Polen bana. Sema hii kitu ya post kung'olew inakwamish
😃 Ahadi ni deni kwa kweliNjoo basi jaman
Fanya mambo basi mtaalam 😅Polen bana. Sema hii kitu ya post kung'olew inakwamish🤐. Leo uhakika wapendwa
Umetufanya tuwe kama mateja wa hii simulizi aisee, shukrani sana, endelea na moyo huo huoMIMI NA MIMI 2
A Story by Elton Tonny
Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Tamaa, Hila, Usaliti, Siri, Mambo Yasiyotazamiwa
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA AROBAINI NA MOJA
★★★★★★★★★★★★★★★★★★★
Miryam akamtazama Stella tena, kisha akasema, "Naitwa Miryam."
"Miryam. Ni vizuri kukufahamu," Stella akamwambia hivyo huku akitabasamu.
Miryam akabaki kimya tu na kuendelea kumwangalia mwanamke huyo kwa njia ya kawaida.
Stella akakiachia kiganja cha Miryam na kuniangalia kwa ufupi, kisha akamtazama Kevin na kusema, "Congrats kwako, new daddy in town!"
Akamsogelea Kevin huku muuguzi wake akiwa anamfata tu kama vile kikaragosi, nao wakaanza kuongea kidogo. Alijuana na Kevin pia. Nikatulia kidogo nikimwangalia Miryam kwa utulivu, naye akatazama pembeni kabisa na kushusha pumzi kwa njia fulani iliyoonyesha kwamba alikuwa ametatizika kiasi baada ya kukutana na Stella namna hiyo. Nikamsogelea tu na kukishika kiganja chake, kisha nikaanza kuelekea upande wenye chumba ambacho Jasmine alikuwemo huku Miryam akifuata nyuma yangu. Habari za Stella zingekuja kuangaliwa baadaye, hivi sasa dada yangu ndiyo alikuwa muhimu.
Tukaingia ndani ya hicho chumba hatimaye, na tuliwakuta Jasmine, mama, mzee, Nuru, marafiki wawili wanawake wa Jasmine pamoja na watoto wao wawili rika la miaka mitano mpaka kumi, ndugu wengine watatu wa familia upande wa mzee ambao walikuwa "wajomba," pamoja na mdogo wake Kevin wa kike aliyelingana rika la Mariam. Dada yangu Jasmine alilala kitandani kwa utulivu, kitanda binafsi kizuri cha VIP aliye yeye, na pembeni kulikuwa na kifaa kipana kama kitanda, ambacho kilikuwa kimegawanyishwa mara mbili humo humo kwa ndani, na ndiyo mapacha aliojifungua Jasmine walikuwemo humo. Ujio wetu ukaongeza furaha ya waliotufahamu, nasi tukasalimiana nao vizuri na kutambulishwa kwa wengine.
Jasmine alikuwa amelala kwa kuegamia mito huku akitabasamu kiasi, nami nikamkumbatia kwa kichwa pamoja na Miryam na kumpa hongera yake kwa dhati kubwa sana, kisha tukaanza kuwaangalia waja wapya wa dunia, waliokuwa wamesinzia kwa wakati huu. Wajomba na marafiki zake Jasmine walinichangamkia vyema maana hatukuwa tumeonana kwa muda mrefu, na nilipomtambulisha Miryam kuwa mpenzi wangu, mwanzoni walifikiri natania eti, lakini mwishowe wakaelewa ilikuwa kweli. Najua baadhi yao walihisi labda mapenzi yangu na Miryam yangekuwa yale ya kufurahishana tu halafu tunatemana, lakini hapo ndiyo nilikuwa nimemleta mke wangu mtarajiwa, na wangekuja tu kushangaa wanapokea kadi za harusi ndani ya kipindi kifupi. Sikuwa natania!
Ndani ya muda huo huo, Stella akaingia ndani ya chumba hiki pamoja na muuguzi wake na kuanza kuwasalimu wengine vizuri, na alimkumbatia mama, mzee, na Nuru, akiongea nao kwa njia ya kirafiki na kumtania Jasmine kidogo pia. Alifanya ionekane wazi kwamba alijuana na familia yangu vizuri, na mimi na Miryam tukatulia tu mpaka Kevin alipoingia akiwa na mama yake mzazi. Akapokelewa vyema pia, naye akawaangalia wajukuu wake na kumpa hongera za dhati Jasmine. Kulikuwa na hali ya upatano baina yake Jasmine na Kevin, hata jamaa akawa karibu na kitanda cha dada yangu huku akikishika kiganja chake, na hilo likanifariji sana.
Stella alikuwa mwanamke mwenye ufasaha, hivyo alipoanza kuongelea mambo fulani yaliyohusiana na utunzaji mzuri wa watoto, wote walimsikiliza kwa umakini. Akagusia kwamba ni muhimu sana kwa watoto kupata utunzaji bora kutoka kwa wazazi wote, wazisikie sauti za baba na mama kutokea udogoni hadi wakikua, na wautambue umuhimu wao kwenye maisha yao yote ili waje kuwa wazazi bora. Mama, Jasmine, na hata wengine waliniangalia sana baada ya Stella kusema hayo, kwa sababu walielewa kwa njia fulani alikuwa akifikisha ujumbe wake kwangu mimi pia kuendana na hali yetu, nami nikaendelea tu kujituliza ili nisije kujikuta napandwa na hisia mbaya kuelekea kauli zake Stella; ingawa alikuwa na pointi.
Baada ya hayo, akawa ameondoka na muuguzi wake walipomaliza kumcheki Jasmine na watoto, ikiwa kwamba sisi wengine tungetakiwa kuondoka pia baada ya muda mfupi ili kumpa mama mpya nafasi ya kupumzika, isipokuwa tu mama yetu na Nuru ndiyo wangebaki hapo kuangalia mengi ya mahitaji yake wakisaidiwa na wauguzi. Jasmine angekaa leo, labda na kesho pia, halafu kesho-kutwa ndiyo angeweza kuondoka hospitalini, na Kevin alikuwa na hamu ya kumrudisha nyumbani kwake hatimaye wakiwa wameshapatana. Watoto wao walikuwa wamewaunganisha, tofauti zao wakaziweka pembeni kabisa, ilipendeza!
