SoC02 Jinsi walaji wa kitimoto walivyo hatarini kupata magonjwa

Stories of Change - 2022 Competition

alwatanpeks

New Member
Aug 16, 2021
3
0
Walaji wa nyama ya nguruwe nchini wako hatarini kupata magonjwa mbalimbali kikiwamo kifafa kutokana na maandalizi duni ya kitoweo hicho maeneo ya baa na nyama hiyo kutokaguliwa na wataalamu.

Pia, kukosekana kwa machinjio za nguruwe za kutosha ni changamoto nyingine inayosababisha watu kuchinja na kuuza nyama ya nguruwe kiholela bila kuthibitishwa na wataalamu kama ni salama kwa walaji.

Biashara ya nyama ya nguruwe imeshamiri katika miji mikubwa nchini hasa katika maeneo ya baa na watu wengi wanapenda kutumia chakula hicho wanapokuwa wakijiburudisha na vinywaji katika sehemu za starehe.

Maandalizi ya nyama hiyo kwenye baa yamekuwa ya haraka, jambo ambalo linawaweka watumiaji katika hatari ya kupata magonjwa hatarishi endapo nguruwe hao wanaochinjwa watakuwa na maambukizi ya magonjwa.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa mahala hii katika mkoa wa Dar es Salaam umebaini kwamba maandalizi ya nyama choma ya nguruwe hadi kufika mezani kwa mteja yanachukua wastani wa dakika 15 hadi 20 na baadhi ya wateja hawapendi iliyokauka, hivyo wanaletewa ambayo haijaiva vizuri.

“Lete kilo moja ya kitimoto, isikauke sana tafadhali,” alisikika mteja mmoja akiagiza kitoweo hicho katika baa moja iliyopo Tabata jijini hapa na baada ya dakika 15, aliletewa kikiwa kimeandaliwa kama alivyotaka.

Katika baa nyingine iliyopo eneo la Ubungo Riverside, mlaji wa kitimoto aliagiza kitoweo hicho na baada kuletewa mezani, alimtaka mhudumu kukikausha kitoweo hicho ili kiive vizuri kama anavyotaka.

“Dada, mbona hii nyama haijaiva? Nataka ikauke kabisa, weka na ndizi mbili,” alisikika mteja mmoja akimtaka mhudumu kurudisha jikoni nyama aliyoletewa ili ikakaushwe.

Baadhi ya walaji wa kitimoto wanatambua kwamba wanaweza kupata madhara kwa kula nyama hiyo lakini hawana namna kwa sababu wamekuwa wakila kwa muda mrefu na hawajawahi kudhurika.

Mkazi wa Mabibo, Frank Tumaini anasema amekuwa akisikia kwamba ulaji wa kitimoto unaweza kusababisha ugonjwa wa kifafa, hata hivyo haamini kwa sababu amekuwa akila na hajawahi kupata tatizo hilo.

“Huwa nasikia wanasema kitimoto ina madhara, lakini nimeanza kula tangu nikiwa mtoto, sijawahi kupata shida yoyote. Hayo ni maneno tu ya watu,” anasema kijana huyo wakati akihojiwa na mwandishi.

Kwa upande wake, Moses Kituka anasema anatambua kwamba kuna madhara endapo mtu atakula nguruwe ambayo haijapikwa ikaiva vizuri. Anasema huwa anasisitiza nyama hiyo kuiva vizuri ili asipate hayo magonjwa.

“Aisee, mimi huwa nakula kitimoto iliyokaushwa kabisa, naamini hapo inakuwa imeiva vizuri. Huwezi kujua, lazima nichukue tahadhari maana kuacha nimeshindwa kabisa,” anasema mkazi huyo wa Vingunguti.

Kukosekana kwa machinjio
Moja ya changamoto zilizopo katika tasnia ya nyama ya nguruwe ni kukosekana kwa machinjio za kisasa kwa ajili ya kuchinja nguruwe na kuwapima kama wana maambukizi yoyote kabla nyama haijakwenda sokoni.

Katika uchunguzi huu, mwandishi amebaini kwamba nguruwe wanachinjwa kiholela kwenye nyumba za biashara au majumbani bila nyama yake kukaguliwa, jambo ambalo linawaweka hatarini walaji.

Mfanyabiashara wa kitimoto katika eneo la Mabibo, Isaack Sawe anasema huwa anafuata nguruwe Mlandizi mkoani Pwani au anaagiza kutoka Morogoro kwa sababu bei zake ni nafuu na gharama za usafirishaji siyo kubwa.

