MBUNGE DKT. FLORENCE SAMIZI, Mbunge wa Muhambwe Akichangia Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Maji, Mwaka wa Fedha 2024-2025 Bungeni, Dodoma.

Stephano Mgendanyi

JF-Expert Member
May 16, 2020
1,994
961

MBUNGE DKT. FLORENCE SAMIZI, Mbunge wa Jimbo la Muhambwe Akichangia Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Maji katika Mwaka Mpya wa Fedha 2024-2025 Bungeni Jijini Dodoma.

"Nampongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi anavyofanya kazi kwa bidii kuhakikisha azma ya kumtua Mama Ndoo kichwani inatimia. Tumeona kwenye majimbo yetu fedha zimemiminika. Jimbo la Muhambwe limepokea takribani Shilingi Bilioni 8.5 ili kutekeleza miradi ya Maji Mjini na Vijijini. Hii imepelekea ongezeko la upatikanaji wa maji Vijijini kutoka asilimia 54 mpaka asilimia 77 na Mjini kutoka asilimia 37 mpaka asilimia 67" - Mhe. Dkt. Florence Samizi

"Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Maji, Jumaa Aweso na Naibu Waziri na Watendaji wote wa Wizara ya Maji. Niwapongeze Watendaji wa Maji Mkoa wa Kigoma kwa jinsi wanavyofanya niweze kutekeleza kazi za miradi ya Maji jimboni Muhambwe kwa urahisi"

"Mheshimiwa Waziri wa Maji, wana Muhambwe tunakushukuru sana kwasababu ahadi ulizoahidi zimekwishatekelezeka, tumepokea gari moja, tumepokea Pikipiki Nane (8), tumepokea Guta ya Tani tatu (3) katika Jimbo letu la Muhambwe"

"Tumeona Wizara ya Maji kwa kufanya kazi kwenu vizuri kumepelekea muwafikishie maji watu milioni 4 badala ya milioni 3 na hii imepelekea mpewe fedha zaidi. Tumeona miradi ya P4R itakwenda kupokea Dola za Marekani Milioni 654 kutoka Dola Milioni 350"

"Wananchi wa Muhambwe wamefaidika, Bilioni 1.3 uliyonipatia kutoka P4R wananchi wa Lukaya wanakunywa maji, wananchi wa Magalama wanakunywa maji na wananchi wa Mikoko wanakunywa maji. Tunaamini tutaendelea kupata fedha zaidi ili miradi katika majimbo yetu iweze kutekelezeka"

"Bado zipo changamoto ndogo ndogo ambazo tunaamini Serikali yetu inaweza, wananchi wa Mkoa wa Kigoma wamefurahi sana kusikia tunakwenda kuingia kwenye historia ya kupata Maji kwenye Ziwa Tanganyika. Jimbo la Muhambwe lina mto Malagarasi. Kutoka mto Malagarasi mpaka Kata ya Busunzu ni Kilomita 8. Wananchi wa Nyalulanga na Busunzu hawana maji ilihali wapo katika mto Malagarasi. Mheshimiwa Waziri ingiza mto Malagarasi, utakwenda kutatua changamoto"

"Jimbo la Muhambwe tunafanya vizuri sana, tunapata maji Lita Milioni tatu (3) kwa siku lakini mahitaji ni Lita Milioni 6.8 kwa siku. Mitambo ya Samia Suluhu Hassan tumechimba maji katika Kata ya Lusohoko, kimeleta maji mengi sana katika Mkoa mzima na kinatoa maji laki 3.5 kwa saa moja"

"Hatuna sababu ya kuleta maji kutoka Nduta kwaajili ya maji ya Mamlaka ya Mji (Kata ya Kibondo Mjini, Bitulana na Kumwambu). Tumeshakuletea andiko linalogharimu Shilingi Bilioni 4.5. Tutakwenda kuweka Tenki kwenye mlima wa Muyaga Kitahana, maji tunatoa Lusohoko badala ya kuhangaika na mto Nduta"

"Naomba Mheshimiwa Aweso, nihakikishie umeniwekea mradi wa Maji kutoka Kisima cha Lusohoko ili wananchi wa Jimbo la Muhambwe waweze kupata maji. Tutaongeza na kutimiza matakwa ya Ilani yetu ambayo inatutaka tufikie asilimia 85 kwa 95 maji Mjini na Vijijini"

"Upo mradi wa Maji wa Nyamkokoma Kata ya Kumwambu wananchi hawana maji kabisa, mradi umeshaanza kwa kununua mabomba tulipopata Shilingi Milioni 300 na mradi huu unahitaji Shilingi Bilioni 1. Naomba Serikali inisaidie kupata fedha tuweze kutekeleza mradi wa Maji Nyamkokoma"

"Tunavyo vijiji sita (6) ambavyo havijapata miradi, naamini vijiji vya Kamkuyu, Kasana, Nyarugusu, Kumuhama, Nyaluranga na Kigina vitafaidikika na visima Mia tisa (900) ambavyo Mheshimiwa Rais ametoa. Kwa niaba ya Wananchi wa Muhambwe nawashukuru sana Serikali kwasababu sasa Tutakwenda kupata miradi ya Maji katika Vijiji vyote vya Jimbo la Muhambwe ili wananchi wapate maji safi na salama" - Mhe. Dkt. Florence Samizi, Mbunge wa Jimbo la Muhambwe
 

Attachments

  • hqdefaultmnbvcft.jpg
    hqdefaultmnbvcft.jpg
    14.1 KB · Views: 1
Back
Top Bottom