Unataka ndugu waoane?Ahaaa huyu bibi nae nn sasa jaman
Ahaa ahaa sasa itakuwaje na washakulanaUnataka ndugu waoane?
Unataka ndugu waoane?
Kulana kawaida tu mbaya kuzalishana!Ahaa ahaa sasa itakuwaje na washakulana
Yeah we believe him, asituangushe kwa leoElton tony tukumbuke ndugu yetu.
Nikwambie tu mwana hapa hamna jibu,kiukweli mi nimejiskia vibaya sana kwasababu nimepitia hiyo hali ya kusaidia na ku give-up.Mimi nina moyo wa kipumbavu sana. Najaribu... nafikiri kufanya hivi ndiyo inafaa, lakini kumbe ndiyo naharibu. Naangukia pua... mwisho wa siku ni mimi tu ndiyo naangukia pua. Hadi mdogo wangu nimeshindwa kumwongoza vizuri? Mpaka ana... hivi kweli jamani... ni nini kama siyo upumbavu? Ndiyo maana hata na wewe uliweza kunifanya nionekane mjinga mara ya kwanza tumekutana, siyo? Ni kwa sababu ya upumbavu wangu..."
MIMI NA MIMI 2
A Story by Elton Tonny
Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Tamaa, Hila, Usaliti, Siri, Mambo Yasiyotazamiwa
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA AROBAINI NA MBILI
★★★★★★★★★★★★★★★★★★★
Baada ya Bi Jamila kuingia tu chumbani kwake na kutuacha na maswali mengi hapo, nikamtazama Miryam usoni na kuona namna ambavyo alikuwa amevunjwa moyo na kitendo cha mama mkubwa wake, naye pia akaniangalia. Nikajitahidi kutoa tabasamu kwa njia yenye kumtia moyo, kisha nikasogea usawa wake Bi Zawadi, ambaye alikuwa akiniangalia kwa njia yenye huruma.
"Naona mrembo wangu mwingine bado anahitaji ushawishi zaidi," nikasema hivyo huku nikitabasamu.
"Ah, yaani me hata simwelewi kwa kweli. Sijui kwa nini amekuwa hivi," Bi Zawadi akaongea kwa huzuni.
"Usijali. Tumwelewe tu, bado ana-process. Unajua... nimeanza kuona anamfanana sana Miryam," nikasema hivyo.
Miryam akanitazama kimaswali.
Shadya akauliza, "Kwa nini?"
"Wakati ndiyo nimeanza kumtokea Miryam, alinizingua!" nikasema hivyo kwa njia yenye kuchangamsha.
"Wewe! Kweli?" Shadya akauliza hivyo kwa shauku.
Miryam akatabasamu kwa mbali, ijapokuwa bado aliniangalia kwa huzuni.
"We! Usipime. Kalikuwa kakali kweli, lakini sasa hivi kameshakufa na kuoza. Mrembo wangu na yeye ataenda kwa style hiyo hiyo tu, mpaka atakubali mambo," nikaongea kwa kufariji.
"Kweli JC. Taratibu tu, shangazi atakubali pia," Shadya akasema hivyo.
Bi Zawadi akasimama na kusema, "Tutaongea naye zaidi pia. Kila kitu kitakuwa sawa."
Nikamtazama Mariam pale alipokuwa amesimama, naye akaacha kuniangalia na kugeuka, akielekea jikoni kimya-kimya.
Nikamshika begani Bi Zawadi na kumwambia, "Ngoja sasa niwaache kwa muda huu. Tutaonana nafikiri... kesho."
Nilipoisema hiyo "kesho," nilikuwa namtazama Miryam usoni, na bado alinitazama kwa njia iliyojaa mfadhaiko.
"Si ungekaa kwa ajili ya chakula JC?" Shadya akaniambia hivyo huku akisimama.
"Ah, haina shida. Inabidi pia nikajimwagie upesi, maana... joto..." nikamwambia hivyo.
Nikamwangalia Bi Zawadi usoni na kukuta ananitazama kwa njia yenye huruma, nami nikamwacha na kumsogelea Miryam kwanza. Alikuwa akiniangalia kwa chini, yaani hakunitazama machoni wakati huu, nami nikakishika tu kiganja chake kimoja na kukikaza, yeye pia akikaza changu kiasi, kisha ndiyo nikatoka sehemu hiyo ya sebule na kuelekea nje. Najua ni lazima Miryam angejaribu kumsemesha Bi Jamila zaidi baada ya kilichotokea, na hivyo kuwaachia nafasi ilikuwa ni muhimu. Huyo mama alikuwa akisumbuliwa na jambo fulani, sijui nini tu, lakini bila shaka ningeweza kumwelewa muda si mrefu ikiwa Miryam angegundua shida yake.
Hivyo, mimi nikaelekea tu kwa Ankia na kumkuta mwenye nyumba wangu akiwa amekaa sebuleni pamoja na Tesha, Bobo, na mwanamke mwingine kijana ambaye sikuwahi kumwona kabla. Walinipokea vizuri kwa salamu, Ankia akiwa amekaa sofa moja na Bobo wake huku Tesha akikaa na huyo mwanamke sofa lingine. Walionekana kuwa marafiki, na baada ya hizo salamu na mimi kukaa sofa lingine pia, Ankia akawa ameuliza ikiwa dada yangu alijifungua salama, na kwa Tesha hii ikawa habari iliyovuta umakini wake pia. Ndiyo nikawaambia kwamba Jasmine alijifungua salama mapacha wawili wa kiume.
Ilikuwa sababu nzuri ya kuwafurahisha wote hapo, lakini mimi kwa kiasi fulani bado nilikuwa nimetatizwa na kilichotokea kwao Tesha. Yaani nilikuwa tu namwaza Miryam, najua aliumia sana kwa kitendo alichofanya Bi Jamila, ila angepaswa kushughulikia jambo hilo yeye kama yeye pamoja na mama mkubwa wake ili tujue ni hatua zipi zaidi zilizofaa kuchukuliwa baada ya hayo. Ankia alikuwa akiandaa msosi kwa ajili ya Bobo na sisi wote pia, ukiwa ndiyo upo kwenye hatua za mwanzo, na baada ya Bobo kuona kama nimetekwa fikira na jambo fulani, akauliza kama nilihitaji kujichangamsha kidogo ili sisi wanaume twende Masai pale. Na Tesha akakubaliana na hilo wazo.
Ankia akaanza kulalamika, akisema yaani sisi twende Masai halafu wenyewe tuwaache vipi hapo, na sababu kutoka kwa Bobo na Tesha ikawa kwamba ilikuwa muhimu wanawake wabaki ili wamalizie kupika, kisha nao wangekuja Masai pia. Ila Ankia akawa bado hajaridhia, na mimi kweli niliona siyo mbaya kwenda kujichangamsha kwa vinywaji, lakini kwa kuwajali wanawake, nikamwambia Bobo na Tesha tutoke ila tusiende Masai, twende kule Rangi Tatu sehemu kama Highway tuchukue mambo kali na nini, kisha tuyalete hapa kushiriki na wanawake. Katika kutotarajia kwa nini nilipendekeza hivyo, Tesha akauliza sababu ya sisi kulazimika kwenda mpaka huko kote, ndiyo nikatoa funguo zangu za gari na kuzitikisa hewani.
