya wananchi maeneo yao ya kulisha mifugo na kilimo kwa kuwa upanuzi huo unafifisha jitihada za wafugaji na wakulima katika uendeshaji wa shughuli zao za uchumi.
 
Back
Top Bottom