Bishop Hiluka
JF-Expert Member
- Aug 12, 2011
- 7,147
- 14,699
- Thread starter
- #41
30
“Ndiyo, ni mrembo kwelikweli na asiye na hatia, kwa hiyo usijaribu kutaka kuchezea hisia zake,” aliongea katika namna ya kunionya kisha akainamia tena kiti cha mbele yake na kufumba macho.
Alionekana kuwaza mbali. Kisha kama aliyekumbuka jambo, alifumbua macho yake lakini akiwa bado ameinamia kile kiti cha mbele yake na kunitahadharisha. “Tena, kuwa mwangalifu sana na wasichana warembo kama huyo, wakati mwingine ni nyoka wenye sumu kali.”
Sikusema neno, niliyapeleka macho yangu kuangalia nje, nikaona tukiupita uwanja wa mpira wa Samora (Samora Stadium) huku basi tulilopanda likizidi kuchukua kasi. Dereva wa basi alionekana kuwa mzoefu sana wa barabara hiyo tuliyopita kutokana na jinsi alivyokuwa anaendesha kwa mbwembwe huku akiwa makini barabarani akiwakwepa waendesha baiskeli, pikipiki na mikokoteni waliokuwa wakipita kandokando ya ile barabara.
Basi lilipofika katika mzunguko wa barabara za Tabora, Shinyanga, Bukene na ile ya Singida tuliyotokea, liliupita ule mzunguko na kuifuata barabara ya Bukene iliyokuwa inapitia Itobo. Hapo nikageuka tena kumtupia jicho yule mrembo wa shani, na wakati huohuo na yeye alikuwa anainua uso wake toka kwenye simu yake na kunitazama.
Alipogundua kuwa nilikuwa natazama upande wake akaachia tabasamu kabambe huku myumbo wa lile basi tulilopanda ukimpotezea umakini. Hata hivyo nilizuga nikajifanya sikuwa namtazama yeye.
Jambo moja lililonitatiza zaidi ni kwamba kila mara alipohisi kuwa nilikuwa namtazama alikuwa anaachia tabasamu, sikujua ni kwa nini, hata hivyo nilijipa subira huku nikiamini kuwa huo ulikuwa mwanzo mzuri wa kujenga daraja la urafiki baina yetu, urafiki ambao hatimaye ungetupeleka kwenye ulimwengu wa mahaba mazito.
Dereva wa basi la Makenga alionekana kuijua vizuri barabara ile, sasa alikuwa akipanga na kupangua gia wakati basi lile lilipokuwa likikatisha kwenye ofisi za Halmashauri na ofisi zingine, kisha tulianza kukatisha katikati ya makazi ya viongozi na watu wenye ukwasi. Baada ya dakika kadhaa tulikuwa tunashusha mteremko fulani kwenye kilima nje kidogo ya ule Mji wa Nzega katika eneo ambalo kulikuwa na majengo ya idara ya ujenzi.
Dereva alionekana kuifurahia sana kazi yake kwani alikuwa anaendesha kwa mbwembwe huku akiwa makini zaidi kuyakwepa mawe madogo madogo na makorongo yaliyosababishwa na mvua katika ile barabara. Niligeuza shingo yangu kutazama nje kupitia kwenye kioo cha dirisha na hapo nikagundua kuwa mwendo wetu ulikuwa wa kasi mno.
Hali hiyo iliifanya ile taswira ya kile kilima jirani na majengo idara ya ujenzi na hata nyumba za makazi ya watu katika Mji wa Nzega kutoweka taratibu katika upeo wa macho yangu kadiri lile gari lilivyokuwa linachanja mbuga.
Niliyatembeza tena macho yangu kuwatazama abiria wengine waliokuwa wameketi kwa utulivu mle ndani ya basi la Makenga na hapo nikagundua kuwa wengi walionekana kuzama katika tafakari, huwenda walikuwa wanawaza juu ya ile safari na wengine walipitiwa na usingizi kutokana na uchovu au njaa.
Muda mfupi baadaye tulikuwa tumeuacha Mji wa Nzega nyuma yetu katika mwendo wa masafa marefu na hatimaye tukatokomea kabisa mbali na mji ule huku tukikatisha katikati ya mashamba, vichaka na miti mirefu na mifupi ya porini. Kimya kiliendelea kutawala ndani ya basi la Makenga na sauti pekee iliyokuwa inasikika mle ndani ilikuwa ni ya muungurumo wa injini kukuu ya basi na mnuko wa harufu nyepesi ya dizeli.