Basi, muda ukazidi kutembea, ikiwa imeshafika saa nane, wengi wa waliokuwa wamekuja kumwona dada yangu tayari waliondoka, nikiwa nimebaki mimi, Miryam, Kevin, Nuru, na mama, na sisi hatimaye ikawa imefika zamu yetu kuondoka pia baada ya muuguzi kusisitiza sana. Angalau tulipata kumbeba pacha mmoja aliyewahi kuamka shauri ya njaa, na tukambeba huku akipiga mwano wa maana kwelikweli, ndiyo akawekwa kwa mama yake ili amtulize. Maumivu ya Jasmine yalifunikwa kwa furaha aliyohisi kuwa mzazi kwa mara ya kwanza. Miryam alikuwa akimtazama Jasmine kwa macho yaliyojaa furaha na matamanio mengi, yaani nilihisi kabisa akiwa anatamani kuvaa viatu vya Jasmine pia vya kuwa mzazi. Ingebidi nifanye mambo na jambo ili kumfikisha mwanamke wangu huko pia!
Kwa hiyo tukawaaga waliobaki vizuri, nikiwa nimewaahidi kuja tena baadaye na hata kesho, nasi tukaanza kuondoka. Tuliondoka pamoja na Kevin, lakini yeye akahitaji kwenda kwanza kuongea na daktari fulani hapo hospitali, hivyo akatuambia tutangulie tu. Hatukuwa na shida kushuka mpaka chini, na wakati tulipokuwa tunaelekea nje ya jengo, yaani kupita huu mwanzo wa sehemu ya kuingilia ndani ya hili jengo kwenye mapokezi na nini, nikawa nimemwona Stella. Alikuwa usawa wa kioo/dirisha la chumba cha mhudumu mmoja wa mapokezi, akiongea naye kama kumpa maelekezo, nami nikataka tumpite tu pamoja Miryam bila kumsemesha wala kumwangalia.
Nadhani Miryam pia alikuwa amemwona, lakini hakukuwa na umuhimu wowote wa kujisumbua kufanya kama vile tunahitaji mno kusema naye, eti kama vile tulijuana sana. Hapana. Tukampita tu, tukiwa tunasikia akicheka kidogo na huyo mwenzake, kisha kikafata kitu ambacho nilikuwa sitaki kitokee kabisa.
"Jayden..."
Stella akawa ameniita bwana, nami nikamwangalia Miryam usoni kukuta ndiyo anasimama na kugeuka pia kuniangalia, nami nikasimama pia. Nikageuka na kumwona Stella akija upande wetu taratibu, kukiwa na watu kadhaa sehemu hiyo waliohitaji huduma na hivyo baadhi yao kututazama sana mpaka mwanamke huyu alipokaribia upande wetu. Wakati huu, alikuwa amevaa miwani yenye mwonekano kama miwani ya macho, pana, lakini najua haikuwa ya kutia macho dawa kabisa. Ila ilimpendeza.
Akiwa amefika mbele yangu, akauliza, "Ndiyo mnaondoka?"
Nikatikisa kichwa kukubali hilo.
"Naweza kuongea na wewe mara moja?" Stella akaniuliza.
"Umeshaanza kuongea," nikamwambia hivyo.
Akamtazama Miryam na kusema, "Dada... samahani, ninaomba niongee na... mume wako... mara moja."
"Stella sema unachotaka kusema, Miryam hana shida," nikamwambia hivyo.
Miryam akawa anamwangalia kwa utulivu tu.
Stella akaniambia, "Ni jambo nyeti Jayden. Langu mimi na wewe."
"Oh well, Miryam tayari ameshazijua na kuziona nyeti zangu zote, kwa hiyo sidhani hilo litakuwa shida," nikamwambia hivyo.
Stella akatabasamu kiasi kwa kukunja midomo yake.
Miryam akasema, "Usijali Jayden. Me nitakusubiria hapo...."
"Hapana, tunaondoka wote. Stella... niambie unataka kusema nini. Nina haraka," nikaongea hivyo.
"Unajua ninataka kusema nini, na unajua ni kitu cha muhimu kuliko hiyo haraka yako. Bado hujaachaga kujifikiria we' mwenyewe tu?" Stella akaniambia hivyo.
Nikahisi kuudhiwa na maneno hayo, nami nikajizuia kumjibu kitu kibaya mbele ya Miryam.
Miryam akasema, "Vipi ukipanga wakati mwingine mzuri ili mwongee?"
Nikasema, "Yeah, Stella... nitakutafuta. Tutaongea."
Stella akanipandishia nyusi yake moja huku akinitazama kwa njia iliyoonyesha hakuamini maneno yangu.
Nikamwambia, "Fine. Chukua namba yangu. We' ndiyo utanitafuta, na utanipanga."
"Namba zako ninazo. We' ndiyo uiondolee ya kwangu block, ikiwa haujaifuta," akaniambia hivyo.
Nikaangalia pembeni kwa kuhisi kukerwa zaidi.
Stella akamwambia Miryam, "Samahani Miryam. Hizi drama hazifai, I know."
"Haina shida. Naelewa," Miryam akamwambia hivyo kistaarabu.
"Unaelewa eh? Vizuri," Stella akamsemesha hivyo.
Nikamtazama kimkazo. Yaani sijui alikuwaje, aliongea kwa njia yenye kutojali kabisa.
Akaniangalia na kusema, "Nipigie kwenye saa nne, Jayden. Saa nne. Usipopiga, nitachukulia uliifuta namba yangu, kwa hiyo me ndiyo nitakupigia. Usipopokea wala kupatikana, nitajua umefanya makusudi, and that won't be good for you."
Khh! Yaani aliniambia hivyo kwa utulivu kabisa mbele yake Miryam, nami nikabaki kumtazama machoni kwa njia makini.
Akamtazama Miryam na kusema, "Aam... muda ule nilisikia mnasema mmekuja kwa usafiri, mnarudi tena kwa usafiri?"
Miryam akatikisa kichwa kukubali.
"Okay, well... nilikuwa natoka mara moja pia. Sijui labda... niwape lifti?" Stella akamwambia Miryam hivyo.
Nikamwangalia kwa ukali kiasi na kusema, "Tutatembea mpaka nyumbani, hatuhitaji lifti yako."
"Jayden..." Miryam akaniita kwa sauti ya chini kama kunizuia.
Stella akacheka kidogo kwa pumzi na kusema, "Ameshazoea kuchukulia kila kitu nachotaka kufanya kuwa kibaya tu. Sijamwambia Miryam hivyo kwa ubaya, usinione kuwa mbaya. Haiko kama ilivyokuwaga tena Jayden. Mambo yamesha-change sa'hivi, move on... huu ukuta unaondelea kuweka moyoni utakuangukia we' mwenyewe tu usipokuja kuangalia. Cheer up."
Nikainamisha uso kiasi na kusema, "Yeah, okay. Samahani. Namba yako ninayo. Nitakutafuta. I mean it."