“Nikinunua nguruwe, kuna vijana wangu wanamchinja na kumwandaa vizuri, kisha anaingia sokoni. Huwa naangalia nguruwe ambaye amenona, najua nitapata pesa za kutosha,” anasema mfanyabiashara huyo.

Kuhusu nyama kukaguliwa, Sawe anasema hapendi kuwatumia wataalamu kwa sababu wanahitaji fedha. Anasema mbinu anayotumia ni kuchagua nguruwe ambaye ana afya, lakini hakuna ukaguzi unaofanyika.

“Sasa nikachinjie wapi nguruwe wangu, ukiniuliza machinjio ya nguruwe hapa Dar es Salaam, sifahamu hata moja. Labda serikali iliangalie hilo, watujengee machinjio kama ile ya Vingunguti,” anasema kijana huyo.

Katika mkoa huu ambao unaongoza kwa idadi ya watu na biashara ya kitimoto imeshamiri, hakuna machinjio maalumu ya nguruwe iliyojengwa na serikali. Machinjio zilizopo zinamilikiwa na watu binafsi ambao wamewekeza kwenye biashara hiyo.

Katika bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi ya mwaka 2022/23 iliyowasilishwa na waziri wake, Mashimba Ndaki, serikali alizielekeza mamlaka za serikali za mitaa kutenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa machinjio ya nguruwe.

“Nitumie fursa hii kuzielekeza mamlaka za serikali za mitaa kutenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa machinjio ya nguruwe,” alisema Ndaki wakati akiwasilisha hotuba yake bungeni na baadaye ikapitishwa na wabunge.

Bodi ya Nyama yafafanua

Mteknolojia wa chakula kutoka Bodi ya Nyama Tanzania, Edgar Mamboi anasema machinjio za nguruwe zipo lakini kwa Dar es Salaam hajaona halmashauri ambayo imejenga machinjio ya nguruwe.

“Machinjio nyingi zilizopo Dar es Salaam zinamilikiwa na watu binafsi, wameiona hiyo fursa wakaamua kuwekeza. Kuna halmashauri kubwa hapa Dar es Salaam hazina machinjio za, ng’ombe, mbuzi na kondoo.

“Mfano mzuri ni Ubungo…hawana machinjio ya ngombe, mbuzi na kondoo, iliyopo kule Kimara ni ya mtu binafsi. Kinondoni hawana, ile ambayo ipo Tegeta ni ya mtu binafsi. Temeke hawana, ile iliyopo Sabasaba ni ya mtu binafsi.

“Leo hii uwaambie wawe na bucha za nguruwe, kwanza wataangalia kama kitakuwa chanzo cha mapato kwao ili hata wakichukua mkopo baadaye utarudi? Ilala peke yao ndiyo wameweza kuwa na machinjio, ile ya Ukonga ni ya mtu binafsi,” anasema Mamboi.

Anasisitiza kwamba kitendo cha serikali kutokuwa na machinjio zake ni fursa kwa watu kufanya uwekezaji na kwamba Bodi ya Nyama imekuwa ikitoa vibali kwa watu wanaokidhi vigezo kuanzisha machinjio.

Mamboi anasema tasnia ya nyama inaongozwa na sheria mbalimbali ikiwemo sheria ya tasnia ya nyama, sheria ya magonjwa ya mifugo, sheria ya ustawi wa wanyama, sheria ya afya ya jamii na sheria ya mazingira.

Anabainisha kwamba hakuna sheria kati ya hizo inayomruhusu mtu kufanya uchinjaji kwa sababu ili uweze kuchinja lazima eneo hilo liwe limekaguliwa, kusajiliwa na kupata kibali cha kupata mkaguzi.

“Mkaguzi anayekagua nyama na kuipiga mhuri, anasimamia sheria zote hizo ikiwemo sheria ya magonjwa ya mifugo. Lakini huyu mkaguzi hawezi kukubali kufanya ukaguzi kwenye mazingira machafu, hawezi kufanya ukaguzi kwa wachinjaji ambao hawajapima afya.

“Mtu anayegusa nyama, kuna baadhi ya magonjwa anatakiwa apimwe, kwa mfano kifua kikuu, ugonjwa wa ngozi, homa ya ini na magonjwa na mfumo wa mkojo. Magonjwa hayo ni rahisi kuhama kutoka kwa mdau, kwenda kwa mnyama na hatimaye kwa mlaji,” anasema Mamboi.

