BARD AI
JF-Expert Member
- Jul 24, 2018
- 3,591
- 8,803
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imesema mfanyabishara maarufu wa Zanzibar, Toufiq Salum Turky, bado hajalipa Sh. milioni 308.5 za kodi kutokana na kuingiza gari la kifahari aina ya Benzi, Januari, mwaka huu.
Naibu Kamishina wa TRA Zanzibar, Juma Bakary Hassan, aliwaambia waandishi wa habari jana ofisini kwake, Kinazini, Unguja kuwa gari hilo ilingizwa na mfanyabishara huyo kupitia kampuni yake ya Mifuko Turky ya Zanzibar.
Juma alisema, kiwango hicho cha kodi kinatakiwa kulipwa baada ya maombi ya masamaha wa kodi kukataliwa mara mbili na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar, Dk. Saada Mkuya Salum.
Alisema, baada ya kutakiwa alipe, aliomba wapewe muda wa kulipa kidogo kidogo kwa madai hali ya kifedha si nzuri na kulazimika kupewa miezi mitatu kuanzia Mei hadi Agosti, mwaka huu.
“Mpaka muda unamalizika Agosti, amelipa Sh. milioni 138 na bado wanadaiwa Sh. milioni 170 kati ya Sh. milioni 308 .5 alizopaswa kulipa. Tunajiandaa kuhakikisha fedha hizo zinalipwa kupitia bodi ya dhamana aliyokuwa ameweka kwa kutumia taasisi moja ya fedha,” alisema.
Barua mbili za maombi ya msamaha wa kodi zilizotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa wa Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), Sheriff Ali Sharif, ziliweka wazi kwamba, mdaiwa anapaswa kunufaika na msamaha wa kodi kupitia Kampuni ya Mifuko Turky kama mwekezaji.
Hata hivyo, maombi hayo yalikataliwa na Waziri Mkuya kwa sababu muda wa kunufaika kisheria ulikuwa umemalizika baada ya ujenzi wa kiwanda cha mifuko kuwa umekamilika na uzalishaji kuanza muda mrefu.
“Unaweza kunufaika na msamaha wa kodi kama mwekezaji wakati wa ujenzi wa mradi na si baada ya ujenzi kukamilika na uzalishaji unaendelea kufanyika,” alisema ofisa mmoja mwandamizi wa ZIPA.
Wakati hayo yakiendelea, Bodi ya Mapato Zanzibar ilishasajili gari hilo la kifahari na kutoa namba Z-1 kwa malipo ya Sh. milioni 15, na kuonekana likitembea barabarani kabla ya kukamilisha malipo ya kodi.
“Sisi tumesajili na kutoa namba kwa masharti gari lisitembee mpaka wakamilishe taratibu za kodi tukazo kutoa kibali cha umiliki wa gari,” alisema Meneja Uhusiano na Huduma kwa Walipakodi ZRB, Makame Mohammed Khamis.
Gari hilo lenye thamani ya Dola za Marekani 214,668.71, liliingizwa kupitia bandari ya Malindi na kampuni ya uwakala wa mizigo ya Kimataifa HT Motors Group LTD (UK) kwa kushirikiana na kampuni ya uwakala wa mizigo ya ZARA Freight Forwaders ya Malindi, Zanzibar.