Akatikisa kichwa kuonyesha uelewa, naye akamwangalia Miryam na kusema, "Haya. Nimefurahi kukutana nawe dada. I hope tuta-catch up soon."
Miryam akamtikisia tu kichwa kukubali hilo, nami nikaanza kutembea na Miryam akifuata kwa ukaribu.
Dah, yaani hii ya kukutana na Stella kwa mara nyingine ilikuwa imenivuruga kweli. Kale kahisia tu kalikoletwa na kuwazia mambo yaliyopita ambayo nilipitia na huyo mwanamke ndiyo kalikokuwa kakifanya nijihisi ovyo kila mara jina lake lilipotajwa, na sasa kukutana naye tena yaani ndiyo ikawa kama vile hiyo "ovyo" imeovyeka zaidi. Hisia ilikuwa mbaya sana hasa kwa sababu ndiyo alikutana na Miryam kwa mara ya kwanza lakini akamwonyesha na kaujeuri kake pia. Ndivyo ambavyo Stella alikuwa, sehemu ya utu wake yaani, lakini hakuwa mtu mbaya. Kilichokuwa kimefanya nimwone vibaya ni historia yetu tu, lakini siyo kwamba alikuwa mke wa Shetani.
Ningetakiwa kujipa utulivu zaidi ili kweli nikija kumtafuta na kuongea naye kuhusiana na suala la mtoto wetu, iwe kwa njia ambayo haingezua ugomvi wowote. Kuijua asili ya mwanamke huyo kungepaswa kuniongoza kujiandaa kwa ajili ya maongezi ambayo hayangekuja kugeukia upande mbaya, kwa sababu nahisi alikuwa ameudhika baada ya kukutana na mwanamke ambaye nilimwita "mke wangu," huku ni yeye ndiye akiwa mama wa mtoto wetu. Hiyo hali ipo, kwa wale wanaosemaga 'wivu sina, ila roho inauma,' ndiyo nadhani Stella alikuwa kwenye hiyo zoni.
Tukaendelea tu mimi na bibie wangu kuondoka kutoka hospitalini hapo, mdogo mdogo tukienda eneo la barabara ili kuchukua kama siyo daladala basi bajaji, na kabla hatujaifikia lami, kweli Stella akawa ametupita akiwa ndani ya gari lake jeupe aina ya Crown Athlete, na hata akatupungia mkono na kusonga mbele. Ni Miryam pekee ndiye aliyerudisha salamu hiyo ya mkono, yaani mimi bado nilikuwa na-process, na baada ya hapo mimi na Mimi wangu tukaelekea lami na kukodi bajaji moja ambayo ingetupeleka moja kwa moja hadi Bamaga. Tukawa tumeiacha Rebinansia kiaina.
★★
Mwendo ndani ya bajaji ukaendelea kutupaisha kuelekea tulipodhamiria, na toka tumepanda bajaji hii, Miryam hakuwa ameongea lolote lile kabisa. Alitulia tu, mara kwa mara nikimwangalia na hata kusisitizia kumtazama ili aniangalie japo mara moja, lakini akawa kama vile amemezwa na fikira zingine na kutonitazama hata kidogo. Kwa haraka nikakisia kwamba alikuwa ameanza kumuwaza sana Stella, labda akiwa amekoseshwa amani kiasi na mwanamke yule, ila kama sivyo, basi kuna jambo lingine lililokuwa linamtafuna akilini.
Nikaamua kutoa simu yangu na kumpigia Salumu, nami nikamwambia kuwa nilielekea huko Bamaga mida hii hii hivyo kama angekuwa mbali basi aniambie wapi pa kuzikuta funguo, ikiwa hakuondoka nazo. Lakini Salumu akasema hakuwa mbali, na kama nimekaribia kufika huko yaani ningemkuta ameshaingia pale kwangu na kupaweka tayari zaidi, ni mimi kufika na kuingia tu kama siku ile. Nikampa shukrani na kusema ndiyo, nimekaribia, hivyo tungeonana ndani ya muda mfupi. Nilipokata hatimaye, nikamwangalia Miryam kukuta nado ametazama pembeni tu, nami nikaona nimshtue kidogo.
Nikafanya kumtumia ujumbe kwenye simu, bado tukiwa humo humo kwenye bajaji, naye alipoupata akafungua simu yake kusoma. Najua alikuta nimemtumia neno 'mambo' na kaemoji kenye kuonyesha busu, na hatimaye aliponitazama, akakutana na mdomo wangu ukiwa umemkaribia huku nikionyesha kutaka kumbusu. Akatabasamu na kuusukuma uso wangu pembeni, nami nikatabasamu kidogo. Kuanzia hapo ndiyo nikaanza kumchokoza zaidi, nikimwonyesha kimasihara kwamba nataka tufanye jambo la faragha humo humo kwenye bajaji, naye akawa anajizuia kucheka na kunisukuma kila mara ili niache kumsumbua.
Nikawa nimefurahi kuwa angalau nilimfanya atabasamu, na ndiyo tukaanza kusemeshana hatimaye. Nikamuuliza kwa nini alikuwa kama hana raha sana, lakini akaniambia alikuwa poa. Ikiwa ni saa tisa inayoelekea kuingia saa kumi jioni wakati huu, nikaona niilaumu njaa, nikimwambia nahisi ni njaa ndiyo inayomsumbua ila hataki tu kusema, hivyo nikamwahidi kupitia msosi wa nguvu ili twende kukamulia pale kwangu. Yote ilikuwa sawa kwake, na bado alionekana kama hana raha kivile, hivyo nikakishika tu kiganja chake na kuendelea kutulia, nikiwa nawaza kwenda kuzungumza naye zaidi tukifika huko mbele.
Si dakika nyingi sana kupita nasi tukawa tumeingia Bamaga, kituoni kabisa, nami nikamwelekeza bajaji atusogeze sehemu niliyojua ilikuwa na mgahawa bomba ili tubebe msosi kabla ya kuingia pale kwangu. Tulipofika, nikalipia bajaji na kuelekea ndani ya huo mgahawa, nikamwelekeza malkia wangu akae kwenye meza moja, kisha nikaenda kutoa 'oda' ya vyakula nilivyohitaji na kuagiza vifungwe, halafu nikarudi kwa bibie nikiwa nimemnunulia soda; na mimi pia. Tukakaa hapo tunashusha soda taratibu, nikimtikisia nyusi kichokozi na yeye akizungusha macho kama vile hataki, halafu nikaanza kuweka macho yangu kimakengeza huku nikimzomea.
