Mahakama ya Rufaa inaenda kupitia upya usahihi wa haki ya raia wa kigeni kumiliki ardhi nchini Tanzania kwa njia ya kurithi

Apr 26, 2022
70
104
Unakumbuka ile kesi ambayo Mahakama Kuu ya Tanzania iliamua kwamba Raia wa Kigeni wanaweza kumiliki ardhi nchini Tanzania kwa njia ya kurithi (where High Court ruled that non-citizen heirs could own land by way of inheritance)?

Uamuzi ambao ulitolewa na Mahakama Kuu mwaka 2011. Lakini serikali haikukata rufaa wala Bunge halikutunga sheria yoyote inayotengua huo uamuzi, na hata muswada ulipoenda bungeni, kipengele cha kuzuia wageni kumiliki ardhi hakikupitishwa kuwa sheria.

Baada ya miaka kama nane (8), sasa Mwanasheria mkuu wa serikali ameibuka anaiomba Mahakama ya Rufaa ipitie upya (ifanyie Revision) ule uamuzi wa Mahakama Kuu ili kujiridhisha usahihi wake.

(Makala hii Imeandaliwa na kuletwa kwako nami, zakariamaseke@gmail.com - Advocate candidate)

Kisheria, muda wa kuomba Revision ni siku 60 tangu siku maamuzi yanapotoka. Kwa hiyo Mwanasheria Mkuu wa Serikali hapa alikua yuko nje ya muda.

Sasa kwa sababu muda wa kufanya Revision ulikuwa umeshapita, hivyo Mwanasheria mkuu wa serikali aliomba kwanza kuongezewa muda wa kufungua maombi ya Revision nje ya muda (Application for extension of time to apply for revision out of time). Maombi hayo ya kuongezewa muda aliyafanya tarehe 25 April, 2019 kupitia kesi ya madai namba 138 ya mwaka 2019.

SABABU ZA KUONGEZEWA MUDA:

Mwanasheria Mkuu wa Serikali alileta hoja zifuatazo kama sababu za kuomba kuongezewa muda.

1: Kwamba, maamuzi ya Mahakama Kuu (yaliyoruhusu raia wa kigeni kumiliki ardhi nchini Tanzania kwa njia ya urithi) yameathiri maslahi ya Serikali (has affected the interests of the Government).

2: *Maamuzi ya Mahakama Kuu yana makosa makubwa (serious
irregularities)*

3: Tafsiri ya Mahakama Kuu kuhusu kifungu cha 20 cha Sheria ya Ardhi ya Tanzania haikuwa inahusu mirathi hadi kupelekea kuamua kwamba mtu asiye Mtanzania anaweza kumiliki ardhi kupitia urithi wakati kisheria mtu asiye Mtanzania hawezi kumiliki ardhi isipokuwa kwa madhumuni ya uwekezaji.

Nanukuu, that “the interpretation of section 20 of the Land Act [CAP 113 R.E 2002] (the Land Act) by the High Court was not based on probate matters which lead to the decision by that court that a non-Tanzanian can own land by way of bequeath while under the law, a non-Tanzanian cannot own land save for investment purposes.”

4: Kwamba, uamuzi wa Mahakama Kuu ni kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Sera ya Ardhi na Sheria ya Ardhi.

Kwenye kesi hii ya maombi ya kuongezewa muda, Mwanasheria Mkuu aliwakilishwa na Wakili wa Serikali (Senior State Attorney) Mr. Camilius Ruhinda akisaidiana na Wakili wa Serikali (learned State Attorney) Miss Doreen Mhina.

Upande wa mjibu maombi namba mbili (Kabidhi Wasii Mkuu) aliwakilishwa na Wakili wa Serikali Mr. Samuel Mutabazi, na wajibu maombi namba tatu na namba nne (Georgio Anagnastou na Ourania Anagnastou) waliwakilishwa na Wakili Msomi (learned counsel) Mr. Emmanuel Safari.

Mjibu maombi namba moja, Emmanuel Marangakisi, ambae ndo alikuwa mwakilishi wa Anastansious Anagnostou (yule raia wa kigeni na mrithi wa marehemu) wakati wa kesi kule Mahakama Kuu mwaka 2011, hakufika Mahakamani awamu hii, pamoja na kutafutwa hadi kupitia njia ya taarifa kwenye magazeti ya Daily News na Mwananchi.

