Mjadala Wangu na Marehemu Mayanja Kiwanuka 1988

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
21,884
31,940
MJADALA WANGU NA MAREHEMU DR. KATAROGE MAYANJA KIWANUKA (AHMED KIWANUKA) 1988

Nimepokea ujumbe huo hapo chini kutoka kwa mmoja wa wasomaji wangu:

‘’Historia hii itufunze mambo mengi.

Kafa Kiwanuka alikuwa mwanajeshi hadi cheo cha Captain.

Alikuwa Mshauri wa Rais Mkapa, alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Kagera, Arusha na Rukwa, alikuwa Balozi wa Tanzania nchini India toka mauti yalipomkuta hatangazwi popote zaidi ya nduguze Waislamu pengine mchango wake katika dini ulikuwa mdogo sana.’’

Nilifahamiana na Mayanja Kiwanuka na tukikutana tulikuwa na mazungumzo marefu.

Siku za nyuma tuliingia katika mjadala mkali baina yetu katika gazeti la Africa Events.

Mimi nikieleza mchango wa Waislam katika kupigania uhuru wa Tanganyika yeye akinipinga.

Nilipopokea taarifa ya kifo chake hakika nilisikitika na swali lililonijia mara moja ni kuwa niseme nini kuhusu msomi huyu makini na mhitimu wa Columbia University, New York?

Mara ya mwisho mimi kukutana na Dr. Kwanuka ilikuwa Msitiki wa Ibadh na tukasimama nje tukazungumza kwa kipindi na nakumbuka akanifahamisha kuwa kimetoka kitabu cha maisha ya Kaluta Amri Abeid nifanye hima nikisome.

Tulipoachana nikaenda kukitafuta kitabu hicho na kukipata.

Miaka mingi imepita hatukujaaliwa kuonana tena.

Nataka kumweleza Dr. Kiwanuka kama nilivyomwandika wakati wa uhai wake na yeye nina hakika aliyasoma yote niliyoandika.

Mjadala wetu wa kwanza ulikuwa mwaka wa 1988.

Africa Events ilichapa Makala yangu ambayo nilimtaja Abdulwahid Sykes na wazalendo wengine katika kuasisi TANU.

Katika makala yale nilifanya jambo ambalo kabla yake lilikuwa halijafanywa na mwandishi yeyote.

Nilisema kuwa Waislam ndiyo walikuwa mstari wa mbele katika kupigania uhuru wa Tanganyika.

Wakati ule ilikuwa mwiko kabisa kunasibisha Uislam au Waislam na harakati za kudai uhuru.

Nilipewa kemeo kali kutoka kwa Dr Mayanja Kiwanuka, kiongozi wa jopo lililoandika kitabu, ‘’Historia ya Chama Cha TANU 1954-1977,’’ kitabu kinachoeleza historia rasmi ya TANU.

Ndani ya kitabu hiki wazalendo wengi hawakutajwa.

Dr. Mayanja Kiwanuka alikuwa na haya ya kusema dhidi ya makala yangu: '’Makala inadai kuwa ingawa Waislam Tanzania walitoa mchango muhimu katika harakati za kudai uhuru, zipo juhudi za makusudi za kufifilisha mchango wao.

Kutokana na hayo, makala nzima ina ngano ili kuipa nguvu fikra zake, zaidi kwa kutaja majina ya wazalendo wa TANU ambao imetokea kuwa ni Waislam.

Ukuu wa TANU, na hasa ukuu wa kiongozi-muasisi wake, Mwalimu Nyerere, ni kuwa, baada ya muda mfupi tu toka kuasisiwa (TANU), ikaweza kuwaunganisha watu katika vuguvugu la utaifa lenye nguvu, lau kama watu hao walikuwa tofauti kwa kabila, utamaduni na dini zao.

Nia ya Said ni kupandikiza chuki, kwa bei yoyote ile, ukweli kwake yeye si kitu muhimu.’’

In Shaa Allah itaendelea...

MJADALA WANGU NA MAREHEMU DR. KATAROGE MAYANJA KIWANUKA (AHMED KIWANUKA) SEHEMU YA PILI NA YA MWISHO

Hizi ndizo zilikuwa fikra za marehemu Dr. Mayanja Kiwanuka, ambae aliaminiwa na CCM kusimamia utafiti na uandishi wa historia mahsusi ya chama cha TANU.

Kilichomkera Dr. Kiwanuka ni kule mimi kusema kuwa Waislam ndiyo waliokuwa mstari wa mbele katika kudai uhuru wa Tanganyika na kutaja jina la Abdulwahid Sykes kama muasisi wa TANU.

Kwa ajili ya kuwataja Waislam, makala ya utafiti ikawa yeye akaichukulia kuwa ni sawasawa na ngano, yaani hadithi.

Dr. Kiwanuka katika makala yake akanituhumu kwa kusema uongo.