Nadhani hiyo ikamfanya ashindwe kujizuia kukaza na kucheka kidogo, nami nilipoendelea, akaniponda na kisoda. Ilipendeza sana yaani hata bila maneno niliweza kumfanya ajihisi kujiachia kwangu, nasi tukawa tunatabasamiana tu huku watu hapa na pale wakitutazama. Dakika ishirini na kitu kupita na vyakula vikawa tayari, hivyo tukanyanyuka, nikalipia, kisha tukatoka hapo na kutembea mwendo mfupi kuelekea makazini kwangu. Jua la saa tisa ya mwishoni lilikuwa linachoma bado, nasi tukakata kama dakika tano tu na tayari tukawa tumeingia getini mwa condo langu.
Salumu alikuwa ndani, naye akaja kutupokea na kutupa salamu kwa shauku kama kawaida yake. Ikawa ni maongezi mafupi baina yangu mimi na yeye baada ya Miryam kutangulia ndani na mifuko ya vyakula, kisha ndiyo Salumu akaondoka hapo na mimi kuelekea ndani pia. Mwanamke wangu alikuwa ameshajua namna ya kujistarehesha hapo, yaani nikamkuta akiwa sehemu ya jikoni ameanza kuandaa sahani na nini, nami nikamfata hapo na kuanza kumshika hapa na pale mwilini na kumbusu shavuni huku nikimkumbatia. Akaniasa niache hayo mambo na niende kutulia pale sehemu yenye masofa, nami nikatii. Leo ni yeye ndiyo alitaka kuandaa mambo kama mke mwema.
Kwa hiyo mzee nikafikia masofani na kusogeza meza ya hapo kati karibu zaidi na sofa moja, halafu nikaenda kuwasha TV. Kulikuwa na makato ya mwezi kwenye king'amuzi ya malipo ya vifurushi vya chaneli na kwa kuwa sikuwepo, chaneli hazikuwa nyingi zenye kuburudisha, hivyo nikaamua tu kuweka flash moja yenye movie na kuchagua moja ya 'animation.' Miryam tayari akawa ameanza kuweka vyakula mezani, nami nikaongozana naye kwenda kunawa, kisha kwa pamoja tukarudi sofani na kuanza kula. Alikaa kwa ukaribu nami huku akila taratibu tu, na hakuongea lolote ila kuniangalia usoni mara moja moja kama vile hajali yaani.
Nikajikuta nacheka kidogo na kuegamia sofa kwa mgongo kabisa, kisha nikakishika kiuno chake na kumtekenya kidogo huku nikisema, "Niambie unawaza nini."
Akautoa mkono wangu kiunoni kwake na kuendelea kula, bila kutoa jibu lolote.
Nikamsogelea mpaka karibu na uso wake na kumwambia, "Naona kuna kitu unawaza sana tokea tumeondoka hospital. Niambie basi."
Akabaki kimya tu.
"Mimi, si nakusemesha?"
"Hebu kula Jayden. Ni vibaya kuongea wakati wa kula," akasema hivyo.
"Toka lini?" nikamuuliza.
Akanikata jicho kali kwa ufupi, kisha akaendelea kula.
Nikaendelea kula pia na kusema, "Sawa. Kama hutaki kuongea fresh."
Akasitisha kula na kuniangalia kwa ile njia ya kuonyesha kama vile nimemkwaza, kwa ile namna ya kwamba anataka tu nione hilo.
Nikamwangalia usoni pia na kuuliza, "Nini?"
Akaacha kuniangalia na kuendelea kula na kuangalia TV.
"Nikikusemesha, hutaki kuongea. Nikikuacha, unaniangalia tena hivyo. Asa' me nifanyeje?" nikamuuliza.
Akashusha pumzi tu na kuendelea kula.
Nikatabasamu kiasi na kusema, "Najua ni Stella ndiyo unayemuwaza."
Akaniangalia kiudadisi na kuuliza, "Stella?"
"Mmm," nikakubali.
"Kwa nini nimuwaze Stella?" akauliza.
Nikapandisha nyusi huku nikimtazama kwa macho ya kumwambia anaelewa vizuri jibu la hilo swali.
Akaacha kuniangalia na kucheka kwa mguno, kisha akaendelea kula tu.
"Najua atakuwa amekukera. Miryam... usimwaze huyo. Yaani hatawe...."
"Wewe ndiyo umenikera, Jayden!" akasema hivyo bila kunitazama.
"Mimi tena? Nimefanyaje?" nikamuuliza.
Akaniangalia na kuuliza, "Kwa nini hukuniambia Stella wako ni daktari?"
"Nikwambie ili iweje? Hata kama angekuwa mkandarasi, ama mwanamuziki, ingesaidia nini?"
"Jayden, yaani unaniambia mimi hivyo?" akaniuliza kwa njia makini.
"Sina maana mbaya... yaani, sioni umuhimu wowote wa... kuanza kukuambia sijui Stella anafanya nini, au nini... I don't care about her. And neither should you," nikamwambia hivyo kwa upole.
"Naweza ku-care ndiyo kwa sababu nimegundua mama wa mtoto wako anafanya kazi iliyo sambamba na yako. So, mnaweza kuwa na ukaribu zaidi ya...."
"Miryam... acha kuwaza hivyo. Kwamba nini, unaona wivu, unafikiri Stella ataniiba, au?"
Akaniangalia kwa macho makali.
"Ahahah... natania. Halafu, usije tena kusema "Stella wako," sitapenda. Hiyo kitu usiiseme tena. Unanielewa?" nikamwambia hivyo.
Akaendelea kuniangalia kwa utulivu.
"Na, in all honesty... yule mwanamke sina, yaani.... sijui hata nikwambieje. Isingekuwa tu kwamba nina mtoto pamoja naye, hata tu kumsemesha leo nisingemsemesha. Unaweza ukadhani zangu na zake zinapanda kisa yeye daktari, lakini hata chembe. Sina shobo na huyu mwanamke kabisa," nikamwambia hivyo.
Akakirudia chakula chake.
"Kwa hiyo hauna haja ya kuhisi wivu, sawa?" nikaongea kichokozi.
"Aliyekwambia nahisi wivu, nani?" akauliza hivyo na kuniangalia kimkazo.
Nikacheka kidogo na kutikisika tu kichwa.
"Sijapenda tu hiyo setting," akasema hivyo na kuendelea kula.
"Najua. Ila ye' yupo Rebinansia, me niko Muhimbili. Cha kuwaza nini? Sema... nisamehe kwa kutokukwambia mapema, sikuona tu haja. Na najua imekukera hasa kwa sababu Stella huwa ana maudhi sana," nikasema hivyo na kuendelea kula pia.
