SoC04 Mageuzi ya msingi ya utendaji wa Jeshi la Polisi Tanzania

Tanzania Tuitakayo competition threads

Damaso

JF-Expert Member
Jul 18, 2018
1,662
2,219
Mara kadhaa kama jamii tumejikuta tukiwa na dhana mbaya sana kuhusu maafisa usalama hususani ni askari polisi, mgambo na kadhalika. Takwimu nyingi zimeonesha kuwa jamii haina imani kabsa na utendaji kazi wa askari polisi kwa kiwango kikubwa, jamii ina hofu ya ajabu sana ukizungumza kuhusu masuala ya polisi, lengo kuu la uwepo wa chombo hiki ni kulinda na Kutumikia jamii yetu. Usalama wa Raia na Mali zao, huku wakielekeza shabaha zao katika malengo la kutoa huduma bora zitakazowezesha kubaini, kuzuia na kudhibiti uhalifu ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

1714637426567.png

Picha kwa hisani ya TCRA.

Matumizi ya nguvu kupitiliza, unyanyasaji wa kijinsia, uvunjaji wa sheria na kanuni na mengine, haya ni machache tu ambayo jamii inaishi nayo katika fikra kuhusu jeshi la polisi. Mfano, unatoka kazini mida ya usiku saa 6 unakutana na mwili wa mtu upo porini, na kwa utamaduni za waafrika na watanzania ni jambo zuri kwenda kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama kuhusu tukio hili, ila jambo la ajabu ni kuwa mtoa taarifa ndo utakuwa mtuhumiwa namba moja katika kesi hiyo, na endapo polisi wakishindwa kumpa mtu aliyehusika basi unaweza kuibeba kesi hiyo kuwa wewe ndo muuaji (Wema wako utakuwa umekupoza).

1714637557199.png

Picha kwa hisani ya DW.

Mtandao wa Mwananchi tarehe 30 Septemba 2022 walichapisha habari kuhusu polisi waliowaua watu watano waliodhaniwa kuwa ni majambazi. Sio mbaya ila kwanini kila wakati polisi akiwa na dhana kwamba fulani ni mwalifu, je anapaswa kufyatua risasi na kutoa uhai wa mtu huyo? Kwa mujibu wa mtandao wa Wikipedia wao wamedadavua neno dhana kuwa ni, wazo lisilo bayana wala la hakika lakini mtu au jamii wanaweza kuwa nalo na kulipendekeza kwa wengine ili lizidi kuchunguzwa upande wa falsafa, sayansi n.k. kwa kutumia hoja, vipimo na njia nyingine za kufikia ukweli. Hivyo ili dhana ipate kuwa na mashiko inapaswa kuchunguzwa vizuri ili ukweli ujulikane, je wangapi wamechunguza dhana zao wakiwa na mtutu wa bunduki.

Sehemu pekee ambayo suala la dhana linapata kuleta kimantiki ni katika uchunguzi tu, na sio katika kufanya vitendo vya kutishia kuua au kuua kabsa. Habari kama vile “Mtu mmoja anayedhaniwa kuwa ni jambazi, ameuawa katika majibizano ya Risasi kati yake na jeshi la Polisi kikosi cha kuzuia ujambazi kwa kutumia silaha, wilayani Kibondo mkoani Kigoma”. Je ni nani aliyeanza kufyatua risasi ya kwanza? Je ni nani aliyeanzisha mashambulizi kati ya anayedhaniwa kuwa jambazi na polisi?

1714637921558.png

Picha kwa hisani ya Millardayo.