Safari ikiwa inaendelea niligeuza tena shingo yangu kiaina kumtazama yule mrembo wa shani na hapo nikamwona akiwa amekiegemeza kichwa chake kwa nyuma kwenye kiti alichokalia huku akionekana kuanza kupitiwa na usingizi.
Japokuwa hata mimi nilikuwa na uchovu mwingi lakini kamwe sikuuruhusu usingizi unichukue kwa kuzingatia kuwa hii ilikuwa mara yangu ya kwanza kusafiri katika barabara hiyo ya Itobo, hivyo nilikuwa mgeni kabisa wa barabara ile na mazingira yake. Kawaida yangu ilikuwa kwamba, kama sehemu niliyokuwa naenda ilikuwa ngeni kwangu sikupenda kusinzia kwa sababu nilitaka kuyakariri maeneo na vituo ili siku nyingine nisipate taabu ya kuuliza.
Nilipomuona yule mrembo wa shani amepitiwa usingizi nilihisi kumhurumia sana kwa hali ile ya uchovu aliyokuwa nayo, hata hivyo sikuwa na namna yoyote ya kumsaidia. Hisia fulani hivi za mahaba ndani yangu zilizidi kunitesa na kunifanya nihisi kuwa na hali isiyokuwa ya kawaida, hasa kitendo cha kukaa mbali na yule mrembo wa shani.
Ingekuwa ni amri yangu ningemwambia Eddy akakae kule kwenye kiti cha nyuma ili yule mrembo wa shani aje kukaa karibu yangu nimkumbatie.
Niligeuza tena shingo yangu kumtazama yule mrembo wa shani na kumwona akiwa ametopea kwenye usingizi. Nilishusha pumzi za ndani kwa ndani na kujiegemeza kwenye kiti changu, na mara nikaanza kuwaza jinsi ambavyo maisha mapya katika Mji wa Kahama yangekuwa baada ya kupata kazi katika mgodi wa dhahabu wa Buzwagi.
Kabla sijazama kwenye mawazo yale nikashtushwa na kupungua ghafla kwa mwendo wa lile basi letu. Haraka nikainua kichwa changu na kuangalia huku na kule na hapo macho yangu yakatua kwa askari mmoja wa usalama barabarani aliyekuwa anaibuka kutoka nyuma ya roli moja la mafuta aina ya Isuzu lililokuwa limeegeshwa kando ya barabara ile.
Yule askari wa usalama barabarani alisimama katikati ya barabara, umbali mfupi mbele yetu akiwa ameshika kitu fulani mfano wa tochi au kamera.
Kitendo cha mwendo wa lile gari letu kupungua ghafla kiliwafanya abiria wengine, akiwemo Eddy, washtuke kutoka usingizini na kuangalia kule mbele. Basi letu liliposogea karibu zaidi nikawaona askari wengine wawili wa usalama barabarani wakiibuka na kusimama kando ya barabara huku wakilitazama lile basi la Makenga kwa umakini na uchu mkubwa wa kupata ‘kitu kidogo’.
Nilipochunguza vizuri nikagundua kuwa yule askari wa usalama barabarani aliyekuwa wa kwanza kujitokeza alikuwa ameshika kamera maalumu ya kuchunguza mwendo kasi wa magari na sasa alikuwa amesimama katikati ya barabara mbele yetu huku akimwonesha dereva wa gari letu ishara ya mkono kumtaka aegeshe gari lake kando ya barabara.
Niliwaona wale askari wengine wawili waliokuwa wamesimama kando ya barabara ile, mmoja alikuwa ameshika mkononi mashine ndogo ya kielektroniki ya kutolea risiti za papo kwa papo baada ya malipo na mwingine alikuwa ameshika bunduki aina ya SMG.
Nilimtazama dereva wetu kwa umakini huku nikijaribu kumchunguza kuona kama alikuwa na wasiwasi wowote juu ya lile tukio la kusimamishwa kwetu na wale askari wa usalama barabarani lakini sikuona wasiwasi wowote usoni kwake na badala yake nikamwona akikazana kupangua gia za lile basi huku akipunguza mwendo taratibu.
Hatimaye basi liliwapita taratibu wale askari wa usalama barabarani na kwenda kusimama mbele kidogo, umbali wa takriban mita therathini kutoka pale walipokuwa wamesimama askari wa usalama barabarani, kisha yule dereva wa basi letu aligeuza shingo yake kumtazama kondakta wake na kumpa ishara ambayo niliielewa vyema, ilikuwa ni kumtaka ampe fedha kwa ajili ya kuwapa wale askari wa usalama barabarani.
Itaendelea...