"Eti alikuwa anataka kutupa na lifti," akasema hivyo huku akiangalia pembeni kwa ufikirio.
"Ni mchokozi," nikasema hivyo huku nikimtazama kwa hisia makini.
Akaniangalia na kusema, "Kwa hiyo kumbe ilikuwa makusudi kabisa. Alifanya hivyo kuni-provoke."
Nikajikuta nacheka kidogo kwa pumzi.
"Unacheka nini?" akauliza.
"Ahahah... si hivi unavyoongea? Unasema hauhisi wivu wala nini, lakini tayari ushaanza kupiga statistics hapa, ku-countermeasure figisu yoyote ile ambayo Stella anaweza kuleta, ili...."
"Simwogopi huyo mwanamke," akasema hivyo.
"Najua. Ila napenda tu unavyokuwa makini hivi," nikamwambia.
Akashusha pumzi na kusema, "Napenda amani. Ila... nahisi tukiendelea ku-cross njia na huyo Stella, ipo siku tutatibuana. Kuna kitu tu ndani yake nimeona kinaniambia anapenda sana... michuano-michuano."
"Achana naye. Na kwa nini ifike hadi huko? Ye' ni mjeuri sawa, ila siyo kwamba ni mtu mbaya. Hakuna sababu ya nyie kutibuana labda muwe mmeibiana mawigi..."
Akasonya kidogo na kutabasamu.
"Ahah... Kila kitu kiko poa. Leo nitampigia, tutaongea kuhusu ishu ya mtoto, then tutapanga tuje tukutane. Na... nataka tukija kukutana na we' uwepo," nikamwambia hivyo.
Akatabasamu kiasi.
"Yaani sasa hivi la muhimu kwa upande wa Stella ni huyu mtoto, isingekuwa hivyo, tusinge-cross njia na yeye kabisa. Besides, atakuwa na mtu wake pia, wala usihisi uhitaji wa kuwa defensive. Na najua we' kweli unapenda amani, ipo siku itafika mtakuwa mashosti... mnakaa mnanisema wee..."
"Ah, hamna. Sidhani kama damu zetu zitaendana," akasema hivyo.
"Eti eeh?"
"Mmm."
"Okay sawa. Basi we' kula zako pamoja nami, na ye' ale zake huko huko. Asitupe stress tena..." nikamwambia hivyo huku nikisugua mgongo wake taratibu.
Tukaendelea kula kiutulivu, naye akaniambia, "Tuongee kuhusu ishu ya nyumbani sasa."
"Mm-hmm... niambie," nikamjibu hivyo.
"Sina... ahh... nawaza tuchukue approach gani sasa hivi ili kuweka mambo sawa zaidi kwa ma' mkubwa. Jana hiyo...."
"Nilivyoongea kwa jazba ikaonekana kama nawadharau. I know. Itabidi nizungumze nao tena. Ndiyo kilichopo. Niwaombe samahani, na... niwashawishi waone upendo wangu kwako kwa kina. Nafikiri bado wanahisi nitakuchezea tu," nikamwambia hivyo.
"Kumbe?" akauliza kikejeli.
"Ah, hivi we' unanionaje?" nikamuuliza hivyo kiutani pia.
Tukacheka kidogo kwa pamoja, naye akaniambia, "Mariam sasa hivi amejua kuhusu me na wewe."
Nikatulia kuendelea kumsikiliza.
"Alisikia maongezi yetu jana wakati yuko chumbani. Ndiyo nimeenda kulala akaniuliza, nikamwambia ukweli... na najua alihuzunika," akaongea kwa hisia.
"Alisemaje?"
"Hakusema lolote. Yaani... akaonyesha tu ameelewa na kulala... ila najua alikuwa hajatarajia. Sijui sana ila nahisi na hapo nimevuruga..."
"Miryam, usiseme hivyo. Na... ahh... ni makosa yangu tu, yaani Shadya hakutakiwa kutukuta namna ile, ila ndiyo yameshatokea. One way or the other, wangejua tu. Na sasa wanajua, ni sisi kufanya iwe wazi kwamba hatutanii. Na, Miryam nasisitiza hili. Hata kama nani asipopenda me kuwa na wewe, hatuwezi...."
"Kuachana," akamalizia maneno yangu.
"Imeisha hiyo," nikamwambia hivyo.
Akatabasamu na kuweka nyama taratibu mdomoni.
Nikala moja pia na kusema, "Nataka nitafute njia nzuri ya kuongea na Mariam pia. Tulikuwa tumeshaongea kwa ufupi na akaniambia atajitahidi kuzoea, ila kwa hii hali mpya itabidi iwe ni kwa level ya juu zaidi ya kuzoea."
"Kabisa. Please do something, sitapenda kumwona mdogo wangu akiwa na distress," akaniambia hivyo.
"Usijali. I got this," nikamwambia hivyo kwa uhakikisho.
Akatikisa kichwa kwa kufarijika.
Tukaendelea kula, kisha nikasema, "Kesho asubuhi utanipa gari lako niondoke nalo."
Akaniangalia na kuuliza, "Kwa nini?"
"Jana ile ndiyo nilienda kufanya process za kukuchukulia gari jipya, nilienda huko Morocco kabla ya hayo ya Shadya kuja kutokea, so... nikaweka na bargain...."
"Kwa gari langu?"
"Yeah."
"Ih! Mbona hukuniambia sasa? Hapo si itahitajika makaratasi na procedure za kuliuza ni...."
"Ah, usijali Miryam. Kila kitu na-handle. We' kesho niachie gari nilipeleke huko, halafu nitarudi na la kwako jipya," nikamwambia hivyo na kutabasamu.
Akatabasamu pia na kusema, "Okay. Nitafanya hivyo, na... unaleta gari la aina gani?"
Nikala nyama na kusema, "Utaona."
"Ahahah... si uniambie?"
"A-a-aah... ni surprise."
"Yaani we' kila kitu lazima iwe surprise..."
"Oh, hii ni baab kubwa, kwa hiyo lazima iwe surprise."
"Ona, Jayden... tafadhali usi...." akaishia hapo.
"Nini?"
"Usiniletee gari la gharama sana," akaniambia hivyo.
"Ahah... kwa nini?"
"No, ikiwa unawaza tu kuleta gari lenye gharama kubwa, usifanye hivyo. Ningependa gari simple tu," akasema hivyo kwa upole.
"Mm? Sasa... mbona nilikuwa nimeshaagiza Escalade kabisa?" nikamwambia hivyo kiutani.
"Nini?!" akashangaa.
