Bishop Hiluka
JF-Expert Member
- Aug 12, 2011
- 7,147
- 14,699
- Thread starter
- #61
50
Mara nikawaona wanaume watatu, wawili walikuwa wameshika marungu mikononi na mmoja alikuwa na panga, walikuwa wanakuja mbio eneo lile na nilipokuwa naondoka wakanizingira huku wakinitazama kwa hasira kama fisi wenye uchu walioona mzoga uliotaka kuwatoroka.
Nilipowaangalia vizuri nikagundua kuwa mmoja wao alikuwa mgambo kutokana na aina ya mavazi aliyoyavaa na wawili walikuwa wamevaa mavazi ya kawaida. Wote walinitazama kwa hasira na uchu wa kunishambulia.
Wakati nikitafakari jinsi ya kujinasua kutoka pale mara nikamwona mwanamume mwingine mrefu ambaye pia alikuwa ameshika panga mkononi akimkokota Kabula kwa nguvu na kumleta pale nilipokuwa nimesimama. Muda huo Kabula alikuwa analia kwa uchungu, kilio cha kwikwi.
Pasipo kuambiwa na mtu niliweza kugundua kuwa huyo ndiye mume wa Kabula, na hapo nikajikuta nikiishiwa nguvu na kubaki nimesimama wima bila kutingishika kama niliyekuwa nimepigiliwa miguu yangu kwa misumali.
Yule mwanamume alimsukuma Kabula kwa hasira pale nilipokuwa nimesimama. Kabula alianguka chini karibu na miguu yangu huku mtandio wake ukimdondoka chini na kumwacha na dela jepesi lililoonesha maungo yake. Alipoanguka, Kabula aliinua uso wake kuniangalia katika namna ya kunilaumu kuwa nimemponza. Aliendelea kulia kilio cha kwikwi.
Yule mume wa Kabula alinitazama kwa hasira akiwa hayaamini macho yake. Mke anauma jamani! Namaanisha mke ambaye kila mtu anayekufahamu basi anamfahamu na yeye kama ubavu wako, mwanamke unayelala naye kitanda kimoja ukimwamini kabisa kuwa ni mtu salama katika maisha yako halafu unakuja kugundua kuwa vile anavyokukumbatia na kukupa mahaba motomoto usiku mkiwa mmezima taa basi anamkumbatia na kumfanyia baharia fulani, tena mchana kweupe na pengine yeye anafanyiwa zaidi yako…
Nilipomtazama mume wa Kabula kwa umakini nilimwona akiwa ameghadhabika sana na alikuwa anajiandaa kunivamia, bahati mbaya hakujua kilichokuwa kinaendelea kwenye akili yangu muda huo. Kufumba na kufumbua, nilichomoka kwa kasi ya ajabu kama farasi wa mashindano na kutimka kama mkizi nikiwa nimejiandaa kwa lolote.
Wakati natoka nduki nilimpiga kikumbo mume wa Kabula kabla hajaniwahi na kumwangusha chini kama peto la pamba, msukumo wa nguvu ulimtupa chini kwa mshindo mkubwa na kumfanya kugaragara huku akitifua ardhi na kusababisha vumbi litimke. Wale wanaume wengine hawakukubali kuniacha niondoke kirahisi namna ile, walichomoka kunifuata kabla sijatokomea.
Nilipata shida kukimbia kwenye matuta makubwa ya lile shamba la mihogo na kupenya katikati ya mihogo iliyostawi, nyasi na vichaka. Mwanamume mmoja alirusha rungu lake likapita milimita chache juu ya kichwa changu na kuangukia mbele yangu. Yule mgambo akawahi kupita kwa mbele yangu kabla sijafika kwenye ile njia nyembamba iliyokuwa inaelekea kule barabarani.
Kabla sijajua nini cha kufanya yule mgambo akaruka kama mkizi na kunikumba, sote tukapiga mwereka chini. Akawahi kusimama huku hasira zikiwa zimempanda kichwani kama mbogo aliyejeruhiwa. Nikaona sasa anatafuta sifa, nami sikutaka kumpa hizo sifa. Nilisimama haraka nikiwa tayari kwa mapambano, na hapo mume wa Kabula naye akawa amefika nilipokuwa na kusimama kunikabili. Kwa sekunde kadhaa tulibaki tumetazamana.
Kisha kufumba na kufumbua nikamkabili mume wa Kabula akiwa bado hajakaa sawa na kumtupia mapigo mawili ya kushtukiza ya ngumi kavu za tumbo, akaguna kwa maumivu makali. Kisha nikaruka juu huku nikijipinda na kuachia teke kwa yule mgambo lililompata sawasawa kwenye kinena chake. Pigo hilo lilimrusha na kumtupa kwenye mihogo huku akitoa ukelele mkali kutokana na maumivu makali yasiyoelezeka. Alipoanguka akatulia pale chini kama mfu huku akionekana kuyasikilizia maumivu.