Ingawa Mahakama iliendelea bila yeye kuwepo lakini walizingatia hoja zake za maandishi (written submission) alizokuwa amepeleka Mahakamani tarehe 25 February, 2021.

Kwenye kusikiliza maombi ya kuongezewa muda, Mwanasheria Mkuu wa Serikali alisema kwamba, yeye kwa sababu hakuwa sehemu ya kesi ya marangakis wakati inasikilizwa Mahakama Kuu mwaka 2011, alikuja kugundua uwepo wa maamuzi hayo tarehe 15 March, 2019 baada ya kupokea barua kutoka ofisi ya Administrator General (Kabidhi Wasii Mkuu - RITA), akielezea ugumu alioupata kumrithisha ardhi mtu asiye Mtanzania.

Upande wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakasema wana sababu nzuri na za kutosha kuongezewa muda. Wakarejea na kesi mbali mbali kukazia hoja zao.

Mahakama ikapitia hoja za maandishi za Emmanuel Marangakis, ambapo Marangakis alipinga maombi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuongezewa muda, akidai kwamba, Serikali inatakiwa kufata maamuzi ya Mahakama Kuu kwenye kesi ya 2011 kwa sababu upande wa mjibu maombi namba mbili (Kabidhi Wasii Mkuu) aliyekua sehemu ya hiyo kesi aliridhia maamuzi hayo.

Na kwamba tafsiri iliyotolewa na Mahakama Kuu ilikuwa wazi kabisa kwa sababu *Mahakama ilitofautisha wazi kati ya kupata ardhi kwa njia ya kununua na kupata ardhi kwa njia ya sheria kuchukua mkondo wake.

Nanukuu, “he contended further that the interpretation made by the trial court was very clear in that it made clear distinction between acquisition of land by disposition and acquisition by the operation of law.”

Mjibu maombi namba mbili (Kabidhi Wasii Mkuu - RITA) yeye alisema anaunga mkono maombi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali aongezewe muda. Hivyo hakua na maneno mengi ya kusema.

Wakili Msomi wa wajibu maombi namba tatu na namba nne (Georgio Anagnastou na Ourania Anagnastou), Mr. Emmanuel Safari, yeye akasema kwamba, Mwanasheria Mkuu wa Serikali alikua anafahamu uwepo wa yale maamuzi ya Mahakama Kuu ya mwaka 2011 yaliyoruhusu mtu asiye Mtanzania kumiliki ardhi kwa njia ya kurithi, kwa sababu zifuatazo:

Moja, kati ya maafisa wa juu kabisa wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (one of his senior officers) Mr. Gilbert Peter Buberwa, ndiye alikuwa Wakili wa Serikali (learned State Attorney) aliyemuwakilisha Mjibu maombi namba mbili (Kabidhi Wasii Mkuu) kwenye ile kesi ya mwanzo mwaka 2011.

Lakini pia, Mwanasheria Mkuu wa Serikali anatakiwa kupokea ripoti kutoka kwa Kabidhi Wasii Mkuu na taasisi zingine za Serikali kwa mujibu wa kifungu cha 10(2) cha Sheria ya Utekelezaji Majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kwa hiyo hawezi kusema alikua hafahamu uwepo wa maamuzi hayo. N.k

Mr. Safari, Wakili Msomi akaendelea kusema kwamba, *Serikali haijatoa maelezo ya kutosha kwa nini ilichelewa kupinga Maamuzi ya Mahakama Kuu muda wote huo tangu 2011 mpaka
2019. Hivyo, hakuna sababu za msingi kuifanya Mahakama iongeze muda wa kuleta revision.*

Kwenye rejoinder, Wakili wa Serikali akamjibu Wakili Msomi Mr. Msafiri, kwamba, Mwanasheria aliyemuwakilisha Kabidhi Wasii Mkuu kwenye ile kesi ya kwanza alikua anafanya kazi RITA ambayo ni ofisi niyingine inayojitegemea mbali na ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Na kwamba, kifungu cha 10 cha Sheria ya Utekelezaji wa Majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kinachompa Mwanasheria Mkuu wa Serikali mamlaka ya kupokea ripoti kutoka taasisi mbalimbali zilizo chini ya ofisi yake, ikiwemo ofisi ya Kabidhi Wasii Mkuu (RITA), kilitungwa baadaye mwaka 2018 muda mrefu baada ya kuwa uamuzi kwenye kesi ya mwaka 2011 umeshatolewa.

