- Source #1
- View Source #1
- Source #2
- View Source #2
Katika pita pita zangu mitandaoni leo nimekutana na "Twit" inayosema kwamba Gavana wa BOT Gilman Rutihinda (1989 - 1993) alifariki kutokana na ajali ya gari mwaka 1993 kama hii tweet inavyojieleza:
Hata hivyo kuna article ya Mwaka 2011 hapa katika Forum inayoelezea kifo cha Gavana Rutihinda pamoja na Waziri wa Fedha wa wakati huo Steven Kibona kwamba vilitokana na 'food poisoning' baada ya kurudi kutoka safarini India.
- Sababu ya kifo cha Steven Kibona na Gilman Rutihinda
Je tunaweza kupata ukweli wa vifo hivi?
- Tunachokijua
- Gilman Rutihinda ni Mtanzania ambaye aliteuliwa kuwa Gavana wa Benki kuu ya Tanzania (BoT) mnamo mwaka 1989 wakati wa utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi. Gilman alifanya kazi akiwa nafasi hiyo mpaka mwaka 1993 umauti ulipomkuta. Kutokana na heshima yake baada ya kifo Shule ya Msingi Darajani ilibadilishwa jina na kupewa jina Gilman Rutihinda Primary School ili kumuenzi.
Kama alivyodokeza na kuhoji Mwanachama wa JamiiForums Lusajo L.M katika andiko hili, baada ya kifo cha Gavana Gilman Rutihinda kuna maswali na hadithi nyingi ziliibuka tangu mwaka kilipotokea mpaka sasa zikihoji na kueleza sababu ya kifo chake.
JamiiForums imepitia vyanzo mbalimbali ili kupata taaarifa zaidi na tahmini hasa juu ya kifo cha Gilman Rutihinda aliyekuwa Gavana wa BoT kwa wakati huo. JamiiForums imepata taarifa tofauti kutoka vyanzo vifuatavyo:
Kifo cha Gilman Rutihinda kilitokana na Saratani ya Kongosho
Mnamo Septemba 1, 1993 Taasisi ya Tanzania Affairs ilichapisha andiko la lugha ya Kiingereza lenye taarifa za kifo cha Gavana Gilman. Ukurasa wa pili wa andiko hilo kulikuwa na kichwa kimeandikwa Bussiness News. ambapo habari ya kwanza iligusia kifo Gavana Gilman Rutihinda. Chanzo hiki kilidai kuwa kifo cha Gavana huyo kilitokana na Saratani ya Kongosho na kilitokea Jijini London nchini Uingereza mnamo Juni 20, 1993. Andiko lilieleza
"Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Gilman Rutihinda (49), amefariki dunia kutokana na saratani ya kongosho jijini London tarehe 20 Juni. Maelfu ya watu walihudhuria mazishi yake Dar es Salaam. Baada ya kifo chake nafasi yake imechukuliwa na Dkt. Idris Rashid ambaye alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa NBC."Andiko hili hili la mwaka 1993 lilidumu kwa zaidi ya miaka 15 mpaka baadaye miaka ya 2000 zilipoibuka taarifa nyingine zikihoji na kuulizia sababu ya kifo cha Gavana huyo kama ifuatavyo:
Kifo cha Gilman Rutihinda kilitokana na kulishwa Sumu
Mnamo February 3, 2011 Mwanachama wa JamiiForums aitwaye Tajiri Mkuu wa Matajiri alianzisha mjadala ndani ya Jukwaa la Jamii Intelligence akidokeza na kuhoji namna kifo cha Gavana Gilman kilivyotokea. katika andiko hilo Tajiri Mkuu wa Matajiri alieleza:
"Kibona alikuwa ni Waziri wa fedha, naye Rutihinda alikuwa ni Gavana wa Benki Kuu. Hawa jamaa wazalendo, walikataa kuprint fedha na kuziingiza kwenye system kwani walijua wakifanya hivyo mfumuko wa bei na ugumu wa maisha ungeongezeka.
