***
‘Una hakika hana silaha?’ Hilo lilitosha kabisa kumdhihirisha Nuru kuwa kifo cha Chongo kwake kilikuwa sawa na kuruka jivu na kukanyaga moto. Hakuwa na shaka tena kuwa kijana huyu mtanashati, ambaye amekuwa akimsikiliza na kumchungulia katika tundu la ufunguo, hakuwa rafiki bali adui yake mkubwa; adui ambaye bila ya shaka yoyote ndiye aliyekuwa akimtumia Chongo na marehemu wenzake wote.
Hofu, ambayo ilimtinga saa mbili zilizopita alipokata tamaa kabisa ya kuendelea kuishi mara Chongo alipomlenga bastola tayari kabisa kuifyatua, ambayo ilianza kumtoka, ilimrudia tena. Akiwa hana la kufanya Nuru alikuwa akiisubiri risasi hiyo wakati jambo ambalo hakulitarajia lilipotokea.
Picha iliyokuwa katika ukuta mmoja wa chumba hicho iliteleza ghafla na kuanguka. Papohapo bastola ambayo ilikuwa na kiwambo cha kupotezea sauti ilichungulia na kufyatuka. Risasi mbili zilimpata Chongo kifuani na kumfanya aanguke chini ambapo alitapatapa kwa muda kabla ya kukata roho.
Nuru alipotazama ilipotokea risasi hiyo aliuona uso wa Banduka ukichungulia na sauti yake kumfikia ikisema, “Usiogope, nakuja.” Baada ya muda alisikia funguo zikichomekwa katika kitasa cha mlango. Harakaharaka, Nuru aliinama na kuiokota bastola ya Chongo akaifutika katika vazi lake la ndani. Banduka alipofungua mlango na kuingia chumbani humo huku akitetemeka alimkuta Nuru kaketi juu ya kochi akimtazama marehemu.
“Nimeua. Sikutegemea kuua…” aliropoka. Kisha, kana kwamba ndio kwanza anamwona Nuru alifoka, “Msichana, huu nani wewe?? Nilikuwa nikichungulia unavopigana. Sijaona mtu akipigana kama wewe.”
“Ni hadithi ndefu, isiyo na kichwa wala miguu,” Nuru alimwambia “Nadhani kwa wakati huu ningekushauri tuwapigie simu polisi ili waje wamwondoe huyo,” alisema akielekeza mguu wake kwa marehemu.
Polisi? La! La! La! Siwezi kuwashirikisha.”
“Lakini umeua katika kujihami. Amekuvamia na angeweza kuniua mimi na wewe pia… Mimi nitakuwa shahidi,” Nuru alijaribu kumwelimisha.
“Na wakati huo nitakuwa mahabusu wanangu wakifa njaa na biashara zangu kuharibika. Polisi hapana” Alisita kidogo akiwaza. Kisha akaongeza. “Labda nikuombe unisaidie tuufiche huu mzigo ndani ya kabati, wakati nafikiria la kufanya. Baada ya hapo unaweza kwenda zako.”
Waliifanya kazi hiyo kwa tabu kuliko Nuru alivyotarajia. Kuua ni jambo moja, kubeba maiti ni jambo lingine. Kwa Nuru ilikuwa kazi ya kutisha na ilimtia kichefuchefu. Alijikaza kisabuni na kustarehe pale tu ambapo maiti hiyo ilifungiwa kikamilifu ndani ya kabati hilo.
Baada ya kazi hiyo ndiyo kwanza Nuru alijitazama na kuona alivyokuwa mchakavu. Nguo hizo chafu pia zilikuwa zimetatuka ovyo hapa na pale. Kwa jumla, nguo zilimfanya awe nusu uchi. Alimtazama Banduka kwa aibu na kumwomba msaada wa kuazimwa nguo za mkewe ili aondoke akiwa katika hali nzuri kiasi.
Bila kusita Banduka alimletea gauni moja zuri, jozi ya viatu na khanga mbili. Nuru alimshukuru na kuingia bafuni ambako alivua na kuufariji mwili wake kwa maji baridi.
Ni wakati alipomaliza kuvaa aliposikia hodi na hatimaye, kuchunguliwa na mtu huyo ambaye alikuwa akizungumza kwa kujiamini; mtu ambaye alionekana hatari zaidi.
Afanye nini? Alijiuliza. Apige kelele? Hilo alilipuuza mara moja. Yeye si msichana wa kufanya hilo. Zaidi, udadisi ulikuwa umeipiku hofu katika moyo wake. Alijisikia hamu ya kufahamu ni kina nani wanaofanya mambo haya yasiyoeleweka na kiini chake. Kujificha bafuni kusingemsaidia. Aliipapasa tena bastola yake na kuhakikisha kuwa imefichika vilivyo. Kisha, alijitazama katika kioo na kurekebisha nywele zake. Baada ya hapo alifungua mlango wa bafu na kutoka taratibu.
