UZUSHI Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya amefariki Dunia kwa Kupigwa Risasi

Baada ya tathmini, tumebaini kuwa taarifa hii ni ya uzushi
Mtumiaji wa Mtandao wa Twitter anayejulikana kwa jina la MchiziMox Juni 8, 2023 amechapisha andiko linalosema kuwa aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya amefariki dunia kwa kupigwa risasi.

IMG_7543.jpeg

Ukweli wa taarifa hii upoje?
 
Tunachokijua
Julai 28, 2018, aliyekuwa Rais wa Awamu ya 5 Hayati John Pombe Magufuli alimteua Lengai Ole sabaya kuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro.

Awali, kabla ya uteuzi huu, Sabaya aliwahi pia kuhudumu kama Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Mkoa wa Arusha na Diwani kata ya Sambasha Wilaya ya
Arusha Mjini mwaka 2015.

Taarifa za Kupigwa Risasi na Kifo
Katika Mtandao wa Twitter, Jioni ya Juni 8, 2023, mtumiaji mwenye jina la MchiziMox aliandika kuhusu kifo cha Sabaya.

Aliandika;

"Daaah, Ole Sabaya Maskini. Amepigwa risasi muda huu na mmasai mmoja wa mgodini aliyekuwa anamdai, almost Risasi kama kumi hivi"

Hadi kufikia majira ya saa 1:30 Usiku, andiko hilo lilikuwa limesomwa na zaidi ya watu 53,400 likiwa limepedwa mara 894 na tayari lilikuwa na maoni 79.

Ukweli upoje?
Baada ya kusambaa kwa taarifa hii, JamiiForums ilifanya mazungumzo na watu wa karibu wa Lengai Ole Sabaya na kuthibitishiwa kuwa ni mzima wa Afya na yupo nyumbani kwake Mkoani Arusha akiendelea na majukumu yake.

Mbali na hapo, hakuna chombo chochote cha habari kilichoripoti taarifa hii na haipatikani sehemu nyingine yoyote hivyo ni taarifa isiyo na ukweli.

Aidha, kwenye andiko hilohilo, baadhi ya wachangiaji wamejaribu pia kuuliza uhakika wa taarifa hii kutoka kwa mwandishi wake bila mafanikio yoyote. Pia, wachangiaji hao wamekuwa na hisia tofauti huku baadhi ya yao wakienda mbali zaidi kwa kutoa lugha za utani kuhusu kifo hicho.

Lengai Ole Sabaya alizaliwa Disemba 26, 1986 ambapo pamoja na mambo mengine alisoma Shahada ya Sayansi katika Elimu kutoka Chuo Kikuu cha Mt. John Dodoma.

Rais wa Awamu ya 6 Mhe. Samia Suluhu Hassan alitengua uteuzi wake wa nafasi ya Mkuu wa Wilaya Mei 13, 2021 kupisha uchunguzi wa Makosa ya Kesi iliyokuwa ikimkabili ikiwemo unyang'anyi wa kutumia Silaha, kuongoza genge la uhalifu na Utakatishaji fedha.

Mnamo Oktoba 15, 2021, Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha ilimhukumu kwenda Jela Miaka 30 na Aprili 5, 2023 aliachiwa huru kwa Sharti la Kutofanya Kosa la Jinai kwa Mwaka mmoja baada ya kukiri makosa na kulipa faini ya Tsh. Milioni 5.
2 Reactions
Reply
Back
Top Bottom