Tesha akaelewa upesi sana kwamba nilimaanisha nimekuja na gari langu, naye akanyanyuka upesi na kuja kuzikwapua funguo huku akimwambia Bobo kwa shauku anyanyuke ili tuondoke upesi. Nikatabasamu kiasi kwa kujua shauku ya kijana ilitokana na yeye kuwa na hamu ya kuendesha gari, na wengine hawakuwa wameelewa bado. Ndiyo Tesha akawafahamisha sasa kwamba JC nilikuwa na gari, Ankia asiweze kuamini kama ni kweli, nami nikamwambia kesho tu ningempa na yeye aendeshe. Bobo akanyanyuka pia, nasi tukawaaga wanawake huku Ankia akitusihi tusiwadanganye na kwenda kushinda huko mpaka usiku sana, angetununia mwezi mzima yaani. Hapakuwa na tabu. Tukaondoka ikiwa ni mida ya saa tatu.
★★
Tukaelekea mpaka Masai na kukuta gari langu likiwa hapo nje bado, na kwa usiku huu hapakuwa pamechangamka sana huko ndani, zaidi tu kulikuwa na watu wengi-wengi kwa hapo nje ambapo grocery ndogo ya vinywaji ilikuwa. Tesha akaanza kuliita gari langu "baby" baada ya kulifikia, akilikumbatia eti kwa furaha kutokana na hamu ya kutaka kuliendesha, nasi tukakaa hapo nje kumsubiri Bobo alipokuwa amekwenda huko ndani ya Bar kuangalia hiki na kile kabla hajarejea ili tutimke. Nikawa nimemtumia Miryam ujumbe kumuuliza hali ikoje kwa sasa, na jibu lake likawa linachelewa kwa hiyo nikaona nimwache tu.
Baada ya Bobo kurudi, tukaingia garini, Tesha akiligeuza hapo nakwambia kwa njonjo ili waliotuona tunaingia wajue linakanyagwa na mtaalamu, naye ndiyo akatuondoa eneo hilo upesi. Alipenda kuendesha kwa sifa, kwa hiyo nikamwambia atulize makeke maana sikutaka gari langu lipate mchubuko hata mmoja, na Bobo akasema hakutaka kufa mapema. Tukaingia lami, nikiwa nangoja tu ujumbe kutoka kwa bibie bila kupata matokeo mazuri, ndiyo kwa dakika chache alizotumia Tesha kutupeleka Rangi Tatu, tukawa tumefikia ile kumbi kubwa ya starehe ya Highway. Kulikuwa na mambo mazuri hapo ila Tesha akaonelea tusonge mbele zaidi mpaka Zakhem ili tubebe yaliyo bora zaidi, hivyo mwendo ukaendelea.
Tukiwa tunasonga taratibu ndiyo nikawa nimekumbuka jambo fulani muhimu; Stella. Muda ulikuwa unaikimbilia saa nne, na mwanamke huyo alinifanya niahidi leo kwamba ningemtafuta saa nne, ama kama angeona niko kimya tu, basi ni yeye ndiye angenitafuta. Nikatoa kizuizi kwa namba zake kwenye simu yangu, maana hakuwa amekosea, hiyo ndiyo ilikuwa sababu ya yeye kutonipata kwa muda mrefu sasa. Alikula block! Kwa hiyo nikaacha tu iwe namna hiyo na kungoja yeye ndiyo anitafute, kwa kuwa sikutaka ahisi majivuno kwa mimi kuanza kumtafuta yeye, kama vile amenitia presha sana mpaka nifanye hivyo.
Tumefika maeneo ya Zakhem, Bobo akawa amemwelekeza Tesha tuelekee sehemu fulani za ndani ndani ambazo sikuwahi kuingia kabla, alikojua kuna sehemu nzuri ambako tungeweza kununua vinywaji na nyama choma ya mbuzi. Mpango ungekuwa kuchanga pesa ili tununue nyama nyingi, kisha kuzibeba na kuzipeleka nyumbani kwa Ankia pamoja na vinywaji vya ukweli, na tulipoifikia sehemu hiyo tukafanya maagizo na kukaa kusubiri nyama itengenezwe.
Wakati tumekaa kusubiri, wenzangu walitumia hiyo nafasi kunywa bia kidogo, lakini mimi nikawa nimeahirisha kunywa baada ya Stella kuwa amenipigia hatimaye. Kwa hiyo nikawaacha walipokuwa wamekaa na kwenda mpaka ndani ya gari langu, kisha nikapokea simu ili nizungumze na huyo mwanamke kwa utulivu.
"Hallo..."
"Hello," Stella akasikika upande wa pili.
"Niambie..." nikasema hivyo.
"Za kwako?"
"Ni nzuri."
"Hata me nimeona ni nzuri. Mambo yako bomba sana kwako sasa hivi, nilijua ungesahau hadi na kunipigia..."
"Stella... naomba tuongelee jambo letu kwanza. Mengine baadaye," nikamwambia hivyo kwa upole.
"Unaposema jambo letu, unamaanisha nini?"
"We' unafikiri namaanisha nini?"
"Mhm... haya. Unapanga kumwona lini mwanao?" akaniuliza.
Nikajikuta nimebaki kimya nikitafakari kwanza.
"Bado ni ngumu kuamua?" akaniuliza.
"Hamna. Nafikiria wakati mzuri..."
"Bullshit," akasema hivyo.
"Nini?"
"Sidhani hata kama ilikuwa imeingia akilini mwako kutafuta muda wa kuonana na mtoto. Kila mara nilipojaribu kukuunganisha naye, ukawa unakimbia. Kwa hiyo sishangai hata kama ulikuwa hujui muda "mzuri" wa kuonana naye...."
"Stella, mambo yalikuwa mengi. Kwanza sikuwa huko, na...."
"Point yangu siyo hiyo. Nachosema ni kwamba sioni kama uko tayari kuonana na mwanangu... kumjua... maana kila kitu kwako ni mpaka wakati uwe "mzuri." Ungekuwa kweli una tamaa ya kumwona, ungekuja kumwona hata sasa hivi," akasema hivyo.
Nikashusha pumzi kwa kuhisi vibaya moyoni, nami nikamwambia, "Uko sahihi."
Akabaki kimya kunisikiliza.
"Nimekuwa mbinafsi, Stella. Ninatamani sana kumwona mtoto wakati huu. Naomba upange muda utakaofaa ili sote tuonane pamoja," nikamwambia hivyo kistaarabu.
"Mh? Ahah... siamini. Huyo ni wewe Jayden unayeongea sasa hivi?" akasema hivyo.
"We' umempigia nani?"
"Naahah... nashangaa tu. Naona kama umekuwa mpole sasa hivi, siyo kama muda ule wakati uko na mpenzi wako," akasema hivyo.
"Hapa tunaongelea mtoto Stella, nimekwambia hayo mengine tuyaweke pembeni."
"Kwa nini? Me naona yanahusiana na mtoto pia. Kwa sababu umejichimbia huko, hujali ikiwa mtoto yuko salama, ama anaumwa, ama nini, kwa kuwa tu umeshapotezwa na penzi la cougar," akasema hivyo.
Nikahisi hasira kiasi, nami nikamwambia, "Stella nakuomba ujiheshimu."
