Athari za kutokuwa na Utawala Bora

JamiiTalks

JF Advocacy Team
Aug 7, 2018
628
952
Nini Maana ya Utawala Bora?

Utawala bora ni matumizi ya mamlaka ya kisiasa, kiuchumi kijamii au vinginevyo katika kusimamia masuala ya nchi kwenye ngazi zote. Utawala bora ni matumizi ya mamlaka ambayo yanakuwa na uwazi, uwajibikaji, ushirikishwaji wa watu, ufanisi, tija, uadilifu usawa na unafuata utawala wa sheria.

Taifa lisilofuata Misingi ya Utawala Bora hukabiliwa na Athari nyingi sana
  • Kutumia vibaya mamlaka ya kisiasa au kiuchumi anayokuwa nayo mtawala, Mtawala asiyefutata misingi ya Utawala bora hatafuata utawala wa sheria na yeye ndiye atakayekuwa anafanya maamuzi ya kila kitu bila kujali madhara ya maamuzi yake hata kama yanawaathiri wananchi.
  • Kutoa matamko ya kisiasa ambayo hayatekelezeki kirahisi ili kukidhi matakwa ya mtawala aidha kupanda kisiasa au apate fedha apande kiuchumi.
  • Taifa litakabiliwa na rushwa na Ufisadi
  • Kutokushirikishwa wananchi katika kufanya maamuzi ya pamoja kama Taifa
  • Ubadhilifu wa rasilimali za Taifa
  • Kupokwa kwa haki za kikatiba
  • Kuvunjwa kwa haki za kibinadamu
  • Umasikini kwa kutokufuata dira ya maendeleo kutokana na ubadhilifu wa rasilimali za Taifa
Ili kukabiliana na mambo haya ni lazimaWatawala wafuate misingi ya Utawala bora na waitekeleze kila wanapokuwa madarakakani.

Ili kufuata Utawala Bora kuna mambo lazima yazingatiwe nayo ni,
  • Matumizi sahihi ya dola
  • Matumizi mazuri ya rasilimali kwa faida ya wananchi
  • Matumizi mazuri ya madaraka, kujua na kutambua madaraka waliyonayo na matumizi yake kwa usahihi.
  • Madaraka yanatumika kulingana na mipaka iliyowekwa na Katiba na Sheria
Utawala Bora ukitekelezwa huleta faida zifuatazo;-
  • Matumizi mazuri ya rasilimali za nchi
  • Maendeleo endelevu
  • Kupungua kwa umasikini, ujinga na maradhi
  • Kutokomea kwa rushwa
  • Huduma bora za jamii
  • Amani na utulivu
  • Kuheshimiwa kwa haki za binadamu
  • Utatuzi wa migogoro kwa mujibu wa sheria na taratibu
  • Kuleta ustawi wa wananchi.

Misingi ya Utawala Bora

Uwazi,
Uwazi ni hali ya kuendesha shughuli za umma bila usiri na kificho ili wananchi wawe na uwezo wa kupima utendaji na uzingatiaji wa kanuni, taratibu na sheria.

Uwazi unajumuisha:
Wananchi kupata taarifa za utekelezaji wa mipango na bajeti za kutekeleza mipango hiyo, kwa lugha rahisi na kwa wakati;
Wananchi kupewa taarifa za mapato na matumizi;
Wananchi kufahamishwa huduma zinazotolewa bila malipo na huduma wanazopaswa kuchangia, na utaratibu wa kupata huduma hizo;

Misingi ya Utawala Bora
Wananchi kujulishwa mahali na wakati muafaka wa kupata taarifa wanazozihitaji na wazipate bila usumbufu; na
Kupewa sababu na uhalali wa maamuzi yaliyofikiwa na viongozi wao.

Uwajibikaji, Uwajibikaji ni hali ya kiongozi na mtendaji kuwa tayari kujibu, kubeba dhamana na kutoa maelezo kwa wananchi juu ya maamuzi au matendo aliyoyafanya katika kutekeleza dhamana aliyopewa.

Kwa mujibu wa Ibara ya 8 (1) (c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 Serikali (viongozi na watendaji) itawajibika kwa wananchi.

Ushirikishwaji, Ni kuwahusisha wananchi wa jinsia zote na makundi yote katika kupanga na kufanya maamuzi ya mambo yanayowahusu. Ushirikishwaji unaweza ukawa wa moja kwa moja au kupitia wawakilishi waliochaguliwa na wananchi.

Utawala wa Sheria, Utawala wa Sheria unamaanisha mambo yafuatayo:-
  • Mfumo wa sheria za nchi ulio wa haki na ambao umejengwa na sheria zisizo kandamizi
  • Usawa mbele ya sheria: watu wote wawe sawa mbele ya sheria
  • Uendeshaji wa shughuli za umma pamoja na maamuzi lazima vifanyike kwa kufuata sheria za nchi
  • Ulinzi na haki sawa mbele ya sheria.
 
Back
Top Bottom