Dr. Kiwanuka hakuweza kuuepuka msimamo wa CCM wa kutia mkazo katika kumsifu mtu mmoja, Nyerere peke yake katika kuasisi TANU kwa kusema ‘’Ukuu wa TANU, na hasa ukuu wa kiongozi - muasisi wake, Mwalimu Nyerere…’’

Wakati Dr. Kiwanuka akiandika maneno haya alikuwa Katibu Msaidizi katika Idara ya Propaganda na Uhamasishaji Umma katika Chama Cha Mapinduzi.

Nilijibu mashambulizi ya Dr. Kiwanuka kwangu kwa kueleza kuwa yote niliyoyaandika ni matokeo ya utafiti na ninao ushahidi kwa yale niliyosema.

Kufuatia majibu haya Dr. Kiwanuka alinijibu kwa ufedhuli kwa kuniita ‘’mwanahistoria nisiye na kimo’’ na akanitisha kwa kuapa kuwa endapo nitajaribu kuibadilisha historia ya Tanzania ataniandama mimi na ndugu zangu.

Baada ya mjadala huu baina yetu watu wengi nje ya Tanzania walijitokeza kuniunga mkono na huo ndiyo ukuwa mwisho wa ubishi.

Leo nikiangalia nyuma na nilipokuja kumfahamu Dr. Kiwanuka kwa karibu na tukawa marafiki nilimwelewa kwa nini aliwajibika kuchukua msimamo ule aliochukua.

Wakati ule nilishangaa kwa nini mimi niliyoiweka historia ya TANU sawasawa kwa kufanya utafiti ndiyo ninaetishwa na wale walioipotosha historia wanaachiwa waendelee kuipotosha na kuifanyia ufisadi kadri watakavyo.

Dr. Kiwanuka ni mwandishi wa sifa anapotaka kunyanyua kalamu kuandika.

Dr. Kiwanuka akiwa mwanafunzi Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, aliandika tasnifu kuhusu uhusiano wa Waislam na Wakristo Tanzania, ‘’The Politics of Islam in Bukoba District,’’ (1973).

Tasnifu hii ni muhimu kwa kila mwanafunzi wa historia ya uhuru wa Tanzania, hasa miaka 10 ya mwanzo baada ya uhuru.

Katika tasnifu hii Dr. Kiwanuka anaeleza chanzo cha uhasama kati ya Bibi Titi na Nyerere.

Uhasama wao ulisababishwa na mgogoro wa EAMWS mwaka wa 1968 ingawa unaweza kusema kuwa mwaka wa 1968 ulilipuka kwa nguvu zaidi kwani mwaka wa 1963 Nyerere na Bibi Titi walishapambana ndani ya kikao cha Kamati Kuu ya TANU kuhusu Aga Khan na EAMWS.

Bibi Titi akiitetea EAMWS.

Leo miaka 36 imepita toka mimi na Dr. Kiwanuka tupambane katika mjadala ule wa historia ya kweli ya TANU.

Ndugu yangu Dr. Mayanja Kiwanuka ametangulia mbele ya haki na kwa kipindi hiki cha miongo minne ameshuhudia mabadiliko makubwa katika historia ya TANU na uhuru wa Tanganyika.

Ameshuhudia kuona Abdul na Ally Sykes wakitunukiwa Medali ya Mwenge wa uhuru kwa mchango wao katika kupigania uhuru wa Tanganyika.

Baada ya mjadala ule mwaka wa 1988 kiasi cha kupita miaka 10 kikachapwa kitabu changu, ‘’The Life and Times of Abdulwahid Sykes (1924 – 1968) The Untold Story of the Muslim Struggle Against British Colonialism in Tanganyika,’’ Minerva Press London, 1998.

Kitabu hiki kimechapwa matoleo manne hadi hivi sasa na kimefungua ukurasa mpya wa utafiti katika historia ya uhuru wa Tanganyika.

Namuomba Allah amsamehe ndugu yangu na mja wake huyu Dr. Ahmed Kiwanuka dhambi zake na amtie katika pepo ya Firdaus.
Amin.

1731730489751.jpeg
1731730893911.jpeg
 
Ahsante mkuu, mimi natafuta shairi la marehemu kaluta amri abeid yenye mstari "ndovu akapita wima, sisimizi akakwama"
 
Nduguze waislamu?, ndugu zake wote ni waislamu?? Na mkapa alimpa vvyeo pia alikuwa muislamu?!
 
Naamini hao waislamu, wakristu au wapagani walipigania uhuru kama Watanganyika au waafrika kuondokana na dhulma ya ukoloni hawakuwa wanapigania uhuru wa wakristu au uhuru wa waislamu kama unavyosadifu mzee Mohamed Said hakuna jamii ikiyounga mkono ukoloni
 
Mama...
Kughitilafiana katika fikra ni silka yetu binadamu.