Anasisitiza kwamba wanaochinjia nguruwe majumbani wanakiuka sheria kwa sababu wanakiuka haki za mnyama kabla ya kuchinjwa ikiwemo kumpumzisha mnyama kwa saa 12 kabla ya kuchinjwa huku akipatiwa maji tu.

Daktari wa mifugo alonga
Daktari wa mifugo, Kessy Joseph anabainisha kuwa changamoto iliyopo ni kwamba hakuna machinjio za kutosha kwa ajili ya nguruwe, hivyo baadhi ya wauzaji wanajichinjia mnyama huyo majumbani mwao bila nyama kukaguliwa.

Anasema mnyama yoyote anayechinjwa ili aliwe na binadamu lazima afanyiwe ukaguzi na mtu ambaye amesomea masuala ya mifugo. Anasema baada ya kukagua, mtaalamu huyo anathibitisha kama nyama hiyo inafaa kuliwa au la.

“Yeye atakagua na kuthibitisha kwamba nyama hii iko salama kwa kuliwa na ikionekana kuna dalili ya magonjwa, inatakiwa atoe tahadhari kwamba nyama hiyo haifai kwa matumizi ya binadamu,” anasema mtaalamu huyo.

Anaonya kwamba nyama haitakiwi kuchinjwa kienyeji, lazima ikaguliwe na wataalamu ili kujua usalama wake kwa mlaji. Anasema mbali na minyoo, nguruwe pia anaweza kusababisha magonjwa mengine kama vile kifua kikuu (TB).

“Shida ni kwamba wengine wanachinja nguruwe ndani ya mageti kwa kuhofia kwamba wakipeleka kwenye machinjio watachajiwa pesa. Sasa ukikwepa gharama madhara yanaweza kuwa makubwa, kuna watu wanapata epilepsy (kifafa) kutoka kwenye minyoo ya nguruwe

“Wale worms (minyoo) wanaweza wakazunguka kwenye damu wakaona ile mishipa ya ubongo ni midogo, yale mayai yakanasa, yakinasa tu yanaathiri ubongo, unaanza kupata nervous disorder (tatizo la fahamu),” anasema Kessy.

Anasisitiza kwamba nyama ambayo tayari imebainika kuwa na mambukizi, inatakiwa isitumike kabisa kwa usalama wa mlaji. Hata hivyo, anasema jambo hilo limekuwa ngumu kutekelezwa kwa sababu wafanyabiashara hawataki kupata hasara.

“Nyama inatakiwa ipikwe vizuri lakini salama zaidi ni kutokutumia. Kwa mfano, mnyama amekaguliwa amegundulika ana TB kwenye mapafu, huyo mnyama anatakiwa afukiwe, asiliwe kabisa, lakini sasa, unakuta mtu kanunua ng’ombe milioni 2, yeye hataki ng,ombe wake afukiwe.

“Naye anayekagua nyama ana njaa zake, basi yanatolewa mapafu yanawekwa pembeni, nyama inaingia sokoni. Lakini ni ugonjwa hatari, sasa inategemea efficiency (ufanisi) ya watu kwenye kazi,” alisema Dk Kessy.

Ili kuondokana na hatari iliyopo, Dk Kessy anasema serikali inatakiwa kuongeza usimamizi kwenye biashara ya nyama. Alisema taratibu zimewekwa, kinachokosekana ni usimamizi madhubuti kwa manufaa ya wananchi.

“Serikali inatakiwa isimamie hizo taratibu zilizowekwa na siyo kwa manufaa tu ya serikali, ni kwa manufaa ya wananchi. Wananchi ni kama watoto wadogo, hawawezi kuambiwa fanya wakafanya…wanatakiwa wasukumwe, siyo kuwaambia,” anasema.

Mtaalamu huyo wa mifugo alibainisha kwamba changamoto iliyopo sasa ni uchache wa machinjio ya nguruwe, jambo linalowalazima watu kujichinjia nguruwe majumbani bila kukaguliwa na wataalamu.

“Changamoto inayoonekana, hatuwezi kuchanganya machinjio ya ng’ombe na nguruwe kwa sababu za kiimani, sasa ufugaji wa nguruwe sasa umekuwa kwa kasi. Kwa hiyo inatakiwa tuwe na machinjio maalumu ya nguruwe,” anasema mtaalamu huyo.
 
Back
Top Bottom