Picha za Nuru ambazo Kakakuona alikuwa nazo zilimdhihirishia kuwa binti huyo ni “kipande kizuri cha kazi ya sanaa ambayo mungu aliifanya kikamilifu.” Hayo aliwahi kuyasema kimoyomoyo. Hata hivyo, hakujua kuwa msichana huyu alikuwa mzuri kiasi hiki. Alimwangalia kwa mshangao tangu alipoufungua mlango na kutoka taratibu kana kwamba anafanya majaribio ya kupigwa picha za sinema. Alimtumbulia macho pia wakati alipowasogelea na kuwasalimu kwa sauti dhaifu, ambayo Kakakuona aliiona tamu. Kisha, alijikusanya na kuukumbuka wajibu wake.
“Pole sana, darling,” alimwambia.
Nuru alimtumbulia macho yake mazuri, huku akiliweka vizuri gauni lake la kuazima, ambalo alihisi linampwaya japo lilimkaa kana kwamba mshonaji alimfikiria yeye.
“Pole kwa misukosuko yote iliyokukumba. Maadamu nimefika hakuna lingine litakalotokea,” aliendelea.
Nuru hakumjibu. Hakuwa na la kumjibu, jambo ambalo lilimfanya Kakakuona ahisi kuwa anamwogopa Banduka. Hivyo, alimwomba akatayarishe chakula ili azungumze faragha na mpenzi wake.
Walipobaki peke yao, Nuru alimuuliza, “Wewe ni mmoja wao?”
“Ndiyo na hapana.”
“Una maana gani?”
“Nina maana hiyohiyo. Ndiyo, mimi ni mmojawao na hapana; mimi si mmojawao.”
Alipoona Nuru hajamwelewa aliongeza baada ya kutoa tabasamu pana, “Maana yangu ni kwamba, mimi ndiye niliyewatuma wakulete. Amri ya kufa au kuishi kwako iko mikononi mwangu. Niliwalipa vizuri sana ili wafanye kazi ndogo sana ya kukuchukua na kukuleta kwangu. Kwa bahati mbaya wamekuwa kundi kubwa la wapumbavu watupu. Wote sasa ni marehemu. Mmoja anaoza humo ndani ya kabati. Sio?”
Nuru hakumjibu.
“Wamekufa wote. Wanaume wanne. Wewe huko hai. Umetulia huna wasiwasi wowote. Ndio kwanza unatoka zako kuoga. Sivyo?”
Nuru alipochelewa kujibu Kakakuona aliongeza, “Sijui una kitu gani. Sielewi umetumia hila gani kuwaangamiza watu wote wale. Ila ninachokuarifu ni kitu kimoja. Naitwa Kakakuona. Mimi na kifo hatutofautiani sana. Nikisema kufa, lazima utakufa. Upo?”
Nuru aliamua kutomjibu.
“Napenda uelewe hivyo. Wala usidhani kuwa najipendekeza kwako. Ngoja nikuonyeshe.”
Aliinama na kuichukua briefcase yake. Akaifungua na kuipekua hadi mkono ulipotoka ukiwa umeshikilia picha ya yule msichana aliyeharibiwa uso.
“Unaona?” alisema akimkabidhi Nuru. “Unaona? Hiyo ni kazi yangu.”
Ilikuwa haitazamika mara mbili. Nuru alimrudishia upesiupesi huku akijisikia kutapika.
“Hiyo ni kazi yangu,” Kakakuona alirudia akicheka. “Nafurahi kuwa umeipenda picha hiyo. Unaonaje hapo utakapojikuta na sura kama hiyo? Utafika mbele ya yule hawara yako, Joram Kiango? Si atakufa kwa uchungu?”
Kutajwa kwa jina la Joram kuliisisimua damu ya Nuru. Alijikuta akirudiwa na maswali ambayo yamekuwa yakimsumbua sana juu ya usalama wake. Alitamani amuulize mtu huyo kama wamemkamata au la. Kwa jumla, alikuwa na maswali mengi ya kumuuliza. Lakini aliamua kutumia silaha ya ukimya na utulivu ili kupambana na mtu huyo ambaye alikuwa akijaribu kupandikiza hofu katika moyo wake, mchezo ambao Nuru hakuwa mgeni nao.
“Nasikia Joram ni shujaa na ana roho ngumu. Nasikia hakutokwa hata na chozi moja baba yake alipofariki. Hivyo, bila shaka hatashtushwa na kifo chako. Lakini atakapokuona uko hai, ukiwa na sura kama hii, hatalia kweli?”
Kana kwamba anajijibu mwenyewe aliongeza harakaharaka, “ Lakini haitatokea, labda kama utakuwa mbishi. Jitahidi akija mwenyeji wetu tuwe kama mtu na mpenzi wake. Baada ya kula tutaondoka zetu kwenda Dar es Salaam, mkono kwa mkono hadikwenye chombo. Tutakaa mkono kwa mkono hadi tuendako. Ukijitia kujua umeumia. Iwe mbele ya watu, iwe mimi na wewe, upo?”