Wewe unaniona mimi mtu hatari wengine wananialika kwenye vyuo vyao Marekani na Ulaya kuzungumza.

Wengine wananitia katika miradi mikubwa ya kuandika historia.
Hata magaidi huwa wana wana watu wanaowapenda. Wewe mtu unayefaa kudhibitiwa.
 
Mwalimu, kwa mawazo yangu naona ni vyema kuwatambua watanganyika wote katika harakati zao za kudai uhuru, kuliko kuwatambua kwa makundi Yao hasa ya uduni na ukabila, wamatengo na wamatumbi kesho watadai wao wanatakiwa wapewe upendeleo Fulani kwa sababu ndg zao wengi waliuawa kwenye harakati za kuutafuta uhuru...

Sidhani kama yana maana sana kuanza kuongelea dini Fulani mchango wake ni upo, ilihali dini zenyewe walizileta wao, kwa maslahi ambayo mpka kesho yapo wazi!
 
Kadhi...
Hakika ni udini.
Nilijiuliza iweje mimi hapa Chuo Kikuu Cha Dar-es-Salaam nasomeshwa historia isiyo ya kweli?

Mwalimu kaniuliza historia ya kweli ni ipi?

Nikamjibu kuwa mimi nawajua waasisi wa harakati hizi mfano Kleist Sykes, Clement Mtamila, Ali Jumbe Kiro, Ibrahim Hamisi, Tatu bint Mzee hawa ni wazee wa mtaani kwangu Gerezani.

Hawa wameunda African Association 1929 na Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika 1933 na vyama vyote hivi vilikabiliana na serikali ya kikoloni.

Wazee wangu hawa nafahamu historia zao.

Iweje hapa chuoni kwenye somo hili la historia ya TANU anatajwa Julius Nyerere peke yake tena baada ya kufika Dar es Salaam 1952?

Aliyempokea Nyerere Abdul Sykes.

Hata Abdul Sykes mbona hatajwi?

Udini naam udini hawa wote niliowataja hapa ukimtoa Clement Mohamed Mtamila ni Waislam waasisi wa Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika (Umoja wa Waislam wa Tanganyika).

Namwambia mwalimu, "Mimi babu yangu alikuwapo na kashiriki katika harakati zote hizi akiishi Mtaa wa Kipata katika miaka hiyo."
 
Hata magaidi huwa wana wana watu wanaowapenda. Wewe mtu unayefaa kudhibitiwa.
Mama...
Nidhibitiwe kwa kosa gani nililofanya?

Kwa kuandika kitabu cha Abdul Sykes?

Mengi katika historia ya Julius Nyerere yaliyokuwa watu hawayajui wamejifunza baada ya kusoma kitabu cha Abdul Sykes.

Wewe ulikuwa unajua kuwa Nyerere aliingizwa katika uongozi wa TAA baada ya kujadiliwa nyumbani kwa Hamza Mwapachu Nansio na Mwapachu , Abdul Sykes na Ali Mwinyi Tambwe?

Ulikuwa unajua kuwa Abdul Sykes, Ally Sykes na Julius Nyerere ndiyo waliopewa jukumu la kuisajili TANU?

Ulikuwa unajua kadi za TANU zikiuzwa misikitini na Mufti Sheikh Hassan bin Ameir na Kariakoo Market ofisini kwa Market Master Abdul Sykes?

Wewe huvutiwi na historia hii?
 
Mwalimu, kwa mawazo yangu naona ni vyema kuwatambua watanganyika wote katika harakati zao za kudai uhuru, kuliko kuwatambua kwa makundi Yao hasa ya uduni na ukabila, wamatengo na wamatumbi kesho watadai wao wanatakiwa wapewe upendeleo Fulani kwa sababu ndg zao wengi waliuawa kwenye harakati za kuutafuta uhuru...

Sidhani kama yana maana sana kuanza kuongelea dini Fulani mchango wake ni upo, ilihali dini zenyewe walizileta wao, kwa maslahi ambayo mpka kesho yapo wazi!
Kind...
Hilo la kuwatambua wale walioanzisha vuguvugu la kudai uhuru ndilo ninalofanya.

Mimi ndiyo niliyokuwekeeni historia ya Dr. Kwegyir Aggrey kutoka Achimota College Ghana alipokutana na Kleist Sykes mwaka 1924 na Dr. Aggrey akampa wazo Kleist la kuunda African Association.

Mimi ndiyo niliyokuwekeeni hapa waasisi wa African Association: Mzee bin Sudi, Ali Said Mpima, Suleiman Majisu, Zibe Kidasi, Ibrahim Hamisi, Kleist Sykes, Cecil Matola, Raikes Kusi na Rawson Watts.

Mengi nimeeleza.

Usitishike na kuwa safari ya Nyerere hafla ya kumuaga safari ya kwanza UNO ilifanyika jengo la Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika.
 
Back
Top Bottom