MAAMUZI YA MAHAKAMA:

Baada ya kusikiliza na kuchambua hoja za pande zote mbili, Mahakama ya Rufaa ikakubali kwamba ni kweli Mwanasheria Mkuu wa Serikali aligundua uwepo wa maamuzi ya Mahakama Kuu, tarehe 15 March, 2019.

Pia Mahakama ya Rufani ikasema kwamba, hata kama Wakili wa Serikali aliyemuwakilisha Kabidhi Wasii Mkuu kwenye kesi ya Marangakis mwaka 2011 alikuwa chini ya usimamizi (supervision) wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, hata hivyo hizi Ofisi mbili (Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Kabidhi Wasii Mkuu) ni Ofisi mbili tofauti. Kama Kabidhi Wasii Mkuu hakumpa taarifa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, sio makosa ya Mwanasheria Mkuu.

Mahakama pia ikakubali kwamba kifungu cha 10 cha Sheria ya Utekelezaji wa Majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kinachompa Mwanasheria Mkuu wa Serikali mamlaka ya kupokea ripoti kutoka taasisi mbalimbali, ikiwemo ofisi ya Kabidhi Wasii Mkuu hakikuwepo mwaka 2011, ila kilitungwa baadaye mwaka 2018 wakati kesi ya Marangakis imeshaamuliwa.

Kuhusu hoja ya ikiwa, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ametoa maelezo ya kutosha alikua wapi siku zote hizo, ambapo alitakiwa aombe revision ndani ya siku sitini (60) tangu uamuzi utoke, lakini yeye akakaa tangu 2011 hadi 2019, amechelewa takribani miaka nane (8).

Mahakama ikasema kwa mujibu wa sheria, mtu anayetaka kuongezewa muda anatakiwa atoe sababu za msingi kwa nini alishindwa kufungua kesi au kufanya alichotakiwa kufanya ndani ya muda husika.

Sheria haijaandika sababu zipi ni za msingi ukitaka kuomba kuongezewa muda wa kufanya kitu fulani na Mahakama, ila kuna kesi mbalimbali ambapo Mahakama ilitoa maamuzi na kutaja baadhi ya sababu ambazo ni za msingi kama mtu unataka kuomba kuongezewa muda. (Soma kesi mbali mbali utaona hizo sababu).

Mfano kesi ya *Lyamuya Construction Company Ltd v. Board of Registered
Trustees of Young Women's Christian Association of Tanzania, Civil Application No. 2 of 2010*, Mahakama ilisema ukiomba kuongezewa muda unatakiwa uoneshe mambo yafuatayo:

{i} The applicant must account for all the period of delay.
{ii} The delay should not be inordinate.
{iii} The applicant must show diligence, and not apathy, negligence or sloppiness in the prosecution of the action that he intends to take.
{iv} If the court feels that there are other sufficient reasons, such as the existence of a point of law of sufficient importance; such as the ILLEGALITY of the decision sought to be challenged.

Mahakama ikakubali kuwa ni sahihi, kuanzia tarehe 13 May, 2011 hadi 15 March, 2019 Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema alikua hajui uwepo wa maamuzi ya Mahakama kuu yaliyoruhusu mtu asiye Mtanzania kumiliki ardhi kupitia urithi.

Lakini tangu hiyo tarehe 15 March, 2019 Mwanasheria Mkuu wa Serikali alipotambua uwepo wa hayo maamuzi ya Mahakama Kuu, alikuja kufungua maombi ya kuongezewa muda tarehe 25 April 2019.

Mahakama ikasema hiki kipindi kingine cha kuanzia tarehe 15 March, 2019 hadi tarehe 25 April 2019 hakijatolewa maelezo. Mahakama ikasema alitakiwa pia aeleze kwa nini alichelewa kuanzia tarehe 15 March, 2019 alipotambua huo uamuzi kwa mara ya kwanza hadi 25 April 2019 alipokuja Mahakamani.