"Kwa kipi ambacho sijiheshimu mimi Jayden? Na kwani ni uwongo? Sasa hivi akili yako yote ipo kwa huyo mwanamke, nimekutafuta sana, ni mara nyingi mno Evelyn anaulizia baba, baba, baba, anataka kukuona baba yake, lakini anaishia kukuona kwenye picha tu. Nikimleta nyumbani, unamkimbia. Kisa? Uko sijui likizo... kwa mke wako... hutaki kurudi, yaani umeyageuza makazi ya jumla huko. Huyo mwanamke ndiyo amekukamata mpaka kivuli hataki kukiachia jamani? Eh? Evelyn anawaona watoto wengine wanacheza na baba zao, na yeye anatamani acheze na baba yake. Ni mdogo, lakini ana akili sana. Anajua umuhimu wako. Kwa nini usiwe tayari kumwonyesha kwamba na yeye ni wa muhimu kwako Jayden? Mpaka lini jamani?" akaongea kwa hisia sana.
Alisema mengi ambayo yangeweza kuniudhi, lakini sikuhisi hasira. Badala yake, nikawa nimeguswa sana na jambo moja katika maneno hayo aliyoniambia, ambalo lilifanya nihuzunike na kujihisi vizuri kwa wakati mmoja. Machozi yakanivizia.
"Jayden, unanisikia lakini?" akauliza hivyo.
"Ndiyo nakusikia," nikamwambia hivyo kiupole.
"Songei kwa ubaya, nachotaka tu ku...."
"No, no, uko sahihi kwa mengi, I'm sorry. Nili... nilikuwa natafakari tu maneno yako," nikamwambia hivyo.
"Unatafakari nini?"
Nikatulia kidogo, kisha nikamwambia, "Evelyn."
"Ahah... eeh, hilo ndiyo jina lake. Ulikuwa hata hujui jina la mwanao, uwongo?" akaniuliza.
Nikafumba macho kwa kujihisi vibaya zaidi.
"Njoo umwone Jayden. Kwangu unapajua, kinachokuzuia ni nini? Nimeshakwambia yale yaliyopita achana nayo, tulikuwa... tulikuwa kama watoto tu," akasema hivyo.
Nikabaki kimya tu na kuendelea kumsikiliza.
"Okay, sawa, najua mimi ndiyo nilikutendea siyo fresh, nimejutia, ndiyo maana ninafanya haya yote ili Evelyn akujue, na katika kila sense... akue vizuri. Kila siku lazima akuulizie, na hata tukienda kwenu na kukuta haupo, huwa anahuzunika sana. Jayden, this is the time. Achana na mambo mengine, kuwa mwanaume. Kuwa baba kwa mtoto wetu basi, mapito achana nayo kabisa mpe...."
Stella akaishia hapo baada ya kuongea kwa hisia sana na kuonekana kutaka kusema kitu fulani kizito, nami nikakaza macho kwa kuwa nilitambua kitu hicho kilikuwa nini.
Akajirekebisha kwa kusema, "I mean... tupotezee yale yaliyopita Jayden. Sasa hivi tuangalie future ya mwanetu. We' unaonaje?"
Nikatulia kidogo, nikiwa makini zaidi wakati huu, nami nikamwambia, "Sawa. Nipange tu kwa muda utaoona kuwa sawa, me nitaenda kwangu halafu utamleta mtoto. Ama, tutakutana sehemu nyingine nzuri kama kazi zikikubana."
"Nafikiria nyumbani kwangu ndiyo itakuwa vizuri. Unaonaje ukija hata kesho? Jioni?" akasema hivyo.
Nikamwambia, "Sidhani sana kama kuja kwako kabisa ni... wazo zuri."
"Kwa nini siyo wazo zuri?"
"Nataka nikikutana na Evelyn, amjue na Miryam pia," nikamwambia.
"What?!" akaonyesha kushangaa.
"Vipi?"
"Yaani Jayden, tuko hapa tunaongelea mtoto kukutana na wewe finally, afu' wewe unawaza tu kumwonyesha mwanamke wako...."
"Siyo hivyo, sikia, siyo unavyofikiria...."
"... kwamba nini, ajue kwamba ana mama wa kambo ama? Itamsaidia nini?"
"Stella sikia. Usiende mbali sana. Miryam ni sehemu muhimu sana kwenye maisha yangu sasa hivi. Na Evelyn ni mdogo. Nataka wajuane pia, na siyo wao tu, hata wewe nataka ujuane vizuri na Miryam..."
"Ili iweje?"
"Nataka amani Stella. Kama ulivyosema, ya nyuma tuyaache, tuangalie future. Na mimi sasa hivi...."
"Utasema Miryam ndiyo future yako, kwa hiyo unataka na yeye awe sehemu ya maisha ya mwanangu. Jayden, give me a break! I care a damn about your woman, and neither does my daughter. Nataka mwanangu akujue wewe, na wewe tu. Mwanamke wako ana faida gani kwa mwanangu?"
"Stella usiongee hivyo..."
"We' ndo' unaharibu! Siyo kila kitu mpaka Miryam akupe approval, umekuwa puppet wake sasa? Nini, kwamba ukija kwangu ndiyo atanuna sana mpaka ushindwe kula, au?"
Nikafumba macho na kukaza meno kwa kuhisi kukerwa kiasi.
"This is about your daughter, and you. Jayden for once, mtangulize mwanao pia. Nimeshajitahidi, ila na me nachoka. Ukiona huwezi, basi tupotezee," akaongea hivyo kwa mkazo.
Nikabaki kimya tu huku nikitikisa kichwa kwa kusikitika. Hakuwa amenielewa.
"Unajua nini... utanitafuta ukiwa tayari, maana nimeshajipendekeza vya kutosha. Enjoy maisha yako na huyo Miryam wako, msahau mtoto..."
"Ah, tatizo lako ndiyo hilo. Unatanguliza maoni yako tu sikuzote, hutaki kusikiliza. Don't jump to conclusions, Stella please!" nikaongea kwa mkazo.
Akabaki kimya.
Kutokea hapo mbele kwa nje nikawa namwona Tesha akiwa anakuja upande wa gari langu, bila shaka akiwa ananifata huku.
Nikashusha pumzi na kusema, "Aisee! Nitakutafuta kesho asubuhi Stella. Tutaongea vizuri zaidi."
"Usiku mwema," akaniambia hivyo tu na kukata simu.
Huyo mwanamke huyo!
Tesha akawa ameufikia mlango wa usukani na kuufungua, akinitazama hapa nilipokuwa nimekaa siti ya pembeni, naye akasema, "Vipi wewe?"
"Vipi nini?" nikamuuliza.
"Mbona uko humu?"
"Si nimewaambia nimekuja kuongea na simu?"
"Eeeh, naona unaongea na simu..." akasema hivyo kikejeli.
"Ah, ndiyo nimemaliza sasa hivi," nikamwambia.
"Twende sa', mzigo unakaribia kukamilika hata hujanywa bia..."
"Me sinywi huku. Nitaenda tu kunywa Dompo home."
"Tunabeba na maK-Vant halafu, tukapombeke haswa!"
Nikatabasamu kiasi na kutazama tu mbele.
"Kwa hiyo unabaki hapa? Tutakukuta?" akauliza.
