SoC04 Mkakati huu una tija zaidi katika hifadhi endelevu ya misitu

Tanzania Tuitakayo competition threads

SottoLee

New Member
May 16, 2024
4
0
Kuna nchi ninayotamani kuona ikijengeka, tena kwa kasi. Hii ni Tanzania iliyosheheni miti, misitu na uoto mwingine. Ili kuipata nchi ya aina hii, tunapaswa kutengeneza mikakati madhubuti, na kuisimamia ipasavyo.

Kama nchi nyingine, Tanzania imeshuhudia changamoto kubwa ya mabadiliko ya tabia nchi. Kupukutika kwa misitu na miti kutokana na uvunaji usiokuwa endelevu ni moja ya sababu kubwa za changamoto hii. Athari zake ni pamoja na mafuriko, kukauka kwa mito, ukame na ongezeko la hewa ukaa linalosababisha ongezeko la joto angani.

Kupukutika kwa misitu na miti kunachochewa na ongezeko la kasi la idadi ya watu na shughuli zao zikiwemo za kilimo, ufugaji, na ujenzi; pamoja na biashara kubwa ya mazao ya misitu inayoendelea kukua. Pamoja na shughuli hizo, uharibifu wa misitu unatokana ana ukataji wa miti kwa ajili ya matumizi ya kuni na mkaa majumbani na katika taasisi, umetia fora nchini. Wakazi wa mijini na vijijini wanategemea sana nishati hii, hivyo miti mingi huangamia kwa ajili hii.

Takwimu zilizochapishwa hivi katibuni na gazeti la HabariLeo zinasema asilimia 80 ya familia nchini Tanzania zinatumia nishati ya kuni na mkaa kwa kupikia. Takwimu nyingine zinaonesha kuwa kasi ya uharibifu wa misitu nchini ni zaidi ya hekta 469, 420 kila mwaka. Imedhihirika pia kuwa matumizi ya kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia ndio chanzo kikubwa cha ukataji miti ovyo.

Upo pia utafiti unaoonesha kuwa ili kupata tani moja ya mkaa unaochomwa kienyeji, tani 10 hadi 15 za miti huangamia. Takwimu hii inatisha, ikionesha kuwa nchi yetu inaelekea katika jangwa. Ili kuiokoa misitu, mikakati kabambe inatakiwa kutengenezwa, na kusimamiwa ipasavyo.

Ukweli ni kwamba, kutumia kuni na mkaa kupikia, kuna athari nyingi za kiuchumi, kiafya, kijamii na kimazingira. Pamoja na athari hizi, tafiti zinaonesha kuwa ni asilimia 6.9 tu ya Watanzania ndio wanatumia nishati safi. Wengi wanatumia kuni na mkaa, wakisababisha misitu kukatwa ovyo.

Nimesema, ninatamani kuiona Tanzania iliyosheheni misitu, hivyo ninaiona mikakati mitatu endelevu inayoweza kufanikisha maono haya, na matunda yake yakaonekana mapema, ndani ya kipindi cha miaka mitano!

Mkakati wa kwanza, ni kuchochea matumizi ya mkaa mbadala. Nikiwa ninaandaa andiko hili, nimeusikia mkakati wa Serikali ukilenga kuwahamisha wananchi kutoka kwenye matumizi ya kuni na mkaa, kwenda kwenye nishati safi. Nimeupenda! Hata hivyo, mkakati huo ni kama unalenga kuwaingiza wananchi haraka, na pengine kwa shuruti, kwenye matumizi ya gesi na umeme, kupikia.

Ni maoni yangu kuwa tusiwapeleke wananchi haraka au kwa shuruti kwenye gesi na umeme. Sababu ni kwamba nishati hizi ni ghali, hivyo uzalishaji na usambazaji wake una gharama kubwa, ikizingatiwa uelewa wao mdogo kuhusu nishati safi, na uwezo wao mdogo kifedha.

Kwa kuzingatia bei za majiko ya gesi na umeme, mitungi ya gesi, uduni wa vipato vya Watanzania, na ugumu katika kuvisambaza vitu hivi nchi nzima, ni vigumu nishati hizi kufika na kupokelewa ipasavyo, hasa vijijini. Serikali inapaswa kwanza kushughulika na elimu na gharama hizo, ili bei za vifaa, gesi na umeme viwe rafiki kwa wengi.

Serikali inaweza kupunguza gharama hizi kupitia punguzo la kodi katika uzalishaji wa majiko ya gesi na umeme, na kupitia punguzo la kodi na tozo katika usambazaji wa vifaa hivyo, na gesi yenyewe. Serikali pia iweke ruzuku ili wadau wengi wamudu kuwekeza katika biashara hii.

Kwa sababu hizi, ni wazi muda wa kutosha wa maandalizi unatakiwa, ukijumuisha pia utoaji wa elimu na hamasa kwa wananchi, ya kuanza kutumia nishati safi. Wananchi wanatakiwa kupewa uelewa mkubwa wa manufaa ya kiuchumi, kijamii na kimazingira unaohusu matumizi ya nishati safi.