Kuona hivyo wale wanaume wengine wakaanza kupiga yowe la kuomba msaada baada ya kuhisi kuwa wasingeweza kunidhibiti wakiwa peke yao. Ili kupata upenyo wa kutoroka ilibidi nimvae mmoja wao aliyekuwa amesimama mbele yangu akiwa amenyanyua panga lake, nikampiga kichwa kikavu kilichompata barabara katikati ya macho na pua yake na kumvunja mshipa wa pua. Pigo hilo lilimfanya mwanamume huyo kupepesuka na kuanguka chini huku akipiga yowe kali la maumivu.
Damu zilianza kumtoka kwenye pua yake mfano wa mrija wa maji uliopasuka. Akaishika pua yake na kuiminya akijaribu kuzuia damu isiendelee kumtoka, kisha nikaanza kutimua mbio kuondoka eneo lile. Bahati mbaya sikujua nielekee uelekeo gani maana jiografia ya eneo lile ilinipa shida, na wakati nikiifuata njia moja nikashtukia nikipigwa na kitu kizito nyuma ya kichwa changu na kunifanya nihisi mwili wangu ukiyumba, maana pigo hilo lilinipata barabara na kunipa kisulisuli kilichonifanya kudondoka chini.
Muda huohuo nikaona watu wakiongezeka na sikuweza kujua idadi yao, nilishtukia tu wakinivamia pale chini nilipoanguka na kuanza kunishushia vipigo vya kila namna mwilini mwangu kama mchanga, udongo na vumbi. Mateke na vipigo vingine vikanigeuza na kunilaza chali. Muda huohuo akatokea Eddy na kuwataka wasichukue sheria mkononi kwani zipo taratibu za kufuatwa.
Kutokana na mwonekano wake na mavazi aliyokuwa ameyavaa wanakijiji wale wakasita kuendelea kunishushia vipigo. Wakaninyanyua na kutuongoza mimi na Kabula ambaye muda wote alikuwa analia tu, wakatupeleka kwenye ofisi ya Mtendaji wa Kijiji kwa ajili ya hatua zaidi.
Nilikuwa namwonea huruma Kabula kwa kuwa nilijua kuwa nimemponza kutokana na ubazazi wangu na nilijua ni kitu gani kilikuwa kinafukuta katika moyo wake, alikuwa anafanania na mtu anayeomba wakati urudi nyuma ili aweze kurekebisha makosa yake lakini kamwe wakati haurudi nyuma. Nilijizuia nisimwangalie maana sikuijua hatma ya ndoa yake baada ya fumanizi hilo.
Wakati tukielekea ofisi ya mtendaji wa kijiji niliwasikia baadhi yao wakisema kuwa adhabu yangu ingekuwa kali sana kwani kitendo nilichokifanya kilikuwa kimemshushia hadhi mtoto wa ‘Ntemi’ (kiongozi wa jadi) wa eneo lile ambaye ni mume wa Kabula. Nilitamani iwe ndoto lakini haikuwa hivyo, ukweli nilikuwa nimefumaniwa na mke wa mtoto wa Chifu wa eneo.
Tulifika kwenye Ofisi ya Mtendaji wa Kijiji na kuwakuta wazee watatu wakitusubiri kwani taarifa za fumanizi letu zilikwisha wafikia kabla hata hatujafika ofisini hapo. Muda wote tangu tulipokuwa tunatoka kule vichakani hadi tunafika pale kwenye ofisi ya mtendaji wa kijiji, Eddy alikuwa ameongozana nasi akiwa kimya kabisa. Sikujua alikuwa anawaza nini muda huo!
Watu wote walikuwa wananitazama kwa jicho kali sana kana kwamba nilikuwa nimesababisha maafa makubwa sana pale kijijini. Nilitamani ardhi ipasuke ili nijifiche chini ya ardhi kukwepa macho ya jamii lakini nilitambua kuwa muujiza huo hauji ovyo ovyo… kwa sababu ilikwisha andikwa kuwa mwisho wa ubaya wowote ule ni aibu!
Nilikalishwa sakafuni, nikamwona mzee mmoja akiinuka na kuanza kuzunguka zunguka pale ofisini huku akinitazama kwa macho makali. Nilimtazama kwa hofu kubwa.
“Sijui tukupe adhabu gani bwana mdogo ili iwe fundisho kwa wapita njia wengine wenye uchu kwa wake wa watu!” yule mzee alisema akionekana kufura kwa hasira.
Kisha niliambiwa nivue mkanda wa suruali, viatu na nitoe vitu vyote mfukoni na kuvikabidhi pale ofisini. Nilikubali kutoa vitu vyangu, na hapo nikavua mkanda wangu na kutoa pochi yangu, kisu kidogo cha kukunja, simu mbili moja ikiwa ni ile Tecno Camon 16 Pro niliyomnyang’anya Tabia au Chausiku kule Nzega na viatu vyangu, ila nilikataa kuvikabidhi vitu vyangu kwa wale wazee bali nilimkabidhi Eddy.
Itaendelea...