"Yeah. Mtanikuta," nikamwambia hivyo.
"Haya. Najua umekuja kupiga pichu humu wewe, unajishaua eti kuongea na simu," akanitania hivyo.
Nikacheka kidogo na kumnyooshea kidole cha kati, naye akanionyeshea chake pia na kuondoka hatimaye.
Nilijitahidi kukaza noma zangu zote wakati naongea na Stella, lakini mambo bado yakawa siyo mazuri. Oh, mimi kumsema Miryam inaonekana ni kitu ambacho kilimkera sana, ikimaanisha labda alihisi wivu, na kama siyo hivyo basi huenda ilikuwa tu ni chuki binafsi isiyo na maana yoyote. Lakini kwa mengi, alikuwa sahihi. Kumwona mtoto lilikuwa jambo lililozidi kukua na kukua katika hamu ndani yangu, yaani kiukweli nilitamani sana kumwona hata muda huo huo. Niliwaza mno kuhusu hali njema ya kimahusiano baina yangu, Miryam, na Stella katika jambo hili, lakini sasa nilitaka tu kujali kwanza mtoto. Mengine yangejipanga tu.
Basi, nikatulia hapo ndani ya gari kwa dakika chache, na kwa huo muda hatimaye Miryam akaanza kuchat pamoja nami. Akaniambia alijaribu kuzungumza na Bi Jamila, lakini mwanamke huyo aligoma kabisa kuongea naye, hata akazila kula. Hakujua kwa nini alishikilia mno msimamo wake wa kukataa uhusiano wetu, ila hilo jambo lilimtatiza sana Miryam wangu. Nikamtia moyo kuwa asipoteze tumaini, na kwa sasa amwache tu mama yake mkubwa; labda tungetafuta nafasi nzuri tena ya kuongea naye, pamoja, na nikamwambia tungepaswa kuifanya hiyo nafasi iwe ya sisi wawili tu pamoja naye. Basi. Huenda angefunguka zaidi kwetu.
Miryam akaonekana kuridhia katika hilo na kunishukuru kwa kuwa mwelewa, naye ndiyo akauliza kama nilikuwa najiandaa kulala. Ndiyo nikamjulisha kwamba sisi tulikuwa huku Zakhem kabisa kubeba mambo mazuri ili kuyapeleka huko nyumbani, na nilihakikisha tunafanya mpango wa kuyashiriki pamoja naye bibie na watu wake wa familia, hivyo asubirie kwa hamu kutafuna nyama choma. Akapendezwa na jambo hilo, akijua ingempa furaha Mariam pia, na ndiyo tukaendelea kuchat tu, nikimtania kwa mambo ya hivi ama vile mpaka hatimaye Bobo na Tesha wakawa wamerejea garini.
Eh bwana eh, nyama zilikuwa nyingi, zigawanyishwa kwa mifuko mitano kabisa, kisha ndiyo tukaondoka hapo kuelekea makwetu kuyapa matumbo na hisia zetu burudani iliyostahili. Nilihitaji sana hii kitu.
★★★
Jumamosi ikawa imekucha baada ya usiku wenye kuburudisha pamoja na marafiki zangu. Baada ya kuwa tumeondoka huko Rangi Tatu na Tesha na Bobo, tulienda kuliacha gari langu pale wanapolaza magari si mbali sana na Masai, kisha ndiyo tukaelekea kwa Ankia. Yaani tulikuja na nyama hapo, chupa za wine ya Dompo, K-Vant, na soda, na Ankia akiwa amemaliza kupika wali pamoja na maharage ikawa ni nyongeza nzuri ya siye kula na kunywa kwa furaha sana. Tesha alikuwa amepeleka mboga kwao pia na kurudi kujiunga nasi, kwa hiyo tulikaa mpaka mida ya saa sita tukiburudika kwa mlo, vinywaji, na story zenye kufurahisha. Hata sikuzihisi tena stress zilizokuwa zikinivizia usiku huo.
Ndiyo nikawa nimeamka mida ya saa tatu asubuhi hii, na nilihisi kichwa kikigonga kwa mbali shauri ya kunywa wine nyingi huo usiku uliotangulia. Bobo alikuwa amelala hapa kwa Ankia hiyo jana baada ya kwenda Masai kuhakikisha hali iko sawa huko, kwa hiyo wakati huu nilipotoka kwenda kujisafisha nikamkuta akiwa sebuleni na Ankia wake, wakikaa sofani kuzungumza kidogo kabla jamaa hajaondoka kuelekea wapi sijui. Mapenzi yao yalikuwa moto sasa hivi. Kwa hiyo mimi nikaingia tu kuoga na kuanza kuvaa vizuri kwa ajili ya kutoka, na Ankia alikuwa na mpango wa kwenda kutafuta supu tuje tunywe pamoja lakini mimi na Bobo sote tulihitaji kuondoka upesi, kwa hiyo haingewezekana.
Kwa kuwa nilitaka kwenda kwake Miryam ili kulichukua gari lake la pickup na sasa nikawa nimetambua kwamba Bobo alitaka kwenda huko Kariakoo kufatilia ishu fulani, nikampatia funguo za gari langu ili alitumie kwenye hiyo mishe yake na baadaye akipenda ampeleke Ankia misele, kwa kuwa mwanamke huyo bado alitaka kuliona gari langu. Hivyo ikabidi tutoke pamoja wakati nilipokuwa naenda hapo kwa Miryam. Tayari nilikuwa nimeshawasiliana na bibie, nikiuliza kama alikuwepo kwake, naye akakubali. Kwa hiyo nikaenda pamoja na Bobo hapo, na ikiwa imeshaingia saa nne, nikakuta wenyeji wakiwa sebuleni wakipata kiamsha kinywa.
Miryam alikuwa amevalia kwa njia iliyoonyesha utayari wa kuondoka kwenda kazini, na wengine walinisalimu vizuri tu isipokuwa Bi Jamila, ambaye hata nilipomsalimia aliitikia salamu yangu kibaridi bila kunitazama. Huu haungekuwa muda unaofaa kuangazia suala hilo zaidi, kwa hiyo tukawa tu tumewaaga wote kwa pamoja. Tukatoka hapo dakika siyo nyingi, mimi, Bobo, na Miryam tukiondoka kwa gari lake ili nimpeleke kazini kwake kwanza, na Bobo alishukia Masai ili kuelekea kule nilikoegesha gari langu, kisha safari yangu na bibie ikaendelea.
Miryam alikuwa na hamu ya kuona gari ambalo ningerudisha, na leo hangekaa sana huko dukani kwake, hivyo wakati ambao ningerejea huku tayari ningemkuta nyumbani. Nikamwambia angelipenda sana, angojee tu kwa subira kulipokea kama zawadi nzuri sana. Nilikuwa pia na mpango wa kuelekea huko hospitalini kumwona Jasmine tena baada ya kufanikisha taratibu za kuliuza gari hili na kuchukua jipya, naye Miryam akaniambia nimpe dada yangu salamu zake na yeye angewasiliana na mama yangu baadaye kuwajulia hali. Kwa hiyo nikawa nimemfikisha Kijichi ikiwa imeshaingia saa tano, nasi tukaagana vizuri kwa busu na yeye kuelekea dukani, halafu nikaendelea na safari yangu upesi.
★★
Sikukawia nilipokuwa nimedhamiria kufika, na leo sikufika kabisa huko Morocco. Niliona kwamba muda mwingi ungepotea na kunifanya kukawia kurudi huku endapo kama ningekwenda mpaka huko na hospitalini tena, kwa hiyo nikawasiliana na hao watu niliofanya nao dili ili tukutane maeneo ya Keko ambako walikuwa na tawi lao pia. Nilipata dili zuri kutoka kwa hawa watu baada ya kuunganishwa na "rafiki" aliyejuana na mzee wangu, akifanya iwe rahisi kuliuza hili gari la Miryam kwa pesa nzuri ambayo ningejumuisha na ya kwangu ili kulichukua gari jipya. Sikuhitaji kuzunguka sana yaani.
Kwa hiyo nikafanikiwa kufika huko haraka, kisha nikakaa kuwasubiri na wenyewe wafike kwa kuwa mimi niliwatangulia. Baada ya dakika kadhaa wakawa wamefika, wakiwa wanaume watatu pamoja na huyo jamaa aliyeniunganisha kwao, tukafanya makubaliano na mapatano mazuri walipohakikisha gari la Miryam limekidhi viwango vyao, kisha nikapatiwa pesa. Kwa kuwa tulikuwa hapo hapo kwenye tawi la kampuni ya uuzaji magari hawa jamaa wayofanyia kazi, nikapitia magari na bei zake, nami nikapendezwa na moja ambalo nilijua lingefaa sana kuendeshwa na Miryam. Alitaka gari lisilo la gharama kubwa sana, na hilo nililolipenda lilikuwa la gharama nafuu kabisa, hivyo nikaamua kulibeba.
Hiyo kampuni bwana ilikwenda kwa jina la Africars, wakiwa wauzaji wa magari mengi bomba sana, lakini nikachagua kuchukua gari unaloweza kuita la "wastani" kwa ajili ya bibie wangu, lakini lilikuwa zuri. Mwanzoni nilitaka kuunganisha pesa ya mauzo ya pickup yake na pesa yangu ili nimchukulie bibie gari la gharama zaidi, lakini kwa kuwa alitaka la bei nafuu, pesa ikawa imebaki. Kwa hiyo tukafunga madili hapo na nini, nami nikamshukuru sana jamaa aliyenisaidia mpaka hizo taratibu kukamilika, kisha nikaingia kwenye ndinga mpya na kuanza kuitembeza barabani. Lilikuwa gari poa sana, Mark X nyeupe modeli mpya iliyoboreshwa zaidi, nami nikasonga kuelekea huko Rebinansia ili nikamwone Jasmine kwanza.
Nilikuwa naseleleka tu, gari lilikuwa jepesi yaani, mpaka nafika hospitali ni saa nane tu ndiyo ilikuwa inaingia. Nikaenda huko juu kumwona dada yangu, na leo alikuwa ametembelewa tena na mama mkwe wake, yaani mama yake Kevin, na Kevin pia alikuwepo pamoja na mama yetu sisi, Nuru, ma rafiki mmoja wa Jasmine. Dada yangu aliendelea vizuri, akiwa ameanza kufanyishwa mazoezi kidogo-kidogo. Mapacha wake walikuwepo pia, vimacho vikiwa bado vimefumba, nami nikatumia muda mwingi pamoja nao wote mpaka ilipofika saa kumi. Mama yangu alitaka kujua ikiwa niliongea na Stella ile jana, nami nikakubali, nikisema tulikuwa tumeshaanza kupanga vitu fulani, na yeye akaonekana kuridhishwa sana na jambo hilo.
Kwa hiyo baada ya kutumia muda huo na familia, ndiyo nikawaaga wote, nikisema kuna mzigo nilihitaji kupeleka huko Mbagala upesi. Hakukuwa na noma, na nilitaka kuondoka kutoka hospitalini hapo bila kuonana na Stella, na nikawa nimefanikiwa. Sikutaka kujikawiza hapo kwa maana tayari Miryam alikuwa ameniambia amekwisharudi kwake mida hiyo ya saa kumi, hivyo nikaharakisha pia kuondoka. Nilikuwa na hamu kweli ya kumpelekea hilo gari zaidi hata ya jinsi yeye alivyotamani kuliona.
★★
Nimekuja kufika Mzinga ikiwa imekwishaingia mida ya saa kumi na mbili jioni, taratibu tu nikilipeleka gari la Miryam kitaani Masai mpaka nilipolifikisha nje ya geti la nyumba yake, nami nikapiga honi. Geti lilipofunguliwa, ni Tesha ndiye aliyekuwa ametoka huko ndani kufungua, naye akalifungua lote kabisa kuniruhusu kuingiza gari mpaka hapo ndani. Varandani kwao walisimama Shadya, Mariam, na bibie Miryam pia, ambaye alionekana kama vile ndiyo alikuwa tu ametokea ndani pale sebuleni muda huo huo nilioingia. Nikaliegesha gari hapo, huku nikiona namna ambavyo Mariam na Shadya walitasadamu, naye Mariam akaelekea ndani kwa namna iliyoonyesha shauku.
Nikashuka, Tesha akiwa ameshafunga geti na kulisogelea gari huku akilitazama kwa njia ya kukubali, nami nikawa namwangalia Miryam hapo varandani kwa jinsi ambavyo alitazama gari lake jipya kwa upendezi. Shadya akaja karibu nalo pia, akionekana kuvutiwa, na Mariam akawa ametoka pale ndani huku akifuatwa na mama zake wakubwa. Bi Zawadi sanasana ndiye aliyeonyesha kufurahi sana, akifikiri nimemnunulia bibie gari kama zawadi kutoka kwangu moja kwa moja, lakini nikawajulisha wote kuwa Miryam pia aliweka jitihada katika kubadilisha gari lake, na sasa angekuwa anateleza barabani kiaina.
Tesha alikubali mwonekano wa gari hili jipya, akielewa kwamba lilimfaa sana mwanamke, na Mariam alionekana kufurahi pia mpaka yeye na Shadya wakaanza kuingia na kukaa humo ndani ili kujistarehesha na huo upya. Lakini, ni Bi Jamila pekee ndiye ambaye alionekana kutovutiwa sana na gari hilo, yaani Bi Zawadi alimsemesha na kumwomba aseme maoni yake juu ya uzuri wa gari jipya la bibie, lakini akasema tu 'ni zuri,' kwa njia isiyo ya furaha wala ninj, naye akarudi zake ndani upesi. Ilituacha mimi, Miryam, Tesha, na Bi Zawadi tukihisi kukosa amani kiasi, na ndipo Mariam na Shadya wakashuka kutoka garini huku binti akiniambia kwamba angependa sana kuendeshwa ndani ya gari hilo jipya.
Kutokana na hiyo kauli ya Mariam, nikawa nimepata wazo. Nikamwambia Tesha alitoe tena gari ili awaendeshe Mariam, Shadya, na Bi Zawadi kuizungukia Mzinga, na labda hata wakipenda wafike hadi Kongowe, naye Mariam akafurahi na kuanza kuniunga mkono. Miryam alitaka kupingana na jambo hilo, lakini nikamtolea ishara kwa kutikisa kichwa kumwonyesha kwamba nilikuwa na maana fulani. Nadhani Tesha na Bi Zawadi wakawa wamenielewa pia, hivyo wakaniunga mkono na kusema wangependa kufanya hivyo; ili nafasi ya pekee ibaki kwa mimi na Miryam kuzungumza na Bi Jamila wakati huo ambao Tesha angewazungusha wengine kidogo. Miryam akawa ameelewa hilo pia.
Ikawa wazo lililoafikiwa na wote, japo Shadya alionekana kama vile hataki kuondoka, lakini wakamshawishi aende pamoja nao, ili wapite na sokoni huko kiaina kuchukua vitu vya kutumia kwa ajili ya mapishi ya usiku. Mariam akaelekea ndani baada ya mimi kumsogelea Miryam hapo varandani, nikitazamana naye kwa njia yenye uhakikisho wa kwamba niko tayari kwenda naye ndani ili tuzungumze vizuri na mama mkubwa wake, na ndiyo Mariam akawa amerejea na akiwa amevaa ndala zake nzuri wakati Tesha alipokuwa amemaliza kufungua geti kwa mara nyingine tena. Miryam akampatia Shadya pesa, kisha watatu hao wakaondoka hapo na mimi kwenda kufunga geti.
Ikawa ni wakati wa vita yetu na Bi Jamila kwenda kupiganwa, na nilikuwa na utayari wote wa kuhakikisha leo inamalizwa. Yaani kingeeleweka. Miryam alikuwa ndani ya dera lake zuri la kijani na kikofia kilichofunika nywele zake, nami nikamsihi kwa kusema yaani tungepaswa kufanya kila jitihada kuhakikisha tunajua tatizo la Bi Jamila lilikuwa nini, na tungemwonyesha kwamba hakuwa na sababu yoyote ya kuhofia lolote. Miryam alikuwa na utayari huo pia, lakini akaniomba nijitahidi kutumia busara zaidi na utulivu kwenye maongezi, na kwa hilp nikamwahidi kutokwangusha.
Tukaingia ndani. Tayari hali ya ugiza ilikuwa imeanza kuvizia huko nje, hivyo taa zilikuwa zimeshawashwa hapa sebuleni. Tulimkuta Bi Jamila akiwa ameketi sofani huku akisoma kitabu fulani cha kidini, nasi tulipoingia akawa ametuangalia kwa utulivu.
Nikiwa naufunga mlango, Miryam akamwambia, "Mama... naomba tuongee tafadhali."
Nikamsogelea Miryam, tukiwa na nia ya kukaa sofani, lakini Bi Jamila akaanza kunyanyuka kutoka alipokaa na kuashiria kutaka kuondoka, hivyo nasi tukabaki tumesimama pia.
"Mama..." Miryam akamwita.
"Mtanisamehe, nahisi... ki-kichwa kimeanza kuuma," Bi Jamila akasema hivyo bila kututazama.
Nikaangaliana na Miryam machoni, tukielewa vizuri kwamba mama mkubwa wake alitaka kutuepuka, na Bi Jamila alipokaribia kumpita bibie, Miryam akamshika mikononi kistaarabu ili kumzuia.
"Mama jamani, hebu acha kufanya hivi. Unanipa wakati mgumu sana kukuelewa. Shida ni nini?" Miryam akamsemesha kwa njia yenye hisia.
Bi Jamila akawa ametazama tu chini kwa kukosa amani.
Miryam akasema, "Ona, niko na Jayden tu hapa, sisi wawili tu. Nakuomba tuongee. Tueleweshe kwa nini uko against... kwa nini unapinga sana mahusiano yetu. Labda ni sababu nzuri, labda tunaweza tukaelewa vyema kabisa na kusaidiana kuona kama kuna njia ya kurekebisha mambo. Au uwongo Jayden?"
"Ni kweli kabisa," nikamuunga mkono.
"Tuambie tu tatizo ni nini mama. Sisi ni watoto wako, chochote unachosrma tutaelewa," Miryam akamwambia hivyo kwa upole.
"Mimi... mimi siwezi kuwa...." Bi Jamila akaishia hapo na kuangalia pembeni tu.
"Usione shida yoyote mama. Niambie tu. Nakuomba," Miryam akamsisitizia kwa upole.
Bi Jamila akabaki kimya na kuangalia chini. Miryam akaonekana kuvunjika moyo, naye akanitazama kwa njia iliyoonyesha hilo. Ikabidi nisogee karibu zaidi na wanawake hawa, nikimtazama Bi Jamila kwa hisia.
"Mama... nakuomba tafadhali niangalie..." nikamwambia hivyo kwa upole.
Bi Jamila akanitazama kwa macho yenye huzuni kiasi.
"Najua jambo langu na Miryam lilikushangaza sana ulipogundua kuhusu uhusiano wetu, na ninataka ugundue kitu kingine muhimu. Sikuja kuyaharibu maisha ya binti yako, nilikuja huku kwa ajili ya likizo ndiyo nikakutana naye, na yeye ndiyo akanifanya nitambue kwamba ninaweza kuyajenga maisha yangu vizuri zaidi kwa kuungana pamoja naye. Ninakwambia hili ili uelewe namna ninavyompenda Miryam... niko tayari kufanya lolote kwa ajili yake, hata kama itakuwa kwenda kinyume na ulimwengu mzima kwa ajili yake, nitafanya hivyo," nikaongea kwa sauti tulivu.
Bi Jamila akaangaliana na Miryam kwa njia zilizoonyesha hisia nzito sana.
"Nimeshaongea hili, na nitalirudia tena mama yangu. Ninampenda sana Miryam. Na yeye ananipenda. Licha ya hali zozote zilizopo, la muhimu ni kwamba tumependana. Lakini anakupenda na wewe pia. Wewe ni mzazi kwake, na ili asonge mbele kwenye jitihada yoyote ile anayoitia kuyasogeza maisha yake, anahitaji baraka zako. Nakuomba tafadhali usimnyime hilo... ataumia sana..." nikaongea kwa hisia.
Bi Jamila akafumba macho na kuanza kudondosha machozi, naye Miryam akaanza kutokwa na machozi pia huku akimshika mama mkubwa wake usoni na kuanza kumfuta taratibu.
"Haupaswi kuogopa lolote mama. Sioni sababu yoyote ya kuogopa chochote. Niko hapa kwa ajili yake, na nyie wote pia. Tutakuwa pamoja siku zote," nikamwambia hivyo.
Bi Jamila akamtazama Miryam kwa hisia, naye akainamisha uso wake tena na kuanza kujifuta machozi mwenyewe.
"Mama..." Miryam akamwita hivyo.
"Mimi... ninakupenda sana. Ila ninaogopa bado. Naogopa utaumia mno mwanangu..." Bi Jamila akasema hivyo kwa huzuni.
Nikamwangalia Miryam usoni kimaswali kiasi, yeye pia akiniangalia kwa mfadhaiko, kwa sababu yaani sikuelewa shida ya Bi Jamila ilikuwa nini. Alikuwa anaogopa nini? Yaani ilikuwa ni kama vile anajua kitu fulani halafu hakutaka kutuambia, lakini sikujua namna ya kumuuliza.
Miryam akamshika mikononi, naye akamwambia, "Mama, ondoa shaka. Jayden ananipenda kweli. Tunapendana. Sikuwa nimefungua moyo wangu kwa mtu yeyote yule, lakini kwake yeye ndiyo umefunguka. Ninampenda. Yeye ndiyo furaha yangu. Lakini nitakuwa na furaha zaidi kama na wewe utafurahi kwa ajili yangu. Hamna sababu yoyote ya kuogopa mama."
Bi Jamila akawa analia kwa kwikwi, yaani kwa njia fulani ya majuto mengi utadhani alikuwa amekosea kitu fulani. Ila nikahisi labda ilikuwa ni ile huzuni kutokana na kujaribu sana kuukataa uhusiano wangu na Miryam.
Nikamshika Bi Jamila begani, na aliponiangalia nikamwambia, "Tafadhali niambie tu nifanye lolote lile unalotaka ili nikuonyeshe namna ambavyo nampenda binti yako. Niko tayari kwa ajili ya chochote kukuhakikishia kwamba hauna sababu ya kuogopa..."
Bi Jamila akaangalia pembeni tu.
Miryam akasema, "Jayden...."
"Hapana Miryam. Kila somo ni lazima liwe na mtihani wake, na me niko tayari kufanya mtihani wowote ambao mama atanipatia kumwonyesha kwamba somo la upendo wangu kwako nalielewa vizuri. Baraka zako ni za muhimu sana kwetu mama. Nitafanya lolote kuzipata. Ninakuomba... fikiria tu Miryam atahisije usipokuwa sehemu kuu ya furaha yake, itageuka kuwa sikitiko la maisha yake yote. Ungependa iwe hivyo?" nikaongea kwa ushawishi.
Miryam akamtazama mama yake, naye Bi Jamila akaniangalia.
"Kwa macho yangu mafupi ya kibinadamu, siwezi kuona hatari zote za mbele wala kujua tutakabili matatizo yapi, lakini niko tayari kupambana na yote kwa ajili ya Miryam. Nipe mtihani wowote ule mama... nitakuthibitishia," nikamwambia hivyo tena.
Nilikuwa natumia nguvu nyingi ya kiakili ili niweze kulitambua suala alilokuwa akiogopa sana, naye Bi Jamila akaonekana kutafakari maneno yangu kwa kina, kisha akaniangalia.
"Sawa. Nimekubali," Bi Jamila akasema hivyo.
Miryam akanitazama usoni, nami nikamwangalia pia. Hatukuelewa.
"Nimekubali,.. ninatambua kwamba mnapendana sana, sina njia ya kupinga hilo," Bi Jamila akaongea kwa hisia.
Tukaendelea tu kumwangalia kwa umakini.
Bi Jamila akasema, "Nimeukubali uhusiano wenu tangu nilipogundua kwamba mnapendana, lakini nilikuwa tu naogopa..."
Miryam akatabasamu kiasi na kumshika mikononi tena, naye akasema, "Uogope nini mama? Wakati umenifundisha kwamba woga ni udhaifu mbaya sana?"
Bi Jamila akaangalia chini.
"Mama... unachohofia ni nini?" nikamuuliza kistaarabu.
Akaniangalia na kusema, "Ninaogopa kwamba Miryam hatapata nafasi ya kutoshea kwenye familia yako."
Tukaangaliana pamoja na Miryam kwa kushindwa kuelewa vizuri, lakini Miryam akamuuliza, "Kutosha? Unaogopa kwamba familia yake itanikataa?"
"Hapana, siyo hivyo... yaani... sijui nisemeje tu..." Bi Jamila akaonekana kubabaishwa na jambo fulani.
Nikawa namtazama kwa umakini sana.
Miryam akamwambia, "Mama... usiwaze mbali sana. Sisi ni watu wazima, na... ukifika wakati wa Jayden kunitambulisha kihalali kwa familia yake, tutakuwa tumeshaona mambo mengi yako vipi na kuchagua jinsi ya kuyashughulikia. Lisiwe suala la kukutatiza kama hivi mama... muda bado..."
Bi Jamila akainamisha uso wake.
Nikamuuliza, "Ndiyo unachohitaji?"
Wanawake kwa pamoja wakaniangalia.
"Unataka nimtambulishe Mimi kama mchumba wangu kwa familia yangu mapema, si ndiyo?" nikamuuliza Bi Jamila.
"Nilikuwa sijataka u..." Bi Jamila akaishia hapo.
"Jayden..." Miryam akaita hivyo kwa sauti ya chini.
"Oh, sasa nimeelewa. Ahah... nimekuelewa mama. Ulikuwa tu unahofia kwamba... labda mama yangu, au baba yangu wangetuwekea kizuizi mimi na Miryam, kwa sababu ya umri na nini, eh? Okay, najua maneno hayatoshi kukuaminisha hili, ila ninakuhakikishia kwamba hilo halina shida. Na nimeelewa unachotaka nifanye mama..." nikamwambia hivyo kwa hisia za furaha.
Wote wakawa wananitazama kwa ufikirio sana, naye Bi Jamila akauliza, "Umeelewa nini?"
Nikamwangalia Miryam na kusema, "Nitafunga ndoa na Miryam haraka sana!"
Miryam akabaki akinitazama kwa utulivu tu, lakini najua alikuwa akiyasikilizia vizuri sana maneno hayo.
Bi Jamila akaanza kutuangalia kwa njia yenye wasiwasi kiasi, naye akasema, "Hapana, sija... sijamaanisha mpeleke mambo haraka sana. JC..."
"Naam..."
"Ninachotaka... ni kwamba... umtambulishe Miryam kwenu, a-amjue mama yako, ndugu zako... baba yako, namaanisha... baba yako mzazi, maju... wamkuba... yaani, nataka... umtambulishe Miryam kwa wakwenu.... na mimi nikiwepo," Bi Jamila akasema hivyo kwa kubabaika.
Miryam akawa anamwangalia mama mkubwa wake kimaswali, lakini mimi hapa nikawa natabasamu kwa furaha sana. Bi Jamila alikuwa ametia tiki kubwa kwenye uhalalisho wa mahusiano yangu na Miryam hatimaye, na alitaka tuyapeleke ngazi ya juu zaidi upesi sana. Kumbe alichokuwa anataka ni kuwepo tu kwenye kutambulishana? Ah, mbona juzi!
Miryam akamwambia, "Mama, unataka..."
"Ondoa shhhaka, mrembo wangu! Yaani pigia mstari mpaka uchane karatasi la makubaliano! Imeenda hiyo..." nikamwambia hivyo Bi Jamila kwa furaha.
Yeye akamtazama tu Miryam kwa njia ya kawaida.
"Jayden..." Miryam akaita.
Nikamshika Miryam begani na kusema, "Jiandae kesho, Mimi. Tunaenda nyumbani kumwona mama!"
Miryam akaonekana kutatizika kiasi kwa jambo hilo, lakini hiyo ilikuwa ni kawaida yake kuwa na mashaka-mashaka, kwa hiyo sikuona maana yoyote kukazia fikira shuku zake.
"Mrembo wangu... asante sana! Nilidhani ungenipa mtihani wa kutembea juu ya maji sijui, lakini we' umenipa zawadi badala yake! Nitafurahi sana ukija kumwona mama, yaani... kesho tu... tunaenda. No problem kabisa," nikamwambia hivyo kwa furaha.
"Lakini Jayden, mama..." Miryam akataka kusema kitu fulani.
"Hapana cha lakini Miryam, uchaguzi wa mama ndiyo huo. Mtihani bomba sana," nikasema hivyo.
Bi Jamila akaendelea tu kuonekana kama bado hana amani.
Nikaushika mkono wake na kuunganisha kiganja chake, changu, na cha Miryam, nami nikasema, "Nashukuru sana mama. Nimemaanisha yote niliyokwambia nitafanya kwa ajili yake Miryam, hata kama ungetaka nimuoe hapa hapa, sasa hivi, nisingesita. Na wewe ndiyo ungeifungisha hiyo ndoa..."
Bi Jamila akatabasamu kiasi na kuangalia chini kwa huzuni.
Nikaangaliana na Miryam, nami nikasema, "Nimeapa kuyatoa maisha yangu yote yaliyobaki nikiwa na wewe Miryam. Sitavunja hicho kiapo. Nakupenda sana, na nitaendelea kulionyesha hilo kwa wote, iwe ni sasa, kesho, na hata milele."
Miryam akatabasamu kiasi huku akiniangalia kwa hisia, na ndiyo hapa Bi Jamila akatoa kiganja chake kutoka mikononi mwetu. Tukamwangalia usoni.
"Nahitaji kunywa dawa... kichwa bado kina.... naenda chumbani," akasema hivyo.
Hakukuwa na wonyesho wowote wa furaha kutoka kwa mwanamke huyo, yaani kama vile alifanya haya yote kwa basi tu, lakini kiukweli mimi sikujali. Ikiwa alikuwa tayari kuja pamoja nami "kumtambulisha" Miryam kwa wazazi, hiyo ilitosha sana kupeleka uhusiano wetu daraja la juu. Sikuwa na hofu hata kidogo juu ya familia yangu, kwa hiyo iliridhisha kuona Bi Jamila akiwa ameacha kukaza chuma chake.
Miryam akaendelea kuangalia upande wa kuelekea vyumbani ambako Bi Jamila alienda, nami nikamwambia, "Finally."
Akanitazama usoni, kisha akasema, "Jayden... do you really think this is right?"
"Kwa nini isiwe sahihi?" nikamuuliza.
"Anachoomba mama ni jambo ambalo...."
"Ndiyo, najua utasema ni jambo ambalo linahitaji muda. Lakini kwa nini isiwe sasa hivi Miryam? Mbona we' walikuwa wanawaleta wakina Festo hapa na wazazi wao, siku za kwanza tu? Au umesahau?"
"Na ndiyo kitu ambacho sikupenda, hivyo... kuharakisha-harakisha mambo. So... ghafla tu, unampigia mama yako simu, baba yako, eti kesho unanipeleka na mzazi wangu. Ina-make sense kweli? Hivi vitu vinahitajika kuandaliwa...."
Nikamshika mabegani na kusema, "Mimi... relax. Kila kitu kitakuwa sawa. Hamna pressure yoyote upande wa familia yangu, mama tayari anakujua, na anakupenda. Mzee, Jasmine, Nuru, wote wanakujua kuwa mpenzi wangu, na wanawajua hadi Tesha na Mamu. In fact, kesho yaani itakuwa kama vile tunampeleka tu mama yako kumtembeza kwa familia yangu... sema ndiyo tutamhakikishia tu kwamba ishu yetu ni halali vibaya mno! Kwa hiyo sioni la kuwaza."
Miryam akaendelea kuniangalia usoni kimashaka.
"Najua umefurahi moyoni pia kwamba mama yako ametuelewa sasa, haka kamtihani alikotoa yaani... tumesha-pass. Huwezi kuniambia hujafurahi!" nikamsemesha kwa furaha.
"Ndiyo, lakini... bado nahisi kama...."
"Tena unajua nini? Nadhani itakuwa bomba zaidi na cheupe wangu akija pia, au siyo?" nikamwambia hivyo.
"Jayden!" Miryam akashangaa.
"Ahahah... alitamani kupaona nyumbani tokea Tesha alipomsimulia kwa kutia chumvi jinsi panavyofanana, so najua atafurahi sana kuja..." nikamwambia hivyo.
Miryam akaangalia pembeni kimawazo.
Nikamshika usoni na kumtazamisha kwangu, kisha nikamwambia, "Usiwe na shaka mpenzi wangu. Huu ndiyo wakati wako. Kuna mtu mwingine ambaye ametamani sana kuja kuona unaolewa kama siyo Bi Jamila? Anataka kuliona hilo, ndiyo maana anatupitisha kwenye hii njia. Kwa nini uwe na wasiwasi wakati njia yenyewe imeshanyooshwa kwa ajili yetu? Please Miryam... enjoy your moment."
Akawa ananiangalia machoni kwa hisia sana, naye akavishika viganja vyangu usoni kwake na kusema, "Kweli Jayden... unataka kunioa sasa hivi?"
Nikamsogelea karibu zaidi na kusema, "Sasa hivi. Hata kama Bi Jamila angenipa mtihani wa kutembea juu ya maji, ningeweza tu, ijapokuwa sijui jinsi gani. Nitafanya lolote lile kwa ajili yako Miryam, na haitatosha nikisema hivyo kwa maneno tu, bali kufanya matendo. Ninataka uwe mke wangu. Nataka tufunge ndoa, Miryam..."
Akatabasamu kwa hisia sana na kufumba macho yake, nami nikaanza kumfata mdomoni ili nimbusu, ila si ndiyo jicho la pembeni likanionyesha kwamba Bi Jamila alikuwa anakuja kutokea chumbani? We!
Nikamwachia Miryam fasta na kujitupia kwenye sofa, nikikaa kwa kujifanya kama vile nilikuwa hapo muda wote. Miryam alinishangaa kiasi, lakini alipomwona Bi Jamila, nadhani akawa amenielewa. Akaendelea tu kusimama hapo hapo huku akimtazama mama yake, mimi nikizuga kutulia pia, naye Bi Jamila akatuangaliaaa... kisha akaenda zake tu jikoni. Tukatazamana na Miryam kwa ufupi, kisha kwa pamoja tukaanza kucheka bila kutoa sauti. Nikasimama na kumwambia Miryam kuwa naenda kuoga kuondoa fukuto nililohisi, na ningemtumia ujumbe baadaye, naye akakubaliana na hilo.
Nikatoka hapo na kusogea mpaka kufikia jikoni na kumkuta Bi Jamila anaweka maji kwenye chombo, nami nikamuaga pia kistaarabu. Hakuniangalia kabisa aliponiitikia kukubali heri yangu, nami nikaona nimwache tu na kurudi kwa bibie Miryam. Nikamshika mkono na kumvuta kuufikia mlango, akiwa anaweka kamgomo kiasi kutokana na kuhofia uwepo wa mama yake mkubwa, nami nikamshika shavuni na kumbusu mdomoni taratibu sana, kisha ndiyo nikafungua mlango na kuondoka. Nilikuwa ndani ya furaha ya ajabu sana. Mambo yalikuwa yameanza kunyooka!
★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★
Pata Full Story WhatsApp au inbox
Whatsapp +255 678 017 280
Karibuni sana