Ukisoma taarifa ya Radio Free Africa ya tarehe 27 Julai 2022 inasema hivi, "Alipogunduwa kuwa anafuatiliwa alijihami kwa kurusha Bomu la kutwa kwa mkono lakini kutokana na kiwewe alichokuwa nacho hakulirusha kama inavyopaswa hivyo halikulipuka ndipo askari wetu walipoanza kujihami kwa majibizano ya Risasi na kufanikiwa kumudhibiti kabla ya kuuawa" kwa mujibu wa Kaimu kamanda wa polisi Kigoma ACP Manradi Sindano. Wote tunafahamu kuwa katika tukio hilo ACP hakuwepo, yeye alipewa ripoti tu, je tutafahamu vipi kwa hakika kuwa mtu huyo alikuwa jambazi? Je tutaamini vipi taarifa ya Polisi ikiwa kila Wakati majambazi wanapouawa basi inakuwa ni majibizano ya risasi?

“Watano wafa katika majibizano ya risasi na polisi Temeke” kwa mujibu wa taarifa kutoka Mwananchi, inasema “Watu watano wanaodaiwa kuwa ni wahalifu wameuawa katika eneo la Toangoma jijini Dar es Salaam, katika majibizano ya risasi na Polisi yaliyotokea usiku wa kuamkia leo Ijumaa". Taarifa ambayo ilitolewa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Emmanuel Lukula. Hapa bado maswali ni yale yale, je Umma utapata hakikisho la kisa hiki wapi? Je tutafahamu vipi hawa watano walikuwa ni wahalifu au laah?

Alex Jonas ambaye alikuwa ni Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Manyoni aliuawa na watu wasiofahamika, na CHADEMA ilipohitaji watu hao wafuatiliwe, Jeshi la Polisi chini ya Sweetbert Njewike ambaye ndo alikuwa ni Kamanda wa Polisi mkoani Singida alidai kuwa Marehemu Alex Jonas hakuwa kiongozi wa CHADEMA bali ni dereva wa Bodaboda tu, ni ajabu sana! Kwani kifo cha dereva wa bodaboda hakina haki ya kuchunguzwa na waliomtoa uhai kufikishwa mahakamani? Je Maisha ya dereva wa bodaboda haya maana tena mbele ya jeshi la polisi ambalo lipo kwa ajili ya kulinda raia na mali zao?

1714638180578.png

Picha kwa hisani ya The Happiness Trap.

Je ni sehemu ipi sahihi ya kuhoji utendaji kazi wa polisi endapo kukitoea tatizo lolote ndani ya jamii? Ni mara ngapi tumepata kushuhudia watu wakilalamikia jeshi la polisi na utendaji kazi wake? Je ni sehemu ipi katika katiba na sheria inampa ruhusa askari polisi kumpiga makofi na ngumi mtuhumiwa? Mwaka 2022 Kibabu Msese alifia mikononi mwa polisi huko Arusha. Ndugu walipoenda kumkagua wanakuta kijana wao amevunjwa shingo na kucha za mikono zimeng’olewa, ni unyama wa aina gani huu? Badala ya Kamanda Justine Masejo kumekea na kukosoa tatizo hili, akiwa kama Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, yeye ndo kwanza anasoma risala ndefu na kuongeza makosa kwa marehemu Kibabu Msese.

1714638300072.png

Picha kwa hisani ya Tovuti ya IPID.

Nimeongea haya kwa sabu moja, Tanzania tunahitaji uwepo wa kuundwa kwa Independent Police Investigative Directorate kama ilivyo Afrika ya Kusini. Chombo huru ambacho kitakuwa na dhamana kuchunguza matukio, malalamiko pamoja na utendaji kazi mbaya wa Askari polisi. Tanzania tukiwa na IPID basi katika miaka mitano mpaka kumi ijayo, tutapunguza utendaji kazi mbovu wa askari polisi. chombo hiki kisiteuliwe na Rais au kiongozi yoyote bali wananchi wapendekeze watu wa kuingia humo.

Haki ya mwananchi haitopatikana kama askari ataendelea kutumia hisia na maono yake kutenda kazi. Lakini pia kuwepo na utoaji wa elimu haswa ya saikolojia, watu kama Dr. Chris Mauki, Dr. Mallewo Charles, Dr. Hellen Mrema na viongozi wa dini wapate kutoa darasa kwa maaskari polisi kuhusu umuhimu wa kuishi kwa amani na wanajamii.