Gharama na uelewa mdogo, ndivyo vinavyowafanya wananchi kung’ang’ania kuni na mkaa, kwa kuwa wanaweza kuzinunua bidhaa hizi kwa mafungu madogomadogo mtaani, kwa bei nafuu. Kwa sababu hii ndio maana naona msisitizo uwekwe kwanza kwenye matumizi ya mkaa mbadala, wakat serikali na wadau wanachakata njia za kupunguza gharama za gesi na umeme; pamoja na upatikanaji na usambazaji wake.

Matumizi ya mkaa mbadala yanaweza kuanza hata sasa, kwa kuhimiza uanzishwaji wa viwanda vidogovidogo vya kutengeneza majiko banifu, na vya kuzalisha mkaa mbadala. Teknolojia hii si ghali, na tayari ipo nchini, inatakiwa kuendelezwa tu.

Uzuri wa majiko banifu ni kwamba yana uwezo wa kutumia kuni na mkaa huu huu wa sasa, kwa kiasi kidogo sana. Tunaweza kuanza na majiko haya, huku tukiikuza teknolojia hii, na tukiwahamasisha wananchi kuhamia katika mkaa mbadala, na baadaye kwenye gesi na umeme.

Uzuri, malighafi ya kutengeneza mkaa mbadala ni mabaki ya mimea au mazao ambayo yamejaa nchi nzima, mijini na vijijini. Matumizi ya mkaa mbadala yana manufaa, ikiwa ni pamoja na kukuza ubunifu, kuchochea usafi wa miji na vijiji, kuongeza ajira kwa vijana, kupunguza magonjwa ya mlipuko, kujipatia nishati kwa bei nafuu, na kubwa zaidi ni kuilinda misitu.

Manufaa mengine ni kwamba, nishati hii itatengenezwa mijini na vijijini, hivyo gharama ya utengenezaji wa vifaa, na usambazaji wake itapungua. Inatakiwa wananchi wafikiwe huko waliko, waelimishwe kugeuza takataka za mazao kuwa nishati ya kupikia. Halafu, waelimishwe kubadili mitazamo yao ya kung’ang’ania matumizi ya kuni na mkaa, kwa kupikia. Kwa njia hii, nishati hii nafuu itasambaa kwa urahisi nchi nzima, ikilinganishwa na gesi na umeme!

Mkakati wa pili, unahusu hifadhi ya misitu na miti kupitia ufugaji wa nyuki. Tafiti zinaonesha kuwa, kipato kinachotokana na mavuno kiduchu ya mazao katika mashamba ya wananchi wengi vijijini, huwafanya kujiegemeza kwenye biashara ya kuni, mbao na mkaa, hivyo kuirarua misitu.

Ili kuipunguza changamoto hii, ni maoni yangu kuwa ufugaji wa nyuki uhimizwe, nchi nzima, kwenye misitu inayovamiwa ovyo. Kwa njia hii, misitu hii haitakatwa kiurahisi, lakini pia mazao yatokanayo na nyuki, yatatunisha mifuko ya wananchi, hivyo kupunguza utegemezi wao kwenye bidhaa ya kuni na mkaa.

Mkakati wa tatu, unahusu kuongeza hamasa ya upandaji wa miti nchi nzima, ukilenga ushiriki wa watu wote. Tozo na faini zinazotozwa na serikali kutoka kwa watu wanaokata kuni au kuchoma mkaa, zisitumike vinginevyo, bali ziende kugharamia upandaji wa miti.

Miti isipokatwa ovyo, kupitia njia zilizoorodheshwa hapo juu, kisha ikapandwa kwa wingi, nchi hii itajaa misitu. Misitu hii itatupatia pesa kupitia biashara ya hewa ukaa inayoshamiri, kutoka kwa nchi tajiri zinazoongoza kwa uchafuzi wa anga. Sheria na kanuni, kuwabana wanaokwamisha mikakati hii, zina nafasi pia katika kuongeza ufanisi wa maono haya.
 
Mkakati wa kwanza, ni kuchochea matumizi ya mkaa mbadala. Nikiwa ninaandaa andiko hili, nimeusikia mkakati wa Serikali ukilenga kuwahamisha wananchi kutoka kwenye matumizi ya kuni na mkaa, kwenda kwenye nishati safi. Nimeupenda! Hata hivyo, mkakati huo ni kama unalenga kuwaingiza wananchi haraka, na pengine kwa shuruti, kwenye matumizi ya gesi na umeme, kupikia.
Mkaa mbadala ndio unamaanisha huuu?
Screenshot_20240516-152601_Chrome.jpg

Hivi ni kwa nini unaishiaga kwenye maonesho hatuuoni mtaani? Mkaa kitofa.


Mkakati wa tatu, unahusu kuongeza hamasa ya upandaji wa miti nchi nzima, ukilenga ushiriki wa watu wote. Tozo na faini zinazotozwa na serikali kutoka kwa watu wanaokata kuni au kuchoma mkaa, zisitumike vinginevyo, bali ziende kugharamia upandaji wa miti.
Nakubali✔
 
1715863621934.png

Ndio, huu ndio mkaa mbadala. Haupatikani kwa wingi, kwa kuwa wengi hawajaujua. Lakini, wazalishaji wengi kwa sasa ni wale wenye uwezo mdogo, hivyo huzalishwa kwa uchache. Serikali ikiamua, teknolojia hii itasambaa hadi vijijini, kuwafikia walio wengi, na kuwahamisha kutoka ktk matumizi ya kuni na mkaa.
 
Back
Top Bottom