NADHARIA Askari Polisi amuua raia Arusha kwa kumpiga risasi 3. Wananchi wamtuhumu kwa mauaji ya mara kwa mara

Taarifa hii ni nadharia tu, tumeitolea ufafanuzi kwa kadiri ilivyowezekana
Kijana mmoja aliejulikana kwa jina la Israel Daudi, amefariki dunia baada ya kupigwa risasi 3 na askari Polisi kwa kile kinachodaiwa kuwa ni kuachia ng'ombe kuingia shambani.

IMG_7960.jpeg

Tukio hilo limetokea katika Mtaa wa Olaresho, Kata ya Olasiti katika Halmashauri ya Jiji la Arusha.

Akizungumzia tukio hilo Diwani wa Kata ya Olasiti, Alex Martin amesema hilo ni tukio la pili kwa askari huyo kufanya mauaji katika Kata hiyo ya Olasiti kwani huko nyuma alishafanya mauaji na Wananchi walitaka kumuua askari huyo lakini diwani aliingilia kati kwa kumuepusha askari huyo kuuliwa na Wananchi.

Lakini cha kushangaza askari huyo amerudia tena kufanya mauaji katika kata hiyohiyo.

Diwani Alex ametoa wito kwa Jeshi la Polisi kutotumia nguvu na mabavu kwa raia wake pasipo sababu.

Wananchi waomba sheria ichukue mkondo wake.
 
Tunachokijua
Baada ya kutolewa dokezo na Mwanachama wa JamiiForums kuhusu Askari kuhusika na mauaji ya Mwananchi jijini Arusha na pia kuhusishwa na mauaji ya mara kwa mara JamiiForums imetafuta taarifa ya kina kutoka eneo la tukio ili kupata uhalisia wa tukio hili. JamiiForums imepitia simu Serikali ya Mtaa ambao tukio hili limeripotiwa kutokea. Diwani wa kata wa Kata ya Olasiti, Alex Martin (eneo la tukio) ameeleza yafuatayo:

"Kulikuwa na vijana wanachunga ng’ombe zaidi ya 30, wakatokea Askari wawili, mmoja ni maarufu kwa jina la Eliwaha, wakawavamia vijana na kuichukua mifugo kisha kuanza kuiswaga pasipo kusema wanawapeleka wapi.

Vijana hao wana umri chini ya miaka 20, wakati wanaendelea kuomba kurejeshewa mifugo yao akatokea Israel Daudi ambaye ni mfanyabiashara wa mifugo, akasaidia kuomba Askari wale kuwarejeshea ng’ombe kwa kuwa maeneo waliyokuwa wakichunga yanatumiwa siku zote kulisha mifugo."

"Baada ya kuona hakuna mafanikio, Daudi akaamua kuondoka, kuona hivyo Askari Eliwaha akampiga risasi ya mguu Daudi sijui alifikiria nini, alivyoanguka Askari akampiga risasi nyingine, wale vijana wachungaji wakakimbia, baada ya mwili kuchunguzwa ikaonekana alishambuliwa kwa risasi tatu japokuwa hiyo risasi ya tatu vijana hawakuiona."

"Baada ya hapo Askari huyo akamburuza Daudi kwenda kwenye gari, alipofikishwa hospitali akafariki."

Mwili haujazikwa tunategemea kuzika kesho (Julai 7, 2023). Tumewasiliana na Polisi wanafanya mchakato wa kurejesha wale ng’ombe."

Hii si mara ya kwanza kwa Askari huyo kufanya tukio la ajabu mtaani, aliwahi kufyatua risasi kwenye jamii na kutishia siku za nyuma na Wananchi wakataka kumshambulia, mimi ndiye nikamuokoa mikononi mwa Wananchi wenye hasira waliotaka kumdhuru."


Ufafanuzi huo kutoka kwa Diwani wa kata ya Olisiti bwana Alex Martin hautofautiani na maelezo ya dokezo lililoletwa na Mwanachama wa JamiiForums.

Zaidi ya hayo, JamiiForums imefanya mawasiliano na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo juu ya kifo cha kijana Israel Daudi kinachodaiwa kusababishwa na kupigwa risasi tatu na Askari Polisi ambaye amesema:

Uchunguzi unaendelea, tunashirikia na timu mbalimbali kwa ajili ya kufanya uchunguzi wetu, pia tunashirikiana na watu waliokuwepo eneo la tukio.

Aidha, kuhusu Askari aliyetuhumiwa Kamanda wa Arusha amesema:

Siwezi kutaja kinachoendelea kuhusu mtuhumiwa tutakuwa tunaharibu uchunguzi, taarifa ikikamilika tutaitoa rasmi kwenye jamii. Tayari mwili umeshazikwa.

Uchunguzi unaendelea, ndugu wanashiriki na wanashirikiana vizuri na Jeshi la Polisi, tusije tukataja mengine ambayo hayahusiki
.

Hata hivyo, kuhusu kukamilika kwa uchunguzi huo, Kamanda wa Arusha amesema uchunguzi huo ni wa kina na hawajui utakamilika lini.

Hivyo, kwa msingi huo kutokana tukio hili kuendelea kuwa katika hatua za kiuchunguzi wa Vyombo vya Usalama. Tutaendelea kusubiri majibu ya uchunguzi ili kupata ukweli wa tukio.
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom