Mag3
Platinum Member
- May 31, 2008
- 13,077
- 22,792
Kwa bahati mbaya sana Mchambuzi, wengi wetu tumekuwa kama watu waliofungwa vitambaa machoni na kuwekewa pamba masikioni; tunakaza macho lakini hatuoni, tunatega masikio lakini hatusikii. Nina wasi wasi kama Mtanganyika alikuwa anaufahamu msimamo wa awali wa Mh. Jaji Warioba kuhusu muundo wa Muungano wakati anateuliwa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Katiba. Ukweli, kama alivyotudokezea moja ya waliokuwa wajumbe wa Tume, Prof. Baregu, ni kwamba msimamo wa Jaji Warioba pamoja na wajumbe wengi kwenye Tume kuhusu muundo wa Muungano, ulikuwa ni wa serikali mbili. Lakini kadiri walivyozidi kuendelea na majadiliano huku wananchi wakizidi kutoa dukuduku zao, taswira iliyokuja kujengeka na kuonekana bora katika kukabiliana na kero za miaka nenda rudi iliegemea kwenye Muundo wa serikali tatu. Hivyo napata shida sana kwa watu wanaomkomalia Jaji Warioba kama vile mapendekezo ya muundo wa serikali yalitokana na utashi wake binafsi kama Mwenyekiti wa Tume na si wananchi. Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Katibu wa Tume wote walikuwa waumini wa muundo wa serikali mbili.Mawazo ya serikali Tatu yalikuwa ni mawazo ya Nani?
Na ni Nani aliyefanya mawazo ya serikali Tatu yasivuke kibaha?
Nikiacha hilo naomba nitoe maoni kidogo kwa Mtanganyika kuhusu msimamo wake anaodai haufungamani na upande wowote; kwamba kwake yeye ufumbuzi wa kero upo katika muundo wa serikali moja. Kusema kweli huu ni msimamo wa kufikirika ambao hata yeye akitaka kuwa mkweli kwa nafsi yake anajua fika kwamba ni msimamo usioweza kutekelezeka...sio sasa, sio kesho na sio katika wakati wowote ulio karibu. Tofauti na mawazo ya wengi, mimi naamini muundo wa serikali tatu utatusogeza karibu kuliko muundo wa serikali mbili.
Kwa nini nasema hivyo? Baada ya miaka 50 kero zimeongezeka na zitazidi kuongezeka na safari hii kutoka kwa waliokuwa wamelala lakini sasa wameamka na wako macho na sasa nao wameanza kudai chao, Watanganyika! Ni bahati sana kwamba mpaka sasa wanaidai kwa amani lakini kwa mizengwe hii wanayowekewa si muda mrefu wataidai kwa shari.
Majirani wanaweza kuishi tu kwa amani na hata kushirikiana kwa mengi tu kama hakuna moja wao anaona ushirikiano unamletea karaha...ushirikiano wenye maelewano unaweza kukua, kukomaa na kadiri siku zinavyoendelea ukazaa muungano imara.