SoC03 Vijana na Kilimo Tanzania

Stories of Change - 2023 Competition

Melkizedeckmassawe9

New Member
Dec 9, 2021
3
2
Muktasari:
Kilimo ni sekta muhimu sana nchini Tanzania, ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa katika uchumi wa taifa na ajira za wananchi. Hata hivyo, katika miaka ya hivi karibuni, sekta hii ya kilimo imekuwa ikikabiliwa na changamoto nyingi, ikiwemo uzee wa wakulima na ukosefu wa ushirikishwaji wa vijana.

Kwa kuwa vijana ni kundi lenye nguvu kazi kubwa na lenye uwezo wa kuleta mabadiliko, ni muhimu kuwekeza katika ushirikishwaji wao katika sekta ya kilimo ili kuendeleza na kuboresha uzalishaji wa kilimo.

Makala hii inalenga kuchunguza umuhimu wa ushirikishwaji wa vijana katika sekta ya kilimo nchini Tanzania na kuangazia faida ambazo zinaweza kuletwa na ushirikishwaji wao. Kwa kufanya hivyo, makala hii pia inatoa mwanga juu ya hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kuvutia, kuwawezesha na kuwajengea vijana uwezo wa kushiriki kikamilifu katika kilimo.

Tukianza na kuangazia umuhimu wa ushirikishwaji wa vijana katika sekta ya kilimo nchini Tanzania na pamoja faida ambazo zinaweza kuletwa na ushirikishwaji wao.

Ushirikishwaji wa vijana katika sekta ya kilimo nchini Tanzania ni muhimu sana kwa maendeleo ya kilimo na uchumi wa nchi. Vijana ni nguvu kazi muhimu katika nchi nyingi za Afrika, ikiwa ni pamoja na Tanzania. Hata hivyo, idadi kubwa ya vijana hawashiriki kikamilifu katika kilimo kutokana na changamoto mbalimbali zikiwemo ukosefu wa elimu na mafunzo ya kilimo, upatikanaji mdogo wa ardhi na mtaji, na kutokuwepo kwa teknolojia za kisasa za kilimo. Kwa kuwa sekta ya kilimo inachangia zaidi ya asilimia 25 ya pato la taifa na ajira kwa zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania, ushirikishwaji wa vijana katika sekta hii utasaidia kuleta mambo yafuatayo.

Kwanza kabisa ushirikishwaji wa vijana katika sekta ya kilimo utasaidia kutatua tatizo la ajira kwa vijana. Vijana wengi nchini Tanzania wamekuwa wakikabiliwa na tatizo la ajira hivyo wamekuwa wakijihusisha na shughuli za ujumla kama bodaboda na ufanyaji kazi za kibarua ambazo zina changamoto nyingi. Kwa kuwapa fursa ya kujiunga na sekta ya kilimo, wataweza kuajiriwa au kuanzisha biashara zao wenyewe na kujipatia kipato chenye uhakika.

Pili Vijana wanaweza kuleta ubunifu katika sekta ya kilimo. Kwa kuwa wengi wao wana elimu ya kutosha kuhusu teknolojia za kisasa, wanaweza kuleta mabadiliko ya kisasa na teknolojia katika uzalishaji wa mazao ya kilimo. Wakiwa na ubunifu huu, wanaweza kupata masoko mapya kwa ajili ya mazao yao na hivyo kuongeza mapato yao.

Tatu kupunguza utegemezi wa chakula nchini. Ushirikishwaji wa vijana katika sekta ya kilimo pia utasaidia kupunguza utegemezi wa chakula kutoka nje ya nchi. Tanzania ina uwezo wa kuzalisha chakula cha kutosha kwa ajili ya matumizi ya ndani na hata kuuza nje, lakini bado inaagiza chakula kutoka nje. Kwa kuwahusisha vijana katika kilimo, uzalishaji utaongezeka na hivyo kupunguza utegemezi wa chakula kutoka nje ya nchi.

Pamoja na hayo yote zipo hatua kadhaa zinazopaswa kuchukuliwa na serikali Pamoja na wadau mbalimbali ili kuvutia, kuwawezesha na kuwajengea vijana uwezo wa kushiriki kikamilifu katika kilimo.

utoaji wa elimu na mafunzo ya kilimo kwa vijana: Serikali na wadau wa maendeleo wanapaswa kuhakikisha kuwa vijana wanapata elimu na mafunzo ya kilimo ili waweze kushiriki kikamilifu katika sekta hiyo. Elimu na mafunzo hayo yanapaswa kuzingatia teknolojia ya kisasa za kilimo ili vijana waweze kutumia teknolojia hizokatika uzalishaji wa mazao.

Kuhakikisha upatikanaji wa ardhi: Vijana wanahitaji ardhi ili waweze kufanya kilimo. Serikali na wadau wa maendeleo wanapaswa kuchukua hatua za haraka kuhakikisha kuwa vijana wanapata ardhi kwa ajili ya kilimo. Aidha, ni muhimu pia kuhakikisha kuwa ardhi hiyo ina miundombinu ya kutosha kama vile maji, barabara na umeme.

Kuhakikisha upatikanaji wa mikopo yenye riba nafuu: Vijana wanahitaji mitaji ya kuanzisha biashara zao. Taasisi za kifedha zinapaswa kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa vijana ili kuwawezesha kukuza biashara zao katika kilimo na hivyo kujikwamua kiuchumi.

Utoa motisha na uhamasishaji kwa vijana: Vijana wanahitaji motisha na kuhamasishwa ili waweze kuona kilimo kama fursa ya kibiashara yenye faida. Serikali na wadau wa maendeleo wanapaswa kutoa motisha kwa vijana kama vile zawadi, tuzo, na ruzuku ili kuwahamasisha kujiunga na sekta ya kilimo.

Hitimisho.
Ushirikishwaji wa vijana katika sekta ya kilimo ni muhimu sana kwa maendeleo ya kilimo na uchumi wa Tanzania. Vijana wanapaswa kuona kilimo kama fursa ya kibiashara yenye faida na serikali na wadau wa maendeleo wanapaswa kutoa motisha, elimu ya masoko, na fursa za uvumbuzi kwa vijana ili waweze kufanya kilimo chenye tija na kufikia malengo yao ya kibiashara. Pia, ushiriki wa vijana katika maamuzi yanayohusu sekta ya kilimo ni muhimu ili kuboresha sera na mikakati ya kilimo. Kwa kufanya hivyo, Tanzania inaweza kuwa na sekta ya kilimo endelevu na yenye manufaa kwa vijana na taifa kwa ujumla.


Rejeo.

Ng’atigwa, Adella Albert, et al. " Uchambuzi wa sababu zinazoathiri ushiriki wa vijana katika biashara ya kilimo cha mboga mboga nchini Tanzania." Agriculture 10.7 (2020): 287.

Mihyo, P. B. "Sera za Kilimo na Jitihada za Kupunguza Umaskni Tanzania." (2019).
 
Back
Top Bottom