(Kwa mujibu wa sheria, kuchelewa hata kwa siku moja lazima kutolewe maelezo ulikua wapi. Soma kesi ya Elius Mwakalinga v. Domina Kagaruki & Five Others, Civil Application No. 120/17 of 2018)

Lakini, Mahakama ya Rufaa ikasema kwamba, pamoja na hayo yote, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameibua hoja ya MAKOSA YA KISHERIA (ILLEGALITY) kwenye yale maamuzi ya Mahakama Kuu yaliyoruhusu mtu asiye Mtanzania kumiliki ardhi, anadai kwamba Mahakama Kuu ilikosea kutafsri kifungu cha 20 cha Sheria ya Ardhi ya Tanzania kinachozuia mtu asiye raia wa Tanzania kumiliki ardhi isipokua tu kwa lengo la uwekezaji.

Mahakama ya Rufaa ikasema kuna makosa ya kisheria (illegality) ya wazi wazi kabisa hapa, ikiwa Mahakama Kuu ilikua sahihi au la sio suala la kujadili kwa sasa. Ila makosa ya kisheria ni sababu nzuri ya kuongezewa muda. Nanukuu:

“the alleged illegality is very much apparent on the face of the record.” Whether or not the trial court was correct in its decision is not the prerogative of this Court at this stage. ...allegation of an illegality is good cause for extension of time even if the applicant has failed to account for each day of delay.”

Mwisho Mahakama ya Rufani ikaamua kwamba, kutokana na kigezo cha illegality, maombi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuongezewa muda yana mashiko.

Mahakama ikamuongezea siku sitini (60) alete maombi ya revision kuomba Mahakama ya Rufaa ipitie usahihi wa maamuzi ya Mahakama Kuu ya mwaka 2011 yaliyoruhusu raia asiye Mtanzania kumiliki ardhi nchini Tanzania kwa njia ya kurithi.

Muda wa hizo siku 60 unahesabika kuanzia tarehe 24 February, 2023 uamuzi huu ulipotolewa.

Tuendelee kusubiri Mahakama ya Rufaa itaamua nini kwenye hiyo Revision, je Mahakama ya Rufaa itakubaliana na Maamuzi ya Mahakama kuu yanayoruhusu watu wasio Watanzania kumiliki ardhi au itapindua meza? Tusubiri!

-----MWISHO----

Natoa angalizo, wale wazee wa kukopi machapisho ya watu na kuweka majina yenu. Ni kosa kisheria. Hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayejimilikisha andiko hili. Unaruhusiwa tu kushare lakini usibadili chochote. Ni heri uanze kuandika ya kwako mpya. (Ukipost popote tutakuona, tupo Twitter, Instagram, Facebook, Jamii Forum na popote pale online). ~Usijitafutie kesi za bure na gharama zisizo na sababu~

Disclaimer: Lengo la hii makala ni kutoa elimu kwa jamii. Huu sio ushauri wa kisheria kwa mtu yeyote. Ikiwa utaamua kufungua kesi kwa kufata haya maelezo na ukapata hasara, mwandishi wa maelezo haya hatawajibika kwa vyovyote vile. KAMA UNAHITAJI USHAURI WA KISHERIA WASILIANA NA MAWAKILI.

Imeandaliwa na Zakaria Maseke -
(0754575246 - WhatsApp) zakariamaseke@gmail.com
(Advocate Candidate)
 
Unakumbuka ile kesi ambayo Mahakama Kuu ya Tanzania iliamua kwamba Raia wa Kigeni wanaweza kumiliki ardhi nchini Tanzania kwa njia ya kurithi (where High Court ruled that non-citizen heirs could own land by way of inheritance)...
Labda kwa vile samia haingilii mahakama sana, ingelikuwa Magufuli hapo hamna kesi washindi ni serikali
 
Awe mdhamini/trustee au mmiliki, ukweli ni huu, hakuna Mtanzania anayemiliki ardhi period.
Duniani kote ardhi ni mali ya dola. Wakazi wa kwenye dola husika ni watumiaji tu wa ardhi hiyo, na ili waendelee kuitumia ni lazima walipe kodi ya pango (yaani kodi ya ardhi/land tax) kwa dola.

Usipolipia kodi ya pango ya ardhi kwa dola, dola itakuondoa kwenye ardhi husika.
 
Back
Top Bottom