1714638628028.png

Picha kwa hisani ya Global Publishers.

Ni mpaka lini ndipo askari watapata ufahamu kuwa bado wanaishi ndani ya jamii, familia zao, baba na mama, watoto, wapendwa wao ambao kila siku hutamani kuwaona wakiwa na tabasamu kama Ben Saanane, wakifurahi kwa bashasha kama Robert Mushi akiwa na Boniphace Jacob wakijadili harakati za Maisha. Ndugu zangu Askari, kazi hii inaisha! Ipo siku utastaafu kazi na utarejea mtaani, jiulize utaishi vipi na watu ambao ulikuwa unawanyanyasa? Fanya kazi yako kwa weledi pasipo kumnyanyasa mtu.
Sio kwa Ubaya! SIo kwa Ubaya
 
Naunga mkono kuundwa kwa taasisi HURU ya kuchunguza matukio tatanishi ya polisi na mengineyo. Ili kila mmoja awajibike kwa wajibu wake. Check and balance.

Japo katika pointi zako upo utata wa popote inapotokea majibizano ya risasi. Kimsingi upo ugumu kujua kama mtuhumiwa angewawahi askari ingekuwaje?

Katika kuliwaza jambo hili, niliwahi kufikia mkataa kwamba raia wasimilikishwe bunduki kabisa. Usalama wa jamii yetu uende kwa mkataba wa kijamii huu hapa;

(Social contract) yetu iwe ni kwamba tunajivua haki za kumiliki mabunduki ili amani itawale kwa mtindo huo. Guns free society. Maana inatisha kuishi miongoni mwa watu wenye uwezo wa kuangamiza waru kumi hadi 45 kwa kuminya kidole tu🤕.

Iko hivi: mtu anaweza kudhani kila mmoja akimiliki bunduki basi kila mmoja atakuwa salama (mtindo wa marekani) lakini sivyo. Wote tukiwa na bunduki inakuwa ziro.

Kama tukikubaliana hakuna kumiliki bunduki, basi watu wote watajilinda kwa mbinu nyingine zisizohusisha maangamizi mfano karate, visu, mapanga na mawe. Yaani kimsingi mtu mmoja awe na uwezo wa kupigana na mtu mmoja mwenzake.

Ili wahalifu wadhibitiwe na jeshi. Askari wengi/wananchi watadhibiti hao majambazi wachache.
 
Naunga mkono kuundwa kwa taasisi HURU ya kuchunguza matukio tatanishi ya polisi na mengineyo. Ili kila mmoja awajibike kwa wajibu wake. Check and balance.

Japo katika pointi zako upo utata wa popote inapotokea majibizano ya risasi. Kimsingi upo ugumu kujua kama mtuhumiwa angewawahi askari ingekuwaje?

Katika kuliwaza jambo hili, niliwahi kufikia mkataa kwamba raia wasimilikishwe bunduki kabisa. Usalama wa jamii yetu uende kwa mkataba wa kijamii huu hapa;

(Social contract) yetu iwe ni kwamba tunajivua haki za kumiliki mabunduki ili amani itawale kwa mtindo huo. Guns free society. Maana inatisha kuishi miongoni mwa watu wenye uwezo wa kuangamiza waru kumi hadi 45 kwa kuminya kidole tu🤕.

Iko hivi: mtu anaweza kudhani kila mmoja akimiliki bunduki basi kila mmoja atakuwa salama (mtindo wa marekani) lakini sivyo. Wote tukiwa na bunduki inakuwa ziro.

Kama tukikubaliana hakuna kumiliki bunduki, basi watu wote watajilinda kwa mbinu nyingine zisizohusisha maangamizi mfano karate, visu, mapanga na mawe. Yaani kimsingi mtu mmoja awe na uwezo wa kupigana na mtu mmoja mwenzake.

Ili wahalifu wadhibitiwe na jeshi. Askari wengi/wananchi watadhibiti hao majambazi wachache.
Ni kweli Mkuu! Safi sana!
 
Back
Top Bottom