"Ahahahah... nakutania. Ndiyo nitaenda kuchagua hiyo hiyo kesho. Nilipanga nikuchukulie zuri sana, na la gharama pia, ila...."
"Hapana, Jayden. Kama ni gari... nichagulie tu la kawaida," akaniambia hivyo.
Nikabaki kumtazama machoni kwa njia yenye utathmini.
"Umeelewa?" akauliza.
Nikatabasamu kiasi na kusema, "Yeah, nimeelewa. Uliniambia me sina makuu, ila kiukweli... hiyo kitu nimeitoa kwako. We' ndiyo beacon ya kutokuwa na makuu kabisa."
"Ahahah... acha mambo yako," akasema hivyo na kuendelea kula.
"Hahah... Kwa hiyo, nikuletee tu gari lolote zuri kesho?" nikamuuliza hivyo.
Akatikisa kichwa kukubali.
"Utapenda uchaguzi wangu kabisa?"
Akasema, "Yeah. Nitapenda chochote utakachopenda."
Nilijihisi vizuri zaidi baada ya maongezi hayo, nasi tukaendelea kula kiutulivu mpaka tuliposhiba, na mwanamke wangu akaenda kuniletea maji ya kunywa na kuigiza kunipatia huku anapiga magoti, nami nikampa shukrani kwa busu ya shavu, kisha akaelekea kusafisha vyombo. Alipomaliza akarejea sofani tena na kupumzika hapo pamoja nami, akinilalia begani na kujiweka karibu zaidi na mwili wangu ili astareheke, nasi tukatulia hapo huku tukitazama movie nzuri ya Coco.
★★
Saa zima na nusu likawa limekata, ikiwa inaelekea kuingia saa moja, na Miryam alisinzia kidogo hapo hapo sofani huku akiwa amenilalia. Yaani alijikunyata kwangu kama mtoto vile, na sikutaka kumwamsha, lakini akawa ameshtuka baada ya mwito wa simu yake kumpigia kelele. Ndiyo akajinyanyua na kupokea, naye akazungumza pamoja na Tesha huku akirudi kunilalia tena. Tesha alikuwa anamjulisha kuhusu ishu fulani ambayo Miryam alimpanga mapema afanye, kwa hiyo yakawa ni maongezi mafupi tu, kisha akakata simu.
Hapa ndani palikuwa pameanza kuingiwa na hali ya ugiza isipokuwa kwa mwanga ambao TV ilitoa, naye Miryam akapendekeza tujiandae kuondoka sasa kurudi Mbagala. Nikamwambia kama angependa basi tungelala hapa, na akasema alitamani, ila kwa leo hakuwa amepangia hilo. Kwa kumwelewa, jibu kwa wazo lake likawa ni kukubali, na baada ya kutulia kwa dakika chache ili amalizie raha yake ya kunilalia, ndiyo tukanyanyuka na kujiweka vizuri zaidi kwa ajili ya kuondoka. Yeye alienda na kunawa uso kidogo, kisha ndiyo akajiweka vizuri na kujiunga nami nje ya nyumba, ambapo nikafunga vizuri na kuanza kulitoa gari langu nje.
Sikuwa na mpango wa kumwita Salumu huku tena maana najua ningerejea mapema, hivyo nikalifunga tu geti, kisha nikaingia garini na kuanzisha mwendo kuelekea Mbagala hatimaye. Nikaongea na bibie kwa ufupi kuhusiana na ishu ya kwenda pale kwake leo, nikisema kama ingemfaa basi twende pamoja ili nijaribu kuzungumzia na mama zake wakubwa, naye akakubaliana na hilo. Kwa vile wakati huu alisema Shadya na Bi Zawadi walikuwa wapole, wa kumshawishi zaidi angekuwa ni Bi Jamila, na baadaye ningehitaji kuongea na Mariam pia. Bado nilikuwa najihisi hatia kiasi kumwelekea huyo msichana, kwa hiyo kweli ningetakiwa kumwajibikia ili kuweka mambo sawa zaidi.
Hakukuwa na misukosuko mingi barabani, tukawa tumeifikia Mbagala ikiwa ndiyo imeingia mida ya saa mbili. Nikaliingiza gari eneo lenye jengo la soko kubwa, naye Miryam akaelekea huko ili aweze kununua vitu fulani kwa ajili ya kupeleka nyumbani. Mimi pia nikashuka na kwenda kuchukua mishkaki ile ambayo tulikula na Mariam na Tesha siku kadhaa nyuma, nami nikarudi na michache kwenye gari kisha kumpatia Miryam ale pia. Hakuwa amekula kwa muda mrefu, hivyo aliifurahia sana. Safari ikaendelea hadi tulipofika Masai, nami nikaliegesha gari langu nje ya hilo jengo. Nilipanga kuja kuliacha gari langu kwa usiku huu kwenye zile sehemu wanazolaza magari, hivyo nikalifunga vizuri na kuanza kuelekea makwetu pamoja na bibie.
Macho ya wengi yalikuwa kwetu kutokea hapo Masai. Tukatembea pamoja hadi tulipoifikia nyumba yake, na hapo dukani kwa Fatuma walikuwepo wanawake kadhaa waliotupa salamu na kuendelea kutuangalia kama vile wameona vyakula, nasi tukaingia ndani ya geti na kukuta gari lake bibie likiwa hapo nje. Miryam akawa ameuliza ikiwa ingetakiwa niende nalo huko Morocco hiyo asubuhi na mapema basi anipatie funguo za gari hili wakati huu huu, lakini nikasema haina shida, angeweza tu kunipa hiyo hiyo kesho maana nisingewahi kihivyo. Kwa sasa akili yangu yote ilivutwa zaidi na kwenda hapo ndani kwake kujaribu kuongea na mama wakubwa vizuri zaidi, naye akanishika kiganja kama kunipa nguvu.
Tukaupita mlango na kuingia ndani baada ya hapo, na sehemu ya sebule alikuwepo Bi Zawadi na Bi Jamila pia, huku Shadya akiwa amekaa sofa lingine pamoja na Mariam wakiangalia TV. Kulikuwa na hali fulani hivi ya ukimya baada ya sisi kuingia, na iliendelea hata tulipotoa salamu na wao wote kutuitikia vizuri tu; isipokuwa Bi Jamila. Mariam akanyanyuka na kumkumbatia dada yake kwa ufupi, kama jinsi tu alivyozoea, naye akaichukua mifuko aliyobeba dada yake na kuelekea jikoni, akituacha "watu wazima" hapo sebuleni.
