Bashungwa Apiga Kambi Lindi, Kuhakikisha Barabara ya Dar - Lindi Inapitika Ndani ya Saa 72

Stephano Mgendanyi

JF-Expert Member
May 16, 2020
1,991
960

BASHUNGWA APIGA KAMBI LINDI, KUHAKIKISHA BARABARA YA DAR - LINDI INAPITIKA NDANI YA SAA 72.

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amewatoa hofu na kuwahakikishia wananchi, wasafiri na wasafirishaji kuwa ameweka kambi Mkoa wa Lindi kuhakikisha anasimamia timu ya watalaamu wa Wakala ya Barabara (TANROADS) na makandarasi, kuhakikisha wanakamilisha kazi ya kurejesha mawasiliano ya barabara ya Lindi – Dar es Salaam ndani ya saa 72.

Waziri Bashungwa ameeleza hayo, leo tarehe 6 Mei 2024 Nangurukuru wilayani Kilwa wakati akikagua na kusimamia zoezi la urejeshaji wa mawasiliano ya barabara yaliyokatika kwa kuharibiwa na mvua kubwa zilizonyesha zikiambatana na kimbunga Hidaya.

“Niendelee kuwatoa hofu wananchi na wasafiri wanaotumia barabara hii inayounganisha mikoa ya kusini, tangu jana nimepiga kambi huku, nilianzia Somanga na sasa hivi tupo upande huu wa Nangurukuru, kama mnavyoona pande zote wanaendelea na kazi, bado tunaamini ndani ya saa 72, kufikia Alhamisi tutakuwa tumekamilisha kazi ya kurudisha mawasiliano ya barabara hii,” amesema Bashungwa.

Bashungwa amemuagiza Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Eng. Mohamed Besta kuhakikisha anaongeza idadi ya malori yanayosomba mawe pamoja na mitambo inayotumika kupakia mawe katika magari ili kuongeza kasi ya kujaza vifusi katika eneo la barabara yaliyosombwa na maji.

Aidha, Bashungwa amesema kuwa pamoja na jitihada za kuagiza makalvati ya plastiki yanayotumika katika dharura za kurejesha mawasiliano ya barabara, ameeleza kuwa ili kukamilisha kazi hiyo kwa wakati watalazimika kutumia makontena kwa kuyakata yatumike kama mbadala wa kalvati na kuwezesha maji kupita.

Kadhalika, Bashungwa amewapongeza wahandisi kutoka TANROADS pamoja na makandarasi wote wanaoendelea na kazi ya kuhakikisha mawasiliano ya barabara katika maeneo yote yaliyokatika yanarejea.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mohamed Nyundo amemshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha Mamlaka ya Hali ya Hewa kuwa na vifaa vya kisasa vinavyotumika kutabiri hali ya hewa ambapo vimesaidia kwa kiasi kikubwa kutoa utabiri wa matukio mbalimbali ikiwa ni pamoja na mafuriko makubwa na kimbunga Hidaya.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Kivinje Singino, Jafari Bakari ameipongeza Serikali kwa kuchukua hatua za haraka na dharura kwa kufanyia kazi changamoto zinazojitokeza ikiwa ni pamoja na kuhamisha wananchi wanaokaa katika maeneo hatarishi.
WhatsApp Image 2024-05-06 at 17.18.20.jpeg
WhatsApp Image 2024-05-06 at 17.18.21.jpeg
WhatsApp Image 2024-05-06 at 17.18.21(1).jpeg
WhatsApp Image 2024-05-06 at 17.18.22.jpeg
WhatsApp Image 2024-05-06 at 17.18.23.jpeg
WhatsApp Image 2024-05-06 at 17.18.23(1).jpeg
WhatsApp Image 2024-05-06 at 17.18.24.jpeg
WhatsApp Image 2024-05-06 at 17.18.24(1).jpeg
WhatsApp Image 2024-05-06 at 17.18.25.jpeg
WhatsApp Image 2024-05-06 at 17.18.26.jpeg
 
Back
Top Bottom