Bwana mkubwa kwa hasira za kukataliwa ombi lake akawapeleka India, waliporudi kutoka huko wote wakaanza kuumwa, na bwana mkubwa akatueleza kuwa wamelishwa vyakula vya Kihindi hivyo basi, walikumbwa na tumbo la kuharisha kwa sababu ya ugeni wa chakula cha Kihindi. Hawakukaa muda mrefu, wakafa. Je ni kweli walidungwa sumu iuayo taratibu? Au ndio kifo chao kilikuwa chakawaida tu?"
Aidha, pamoja na Tajiri Mkuu wa Matajiri kudokeza kuwa kifo cha Gilman kilitokana na kupewa sumu inayosadikiwa kuwekwa kwenye chakula cha kihindi, bado anaonesha kutokuwa na uhakika na taarifa yake kutokana na kumalizia andiko lake kwa swali linaloashiria naye kutaka kupata uhakika. Hivyo, andiko lake bado halitoshelezi kuthibitisha madai ya Gilman kufariki kwa kupewa sumu.
Kifo cha Gilman Rutihinda kilitokana na ajali ya gari
Mnamo mwaka Machi 7, 2014 Blog ya Dira Yetu ilitoa andiko lenye kichwa Vifo Tata ndani ya CCM. Andiko hili limegusaia vifo vya watu wengi mashuhuri. Kuhusu kifo cha Gilam Rutihinda andiko hilo linadokeza kuwa kilitokana na ajali ya gari ambayo aliipata asubuhi akitoka nyumbani kwake.
Pamoja na Andiko hilo kuwa na kichwa Vifo Tata ndani ya CCM lakini halijaweka wazi utata hasa wa kifo cha Gavana Gilman upi kwenye nini hasa katika ajali hiyo. Mwandishi wa andiko hilo amemalizia kwa kueleza kuwa taarifa zilizokuwapo zilidai ajali iliyotokea ilikuwa ya kawaida.
Aidha, andiko la Blog hiyo linafanana na andiko lililoletwa na kufutwa kwenye Ukurasa wa Twitter wa HistoriaYetu mnamo Juni 25, 2023. Mdau huyu naye alieleza kuwa kifo cha Gavana Gilman kilitokea kwa ajali ya kawaida ya gari, asubuhi alipokuwa akitoka kwake. Andiko hili halielezi chochote kuhusu utata wa kifo hicho. Tazama hapa Chini:
Zaidi ya hayo, katika andiko hilo la HistoriaYetu alijikeza mdau mwengine anayetumia jina la Daktarijamii ambaye alitoa maoni yake akipinga sababu ya kifo cha Gavana Gilaman iliyotolewa na andiko hili. Katika maelezo yake yaye anaeleza kuwa Gavana Gilman alifia nchini Marekani alipoenda kuhudhuria Mkutano wa Magavana. Anaongeza kuwa, mwili uliporudi nchini taarifa zilieleza kuwa Gavana huyo alifariki kwa shinikizo la damu. Mdau huyo alisema:
"Gilman Rutihinda alifia marekani alikokwenda kwenye mkutano wa magavana wa benki kuu duniani. Alirudi Maiti wakasema alikufa kwa shinikizo la damu."
Je, nini kilisababisha kifo cha Gilman Rutihinda?
JamiiForums imefanya jitihada kutafuta taarifa za kifo cha Gavana huyu kutoka katika vyanzo rasmi bila mafanikio. Benki Kuu ya Tanzania ambako ndiko alikuwa akifanya kazi kunaeleza kwa ufupi kuhusu muda aliofanya kazi (1989 - 1993) lakini hakuna taarifa zinazoeleza undani au sababu ya kifo chake.
Hivyo, kutokana na kuwepo kwa hadithi nyingi na kukosekana kwa taarifa zaidi kutoka katika vyanzo rasmi JamiiForums inaona sababu za kifo cha Gavana huyu zibaki kuwa ni nadharia.