Nikakaa sofa moja na Miryam, kwa utulivu tu, nami nikawaangalia wakubwa wote. Shadya alikuwa ametulia tu akitutazama kwa njia ya kawaida, na Bi Zawadi alituangalia kwa macho yenye subira, huku Bi Jamila akishikisha kiganja chake kwenye taya na kuegamiza mkono sofani, asitake kutuangalia moja kwa moja. Kulikuwa na tamthilia ya kibongo hapo runingani, Bi Jamila akiitazama kama vile imemteka sana kifikira, lakini najua alikuwa akisubiri kusikia kutoka kwangu mimi na Miryam, vilevile na wengine pia.
Miryam akasema, "Za hapa jamani?"
"Nzuri tu mama," Bi Zawadi akamjibu kwa utulivu.
"Salama tu," Shadya pia akajibu.
"Huyu yuko poa?" Miryam akauliza hivyo, akimaanisha Mariam.
"Eeh, ametulia tu leo," Bi Zawadi akamwambia.
"Okay. Nilikuwa nimemtuma Tesha ile mchana, ameshafanya ile ishu?" Miryam akasema hivyo kumwelekea Shadya.
"Eeeh, tayari. Alikuja dukani kwangu akaniambia, ndiyo nikampa, akayaleta," Shadya akamwambia hivyo.
"Sawa. Yupo?" Miryam akauliza.
"Hamna, yupo hapo kwa Ankia na yule rafiki yake mrefu hivi..." Shadya akamwambia.
"Bobo?" Miryam akauliza.
"Eeeh," Shadya akajibu kistaarabu.
"Sawa," Miryam akasema hivyo.
Miryam akaniangalia kwa ufupi, mimi pia nikamwangalia, kisha tukawatazama mama wakubwa kwa pamoja.
Bi Zawadi akamwangalia mwenzake pembeni pia, halafu akatutazama sisi na kusema, "Habari za huko mlikokuwa?"
"Nzuri tu. Tulikuwa tumeenda hospitali," Miryam akamjibu.
"Kumwona nani? Nani anaumwa?" Bi Zawadi akauliza.
Miryam akatabasamu kiasi na kuniangalia, nami nikasema, "Dada yangu amejifungua leo."
Wengine pia wakanitazama.
Bi Zawadi akatabasamu na kuuliza, "Kweli?"
"Ndiyo. Amejifungua mapacha," nikasema hivyo.
"Eh! Jamani, hongera," Bi Zawadi akaniambia hivyo kwa hisia.
"Asante. Ila... me sijafanya chochote," nikatania kidogo.
Miryam, Bi Zawadi, na Shadya wakacheka kidogo, naye Bi Jamila akaangalia tu TV tena.
"Namaanisha hongera umekuwa uncle. Si... ni Jasmine ndiyo amejifungua?" Bi Zawadi akauliza.
"Eeeh," nikamjibu hivyo.
"Mapacha wa kiume au wa kike?" Shadya akaniuliza.
Nikamwangalia na kusema, "Wa kiume wote. Wana sura za baba yao."
Shadya akatabasamu kiasi. Inaonekana kweli alikuwa amelegeza.
Miryam akamwangalia Bi Jamila, naye akasema, "Mama..."
Bi Jamila akatugeukia na kutuangalia kwa njia ya kawaida.
"Jayden... namaanisha... JC ana maongezi na nyie kidogo. Ikiwa hautojali," Miryam akamwambia hivyo.
Bi Jamila hakutoa jibu, lakini akaendelea kutuangalia kwa njia iliyoonyesha alikuwa tayari kusikiliza pia. Shadya akachukua rimoti na kupunguza sauti ya kwenye TV.
Nikamwangalia Miryam kichini na kusema, "You are making this intense."
Miryam naye akanijibu kwa sauti ya chini, "Well regardless, you have to go for it."
Sisi wawili tukatabasamiana kiasi baada ya yeye kuniambia hivyo, nami nikamwangalia Bi Zawadi kukuta anatutazama huku akitabasamu kwa hisia.
Nikaanza kusema, "Wazazi wangu... kwanza naomba nianze kwa kusema samahani kutoka ndani ya moyo wangu kwa kilichotokea jana. Sikutenda ilivyofaa, na najua niliwaumiza pia kwa sababu hamjanizoea kwa njia hiyo. Sina kisingizio chochote cha kutetea namna nilivyowasemesha bila heshima... cheupe wangu... Bi Jamila... Shadya... naombeni mnisamehe..."
Niliongea hivyo kwa njia yenye kuonyesha toba ya kweli, naye Shadya akasema, "Ah, JC usijali. Usijali kabisa kijana wangu. Naelewa na mimi nilichangia kuku-push mpaka yakawa vile, yaani... nisamehe tu na mimi jamani. Nili-panick mno..."
"Hamna shida Shadya, huna haja ya kuomba samahani..." nikamwambia kiupole.
Akasema, "Jamani! Tatizo langu na mimi nina mdomo tu, naomba unizoee. Nilikuwa tu naogopa kwa ajili ya Miryam, lakini... sasa hivi nimeshaelewa na ninajua mnapendana. Yote yanayofata, ni ya kwenu kuamua, na kuyachagua, na kuyaishi. Mna baraka zangu. Sina lolote tena la kuongezea..."
Nikasema, "Imeshaenda hiyo..."
"Imeenda," Shadya akamalizia maneno yangu, nasi tukatabasamu kidogo kwa pamoja.
"Usiwaze tena kuhusu ya jana JC. Kila kitu kiko sawa upande wetu. Wewe na Mimi mnafaana sana," Bi Zawadi akasema hivyo.
"Umeona eh?" nikamwambia hivyo.
Bi Zawadi akacheka kidogo na kutikisa kichwa kidogo, naye Miryam akanisukuma kiasi kwa mguu wake.
Nikamwangalia Bi Jamila, ambaye alikuwa ananitazama kwa njia yenye huzuni fulani hivi, nami nikamwambia, "Mrembo wangu... JC nimefika. Yaani, niko hapa sasa kutimiza kile kitu ambacho ulisema siku ile. Uliniambia unatamani sana kumwona Miryam akipata mume, akianzisha familia, na hadi uje kucheza na wajukuu wako kutoka kwake...."
Bi Zawadi na Shadya wakacheka kidogo.
"Nilikusikia vizuri na kutilia maanani kila kitu ulichosema unatamani binti yako akipate ili afurahi, na mimi ndiyo nataka kujitoa kwake kwa asilimia zote ili nimpe furaha ambayo anastahili... kupita hata ile ambayo unaweza kufikiria yaani. Ninampenda sana Miryam," nikasema hivyo kwa hisia na kumwangalia bibie.
Miryam akawa ananiangalia kwa uvutio na utulivu wa kihisia.
Nikawa nimemtazama Bi Jamila tena, na mwanamke huyo akatazama tu pembeni kama kuonyesha kwamba bado anatatizwa kiasi na jambo hili. Tukaangaliana na wengine pia, Shadya akinionyesha kwa ishara ya mdomo na macho kwamba hali bado ni tete kwa upande wa mama mkubwa mkubwa, na Bi Zawadi akaonekana kukosa amani kiasi kutokana na jinsi mwenziye alivyokuwa na ubishi. Nikamtazama Miryam pia, ambaye alikuwa anamwangalia Bi Jamila kwa njia yenye kujali, nami nikaona ninyanyuke.
Nikasogea mpaka usawa wa sehemu ambayo Bi Jamila alikaa, nami nikashuka na kukaa chini kabisa kwa kukunja miguu katikatu karibu na miguu yake, huku wengine wakinitazama kwa umakini. Niliweza kuona kutokea hapo pale sehemu ya dining, Mariam akiwa amesimama kwa kuegamia ukuta karibu na friji, akiwa ananiangalia kwa njia makini. Inawezekana alikuwa amefatilia kila kitu kilichoendelea hapo kwa ukimya tu. Bi Jamila sasa akawa ananiangalia usoni, kwa njia yenye huzuni, nami nikakishika kiganja chake kimoja na kukiunganisha na vya kwangu kwa pamoja.
Kwa sauti yenye hisia, nikamwambia, "Mama... najua sikuongea vizuri sana jana, ila kwenye mengi niliyosema... niliyamaanisha. Ninampenda sana mwanao, na nitakuwa tayari kumwoa muda mwafaka ukifika. Sijaja kwenye maisha yake kucheza tu, nimeingia kwenye maisha yake ili niyashiriki pamoja naye pia, kwa sababu amenisaidia sana nijue tena nini maana ya kupenda... na ni kwa kuendelea kuwa pamoja naye sikuzote ndiyo itanifanya nisije kusahau tena nini maana ya kupenda. Nakuahidi. Hautakuwa na sababu yoyote ya kuhofu juu ya uhusiano wetu ukishaanza kujionea mwenyewe kwamba ni mahusiano yenye nguvu sana, na tutayafikisha kule ambako sikuzote umekuwa ukipaota kwa ajili ya Miryam. Niko hapa kutimiza ndoto hizo kwa ajili ya binti yako, na za kwako pia. Ninakuomba utupatie baraka zako za kutoka moyoni mama. Ndiyo zitakamilisha zaidi azimio la upendo wetu ili usije kamwe kuisha..."
Niliongea hivyo huku nikimwangalia kwa njia yenye hisia, nikiona wazi jinsi ambavyo Bi Zawadi na Miryam waliniangalia kwa matumaini, naye Bi Jamila akaweka kiganja chake kimoja mdomoni kama mtu anayejikaza kutolia.
Nikatabasamu kiasi na kumwambia, "Wewe ni sehemu muhimu sana ya furaha yake Miryam... pamoja na wengine... sasa ukijumuisha na mimi, yaani ndiyo tutakuwa tunampa bonge moja la furaha. Na hapo ni mwanzoni tu... bado na ya mbeleni yanayokuja ambayo ndiyo yatafanya hiyo furaha ipambe moto zaidi."
Bi Zawadi akatabasamu na kumtikisa mwenzake kwa bega huku akisema, "We' mwenyewe uliniambia, huyu kijana ni mzuri sana. Me hapa yaani kama asingenikuta nimeshazeeka, Miryam asingepata nafasi."
Kauli yake ikafanya tucheke kwa pamoja, naye Shadya akasema, "Ungemwiba mapema!"
"Nisingechelewa yaani. Anafaa kabisa. Na sasa hivi yeye kuwa na Mimi... ni bahati nzuri sana, Jamila unaelewa hilo. Hebu ruhusu vijana wafurahie maisha kwa kufurahi kwa ajili yao," Bi Zawadi akaongea kwa ustaarabu.
Nilifarijiwa sana na maneno yake Bi Zawadi, hata nikamwona Miryam akianza kulengwa na machozi. Bi Jamila akaniangalia, halafu akafumba macho yake akionekana kutafakari sana, halafu akafumbua tena na kuniangaliaaa... kisha akajisogeza upande wangu na kukileta kiganja chake kuushika uso wangu. Nikakishika kiganja chake pia huku nikitabasamu kwa hisia, yeye akiwa ananiangalia kwa njia ya kukaribia kulia kabisa.
Kisha akasema, "Nisamehe sana JC.... sitaweza kulibariki hili."
Kauli yake ikafanya tabasamu langu lififie, kwa kuwa kiukweli sikutarajia aseme hivyo. Nadhani aliwaacha wengine wakishangaa kiasi pia, naye akaashiria kutaka kunyanyuka. Nikasimama upesi nikiwa namwangalia kwa njia yenye kutatizika, nami nilipojaribu kumsemesha, akanyanyua kiganja kunikataza, halafu sasa yeye akiwa ameshasimama pia akaanza kuelekea upande wa Miryam ili bila shaka akimbilie chumbani. Nikawa namwangalia kwa umakini sana.
Miryam akasimama pia Bi Jamila alipokaribia usawa wake na kumsimamisha, naye akamwambia, "Mama... mbona... kwa nini umesema hivyo?"
Bi Jamila akawa anatikisa kichwa huku ameinamisha uso wake, naye akasema, "Hauwezi kuelewa, Mimi. Hauwezi..."
"Kuelewa nini?" Miryam akamuuliza.
Bi Jamila akawa tu anatikisa kichwa na kuendelea kuelekea upande wa vyumbani, akituacha sote tumeishiwa pozi hapo.
Bi Zawadi akainamishia uso wake kwenye kiganja, akiwa amechoka yaani. Nikamwangalia Miryam usoni na kukuta yeye pia ananitazama kwa namna iliyoonyesha ameghafilika sana yaani, na hakuelewa kwa nini bado mama mkubwa wake alishikilia huo msimamo. Hata mimi kiukweli nilishindwa kuelewa, kwa sababu mambo yote ambayo yangeweza kuonwa kuwa tatizo kwenye uhusiano wetu yalikuwa yamewekwa pembeni, lakini mwanamke huyo alionekana bado kusumbuliwa na uhusiano wangu na Miryam kwa sababu fulani isiyoeleweka kabisa. Hapa tatizo lilikuwa nini?
★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★
Pata Full Story WhatsApp au inbox
Whatsapp +255 678 017 280
Karibuni sana
Kabisaa😃 Ahadi ni deni kwa kweli